Thursday, July 23, 2015

MIMI NI ASILI YA MBINGUNI (Samson Mollel - Uzima wa Milele International Ministries)

Nimefunuliwa juu ya somo hili kwaajili yako ili kukupa ujasiri na nguvu zaidi za rohoni kwa kuifahamu kweli na kuwa na maarifa ya Mbinguni yatakayo kuwezesha kujua Neno la Mungu na uweza wa Mungu. Neno la Mungu linasema katika injili ya Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Hatujui yakuwa sisi ni watoto wa Mungu kwakua Neno la Mungu linasema hivi “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” Yohana 1:12. Kama wewe ni mtoto wa Mungu na Mungu wetu anakaa mbinguni basi wewe pia ni wa asili ya Mbinguni. Kuthibisha hili; Biblia inasema katika 1Yohana 3:9-10 “9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. 10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” Katika mistari hii tunajifunza yakuwa Mungu anazaa watoto ambao ni wale waliompokea Yesu Kristo, na wale waliozaliwa na Mungu uenyeji wao ni Mbinguni yaani wanayo asili ya Mbinguni. Hata hivyo usisahau kwamba kuna watoto wa ibilisi ambao watachomwa moto pamoja na baba yao ibilisi.
Ninakupa moyo mtu wa Mungu ya kuwa ukiijua nafasi yako katika ufalme wa Mungu na kuliamini Neno la Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya 55:10-11 “10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.” Basi hakika ni kwamba utafanikiwa katika mambo yote sawasawa na Neno laMungu.
Karibu msomaji wangu ujifunze baadhi ya mambo yatakayokupa ujasiri wa nafasi yako katika ufalme wa Mungu.



1.      MIMI NI MFANO NA SURA YA MUNGU
Biblia inasema wazi kwamba hapo mwanzo Mungu aliamua kumuumba mtu kwa mfano wake (Mungu) na kwa sura yake (Mungu) mwenyewe kama tunavyosoma katika maandiko matakatifu katika kitabu cha Mwanzo 1:26 – 27 “26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Nataka ufahamu kwa uhakika ya kwamba mtu anayeongelewa hapa ni ROHO na sio mwili kama vile watu wengi wanavyodhani, unaposikia wewe ni mfano wa Mungu, basi fahamu anayeongelewa hapa ni mtu wa ndani (Roho yako) ndiye mfano wa Mungu. Uhakika wa kwamba mtu ni roho tunaupata katika maandiko matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu yeye ni ROHO hivyo yoyote aliye mfano wa Mungu naye pia ni ROHO kama tunavyosoma katika kitabu cha Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”.
Nataka nikupe uhakika ya kwamba umepewa nafasi kubwa sana katika ulimwengu wa mwili na ulimwengu wa roho, nafasi hiyo ni kuwa sura yake Mungu kama vile alivyo Kristo Yesu (2Korintho 4:4  “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”), kumbe nasisi tumepewa nafasi kama ile ya Yesu kama tunavyosoma katika Mwanzo 1:26 “26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Kuwa sura yake Mungu maana yake ni kuwa ishara na kielelezo cha Nguvu, Uweza, Mamlaka, Utukufu na Ukuu wa Mungu kila tutakapokuwa na ndio maana tukapewa kumiliki na kutawala.


2.      NDINYI MIUNGU (MIMI NI MIUNGU)
Muimba zaburi anasema katika Zaburi 8:4-5 “4 Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? 5 Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima”. Mungu amemfanya Mtu/Mwanadamu kuwa baada tu ya Mungu, yaani kimamlaka unaweza kusema Mtu/Mwanadamu ndi wa pili kwa nguvu kutoka kwa Mungu. Ni kama vile nchi ambayo inayoviongozi wakuu wawili yaani raisi (mwenye nchi) na waziri mkuu (Mtendaji mkuu wa serikali) ndivyo ilivyo katika utawala wa Mungu, yaani Mungu (Muumbaji wa vitu vyote) na Mwandamu (Mmiliki na mtawala/mtendaji). Katika injili kama ilivyoandikwa na Yohana 10:34 “Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?” vile vile tunasoma katika Zaburi 82:6 “6 Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”. kwahiyo tunao uthibitisho kwamba sisi tumepewa nafasi ya UUNGU, yaani baada ya Mungu ni mimi mwanadamu.

