Saturday, August 27, 2016

TAIFA TAKATIFU

JITAMBUE YAKUWA WEWE NI TAIFA TAKATIFU KWA MUNGU ALIYE HAI/MPATE YESU ILI UWE TAIFA TAKATIFU KWA MUNGU ALIYE HAI
Imefundishwa na Mtumishi Isaac Ridhiwan Omary (Semina ya MVUMO – Morogoro, 26th August 2016)
Imeandikwa na Samson Mollel – 0767 664 338 (www.uzimawamileleministries.blogspot.com)

Kumbukumbu la torati 26:16-19 “16 Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote. 17 Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; 18 naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; 19 na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.”

Kumbukumbu la torati 7:6 “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”

Somo la leo lina vichwa viwili kama ifuatavyo
         i.            Kama umeokoka – “JITAMBUE YAKUWA WEWE NI TAIFA TAKATIFU KWA MUNGU ALIYE HAI”
       ii.            Kama haujaokoka -  “MPATE YESU ILI UWE TAIFA TAKATIFU KWA MUNGU ALIYE HAI”

Ukizungumza kuwa wewe ni Taifa kwa Mungu bila ya kujua thamani ya utaifa hauwezi kuelewa vizuri.

Kama leo ungepewa na Mungu nafasi ya kuchagua uzaliwe bara/nchi ipi, na ukaangalia duniani kila nchi ilivyo ndipo uchague, kila mtu anayosababu ya msingi angechagua nchi gani (Wengi katika mkutano wamechagua nchi za ulaya na Marekani)

Nchi za wenzetu (ulaya na Marekani) wanayotabia ya kuwajali sana watu wa taifa lao mahali popote walipo. Kwamfano pakitokea vurugu yoyote ambayo hata haijafikia kuwa ni vita katika nchi yoyte ambayo raia wa Marekani wapo, mara moja utasikia Marekani inawarudisha raia wake; hivyo watawatumia ndege na wanajeshi wa kuwarejesha kutoka mahali popote duniani walipo ili wasije wakadhurika na machafuko.

Sasa kama nchi za wanadamu wanaweza kufanya hivyo; si zaidi sana ukiwa taifa la Mungu?

Wewe haijalishi katika mwili umezaliwa wapi, kuzaliwa Tanzania ni kusudi la Mungu. Mungu anakufanya wewe kuwa Taifa lake.

Unapotaka kwenda kwenye taifa Fulani (mfano marekani), hauwezi kujiamulia tu kwenda bila kufuata taratibu za kuingia katika taifa hilo. Hii ni kwasababu nchi ya Marekani inayo mipaka yake na sheria zake na utaratibu wa namna ya kupokea wageni.

Hivyo basi unapotaka kwenda marekani lazima uwe na kusudio linalofahamika na kukubalika na taifa la marekani ili uruhusiwe kuingia katika nchi yao.

Kuwa taifa la Mungu ni zaidi ya kuwa mtumishi wa Mungu. Kuwa taifa maana yake unakuwa na watu wako, unakuwa na mipaka yako, unakuwa na utaratibu na kanuni na sheria za kufuata. Na kwasababu hiyo huwezi kuruhusu kila mtu kuingia katika taifa lako bila ya kufuata taratibu na sheria za taifa lako.

Unapokuwa taifa la Mungu unakuwa umekubali kufuata sheria na taratibu za taifa la Mungu kama ilivyoandikwa kuwa umemkubali BWANA na sheria zake nayeye amekukubali ili uzifuate hizo sheria/maagizo yake:

Kumbukumbu la torati 26:17-18 “17 Umemwungama [UMEMKUBALI] Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; 18 naye Bwana amekuungama [AMEKUKUBALI ]hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote;”

Na kwasababu hiyo; kwakuwa umekubali kufuata sheria na taratibu za Taifa la Mungu naye Mungu amekukubali wewe, basi umekuwa Taifa la Mungu na unaishi kwa kufuata sheria za Taifa la Mungu.

