Thursday, July 17, 2014

JIHADHARI NA MAFUNUO

JIHADHARI NA MAFUNUO
(FROM THE OFFICE OF DIANA & C. MWAKASEGE)
Utangulizi
Nafahamu ya kuwa mara tu baada ya kusoma kichwa cha somo hili, ulianza kujiuliza maswali mbali mbali juu ya mafunuo.         
                Jihadhari na Mafunuo! Huu ni ujumbe muhimu uliomo katika somo hili. Si mafunuo yote ni ya Mungu au yanatoka kwa Mungu. Mafunuo maana yake nini? Chanzo cha kuwepo mafunuo ni nini! Utayafahamu kwa njia gani au kwa namna gani mafunuo yasiyokuwa ya Mungu?     
                Haya ni baadhi tu ya maswali mengi yanayojibiwa katika somo hili. Naamini kabisa ya kuwa Roho Mtakatifu aliyekuongoza kulisoma somo hili hivi sasa, atakuwa pamoja nawe katika kukuelewesha kwa undani na ufasaha zaidi mambo niliyoyaandika.  
                Kumbuka hizi ni siku za mwisho na kurudi kwa Bwana Yesu Kristo mara ya pili kuja kulichukua kanisa kumekaribia sana. Bwana na atuwezeshe katika kutafakari  maneno yaliyomo katika somo hili, ili siku ajapo tusiwe watu wa kuaibika mbele zake – bali tuwe watu wa kufurahi na kumsifu milele na milele – Amina! Kila wiki kwa wiki sita mfululizo tutakuwa tunajifunza sehemu ya somo hili. Ni matumaini yangu utakuwa pamoja nami kila wiki!
MAFUNUO
Neno hili MAFUNUO linatokana na neno FUNUA. Hili neno FUNUA limetafsiriwa toka kwenye neno la kiingereza la ‘Reveal’. Neno ‘Reveal’ kwa kiswahili lina maana ya funua, fumbua, fichua, dhihirisha, eleza siri, onyesha au vumbua.
Kwa hiyo neno ‘Mafunuo’ lina maana ya;
1. Mambo yaliyofumbuliwa ambayo yalikuwa yamefumbwa;
2. Mambo   yaliyofichukuliwa ambayo yalikuwa yamefichwa;
3. Siri iliyowekwa wazi;
4. Mambo yaliyodhihirishwa ambayo yalikuwa yamesitirika.
Wakristo wengi hasa waliookoka wanalitumia neno ‘Mafunuo’ bila kujua na kujali uzito wa maana yake. Utawasikia wanasema nimefunuliwa hili au lile. Lakini ukiangalia matokeo ya mafunuo hayo katika maisha yao yamewaletea madhara badala ya kuwaletea baraka.

Historia ya Mafunuo:

Mungu alipomuumba mtu kwa mfano wake, alitaka akae, aishi, afurahi na huyo mtu katika utukufu na utakatifu wake milele milele. Lakini mtu alipoasi maagizo ya Mungu, kulitokea mafarakano katika uhusiano huo. Mtu huyo akafukuzwa toka katika uwepo wa Mungu, na akaondolewa kabisa toka katika bustani ya Edeni. Mungu akawaweka Makerubi wailinde njia ya mti wa uzima. Soma kitabu cha mwanzo sura yote ya tatu.
Madhara ya uasi huo yalileta mauti kwa mwanadamu. Bwana Mungu alipomwambia Adamu ya kuwa hakika atakufa, hakuwa anamaanisha kifo cha kimwili, bali kifo cha kiroho ingawa kifo cha kimwili kilifuata baadaye. Maana yake ni kwamba Adamu na kizazi chake chote kitatengwa na uso wa Mungu. Uhusiano ule wa karibu uliokusudiwa na Mungu ukapotea. Kukaingia ukuta wa giza kati ya Mungu na mwanadamu. Imeandikwa hivi:
“Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa; wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zime uficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong’ona ubaya. Hapana adaiye kwa haki wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili; hunena uongo; hupata mimba ya madhara na kuzaa uovu.” (Isaya 59: 1 – 4)
Kwa maneno mengine Nabii Isaya anatuambia sababu za uso na sauti ya Mungu kutokuwa wazi kwa Mwanadamu. Kitabu cha 1Yohana 3:4, kinatuambia ya kuwa dhambi ilipokaribishwa katika jamii, ilimfanya Mungu kuwa FUMBO kwa mwanadamu. Mpaka hivi leo dhambi ikiendekezwa katika moyo wa mtu, mambo ya Mungu yanakuwa ni kitendawili kigumu kwa huyo mtu.
Tangu wakati dhambi iliporuhusiwa na mwanadamu imtawale, imekuwa haiwezekani kwa mwanadamu kumwona au kumsikia Mungu, bila ya Mungu mwenyewe kujifunua kwanza kwake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa Mungu amekuwa fumbo kwa mwanadamu, Fumbo hili linafumbuliwaje? Yanenaje Maandiko? Imeandikwa hivi;
“Lakini kama ilivyoandikwa, mambo ambayo jicho halikuyaona  wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu), Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu AMETUFUNULIA sisi kwa Roho. Maana roho huchunguza YOTE, hata MAFUMBO YA MUNGU. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1 Wakoritho 2: 9-12).
Watu wengine wanadhani wanaweza kumfahamu Mungu na mambo yake kwa uwezo wao wenyewe. Lakini Biblia inasema hivi “Mambo ya Mungu HAKUNA ayafahamuye ila Roho wa Mungu”. Kwa maneno mengine ina maana ya kuwa, ikiwa tunahitaji kuyafahamu mambo ya Mungu inatubidi tujifunze kushirikiana na Roho Mtakatifu.
Ndani ya mafunuo hayo ya Roho Mtakatifu, Mungu anatufundisha, anatukumbusha, anatuongoza, na mambo yajayo anatupasha habari yake. Yesu Kristo alisema; “Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE, na KUWAKUMBUSHA YOTE niliyowaambia ….. ATAWAONGOZA awatie kwenye kweli YOTE; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na MAMBO YAJAYO ATAWAPASHA habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari” (Yohana 14:26; Yohana 15:13,14)
Ukiendelea zaidi kuzisoma habari za Roho Mtakatifu, utazidi kuona ya kuwa bila msaada wake, mwanadamu hawezi kabisa kuyafahamu makusudi na siri ya Mungu. Nawasikitikia watu wale ambao wanadai kuwa wao ni wakristo, lakini hawampi Roho Mtakatifu nafasi anayostahili katika maisha yao. Mafanikio ya ukristo wetu yanategemea sana jinsi sisi tunavyoshirikiana na Roho Mtakatifu.
Roho zenye uwezo wa kufunua mambo:
Kuna roho za aina tatu zenye uwezo wa kufunua mambo mbali mbali ambayo yalikuwa yamefichwa. Roho hizi ni 1. Roho Mtakatifu; 2. roho ya Mwanadamu; 3. roho ya shetani.
Ni muhimu ufahamu ya kuwa wakati mwingine roho ya mwanadamu au roho ya shetani inafunua mambo  na kudai ya kuwa mambo hayo yametoka kwa Mungu. Wakati mwingine mafunuo hayo yanasindikizwa na mistari mingi ya biblia, lakini ukiyachunguza kwa uwezo wa Mungu utafahamu kuwa mafunuo hayo si ya Mungu.
Maisha, ushuhuda, huduma za wakristo wengi zimeharibika kwa kutokuwa waangalifu mafunuo yanapotokea. Kuna wengine hata wamefikia hatua ya kuidharau biblia, na kusema kuwa wao wanaishi na wanakwenda kwa mafunuo wanayodai kuwa wanayapata moja kwa moja toka kwa Mungu. Mawazo ya namna hii ni ya uharibifu na ya upotovu kabisa. Mafunuo ya Mungu hayawezi kupingana na neno lake lililomo katika biblia.
Tukiziangalia na kuzichunguza hizi roho tatu zenye uwezo wa kufunua mambo, tunaona habari zifuatazo:
1.      Roho Mtakatifu:

“ Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1 Wakoritho 2:10,11)

