MILANGO YA FAHAMU KATIKA HALI YA MWILI
Milango ya fahamu ni ogani za mwili
zinazoturuhusu kujua na kuyamudu mazingira yetu kwa usahihi. Kibailojia
inaelezwa kuwa ogani yenye uwezo wa kupokea habari za nje ya mwili kama vile;
Nuru, Sauti, Halijoto, Mwendo, Harufu na ladha ili kuzibadilisha katika mfumo
wa kiumeme inachukuliwa kwa njia ya mfumo wa neva hadi kwenye ubongo.
Kuna milango mitano ya fahamu katika mwili wa
mwanadamu ambayo ni Jicho/Macho (Kuona), Sikio/Masikio (Kusikia), Pua (Kunusa),
Ulimi (Kuonja) na Ngozi (Kugusa)
Kama milango ya fahamu imeharibika,
tunasema mtu ni kipofu, bubu au kiziwi, ana matatizo kuelewa
mazingira yake sawa na jinsi wanavyoweza watu wengine.
Milango ya fahamu ni muhimu sana kwa viumbe hai kutokana na kwamba inasadia kiumbe hai
katika shughuli zake za kila siku, hasa katika kufatuta mahitaji muhimu.
MTU NI ROHO
Biblia
inasema wazi kwamba hapo mwanzo Mungu aliamua kumuumba mtu kwa mfano wake
(Mungu) na kwa sura yake (Mungu) mwenyewe kama tunavyosoma katika maandiko
matakatifu katika kitabu cha Mwanzo 1:26
– 27 “26 Mungu akasema, Na tumfanye
mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa
angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu
ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba,
mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Nataka ufahamu kwa uhakika ya kwamba mtu
anayeongelewa hapa ni roho na sio mwili kama vile watu wengi wanavyodhani,
unaposikia wewe ni mfano wa Mungu, basi fahamu anayeongelewa hapa ni mtu wa
ndani (Roho yako) ndiye mfano wa Mungu. Uhakika wa kwamba mtu ni roho tunaupata
katika maandiko matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu yeye ni Roho hivyo
yoyote aliye mfano wa Mungu naye pia ni Roho kama tunavyosoma katika kitabu cha
Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na
kweli.”
Hivyo
basi kama mtu ni roho na milango yake ya fahamu ipo rohoni pia kama ilivyo
milango ya fahamu ya mwilini.
FAHAMU ZA ROHONI
Kama
vile ulivyo mwili, mtu ambaye ni roho anazofahamu katika hali ya roho ambazo
zinamuwezesha kuwelewa/kutambua mazingira ya rohoni kama vile mwili unavyoweza
kutambua mazingira yake ya mwilini. Fahamu zilizopo katika ulimwengu wa roho ni
kama zile za ulimwengu wa mwili zinazohusiana na Kugusa, Kuona, Kusikia, Kuonja
na Kunusa/Harufu.
KUONA ROHONI (MACHO YA ROHONI)
Ili
uweze kupata uelewa sawasawa kwanza vuta picha ya mwanadamu mwenye macho ambaye
anaangalia na kuona mambo mbalimbali katika maisha ya kawaida, macho yanampa
uwezo wa kutambua watu na vitu. Kwa kutumia macho mtu anaweza kuweka kumbukumbu
ya matukio fulani katika ufahamu wake na mambo hayo aliyoyaweka yakamsadidia
kuja kufanya maamuzi sahihi au kuwasaidia wengine kufanya maamuzi sahihi katika
maisha yao ya kila siku. Ndivyo ilivyo kwa mtu wa rohoni, mtu wa rohoni anayo
macho ambayo yanamsaidia kuona vya rohoni na kufahamu vitu vya rohoni vilevile
kuweka katika ufahamu wake kumbukumbu za rohoni kwa matukio aliyoyaona ili
imsaidie katika kufanya maamuzi ya kiroho.
