Wednesday, February 11, 2015

FAHAMU UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO (BY MWL, C.MWAKASEGE)

FAHAMU UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO

(BY MWL, C.MWAKASEGE)

Utangulizi

Siku moja usiku nikiwa katika chumba cha hoteli moja hapa hapa nchini, baada ya kutoka kwenye semina ya kiroho; Roho Mtakatifu alisema ndani ya roho yangu kuwa; “Fundisha juu ya Damu ya Yesu Kristo”.

Tangu wakati huo nimekuwa na maombi ya mara kwa mara, nikiomba Roho Mtakatifu anifundishe juu ya Damu ya Yesu Kristo. Nimekuwa nikisoma na kutafakari neno la Mungu linalofundisha juu ya damu ya Yesu Kristo. Ni muda umepita sasa tangu nipate agizo hili. Ndani ya moyo wangu naona ya kuwa muda umefika wa mimi kuanza kuwashirikisha wenzangu yale ambayo tayari yamo ndani yangu ingawa ni machache, juu ya Damu ya Yesu Kristo.

Katika mfulilizo wa somo hili,tutashirikiana juu ya mambo manne tunayopata katika Damu ya Yesu Kristo. Ukweli ni kwamba katika damu ya Yesu Kristo kunapatikana zaidi ya mambo manne nitakayokushirikisha humu; lakini kwa sasa naona nianze na haya manne:-
  1. Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kuondoa dhambi. Imeandikwa katika kitabu cha 1Yohana 1:9 kuwa; “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata ATUONDOLEE dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote”.

  1. Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kupatanisha. Imeandikwa katika kitabu cha Waefeso 2:13-16 kuwa; “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amanin yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu  mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. AKAWAPATANISHA wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba”


  1. Uzima wa Milele katika Damu ya Yesu Kristo. Imeandikwa katika kitabu cha Yohana 6:53-54 kuwa; “Basi Yesu akawaambia Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili wake mwana wa Adamu nakuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao UZIMA WA MILELE…..”

  1. Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kutulinda. Imeandikwa katika kitabu cha ufunuo wa Yohana 12:11a kuwa; “Nao wakamshinda (shetani) kwa damu ya mwana-Kondoo….”

Mtihani mkubwa sana kwetu sisi wakristo ni kuyaweka katika matendo yale tunayofahamu katika Biblia. Nakushauri kwa Jina la Yesu Kristo kuwa uwe mtendaji wa neno, na usiwe msomaji tu.
Ni maombi yangu kwa Bwana ya kuwa Roho wa ufahamu wa Bwana atakuwa juu yako unaposoma na kutenda unayofundishwa katika kitabu hiki.



UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUONDOA DHAMBI
“Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake” (Zaburi 32:1).
“Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishw mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi?  Lakini katika dhabihu hizo liko KUMBUKUMBU LA DHAMBI KILA MWAKA. Maana HAIWEZEKANI damuya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi”. (Waebrania 10:1-4).
Kuna tofauti kubwa sana kiuwezo juu ya dhambi, kati ya damu ya mafahali na mbuzi ukilinganisha na Damu ya Yesu Kristo.
Biblia inatuambia wazi kabisa kuwa kuna mapungufu yaliyomo katika dhabihu ya damu ya mafahali na mbuzi. Imeandikwa hivi; “Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi” (Waebrania 10:3,4).

Katika dhabihu ya damu ya mafahali na mbuzi kuna; ‘kumbukumbu la dhambi kila mwaka’  kwa kuwa dhabihu hizi HAZIWEZI KUONDOA DHAMBI.
  Dhabihu hizi zilipokuwa zinatolewa; dhambi za taifa la Israeli zilikuwa haziondolewi, bali zilikuwa zinasitiriwa au kufunikwa.
  Kwa hiyo Kuhani Mkuu wa wakati huo wa Agano la Kale ilimbidi atoe dhabihu hizo kila mwaka ili Mungu aweze kukaa KATI YAO na wala SIYO NDANI YAO!
 Kwa maneno mwengine naweza kusema hivi, katika agano la kale Mungu aliwasamehe watu dhambi zao walipotubu LAKINI HAKUZISAHAU BALI ALIZIKUMBUKA!

Ndiyo maana ilibidi kuwekwe agano jipya, kwa kuwa agano la kale lilikuwa na upingufu (Waebrania 8:7)! Kwa sababu hiyo tunasoma ya kuwa Yesu Kristo “amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu y ahadi zilizo bora” (Waebrania 8:6).

Katika agano jipya, Mungu anawasamehe watu wanaotubu dhambi zao, wala hazikumbuki tena! Katika dhabihu ya Yesu Kristo halipo kumbukumbu la dhambi kila mwaka, kwakuwa damu ya Yesu Kristo haifuniki dhambi bali HUIFUTA au KUIONDOA DHAMBI ISIWEPO KABISA! Hebu soma maneno yafuatayo ya  biblia; “Na kila Kuhani husimama kila siku akifanya  ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi ambazo (Yesu Kristo), alipokwisha kutoa kwa  ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata  milele aliketi mkono wa kuume wa Mungu;tangu hapo akingojea hata adui wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja AMEWAKAMILISHA HATA MILELE hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye atushuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano (Jipya) ni takaloagana nao baada  ya siku ziel, anena Bwana, nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaandika; ndipo anenapo, dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi” (Waebrania 10:11 –18)

Oh! Mpendwa msomaji, ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa Roho wake akufunulie zaidi na zaidi juu yauwezo wa damu ya Yesu Kristo. Utaifahamu kweli, nayo hiyo kweli unayoifahamu juu ya damu ya Yesu Kristo itakuweka huru kabisa!

Biblia inatuambi ayakuwa kwa toleo MOJA TU! Haleluya! – ametukamilisha HATA MILELE sisi tunaotakaswa. Pia, kwa toleo moja la dhabihu ya damu ya Yesu Kristo, Mungu hakumbuki TENA KABISA dhambi na uasi tuliotubu. Kwa nini? Kwa sababu Damu ya Yesu Kristo ina uwezo wa kuondoa dhambi zilizo MIOYONI MWETU na zile zilizoandikwa katika VITABU MBINGUNI ili tuhukumiwe.
Hati za Kutushtaki

Mtu anapotubu dhambi zake na kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake; Damu ya Yesu Kristo inafuta dhambi hizo moyoni mwake, pamoja na kufuta dhambi zilizoandikwa katika vitabu vya mbinguni kwa ajili ya kutushitaki.
“Na katika Torati Karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini  mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa  dhabihu zilizo bora kuliko hizo. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia Mbinguni hasa, aonekane sasa usoni  pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani Mkuu aingiavyo  katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake;kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa  MARA MOJA TU, katika utimilifu wa nyakati amefunuliwa, AZITANGUE DHAMBI KWA DHABIHU YA NAFSI YAKE” (Waebrania 9:22-26)

Je! umewahi kujiuliza kwa nini Yesu Kristo baada ya kufufuka alimkataza Mariamu Magdalena asimguse pale kaburini – Huku baadaye akamruhusu Tomaso aitwaye Pacha amguse?

Je! Yesu Kristo alikuwa hawapendi wanawake? Je! Yesu Kristo alikuwa na kinyongo na Mariamu Magdalena? La hasha – si hivyo! Yesu Kristo alipomkataza Mariamu Magdalena asimguse, alikuwa njiani kwenda kwa Baba – Patakatifu pa Mbinguni, kama Kuhani Mkuu aliyebeba damu yake mwenyewe ili tupate ondoleo la dhambi mbkele ya Mungu na kutupatanisha naye.

Ndiyo maana Yesu Kristo alimwambia Mariamu Magdalena “Usinishike kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni baba Yenu.., kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu” (Yohana 20:17).

Yesu Kristo aliingia patakatifu kwa ajili yetu kwa damu yake mwenyewe baada ya kupata ushindi mkuu dhidi ya shetani na majeshi yake. Hebu tusome maneno yafuatayo;“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa  mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiishakuifuta  ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa  hukumu zake, iliyokuwa na auadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,akaigongomea msalabani isiwepo tena, akaigongome msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”  (Wakolosai 2:13-15).
Katika tafsiri ya Kiswahili cha kisasa maneno hayo yanaeleweka vizuri zaidi kwani yanasomeka hivi; “Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi Uzima pamoja na Kristo MUNGU AMETUSAMEHE DHAMBI YA DENI ILIYOKUWA INATUKABILI NA MASHARTI YAKE, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. Huko Kristo ALIWAPOKONYA NGUVU ZAO HAO PEPO WATAWALA NA WAKUU; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwa-buruta kama mateka katika msafara wa ushindi wake” (Wakolosai 2:13-15)

Mungu Baba alipoiona damu ya Kristo imeletwa mbele yake kwa ajili yetu, ALITUSAMEHE DHAMBI TULIZOMFANYIA, AKATUMIA HIYO DAMU KUFUTA DHAMBI HIZO KATIKA VITABU AU HATI ZILIZOANDIKWA ILIKUTUSHITAKI – NA BAADA YAKUZIFUTA DHAMBI HAZIKUMBUKI TENA!