Kama tunavyofahamu “ Mafumbo ya Mungu” maana yake ni “Siri za Mungu”. Pamoja na kufanya kazi zingine, Roho Mtakatifu ana wajibu wa kutufunulia siri za Mungu.
Nilipokuwa natafakari juu ya jambo hili, niliweza kuona ya kuwa katika agano jipya, Roho Mtakatifu ana wajibu wa kutufunulia siri zisizopungua saba toka kwa Mungu. Ndani ya siri hizi, kumefichwa utajiri mkuu na makusudi makuu ya Mungu juu yetu.
Wakati mwingine Mungu akipenda, nitaandika juu ya siri hizi saba kwa undani lakini katika somo hili nitazitaja tu na kuonyesha mahali zilipoandikwa. Siri hizi saba ni hizi zifuatazo:-
(a)  Siri yake Kristo – Waefeso 3:4
(b)  Siri ya Mapenzi ya Mungu – Waefeso 1:8
(c)  Siri ya ndoa na uhusiano uliopo kati yake na uhusiano wa Kristo na Kanisa – Waefeso 5:32
(d)  Siri ya injili iletayo Wokovu – Waefeso 6:19, Warumi 1:16; 17
(e)  Siri ya Mungu yaani Kristo – Wakolosai 2: 1- 3
(f)   Siri ya utauwa, au Utatu Mtakatifu – 1Timotheo 3:16
(g)  Siri ya Kristo ndani yetu tumaini la Utukufu – Wakolosai 1:26 – 29
Hakuna mtu anayeweza kufahamu yaliomo ndani ya siri hizi bila kufunuliwa na Roho Mtakatifu. “Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho (Mtakatifu) atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa (tuliyopewa bure) na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1Wakoritho 12 – 14)
2.    Roho ya Mwanadamu:
“Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?” (1 Wakorintho 2:11a)
Tafsiri nyingine ya swali hili tunaweza  kuulizwa hivi; ‘Maana ni nani katika binadamu  ayajuaye mambo ya moyoni mwako, kama siyo roho yako mwenyewe iliyo ndani yako?
Nadhani utakubaliana na mimi ya kuwa, unayo mambo fulani moyoni mwako ambayo hujamwambia mtu yeyote. Hayo mambo wakati mwingine yanaitwa siri ya moyo. Siku ukiamua kuitoa, basi inakuwa ni siri iliyowekwa wazi au siri iliyofunuliwa. Mambo hayo uliyoyaficha moyoni mwako, siku ukiyasema yanakuwa mafunuo kwa wengine.
Wakati fulani tulikuwa katika semina nzuri sana ya Neno la Mungu, na uwepo wa Mungu ulidhihirika wazi mbele ya watu wote waliohudhuria. Karama mbalimbali zilijitokeza kwa kadri ambavyo Roho Mtakatifu alivyoamua kuwatumia watu waliokuwepo.
Katikati ya baraka hizi kuliinuka mtu mmoja ambaye alisema hivi; “Wewe uliyechukua vitu vyangu urudishe.” Jinsi ambavyo maneno haya yalisemwa, ilionekana kana kwamba ni ujumbe kutoka kwa Mungu unaotolewa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Lakini ukiyachunguza maneno hayo kwa undani, mtu huyu hakuwa anatumiwa na Roho Mtakatifu, bali ni roho wa mtu huyo alikuwa akifunua mawazo yaliyokuwa ndani yake. Labda alifikiri kuwa akisema kwa njia ya kutoa ‘Ujumbe’ yule aliyechukua vitu vyake ataogopa!
Kuna jumbe nyingi zinazotolewa hasa katika vikundi vya uamsho na katika makusanyiko walipo watu waliojazwa Roho Mtakatikfu, ambazo si zote zinakuwa zimetolewa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kuna unabii mwingine unakuwa umechanganywa na mawazo ya mtu anayetoa ujumbe. Lakini tumshukuru Mungu kwa kuwa kuna watu wanaotumiwa na Roho Mtakatikfu kutoa ujumbe bila ya kuongeza mawazo yao ya kibinadamu ndani yake.
Kuna ugonjwa mwingine ulioingia kwa wahubiri, hasa kati ya wale wasiopatana au walio na uchungu na wenzao. Utakuta akisimama kuhubiri badala ya kusema Neno la Mungu lilivyo, anaanza kulitumia neno hilo kuwasema watu asiopatana nao, na huku anadai kuwa ni mafunuo ya Mungu!
Je! Ni vizuri kuzitumia nafasi tulizopewa na Mungu kuhubiri Neno lake, kwa kusemana na kulaumiana! Je! Hayo ni mafunuo ya Mungu? Ni wazi ya kuwa hayo si mafunuo ya Mungu bali ni mawazo ya roho ya binadamu.
Bwana Mungu alisema na kuuliza kwa kutumia kinywa cha Nabii Yeremia maneno haya; “Maana ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu na kulisikia?
“Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri. Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao. Mimi ni Mungu aliye karibu, asema Bwana, mimi si Mungu aliye mbali…..
“Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? (Yeremia 23:18,21-23, 28, 29)
Kwa hiyo ni vizuri uwe mwangalifu, kwa kuwa si kila mtu anayesema ana mafunuo ya Mungu, amepewa ufunuo huo na Mungu kweli. Wengine wana ufunuo wa Mungu lakini wengine wanasema maneno yao na kudai ni mafunuo ya Mungu.
3.         Roho ya shetani :
Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali kijakazi kimoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” (Matendo ya Mitume 16:16 – 18)
Jambo la kushangaza juu ya tukio hili ni kwamba huyo pepo wa uaguzi alijificha ndani ya mtu kwa kujifanya anasema kweli juu ya utumishi wa Paulo na wenzake!
Kuna mambo muhimu sana ya kujifunza katika habari hii ikiwa tunataka kufahamu jinsi ambavyo shetani anaweza kupenyeza mafunuo katikati ya wakristo na kuwadanganya wengi.
Hebu tuangalie na kujifunza kama ifuatavyo:-
(a)        Shetani anapotaka kuleta machafuko katikati ya wakristo, – nyumbani mwao, katika makanisa na pia katika mikutano ya kiroho anatumia WATU au MTU. Imeandikwa hivi; “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi kimoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.” (Matendo ya Mitume 16:16)
Tunaona hapa ya kuwa mtu huyu mwenye pepo wa uaguzi aliwafuata Paulo na wenzake mahali walipokuwa wakisali. Kwa lugha ya siku hizi tungesema aliwafuata kanisani, au kwenye mkutano wa kiroho, au kwenye semina ya kiroho, au kwenye somo la biblia, au kwenye kikundi cha maombi.
Huyu pepo wa uaguzi, kwa nini alimwongoza mtu huyu kwenda mahali ambapo watu wa Mungu walikuwa wanafanya sala? Lazima alikuwa na lengo maalum. Huyu mtu mwenye pepo wa uaguzi hakuenda mahali pa kusali kwa sababu alikuwa anataka kusali, bali kwa kuwa alikuwa ana lengo la kutaka kuchafua ibada au sala zilizokuwa zinafanyika pale.
(b)        Shetani akiisha pata nafasi ya kumweka mtu wake katikati ya wakristo, atatafuta kila njia ya kuchafua masikilizano yao huku akijitahidi kusema maneno ya Mungu wakati huo huo, ili ASIJULIKANE!
Imeandikwa hivi, “(Mtu huyu mwenye pepo wa Uaguzi) Akamfuata Paulo na sisi akipiga KELELE, akisema, watu hawa ni watumishi , wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu” (Matendo ya Mitume 16:17)
(c)         Kwa sababu alishuhudia mambo ya kweli juu ya Paulo na wenzake kuwa ni “watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu;” aliweza kukaa katikati ya watu wa Mungu kwa MUDA MREFU BILA KUGUNDULIKANA. Ndiyo maana imeandikwa; “Akafanya hayo siku nyingi.”
Watu wa Mungu nataka kuwaambia ya kuwa iweni macho! Huu si wakati wa kusinzia! Si kila mtu asemaye ni mkristo – ni mkristo kweli. Si kila mtu asemaye ‘Bwana Asifiwe’ – ameokoka kweli! Wengine wametumwa na shetani.
Kuna watu ambao shetani amewaweka kati yenu ili kuwachonganisha na kuwatenganisha. Je! hujaona hali ilivyo katika makanisa, au vikundi vya maombi, ambapo kila wakati wakiwepo watu fulani, kunakuwa hakuna maelewano na mapatano, na wakati mwingine ibada na mikutano kuvurugika? Watu hao wasipohudhuria, kunakuwa na amani, mapatano na ushirikiano. Ukiona hali ya namna hii ujue inawezekana ya kuwa tayari shetani amekwisha weka askari wake katikati yenu.
Yesu Kristo akijua hili alitoa mausia kwetu sisi tulio watu wake; alisema: “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Mtawatambua kwa matendo yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? … Si kila mtu aniambiaye Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengine wataniambia siku ile, Bwana, Bwana hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mathayo 7:15,16, 21 – 23)
Hii inaonyesha wazi ya kuwa, si kila mtu atoaye mafunuo ya neno la Mungu – ametumwa na Mungu kweli. Tuwe waangalifu na watu tunaoshirikiana nao katika sala na ukristo wetu. Tusisikilize maneno yao tu na kuamini kuwa wao ni wenzetu katika Bwana; bali tuangalie na mienendo yao kama ina ushuhuda wa kikristo! Tukumbuke ya kuwa, “Imani pasipo matendo imekufa.” (Yakobo 2:26)
(d)        Mtu huyu aliyekuwa na pepo wa uaguzi alifunua jambo ambalo Paulo na wenzake walikuwa wanafanya, na pia alifunua ya kuwa wao ni watumishi wa Mungu aliye juu.
Ingawa mafunuo hayo yalikuwa kweli, yalimkosesha amani Mtume Paulo. Imeandikwa hivi, “Lakini Paulo akasikitika (akasononeka au akakosa amani) akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu akamtoka saa ile ile.” (Matendo ya Mitume 16:18)
Nataka uone jambo moja muhimu sana hapa. Biblia inasema; “ Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule PEPO ….”