Kumbukumbu la torati 7:6 “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”

Ukiwa taifa mbele za BWANA wewe ni mmoja katika ya wengi “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana” na wengi katika mmoja “amekuchagua kuwa watu wake hasa


TANGU UMERUHUSU WATU KUINGIA KATIKA MIPAKA YAKO UMEKWAMA
Basi sasa kwakuwa umefahamu kuwa wewe ni Taifa kwa Mungu, huwezi kuruhu kila mtu akaingia katika mipaka yako.

Tangu umekaribisha watu fulani katika maisha yako mambo yako yamekwama, tangu umeruhusu watu Fulani washauri kwenye ndoa yako ndoa imekwama, tangu uwaruhusu watu fulani kwenye biashara, kazi, masomo, huduma vyote vimekwama.

Wewe haukujua kwamba ni Taifa, na haupaswi kumruhusu mtu yoyote kuingia kwenye taifa lako bila kufuata sheria ya ufalme wa Mungu hata kama mtu huyo ameokoka. Pale ulipowaruhusu watu waingie wameingia na miungu yao na umepata matatizo katika Taifa lako.

Kuna watu umewakaribisha katika huduma yako kwasababu wameokoka kumbe wao sio wa Taifa lako.

Kuna watu umewashirikisha kwenye biashara, kazi, masomo, uchumi na mambo mengi ya maisha yako kumbe sio wa Taifa lako na mambo yako yameharibika, wewe ulidhani ni ndugu zako au watu wa karibu yako lakini wamekusababishia matatizo makubwa (Mathayo 10:36 “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.”)

Fahamu yakuwa watu wote wanaoingia ndani ya mipaka yako wanayo nafasi kubwa ya kuathiri maamuzi yako.

Ukishakuwa Taifa la Mungu mbingu ndio zinatawala, serikali ya Mungu ndio inatawala ndani ya utaifa wa ki-Mungu

Hao watu walioingia ndani ya mipaka usigomabne nao wewe kwakuwa kuna mkono wa BWANA utawachomoa na kuwatoa nje ya mipaka yako kwa jina la YESU, mkono wa BWANA unawatoa sasa nje ya ndoa yako, nje ya kazi yako, nje ya huduma yako, nje ya ukoo na familia yako, nje ya miradi yako, nje ya kila mpaka waliongia wanatolewa sasa kwa mkono wa BWANA kwa jina la YESU.

KWA MASOMO MENGINE BOFYA HAPA: www.uzimawamileleministries.blogspot.com

Friday, August 26, 2016

KUKATA KAMBA ZA UOVU NA LAANA NA KUFUTA MAAGANO NA MAUTI

Imefundishwa na Mtumishi Isaac Ridhiwan Omary (Semina ya MVUMO – Morogoro, 25th August 2016)
Imeandikwa na Samson Mollel – 0767 664 338 (www.uzimawamileleministries.blogspot.com)


Ezekieli 18:1-4 “1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 2 Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? 3 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. 4 Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.”

Isaya 28:15-18 “15 Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; 16 kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka. 17 Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri. 18 Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.”

Jambo la kwanza la kuangalia katika somo hili:
Nakubalina kabisa na wala sipingani na ukweli kwamba laana/uovu/mapigo kutoka kwa wazazi hufutilia vizazi hata kama mtoto hakufanya jambo hilo ubaya uliosababishwa na wazazi unaweza kumpata, huu ni ukweli kabisa na inawezeka kutokea kabisa kwakuwa ni Mungu mwenyewe amesema, imeandikwa katika Kutoka 20:5 “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”)
Lakini kuna sehemu tunaacha katika hilo agizo la Mungu ya kuwa Mungu anawarehemu wale wanaoshika amri zake, tunasahau kuwa Mungu ni wa rehema, imeandikwa katika Kutoka 20:6 “nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.”
Haijalishi umefungwa kiasi gani na laana/uovu wa kifamilia. Katika dunia nzima ufunguo wa kutoka katika kifungo haujakabidhiwa kwenye dini au dhehebu Fulani au taifa lolote unalolijua au usilolijua, hata taifa la Mungu Israeli hawajaachiwa huo ufunguo wa kumng’oa mtu kwenye hiyo laana. Funguo anazo Yesu peke yake kama tunavyosoma katika Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.. Usidanganywe kuwa kuna dini/dhehebu ambalo limeshikilia hizo funguo kwamba hakuna mtu mwingine anayemiliki na anayeweza kufungua, usiwasema watu wa dini au dhehebu lingine; unapokaa katikati ya watu wa madhehebu/dini tofauti ongelea habari ya ubora wa Yesu mwenye funguo na sio ubora wa dini/dhehebu.