Kama nilivyokuoambia hapo mwanzoni katika agano jipya Mungu anasamehe dhambi na kuzisahau – wala hazikumbuki tena (Isaya 43:25; Waebrania 10:17

Ikiwa umetubu dhambi zako – Mungu amekusamehe na wala hazikumbuki tena kabisa. Kwa kuwa Mungu hazikumbuki dhambi zako tena kabisa, kwa nini wewe unazikumbuka na hata wakati mwingine unamkumbusha Mungu?

Ukizikumbuka dhambi ulizokwishatubu na kusamehewa utajisikia kuhukumiwa rohoni mwako. Na ukijisikia kuhukumiwa moyoni unakosa ujasiri wa kufanya maombi na huduma zingine ulizopewa na Bwana mwisho wake ni kupoa kiroho na kurudi nyuma.
Imeandikwa hivi; “Wapenzi mioyo yetu isipotuhukumu tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (1Yohana 3:21).

Ujasiri wa kupaingia Patakatifu
Kutokufahamu na kutokuamini juu ya uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kuondoa dhambi, kumewanya wakristo wengi waishi maisha yaliyo duni sana kiroho, kimwili na kiakili.

Ili Mtume Paulo aweze kutumika vizuri katika ule wito alioitiwa na Bwana, ilimbidi ASAHAU KWANZA dhambi alizofanya na kutubu. Mtume Paulo alisema hivi;
“Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; NIKISAHAU YALIYO NYUMA, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza  mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya  mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 3:13,14).Ni mambo gani ya nyuma ambayo Paulo anasema anayasahau kabla ya kuchuchumilia yaliyo mbele?

Kwa msomaji wa Biblia ni rahisi kukumbuka jinsi ambavyo Mtume Paulo, wakati huo akiitwa Sauli, alivyowatesa Wakristo na hata kushiriki katika Kifo cha Stefano. Lakini kwa rehema za Mungu Paulo alitubu na kusamehewa, na wala Mungu hakumbuki tena kama Paulo aliwahi kushiriki katika mambo hayo.

Unadhani Mtume Paulo angekuwa bado anasumbuliwa moyoni mwake na matendo hayo aliyoyafanya kabla ya kutubu angeweza kumtumikia Mungu vizuri? Ukweli ni kwamba angekwama na kudumaa kihuduma. Ndiyo maana anasema “…ila natenda neno moja tu; NIKIYASAHAU YALIYO NYUMA nikiyachuchumilia yaliyo mbele….”.

Je! Unakumbuka baadhi ya maneno aliyomwandikia Timotheo juu ya kuushinda mtihani huu? Kama unakumbuka ni vizuri. Bali kama hukumbuki naomba tusome pamoja 1Timotheo 1:12-16). Imeandikwa hivi:-
“Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake,  ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji  mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri; lakini  nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja  ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote niwe kielelezo kwa wale watakaomwamin baadaye, wapate Uzima wa Milele”.
Ni wazi kwamba Mtume Paulo alifanya mambo makubwa mawili kabla ya kusonga mbele kwenye wito wake, ambayo tunahitaji kujifunza kutoka kwake ili na sisi tusonge mbele katika kazi ya Bwana na katika ukristo wetu.

Baada ya kujua ya kuwa amesamehewa na Mungu, Mtume Paulo alifanya mambo haya mawili (1) Mtume Paulo alijisamehe makosa aliyofanya; na pia (2) Aliyasahau yaliyo nyuma.
               
Nakumbuka nilikwenda wilaya fulani na nilikuwa nazunguka katika vikundi na makanisa mbalimbali kuhubiri na kufundisha neno la Mungu; Kuna mtu mmoja ambaye alijitokeza kutubu kila nilipoita watu waliokuwa wanahitaji kutubu.
Mtu huyo alipojitokeza tena mahali pengine Kabla ya kumwombea, niliamua kumuuliza shida yake.“Je! Ni kosa gani ulilolifanya linalokufanya utubu kila wakati?” Nikamuuliza
               
Akajibu akaniambia, “Nilianguka katika dhambi ya uasherati, naomba uniombee Mungu anisamehe”.
               
Nikamuuliza tena “Je! ulipoanguka katika dhambi hiyo ulitubu?”
               
Akasema; “Ndiyo – tena si mara moja bali mara nyingi, na naendelea kutubu; kwa hiyo naomba uniombee na wewe kwani nataka kwenda mbinguni”.
               
Baada ya kuzungumza naye kwa muda, pia alinieleza ya kuwa imembidi aache hata kufanya kazi ya Mungu mpaka tatizo hilo liishe, kwani anajisikia kuhukumiwa moyoni anaposimama mbele za watu kuhubiri, kufundisha au kuimbisha nyimbo.
               
Kwa kuyaangalia maandiko nilifahamu ya kuwa huyo Mkristo alikuwa na matatizo matatu makubwa; (1) Haamini kuwa Mungu anasikia maombi yake; (2) Haamini kuwa alipoomba msamaha mara tu baada ya kutenda dhambi Mungu alimsamehe na kusahau;(3) Ameshindwa kujisamehe mwenyewe baada ya kutubu, kwa hiyo moyo wake unamhukumu, na kwa ajili hiyo amekosa ujasiri wa kusimama na kuhudumu mbele za Mungu.
                Ndipo nilipompa mistari ya Biblia ya kutafakari na baadhi ya mistari hiyo ambayo nataka na wewe uitafakari ni hii ifuatayo:-
“Mimi, naam, mimi, ndimi niiyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala  sitazikumbuka dhambi zako” (Isaya 43:25)
“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na  kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).
“Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake,  kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (1Yohana 3:21,22).
“Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia Patakatifu kwa DAMU YA YESU…” (Waebrania 10:19)
“Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupate rehema, na kupata neema ya kutusaidia  wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:16).
“Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia,  tuombacho chote, twajua kwamba atusikia tunazo  haja tulizomwomba” (1Yohana 5:14,15).
               
Ujasiri wa kusimama mbele za Mungu katika maombi na katika kumtumikia tunaupata katika imani tuliyonayo juu ya uwezo wa Damu ya Yesu Kristo kuondoa dhambi.
Baada ya miezi michache kupita huyo mtu aliyekuwa na shida alivyosaidika na mistari hiyo; na jinsi anavyosonga mbele vizuri katika wokovu na katika kumtumikia Mungu.
               
Fahamu na amini kuwa Damu ya Yesu Kristo ni ufunguo wa kwenda mbele za Mungu na kukubaliwa naye. Damu ya Yesu Kristo inakukaribisha mbele za Mungu ili uongee naye, huku ukimkumbusha ahadi alizokuahidi ndani ya Kristo.

 

UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUTUPATANISHA

Mzee Yohana alipokuwa akituandikia waraka wake wa kwanza sura ya tatu mstari wa nne, alisema; Kila atendaye dhambi, afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi”.
Dhambi ilipoingia ndani ya moyo wa mwanadamu ilileta mafarakano kati ya Mungu na mwanadamu. Uhusiano uliokuwapo hapo mwanzo mtu alipoumbwa ulitoweka; na sura ya Mungu ndani ya mtu ikaondoka, badala ya mwanadamu kuishi katika baraka alijikuta amejiingiza katika maisha ya laana.

Usiwasingizie jirani zako, au wazazi wako, au watoto wako; au ndugu zako, au shida uliyonayo ya kuwa ndivyo vinakufanya utengwe na baraka za Mungu. Fahamu ya kuwa dhambi iliyo ndani yako ndiyo iliyoleta mafarakano kati yako na Mungu, dhambi hiyo inafanya hata maombi yako yasijibiwe. “Tazama mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa; wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarakisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone hata hataki kusikia” (Isaya 59:1,2)
Habari njema iliyomo katika injili ni kwamba Yesu Kristo ndiye MPATANISHI PEKEE kati yetu na Mungu. Imeandikwa hivi;
“Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu  Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata  kujua yaliyo kweli.  Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi  kati ya Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati  ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu” ambaye alijitoa mwenyewe kuwa  ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa  kwa majira yake” (1Timotheo 2:3-6).