Kwa nini Paulo akamwambia yule pepo na siyo yule mtu aliyekuwa na pepo? Kwa nini Paulo aliamua kumkemea yule pepo na hakumkemea yule mtu ambaye alikuwa na pepo? Inaonyesha wazi kuwa Paulo hakusikitika kwa sababu ya yule mtu kuwa pamoja nao; bali alisikitika kwa sababu ya yule pepo kuwa pamoja nao, akiwafuata na kuwapigia kelele!

Tunajifunza nini katika hili?

Tunajifunza ya kuwa; “Ingawa tunaenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili …. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu …………” (2Wakoritho 10;3, Waefeso 6:12, 13a)
Unapoona Roho wa Mungu anakushuhudia ya kuwa kuna pepo anayemtumia mtu katikati yenu, mkemee pepo huyo amtoke huyo mtu kwa jina la Yesu, na matatizo yaliyokuwa yanawasumbua yatatoweka. Kushindana na mtu juu ya machafuko fulani katikati yenu, na kumbe ni shetani amejificha ndani yake, ni kukosa maarifa ya kiroho. Na hii haitatui tatizo, bali inachochea ugomvi na mafarakano.
Ugomvi unaoletwa na shetani katikati ya watu wa Mungu hautatuliwi na vikao vya usuluhishi wala mahakama, bali kwa kutumia mamlaka ya Jina la Yesu Kristo na kumkemea shetani aliye chanzo cha ugomvi pamoja na hekima ya Roho Mtakatifu.

MAMBO MATANO MUHIMU UNAYOHITAJI KUJUA JUU YA MAFUNUO
Napenda kukumbusha ya kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kuyafahamu mambo ya Mungu kama hakufunuliwa na Roho Mtakatifu.
Lakini tukumbuke tumeona ya kuwa roho ya mwanadamu na roho ya shetani huwa mara nyingi zinapenda kufunua mambo katikati ya wakristo ili yaonekane na kupokelewa kama vile ni mafunuo ya Mungu.
Kwa kutofahamu, watu wengi na wakristo wengi wanahangaika kiroho, wengine wamepoteza hata ushuhuda, na wengine huduma walizopewa na Mungu zimeharibika! Yote hii ni kwa sababu ya kutokuwa waangalifu wanapokutana na mafunuo. Hali ni mbaya na inasikitisha.
Wakati fulani niliona nimuulize Mungu juu ya hali hii iliyoletwa na mafunuo. Na hasa nilitaka kufahamu mtu afanyeje anapokutana na mafunuo? Pia, nilitaka kujua mtu atatofautishaje mafunuo ya Mungu na yale yasiyo ya Mungu?
Siku moja alfajiri nilisikia sauti ya Roho Mtakatifu ikisema hivi ndani ya roho yangu; “Andika mambo matano yafuatayo, ambayo ni muhimu uyajue unapokutana na mafunuo”.
Nilijifunua blanketi, na kuondoka kitandani. Nikachukua kalamu na karatasi, huku taa ikiwaka, nilianza kuandika mambo haya matano ambayo nataka nikushirikishe yakusaidie. Nilipomaliza kuyaandika, Roho Mtakatifu akaniambia; ‘ Wape watu wangu maneno hayo wayatafakari na kuyafanyia kazi”. Maneno yenyewe ni haya yafuatayo:
1.   Kila ufunuo lazima upimwe na neno la Kristo:
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni (zipimeni) hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani (1Yohana 4:1)
“Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni (pimeni) mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna” (1 Wathesalonike 5:19 – 22).
Kwa mistari hii tumeruhusiwa kujaribu au kupima mafunuo yanayotolewa na roho yoyote, hata ile ya Mungu! Utashangaa kuona watu wengine wanadai wana mafunuo, lakini hawataki au hawapendi yapimwe!
Biblia inatuambia tuzipime hizo roho zinazoleta mafunuo, kwa kuwa zingine hazijatokana na Mungu. Ukiona mtu anasema ana mafunuo au ufunuo toka kwa Mungu lakini hataki upimwe, hiyo ni dalili ya kutosha ya kuonyesha kuwa ufunuo huo una ‘short’ au una kasoro!
Ikiwa biblia inasema tupime, kwa nini yeye akatae? Makanisa mengi, vikundi vingi vya maombi, na mikutano mingi ya kiroho imevurugika kwa sababu ya kupuuzia juu ya jambo hili la kuyapima mafunuo ya roho mbalimbali. Kwa wale waliofuata ushauri huu, wameokoka na mambo mengi ambayo shetani alinuia kuwafanyia vibaya.
Kwa kutoyafahamu maandiko vizuri, watu wengi wamejikuta katika masononeko ya kiroho, hasa wakati wa kufanya huduma ya kuwaombea wagonjwa.
Utasikia wakati mwingine, mgonjwa anaambiwa ya kuwa ugonjwa alionao hauponi kwa sababu kuna dhambi moja aliyoifanya kabla ya kuokoka ambayo haijasamehewa. Mhudumu huyo mara nyingi atadai kuwa huo ni ufunuo aliopewa na Roho Mtakatifu ili kutatua tatizo la ugonjwa huo.
Kwa hiyo huyo mgonjwa kwa kuwa hafahamu vizuri juu ya msamaha wa dhambi anaanza kutubu tena juu ya hiyo dhambi.
Lakini ni muhimu tufahamu kuwa mtu anaposema kuwa dhambi iliyofanywa kabla ya mtu kuokoka haijasamehewa, mambo yafuatayo yanajitokeza ambayo ni haya:
(i)        Mungu hasamehi dhambi zote mtu anapookoka, - kuna zingine zinabaki, AU
(ii)       Mtu aliyekuwa anaomba msamaha, hakutubu sawasawa, kwa hiyo hata kuokoka kwake kuna walakini.
Je! haya mawazo ni ya kweli? Biblia inasema- je juu ya msamaha wa dhambi kwa mtu anayetubu? Naomba uyasome kwa kuyatafakari maneno yafuatayo kutoka katika Biblia.
“Haya njooni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:8)
“Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi;.. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako” (Isaya 43:14, 25)
“Na Roho Mtakatifu naye atushuhudia; kwa maana, baada ya kusema; hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao SITAUKUMBUKA TENA KABISA” (Waebrania 10:15 – 17)
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu WOTE” (1 Yohana 1:9)
“Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote; Akusamehe maovu yako YOTE, akuponya magonjwa yako YOTE” (Zaburi 103: 2,3)
Sijui umepata ujumbe gani katika mistari hii; kwa upande wangu najifunza na kuwa na uhakika ya kuwa; mtu anapotubu na kuokoka  (au kuzaliwa mara ya pili), Mungu anamsamehe dhambi zake ZOTE, wala hazikumbuki TENA.
Kwa kufahamu hivi, ninasita kukubali kuwa ni ufunuo wa Roho Mtakatifu kusema kuwa dhambi ndizo zinazomfanya asipone ugonjwa wake baada ya kuokoka. Kwa nini nasema hivi? Kwa sababu Mungu anasemehe, anafuta dhambi na wala hakumbuki tena kama uliwahi kuzifanya! Kitu unachohitaji kujua zaidi ni kwamba, baada ya kusamehewa dhambi – Roho Mtakatifu atakuongoza kwenye kuyatengeneza maisha yako mapya. Kuna tofauti ya kutubu dhambi na kutengeneza maisha yako baada ya kutubu. Kutotengeneza maisha kunaweza wakati mwingine kuzuia uponyaji wako kama unaumwa.
Ni roho yupi huyu ambaye kwenye biblia anasema Mungu hakumbuki dhambi alizosamehe halafu asema kwa kinywa cha mtu kuwa kuna dhambi ambazo Mungu anazikumbuka baada ya mtu kutubu?
Ukiona namna hii, ningekushauri ufuate maelezo ya Biblia. Mtu akikupa ufunuo mwombe akuonyeshe ni wapi katika biblia ufunuo huo umeelezwa.
Kumbuka imeandikwa: “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho kama zimetokana na Mungu: kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1 Yohana 4:1)
2.   Mtu anapewa ufunuo kwa sehemu
“Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika, zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu KWA SEHEMU; na tunafanya unabii KWA SEHEMU; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika: Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga; nalifahamu kama mtoto mchanga nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo, wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu, wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1 Wakorintho 13:8-12)
Si hekima bali ni kiburi kwa mkristo yeyote kudai kuwa anafahamu kila kitu juu ya neno la Mungu. Hata Mtume Paulo hakudai kuwa anafahamu kila kitu PEKE YAKE. Ni kweli mtu anaweza kupewa mafunuo mengi juu ya neno la Mungu lakini hawezi kupewa mafunuo YOTE.
Nasema haya kwa sababu ya yale tunayojifunza tunaposhiriki pamoja kula chakula cha Bwana. Imeandikwa hivi;
“Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki: kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu” (Mathayo 26:26 –29)
Ni wazi kwamba wakati walipokuwa wakishiriki Pasaka, Yesu Kristo alikuwa anawapa wanafunzi wake mafundisho makubwa sana. Mojawapo ya fundisho tunalolipata hapa ni UMUHIMU WA KUTEGEMEANA NDANI YA KRISTO NA KWA AJILI YA KRISTO.
Yesu Kristo alichukua MKATE MMOJA. Mkate huu mmoja akaubariki na kisha AKAUMEGA VIPANDE KUMI NA TATU. Unaweza kuniuliza kuwa ninajuaje kuwa ni vipande kumi na vitatu na huku haijaandikwa hivyo mahali popote?
Lakini napenda ufahamu kuwa katika sikukuu hiyo ya Pasaka, kulikuwa na washiriki kumi na tatu katika chumba hicho kinachozungumzwa.
“Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka PAMOJA NA WANAFUNZI WANGU …. Basi kulipokuwa jioni (Yesu) aliketi chakulani PAMOJA na wale THENASHARA”  (Mathayo 26:18-20)
Tunafahamu kuwa “Thenashara” maana yake ni “Kumi na mbili”. Kwa hiyo tunaweza kusema Yesu aliketi chakulani pamoja na wale kumi na wawili. Hii inatupa jumla ya washiriki KUMI NA WATATU jioni ile-tukimhesabia na Yeye!
Yesu alipokuwa anagawa mkate, kila mmoja wao alipata KIPANDE CHA MKATE HUO HUO MMOJA, hii ni pamoja na Yesu mwenyewe.