Unapotaka kufunguliwa na Yesu ili kuwa huru kabisa zingatia mambo yafuatayo
  •          i.            Tembea na Neno la BWANA
  •        ii.            Kuwa muombaji/Fanya maombi
  •      iii.            Kuwa mtoaji wa sadaka

Ukitembea na mambo hayo lazima utafanikiwa
Kama kuna jambo lolote la laana/uovu au majini/mizimu, hilo jambo linalokusumbua libebe na ulipeleke pale msalabani, haijalishi watu wamekunenea maneno ya jinsi gani au laana za jinsi gani, wewe beba na upeleke pale msalabani kwa Yesu (Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”) Vilevile imeandikwa katika Wakolosai 2:3-4 “13 Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; 14 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;” 
Kuna nguvu ya ziada kwenye madhabahu ya Yesu Kristo inayozidi nguvu zingine zote, inazidi nguvu za majini , laana, mizimu, makaburi, ajali, magonjwa. Ni kazi ya Yesu kubeba laana na madhaifu mengine yote na akiisha kubeba hizo laana anaachilia Baraka, anaachilia uzima na afya. Ndipo linatimia lile Neno kutoka Ezekiel 18:3 “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli.” Hautakuwa na sababu tena ya kuitwa umeirithi laana ya mababu au umeurithi ugonjwa au taabu yoyote ile kwani Yesu anakuwa amezichukua zote na kukuachia Baraka zake.


Jambo la pili la kuangalia katika somo hili:
Kuna watu wanayo maagano na mauti na mapatano na kuzimu Isaya 28:15 “15 Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;” Watu hawa vita yao kubwa wanaielekeza kwa wana wa amani (Yerusalemu).
Yaani baada ya kukata kamba za laana na kuzipeleka msalabani, baada ya kutoka kwenye balaa na mikosi ya kifamilia kwa nguvu ya madhabahu ya Yesu Kristo. Huko duniani kuna watu wanayo maagano na mauti na mapatano na kuzimu ambao ukikutana nao tu wanakunenea/unabii wa kipepo kuharibu maisha yako na Baraka zako.
Zipo roho za uonevu ambazo zinawavaa watu wasiojua kutembea na ulinzi wa Yesu Kristo, roho hizi zinaweza zikakuvaa darasani, kazini, shambani, kwenye biashara, uwanjani unapocheza mpira, njiani unapopita, kwenye basi/daladala unapopanda. Yaani unakuta kuna mtu/watu wameweka mazindiko yao kwa sababu zao ambazo hata hazikuhusu lakini kwakuwa umepita maeneo yao kama nilivyotaja hapo juu hizo roho zinakuvaa na kukutesa.
Isaya 28:16 “kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka”.
Yesu Kristo ndio jiwe la pembeni, ukiwa ndani ya Yesu Kristo kama BWANA na mwokozi wa maisha yako hawataweza kukuonea au kukunyanyasa.
Unapokuwa na Yesu Kristo yeye ambaye ni jiwe la pembeni; kila jambo unalolifanya fanya ukiwa juu ya jiwe, ukijenga jenga juu ya jiwe, ukihudumu hudumu juu ya jiwe, ukisafiri safari juu ya jiwe, ukisoma, ukifanya biashara, ukilima, ukifanya kazi vyote fanya juu ya jiwe na hakuna kitu kitakushinda. Hakuna laiyefanya mapatano/maagano na mauti na kuzimu atakayekuweza kwa jina la YESU.