3.      MIMI NI HEKALU LA MUNGU
Bwana Yesu alipoileta kweli ulimwenguni, alihamisha hekalu la Yerusalemu na kuwa mwili wake kwa yule mwenye kuamini kama vile alivyoamisha sanduku la agano na kutufanya sisi ndio sanduku la agano jipya amabapo Mungu anakaa ndani yetu. Bwana Yesu akaleta wokovu kwa mwanadamu kwamba inatupasa tuokoke ili miili yetu ifanyike hekalu la Roho mtakatifu kama ilivyoandikwa katika 1Kor 3:16 - 17 “16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” Vilevile imeandikwa katika 2Kor 6:16, 18 “16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu…………18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”. Mtu wa Mungu hebu turudi nyuma kidogo tuangalie katika hekalu la wayahudi ambapo Mungu alikaa ndani yake na kulikuwa na nguvu kubwa kiasi gani.
Tunasoma katika Kutoka 30:10 “Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa Bwana.” Tunaona katika patakatifu pa patakatifu ndipo Haruni alipokutana na Mungu mara moja tu kwa mwaka ili kufanya upatanisho wa dhambi za wana wa Israeli, kwa kifupi Mungu alishuka ndani ya hekalu patakatifu pa patakatifu ili kukutana na kuhani aliyebeba sadaka ya upatanisho. Baada ya kufa kwa Yesu Kristo kuna jambo lililotokea ambalo lilibadisha kabisa taratibu za awali kama tunavyosoma katika  Waebrania 9:12-14 “12 wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; 14 basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”. Sasa miili yetu ndiyo imekuwa hekalu la Mungu mwenyewe na ndiye anaishi ndani yetu.
Ndugu fahamu kwamba Mungu aishiye ndani yako (Kwakuwa wewe ni hekalu la Mungu) ndiye Mungu yuleyule aliyeumba mbingu na dunia, ndiye yule aliyewavusha Israeli katika bahari ya shamu, ndiye yuleyule aliwaokoa Shedrack, Meshack na Abednego kutoka katika ule moto mkali sana na ndiye aliyemuokoa Daniel na makanwa ya samba wenye njaa kali; vile vile huyu ndiye Mungu wa Eliya, Elisha, Daudi na manabii na mitume wakubwa katika Biblia. Swali ni hili sasa; Iweje huyu Mungu mwenye nguvu kuu namna hii anaishi ndani yako halafu wewe kila siku unalalamika kwamba unaonewa na nguvu za giza, unalalamika kuporomoka kiuchumi, unalalamika afya yako kuvurugika; AMKA!!! Tambua nguvu inayofanya kazi ndani yako! Tambua ya kwamba Mungu mwenye nguvu za kutisha yupo ndani yako, amini kwamba anaweza nayeye atatenda jambo kubwa sana katika maisha yak oleo.
MAOMBI
Katika jina la Yesu Kristo nimetambua leo yakwamba mimi ni hekalu la BWANA na Roho wa BWANA anakaa ndani yangu, na kwakuwa Mungu anakaa ndani yangu Neno la Mungu linasema katika Waebrania 12:29 “maana Mungu wetu ni moto ulao”. Chochote kilichokaa ndani yangu kutoka katika ufalme wa giza nakiamuru kiteketee kwa moto wa BWANA aishiye ndani yangu, vyakula vya kichawi/kipepo nilivyolishwa katika ulimwengu wa roho naamuru viteketee kwa moto ulao katika jina la Yesu. Magonjwa ya aina zote naamuru yateketee kwa moto ulao katika jina la Yesu, Amen.

4.      MIMI NI TAWI NA MUNGU NI SHINA LANGU
Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”
Ukiisha kumpokea Yesu, Yesu anasema wewe unakuwa tawi lake na yeye (Yesu Kristo) anakuwa Shina. Sasa ufahamu ya kuwa mti hutambulikana kwa matawi yake kasha kwa matunda yake, maana yeke ni; Mti/Shina ni Yesu Kristo, ili uweze kuutambua mti/shina inabidi utazame matawi yake na matunda yake yaani Mkristo na yale anayoyatenda (Ukitaka kumtambua Kristo Yesu inabidi umuangalie Mkristo na matendo yake). Kama ilivyo kwa mti wa kawaida, chakula kinachopita katika shina ndicho kinachoingia katika matawi, hii inamaanisha kwamba kwakuwa sisi ni matawi ya Kristo Yesu, basi kila kinachotoka kwake Yesu ndicho kinaingia kwetu. Nguvu alizonazo Yesu zinaingia kwetu kwani tumeunganishwa na Yesu sawasawa na Neno lake kutoka Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi……..)
Mtu wa Mungu AMKA!!! Fahamu yakuwa upako alionao Yesu Kristo unaingia na kwako pia, fahamu ya kuwa Nguvu, Uponyaji, Baraka, Maarifa, Uweza na kila kilichopo kwa Yesu ni cha kwako. Fahamu yakuwa hakuna kinachopita katika shina kisiingie katika matawi.
MAOMBI (Omba kwa sauti kama unaweza)
Wewe shetani!! Wewe ni nani hata uweze kukaa katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi, Kazi, Mahusiano, Kibali na upendeleo!!!! Mimi nimejua, nifahamu ya kuwa mimi ni sehemu ya Yesu Kristo na kila kinachotoka kwa Yesu Kristo kinaingia na kwangu. Katika Jina Lenye Nguvu sana Jina la Yesu Kristo nakuamua TOKAAAA!!! Katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi, Kazi, Mahusiano, Kibali na upendeleo, ACHIAAA!!! Kwa Jina la Yesu kila ulichoshikilia katika maisha yangu katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareth. Chochote kilichojishikamanisha na maisha yangu naamuru kikutane na nguvu ya damu ya Yesu kwakuwa imeandikwa katika Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Namimi nakushinda shetani kwa damu ya Yesu Kristo katika jina la Yesu, Amen.