Tunajifunza nini katika hili?

Yesu Kristo ni ‘mkate’ ushukao toka mbinguni kwa ajili ya uzima wa ulimwengu (Yohana 6:47-59). Pia, fahamu ya kuwa Yesu Kristo ndiye Neno aliyefanyika mwili (Yohana 1:14).
Kwa hiyo Yesu Kristo alipokuwa anawapa kila mmoja kipande cha mkate alitaka wafahamu yafuatayo.
(a)        Hakuna mtu aliyepewa Mkate mzima bali sehemu tu ya mkate, kwa hiyo ana sehemu tu ya Ufunuo wa Neno la Mungu toka kwa Kristo Yesu
(b)        Waone umuhimu wa kufanya kazi pamoja, kwa kuwa akienda mtu mmoja akawaacha wengine kumi na mbili, watu watakaomsikiliza hawatafahamu siri ya sehemu iliyobaki ya mkate. Hata kama hao kumi na mbili, wakiamua kumwacha mmoja, watu watakaowasikiliza hawatafahamu siri ya sehemu ya mkate iliyobaki kwa yule mmoja.
(c)        Wajue siri ya AGANO jipya ya KUTEGEMEANA, KUSAIDIANA NA KUFAIDIANA. Hii ni kati ya Yesu na wanafunzi wake: na pia kati ya wanafunzi wake wenyewe kwa wenyewe.
Bila Yesu wanafunzi hawawezi kufanya lolote. Hii haimaanishi ya kuwa wanafunzi wanaweza kuikwamisha kazi ya Kristo-kwani wakikataa kumtumikia, Yesu Kristo atainua wengine!
Kwa nini iwe hivyo?
Hii ni kwa sababu Yesu ni kichwa cha Mwili na wanafunzi wake ni viungo mbali mbali vya mwili wake (1 Wakorintho 12:12 – 27; Warumi 12:3-7; Waefeso 1:17 – 23). Yesu akiamua kufanya kazi hapa duniani bila wanafunzi wake, ni sawa na kichwa kuamua kutembea bila mwili.
Je hii inawezekana?
Imeandikwa katika kitabu cha Amosi 3:7 hivi;
“Hakika Bwana Mungu HATAFANYA NENO LOLOTE, BILA kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake”.
Ukisoma mstari huu swali linalokujia ni-kwa nini iwe hivyo wakati mahali pengine katika biblia anasema hakuna neno lisilowezekana kwa Bwana (Luka 1:37).
Jibu lake ni kwa sababu Bwana anatekeleza agano aliloliweka na wanafunzi wake kwa damu yake na mwili wake mwenyewe.
Kuna mambo mengi ya kujifunza hapa lakini nadhani kwa maelezo haya machache utaelewa jambo nililotaka ulielewe juu ya mafunuo; nalo ni hili; KILA KIUNGO KATIKA MWILI KWA KRISTO KINA FAIDA NA WAJIBU WAKE. KILA KIUNGO NI SEHEMU TU YA MWILI – KWA HIYO KINA SEHEMU TU YA UFUNUO MZIMA WA KRISTO (NENO LA MUNGU).
Ni hatari na ni mwanzo wa kuwa na kiburi kwa mkristo yeyote kudhani kuwa ANAJUA KILA KITU JUU YA NENO LA MUNGU BILA kupata msaada wa wakristo wenzie ndani ya Kristo. “Katika yeye (Kristo) mwili wote ukiunganishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo” (Waefeso 4:16).
3.  Ufunuo unakuja kwa ajili ya KUFAIDIANA, KUJENGANA, KUJIFUNZA, KUONYA NA KUFARIJI.
Neno la Mungu linalofundishwa na Roho Mtakatifu haliwagawi wakristo kwa wakristo bali HUWAUNGANISHA KATIKA KRISTO – bila kujali dhehebu la Kikristo wanakotoka, nchi, rangi na kabila lao mradi tu wanamkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wao katika roho na kweli.
Ni budi tuwe waangalifu tunapoona mtu analeta mafunuo yanayowafanya wakristo kugombana na kuchukiana. Ni muhimu kuipima roho ili tuifahamu ni ya namna gani kabla ya kuifuata.
Nafahamu kuwa Neno la Mungu linalofundishwa na Roho Mtakatifu linawatenga watu mbali na dhambi, hukumu, na toka ufalme wa shetani ILI kuwaunganisha katika Kristo.
Ufunuo wa Kristo unakuja katikati ya wakristo kwa ajili ya kufaidiana, kujengana, kujifunza, kuonya na kufariji. Imeandikwa hivi;
“Basi, ndugu (wakristo), imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana UFUNUO, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la KUJENGA …. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate KUJIFUNZA, na wote WAFARIJIWE… kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu”    (1Wakorintho 14:26,31,33).
Soma zaidi katika kitabu cha Matendo ya Mitume ili ufahamu kwa undani jinsi wakristo walivyoshirikiana na walivyotumika na Roho Mtakatifu.
Ni muhimu kutokuwa wepesi kuupokea ufunuo ambao unaleta ugomvi na dharau baina ya wakristo wenyewe kwa wenyewe.
4.   Mungu hampi mtu ufunuo bila ya kumpa KWANZA hekima ya kuutumia huo ufunuo.
Hekima maana yake ni uwezo ulionao wa kutumia vitu ulivyonavyo. Kuna hekima za aina tatu duniani (a) Hekima ya Mungu (b) Hekima ya mtu (c) Hekima ya shetani.
Hekima ya Mungu ndani ya mtu ni uwezo wa Mungu ulio ndani ya mtu unaomwezesha mtu huyo kuvitumai vitu alivyonavyo kwa UTUKUFU WA MUNGU.
Hekima ya mtu ni uwezo alionao mtu unaomwezesha mtu huyo kutumia vitu alivyonavyo kwa utukufu wake – au kwa ubinafsi.
Hekima ya shetani ni uwezo wa shetani ulio ndani ya mtu unaomwezesha kuvitumia vitu alivyonavyo kwa faida ya shetani.
Biblia inasema hivi;
“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba wa utukufu,  awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye ….” (Waefeso 1:17)
“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote ….”             (Wakolosai 3:16).
Mtume Paulo alipokuwa akiomba kwa ajili ya wakristo, aliomba tupewe KWANZA roho ya hekima ndipo baadaye akaomba tupewe roho ya ufunuo. Aliomba hivi ili ufunuo tutakaopewa utumike kwa ajili ya UTUKUFU WA MUNGU na sio utukufu wa mtu wala wa shetani.
Pia, tunajifunza katika maneno tuliyoyasoma toka kitabu cha Wakolosai 3:16 kuwa Neno la Kristo linaambatana na hekima yote ya Mungu.
Imeonekana katika sehemu nyingi ya kuwa mtu akitoa ufunuo, na Neno la Kristo pasipo kutumia hekima ya Mungu, mara nyingi mahali alipotoa ufunuo huo patakuwa na machafuko; pia yeye mwenyewe anakosa maisha ya ushuhuda ndani ya Kristo.
Utaipataje hekima hii ya Mungu? Imeandikwa hivi; “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana” (Yakobo 1:5-7).
Kwa hiyo ikiwa unaona umepungukiwa hekima, usisite kuomba kwa Mungu naye atakupa!
Pamoja na maombi ni muhimu uwe mtendaji wa Neno la Mungu. Kuwa mwombaji bila utendaji wa Neno ni sawa na mtu aliye na nguvu lakini hazitumii wala hajui namna ya kuzitumia vizuri.
Imeandikwa hivi; “ Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu aliyefanywa kwenu HEKIMA ITOKAYO KWA MUNGU, na haki, na utakatifu, na ukombozi” (Wakorintho 1:30
Unapompokea Yesu Kristo, unapokea hekima ya Mungu. Yesu Kristo ni neno la Mungu (Yohana 1:14). Kwa hiyo utaona yakuwa kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako, maombi, na utendaji wa Neno kwa pamoja ni msingi mzuri sana wa kupata hekima ya Mungu na kutembea ndani yake.
Ili kutunza heshima ya Mungu katikati ya watu wa Mungu walio wakristo, hekima ya Mungu inahitajiwa kuongoza mambo yote – hii ni pamoja na mafunuo.
5.   Ufunuo wa Mungu una Majira yake.
Naomba tuisome na kuitafakari pamoja mistari ifuatayo inayotupa msingi wa kusema ufunuo wa Mungu hauji bila mpango maalum kwa kufuata majira aliyoyakusudia Mungu juu ya ufalme wake:
“Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na UFUNUO wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele, IKADHIHIRISHWA (Ikafunuliwa) WAKATI HUU KWA maandiko ya manabii, IKAJULIKANA na mataifa yote kama alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani” (Warumi 16:25.26).
“Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Yesu Kristo; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, UTAKAOSHUHUDIWA KWA MAJIRA YAKE” (1 Timotheo 2:5,6).
Yesu Kristo akizungumza na wanafunzi wake alisema:
“Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini HAMWEZI KUYASTAHIMILI hivi sasa” (Yohana 16:12)
Inaonekana wazi ya kuwa Mungu ameyaratibu mambo yake ili yafunuliwe kwa wanadamu katika majira mbalimbali. Pia, tukumbuke ya kuwa imeandikwa ya kuwa “mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1 Wakorintho 2:11b).
Lakini Mungu anatufunulia mafumbo na mipango yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa maneno mengine napenda kukushauri ya kuwa, mtegemee sana Roho Mtakatifu ili ufahamu MUDA au MAJIRA au WAKATI wa kuusema ufunuo uliopewa.
Wote tunafahamu ya kuwa mtoto mchanga na mtu mzima wanakula chakula chenye matayarisho tofauti ikiwa wanataka kuishi katika afya nzuri. Mtoto mchanga akipewa chakula cha mtu mzima – kwa mfano kande, ni wazi kwamba atapata madhara tumboni.
Vivyo hivyo na mambo ya kiroho. Walio wachanga kiroho, hupewa maziwa ya kiroho. Wakipewa chakula kigumu au mafunuo mazito, wanadhurika katika maisha yao ya kiroho- wengine hufikia hatua ya kuchanganyikiwa, kupoa kiroho na wakati mwingine kufa kiroho.
Narudia tena kusema ya kuwa tujifunze kila wakati kumtii Roho Mtakatifu ili atuongoze wakati wa kuyatoa mafunuo tuliyopewa.

