Thursday, September 22, 2016

UFALME WA SHETANI DUNIANI (Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016)

UFALME WA SHETANI DUNIANI
Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)

www.uzimawamileleministries.blogspot.com


UTANGULIZI

Sio mpango wa Mungu shetani ammiliki na kumtawala mwanadamu lakini mwanadamu alipewa na Mungu kumiliki na kutawala (Mwanzo 1:28 “28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”), ila kwasababu ya ile dhambi pale bustani ya edeni ndipo shetani alipouchukua tena umiliki ambao Mungu alimpa mwanadamu.

Ashukuriwe Mungu (Jehova) kwa upendo na neema yake kwa kumtoa Yesu Kristo kuwa kafara (sadaka) ili atukomboe kutoka katika uovu ule tuliofanya sisi kama ilivyoandikwa katika Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Pamoja na jambo hili kubwa la ukombozi, shetani ameendelea kufanya mbinu nyingi za kuwaumiza na kuwashinda watakatifu wa Mungu kama tunavyosoma katika Ufunuo 13:2, 7 “2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. 7 Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.”

Kama anavyosema mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso 3:20 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;”, namimi naungana na mtume Paulo kwa kumtukuza Mungu kwa mamb makuu anayoyatenda katika maisha yetu na kutupa ushindi dhidi ya shetani na nguvu zote za giza kama ilivyoandikwa kuwa tumemshinda shetani kwa damu ya Yesu Kristo (Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”)

Na kwasababu hiyo basi Mungu ametupa silaha saba muhimu za kumshinda shetani na kumuondoa katika mipaka yetu kwa Jina la Yesu, ukisoma Waefeso 6:13-18 “13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI, na kuvaa DIRII YA HAKI KIFUANI, 15 na kufungiwa miguu UTAYARI TUPATAO KWA INJILI YA AMANI; 16 zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni CHAPEO YA WOKOVU, na UPANGA WA ROHO AMBAO NI NENO LA MUNGU; 18 KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”


Kama linavyosema Neno la Mungu katika Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya FALME na MAMLAKA, juu ya WAKUU WA GIZA HILI, juu ya MAJESHI YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho.” Ninachotaka ukione hapa ni mgawanyiko wa kiutawala katika ulimwengu wa roho ambao sisi watakatifu (waliookoka) ndio tunapambana nao katika ulimwengu wa roho.


UFALME WA ROHONI UNAVYOFANYA KAZI DUNIANI
Jambo la muhimu la kufahamu hapa ni kwamba katika nchi mmoja kunakuweko na falme mbili, yaani ufalme/utawala wa kiroho na ufalme/utawala wa kibinadamu. Na utawala/ufalme  ule wa kiroho unakuwa na nguvu sana kuliko ule ufalme/utawala wa kimwili/kibinadamu. Kimsingi utawala/ufalme uliopo rohoni ndio unaoongoza tawala za kibinadamu. Mfano mzuri ni pale ambapo Yesu Kristo anaitwa Mfalme wa wayahudi (Luka 23:3 “Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema.” Vilevile tunasoma katika (Luka 23:28 “Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.”) wakati huo huo kulikuwa na Herode ambaye ndiye aliyekuwa mfalme wa wayahudi (Mathayo 2:1 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,….”;) Yaani Yesu yupo rohoni kwenye kiti cha enzi cha Daudi baba yake na Herode yupo mwilini kama mfalme wa kawaida


MUNGU (JEHOVA) ANAO UFALME
Wakati Fulani Bwana Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake nanma ya kusali akawaambia katika Mathayo 6:9-13 9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE…………….. KWA KUWA UFALME NI WAKO, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.”

Kwahiyo tunaona kuwa Mungu anao ufalme wake unaoweza kuja na kumiliki hapa duniani kama Mbingu. Soma mistari ifuatayo kuona Yesu akiongelea ufalme wa Mungu/Mbinguni
Mathayo 3:2 “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”

Marko 4:11 “Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,”

Kwahiyo tunajifunza kuwa Mungu anao ufalme wake ambao kama ukiukaribisha hapa duniani unaweza kutawala, maana yake unakuwa na utawala wa kibinadamu lakini unapokea maelekezo kutoka kwa Mungu mwenyewe.