Ikiwa Mungu anaona ni ZURI na KUKUBALIKA MBELE ZAKE watu wote waokolewe, kwa nini watu wengine wanapinga na kuuchukia wokovu mkuu namna hii ulio ndani ya Yesu Kristo?
               
Kwa nini hawataki kuiamini na kuipokea injili yenye uwezo wa kuokoa? (Warumi 1:16).Mtume Paulo anatupa jibu anaposema, “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao Mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasiamini (wasiookoka), isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu” (2 Wakorintho 4:3,4).
               
Jambo ambalo Ibilisi hataki watu waone, ni uwezo wa damu ya Yesu Kristo kama sadaka ya kuwapatanisha kati yao na Mungu. Shetani hataki watu wafahamu ya kuwa milango ya gereza la dhambi, ugonjwa, mauti, ugomvi na umaskini imefunguliwa – wasije wakatoka wakamwacha peke yake.
               
Shetani amewadanganya watu wengi, yamkini hata waliookoka, kuwa watakubalika mbele za Mungu kwa kushi matendo mazuri peke yake bila kujali umuhimu wa Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yao.
               
Ndiyo maana madhehebu mengi ya Kikristo na yale yasiyo ya Kikristo yamewafundisha waumini wake kuwa wakifuata na kutimiza masharti fulani waliojiwekea, Mungu atawasamehe na kuwakubali.

Ndiyo maana utawasikia kundi fulani la waliookoka wakiwashutumu kundi lingine la waliookoka kuwa hawajaokoka sawasawa kwa kuwa hawajafanya kitu fulani – sijui huwa wanasoma Biblia ipi;
Naamini Biblia unayosoma ni sawa na ninayoisoma mimi wakati huu nayo inaniambia hivi;“Kwa maana mmekombolewa kwa neema, kwa  njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi  zenu ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo  mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8,9).
“….hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi  haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe  haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana  kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure” (Wagalatia 2:16,21).
               
Ni kweli kabisa ikiwa wokovu unapatikana kwa njia ya mtu kujitahidi kutimiza sheria fulani, au utaratibu wa dhehebu fulani, basi Kristo wetu alikufa bure, na damu yake ya thamani ilimwagika bure!
               
Lakini nataka nikukumbushe ya kuwa, Yesu Kristo hakufa bure, wala damu yake haikumwagika bure!
               
Kwa nini? “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi bali kwetu sisi tunaookolewa ni NGUVU YA MUNGU” (1Wakorintho 1:180.
               
Hakuna sababu ya kuendelea kukaa ndani ya jela ya dhambi, magonjwa shida, mauti huzuni na umaskini.
               
Karibu kila mwaka tunasikia viongozi wa nchi mbalimbali wakitangaza msamaha kwa wafungwa kadhaa kwa ajili ya kusherehekea sikukuu zao.
               
Nadhani tutashangaa sana kama bado tutasikia kuwa wafungwa hao wameng’ang’ania kukaa gerezani hata baada ya msamaha kutangazwa, na milango ya gereza kufunguliwa.
               
Mungu wetu ametutangazia msamaha ndani ya Kristo, tunatakiwa kuupokea, na kuwaeleza watu wengine upatanisho huu ulio katika damu ya Yesu Kristo. Hii ndiyo Injili ya kweli – kuwatangazia watu msamaha wa dhambi na ushindi dhidi ya dhambi unaopatikana ndani ya Kristo Yesu.
               
Wakristo wanahitaji kujua ya kuwa baada ya kupatanishwa na Mungu katika Kristo, shetani hana mamlaka tena ya kuweka dhambi, magonjwa, huzuni, faraka, na umaskini juu yao. Shetani hana mamlaka tena juu ya yule aliyepatanishwa na Mungu katika damu ya Yesu Kristo.
               
Kwa nini? Kwa sababu Mungu mwenyewe, “alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye (Kristo) tuna ukombozi, Yaani msamaha wa dhambi” (Wakolosai 1:13,14).
               
Unapotakaswa na Damu ya Yesu Kristo, unawekwa huru mbali na dhambi na hukumu yake – tena unakuwa huru kweli kweli.
               
Kwa Damu ya Yesu Kristo unaweza ukasimama na kuomba mbele za Mungu bila hofu. Imeandikwa hivi; “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu; ….”(Waebrania 10:19)
               
Kwa Damu ya Yesu Kristo unaweza ukasimama mbele ya shetani na majaribu yake bila hofu – kwa kuwa hana kitu anachokudai wala cha kukushitaki mbele ya Mungu. Bwana Yesu Kristo amekwisha kukulipia deni lako! Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo  amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita  tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na  nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma  ya upatanisho” (2 Wakorintho 5:17,180.
               
Ewe Mkristo, Usikubali dhamiri yako ikuhukumu kwa kosa ulilokwisha litubia, na kufutwa na damu ya Yesu Kristo. Pokea msamaha na upatanisho kwa imani ndani ya Kristo kama yanenavyo maandiko. Songa mbele katika ahadi na utumishi wa Bwana. Usichoke wala kuona aibu kuwaeleza watu wengine habari hii njema ya kuwa Mungu amewasamehe dhambi zao katika Kristo, - wampokee Yesu Kristo mioyoni mwao kama Bwana na Mwokozi wao.
               
Ulimwengu mzima na kila mtu akaaye ndani yake anapaswa kujua ya kuwa “MUNGU ALIKUWA NDANI YA KRISTO, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” (2Wakorintho 5:19).

 

UPATANISHO KATI YA MTU NA MTU

Nakumbuka mtu mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri juu ya tatizo lililokuwa linamkabili, akasema; “ Kuna mtu ambaye tulikwaruzana na kugombana na mimi nimemsamehe; lakini tatizo nililonalo ni kwamba naona hanisemeshi wala hanisalimii. Mimi nikimsalimia haitiki. Naona kuna uzito fulani unaokwamisha uhusiano wetu na mimi sijui nifanye nini – kwa kuwa si vizuri tuishi namna hii”.
               
Mara kwa mara nimekutana na watu wenye matatizo yanayofanana ya shida ya mtu huyu niliyokueleza. Wengine hawaelewani na wenzao kazini. Wengine hawaelewani na ndugu zao. Wengine hawaelewani katika ndoa zao. Mume na mke hawazungumzi, ingawa wakati mwingine wanaishi chumba kimoja.
               
Swali kubwa nililokuwa nalipata katika maelezo yao ni – wafanyeje ili wapatane tena na hao waliogombana nao? Swali hili naamini lilikuwa linawasumbua kwa sababu wanafahamu imeandikwa kuwa; “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao, mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengine wakatiwa unajisi kwa hilo” (Waebrania 12:14,15).
               
Baada ya kukabiliwa na swali hili mara kwa mara; sikuchoka kumwomba Mungu ili anipe jibu sahihi la kuwapa watu hao, ili WAPATANE UPYA na hao ambao hawaelewani nao.
               
Ndipo Roho Mtakatifu akaniongoza kusoma mistari ifuatayo kwa upya;“Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa  mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa DAMU  YAKE KRISTO. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja;  akakibomoa kiambaza cha kati KILICHOTUTENGA.  Naye  akiisha kuuondoa ule UADUI KWA MWILI WAKE;  ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa MTU MPYA MMOJA  ndani ya nafsi yake; akafanya AMANI.  AKAWAPATANISHA WOTE WAWILI NA Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya MSALABA,  AKIISHA KUUFISHA ULE UADUI KWA HUO MSALABA”  (Waefeso 2:12-17).
               
Baada ya kusoma na kuyatafakari maneno haya nilijua hakika ya kuwa Roho Mtakatifu ananionyesha ya kuwa kuna UWEZO KATIKA DAMU YA YESU KRISTO kuwapatanisha watu wawili ambao hawaelewani.
               
Niliamini hivyo; na bado naamini hivyo na nitaendelea kuamini hivyo kuwa kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo – kuwapatanisha watu wawili waliogombana, na kuuondoa uadui uliokuwa katikati yao ukiwatenganisha. Nadhani sitakosea nikisema na wewe unaamini hivyo – Je! ni kweli?
               
Ingawa niliamini katika uwezo wa damu ya Yesu Kristo katika kuwapatanisha watu wawili waliogombana – bado nilikuwa nimekabiliwa na swali moja kubwa.
               
Swali hilo nililojiuliza ni hili; “ Nitawezaje kuichukua damu ya Yesu Kristo toka mbele ya kiti cha enzi ilipowekwa na Yesu Kristo mwenyewe miaka karibu 2,000 iliyopita – niichukue ili inisaidie kuondoa ugomvi uliopo kati yangu na mtu mwingine na hatimaye kutupatanisha?”
               