Mausia Mengine

Si rahisi kuandika kila kitu kinachotakiwa kuandika juu ya mafunuo, katika andiko fupi kama hili; lakini naamini haya niliyoongozwa na Roho Mtakatifu kukushirkisha yatakusaidia katika kutafakari zaidi na kukutahadharisha juu ya mafunuo.
Napenda ufahamu ya kuwa, si kila mtu aliye na ufunuo usio wa Mungu ana ‘mapepo’ kama watu wengine wanavyodhani. Kumbuka inawezakana ikawa ni roho yake inayotoa mafunuo hayo.
Kama nilivyotangulia kukueleza kuna roho tatu zenye uwezo wa kufunua mambo; (i) Roho Mtakatifu, (ii) roho wa mtu na (iii) roho wa shetani. Kwa hiyo tusiiamini kila roho bali tuzipime ili tujue kama ni kutoka kwa Mungu au hapana.
Muhimu:         Wiki ijayo ya tatu tunaendelea na somo hili la JIHADHARI NA MAFUNUO  na tutajifunza juu ya “KWA NINI TUPIME MAMBO YOTE?” Kwa hiyo usiache kulisoma somo hili.

KWA NINI TUPIME MAMBO YOTE?
“Msimzimishe Roho; msitweze unabii; JARIBUNI MAMBO YOTE, lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna” (1 Wathesalonike 5:19 – 22)
Tafsiri nyingine ya maneno haya inasema hivi; “Msimpinge Roho Mtakatifu; msidharau unabii. PIMENI KILA KITU: zingatieni kilicho chema, na epeni kila aina ya uovu”. Jaribuni mambo yote, hapa imetafsiriwa kuwa pimeni kila kitu.
Swali la kwanza lililonijia moyoni mwangu nilipokuwa nayasoma maneno haya ni, “kwa nini tujaribu mambo yote? Kwa nini Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuwaeleza wakristo wa mji wa Thesalonike kuwa WAJARIBU MAMBO YOTE?
Kwa nini wapime mambo YOTE na siyo wapime mambo MACHACHE?
Kwa kukukumbusha tu ni kwamba nyaraka zote mbili za Paulo kwa Wathesalonike ziliandikwa kwa ajili ya wakristo, na siyo kwa wale wasiomjua Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Ndiyo maana nyaraka hizi zote mbili zimeanza na maneno haya; “Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa KANISA (wakristo) la Wathesalonike,…..”
Kwa hiyo Mtume Paulo alipoandika kuwa wajaribu mambo yote, lazima alikuwa na sababu muhimu za kuandika hivyo. Hili si jambo dogo. Kwa maneno mengine alikuwa anawaangaliza wakristo ya kuwa wawe WAANGALIFU KATIKA MAMBO YOTE.
Kama onyo hili lilikuwa muhimu kwa wakristo wa Thesalonike, basi hata leo kwetu sisi tulio wakristo ni onyo la muhimu na la maana sana kwa maisha yetu ya kiroho.
Nilipoendelea kuyasoma maandiko Matakatifu yaliyomo katika Biblia, niliweza kuona sababu tisa zinazoeleza kwa nini wakristo tunatakiwa kujaribu au kupima mambo yote.
Sababu ya kwanza:
SI ROHO ZOTE ZINATOKANA NA MUNGU.
Ni muhimu ufahamu ya kuwa kuna roho za aina tatu.
  1. Roho wa Mungu; 2. roho wa mwanadamu; 3. roho wa shetani. Na roho zote hizi zina uwezo wa kusema na kujieleza. Na pia zina tabia zinazotofautiana. Ndiyo maana imeandikwa hivi;
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali ZIJARIBUNI HIZO ROHO, kwamba zimetokana na Mungu …..” (1Yohana 4:1a).
Kwa maneno mengine anatuonya ya kuwa si roho zote zinazojitokeza katikati ya wakristo zimetokana na Mungu. Kwa hiyo tunatakiwa tuzijaribu hizo roho wala tusiiamini kila roho!
Tena imeandikwa hivi:
“Basi roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo …….” (Timotheo 4:1a)
Nina uhakika unafahamu yakuwa siku hizi ni nyakati za mwisho. Kwa hiyo si busara kuiamini kila roho inayojitokeza katikati ya wakristo, wengine wameziamini roho zote na kuzisikiliza na mwishoni wameacha wokovu.
Sababu ya Pili:
KUNA WAPINGA KRISTO KATIKATI YA WAKRISTO.
Unaweza kushangaa na kutokuamini kuwa kuna wapinga Kristo katikati ya wakristo. Lakini ndivyo ilivyo! Wapinga kristo kwa jina lingine ni wapinga wokovu. Inatubidi kujaribu mambo yote kwa kuwa kuna wapinga wokovu katikati ya watu waliookoka.
Kumbuka Mzee Yohana alituandikia hivi:
“Watoto (watoto wa kiroho), ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga kristo yuaja, hata sasa WAPINGA KRISTO wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu” (1 Yohana 2:18,19).
Neno “wafunuliwe” linatueleza na kutupa picha ya kuwa hawa wapinga Kristo, ingawa wapo katikati ya wakristo huwa hawaonekani kwa urahisi, mpaka WAFUNULIWE ndipo tutakapowafahamu. Kumbuka mithali ya kiswahili isemayo, kikulacho ki nguoni mwako!
Nakumbuka wakati fulani nilikwenda mahali fulani kuhubiri nakuombea wagonjwa; wakati nilipokuwa naombea wagonjwa mtu mmoja aliangushwa chini na pepo.
Watu kadha wakambeba na kumleta mahali nilipokuwa nimesimama. Na lile pepo likasema hivi toka ndani ya yule mtu; “ Wamenigundua, wamenigundua”.
Mimi nikauliza lile pepo, “Kwa jina la Yesu, wewe ni nani?” Lile pepo likajibu hivi toka ndani ya yule mtu; “Mimi napinga wokovu, mimi napinga wokovu”.
Nilivyosikia hivyo nilijua ya kuwa hiyo ni roho ya mpinga kristo, kwa hiyo nikaliamuru litoke nikasema, “ kwa jina la Yesu wa Nazareti, wewe roho ya mpinga kristo toka ndani ya mtu huyu sasa hivi”. Na wakati ule ule mtu akafunguka na akawa mzima!
Baada ya mtu yule kufunguka nikamuuliza; “Je! wewe umeokoka? Naye akajibu; “Ndiyo nimeokoka”. Mimi nikashangaa sana moyoni mwangu, kwani nilijiuliza peke yangu inakuwaje mtu aliyeokoka awe na pepo linalopinga wokovu?
Kwa kuwa nilitaka kufahamu zaidi, nilimdadisi zaidi kwa maswali, nikamuuliza tena; “Ulikuwa unasumbuliwa na nini kabla ya kuanza maombi kwa wagonjwa”
Akajibu hivi; “Tangu niokoke nimekuwa nashindwa kushuhudia wala kuimba nyimbo za kumsifu Yesu Kristo. Kila nikitaka kushuhudia au kuimba napata hofu nyingi, na wakati mwingine naona kitu kikinikaba kwenye koo”.
Nikamwambia; “ Enenda kwa amani, jina la Yesu Kristo limekuweka huru”.
Hebu jiulize hata wewe inakuwaje mtu aliyeokoka awe na roho ya mpinga kristo inayopinga wokovu? Hili ni jambo la kushangaza sana. Mambo haya niliyokueleza si hadithi. Nimeyaona kwa macho yangu na kuyasikia kwa masikio yangu! La kushangaza zaidi ni kwamba ndugu zake waliookoka hawakufahamu kuwa katikati yao kulikuwa na mtu aliyekuwa na roho inayopinga wokovu; wala yule mtu mwenyewe hakufahamu kuwa ana roho ya namna hiyo!
Wapendwa katika Bwana, ni muhimu kujaribu mambo yote, kwani kuna roho ya mpinga kristo katikati ya wakristo. Kumbuka hizi ni siku za mwisho.
Sababu ya Tatu:
KUNA WAALIMU WA UONGO KATIKATI YA WAKRISTO
Imeandikwa hivi katika 2 Petro 2: 1a; “Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu,kama vile kwenu kutakavyokuwako WAALIMU WA UONGO …”
Kufuatana na Biblia kuna waalimu wa uongo wa aina mbili:
  1. Waalimu wa uongo wanaofundisha wakristo mapokeo ya wanadamu, soma Wakolosai 2:18, 20-23; na 2. Waalimu wa uongo wanaofundisha wakristo mafundisho ya mashetani. Soma 1 Timotheo 4:1-3 na 2 Petro 2:1-3.
Si busara kukubali kila kitu kinachofundishwa na mtu kwa sababu tu ameshika biblia au kwa kuwa anasema ‘Bwana Asifiwe’ Hii ni hatari sana! Si wote walio waalimu wa kweli wafundishao mafundisho ya kristo yenye uzima.
Na hii inanikumbusha mambo tuliyokuwa tunafanya tukiwa watoto wadogo (tulipokuwa hatujaokoka bado), wakati tulipokwenda kuwinda ndege kwa manati.
Wakati mwingine tulikuwa tunajikuta tumemuua ndege ambaye alikuwa na vitoto vidogo katika kiota chake. Na tukivikuta vitoto hivyo bila kujali vina UMRI GANI na vinakula CHAKULA GANI, tulivitafutia panzi au sisimizi na kuviletea vipate kula kama chakula.
Nadhani unafahamu ya kuwa ukigusa tu kiota cha ndege, vile vitoto vinadhani ni mama yao ameleta chakula, kwa hiyo kila kimoja kinafungua mdomo wake tayari kupokea chakula, Na vikipanua mdomo sisi tulikuwa tunavipa panzi au sisimizi. Na matokeo yake ni kwamba vilikuwa vinakufa!
Hivi ndivyo shetani anavyowafanya wakristo walio wengi, hasa wale waliookoka. Wengi wa wale waliookoka akija mtu kwao na kusema ‘Bwana Asifiwe’, wote wanafungua midomo ya kiroho tayari kupokea watakacholishwa na mtu huyo. Na baada ya muda unawaona wengi wao wamejitenga na imani, na hata wengine kufa kiroho! Wanapokea mafundisho kama vile vipofu.
Ndiyo maana katikati ya watu waliookoka kuna migawanyiko ya aina tatu;
  1. Kuna wale wanaofuata mafundisho ya Kristo yenye uzima; 2. Kuna wengine wanafuata mapokeo ya wanadamu katika wokovu wao; na 3. kuna wale wanaofuata mafundisho ya mashetani katika wokovu wao. Na matokeo yake ni ugomvi, migawanyiko na kunyoosheana vidole.
Na ili kuepukana na mambo haya Mtume Paulo akaandika hivi; “Msimzimishe Roho; msimtweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna” (Wathesalonike 5:19 – 22)
Wapendwa katika Kristo, na tusiwe kama makinda ya ndege, na tujaribu mambo yote kwa hekima, ili tusije tukajikuta tumekula mafundisho yenye ‘sumu’ badala ya mafundisho ya kristo yenye uzima!
Sababu na Nne:
KUNA WADANGANYIFU WALIO KATIKATI YA WAKRISTO
Soma kama ilivyoandikwa katika kitabu cha 2 Yohana 1:4-7. ya kuwa:
“Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri ya Baba. Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. Na huu ndio upendo tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.”
Sababu ya Tano:
KUNA WAJIINGIZAO KWA SIRI KATIKATI YA WAKRISTO
Inatubidi tujaribu mambo yote kwa kuwa kuna watu wanaojiingiza kwa siri katikati ya wakristo wakiwa na nia ambayo siyo nzuri kwa imani yetu.
“Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari za wokovu ambao ni wetu sisi sote, niliona imenilazimu kuwaandikia,   ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa   watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu WALIOJIINGIZA KWA SIRI, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke  yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo …. Watu hawa ni miamba   yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa; ni mawimbi ya bahariyasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele”(Yuda 1:3,4,12,13).
Maneno haya aliongozwa kuyaandika Yuda kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya “hao walioitwa, waliopendwa katika Mungu Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo” (Yuda 1:1). Ni watu gani walioitwa na Yesu Kristo na kuhifadhiwa ndani yake kama siyo sisi tunaoitwa wakristo? Kwa kuwa sisi ni wakristo maneno haya ya Yuda yanatuhusu hata hivi leo. Kwa hiyo na tujaribu mambo yote, na kuambatana na lililo jema, kwa kuwa kuna waliojiingiza kwa siri katikati yetu.
Sababu ya Sita:
KUNA MAKRISTO WA UONGO KATIKATI YA WAKRISTO.
Wakati mmoja wanafunzi wa Yesu Kristo walimuuliza Yesu juu ya kurudi kwake mara ya pili duniani. Na Yesu Kristo aliwajibu hivi:
“Angalieni, mtu asiwadanganye, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao WATAWADANGANYA WENGI ...  Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki. Kwa maana watatokea MAKRISTO WA UONGO … nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate KUWAPOTEZA, kama yamkini hata walio wateule, Tazama, nimekwisha KUWAONYA MBELE” (Mathayo 24:5, 23-25).
Angalia Yesu Kristo hakusema ‘watatokea WAKRISTO WA UONGO’ bali ‘watatokea MAKRISTO WA UONGO’. Wakristo  wa uongo na makristo wa uongo ni maneno yenye maana zinazotofautiana. Kristo wa uongo ni mtu yule ambaye anajifanya yeye ndiye kristo aliyetabiriwa kuwa atakuja mara ya pili na kumbe siye. Yesu Kristo alikwishatuonya ya kuwa watu wengi wa jinsi hii watatokea siku za mwisho na KUWADANGANYA WENGI YAMKINI HATA WALIO WATEULE.
Nakumbuka habari za mtu mmoja aliyetokea katika nchi fulani ya jirani na kujifanya yeye ndiye Kristo na kuna watu waliomfuata; ingawa watu walimfahamu historia yake! Huu uwezo wa kuwadanganya aliupata wapi?
Wengine huwa wanayatumia maneno haya ya Bwana Yesu Kristo vibaya. Utawasikia wakiwaambia watu wasiende kwenye mikutano ya hadhara ya injili kwa sababu wanasema kuwa hao ndio makristo wa uongo au manabii wa uongo aliowasema Yesu Kristo kuwa watatokea. Lakini maneno hayo si kweli, bali mbinu za ibilisi kuwazuia watu wasiende kusikiliza Injili. Kabla ya kukataa kwenda kwenye mikutano hiyo, ulizia  kwa Mungu kwanza ili uone kama inafaa kwenda au kutokwenda. Au ukienda usisahau kupima kinachohubiriwa na kinachofanyika kama ni sawa na Neno la Mungu.
Ndiyo maana tunaambiwa tujaribu mambo yote, halafu tulichukue lile lililo jema! Makristo hawa wa uongo watawafuata wale wanaomsubiri Kristo anayekuja kulichukua kanisa. Kwa hiyo na tuwe waangalifu sana, kwa kuwa wana nia ya kuwapoteza na kuwadanganya yamkini hata walio wateule.
Sababu ya Saba:
KUNA MANABII WA UONGO KATIKATI YA WAKRISTO.
Inatubidi tujaribu mambo yote, na kulichukua lile lililo jema; sababu mojawapo ya kufanya hivyo ni kwa kuwa manabii wa uongo wamejificha katikati ya wakristo. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi:
“Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali” (Mathayo 7:15)
Sehemu ambazo zimeonya juu ya manabii wa uongo ni pamoja na Mathayo 24:24 pia 1Yohana 4:1.
Sababu ya nane:
KUNA MASHAHIDI WA UONGO KATIKATI YA WAKRISTO.
Kwa kuwa kumetokea mashahidi wa uongo wa kristo ni muhimu tujaribu na kupima mambo yote, na kuwakataa wale walio mashahidi wa uongo na tuwapokee wale walio mashahidi wa kweli wa Kristo. Imeandikwa hivi:
Tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa MASHAHIDI WA UONGO WA MUNGU ……” (1 Wakorintho 15:14 – 15a).
Mtume Paulo asingesema sisi tunaosema kuwa Yesu Kristo alifufuka tunaonekana mashahidi wa uongo kama Kristo hakufufuka, ikiwa mashahidi wa uongo hawapo. Mashahidi wa kweli wapo na mashahidi wa uongo wapo. Ni kazi yetu kuwachambua na kuwafahamu ili wasiendelee kuleta vurugu katikati yetu.
Sababu ya tisa:
KUNA MITUME WA UONGO KATIKATI YA WAKRISTO.
Imeandikwa hivi: Maana watu kama hao ni MITUME WA UONGO, watendao  kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa  MALAIKA WA NURU. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao” (2Wakorintho 11:13 – 15).
Nia ya shetani ni mitume wake kujigeuza kuwa malaika wa nuru na watumishi wa haki ni ili kuwapata WANA WA NURU NA WATU WA HAKI. Kwa hiyo ni muhimu kujaribu mambo yote. Usiwe mwepesi kupokea kila kitu toka kwa watu wanaosema wametumwa na Bwana kwako. Pima kwanza! Chukua lililo jema. Acha lililo baya
Muhimu:              Wiki ijayo ya Nne katika mfululizo wa somo hili la JIHADHARI NA MAFUNUO tutajifunza juu ya “TUTAPIMA MAMBO YOTE KWA NAMNA GANI?” Kwa hiyo usikose kulisoma!