 KWA MAFUNDISHO ZAIDI TEMBELEA: www.uzimawamileleministries.blogspot.com


Thursday, August 25, 2016

UCHAWI NDANI YA KANISA LA MUNGU

Samson Mollel – Uzima wa Milele International Ministries +255 767 664 338

www.uzimawamileleministries.blogspot.com

Uchawi ni nguvu ya giza isiyoonekana na macho ya kibinadamu ikiwa na lengo la kuleta uharibifu kwenye maisha ya watu. Nguvu hii hutenda kazi kwa kuloga, kuloga ni maneneo/manuizo ya uharibifu yanayotamkwa kwa imani kubwa ili kuleta madhara kwa mtu aliyekusudiwa.
Biblia inamtambua mchawi katika mazingira tofauti tofauti, moja kati ya mazingira hayo ni pale mtu anapokuzuia wewe kutimiza lile kusudi ambalo Mungu amekupangia katika maisha yako, huyo anayekuzuia kulitimiza kusudi la Mungu ni mchawi hata kama ni mtumishi wa Mungu (Askofu, Nabii, Mtume, Mchungaji, Padri, Katekista n.k.). yeyote anayekukwamisha usifikie lengo lako katika kuylitimiza kusudi la Mungu huyo ni mchawi wako hata kama ni ndugu yako wa karibu (Baba, Mama, Kaka, Dada, Shangazi, Mjomba n.k.) kwani Yesu alisema “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.” (Mathayo 10:36). Maana yake ni kwamba yeyote anayekukwamisha katika maisha yako (Mchawi) lazima awe anakufahamu vizuri njia zako, uimara wako na udhaifu wako, kimsingi lazima awe anakujua ili aweze kukusababishia ukwazo/kukwama.

MAKUHANI WA KICHAWI
Ninasema kuwa mtu yeyote anayekusababishia ukwazo/mkwamo katika maisha yako ili ushindwe kulifikia lile kusudi la Mungu huyo ni mchawi kwani Biblia imewatambua hivyo. Ukisoma habari ya Baalamu katika kitabu cha Hesabu utaona jinsi gani Baalamu alikuwa ni Nabii wa Mungu na alimtegemea Mungu na alikuwa akipokea maelekezo kutoka kwa Mungu, pamoja na kuwa yeye ni kuhani wa Mungu aliye hai, Baalamu alianza kukubali kumsadia Balaki mfalme wa Moabu Hesabu 22:7-8 “7 Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. 8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu..”.
Baada ya Balaki mfalme wa Moabu kuwaona wana wa Israeli wakiijia nchi ya Moabu kwa mbali wakielekea nchi ya ahadi aliogopa kwakua alisikia mambo makuu Mungu aliyotenda kwa habari ya Israeli juu ya mataifa mengine kwamba Israeli iliwapiga mapigo makuu, hivyo akwatuma wajumbe wake Nabii Baalamu aliyejua habari za Mungu wa kweli ili awalaani Israeli Hesabu 22:5-6 5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. 6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”

Ukiendelea kwa wakati wako soma Hesabu mlango wa 22 na 23 utaona kuna wakati BWANA alitaka kumwangamiza kabisa Baalamu kwakuwa alitia nia ya kuweka ukwazo kwa wana wa isareli japokuwa BWANA alimkataza hapo awali Hesabu 22:12 “Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”. Lakini Baalamu aliendelea kumsadia mfalme wa Moabu kufanya jitihada mbalimbali ili kuwazuia wasifike katika nchi ya Moabu wakielekea nchi ya ahadi.

Hayo yote aliyoyafanya Baalamu pamoja na kuwa ni Nabii wa Mungu ni uchawi, na ndio maana tunasoma katika Yoshua 13:22 “Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.”.

Sasa kumbe inawezekana kabisa kuwa na kuhani wa Mungu aliyekengeuka na kufuata namna ya dunia na akafanya uchawi katika maisha ya watu wa Mungu, yaani akawa anatia ukwazo/kukukwamisha katika kila mipango inayokupelekea kulitimiliza kusudi la Mungu kama alivyofanya Baalamu pamoja na maonyo yote aliyopewa na Mungu juu ya kuwalaani wana wa Israeli. Ashukuriwe BWANA anayetupigania na kutushindia ambaye aliwawezesha Israeli kushinda na kumwua kabisa Baalamu na kuthibitisha lile Neno la Mungu alilonena kupitia kinywa cha Baalamu yakwamba “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!” (Hesabu 23:23)

MANABII WA KICHAWI
Wakati mwingi wachungaji wamekuwa wakiwafundisha washirika wao habari za wokovu na kuacha dhambi lakini washarika wanonekana kama wameelewa ila wakitoka nje ya kanisa wanakuwa kama vile sio wao waliokuwa wakifundishwa habari wokovu, utawakuta ni walevi, wazinzi waasherati na kila jambo la uovu linafanywa kupitia hao washarika waliofundishwa habari za Kristo.