Hili swali halikuwa jepesi – kwa hiyo nilianza tena kumwomba Mungu ili anifafanulie na kunifundisha juu ya jambo hili.
               
Roho Mtakatifu akanikumbusha tena mistari ifuatayo;“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo  amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia  vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha nafsi  yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya  Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu NENO LA UPATANISHO! Basi tu wajumbe  kwa ajili ya Kristo, kana kwamba MUNGU ANASIHI KWA VINYWA VYETU; twawaomba ninyi kwa ajili  ya Kristo mpatanishwe na Mungu”  (2Wakorintho 5:17-20).

Kwa kuniongoza kusoma na kutafakari maneno haya, Roho Mtakatifu alitaka nifahamu ya kuwa;
(a)      Mtu aliye ndani ya Kristo (aliyeokoka), Mungu mwenye uwezo wa kupatanisha anakaa ndani yake, naye amempa HUDUMA YA UPATANISHO na NENO LA UPATANISHO.
(b)     Ugomvi kati ya mtu na mtu umeletwa na UASI na upatanisho unaletwa na UTII – kutii maagizo ya Mungu.
Ndipo Roho Mtakatifu aliponikumbusha Marko11:22,23, nayo inasema hivi; “Yesu akajibu, akamwambia, Mwamini Mungu. Amin, nawaambia, Yeyote atakayeuambia mlima huu ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.”
Kwa kuniongoza kusoma na kutafakari maneno haya Roho Mtakatifu alitaka nifahamu ya kuwa NATAKIWA KUSEMA KILE NINACHOKIAMINI WALA NISIONE SHAKA MOYONI MWANGU, BALI NIAMINI KWAMBA KILE NIKISEMACHO KIMETUKIA  NACHO KITAKUWA CHANGU!

Naamini kitu gani? Kumbuka nilikuambia naamini kuwa kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo kupatanisha watu wawili wasiopatana au waliogombana.
Kwa hiyo nikiona uzito fulani unaingia kati yangu na mtu mwingine na hata kusababisha kutoelewana, NILISEMA NINACHOKIAMINI JUU YA DAMU YA YESU KRISTO.

Huwa nasema maneno haya; “ Katika jina la Yesu Kristo nanyunyiza damu ya Yesu Kristo juu ya Uadui na Kiambaza kinachotufanya tusielewane mimi na – (nataja jina la mtu huyo). Uadui na ugomvi uondoke kwa damu ya Yesu Kristo, tupatane na tuwe na Amani na maelewano – Amina”.
Halafu baada ya kusema hivyo, naamini kuwa hayo niliyoyasema yametukia, nayo yamekuwa yangu – yaani uadui haupo tena, bali tumepatanishwa na Damu ya Yesu Kristo.

Nataka nikuambie, namshukuru sana Mungu kwa kunifundisha hili, kwa kuwa nimepata msaada mkubwa wa kutatua matatizo yangu na ya wengine pia.

Mama mmoja aliwahi kuja kuomba ili tusaidiane kuomba kwa kuwa alikuwa amefukuzwa toka nyumbani kwake na mume wake, bila nguo za kubadili wala fedha. Mpaka wakati huo tulipokuwa tukiongea alikuwa anakaa kwa jirani.

Katika mazungumzo tuliyokuwa nayo na yule mama nilifahamu kuwa alikuwa hajaokoka – yaani hayuko ndani ya Yesu Kristo. Nikamshauri nikasema; ‘Mama, ukimpokea Yesu Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, Yeye ni kazi yake kutua mizigo ya uliolemewa nayo ili akupumzishe. Na Yeye ukimpa maisha yako atakusaidia kuondoa tatizo lako’.
Huyu mama alikubali ushauri huo, kwa hiyo nikamwongoza  kusema sala ya toba na ya kumpokea Yesu Kristo moyoni mwake.

Nikamuuliza; “Unataka tuombe nini juu ya tatizo lako?”
Yule mama alinieleza mambo mengi aliyotaka aombewe, na mojawapo ya hayo ni kwamba uadui uliopo kati yake na mume wake uondoke, waishi kwa amani, pia amwite arudi nyumbani bila masharti.

Baada ya kusema mahitaji hayo tukaanza kuomba. Kati ya maneno niliyosema katika sala ile ni haya “Katika jina la Yesu Kristo nauondoa uadui uliopo kati ya mama huyu na mume wake – uondoke kwa damu ya Yesu Kristo , wapatane na kuwa na amani. Mume wake asipate amani moyoni mwake mpaka amrudishe mke wake nyumbani bila masharti …..” Halafu nikaamini kuwa hayo niliyosema yametukia nayo ni yangu. Tukaagana na mama huyo baada ya maombi hayo.Kesho yake nililetewa ushuhuda ya kuwa mume wa yule mama alimrudisha mke wake siku ile ile baada ya maombi hayo.

Damu ya Yesu Kristo ibarikiwe! Jina la Yesu Kristo libarikiwe! Nataka usikate tamaa unapokosa maelewano na mtu, kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo wa kukupatanisha naye.

Kabla ya kuchapa mafundisho haya ya Damu ya Yesu Kristo katika kitabu, nilikuwa kwanza nimeyasambaza kwa watu wachache kwa njia ya jarida. Baada ya muda nilipata barua ifuatayo toka kwa mtu mmoja aliyekuwa amesoma mafundisho hayo:

“Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya upendo uliomo ndani yako katika kuzihudumia roho za watu wake ambao wanaangamia kwa kukosa MAARIFA.

Ninamshukuru Mungu mwenye uweza wote, katika jina la Yesu Kristo kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu, jinsi alivyokuamsha kuweza kuniletea masomo kwa wakati unaohitajika sana kwangu – MUNGU AKUBARIKI SANA.

Nakala ya somo la FAHAMU UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO nililipata. Kwa kweli baada ya kuisoma hiyo nakala, kukatokea upingamizi mkubwa sana katika ulimwengu wa roho kiasi kwamba ni wiki mbili sasa sijapata usingizi vizuri. Nafahamu ni kwa sababu ya kujua UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO – Hasa katika UPATANISHO KATI YA MWANADAMU NA MWANADAMU na pia katika ULINZI NA KINGA. Hivyo nikasoma kwa uangalifu sana na kuweka katika matendo niliyoyasema. Jambo la kushangaza ni kuwa jirani yangu ambaye alikuwa haongei nami baada ya kuomba toba kwa ajili yake na kunyunzia damu ya Yesu katika ukuta unaoleta adui sasa tunaongea vizuri. Na pia nguvu za kichawi ambazo zinaelekea zilikuwa zinazunguka sana nyumba yangu ziliweza kujidhihirisha wazi usiku kwa kuzungumza dhahiri huko nje ya nyumba kwenye saa 9:30 usiku wakati ninapoamka ili kufanya maombi ya usiku wa manane; sasa zimetoweka kabisa…

Pia nilikuwa kwa muda wa miezi mingi kiasi cha nusu mwaka nilikuwa nashindwa kuamka usiku wa manane ili kufanya maombi kama ilivyokuwa kawaida yangu siku za nyuma, maana usingizi ulinizonga kiasi cha kukosa kuzinduka usiku, lakini la KUMSHUKURU MUNGU ni kuwa baada ya kumkemea shetani na kuifunga roho ya usingizi na kunyunyizia DAMU YA YESU kwa ajili ya ULINZI NA KINGA, sasa naamka usiku wa manane na kufanya maombi mpaka saa 11:30 asubuhi. JINA LA BWANA LIBARIKIWE SANA.” 

UZIMA WA MILELE KATIKA DAMU YA YESU KRISTO

“Basi Yesu akawaambia, Amini, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kunywa damu yake, hamna Uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao UZIMA WA MILELE; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli; na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa  mimi” (Yohana 6:53-57).
Mtu ambaye ameula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake ile iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye anakaa ndani ya Yesu Kristo, na Yesu Kristo anakaa ndani yake. Kwa maneno mengine amepokea uzima wa Mungu, ambao ni uzima wa milele.
Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako unapokea uzima wa milele; kwa kuwa, “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yohana 1:4).
Inatupasa tukumbuke ya kuwa, kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.
Pia, inatupasa tukumbuke ya kuwa, “ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika UZIMA kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).
Dhambi inapoingia mahali inaleta mauti, magonjwa, uasi, ubishi, umaskini na kutokufanikiwa. Uzima wa milele unapoingia ndani ya mtu unaleta, - Uzima, uponyaji, amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu.