SHETANI ANAO UFALME (KINGDOM)

Baada ya Yesu kumponya Yule mtu mwenye pepo kipofu na bubu na mtu Yule akapata kuona na kusikia vizuri, mafarisayo wakamdhihaki kwamba anatoa pepo kwa beelzebuli mkuu wa pepo, lakini Yesu alifahamu mawazo yao na kuwajibu.

Mathayo 12:25-26 25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. 26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”

Majibu haya ya Yesu yanatuonesha kuwa shetani anao ufalme ambao uko imara (haujafitinika) na umesimama “Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”

Vilevile ukiendelea kusoma Biblia yako utagundua kuwa shetani kama mfalme anacho kiti chake cha enzi kama tunavyosoma katika Ufunuo 13:2 “2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”
Vilevile ufalme wa shetani unaweza kutawala katikati ya falme za wanadamu kama ukikaribishwa.


1.     UFALME WA SHETANI KATIKA NCHI YA TIRO

Ezekiel 28:1-19 “1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 2 Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. ………………….. 9 Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha. ……………….11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema, 12 Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri. 13 Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. 14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. ……………..”


Tiro ni nchi kama nchi nyingine, yaani kama ilivyo Tanzania, lakini katika nchi ya Tiro kuna kuna watawala wa aina mbili wenye mamlaka juu ya nchi ya Tiro, kwanza kuna mkuu wa nchi ya Tiro Ezekiel 28:2 Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.”

Hapa mkuu wa Tiro ni mkuu wa nchi ya Tiro katika ulimwengu wa mwili ambaye anaonekana kwa macho ya mwilini kuwa ndiye anyetawala nchi ya Tiro. Hii ni kama vile unavyoweza kumuona Raisi wan chi au Waziri mkuu wa nchi au kiongozi yoyote katika nchi mwenye mamlaka ya mwisho katika ulimwengu wa mwili.

Lakini tunaona nchi hiyo hiyo moja ya Tiro kuna kiongozi mwingine mwenye madaraka makubwa katika nchi ya Tiro kama tunavyosoma katika Ezekiel 28:12 “Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.”

Huyu ni mkuu wa Tiro katika ulimwengu wa roho, nasema ulimwengu wa roho kwasababu; kwanza nchi moja haiwezi kuwa na viongozi wakuu wawili wenye mamlaka sawa, halafu pili Biblia imemtaja mmoja kuwa ni mwanadamu na wa pili kuwa ni kerubi, hivyo mtawala wa pili wa Tiro yupo rohoni japo anaitawala nchi ya Tiro.

Hapa ndipo tunapopata ufahamu kuwa nchi moja ya Tiro imetawaliwa mwilini na imetawaliwa rohoni, na rohoni imetawaliwa na ibilisi na mwilini imetawaliwa na mwanadamu


2.     UFALME WA SHETANI KATIKA NCHI YA UAJEMI

Daniel 10:1-21 1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo. 2 Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. 3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia. 4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli; 5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi………….. 20 Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja…….”
Uajemi ni nchi ambayo inayo kiongozi wake anaitwa mfalme koreshi kama tunavyosoma katika Daniel 10:1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi,……….” Huyu ni binadamu ambaye katika hali ya maisha ya kawaida anaonekana kuwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi ya Uajemi na ndiye mwenye mamlaka kwa jinsi ya mtazamo wa kawaida.
Lakini jambo la kustaajabisha; baada ya maombi ya Daniel, Mungu (Yesu) alikuja kumletea majibu na alipokuwa anakuja Biblia inasema alizuiwa na mkuu wa uflame wa Uajemi kwa muda wa siku 21 kama ilivyoandikwa katika Daniel 10:13 “Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja;………………….