Baadhi ya makanisa hata wameweka utaratibu wa kuwatenga wakristo wao (kuwaweka kwenye uangalizi maalum au kuwaonya) ili wasishiriki katika baadhi ya huduma za kikanisa na hata makanisa mengine yamewafukuza kabisa baadhi ya waumini bila kujua hilo sio suluhisho kwani mara nyingi sio wakristo wanao fanya hayo ila ile roho ya mpinga Kristo ndio inayotekeleza hayo na wakati mwingine kupitia hao hao viongozi wa kanisa.

Tunasoma katika Matendo 13:6 – 12 “6 Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; 7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. 9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, 10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? 11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. 12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.” Kuna wakati sio tatizo la Mkristo kutoelewa ila ni tatizo la kiongozi kutoangalia kwa macho ya rohoni kwanini wakristo hawafunguliwi na mafundisho/mahubiri yanayotolewa kila siku katika nyumba za ibada. Hapa tunamuona mtu anaitwa Bar-Yesu au Elima akimzuia Yule liwali aliyeitwa Sergio Paulo asiweze kuelewa anachofundishwa na mtume Paulo. Yaani wapo watu ambao wanajifanya kuilewa njia ya kweli lakini lengo lao ni kuipotosha na kuwaangusha wakristo, inawezekana ni kwa matamshi yao au kwa kutumia nguvu za giza kuwapiga bumbuwazi la mawazo washarika na hii inapelekea washarika kukaa wakisikiliza pasipo kuelewa kila jumapili na miaka inazidi kwenda nao wanzidi kupotea.

Vilevile wapo manabii wa uongo (ambao kimsingi ni manabii wa Jehova lakini kwa tamaa zao binafsi wameamua kusema uongo). Tunasoma katika 1Falme 13:1-24 “1 Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba …………... 5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana………………………….7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu. 8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa; 9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. ……………………11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao…………………………..14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye. 15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula. 16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa; 17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. 18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo. 19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake. 20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha; 21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, 22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako………………..24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.” Kumbe wapo manabii wanosema BWANA kasema lakini wanatumia akili zao wenyewe na wala BWANA hajasema Neno lolote, manabii kama hawa ni wa uongo kwakuwa huyasema mawazo yao na maneno yao na sio kusudi la BWANA.

Kazi hii (Unabii wa uongo) unafanywa na shetani mwenyewe kupitia mawakala wake ambao wanahakikisha ile kazi ya kuwapofusha wakristo inaenda kwa kasi kubwa ili wazidi kutiwa giza na wasiione Nuru (Yaani Yesu Kristo) 2Korintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

Ni maombi yangu kwako mtu wa Mungu Nuru ya BWANA ikujie sawa na Isaya 60:1 “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.”  na pia namuomba Mungu akufungue macho yako wewe unayesoma somo hili uelewe ulichokisoma na utakachoendelea kusoma kama vile Paulo alivyowaombea Waefeso katika Waefeso 1:17-19 “17 Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; 18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; 19 na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;”

MADHABAHU ZA KICHAWI
Inawezekana umestuka kuwa inawezekanaje ndani ya kanisa kukawa na madhabahu za kichawi, ni kweli kuna madhabahu za kichawi ndani ya kanisa ambazo kazi yake ni kupingana na kazi ya Mungu. Hii madhabahu ni ya shetani mwenyewe lakini ipo ndani ya kanisa la Mungu na wapo makuhani wa shetani wanaoihudumia; kama inavyofahamika kuwa panapokuwa na madhabahu lazima awepo na kuhani wa madhabahu hiyo. Ufunuo 2:12-13 “12 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili. 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.” Hapa Bwana Yesu mwenyewe anatuma barua yake kwa kanisa la Pergamo ambalo mahali lilipo ndipo penye kiti cha enzi cha shetani, na kama tunavyofamu kuwa mahali penye kiti cha enzi cha ufalme Fulani ndipo makao makuu ya ufalme huo yalipo (Ikulu), vilevile mahali penye kiti cha enzi cha shetani ndipo mahali palipo na madhabahu ya shetani. Hii ndio maana utashangaa kuona Yesu analiambia kanisa la Pergamo kwamba katikati ya kanisa ndipo alipouwawa shahidi wa Yesu Antipa “…….hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.”.