UZIMA WA MILELE NA UPONYAJI

Kabla sijampokea Yesu Kristo moyoni mwangu awe Bwana na Mwokozi wangu, nilisumbuliwa sana na magonjwa.
Nakumbuka nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara. Nilipokwenda kupimwa hospitali kwa daktari, niliambiwa nina ugonjwa wa vidonda vya tumbo ‘Ulcers’ na pia ‘High blood pressure’.
Nilipewa dawa za kutumia, na pia niliambiwa nisile vyakula vya aina fulani maana vitaniongezea ugonjwa.
Niliyafuata masharti ya daktari, na nilipata nafuu kidogo. Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba mara kwa mara magonjwa yalinirudia na kunisumbua sana – sikujua kitu cha kufanya. Baada ya miaka kadha neema ya Bwana ilifuniliwa moyoni mwangu, nikaokoka baada ya kutubu na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wangu. Mabadiliko yaliyotokea katika maisha yangu ni makubwa mno. Wakati huo nilikuwa sijajua ni kitu gani kimetokea – lakini nilijua kuwa ninaishi maisha mapya.
Nilishangaa kuona kuwa miezi kadhaa imepita bila kusumbuliwa na magonjwa. Kichwa hakikiniuma tena, moyo uliacha kwenda mbio tena vyakula vingine nilivyokatazwa nisile na daktari havikunidhuru nilipovila tena kama mwanzo. Nilijua hakika kuwa nimepona!
Wakati huo sikuweza kufahamu kitu kilichotokea hata nikapona mara moja namna hiyo. Lakini kwa kadri ambavyo Roho Mtakatifu alivyoendelea kunikuza katika wokovu nilikuja kufahamu ya kuwa MSAMAHA WA DHAMBI UNAONGOZANA NA UPONYAJI WA MWILI.
Kabla ya mwanadamu kutenda dhambi, hakukuwa na magonjwa. Dhambi ilipoingia ilileta na magonjwa pia. Sadaka ya uhai wa Yesu Kristo msalabani ilileta msamaha na ondoleo la dhambi na madhara yake yote ikiwa ni pamoja na MAGONJWA.
Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, unampokea MPONYAJI. Roho wa Uzima wa milele anayeingia kutawala maisha yako, ni Roho wa Uponyaji anayefukuza magonjwa yote ndani yako na kukupa afya.
Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea (Yesu Kristo) wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na KUYACHUKUA MAGONJWA YETU” (Mathayo 8:16,17). Soma pia (Isaya 53:4,5)
Kwa kuwa alichukua dhambi zetu, dhambi hizo zimeondolewa kwetu, na tumepokea utakatifu wake. Kwa kuwa alichukua magonjwa yetu, hakuna sababu ya sisi kuendelea kuumwa kwa kuwa tumepokea uponyaji wake. Ndiyo maana imeandikwa hivi;
“Yeye mwenyewe (Yesu Kristo) alizichukua dhambi  zetu katika mwili wake juu ya mti; ili tukiwa wafu kwa  mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na   KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA” (1Petro 2:24).
Angalieni anasema, “ Kwa kupigwa kwake MLIPONYWA” na siyo ‘MTAPONYWA’. Ikiwa TULIPONYWA kwa hiyo sasa TUMEPONA!
Ndiyo maana watu wengi sana nimewasikia wakishuhudia ya kuwa magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua kwa muda mrefu yamepona baada ya kumpokea Yesu Kristo mioyoni mwao na kuokoka.
Kuna mama mmoja alinishuhudia ya kuwa alisumbuliwa sana na majini kwa muda wa miaka kumi na mitatu. Alikwenda hospitali – hakupona. Alikwenda kwa waganga wa kienyeji – hakupona. Mwili wake ulidhoofu sana.
Siku moja neema ya Mungu ilimzukia aliamua kuokoka. Mhubiri aliposema watu wanaotaka kuokoka waje mbele, huyo mama naye alikwenda – akafanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu Kristo moyoni mwake.
Mama huyo alinambia tangu wakati huo maumivu aliyokuwa nayo mwilini kwa miaka 13 yaliondoka. Mume wake na ndugu zake walishangaa sana. Tangu wakati huo aliookoka na kupona hadi alipokuwa ananisimulia ilikuwa imepita miaka minne, na bado alikuwa amepona na afya njema.
Kama wewe unayesoma haya unaumwa na hujaokoka, nakushauri utubu dhambi zako na umpokee Yesu Kristo moyoni mwako, na DAMU YAKE itakutakasa, na utapokea uponyaji unaouhitaji sasa. Kwa sababu imeandikwa, “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote” (Zaburi 103:3).
UZIMA WA MILELE NA MABADILIKO YA TABIA:
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa  mapya” (2Wakorintho 5:17)
 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;  ambaye katika yeye tuna ukombozi yaani, msamaha wa dhambi”.(Wakolosai 1:13,14).
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na ukiinywa damu yake yeye anakaa ndani yako na wewe unakaa ndani yake – unapokea uzima wake au uzima wa milele.
Mtu akiwa ndani ya Kristo, anakuwa mtu mpya. Mtu anapokuwa ndani ya Kristo anabadilika tabia yake kwa kuwa amehamishwa toka katika nguvu za giza na tabia yake na kuingia katika ufalme wa Kristo na tabia ya Kikristo.
Mtu akiwa ndani ya Kristo anavua utu wake wa kale na kuvaa utu mpya – anavaa tabia mpya.
Wakati fulani nilikuwa mji fulani hapa nchini nikihubiri mkutano wa siku nane, asubuhi moja alikuja mzee mmoja kuniona katika hotel niliyokuwa ninakaa.
Yule mzee akasema; “ Unakumbuka jana ulipoita watu wanaotaka kuokoka waje mbele waombewe, kuna mtoto mmoja alikuwa wa kwanza kufika mbele”.
“Ndiyo, nakumbuka”; Nikamjibu.
Yule mzee akaendelea kusema; “Yule mtoto ni wa kwangu, na tangu jana kumetokea mabadiliko makubwa mno ya tabia, nikaona heri nije nikushirikishe”.
Nikamuuliza, “Kumetokea mabadiliko gani?”
“Huyu mtoto wangu”; yule mzee alieleza; “Kabla ya jana alipoamua kuokoka, alikuwa si mtii, alikuwa hapendi usafi, alikuwa hawezi hata kutandika kitanda chake akiamka asubuhi. Hata tukimwambia afagie uwanja unaozunguka nyumba yetu alikuwa hasikii. Kweli, tumempiga fimbo mpaka tuliogopa tutamuumiza. Lakini kuanzia jana alipookoka (sisi tulifikiri anatania) tabia yake imebadilika kabisa. Amekuwa  mtii, kazi anajituma kufanya, amekuwa msafi, hata wakati wa usiku, anachukua biblia na kusali yeye mwenyewe – maajabu haya”.
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na kuinywa damu yake, yeye atakaa ndani yako na wewe utakaa ndani yake unapokea uzima wake wa milele unaokuvika tabia ya Uungu.
Haya ndiyo yaliyotokea kwa huyu mtoto mdogo wa umri wa miaka kumi na miwili. Huyu mtoto alipompokea Yesu Kristo na kuokoka – Kiroho aliula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake – akapokea uzima wa milele, Yesu Kristo aliingia ndani ya mtoto, na mtoto akaingia ndani ya Yesu Kristo – yote yalifanyika kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu.
Unadhani mtoto huyu alipata wapi ujasiri wa kufanya sala yeye mwenyewe, kitu ambacho alikuwa anaogopa kufanya kabla hajaokoka?
Jibu lake ni – Damu ya Yesu Kristo! Imeandikwa hivi; “Basi ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu…….” (Waebrania 10:19).
Niliwahi kukaribishwa katika mkoa mwingine kuhubiri katika Kanisa fulani, nakumbuka kuwa nilihubiri juu ya Bartimayo yule kipofu aliyeponywa na Yesu Kristo kule Yeriko. Nilipomaliza mahubiri nilikaribisha watu waje mbele wale wanaotaka kuokoka na kuombewa magonjwa.
Watu wengi waliokoka na pia kuponywa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua.
Baada ya wiki moja kupita, alikuja mtu mmoja nyumbani kwangu tukasalimiana na nikamkaribisha aingie ndani. Alipokwisha kukaa kwenye kiti, akaniuliza akasema; “ Mlimpa kitu gani ndugu (alitaja jina lake) siku mlipokuja kuhubiri kanisani kwetu – maana mimi sikuwepo.”
Nikamuuliza, “Kwani kumetokea nini?”
Yule mgeni akasema; “Huyo ndugu alikuwa hawezi kunywa chai ya maziwa wala maziwa – akinywa maziwa alikuwa anaugua. Nilishangaa siku moja alifika nyumbani, nilipomkaribisha chai ya rangi alikataa, akasema sasa anakunywa chai ya maziwa bila shida yoyote."
“Nilipomuuliza ameanza lini kunywa chai ya maziwa, akasema tangu baada ya maombi ya Jumapili pale Kanisani. Lakini pia, niliona tabia yake imebadilika. Alikuwa hachani nywele- sasa anachana. Alikuwa mlevi sana – sasa haonji tena pombe. Alikuwa mchafu, hajijali – nilishangaa kumwona amevaa nguo safi. Ni kitu gani mlimpa?”
Nikamjibu nikasema; “ Sisi tulichokifanya ni kuhubiri habari za Yesu Kristo na uwezo wake. Ndugu yako alifungua moyo wake siku ile, akampokea Yesu Kristo moyoni mwake ili awe Bwana na Mwokozi wake akaokoka. Pia tukamuombea tatizo la ugonjwa alilokuwa nalo na Bwana akamponya”.
Ni jambo la kumsifu Mungu sana katika Kristo, kwa sababu baada ya huyo ndugu kuokoka, na maisha yake kubadilika – sasa hivi ana kazi nzuri ya kuajiriwa na pia, ni mhubiri wa injili. Jina la Bwana libarikiwe!
Huwezi ukampokea Yesu Kristo moyoni mwako na bado ukawa na tabia uliyokuwa nayo zamani. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako – unapokea Uzima wa milele unaokupa tabia ya Uungu.
Yesu Kristo alisema hivi; “ Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna Uzima ndani yenu…..Aulaye mwili wangu na kuinywa DAMU YANGU hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa pekee yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote…….Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana 6:53,56; Yohana 15:4,5,7)
Mtume Paulo alisema; “ Hata imekuwa, mtu akiwa NDANI YA KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
Mtume Paulo alisema hivi katika waraka wake wa pili kwa watu wote, sura ya kwanza mstari wa tatu na wa nne; “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima wa utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo atumetukirimia ahadi kubwa mno, za THAMANI, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.


UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUTULINDA

Wajenzi wa nyumba huwa wanasubiri msimu wa mvua ili kuwa na uhakika wa kusema nyumba imekamilika au bado. Wakati huo wa mvua inakuwa rahisi kufahamu kama nyumba inavuja au haivuji.
Watu wengi walio wakristo hawaamini kuwa kuna nguvu na uwezo wa ajabu, usiotamkika, na usiopimika katika DAMU YA YESU KRISTO unaoweza kutulinda dhidi ya mshambulizi ya adui yetu shetani.
Wakristo wengi wanaamini ya kuwa katika damu ya Yesu Kristo kuna utakaso, kuna msamaha, na pia kuna upatanisho. Lakini ni wakristo wachache wanaofahamu ushindi wa ulinzi uliomo ndani ya damu ya Yesu Kristo.
Kwa mfano kwa muda mrefu nilikuwa naisoma mistari ifuatayo bila kufahamu maana yake hasa ya kiroho. Imeandikwa hivi;
“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa” (Ufunuo 12:11)
Hatua kwa hatua, Roho Mtakatifu alianza kunionyesha na kunifafanulia maana ya maneno hayo.
Niliwahi kusoma ushuhuda ufuatao katika gazeti moja juu ya uwezo wa damu ya Yesu Kristo, ambao ulinifanya nitafakari mara kwa mara juu ya uwezo wa damu ya Yesu Kristo ili kutaka kujua undani wake hasa.
Hilo gazeti liliandika ya kuwa kuna mhubiri mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya kueneza neno la Kristo katika kijiji fulani.
Siku moja huyo mhubiri alikuwa sehemu moja ya kijiji hicho akifungua – fungua mizigo, mara ghafla akasikia maumivu makali mkononi, kama vile ameumwa na kitu fulani. Alipoinua mkono unaoumwa ili auangalie alimwona nge mwenye sumu kali ameng’ang’ania katika mkono wake. Wanakijiji wengi waliokuwa wakisaidiana naye mahali hapo walipomwona huyo nge akimuuma – wakaingiwa na hofu kubwa wakidhani ya kuwa mhubiri huyo hakika atakufa.
Mhubiri huyo wa neno la Kristo, alikuwa si mwenyeji wa kijiji hicho. Yeye hakufahamu kuwe nge wa aina hiyo kama aliyemuuma ana sumu kali ya kuua. Kwa hiyo alibaki anashangaa kwa nini wanakijiji waliomzunguka wameingiwa na hofu kubwa kwa tukio hilo.
Huyo mhubiri akakung’uta mkono wake uliokuwa umeng’ang’aniwa na nge huku akisema; “Katika jina la Yesu Kristo nanyunyiza damu ya Yesu”. Yule nge akaanguka chini.
Baada ya hapo, huyo mhubiri akaondoka hapo alipokuwa akiangalia mizigo, na kuelekea ofisini kwake karibu na jengo la kuabudia. Wanakijiji wengi wakamfuata nyuma kwa huzuni wakijua kuwa atanguka chini afe kwa sababu ya sumu ya nge huyo. Pia walijua kijijini hapo hapakuwa na dawa ya kuondoa sumu ya nge huyo katika damu ya mtu – kwa hiyo walijua mhubiri huyo atakufa tu.
Yule mhubiri alipoona watu wengi wamemfuata, akaamua kuhubiri injili na kuwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi ya kuwa hatakufa kwa kuwa hatakufa maana alisema “ Katika jina la Yesu Kristo nanyunyizia damu ya Yesu dhidi ya sumu ya nge”. Na kweli yule mhubiri hakufa kwa sababu ya ile sumu ya nge.
Nilipoisoma habari hii katika gazeti hilo, nilianza kutafakari kwa upya juu ya damu ya Yesu Kristo. Nilikuwa sijawahi kusikia – mpaka nilipoona katika gazeti hilo – kuwa mtu anaweza kutumia Jina la Yesu Kristo na damu yake kwa pamoja namna hiyo.
Ndipo Roho Mtakatifu aliponikumbusha ya kuwa uwezo tuliopewa wa kulitumia jina la Yesu Kristo, unatokana na uhusiano wetu na Kristo tulionao katika agano jipya ndani ya DAMU YA YESU KRISTO. Na bila kujua kazi ya damu ya Yesu Kristo kwetu, ni vigumu kujua siri ya kulitumia na kuliamini jina la Yesu Kristo kama inavyostahili.
Wakati fulani tulikuwa tunafanya maombi nyumbani kwangu na wenzetu fulani, Roho Mtakatifu alisema maneno yafuatayo “ Waambie watu wangu, wajitakase, wapake damu yangu katika miimo ya milango. Waambie watu wajitakase, kila mtu na nyumba yake.
Waomboleze kwa ajili ya jambo hilo…..Watu wangu wamenitenda dhambi. Lakini  kama watatubu na kuacha nitaghairi….Nataka Kanisa (Wakristo) linalofaa. Wote mvae vazi jeupe lisilo na doa wala waa. Muwe tayari kwa arusi – arusi i karibu ndiyo maana nimekueleza hayo…….”
Nilipousikia ujumbe huo, nilikumbuka maneno ambayo Mungu alimwambia Musa kabla ya kuwapiga wamisri pigo la kumi. Baada ya Musa kupokea maneno ya Mungu biblia inatuambia ya kuwa;
“Hapo ndipo Musa akawaita Wazee wa Israeli, na kuwaambia  Nendeni, mkajitwalie wana-Kondoo kama jamaa zenu zilivyo  mkamchinje pasaka.  Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye  katika  ile damu iliyo bakulini, na kukipiga kizingiti cha juu na  miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli,  tena mtu yeyote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba  yake  hata asubuhi. Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha  juu, na katika ile miimo miwili,  Bwana atapita juu ya mlango,  WALA HATAMWACHA  MWENYE KUHARIBU AINGIE NYUMBANI MWENU KUWAPIGA NINYI. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele” (Kutoka 12:21-24).
Jambo hili tanatakiwa tulitunze kuwa amri kwetu na watoto wetu milele kwa DAMU YA YESU KRISTO ambaye ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili yetu. Katika msamaha na Upatanisho wa damu yake tunapata ULINZI juu yetu na watoto wetu dhidi ya mashambulizi ya shetani aliye mharibifu.
Nilipokuwa nikiyalinganisha maneno aliyoambiwa Musa na Mungu, na yale tuliyoambiwa sisi na Roho Mtakatifu tulipokuwa tunaomba nilifahamu ndani ya moyo wangu mambo mawili yanayokwenda kutokea juu ya kizazi hiki cha sasa.
Jambo la KWANZA litakalotokea ni; hukumu au pigo juu ya watu na familia zao kwa sababu wamemtenda Mungu dhambi – wameasi maagizo yake.
Jambo la PILI litakalotokea ni; Mungu atawalinda wasipatwe na hukumu au pigo hilo wale wote watakaotubu dhambi zao. Damu ya Yesu Kristo itakuwa ulinzi juu ya roho zao, miili yao, akili yao, watoto wao na mali zao. Yule mharibu hatawadhuru kwa kuwa ATAIONA DAMU YA YESU KRISTO IKIFANYA KAZI KATIKA MAISHA YAO.
Nilipokuwa naendelea kuomba na kutafakari juu ya ujumbe huu, Roho Mtakatifu alinikumbusha maneno yafuatayo;
“Ninyi nanyi kama mawe yaliyo hai, mmejengwa  mwe nyumba ya Roho, UKUHANI MTAKATIFU, mtoe dhahibu za roho, zinazokubaliwa na Mungu,  kwa njia ya Yesu Kristo……. Ninyi ni mzao mteule,  UKUHANI WA KIFALME, taifa takatifu, watu wa  Milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:5,9)
Kuhani wa agano la kale alipokuwa anakwenda mbele za Mungu kufanya upatanisho wa watu wa Israeli na Mungu – alikuwa kwanza anachukua damu ya mafahali au ya kondoo- halafu anafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe halafu ndipo afanye upatanisho kwa ajili ya watu. Baada ya toba hiyo wana wa Israeli walikuwa wana uhakika wa msamaha na kwamba MUNGU ATAWALINDA TOKA MASHAMBULIZI YA MAADUI NA YA MAGONJWA.
Katika agano jipya lililosimikwa kwa damu ya Yesu Kristo, kila mtu aliyeokoka au aliye mkristo wa kweli na si mkristo wa jina tu – ni KUHANI MTAKATIFU, KUHANI WA KIFALME, MZAO MTEULE, MTU WA MILKI YA MUNGU, ANAO UJASIRI WA KUPAINGIA PATAKATIFU KWA DAMU YA YESU KRISTO kwa ajili yake, ndugu zake na watu wengine pia!