Sasa huyu mkuu wa mfalme wa uajemi ni nani hasa wakati tayari uajemi inayo mfalme na jina lake ni Koreshi? Ukiendelea kusoma Daniel 10:13, Yesu anasema maneno haya “………..bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi Kwahiyo tunajifunza jambo kubwa hapa kwamba kama malaika Mikaeli alishuka kuja kumsaidia Yule alitumwa; basin i dhahiri kwamba alizuiwa rohoni na sio mwili; na kwasababu hiyo tunapata jibu kuwa mkuu wa ufalme wa uajemi ni roho iliyokuwa inamiliki na kutawala nchi ya uajemi na ndio ilikuwa na nguvu ya kuruhusu nini kingie uajemi na nini kisiingie uajemi. Na kwakuwa roho hiyo ilifanya vita na Mungu (Jehova) basi ni wazi kabisa kuwa ni roho ya ibilisi.


VITA NA UFALME WA SHETANI DUNIANI
Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya FALME na MAMLAKA, juu ya WAKUU WA GIZA HILI, juu ya MAJESHI YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho.”

Maana yake ni kwamba katika ulimwemgu wa roho unaotawala ulimwengu wa mwili, umegawanyika katika ngazi mbalimbali za uongozi kama ifuatavyo

  •   FALME
  •  MAMLAKA
  •  WAKUU WA GIZA
  •  MAJESHI


Ndio maana tunaona katika nchi ya Tiro kuna mfalme (FALME) katika ulimwengu wa roho ambaye anaongoza na kuimiliki Tiro, vilevile tunaona katika nchi ya Uajemi kuna mkuu (WAKUU WA GIZA) mwenye mamlaka na sauti ya mwisho katika nchi ya Uajemi.
Nasema hao viongozi wa rohoni (katika ulimwengu wa roho) wanayo mamlaka kubwa kwa kuzingatia kuwa waliweza kumzuia Malaika wa BWANA kwa muda wa siku 21 asiingie katika nchi ya Uajemi na Pia waliweza kumpa kiburi na maarifa mengi mkuu wa tiro (ambaye ni mwanadamu) na kumpa kujiinua hadi akajiita mungu.


TUMEPEWA MAMLAKA YA KUSHINDA UFALME WA SHETANI

Baada ya anguko la mwadamu pale bustani ya Edeni, shetani alinyakuwa mamlaka ya kumiliki na kutawala tuliyoipewa na Mungu wakati wa uumbaji, lakini unapo mpokea Yesu Kristo unahamishwa kutoka utawala wa giza na kuingizwa kwenye utawala wa nuru kwa kufufuliwa pamoja na Kristo na unaketishwa pamoja na Kristo na kupewa mamlaka juu ya tawala zote za muovu.

Waefeso 2:6, 1:21-23 “6 Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; 21 juu sana kuliko UFALME wote, na MAMLAKA, na NGUVU, na USULTANI, na KILA JINA LITAJWALO, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”
Tumepewa mamlaka juu ya falme na mamlaka za giza katika ulimwengu wa roho, yaani tunayo mamlaka ya kumshinda mwovu shetani kwa jina la Yesu, kwasababu tumewekwa juu ya mamlaka zote katika ulimwengu mwili na ule wa roho.


FAHAMU KWAMBA KUNA MAMLAKA YA ROHONI INAYOKUTAWALA

Katika maisha ya kawaida tunayoishi kuna mamlaka/falme/wakuu katika ulimwengu wa roho wanao miliki maisha ya wanadamu waliopo mwilini. Kuna mamlaka ya rohoni inayoshughulika na mambo yako ya kiukoo, kifamilia, kikazi, kiafya, kibiashara, kielimu, ndoa na mengine mengi. Kama usipoweza kushughulika na mamlaka za giza zinazoruhusu au kuzuia mafanikio yako lazima utakwama katika mambo mengi ya maisha yako. Utaona mfano wa Daniel alivyochukua muda mrefu kupokea majibu ambayo yapo tayari yalishatolewa na Mungu lakini hayakumfikia kwa wakati kwasababu roho Yule anayetawala katika ulimwengu wa roho katika nchi ya Uajemi alikataa kufungua njia kuruhusu majibu ya BWANA yamfikie Daniel.