TUTAPIMA MAMBO YOTE KWA NAMNA GANI?
Mabwana afya walipoanza kampeni ya kuwaambia watu wachemshe maji kabla ya kunywa, swali walilokutana nalo mara kwa mara ni: “Kwa nini tuchemshe maji ya kunywa?” Hii ilionyesha wazi ya kuwa ingawa watu wengi walikuwa wanakufa kwa sababu ya magonjwa yanayotokana na maji machafu, hawakuona umuhimu wa kuchemsha maji. Kwa maneno mengine hili jambo lilikuwa jipya kwao, walikuwa hawajazoea kuchemsha maji kabla ya kunywa.
Jibu la mabwana afya juu ya swali hilo lilikuwa ni hili; “Ingawa maji yanaonekana ni MEUPE, hii haimaanishi ya kuwa ni SALAMA!”
Hii ni kweli kabisa, watu wengi wanadanganyika na weupe wa maji, na wanayanywa bila kuyachemsha. Matokeo yake wengi wanaugua magonjwa kama kipindupindu na kuharisha damu! Laiti wangetii ushauri wa mabwana afya, wasingeteseka namna hiyo na hayo magonjwa.
Katika wiki ya kwanza ya somo hili, tumeona sababu tisa zinazotueleza kwa nini Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kutushauri wakristo kuwa TUJARIBU AU TUPIME MAMBO YOTE.
Lakini kuzijua sababu hizo peke yake, hazitatusaidia sana kama hatuna kipimo cha kuyajaribu mambo hayo tuliyoambiwa.
Tutajaribu mambo yote kwa namna gani? Kwa wauzaji  na wanunuzi wa dhahabu, wote wana vipimo vyao vya kupimia dhahabu ili kutofautisha dhahabu ya kweli na ya uongo.
Katika maisha ya ukristo tuliyo nayo ndani ya Kristo Yesu, hatujaachwa bila kipimo cha kupimia mambo ya kiroho. Kipimo hicho ni NENO LA MUNGU tunalolipata katika biblia. Imeandikwa hivi;
“Maana Neno la Mungu LI HAI, tena LINA NGUVU, tena LINA  UKALI KULIKO UPANGA UWAO  WOTE UKATAO KUWILI, tena  LACHOMA HATA KUZIGAWANYA NAFSI NA  ROHO NA VIUNGO NA MAFUTA YALIYOMO NDANI YAKE: tena LI JEPESI KUYATAMBUA MAWAZO NA  MAKUSUDI YA MOYO. Wala HAKUNA KIUMBE KISICHOKUWA WAZI MBELE ZAKE, lakini VITU VYOTE VI UTUPU NA KUFUNULIWA MACHONI PAKE YEYE ALIYE NA MAMBO YOTE” (Waebrania 4:12,13)
“Ee Bwana, Neno lako lasimama imara mbinguni hata milele … Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa …. Hunitia hekima kuliko  adui zangu, kwa maana ninayo (ninalo) siku zote. Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, maana shuhuda zako ndizo nizifikiriazo.  Ninao UFAHAMU kuliko wazee, kwa kuwa NIMEYASHIKA MAUSI YAKO …. Kwa mausia yako najipatia ufahamu, ndiyo maana  naichukia kila njia ya uongo. Neno lako ni TAA ya miguu yangu,  na MWANGA wa njia yangu” (Zaburi 119:89, 97-100, 104, 105).
Kweli kabisa kama maneno hayo yanavyosema Neno la Mungu liko wazi sana kutuongoza namna ya kujaribu mambo yote. Katika wiki  hii tutaangalia namna ya kujaribu au kupima mambo tisa.
  1. KUZIPIMA ROHO
Neno la Mungu linatushauri hivi; “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali ZIJARIBUNI (ZIPIMENI) HIZO ROHO, kwamba zimetokana na Mungu …….” (1Yohana 4:1a)
Nakushauri usiifuate roho yoyote bila kujiuliza maswali yafuatayo:-
(a)  Je! inamtukuza Kristo? (Yohana 16:13-14; Yohana 7:18, 1Wakorintho 12:1-3)
(b)  Je! inakiri na kukubali kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu? (1Yohana 5:5, 10 –12).
(c)  Je! inanena sawa na Neno la Mungu? (Mathayo 4:6)
(d)  Je! inakiri na kukubali ya kuwa Yesu Kristo amekuja katika mwili? (1 Yohana 4: 2,6).
(e)  Je! inaleta uhuru katika roho? (2 Wakorintho 3:17; Rumi. 8:2-4; Yohana 8:36).
Kwa maneno mengine nataka kukuambia ya kuwa usikubali kuifuata roho yoyote hata kama inafanya miujiza IKIWA haimtukuzi Kristo, ikiwa haikubali kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, ikiwa haineni sawa na Neno la Mungu, ikiwa haikubali kuwa Yesu Kristo amekuja katika mwili, na pia ikiwa haileti uhuru katika roho yako.
Wakati mwingine karama ya kupambanua roho inaweza kutumika kuzipima roho za kweli na roho za uongo. Lakini ni vizuri tukumbuke ya kuwa karama hii ya kupambanua roho inatumika kama apendavyo Roho Mtakatifu (1 Wakorintho 12:4, 10-11).
  1. WAPINGA KRISTO:
Imeandikwa hivi katika kitabu cha waraka wa kwanza wa Yohana Sura ya 2:8; “Watoto, ni wakati wa mwisho; WAPINGA KRISTO WENGI WAMEKWISHA KUWAPO. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho”.
Ikiwa wapinga kristo wapo katikati yetu, tutawajuaje? Utamjuaje mtu aliye na roho ya mpinga kristo ndani yake? Soma mistari ifuatayo kwa makini:
“Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni  Kristo? HUYO NDIYE MPINGA KRISTO, yeye amkanaye  Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia” (1 Yohana 2:22-23).
“Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo  roho ya MPINGA KRISTO ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani” (1 Yohana 4:3).
Kwa mistari hii michache tunaona ya kuwa tabia ya mpinga Kristo ni:
(a)      Anakana na wala hamkiri Yesu ya kuwa ni KRISTO;
(b)      Anakana kuwepo kwa Baba na Mwana au tunaweza kusema anakataa kuwakuna Baba na Mwana kwa wakati mmoja au anakana juu ya utatu Mtakatifu.
Nadhani umewahi kuwasikia watu wakisema wao ni wakristo lakini wanasema Yesu siye Kristo au siye masihi. Tutajuaje ya kuwa Yesu tunayemwabudu ndiye Kristo? Hapo zamani Wayahudi walisumbuliwa na swali kama hili. “Basi wayahudi walimzunguka, (Yesu), wakamwambia, hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe KRISTO,  utuambie waziwazi. Yesu akawajibu, naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. KAZI HIZI NINAZOFANYA KWA JINA LA BABA YANGU NDIZO ZINAZONISHUHUDIA” (Yohana 10: 24 – 25).
Kwa maneno mengine Yesu alikuwa anasema ukiziona kazi anazozifanya kwa jina la Baba yake utafahamu kuwa yeye ndiye Kristo au la. Ni kazi gani hizi anazozifanya? Soma Luka 4:18-19 na Luka 7:18-23. Kazi hizi bado zinafanyika hadi leo kwa JINA LA YESU KRISTO!
Pia, kuna watu wengine wanaosema wao in wakristo lakini wanakana kuwa hakuna Baba ila Mwana tu, au wakati mwingine wanakana kuwepo kwa Baba na Mwana. Jihadhari na watu hawa!
Wakati mwingine wanaanza kwa kusema kuwa; “Hakuna nafsi tatu, kwa hiyo wanaosema kuna nafsi tatu (yaana Baba, Mwana, Roho Mtakatifu) ni waongo.” Sijui watu hawa huwa wanasoma Biblia ipi, kwa kuwa haya mambo yako wazi sana katika Biblia. Kwa kuwa katika somo hili sielezi juu ya nafsi tatu. Napenda tu kukupa mistari ya kutafakari inayoonyesha juu ya hizi nafsi.
Mathayo 3:16-17; “Naye YESU alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama mbingu zikamfunukia, akamwona ROHO wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake, na tazama, sauti (YA BABA)kutoka mbinguni  ikisema, huyu ni MWANANGU, mpendwa wangu ninayependezwa naye”.
Habari hii inaeleza wazi kuwepo kwa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wakati mmoja. Soma na maneno haya;
“Maana kama vile BABA alivyo na uzima NAFSINI mwake, vivyo hivyo alimpa na MWANA kuwa na uzima NAFSINI MWAKE" (Yohana 5:26)
Mstari huu unaeleza wazi juu ya BABA kama nafsi tofauti! Ukisoma mistari hii na mingine mingi unabaki unajiuliza kwa nini wakristo wengine wanakana kuwepo kwa nafsi hizi tatu.
Lakini ninaposema juu ya nafsi tatu, simaanishi kuwa kuna miungu watatu. La hasha, naomba usinielewe vibaya. Tuna MUNGU MMOJA. Lakini kuna nafsi tatu. Soma mwenyewe 1Timotheo 3:16 na Yohana 17:21,23.
Biblia inasema anayekataa kumkiri Yesu ya kuwa ni Kristo, ndiye MPINGA KRISTO. Pia, biblia inasema anayemkana Baba na Mwana, ndiye MPINGA KRISTO. Kama kuna wakristo walio na tabia ya namna hii uwe macho nao maana sasa unajua wako upande gani.
  1. WAALIMU WA UONGO:
Kinyume cha uongo ni ukweli. Kwa hiyo waalimu wa uongo ni watu wanaosema wao ni wakristo lakini wanafundisha mafundisho yaliyo kinyume na KWELI. Kumbuka KWELI ni Neno la Mungu. Yesu Kristo aliomba; “Uwatakase kwa ile KWELI; neno lako ndiyo KWELI” (Yohana 17:17). Kwa maana nyingine mwalimu wa uongo atafundisha kinyume cha Neno la Kristo – ambalo ndilo Neno la Mungu wa Kweli.
Imeandikwa hivi katika 2Petro 2:1-3; “Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako WAALIMU wa UONGO, watakaoingiza kwa werevu UZUSHI wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na  wengine watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli (njia ya wokovu) ITATUKANWA. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno YALIYOTUNGWA; wala uvunjifu wao hausinzii”.
Waalimu wa uongo utawatambuaje?
Utawatambua kwa kuangalia mafundisho wanayofundisha. Waalimu wa uongo wanafundisha:
(a)           Mafundisho au mapokeo ya kibinadamu. Soma Wakolosai 2:8, 16 – 23, Yohana 7:14 – 18; na
(b)           Mafundisho au mapokeo ya kishetani. Soma 1Timotheo 4:1 –7. Ukiona mtu anasema yeye ni mkristo na huku anafundisha mafundisho ya kibanadamu au ya kishetani, usiyapokee mafundisho hayo, ni sumu ya kiroho!
Tunatakiwa kuyapokea mafundisho ya Kristo (Wakolosai 2:8), mafudisho yenye uzima (Tito 2:1-15), na mafundisho yenye pumzi ya Mungu yaani yaliyovuviwa Roho Mtakatifu (2 Timotheo 3:16 – 17). Soma pia uone tunavyoshauriwa katika 2Timotheo 4:1-5. Uwe mwangalifu na waalimu wa uongo hata kama mafundisho yao yameambatana na miujiza. Kwani si miujiza yote inayofanywa na Mungu. Kuna miujiza mingine ni ya kishetani!
  1. WADANGANYIFU:
“Na huu ndio upendo; tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa maana WADANGANYIFU wengi wametokea duniani, WASIOKIRI ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika MWILI Huyu ndiye MDANGANYIFU na mpinga Kristo” (2 Yohana 1:6-7).
Kwa maneno mengine mistari hii inatuambia ya kuwa WADANGANYIFU waliopo katikati yetu tutawatambua tutakapowasikia wakipinga kuja kwa Yesu mara ya pili ya kwamba hatakuja katika MWILI.
Biblia inaposema “Yesu yuaja (mara ya pili) katika mwili” ina maana ya kueleza kitu gani?
Hebu soma habari hii kwa upya; “Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone, kwa kuwa roho haina MWILI na MIFUPA kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake” (Luka 24:36 – 40).
Yesu Kristo alipofufuka mwili wake haukuonekana kaburini, kwa sababu ALIFUFUKA NAO! Ndio maana alipowatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka aliwaambia, “Nishikenishikeni, mwone; kwa maana roho haina MWILI na MIFUPA kama MNAVYONIONA MIMI KUWA NAYO”. Yesu Kristo alipaa akiwa na MWILI wake na atarudi tena kutuchukua akiwa na MWILI wake. Soma Matendo ya Mitume 1:6-11.
Kwa hiyo ukiwaona watu wasiokiri au wasiokubali ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika MWILI ujue hao ni WADANGANYIFU – Jiepushe nao!
  1. WAINGIZWAO KWA SIRI:
Mtu anapojiingiza kwa siri katikati yenu, ina maana anaingia kwa kujificha asijulikane AMEKUSUDIA KUFANYA NINI. Mkisema ninyi ni wakristo, atakuja kama mkristo. Mkisema ninyi mmeokoka atakuja kama aliyeokoka. Mkisema ninyi ni wa dhehebu fulani, atakuja akisema naye ni wa dhehebu hilo hilo.
Wakati mwingine watu kama hawa wanakuwa ni wakristo au wanakuwa wameokoka; lakini KUSUDI au LENGO lililomo ndani yao kwa ajili yenu linakuwa si zuri.
Maneno ambayo Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuwaandikia Wagalatia juu ya watu wa namna hii, yanatufaa hata sisi hivi leo. Mtume Paulo aliwaambia hivi;
“Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani ….” (Wagalatia 2:4).