WEKA KATIKA MATENDO MANENO ULIYOYASIKIA

Musa aliposikia maneno hayo toka kwa Mungu, ALITII akawaita wazee wa Israeli na kuwaeleza yote maagizo hayo. Wazee wa Israeli waliposikia WALITII, na wakawaeleza na kuwaongoza wana wa Israeli kufanya maagizo hayo. Wana wa Israeli wasingetii maneno hayo waliyoyasikia toka kwa Mungu, wao pia wangepatwa na pigo lile lililowapata Wamisri.
Wana wa kwanza wa familia za Israeli walipona kufa kwa sababu WALISIKIA, WAKATII, WAKAYAFANYA MAAGIZO YA MUNGU. Na sisi tukitaka kupona mapigo yanayozidi kushuka juu ya kizazi hiki kwa sababu ya dhambi basi tunahitaji KUSIKIA MANENO AMBAYO ROHO MTAKATIFU ANAWAAMBIA WATU WAKE LEO; TUTII NA KUYAFANYA MAAGIZO YAKE – TUSIPOTII NA KUTUBU HAKIKA TUTAANGAMIA!
Kwa hiyo ukitaka wewe na wote walio katika nyumba yako mlindwe na DAMU YA YESU KRISTO – fanya hivi;
1.       Tubu kwa ajili yako mwenyewe kwanza, halafu;
2.       Tubu kwa ajili ya kila mmoja aliye pamoja nawe katika nyumba hiyo unayokaa.
Mungu atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi nyote KUWALINDA dhidi ya mashambulizi ya Ibilisi, soma Kutoka 12:21-24.
Ukitaka wewe na wote walio katika nchi yako mlindwe na DAMU YA YESU KRISTO –fanya hivi;
1.       Tubu kwa ajili yako mwenyewe kwanza, halafu;
2.       Tubu kwa ajili ya watu wote walio katika nchi hiyo pamoja na wewe.
Mungu atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi nyote humo nchini KUWALINDA dhidi ya maharibifu ya Ibilisi, soma 2 Mambo ya Nyakati 7:14.
Ukitaka wewe na wote walio katika chombo unachosafiria, gari dogo au basi la abiria, au ndege au meli mlindwe na DAMU YA YESU KRISTO – fanya hivi kabla ya kuanza safari;
1.       Tubu kwa ajili yako mwenyewe kwanza, halafu;
2.       Tubu kwa ajili ya wote mtakaosafikiri nao hata kama hawafahamu.
Mungu Baba atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi katika safari hiyo KUWALINDA dhidi ya mashambulizi na mitego ya Ibilisi soma, Matendo ya Mitume 27:21-26.
Nakumbuka wakati fulani mimi na rafiki yangu (wawili tu) tulikuwa tunasafiri kwenda Tukuyu kwenye mkutano wa injili. Tulikuwa kwenye gari lenye uwezo wa kuchukua abiria watano, lakini tulikuwa wawili tu na mimi nikiendesha. Kabla hatujaondoka tulifanya sala kama ninayokuambia hapo juu.
Tulipofika kati ya miji ya Dodoma na Morogoro, tulisimamishwa na askari wa usalama barabarani. Niliposimamisha gari, yule askari wa usalama barabarani akatusalimu, na tukaona kuwa ameongozana na mtu mwingine aiyekuwa na mizigo. Na tuliwaza kuwa alitaka kutuomba tumchukue,ingawa alikuwa hajatuambia.
Basi, yule askari baada ya kutusalimia, akatazama – tazama ndani ya gari letu, halafu kama vile mtu aliyeona kitu akasema ‘Aaa” naona MMJAA – basi unaweza kwenda.
Na mimi nikamjibu; “kweli TUMEJAA, ahsante sana”. Halafu nikawasha gari – tukaondoka.
Tulipofika Morogoro tukaamua kumpumzika ili tupate chakula cha mchana. Ndipo mwenzangu akaniuliza; “Hivi yule askari alipokuwa anasema tumejaa, aliona watu wangapi kwenye gari wakati tulikuwa wawili tu?”
Ndipo na mimi niliposhituka, nikasema; “Lakini kweli, hata mimi sijui kwa nini nilimjibu kuwa tumejaa wakati nilikuwa nafahamu kuwa gari lilikuwa bado na nafasi ya watu watatu!”
Wote tukabaki tunashangaa! Lakini ni wazi kwamba Mungu aliyekuwa pamoja nasi alijua hatari iliyokuwa mbele yetu kama tungemchukua yule mtu, Kwa hiyo Mungu alimfungua macho ya kiroho yule askari, naye akawaona watu wamejaa kwenye gari – lakini ukweli walikuwa ni malaika ambao Mungu aliwatuma watulinde njiani – ingawa sisi  tulikuwa hatuwaoni!
Soma Zaburi 91:1-12. Yote haya yanafanyika kwa sababu ya imani katika Damu ya Yesu Kristo!
Ukitaka wewe na wote unaowahubiria neno kwenye mikutano ya hadhara au ndani ya nyumba mlindwe na Damu ya Yesu Kristo – fanya hivi kabla ya kwenda kuwahubiria;
1.       Tubu kwa ajili yako mwenyewe, halafu;
2.       Tubu kwa ajili ya wote utakaowahubiria ingawa wewe huwafahamu. Kumbuka Mungu anawafahamu.
Basi Mungu wetu tunayemwabudu katika Yesu Kristo atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi KUWALINDA katika kusanyiko hili dhidi ya mashambulizi na machafuzi ya Ibilisi.
Ndiyo maana imeandikwa kuwa; “Hao wakamshinda (shetani-mshitaki wao) kwa DAMU YA MWANA-KONDOO na kwa neno la ushuhuda wao…..” (Ufunuo 12:11) Fahamu hili ya kuwa PALIPO NA DAMU YA YESU KRISTO – shetani HAWEZI KUSTAHIMILI KUKAA.
Kwa hiyo HAKIKISHA kila wakati unaishi na kutembea katika TOBA YA KWELI ili DAMU YA YESU IWE PAMOJA NAWE KILA MAHALI ULIPO NA UENDAKO.
SHUHUDA
Siku moja msichana mmoja aliyekuwa anahitaji msaada wa maombi- alinieleza jinsi ambavyo usiku akilala anajikuta anafanya uasherati na watu asiowaona. Kilichoshangaza ni kuona ya kuwa huyu msichana alikuwa ameokoka, lakini aliendelea kupata shida hiyo ya kufanya uasherati usiku na watu asiowaona.
Nikamuuliza; “ Unataka nikusaidie kitu gani katika tatizo hili?”
Huyu msichana akajibu akasema; “nahitaji maombi na ushauri juu ya jambo la kufanya ili shida hii iniondokee”
Nikamuuliza tena; “Je! unafahamu uwezo uliomo katika damu ya Yesu Kristo wa kutulinda ili usipatwe na shida za namna hii?
Kabla hajajibu hilo swali, nilimwambia nitampa jarida linalo-zungumza juu ya Damu ya Yesu Kristo (ambalo ndilo mwanzo wa mawazo ya kitabu hiki), na kwamba alisome na kutafakari yaliyo ndani yake. Pia, nikamsisitizia ya kuwa kabla ya kulala kila siku aombe damu ya Yesu Kristo imfunike na ulinzi wa Mungu, ili nguvu za shetani zisimsumbue.
Yule msichana aliondoka na akaenda akafanya kama nilivyomweleza; - baada ya wiki moja akarudi tena na kuniambia ya kuwa baada ya kufanya kama nilivyomweleza ile shida ya kufanya uasherati na watu asiowajua usiku au kwenye ndoto ilikwisha na wala ilikuwa haijarudi tena.
Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe kwa maana fadhili zake ni za milele zilizomo katika Damu yake iliyomwagika pale msalabani kwa ajili yetu.
Kwa hiyo wewe unayesoma kitabu hiki nakushauri ya kuwa usisahau kuomba damu ya Yesu Kristo ikufunike usiku unapolala na mchana pia.
Na kwa wale walio na watoto, kumbuka kila siku kuomba ulinzi wa Damu ya Yesu juu yao – wakiwa nyumbani au shuleni au po pote pale.
Kumbuka Biblia inasema; “Mwe na kiasi na kukesha kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1Petro 5:8). Lakini Biblia inatutia moyo na kutuangaliza juu ya uwezo wa damu ya Yesu Kristo inaposema; “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo……” (Ufunuo wa Yohana 12:11)
Usiogope vitisho vya shetani ikiwa umejificha ndani ya Damu ya Yesu Kristo. Shetani hawezi kupenya mahali palipo na Damu ya Yesu Kristo kwa maana anaiogopa sana.
SALA YA TOBA
Inawezekana kabisa ya kuwa wewe unayesoma somo hili hujaokoka-hujampokea Yesu Kristo ndani ya moyo wako kama Bwana na Mwokozi wako- na baada ya kusoma somo hili umeona umuhimu wa Damu ya Yesu Kristo katika maisha yako.
Naamini Roho Mtakatifu amekiweka kitabu hiki mikononi mwako kwa mpango maalum wa Mungu ili ufike mahali pa kutubu na kuokoka. Inawezekana kabisa, pia ya kuwa hujawahi kuambiwa juu ya umuhimu wa wewe kuokoka. Lakini napenda kukuambia ya kuwa ni mpango wa Mungu uokoke. Soma Wakolosai 1:13,14 na Yohana 1:12-14 na 1 Timotheo 2:3-6 na Warumi 1:16,17 na Yohana 3:7. Ni vigumu kuona baraka za Damu ya Yesu bila ya kuokoka.
Kwa hiyo kama unataka kuokoka-tafuta mahali palipo na utulivu, na usome kwa sauti sala ifuatayo: (ukiweza unaweza kupiga magoti unapoomba sala hii)
“Ee Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha  yangu. Ninatubu kweli. Naomba damu ya Yesu  Kristo iliyomwagika msalabani kwa ajili yangu initakase sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu. Bwana  Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia kwa uwezo wa Roho wako – uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa  kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako  nikutumikie katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu yangu katika jina  la Yesu Kristo. Amina.
Ikiwa umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe umeokoka na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.
Unapoanza maisha haya mapya katika Yesu Kristo nakushauri mambo yafuatayo:
1.       Zungumza na Mungu kwa maombi kila siku (Yohana 15:7)
2.       Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku (Matendo ya Mitume 17:11)
3.       Mruhusu Roho Mtakatifu akutawale (Wagalatia 5:16-25; Warumi 8:14-17)
4.       Umtumaini Mungu kwa kila jambo katika maisha yako (1Petro 5:7; Zekaria 4:6)
5.       Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wao kama wewe ili uimarike zaidi (Waebrania 10:25)