Jambo la muhimu sana la kufanya ili uweze kushinda hizo mamlaka za giza ni kumkubali/kumpokea ili Mungu akutoe katika umiliki wa falme za giza na kukupa nafasi ya kutawala kutokea rohoni sawasawa na Neno la Mungu kutoka katika maandiko; Wakolosai 1:13, Waefeso 2:6, Ufunuo 5:10 na Waefeso 1:21-23 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

Kama jinsi nilivyosema hapo awali kuwa tumepewa mamlaka juu ya falme na mamlaka za giza katika ulimwengu wa roho, yaani tunayo mamlaka ya kumshinda mwovu shetani kwa jina la Yesu, kwasababu tumewekwa juu ya mamlaka zote katika ulimwengu wa mwili na ule wa roho.
Nakushauri mtu wa Mungu utumie mamlaka uliyopewa kuuharibu utawala wa giza katika anga la maisha yako.



Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)

www.uzimawamileleministries.blogspot.com

BARAKA NA LAANA HADI KIZAZI CHA NNE (Samson Mollel 0767 664 338)

BARAKA NA LAANA HADI KIZAZI CHA NNE
Samson Mollel 0767 664 338
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)

www.uzimawamileleministries.blogspot.com


UTANGULIZI


Baraka na laana ni maneno yanayotumiwa mara kwa mara na watumishi wengi wa Mungu nahii ni kwasababu katika maisha ya kiroho na kimwili kuna aina mbili tu za maisha ambazo ni maisha ya Baraka au maisha ya laana. Baraka maana yake ni kupata mema au mafanikio, Baraka ni neno linalobeba nguvu Fulani ya kufanya maneno ya heri yawe kweli au ni nguvu inayobeba mafanikio kutokana na kufuata maelekezo uliyopewa. Laana nayo ni nguvu inayobeba taabu na mateso kutokana na maneno yasiyo mema au kutokana na kutofuata maelekezo uliyopewa. Haijalishi umeokoka kiasi gani, unaweza kuwa umeokoka lakini bado ukaishi kwenye laana ambayo hukuisababisha wewe ilisababishwa na baba/babu zako (Kutoka 20:5 “……….nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”).
Fahamu kwamba Baraka au laana inaweza kutolewa kwa kinywa cha Mungu au cha shetani kwa njia ya vinywa vya wanadamu na pia wanadamu wanaweza kutoa Baraka au laana kwa kumtaja Mungu au miungu yao.
Melkizedeki alimbariki Abramu kwa jina la Mungu aliye juu “Mwanzo 14:18-19 “18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. 19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.”
Ndugu za Rebeka walimbariki Rebeka Mwanzo 24:60 “Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.”

BARAKA NA LAANA KUTOKA KWA MUNGU (JEHOVA)

Neno la Mungu limeshaweka wazi kabisa kuwa Baraka zinapatikana kwa njia gani na laana zinapatikana kwa njia gani kama tunavyosoma katika maandiko matakatifu.
Kumb 30:15-20 “15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; 16 kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. 17 Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; 18 nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. 19 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; 20 kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”
Vilevile ukisoma kitabu cha Kumbukumbu la torati mlango wa 28 utaona maelekezo na maagizo aliyoyatoa Mungu ili kujipatia Baraka kutoka kwake na mambo ambayo mtu akifanya atapata laana; Kumb 28:1-2, 151 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; 2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako…….. 15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.”
Kimsingi katika ulimwengu wa roho Mungu anaviona vizazi vyote katika sehemu moja, yaani katika ulimwengu wa roho hakuna umbali wa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine na ndio maana Mungu alipombariki Adamu na sisi tulibarikiwa wote, Mwanzo 1:27-28 “27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. 28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”
Lakini pia hata Adamu alipolaaniwa na sisi sote tulipokea hiyo laana kwakuwa tumezaliwa na Adamu, yaani tulikuwa katika viuno vyake nasisi tukapokea hiyo laana; Mwanzo 3:16- 16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. 17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; 18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; 19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Bada ya laana hii hata wewe ambaye haukuwepo wakati huo leo umerithi laana ambayo Adamu alipewa baada ya kuasi.