Mtume Paulo anaposema ‘ndugu wa uongo’ anamaanisha watu ambao kwa nje wanajifanya ni ndugu zako kiroho, lakini rohoni mwao hawana ushirika nawe wa kindugu – wanakudharau.
Lengo lao si kushirikiana pamoja kiroho, bali ni kuupeleleza uhuru wetu (wa wokovu) tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani
Biblia inasema; “ Basi ‘Bwana’ ndiye Roho walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru”. (2Wakorintho 3:17)
Nadhani umeona vikundi vingi vya watu waliookoka ambavyo havielewani na hatimaye kugawanyika. Pia, nadhani umeona mtu aliyeokoka akihama toka kikundi kimoja kwenda kikundi kingine, na kuanza kukidharau kikundi alichotoka.
Nimewahi kusikia watu fulani waliookoka wakisema wao hawawezi kusali pamoja, wala kufanya ibada pamoja kwa kuwa hawapatani.
Pia, nimewahi kuona watu waliookoka wakidharauliana na kutokuheshimiana kwa sababu ya tofauti za mapokeo ya madhehebu yao; huku kila upande ukidai kuwa mapokeo yake ni bora kuliko ya upande mwingine.
Lakini tukumbuke ya kuwa kinachomfanya mtu azaliwe mara ya pili, na kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo ni Roho wa Bwana. Na Roho wa Bwana akikuweka huru, unakuwa huru kweli kweli.
Ngoja nikuulize swali halafu tusaidiane kulijibu “Ikiwa Roho wa Bwana ametuweka huru mbali na dhambi na tofauti zetu za kidhehebu, inakuwaje basi tunajikuta tumeingia katika UTUMWA WA KUTOKUSHIRIKIANA? Kwa nini tunaruhusu ushirika wa KINAFIKI katikati yetu? Uhuru tuliopokea ndani ya Kristo tumeupeleka wapi?”
Ni wazi kwamba kuna walioingizwa kwa siri na yule adui ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika wokovu ndani ya Kristo, na wameona udhaifu wetu wa kutokulifahamu Neno la Kristo vizuri. Bila kuchelewa wametumia nafasi wanayosema “ya kutujenga kiroho” kutupa mafundisho na misimamo yao ambayo siyo ya Kristo – na kudai kuwa tuishi au tufanye kama wanavyosema.
Kinachosikitisha ni kwamba mafundisho hayo yanakutia utumwani na kukutenga mbali na waliookoka wenzako; badala ya kukuweka huru kama biblia inavyosema.
Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume 15: 1-33 utaona matatizo yanayotokea mtu akitaka kuchanganya kati ya mapokeo ya kidhehebu na uhuru wa wokovu ulio ndani ya Kristo Yesu.
Si rahisi kuwatambua watu wa namna hii kama neno la Kristo halimo kwa wingi ndani yako katika hekima yote. Lakini ukilijua neno la Kristo na kulitenda ni rahisi kutambua mtu wa jinsi hii na kumsaidia.
Ningekushauri hivi – kila kitu kiweke kinapostahili. Mapokeo ya dhehebu – weka katika dhehebu. Msimamo wa wokovu katika Kristo Yesu, weka mahali unapostahili katika maisha yako ya kila siku. Ukichanganya hivi vitu viwili utayumba sana kiroho.
Haitoshi kuisafisha nyumba na kuipamba kwa maua halafu ukasema ni safi. Usafi wa nyumba ni zaidi ya kufanya hayo – ni pamoja na kukiweka kila kitu mahali pake. JIKO likae jikoni na kadhalika – ukiliweka jiko juu ya kitanda ni uchafu hata kama nyumba imefagiliwa! – na hata kama jiko hilo ni jipya!
Kusimamia mapokeo ya dhehebu lako katika wokovu na kutaka watu wote wafuate dhehebu lako mara nyingi huleta utumwa wa kiroho na siyo uhuru.
  1. MAKRISTO WA UONGO
“Hata (Yesu) alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituini, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie,  mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu,  wakisema, Mimi ni Kristo; nao watawadanganya wengi ….” (Mathayo 24:3-5)
Nataka uone ya kuwa Yesu Kristo hasemi hao watu watakaokuja kwa jina lake, watasema, “Mimi ni ‘MKRISTO’, bali watasema ‘Mimi ni KRISTO’. Kristo maana yake ni masihi au Bwana au mpakwa mafuta wa Bwana. Kwa hiyo Yesu Kristo anataka tufahamu mapema kuwa kuna watu ambao watakuja kwetu na kudai wao ni ndio masihi wa Bwana.
Naamini ya kwamba unafahamu ya kuwa siku hizi ni siku za mwisho, na kwamba kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo kutuchukua kumekaribia. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kufahamu kwa makini ni mambo gani alisema yatatokea, tusije tukadanganywa. Yesu Kristo aliendelea kusema hivi;
“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu) …… wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo  hapa, au yuko kule, msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa  uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama,  imekwisha kuwaonya mbele. Basi, wakiwaambia, yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umemeutokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo  kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu”. (Mathayo 24:15, 23 – 27).
Katika maneno haya Bwana Yesu Kristo tunajifunza mambo mengi ya kutusaidia tunapozungumza juu ya kuwafahamu makristo wa uongo pindi watokeapo. Baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo;
(i)         Baada ya chukizo la uharibifu kusimama katika patakatifu, inaonekana wazi kuwa kutatokea mahangaiko ya kiroho na ya kimwili. Na kwa sababu hii watu wengi watatamani kumuona Kristo au Masihi ili waondokane na mahangaiko hayo.
(ii)       Wakati wa mahangaiko hayo makristo wa uongo watatokea, nao watatoa ishara kubwa na maajabu, wapate kuwapoteza, hata ikiwezekana hata walio wateule.
(iii)      Ingawa watakuja na ishara kubwa na maajabu ili wapate kutupoteza, Yesu Kristo anasema hawa watu tutawafahamu kwa kuwa sisi tunamfahamu yeye Kristo wa kweli atakavyotokea. Yesu Kristo alisema, “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, kristo yupo hapa, au yuko kule, MSISADIKI …… tazama , nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki” (Mathayo 24:23,25,26). Baada ya maneno hayo akaanza kueleza jinsi yeye atakavyokuja;
“Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa KUJA KWAKE MWANA WA ADAMU …… ndipo itakapoonekana ishara ya mwana wa Adamu MBINGUNI; ndipo mataifa yote ya ulimwengu  watakapoomboleza, nao WATAMWONA Mwana wa Adamu AKIJA JUU YA MAWINGU YA MBINGUNI pamoja na nguvu  na utukufu mwingi…… Walakini habari ya siku ile na saa ile HAKUNA AIJUAYE; hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila Baba peke yake. Kwa maana KAMA VILE ILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu…..” (Mathayo 24:27,30,36-37).
Omba kila wakati Roho Mtakatifu akukumbushe maneno haya aliyoyasema Bwana Yesu Kristo, na usiache kuyasoma na kuyatafakari, usije ukapotezwa na makristo wa uongo. Ndiyo maana Yesu alisema; Kesheni basi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakapokuja Bwana wenu” (Mathayo 24:42)
  1. MANABII WA UONGO:
Katika kitabu cha kwanza cha Wafalme sura ya ishirini na mbili tunasoma habari za manabii wawili, wote wakitabiri mbele ya Mfalme Ahabu juu ya matokeo ya Vita. Mikaya mwana wa Imla alitabiri kushindwa kwa mfalme, na Zedekia mwana wa Kenaana alitabiri kushinda kwa mfalme. Je, hapa angetambulikanaje nabii wa kweli na nabii wa uongo?
Katika Kitabu cha Yeremia sura ya ishirini na nane, Nabii Yeremia na Hanania walitabiri wote wawili kwa kutumia mfano wa nira. Je, angetambulikanaje nabii wa kweli na nabii wa uongo?
Unaposoma katika 1 Wafalme 13:18 – 22 utaona jinsi ambavyo nabii mmoja mzee wa Betheli alivyompotosha mtu wa Mungu toka Yuda kwa uongo, na mwisho wake akamalizia kwa kumpa ujumbe wa kweli. Je! ungewezaje kujua wakati aliposema maneno ya kweli na wakati aliposema maneno ya uongo?
Kwa mifano hii michache utaona jinsi ambavyo si kitu chepesi kutofautisha kati ya nabii wa kweli na nabii wa uongo. Kama walipata shida katika agano la kale, je si zaidi sana katika agano jipya hasa wakati huu wa siku za mwisho?
Ndiyo maana Mzee Yohana anatuambia hivi; “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali ZIJARIBUNI HIZO ROHO, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu MANABII WA UONGO WENGI Wametokea duniani” (1Yohana 4:1)
Unapokutana na manabii au nabii kabla ya kupokea ujumbe wake jiulize maswali yafuatayo na linganisha na maandiko katika biblia.
(a)          Je! matendo yake yana ushuhuda wa kikristo? Yesu Kristo alipokuwa anatutahadharisha juu ya manabii wa uongo alisema;
“Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda (matendo) yao. Je! watu  huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi! Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:15-23).
(b)     Je! Unabii unatimia?
“Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo  sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa. Nawe ukisema moyoni mwako, tutajuaje neno asilolinena Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope” (Kumbukumbu 18:20 – 22).
c)      Je! unabii huu unakuelekeza kwa Yesu Kristo au kwa mwingine?
“Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia, akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto….” (Kumbukumbu 13:1-3)
“Kisha (Yesu Kristo) akawaambia, hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote yaliaondikwa katika TORATI YA MUSA, na katika MANABII, na ZABURI.  Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko” (Luka 24:44,45)
(d)    Je! nabii huyo anasema neno alilopewa na Bwana au anasema mawazo yake ili kuwafurahisha wanadamu wanaomsikiliza? Soma Yeremia 23:15-19.
  1. MASHAIDI WA UONGO:
“Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu,mbona baadhi yenu   (wakristo waliokuwa Korintho) husema kwamba hakuna kiyama ya wafu! Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa MASHAHIDI WA UONGO wa Mungu, kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo; ambaye hakumfufua ikiwa wafu hawafufuliwi” (1Wakorintho 15:12 –15)
Kwa mistari hii michache iliyoandikwa na Mtume Paulo tunatambua ya kuwa mashahidi wa uongo ni watu wanaosema wao ni wakristo au wakati mwingine wanasema wameokoka huku wanakataa kuwa iko siku ya wafu kufufuliwa. Hawa watu wanaosema ni wakristo, lakini hawaamini kuwa kutakuwa na ufufuo wa wafu.
Mtume Paulo analiweka wazi jambo hili unaposema kama wafu hawafufuliwi, Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote” (1 Wakorintho 15:17-19)
Yesu Kristo alifufuka, kwa hiyo imani yetu ya kikristo si bure!
Kiyama ya wafu ipo tupende au tusipende! Kufufuliwa kwa wafu kupo, tuamini au tusiamini! Yesu Kristo alisema: “ Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa UFUNUO WA UZIMA, na wale waliotenda mabaya kwa UFUFUO WA HUKUMU” (Yohana 5:28-29). Soma pia 1Wathesalonike 4:13-17 na Ufunuo wa Yohana 20:11 – 15).
Kwa hiyo uwe mwangalifu unapokutana na watu wanaodai kwamba wao ni wakristo au wameokoka huku wanakataa juu ya kuwepo kwa ufufuo wa wafu.
  1. MITUME WA UONGO:
“Maana watu kama hao ni MITUME WA UONGO, watendao kazi kwa  hila, wanao jigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu.Maana shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao” (2Wakorintho 11: 13-15)
Ukisoma 2 Wakorintho 11:1-33 utaona ya kuwa mitume wa uongo wana tabia zifuatazo:-
(i)      Huwa ni mzigo kwa wenzao – Huwalemea;
(ii)      Wanajifanya na kusema kuwa wametumwa na Bwana, lakini ukweli ni kwamba wametumwa na shetani
(ii)      Wanatenda kazi kwa hila – yaani bila uaminifu na ukweli;
(iii)      Wanaopenda kusifiwa.
Muhimu: Wiki ijayo ya tano katika mfululizo wa somo hili la JIHADHARI NA MAFUNUO tutajifunza juu ya “HILA ZA IBILISI NDANI YA KANISA”. Kwa hiyo usikose kulisoma!