Neno
la Mungu linatuthibitishia kuwepo kwa macho ya rohoni ambayo mtu wa rohoni
anaweza kuyatumia kuona na kutambua mambo ya rohoni kama tunavyosoma katika Waefeso 1:17-18 “17 Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho
ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; 18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru,
mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake
katika watakatifu jinsi ulivyo;”
Hapo
mtume Paulo anawaombea Waefeso kwamba macho ya mioyo yao yatiwe Nuru, kumbe
waefeso walikuwa na macho ya rohoni lakini yenye giza sawa na vipofu, walikuwa
hawaoni ukuu wa Kristo Yesu na utajiri wa Utukufu wa Yesu. Inawezekana hata
wewe unayesoma sasa hivi umepewa neema ya kupata somo hili ili macho yako ya
rohoni yatiwe Nuru ya Kristo upate kuuona Ukuu wake na utukufu wa Kristo;
Mwambie Bwana Yesu aachilie nuru yake katika macho yako sasa ili giza
likuondoke upate kuona rohoni sasa kwa jina la Yesu!
Neno
la Mungu linazidi kututhibitishia kwamba yapo macho ya rohoni na watu wenye
macho hayo wamefungwa (wamepofushwa) macho yao na hata hawaoni kama tunavyosoma
habari ya mtumishi wa Nabii Elisha katika 2Wafalme
6:15-17 “15 Hata asubuhi na mapema
mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi
la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia,
Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? 16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja
nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. 17 Elisha akaomba, akasema, Ee
Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule
mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari
ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.” Loh! Kumbe unaweza kuwa na macho
na wakati huo usione kinachoendelea! Sema na Yesu sasa kwamba macho yako
yafunguke na upate kuona tena Utukufu wa Jehova.
KUSIKIA ROHONI (MASIKIO YA ROHONI)
Katika
hali ya kawaida (hali ya mwili wa damu na nyama) mwandamu anakuwa na masikio
ambayo yanaweza kuwa na uwezo wa kusikia au yasiwe na uwezo wa kusikia, kama
masikio yakiweza kusikia hiyo ndio sahihi lakini kama hayawezi kusikia basi
hapo kuna shida; yaani inawezekana mtu huyu ni kiziwi au anayomatatizo ya
yanayomzuia kusikia sawasawa.
Katika
ulimwengu wa roho yapo masikio ya rohoni yanayomuwezesha mtu wa rohoni kusikia
sauti za rohoni na kufahamu/kuelewa yale yanayonenwa katika ulimwengu wa roho.
Kama mtu hana masikio ya rohoni basi huyo ni mlemavu wa rohoni na anahitaji
kuponywa mlango huo wa fahamu ili aondoke katika ulemavu huo.
Tunasoma
katika kitabu cha Ufunuo 1:9-11 “9 Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye
kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo,
nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda
wa Yesu. 10 Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma
yangu, kama sauti ya baragumu, 11 ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo,
ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira,
na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”Yohana anasema alikuwa katika Roho
akasikia sauti, kumbe unaweza kuwa rohoni ukasikia. Kama mtu aliyeko rohoni
anasikia basi mtu huyo anayo masikio ya rohoni yanayofanya kazi sawasawa. Hivi
umeshawahi kuwaza kwamba kama hausikii ukiwa rohoni basi ni hakika kwamba
umekuwa kiziwi wa rohoni! Achilia damu ya Yesu katika masikio yako ya rohoni
uondowe kwa jina la Yesu uziwi wa kiroho.
Wakati
mwingine unaweza kuwa unasikia sauti ya rohoni lakini hauelewi wala hauwezi
kutambua unaongea na nani, Neno la Mungu linatufundisha kwamba hali ya namna
hiyo inaweza kutokea kama ilivyomtokea mtoto Samweli, tunasoma katika 1Samwel 3:1-10 “1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana
lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. 2 Ikawa wakati huo, Eli
alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata
asiweze kuona), 3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa
amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; 4 basi, wakati
huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. 5 Akamwendea Eli kwa
haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale
tena. Naye akaenda, akalala tena. 6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli!
Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita.
Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. 7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana
bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. 8 Bwana akamwita
Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa
maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.
9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema,
Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala
mahali pake. 10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli!
Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.”
Kilichomkuta
mtoto Samweli kinaweza kumkuta mtu yeyote aliyeokoka hata sasa hivi,
inawezekana kwamba bado ufahamu wako haujafunguliwa kuweza kuitambua sauti ya
Mungu hivyo sauti ikitoka rohoni huwezi kuitambua. Neno la Mungu linasema kwa ……..7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na
neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake…………. Kumbe samweli pamoja
na kwamba alikuwa anamtumikia Jehova lakini alikuwa haijui sauti ya Mungu
anayemtumikia.