LAANA NA BARAKA INAVYOWEZA KUHAMA KUTOKA KIZAZI KWENDA KIZAZI

Kutoka 20:4-5 “4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”
Mungu wetu (JEHOVA) ni Mungu mwenye wivu, yaani hataki kushirikiana vile vitu vinavyompa yeye utukufu na kiumbe au kitu chochote. Anapenda aabudiwe na kusifiwa na kutukuzwa YEYE peke yake tu na sio kumchanganya. Neno la Mungu linasema Mungu hashirikiani utukufu wake na mwingine yeyote (Isaya 42:8 “Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.”)
Inapotokea mtu hakufuata maagizo ya BWANA na kufanya ibada za miungu na kuacha kumwabudu Mungu pekee, basi mtu huyo au familia hiyo na vizazi vyake vyote vinaingia katika laana “…… kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao…………”

BARAKA KUTOKA KIZAZI KIMOJA KWENDA VIZAZI VINGINE

Katika kipengele hiki nataka ujifunze kwa habari ya Baraka inavyoweza kutoka kizazikimoja kwenda kizazi kingine hata kama hicho kizazi hakikufanya mema lakini zile Baraka zinawafuata tu.

Baraka za Mungu kwa Ibrahimu

Biblia inatuambia habari za Abramu (Ibrahimu) alipotoa sadaka (sehemu ya kumi) kwa Melkizedeki mfalme wa Salemu na Melkizedeki akambariki Abramu (Ibrahimu) “Mwanzo 14:18-19 “18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. 19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.”
Neno la Mungu linatufundisha kuwa Abramu (Ibrahimu) alibarikiwa na Melkizedeki ambaye ni kuhani wa Mungu aliye juu sana (JEHOVA) kwasababu alitoa sadaka kwake. Baada ya kutoa sadaka hiyo kuna jambo lilitokea ambalo halionekani vizuri pale katika kitabu cha Mwanzo ila tunaona kwa uzuri katika Agano Jipya kitabu cha Waebrania;
Waebrania 7:9-10 “9 Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; 10 kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.”
Fahamu kwamba Lawi anayetajwa ni uzao wa nne kutoka kwa Ibrahimu kwani Ibrahim alimzaa Isaka, Isaka akamzaa Yakobo, Yakobo akamzaa Lawi. Tunajifunza kwamba unapotoa sadaka wewe hata vitukuu wako walioko katika viuno vyako wanakuwa wametoa hiyo sadaka, na Baraka unazopata zinamfikia mpaka na kitukuu cha yaani zinafika mpaka kizazi cha nne.

