Monday, November 21, 2016

MAOMBI NA DUA YA KUFUNGULIWA KUTOKA UTUMWA WA KUZIMU (S. Mollel)

Maombi haya yanatoka (Isaya 1:18, Zaburi 103:12, Isaya 43:25, 41:21, 43:26  na Daniel 9:4-19, Isaya 53:5)

Baba katika jina la Yesu umesema katika Neno lako kwamba; Haya, njoni, tusemezane, dhambi zetu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Umesema pia BABA yangu kwamba; Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. BABA umemsema wewe, naam, wewe, ndiwe uyafutaye makosa yangu kwa ajili yako mwenyewe, wala hutazikumbuka dhambi zangu. Na BWANA umeniagiza kuwa nilete maneno yangu, nitoe hoja zangu zenye nguvu, umesema mfalme wa Yakobo kwamba nikukumbushe, na tuhojiane; nieleze mambo yangu, nipate kupewa haki yangu kutoka kwako.


Ninaungama kwako, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ushikaye maagano na rehema kwao wakupendao, na kuzishika amri zako; mimi na familia yangu na ukoo wangu na jamaa zangu na taifa langu tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa familia yangu, na kwa ukoo wangu, tulio katika vifungo vya ibilisi, kwa sababu ya makosa yetu tulikukosea. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, viongozi wa familia zetu, na viongozi wa ukoo wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, familia na ukoo wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, kwa sababu tumemtenda dhambi. Basi Bwana ameyavizia mabaya hayo, ukatuletea; maana Wewe Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zako zote uzitendazo; na sisi hatukuitii sauti yako.


Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha ukoo wangu na familia yangu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, ukoo wangu wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi yangu mimi mtumishi wako, na dua zangu, ukaangazishe uso wako juu ya ukoo na familia yangu palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mimi mtoto wako ninayeitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mimi na familia yangu tunaitwa kwa jina lako.



Asante BABA kwani umemtuma Kristo Yesu ambaye alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona katika jina la Yesu Kristo, AMEN!


*Samson Mollel – Uzima wa Milele International Ministries +255 767 664 338*
_www.uzimawamileleministries.blogspot.com_