Hebu
fungua kinywa chako Omba maombi haya pamoja na mimimi “Bwana Yesu Ninakuomba Uyafungue Masikio Yangu Ya Rohoni Na Unipe Roho
Ya Ufahamu Ili Niweze Kutambua Sauti Yako Unaposema Namimi, Ninaomba Katika
Jina La Yesu, Amen!”
Mwana
wa Mungu aliye hai inawezekana kabisa ukasikia sauti ya mtu akisema kutoka
rohoni hata kama kinywa chake cha milini kimefungwa. Neno la Mungu
linatufundisha kwamba Sara mke wa Ibrahim alicheka rohoni na Bwana akamsikia Mwanzo 18:12-15 “12 Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe,
nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13 Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara
amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14 Kuna neno gani
lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu
mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. 15 Akakana Sara, akisema, Sikucheka,
maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.”
Lakini
pia tunajifunza kuwa hata shetani alipoamua kuasi alisema maneno ambayo
yalisikika rohoni kama ilivyoandikwa katika Isaya 14:12-15 “12 Jinsi
ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi
ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! 13 Nawe ulisema moyoni mwako,
Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu;
Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. 14
Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. 15 Lakini
utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.”
Hapa
tunajifunza kuwa mtu anaweza kunena kutokea rohoni/moyoni maneno ambayo
yanasikika katika ulimwengu wa roho na hata kumtenda Mungu dhambi au kumpa
shetani nafasi ya kushambulia maisha yako.
KUONJA ROHONI (ULIMI WA KIROHO)
Kuna
watu wamekua wakiota ndoto ama wanakula wenyewe au wanalishwa katika ndoto vitu
vya aina mbalimbali, mwingine atakuambia nilipewa maji machungu kwenye ndoto au
nilikula chakula kibaya sana kwenye ndoto au nilikula chakula kitamu kwenye
ndoto (Kumbuka ndoto ni ulimwengu wa roho). Kama inavyokuwa katika hali ya
mwili huu wa damu na nyama kwamba unaweza kujua ladha mbalimbali za
vyakula/vinywaji au chochote kinachoingia kinywani, ndivyo ilivyo na kwa
ulimwengu wa roho. Unapokuwa rohoni unaweza kutambua ladha ya vitu kwani Biblia
inatufundisha kwamba upo ulimi wa rohoni kama tunavyosoma katika Luka 16:22-24 “22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani
kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. 23 Basi, kule kuzimu aliyainua
macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro
kifuani mwake. 24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro
achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe
ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.” Kumbuka mfano huu
alioutoa Yesu alikuwa anazungumzia habari za roho ya masikini Lazaro na roho ya
Yule tajiri baada ya kufa kwao, sasa tunaona kumbe tajiri alitani kuburudishwa
ulimi wake kwa tone la maji katika ulimwengu wa roho.
Mtu
wa Mungu ukizidi kusoma Neno la Mungu utafahamu kwamba mtu akiwa rohoni kwa
kutumia mlango wa fahamu wa kuonja (ulimi) anaweza kujua ladha ya vitu katika
ulimwengu wa roho kama tunavyosoma katika Ezekiel
3:1-3 “1 Akaniambia, Mwanadamu, kula
uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. 2 Basi
nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. 3 Akaniambia, Mwanadamu,
lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu
lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.”
Kumbe
nabii wa Mungu Ezekiel aliweza kula na kutambua ladha ya gombo kuwa lilikuwa na
utamu wa asali. Mwombe Yesu leo ahuishe milango yako ya fahamu katika ulimwengu
wa roho uweze kufahamu kile kinacholetwa kwako kama chakula cha rohoni, hii
itakusaidia kujua nini kimeletwa kwako na kama ni kitu kibaya au kizuri.
HARUFU YA ROHONI/KUNUSA ROHONI (PUA ZA ROHONI)
Ukiwa
katika hali ya mwili na kama hauna kasoro zozote katika pua zako, unaweza
kufahamu/kutambua harufu za aina Fulani na ukaziweka katika kumbukumbu zako na
zikakusaidia katika kufanya maamuzi siku za mbele/baadae. Kwamfano unaweza
kufahamu harufu ya kitu kinachoungua na siku ukinusa hata bila kuona utatambua
kwamba kuna kitu kinaungua; hivyo ndivyo ilivyo kwa jinsi ya rohoni, kama pua
zako za kiroho zinafanya kazi sawasawa unaweza kugundua mambo ya rohoni hata
kabla ya kuyaona.