Baraka za Mungu kwa Mfalme Daudi

Daudi ni mfalme aliyewakuwa na mahusiano mazuri na Mungu kuliko mfalme mwingine yeyote katika historia ya ulimwengu kiasi cha Mungu mwenyewe kuweka agano la chumvi na Daudi na kumuahidi kuwa ufalme utadumu milele katika uzao wake kama tunavyosoma katika 2Nyakati 13:5 “je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?”; Vilevile Mungu alimuimarisha sana Daudi mbele ya maadui zake, tunasoma Zaburi 89:20-24 “20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. 21 Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. 22 Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa. 23 Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia. 24 Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.”
Kwasababu ya Mfalme Daudi kumpendeza sana Mungu, Mungu alimbariki na kumuahidi kuwa ufalme hautatoka katika uzao wake. Lakini alitokea mtoto wa Mfalme Daudi aliyeitwa Sulemani  ambaye aliziacha njia za BWANA na kuanza kufuata miungu mingine na kuiabudu.
1Wafalme 11:1-13 “1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, 2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. 3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. 4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. 7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu. 9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, 10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana. 11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. 12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako. 13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.”
Pamoja na mfalame Sulemani kumuasi Mungu, Mungu anamrehemu mafalme Sulemani na kuacha kumuadhibu kwasababu ya ahadi ambazo Mungu alizifanya na mfamle Daudi baba yake 1Wafalme 11:11-12 “11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. 12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako”; lakini sio hivyo tu, hata katika adhabu ambayo Mungu ameitoa kwa mfalme Sulemani juu ya mtoto wa Mfalme Sulemani, adhabu hiyo imepunguzwa kidogo kwasababu ya mahusiano mazuri kati ya Mungu na Daudi 1Wafalme 11:13Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.
Pamoja na makosa yote aliyoyafanya mfalme Sulemani na kumkasirisha Mungu, bado tunaona Mungu anaacha kumuadhibu mfalme Sulemani kwaajili ya kumbukumbu nzuri za Baraka alizomuahidia mfalme Daudi.

LAANA KUTOKA KIZAZI KIMOJA KWENDA VIZAZI VINGINE

Katika kipengele hiki nataka ujifunze kwa habari ya laana inavyoweza kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine (Kibiblia) hata kama hicho kizazi hakikufanya jambo baya lakini ubaya uliofanywa na watangulizi wao unawafuata na kuwatesa.

Laana ya kutoisikiliza sauti ya BWANA

Neno la Mungu limeweka waziwazi kuwa ikiwa wewe haujaisikiliza sauti ya BWANA na kuyaacha maagizo ya BWANA basi utalaaniwa katika uzao wa tumbo lako, Kumbukumbu 28:15, 18 “15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. 18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.” Imeandikwa kuwa dhambi/makosa utakayofanya, laana yake inageuzwa kwenda kwa uzao wa tumbo lako na sio kwako wewe uliyefanya kosa hilo. Sasa unaweza kuelewa kwanini inakubidi ushughulikie sana makosa na dhambi walizofanya baba/babu zako kuliko ulivyodhani hapo kabla kwani laana zinazoleta ugumu wa maisha sasa zilisababishwa na wazazi wako au watangulizi wako.

Laana zilizompata mtoto wa mfalme Sulemani

Mtoto wa mfalme Sulemani (Rehoboamu) alirithi laana kwa kosa alilolifanya baba yake (Sulemani), yaani inamaana kuwa laana aliyoipata Rehoboamu ilitokana na dhambi/maovu/makosa ambayo yeye hakuyafanya. Sulemani alijikuta akipokea sehemu ndogo ya urithi wa ufalme (yaani kabila ya Yuda pekee na mji wa Yerusalemu) kutoka kwa baba yake bila kujua kwamba ilikuwa ni laana kwa alistahili kuongoza kabila kumi na mbili.
1Wafalme 11:1-12 “……………. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. 7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. ………………. 9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, ………………. 11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. 12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.
Wakati Rehoboamu anakuwa mtu mzima ili aanze kumiliki kama mfalme katika nafasi ya baba yake (Mfalme Sulemani) yeye hakujua kuwa kwa dhambi na makosa ya baba yake na yeye amefanya hiyo dhambi na kuayabeba maovu na adhabu ya baba yake ijapokuwa hakutenda kosa lolote (Maombolezo 5:7 “Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.”), hivyo Rehoboamu hakuomba toba na ile laana ikamkuta kama tuanavyosoma katika Neno la Mungu.
1Wafalme 12:18-20 “18 Ndipo mfalme Rehoboamu akampeleka Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, nao Israeli wote wakampiga kwa mawe hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda katika gari, ili akimbilie Yerusalemu. 19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo. 20 Ikawa, Israeli wote waliposikia ya kwamba Yeroboamu amerudi, wakapeleka watu wakamwita aje mkutanoni, wakamfanya mfalme juu ya Israeli wote; wala hapakuwa na mtu aliyeshikamana na nyumba ya Daudi, ila kabila ya Yuda peke yake.”
Hivyo laana aliyoinena BWANA juu ya mtoto wa Mfalme Sulemani (Rehoboamu) kwa dhambi ya baba yake ikatimia. Inawezekana hata wewe unaishi katika laana inayotokana na dhambi/maovu/makosa yaliyofanywa na wazazi au mababu zako na wewe hujui kwanini umekwama, omba toba na msamaha.