Ukipenda unaweza kuniandikia kwa anwani hii hapa chini juu ya uamuzi uliofikia leo wa kuokoka, ili tumshukuru Mungu pamoja, na tuzidi kukuombea; na pia, tukutumie maandiko mengine ya kukusaidia: KWA WALE WANAOTAKA KUJISOMEA ZAIDI JUU YA DAMU YA YESU

Mungu aliwahi kuwaangalia watu wake jinsi wanavyohangaika na kuangamia kiroho, na kwa masikitiko makubwa alitamka maneno haya kwa kinywa cha nabii wake Hosea;
“Watu wangu wanaangamizwa kwa  kukosa maarifa….” (Hosea 4:6)
Hata hivi leo kuna watu wengi sana wa Mungu wanaangamizwa kiroho, siyo kwa sababu hawapendi kuishi maisha ya ushindi kiroho, bali wanaangamizwa kwa kukosa maarifa!
Yesu Kristo aliwahi kuwaambia wanafunzi wake maneno yafuatayo alipokuwa anajibu moja wapo ya maswali waliyokuwa wanamuuliza mara kwa mara:
“…Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29).
                Hata hivi leo ukisikiliza na kufuatilia sababu kubwa zinazowafanya wakristo wapotee kimafundisho, mojawapo ya sababu hizo ni kutoyajua maandiko yanayozungumzia juu ya uweza wa Mungu katika Damu ya Yesu Kristo.
Hapa chini nimeorodhesha sehemu chache ambazo katika Biblia zinazungumzia juu ya sehemu ya Damu ya Yesu Kristo katika maisha yako ya kila siku.
Unaweza kuzisoma sehemu zote hizi kwa siku moja, lakini nimezipanga kwa muda wa siku saba ili mpango huu ukusaidie kusoma na kutafakari kwa undani juu ya Damu ya Yesu Kristo:
Siku ya 1
Agano jipya na Maisha mapya ( sehemu ya 1):
Yohana 6:53-56; Mathayo 26:28; 1Wakorintho 11:17-34
Siku ya 2
Agano Jipya na Maisha mapya ( Sehemu ya 2):
Waebrania 8:1-13; Waebrania 9:1-28; Waebrania 10:1-25 
Siku ya 3
Ushindi dhidi ya dhambi (sehemu ya 1):
1Yohana 1:9; 1Petro 2:24; Wakolosai 1:13,14; Ufunuo wa Yohana 1:4-6 
Siku ya 4
Ushindi dhidi ya dhambi (sehemu ya 2):
Wakolosai 2:13-15; Waebrania 10:17; Isaya 43:25
Siku ya 5
Ulinzi na nguvu za Mungu katika Damu ya Yesu:
Ufunuo wa Yohana 12:11; 1 Wakorintho 1:18; Kutoka 12:21-24
Siku ya 6
Upatanisho katika Damu ya Yesu:
Waefeso 2:12-17; 2Wakorintho 5:17-20
Siku ya 7
Ujasiri katika maombi:
Waebrania 10:19; Waebrania 4:14-16
Pamoja na vifungu hivi nilivyokuwekea hapa, Biblia ina vifungu vingine zaidi ambavyo kwa pamoja ukivitafakari mara kwa mara – Roho Mtakatifu atakutia nuru katika macho yako ya ndani ili sehemu ya Damu ya Yesu Kristo katika maisha yako ionekane kwa wazi kwako kuliko ilivyo sasa.
                                                Christopher Mwakasege,
                                    S.L.P. 2166, ARUSHA, Tanzania.
                                     
Email: tasoet@nexusdigital.co.tz




5 comments:

Injili ya Neno la Mungu isiyopindishwa lazima niihubiri said...

Amina!
Mungu azidi kuwabariki katika huduma hii ya mafunzo ya mtandaoni, inanisaidia sana hata mimi ninaekuwa sikuhudhuria aidha ni kwenye makongamano au mikutano ili kupata mafunzo hayo.
Nabarikiwa mnooo!

Unknown said...

mungu aikumbuke sadaka yenu

Unknown said...

Mungu awabariki sana na kuwatia nguvu katika huduma hii aliyowapatia.

ufalme wa Mungu said...

Amina nimebakiwa Sana, Mungu azidi kumwinua Mtumishi wake katika huduma aliyo weka ndani yake.

Mbarikiwa said...

Nimelisoma andiko hili kwa wakati sahihi,la zaidi ni juu ya uwezo wa Damu ya Yesu katika maisha yetu ya kila siku .