Unaweza kuwa unawaza kuwa haya yalitendeka zamani na sasa hayapo, ninakuhakikishia yapo tena kwa wingi ajabu. Ninaposema yapo usije ukamtazama mchungaji wako ukadhani yeye ndiye tatizo au mwinjilisti n.k.; inawezekana kabisa wakatumiwa na shetani kuweka ukwazo katika kazi ya Mungu ili isisonge mbele, lakini hata mkristo wa kawaida au mzee wa usharika au kiongozi yeyote ndani ya kanisa la Mungu anaweza kutumika kama kuhani wa madhabahu ya shetani. Kulingana na maneno ya Yesu mwenyewe inaonekana kuwa kanisa la Mungu (Watakatifu) wamejitahidi kuishi kwa uaminifu “…………..nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu………” lakini pamoja na kulishika jina la Yesu kwa uaminifu bado kuna shida ndani ya kanisa kwani yesu anasema katika Ufunuo 2:14-15 “14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. 15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.” Yesu anasema kuna watu ndani ya kanisa wanaohudhuria kanisani lakini hawafuati mafundisho matakatifu ila wanashika mafundisho ya mizimu na kipepo (yaani ya kichawi)


WASIO HAKI NA WAOVU WAKISTAWI

WASIO HAKI NA WAOVU WAKISTAWI
Samson Mollel 0767 – 664 338

WASIOHAKI NA WAOVU NI NANI?

Wasio haki na waovu ni watu wasiotenda mapenzi na makusudi ya Mungu, ni wale watu wanaotenda kinyume na maagizo ya BWANA. Ipo mifano mingi sana ya wasio haki, ifuatayo ni baadhi ya mifano ya wasio haki na waovu:-

Ø  Wasio haki na waovu ni wale wasio kwenda katika sahuri la BWANA

Zaburi 1:1-4 “1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. 2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. 3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. 4 Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

Ø  Wasio haki na waovu ni wale wanaoshindana na wateule wa Mungu

Zaburi 11:2 “Maana, tazama, wasio haki wanaupinda uta, Wanaitia mishale yao katika upote, Ili kuwapiga gizani wanyofu wa moyo.”

Ø  Wasio haki na waovu ni wauaji

Zaburi 37: 14 “ Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu.”

Ø  Wasio haki na waovu ni wale wenye hila na wategao mitego

Yeremia 5:25-26 “25 Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate. 26 Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu. 27 Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali. 28 Wamewanda sana, wang'aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.”


MALALAMIKO YA WATAKATIFU KWA MUNGU
Watakatifu wengi, yaani wale walioitwa kwa jina la Yesu na wamempokea Yesu wamekuwa na malalako/kilio kwa Mungu. Sababu ya kilio/malalamiko haya ni kumhoji Mungu kwamba kwanini wasio haki na waovu wanafanikiwa lakini watakatifu hawafanikiwi, na pia kwanini wanapata mali kwa njia isiyo halali na kuwaonea watoto wa Mungu?

Zaburi 94:3-5 “3 Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia? 4 Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi? 5 Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako;”

Watakatifu wanamlilia Mungu na kumweleza kuwa wasio haki na waovu wamewadharau hadi wanasema Mungu hasikii; Zaburi 94:7 “Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.”

Lakini Mungu anajibu na kusema na wasio haki na waovu na kuwaonya kuwa yeye anajua na kufahamu kila kitu kwakuwa ndiye muumbaji, Zaburi 94:8-11 “8 Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? 9 Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione? 10 Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? 11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.”