Laana zilizompata Gideoni

Gideoni aliishi katika maisha ya shida na dhiki na umasikini mkubwa hata kiasi cha kuona kwamba Mungu amewaacha lakini tatizo ni baba yake kuwa kuhani wa baali na madhabahu ya baali imejengwa katika kijiji/mji wao. Na kwasababu hiyo badala ya Gideoni kubarikiwa na Mungu na kupokea  ahadi za Mungu katika maisha yake, kwamba inafahamika kuanzia Mbinguni kuwa Gideoni ni shujaaa, anapendwa na Mungu nani tajiri japokuwa yeye Gideoni aliona hapendwi na Mungu na kwamba Mungu amemuacha napia yeye ni masikini kama tunavyoona Gideoni akiongea na Malaika wa Bwana.
Waamuzi 6:1-16 “1 Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba 2 Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. ………………….. 7 Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani, 8 Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; …………. 11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. ………. 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. 16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.”
Kumbe tatizo lililo kwamisha maisha ya Gideoni na kushindwa kuishi kama vile Mungu alivyompangia ni madhabahu ya baali katika eneo lile ambayo baba yake na Gideoni alikuwa ndiye kuhani wa madhabahu. Sasa unaweza kuona kuwa Gideoni hakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na madhabahu ya baali ila baba yake ndiye aliyekuwa kuhania wa madhabahu na hali hiyo ikakwamisha maisha ya Gidioni mpaka alipoivunja ile madhabahu.
Waamuzi 6:25-31 25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. 27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. 29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. 30 Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. 31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake.
Baada ya Gidioni kugundua tatizo na kuvunja madhabahu ya baali na kumtumikia Mungu wa kweli tunaona mambo yanabadilika na maisha ya Gidioni yanakuwa mazuri na Israeli wanaondoka katika mikono ya Wamidiani na kuishi kwa amani kama tunavyosoma katika Waamuzi 8:28 “Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni.”

Laana zilizompata Kaanani kwa kosa la baba yake, Hamu.

Neno la Mungu linatufundisha kuwa baada ya gharika kipindi Nuhu, Nuhu alikuwa mkulima mzuri na alilima zabibu na kutengeneza divai akalewa akawa uchi, akiwa uchi mtoto wake Hamu (Baba yake Kaanani) akamuona uchi wake lakini hakumfunika akaenda kuwaambia ndugu zake (Shemu na Yafethi) na hao ndugu zake ndio walio kuja kumsitiri baba yao (Nuhu). Mwanzo 9:20-23 “20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; 21 akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. 22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23 Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.
Jambo alilolifanya Hamu lilimuudhi sana baba yake “yaani Nuhu”, hivyo Nuhu akatamka laana; Mwanzo 9:24-27 “24 Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. 25 Akasema,Na alaaniwe Kaanani;Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. 26 Akasema,Na atukuzwe Bwana,Mungu wa Shemu;Na kaanani awe mtumwa wake. 27 Mungu akamnafisishe Yafethi,Na akae katika hema za Shemu; Na kaanani awe mtumwa wake.” Jambo la kushangaza hapa ni kwamba kwanini laana haikutamkwa kwa Hamu aliyefanya kosa? Tunachokiona hapa ni kwamba laana zinamuendea Kaanani mtoto wa Hamu ambaye hakuhusika na kosa hilo. Hivi ndivyo laana zilizotamkwa na watu kwa wazazi wako zilivyokufikia hata kama hukushiriki katika kufanya jambo hilo.