HILA ZA IBILISI NDANI YA KANISA
"Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani" (Waefeso 6:11)
"….na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake" (Mathayo 10:36)
Mtume Paulo aliwaandikia wakristo waliokuwa Efeso kuwa wanahitaji kuvaa silaha zote za Mungu ili wapate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema alikuwa anawatahadharisha nakuwaangaliza juu ya hila za shetani dhidi yao; - na kwamba bila kuvaa silaha zote za Mungu hawataweza kuzipinga hila hizo.
Yesu Kristo aliingia kwa undani zaidi juu ya jambo hili aliposema "adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake". Tukilitafsiri neno hili kikanisa, tunaweza kusema ya kuwa "adui za kanisa ni wale waliomo ndani ya kanisa".
Ni wazi kwamba si wakristo wengi wanaofahamu ya kuwa shetani ana hila zinazomfanya afanye mambo yake ndani ya kanisa au katikati ya wakristo. Kwa sababu ya hila hizi kutokutambulikana upesi na watu wa Mungu, huduma nyingi za kiroho zimevurugika.
Barua ya kusikitisha
Niliwahi kupokea barua moja ya kusikitisha kwa mkristo mmoja hapa nchini akinieleza juu ya mambo yaliyotokea katika ‘faragha’ au ‘fellowship’ yao. Kwa wale wasiofahamu ‘faragha’ au ‘fellowship’ ni mkusanyiko wa watu waliokoka kutoka madhehebu mbalimbali unaowasaidia kufahamiana na kulitafakari Neno la Mungu kwa pamoja.
Katika ‘faragha’ au ‘fellowship’ hizi watu wengi sana wamejengeka kiroho, na pia zimekuwa ni changamoto kubwa kwa madhehebu mengi ya kikristo nchini katika kuleta msukumo wa uamsho.
Katika barua hiyo, huyu mtu alisema wakati fulani alipata mapambano makali kutoka kwa ibilisi dhidi ya mimba aliyokuwa nayo, ili iharibike. Tatizo hili alimshirikisha mwenzake, ambaye baadaye alimwambia kiongozi wa ‘fellowship’ aliyeokoka. Kiongozi huyu akamchukua mganga wa kienyeji (mchawi?) aliyekuwa pia katika ‘fellowship’ hiyo akisema naye ameokoka. Wote wawili wakamwendea huyo mama ili wamsaidie – lakini badala ya kumwombea kama ilivyo desturi ya waliookoka wakasema wamekuja kumchanja chale ili akingwe dhidi ya mashambulizi ya shetani!
Yule mama alikataa kuchanjwa chale na wale ‘waliookoka’ wanzake. Walipoona amekataa, akaambiwa ya kuwa wataivuruga ndoa yake – na wakati alipokuwa akiniandikia barua hiyo alikuwa tayari amekwisha tengana na mume wake. Lakini Mungu alimlinda hata akajifungua mtoto wake salama.
Barua hiyo niliisoma kwa mshangao na masikitiko makubwa. Niliisoma kwa kuirudia mara nyingi – huku nikiugua rohoni. Maana hao watu wanaojifanya wameokoka kumbe ni wachawi ni watu ninaowafahamu kwa kusoma majina yao aliyoyaandika.
Maswali mengi yalinijia moyoni baada ya kuisoma barua hii. Je! Ni wazi ya kuwa shetani amewaweka watu wake katikati ya watu waliookoka – na waliookoka hawajui? Hawa watu waliwezaje kupata nafasi hata kuchaguliwa kuongoza ‘fellowship’ na huku wao ni wachawi na wanaojuana kuwa hawajaokoka? Shetani alipataje mwanya huu?
Hebu fikiria jambo hili mwenyewe! Hebu mfikirie huyu mama ambaye ghafula anatambua ya kuwa viongozi wake wa ‘fellowship’ ni waganga wa kienyeji. Utamsaidiaje mtu wa namna hii? Je! na wale wakristo wengine wasiojua hali ya kiroho ya viongozi wao hao wataponaje?
Si bure Yesu Kristo alisema "na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake"! Si bure Mtume Paulo alisema "Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani"!
Si ajabu basi kuona vikundi vya maombi vikivurugika, wakristo wakigombana, makanisa yakigombana na kazi ya kuhubiri injili ikipoa. Si ajabu kuona mambo haya kwa kuwa chanzo chake ni shetani, ameweka watu wake katikati ya Kanisa!
La kujiuliza ni kwamba kwa nini hali iwe hivi wakati Yesu Kristo aliahidi kulisimamisha kanisa lenye ushindi dhidi ya shetani? Lazima kuna kasoro mahali fulani katika kanisa.
Ukisoma maisha ya wakristo katika agano jipya unaona hali hii ilivyojitokeza pia.
Barua za kitabu cha Ufunuo
Yesu Kristo alimwambia Yohana akiwa katika kisiwa cha Patmo kuwa "Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo na Thiatira, na Sardi na Filadelfia na Laodikia" (Ufunuo wa Yohana 1:11).
Ndani ya barua hizi saba, kuna sehemu ambazo zinaonyesha wazi kuwa hila za shetani zilikuwa zipo ndani ya makanisa hayo, kwa mfano,
Kanisa lililokuwa Efeso, liliambiwa hivi, "Nayajua matendo yako, na taabu yako na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajabiru wale wajiitao MITUME, nao sio ukawaona kuwa WAONGO" (Ufunuo wa Yohaha 2:2). Mitume hao wa Uongo walitumiwa na baba wa Uongo-shetani.
Kanisa lililokuwa Smirna, liliambiwa hivi, "Najua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni wayahudi nao sio bali ni SINAGOGI LA SHETANI" (Ufunuo wa Yohana 2:9). Kwa lugha ya sasa tungeweza kusema " hao wasemao ya kuwa ni wakristo, nao sio, bali ni kusanyiko la shetani"!
Kanisa lililokuwa Pergamo, liliambiwa hivi " Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha shetani; nawe walishika sana jina langu wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu mwaminifu wangu aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo shetani" (Ufunuo wa Yohana 2:13)
Kanisa lililokuwa Thiatira liliambiwa hivi, "Lakini nawaambia ninyi wengine mlio Thiatira, wowote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, sitaweka juu yenu mzigo mwingine" (Ufunuo wa Yohana 2:24)
Kanisa lililokuwa Sardi liliambiwa hivi, "Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai nawe umekufa" (Ufunuo wa Yohana 3:1)
Kanisa lililokuwa Filadelfia liliambiwa hivi; "Tazama, nakupa walio wa sinagogi la shetani wasemao kwamba ni Wayahudi nao sio bali wasema uongo" (Ufunuo wa Yohana 3:9).
Kanisa lililokuwa Laodikia liliambiwa hivi, "Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto" (Ufunuo wa Yohana 3:15)
Ukizisoma barua hizi saba kwa makini utaona ya kuwa katika makanisa yote haya shetani alijitokeza ingawa ni kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:-
Katika Kanisa la Efeso, shetani alijitokeza kama MITUME WA UONGO,
Katika Kanisa la Smirna, shetani alijitokeza kama WAKRISTO WA UONGO,
Katika Kanisa la Pergamo, shetani alijitokeza kama KIONGOZI na MWALIMU WA UONGO na MLETA MAKWAZO,
Katika Kanisa laThiatira, shetani alijitokeza kama ROHO YA UZINZI,
Katika Kanisa la Sardi, shetani alijitokeza kama MKRISTO ALIYE NA MATENDO KINYUME NA UKRISTO ANAOKIRI au Mkristo aliyekufa kiroho.
Katika Kanisa la Filadelfia, shetani alijitokeza kama WAKRISTO WA UONGO,
Katika Kanisa la Laodikia, shetani alijitokeza kwa kuwafanya wakristo WAPOE KIROHO. Suala la maombi linapoa na kuhubiri injili kunapoa.
Je! mambo haya hayapo leo katika Kanisa? Kama yapo, tunafanya nini ili tuondokane nayo na kuyashinda? Je! unategemea wakristo washirikiane kwa ushindi wakati wameingiliwa na shetani namna hii?
Maonyo ya Yesu Kristo
Bwana Yesu alijua kuwa hali hii itatokea na watu wake watapata shida – kwa hiyo alitoa maonyo mapema kabisa akiwa bado hapa duniani katika mwili. Lakini inavyoonekana, ni wakristo wachache ambao wanayafuata kwa makini maonyo haya.
Yesu Kristo alisema hivi; " Jihadharini na manabii wa Uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali" (Mathayo 7:15)
Kwa maneno mengine tunaweza kusema jihadhari na watu wanaosema wao ni wakristo kumbe ni mbwa mwitu wakali; Au jihadhari na watu wasemao wao wameokoka walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
Mtume Paulo alipokuwa akiwaaga Wazee wa kanisa wa kanisa la Efeso alisema, "Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa –mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandame wao" (Matendo ya Mitume 20:29,30).
Yesu Kristo aliendelea kusema juu ya mbwa mwitu hawa na namna ya kuwatambua aliposema;
"Mtawatambua kwa matunda yao …." (Mathayo 7:16a)
Hakusema mtawatambua kwa maneno yao, wala ishara na miujiza wanayofanya, bali kwa MATUNDA YAO YA KIROHO! Kila wakati jiulize swali hili ‘Ukristo wa hao unaoshirikiana nao unazaa matunda gani?’ Yesu Kristo alisema;
"Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti! Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni. Bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu" (Mathayo 7:16-23).
Tafadhali rudia tena kuyasoma maneno hayo ya Yesu Kristo halafu linganisha na yale ya Wagalitia 5:19-23. Haya ni maonyo muhimu ambayo tunatakiwa kuyatumia kila wakati.
Matendo ya Mitume
Wenzetu kama tunavyosoma katika kitabu cha matendo ya mitume waliyafuata maonyo haya ya Bwana Yesu, na huku wakiongozwa na kushirikiana na Roho Mtakatifu walimpinga shetani alipojitokeza.
Mfano 1: Biblia inatuambia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:6 –12 habari za mtume Paulo alipokutana na "mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo! Huyu mtu alikuwa katika kundi la watu wa Mungu – alijifanya nabii kumbe ni mchawi na nia yake ni "kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile Imani". Kwa lugha nyingine alitaka liwali aache Wokovu.
Biblia inasema hivi; "Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyooka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana".
Mfano 2: "Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi kimoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia Bwana zake faida nyingi na kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya Wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile" (Matendo ya Mitume 16:16-18).
Ni wazi kwamba huyu kijakazi aliungana na wakristo katika kusali si kwa sababu alitaka kusali, bali alitaka kuvuruga maombi. Hata sasa kuna watu wengi ambao wakiingia katika vikundi vya maombi wanaleta vurugu badala ya amani. Jihadhari na watu wa jinsi hii – kemea roho ya shetani iliyo ndani yao.
Mtume Paulo akiwaandikia Wathesalonike alisema, " Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam mimi Paulo mara ya Kwanza, na mara ya Pili, na shetani AKATUZUIA" (1 Thesalonike 2:18). Ni wazi kuwa mara nyingi shetani hutumia watu ili Injili isihubiriwe. Tafadhali uwe macho na vipingamizi hivi. Bwana Yesu Kristo atakuongoza namna ya kukabiliana navyo.
Unalotakiwa kufanya
Katika kuwashauri wakristo namna ya kupambana na shetani, Biblia inatoa mashauri mengi ambayo hata wewe ukishirikiana na Roho Mtakatifu atakuongoza kuyatumia.
Dumu katika maombi. Mtume Paulo akiwatahadharisha wazee wa kanisa la Efeso juu ya mbwa-mwitu wakali alisema "Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi" (Matendo ya Mitume 20:31). Yesu Kristo alitangulia kusema; "Kesheni, Mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi lakini mwili ni dhaifu" (Mathayo 26:41). Ni wazi ya kuwa mahali ambapo maombi yamepoa ni vigumu sana kuzitambua na kuzipinga hila za shetani.
Mpingeni shetani. "Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani naye atawakimbia" (Yakobo 4:7). Unaweza ukawa unajiuliza juu ya namna ya kumpinga shetani. Mtume Paulo anatupa jibu anasema "Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani" (Efeso 6:11). Endelea kusoma Waefeso 6:11-20 uone silaha hizi zinazotajwa – zitumie zitakusaidia sana.
"Wala msimpe ibilisi nafasi" (Waefeso 4:27). Ukiwa msomaji na mtendaji wa Neno-Roho Mtakatifu atakusaidia na kukuongoza kuona mahali au mlango au nafasi katika maisha yako au kikundi chenu cha maombi au cha ibada ambayo shetani anaweza kupita. Ziba mwanya huo shetani asipite.
Uwe mtii wa Neno la Mungu. Pia muwe wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya. Soma vizuri Warumi 16:17-20. Ukiyafanya hayo biblia inasema, " Naye Mungu wa amani atamtesa shetani chini ya miguu yenu upesi".
Jifunze kutumia, Karama za Roho Mtakatifu – hasa ile ya ‘kupambanua roho’ ili uweze kujua wakati shetani inapojiinua katikati yenu. Soma 1 Korintho 12:4-11.
Muhimu: Wiki ijayo ya sita katika mfululizo wa somo hili la JIHADHARI NA MAFUNUO tutajifunza juu ya "TATIZO LA WAKRISTO NA DAWA YAKE". Kwa hiyo usikose kulisoma!
TATIZO LA WAKRISTO NA DAWA YAKE
Ninashangaa na wakati huo huo ninamshukuru Mungu kuona ya kuwa mambo yote tunayohitaji kuyafahamu hakutuficha, bali ameyaweka wazi. Katika wiki zilizotangulia tumezungumzia kwa nini tujaribu mambo yote na tuyajaribu kwa namna gani.
Kitu kinachoshangaza zaidi ni kuona ingawa mambo haya yamewekwa wazi kwetu, bado wakristo wengi wanajikuta wameingia katika mtego wa udanganyifu wa hizo roho za uongo, kutoka kwa Baba wa uongo yaani ibilisi (Yohana 8:44).
Tatizo hili linatoka wapi? Nini chanzo cha wakristo kudanganywa na roho hizi za uongo, wakati biblia imeweka wazi namna ya kuzitambua?
Tatizo la wakristo ni hili; Wakristo hawana uhusiano wa karibu na Neno la Kristo lililovuviwa Roho Mtakatifu. Tatizo hili naona limegawanyika katika sehemu mbili kubwa;
(a) Kutolifahamu Neno na uweza wa Mungu
Neno la Bwana lilitoka katika kinywa cha Nabii Hosea kusema "Watu wangu wa-naangamizwa kwa kukosa maarifa …." (Hosea 4:6a).
Katika kitabu cha Mathayo sura ya 22:29, tunamsikia Yesu Kristo akitujibu swali letu akisema;
"Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu."
Kwa mistari hii michache tunaona ya kuwa tunapotea, tunadanganywa, na kuangamizwa, kwa sababu tumekosa maarifa ya Mungu yaliyo katika Neno lake, na kwa kuwa hatuufahamu uweza wake.
Kinyume chake ni kwamba tukilifahamu Neno la Mungu tutapokea maarifa ya kiungu na kuufahamu uweza wake, na kwa ajili hiyo hatutapotea, hatutadanganywa, wala kuangamizwa na yule mwovu.
Wakristo wanapokosa mafundisho ya Neno la Mungu, madhara yake huwa makubwa. Mtu aliyeokoka akikosa mafundisho ya kumkuza kiroho, huwa anapoa kiroho na kurudi nyuma; na hata wakati mwingine kuchanganyikiwa katika wokovu, kwa sababu ya kupokea mafundisho yaliyochanganywa.
Wote tunafahamu jinsi mtu anavyokuwa na kiu ya kusikia Neno la Mungu mara baada ya kuokoka. Lakini si rahisi kupata mafundisho ya Neno la Mungu kwa kuwa watu wengi wanapenda kuhubiri na siyo kufundisha.
Katika harakati za kutafuta malisho ya Neno la Mungu, wakristo wengi wamejikuta wamepokea na kuyakubali na kuyatekeleza mafundisho bila kuyapima, na madhara yake ni mahangaiko, masononeko na ugomvi baina yao.
Mabwana afya huwa wanatushauri tuchemshe maji ya kunywa ili tusije tukaugua ugonjwa wa kipindupindu. Nakushauri unapopata mafundisho ya Neno la Mungu, kabla ya kuyatekeleza yachemshe katika Neno na Roho Mtakatifu, uone kama ni sahihi. Hii itakusaidia kutougua ugonjwa wa "kipindupindu cha kiroho", kinachopindua misimamo mingi ya watu waliookoka.
Natamani wakristo wote tungekuwa tunatafakari maandiko kama watu wa Beroya katika sinagogi la wayahudi. Biblia inasema; "Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, WAKAYACHUNGUZA MAANDIKO KILA SIKU, WAONE KWAMBA MAMBO HAYO NDIVYO YALIVYO" (Matendo ya Mitume 17:11).
Kutafakari neno unalofundishwa katika mikutano au semina za kiroho ni sawasawa na kula wali. Kuna wakati mwingine unapokula wali unatafuna jiwe. Sidhani kama utatupa wali wote, bali unatupa jiwe na unaendelea kula wali. Hata unapotafakari mafundisho ya kiroho, ukikutana, na ‘jiwe’ ndani yake; tupa ‘jiwe hilo’ endelea kula wali (Neno la Mungu)
(b)  Kutolitii Neno unalolifahamu
Yesu Kristo alisema hivi alipokuwa mlimani akiongea na wanafunzi wake;
"Na kila asikiaye hayo maneno yangu ASIYAFANYE, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa" (Mathayo 7:26-27).
Ugonjwa mbaya uliowakumba wakristo ni ugonjwa wa kutolitii Neno la Mungu. Ni kweli wanasoma na kutafakari Neno, lakini inapofika wakati wa kulitii na kufanya linachoagiza wanakwepa au wanaahirisha, huku wakisema ‘nitafanya wakati mwingine’.
Lakini ni wazi kwamba wakristo wa namna hii msingi wao wa kiroho unakuwa dhaifu, majaribu yanapowakumba wanarudi nyuma na kupoa.
Naamini unakumbuka mambo yaliyompata mfalme Sauli alipoamua kutotii alivyoagizwa na Bwana. Soma 1Samweli 15:22-28 na 1 Samweli 16:1
Ulimwengu mzima mpaka sasa unaomboleza kwa sababu ya kutotii kwa Adamu katika ile bustani ya Edeni. Soma Warumi 5:12-14
Anania na Safira walipoteza maisha yao kwa kutofanya walivyoagizwa na Roho Mtakatifu. Soma Matendo ya Mitume 5:1-11
Biblia inatuambia, tujaribu mambo yote tena tuzipime roho, lakini ni wachache wanaokumbuka kuyafanya haya maagizo. Kwa kutoyatii maagizo haya, wakristo wengi wameanguka kiroho, na Yesu Kristo anasema anguko la watu wa namna hii linakuwa kubwa.
Dawa ya Ugonjwa huu:
Ugonjwa huu uliowakumba wakristo, unaoitwa "kutokuwa na uhusiano wa karibu na Neno la Kristo", una dawa za vidonge vya aina mbili ambavyo vyote tunatakiwa kuvimeza kwa Roho Mtakatifu.
Kidonge cha Kwanza:
Hakikisha unalijaza Neno la Kristo kwa wingi ndani yako. Imeandikwa; "Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote" (Wakolosai 3:16a)
Kidonge cha Pili:
Hakikisha unakuwa mtendaji wa Neno. Yesu Kristo alisema; "Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na KUYAFANYA, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba" (Mathayo 7:24-25).
Napenda kukushauri kuwa tumia vidonge hivi siku zote katika Roho Mtakatifu na utaona ushindi wa kiroho katika maisha ya wokovu ulio ndani ya Kristo Yesu.