Zaidi sana BWANA anasema kuwa hakuna sababu ya kushangaa kwanini waovu na wasio haki wanafanikiwa kwanini huo ni mpango wake kwa kusudi lake; Zaburi 92:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;”


MUNGU HUSHUGHULIKA NA WASIO HAKI

Kama tunavyosoma katika Zaburi 92:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;”

Mungu mwenyewe anawashughulikia wasio haki na waovu ambao wamekuwa wakiwatesa watakatifu wa Mungu.

Zaburi 3:7 “Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu wote; Umewavunja meno wasio haki.”

Zaburi 17:8-9 “8 Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako; 9 Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.”

Zaburi 37:10, 13 “10 Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.13 Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.”

Zaburi 75:10 “Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.”

Mithali 13:22 “22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.”


MAOMBI YA KUWAPIGA WASIO HAKI

Zekaria 2:8-9 “8 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. 9 Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma.”

Hesabu 23:22 “Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.”

1Samwel 2:10 “Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.”


WASIO HAKI NA WAOVU WAKISTAWI
Samson Mollel 0767 – 664 338


ZIFUTE NA KUZIKATAA KALENDA ZA KIPEPO ZISIFUATILIE MAISHA YAKO WALA UZAO WAKO

Imefundishwa na Mtumishi Isaac Ridhiwan Omary (Semina ya MVUMO – Morogoro, 24th August 2016)

Imeandikwa na Samson Mollel – 0767 664 338 (www.uzimawamileleministries.blogspot.com)

Mwanzo 24:63-67 “63 Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. 64 Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. 65 Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. 66 Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. 67 Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.”

Matendo 12:1-4 “1 Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. 2 Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. 3 Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. 4 Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.”

Unapoongelea habari ya uzao ni kila aina ya mbaraka ambazo Mungu ameruhusu zizaliwe ndani yako iwe katika Afya, ndoa, Elimu, Biashara……

Shetani ndiye adui yetu mkubwa (Mratibu wa  kila aina ya uovu), ndiye chanzo cha kila aina ya uharibifu.

Anapofanya uharibifu shetani, kila tarehe anayofanya huo uharibifu anaweka kumbukumbu (anarekodi). Kumbukukumbu hiyo ya uharibifu au ya jambo baya kutoka kuzimu hujirudia kila mwaka wakati na majira yaleyale kama ilivyorekodiwa katika kalenda za kipepo.

Tunachokitafuta hapa leo ni hiyo nguvu inayopelekea hilo tatizo kujirudia
Kwamfano Ibrahimu alimdanganya mfalme wa Gerari (Abimeleki) kuwa Sara ni dada yake na Mungu akamuonya Yule mfalme kwa habari ya dhambi ambayo alikaribia kuifanya. Mazingira kama yale yale (Majira yale yale) Isaka naye akamdanganya Abimeleki (Mfalme wa wafilisti huko Gerari) Kuwa Rebeka ni dada yake.

Mwanzo 24: 67 “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

Isaka hata kabla ya kumtwaa Rebeka kama mke wake (Kabla ya kulala naye) alimuingiza kwenye hema ya mama yake Sara ambaye alikuwa ni tasa kwa muda mrefu, baada ya kumuingiza katika hema ya mama yake ndipo akamtwaa (akalala naye) katika hema ya mama yake. Hapo Rebeka akachukua ile roho ya utasa iliyomsumbua Sara mama yake Isaka

Swali lililopo hapa, Ni nguvu gani iliyompeleka Isaka akalala na Rebeka kwenye hema ya mama yake Sara, na nguvu hii inatumwa na nani?

Shetani anayotabia ya kufuatilia panapo majira yaleyale, Yesu aliuawa majira yaleyale, akafuata Stephano, akafuata Yakobo hala akakamatwa na Petro majira yaleyale.

Ni kwanini Stephano hakuokolewa, ni kwanini Yakobo hakuokolewa na ni kwanini Petro aliokoka na kifo kutoka kwa Herode? Ni kwasababu kanisa lilimlilia Mungu na kuomba kwaajili ya Petro.

Matendo 12:5, 7 “5 Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. 7 Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.”

Kumbe kabla ya hapo kanisa lilikuwa limepigwa usingizi wa kipepo hata lisikumbuke kuomba kwaajili ya Stephano na Yakobo. Lakini kanisa lilipoamka likafuta kalenda ya kipepo/kishetani ya kurudia matukio ya uharibifu majira yale yale

Isaka naye baada ya muda mrefu alimlilia BWANA na Mungu akamsikia na kufuta kalenda za kishetani juu ya maisha yake

Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.”