FAHAMU KWAMBA YESU ALICHUKUA LAANA ZETU

Neno la Mungu linasema katika waraka wa mtume Paulo kwa Wagalatia 3:13-14, 29 “13 Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; 14 ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani……..29 Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”
Wakati mwingine katika maisha ya ukristo, wakristo wamekuwa wakiishi maisha yenye taabu na mateso mengi kutokana na laana ambazo wamerithi kutoka kwa wazazi/mababu na mabibi/wahenga (vizazi vya zamani sana). Hata wewe unayesoma sasa; hebu jaribu kurudi nyuma miaka 150 hadi 200, mababu zako wote walikua waabudu miungu (walimwabudu shetani) nasema hivyo kwani ukristo uliingia Afrika na Tanzania kati ya miaka 100 – 150 iliyopita na kabla ya hapo babu zetu walimwabudu shetani (kupitia mizimu). Kama ndivyo basi kuna laana ambayo ilisababishwa na mababu zetu nasi tumeirithi hiyo laana na inaleta madhara makubwa katika maisha yetu kama madhara yaliyompata Gideoni na Rehoboamu kama tulivyojifunza hapo awali.
Lakini unapompokea Yesu Kristo yeye anayabeba maovu na makosa yetu ambayo yalisababisha laana katika maisha yetu na sisi tunapokea uponyaji wa laana zote sawa na Neno la Mungu kutoka Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Ni ukweli kwamba baba zetu walitenda dhambi na sisi tumerithishwa maovu yao (Maombolezo 5:7 “Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.”) lakini ni ukweli kwamba baada ya kifo cha Yesu dhambi zetu zote zimefutwa kwa damu ya Yesu na hakuna laana yoyote tena inayoweza kukushinda, wewe unapaswa kuamini kuwa damu ya Yesu inaweza kukuosha uovu wote.


MAOMBI

1.      Omba toba kwa dhambi na maovu na makosa waliyofanya wazazi na mababu (Soma Zaburi 51 na Daniel 9:1-11
2.      Fanya ukiri wa nguvu ya damu ya Yesu katika kukusafisha dhambi, maovu, makosa na laana zote (Soma Isaya 1:18, Waebrania 12:24, Isaya 53:5, Wagalatia 3:13)
3.      Kwa jina la Yesu kata laana zote ulizosababisha mwenyewe, ulizorithishwa na wazazi/mababu au ulizorushiwa na mawakala wa shetani, achilia damu ya Yesu kufuta historia mbaya zote zilizoandikwa kuzimu ili kukufuatilia (Soma Ufunuo 12:11)
4.      Mshukuru Mungu kwa kukuhamisha kutoka katika laana na kukuingiza katika Baraka na katika Nuru yake (Soma Wagalatia 3:-29, Wakolosai 1:12-14)

MAOMBI YA KUFUNGULIWA MACHO YA ROHONI

MAOMBI YA KUFUNGULIWA MACHO YA ROHONI
(Maombi haya yametoka Waefeso 1:17-23, 2:6)

Mungu wa Bwana wangu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, unipe mimi roho ya hekima na ya ufunuo katika kukujua wewe; macho ya moyo wangu yatiwe nuru, nijue tumaini la mwito wako jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wako kwangu mimi mtakatifu jinsi ulivyo; Nijue  ubora wa ukuu wa uweza wako ndani yangu mimi niaminie jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wako; ulioutenda katika Kristo ulipomfufua katika wafu, ukaniketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho. Ukamweka mkono wako wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; ukavitia vitu vyote chini ya miguu yake, ukamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake.

Samson Mollel
Uzima wa Milele International Ministries +255 767 664 338
www.uzimawamileleministries.blogspot.com