Ukisoma
2Kor 2:14-16 “14 Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na
kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. 15 Kwa maana
sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika
wao wanaopotea; 16 katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao
wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?”
Mtume
Paulo akijaa Roho Mtakatifu anaongelea habari ya manukato (Perfume) katika
ulimwengu wa roho. Kama ukiweza kugundua aina ya manukato katika ulimwengu wa
roho, maana yake ni kwamba mlango wako wa fahamu wa kunusa (pua) wa rohoni
unafanya kazi sawasawa. Hii ndio sababu Mtume Paulo anazungumzia harufu za aina
mbili yaani harufu ya mauti na harufu ya uzima, ………….katika hao wa pili harufu ya
mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima…………..
Vilevile
tunamuona Yohana akiwa rohoni anatambua kwamba maombi ya watakatifu yalikuwepo
kwa Mungu kwenye mabakuli (vitasa) kama manukato; aliwezaje kujua kwamba yale
maombi ni manukato? Maana yake mlango wa Yohana wa fahamu katika kunusa (pua za
rohoni) ulimfahamisha kwamba yale ni manukato kwa kunusa. Ufunuo 5:8 “Hata alipokitwaa
kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka
mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu
vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.”
Hii
inazidi kudhihirishia kwamba ukiwa rohoni unaweza kunusa na kutambua harufu ya
vitu vya rohoni.
KUGUSA/KUGUSWA ROHONI (NGOZI YA KIROHO)
Siku
moja Yesu alikuwa katika kazi ya kuihubiri injili, watu wengi mno walimsonga
huku na kule pengine wengine walimvuta na kumuita ili awaponye. Lakini kuna
mwanamke mmoja ambaye aligusa vazi la Yesukwa imani na Yesu akatambua kwamba
kuna mtu amemgusa na kuuliza kwamba ni nani huyo kama ilivyoandikwa katika Luka 8:43-46 “43 Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na
miwili, aliyekuwa amegharimiwa mali
zake zote kwa kuwapa waganga asipate kuponywa na mtu ye yote, 44
alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu
kwake kulikoma. 45 Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote
walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na
kukusonga. 46 Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu
zimenitoka.”
Swali
la msingi sana la kujiuliza hapa ni hili, Yesu aligunduaje kwamba ameguswa na
nguvu zimemtoka wakati alikuwaamezongwa na watu wengi? Iwezje mtu mmoja amguse
na afahamu dhahiri na kusisitiza kwamba ameguswa? Kwa uhakika kabisa mama yule
alimgusa Yesu kwa imani kutokea rohoni na kwakuwa yesu alikuwa wa rohoni
alitambua mara ile ile, alitambua kwakuwa alitumia mlango wa fahamu wa rohoni
wa kugusa na kufahamu kwamba kuna mtu amemgusa.
Vilevile
tunasoma katika Ufunuo 1:17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake
kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope,
Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,” Yohana alitambua kwamba Yule mtu ameweka
mkono juu yake kwakuwa akiwa rohoni mlango wake wa ufahamu katika kugusa ulikua
ukifanya kazi.
MAOMBI YA KUFUNGULIWA MILANGO YA FAHAMU YA ROHONI
Mungu wa Bwana wangu Yesu Kristo, Baba
wa utukufu, unipe mimi roho ya hekima na ya ufunuo katika kukujua wewe; milango
ya fahamu (Macho, Masikio, Ngozi, Ulimi na Pua) ya roho yangu itiwe nuru, nijue
tumaini la mwito wako jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wako
kwangu mimi mtakatifu jinsi ulivyo; Nijue ubora wa ukuu wa uweza wako ndani
yangu mimi niaminie jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza
wako; ulioutenda katika Kristo ulipomfufua katika wafu, ukaniketisha pamoja
naye katika ulimwengu wa roho. Ukamweka mkono wako wa kuume katika ulimwengu wa
roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila
jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; ukavitia
vitu vyote chini ya miguu yake, ukamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili
ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake.
No comments:
Post a Comment