Kumbe ukinyamaza wewe na mbingu zinanyamaza na ukitaa kalenda za kipepo na mbingu zinakataa, ukifunga wewe na mbingu zinafunga, ukifungua na mbingua zinafungua. Hivyo ukikaa kimya ukanyamaza na Mungu naye ananyamaza.

Wapo watu wamewekewa nembo mbalimbali katika maisha yao na uzao wao na wamenyamaza, na kila yakifika majira yaleyale mambo mabaya huwapata kulingana na kalenda ya uharibifu ya kuzimu ilirekodi jambo gani, inawezekana ni kutokuolewa, kutokujenga nyumba, kuzaa nyumbani, utasa, ajali, kansa n.k.



MAOMBI YA KUFUTA NA KUKATAA KALENDA ZA KIPEPO

Tuesday, August 23, 2016

UWATAKASE KWA ILE KWELI

UWATAKASE KWA ILE KWELI
Samson Mollel 0767 – 664 338

Kweli ni nini? – Kweli ni Roho kutoka kwa Mungu Neno la Mungu yaani Yesu mwenyewe

ü  Kweli inatakasa

Unaposoma kitabu cha Injilia ya Yohana 17 tunaona maombi ya Yesu kwa Baba yake akituombea sisi wanadamu, zaidi sana anatuombea ulinzi dhidi ya nguvu za giza (shetani) na kumuomba Baba atutakase kwa ile kweli ambayo ni Neno la Baba.

Yohana 17:17 “14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. 15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 Uwatakase kwa ile kweli; NENO LAKO NDIYO KWELI.”

ü  Neno Yaani Yesu ndio Kweli

Tukisoma katika Yohana 1, tunajifunza jambo jingine ambalo linafungua macho ya mioyo yetu na kutufundisha kuwa Neno (Yaani ile kweli) alikuwa tangu mwanzo na Neno aliumba vitu vyote na wala pasipo Yeye (Neno) hakuna kitu amabacho kingeumbwa

Yohana 1:1, 14 “1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu……… 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; AMEJAA NEEMA NA KWELI.”

ü  Kweli Itakuweka Huru mbali na kuonewa

Napenda ufahamu sasa kama ukimpokea Yesu kwa kumaanisha ndani yako, unakuwa umeipokea ile kweli na ukiipokea ile kweli ndipo utakapokuwa huru mbali na uongo na kuonewa.

Yohana 8:31-32 “31 Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; 32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo KWELI ITAWAWEKA HURU.”


SHETANI NI CHANZO CHA UONGO

Fahamu ya kwamba shetani ni baba wa uongo ambaye anaweza kulitumia Neno la Mungu na kukupotosha kama wewe hauna nguvu ya Mungu na ufahamu wa ki-Mungu ndani yako

Mwanzo 3:1-5 “1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. 4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

Ninachotaka ufahamu hapa ni kwamba shetani alifahamu wazi wazi kuwa wakila tunda lile watakufa lakini aliwaambia uongo ili wapotee kwakuwa Mungu alishawaonya na kumwambia Adamu kuwa asile yale matunda ya mti wa katikakati na kama atakula basi atakufa hakika.

Mwanzo 2:16-17 “16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”


WOTE WAUPENDAO UONGO WANAMTUMIKIA SHETANI
Kimsingi au jambo la muhimu unapaswa kulifahamu ni kwamba shetani ndie uongo mwenyewe, yaani kila uongo unaotokea chanzo chake ni shetani kama Neno la Mungu linavyotufundisha.

Yohana 8:44-45 “44 Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. 45 Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.”


UONGO NI ROHO
Kama vile zilivyo roho zingine za uzinzi/uasherati/umasikini…. uongo nao ni roho, yaani pepo linaweza kutoka kuzimu au katika madhabahu yoyote ya kichawi na kuwa roho ya uongo na kumtawala mtu kwa lengo la kuwapotosha watu au mtu Fulani.

1Wafalme 22:20-22 “20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. 22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.”


Samson Mollel 0767 – 664 338