5.      MIMI NI MBONI YA JICHO LA MUNGU
Zekaria 2:8.Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.”
Jaribu kufikiri katika hali ya kawaida kabisa ambayo wewe ni mwanadamu ambaye unavyo viungo vingi na kimojawapo ni jicho, ndani ya jicho kuna kitu muhimu sana ambacho ni “mboni”. Kama ikitokea mdudu au kitu chochote kinaelekea kuingia ndani ya jicho lako utafanya jambo lolote kuhakikisha kwamba hicho kitu hakiingii ndani ya mboni ya jicho lako, unaweza kutumia mkono wako, au ukainama au ukakimbia au vyovyote vile lakini kitu chochote kisiingie ndani ya jicho lako. Kwa kutumia mfano huu jenga picha ya kwamba Mungu amekufanya wewe kuwa ni mboni ya jicho lake, yaani Mungu amekuweka wewe kuwa ni sehemu muhimu kabisa ambayo hakuna kitu kitapita au kitakuja kudhuru mboni ya jicho bila kuonekana, na kama hicho kitu kitakaribia jicho hata kabla ya kuleta madhara kitakuwa tayari kimeondolewa na Mungu mwenyewe. Tunasoma pia katika Kumbukumbu la torati 32:9-10 “9 Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. 10 Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho;” Biblia inatueleza kuwa katika jangwa tupu litishalo Mungu alimzunguka akamhifadhi/akamlinda kama mboni ya jicho lake yaani mboni ya jicho la Mungu wa Israeli.
Kwa lugha nyingine unaweza kusema kwamba yoyote anayeshindana na wewe uliyeokoka (Kwa maana ukiokoka unakuwa ndani ya Mungu) anashindana na Mungu mwenyewe na wala hashindani na wewe. Na kama ikiwa yeyote yule (shetani na mawakala wake wote, mapepo na roho zote chafu kutoka kuzimu) watashindana na wewe basi wananshindana na Mungu na Neno la Mungu linasema “Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.” 1Samweli 2:10. Basi sasa fahamu mtu wa Mungu yakuwa yeyote aliyesimama kinyume na wewe anapingana na Mungu.
MAOMBI
Katika jina la Yesu kristo wa Nazarethi; yeyote anayeshindana namimi anashindana na BWANA. Kila roho inayotoka kuzimu majini, mapepo, mizimu, wachawi, wasoma nyota, waganga …….. mnaoshindana namimi; sawasawa na Neno la Mungu nawaponda kwa nyundo ya Mungu, nawaagizia radi kutoka mbinguni, nawaagizia umeme mkali kutoka mbingu, nawateketeza kabisa kwa jina la Yesu. Amen

6.      MIMI NI MTOTO WA MUNGU
Neno la Mungu linaweka bayana kwamba, mara unapokubali kuokoka (Yaani unapomkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni BWANA na Mwokozi wa maisha yako) basi unakuwa motto wa Mungu sawa na Neno la Mungu katika Yohana 1:12 – 13 “12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; 13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Vilevile tunapata ushuhuda zaidi yakwamba Roho Mtakatifu (Ambaye ni Mungu) hushuhudia pamoja na roho zetu yakwamba wale waliompokea Yesu ni watoto wa Mungu kama tunavyosoma katika Warumi 8:16 - 17 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” Zaidi tunaona katika 2Kor 6: 18 “Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”
Mtu wa Mungu kwanza pata picha ya kuwa wewe ni mtoto wa Mfalme/Rais/Waziri mkuu katika nchi Fulani au katika nchi yako unayokaa, halafu jaribu kuvuta picha ya heshima unayopewa wewe kama mtoto wa kiongozi katika nchi yako, watu wengine hata viongozi watakuheshimu kwakulinda nafasi zao za uongozi kwani wanajua wakikutendea vibaya na ukamweleza baba yako ambaye ni rais/waziri mkuu huenda wakashughulikiwa hata kupoteza nafasi zao, kwa ujumla kila mru atakuheshimu hata kama hapendi kufanya hivyo.
Sasa nikupe uhakika kuwa wewe ambaye umeokoka nafasi yako ni kubwa mno katika ulimwengu wa roho, baada yaw ewe kumpokea Yesu umezaliwa upya katika ulimwengu wa roho na baba yako ni Mungu mwenyewe. Mungu huyu ambaye ni baba yako ndiye Mungu wa Israeli yule aliyetenda mambo makuu kwa manabii na mitume waliomtegemea yeye tu. Hebu pata ujasiri sasa mtoto wa Mungu kwakuwa wewe ni mtoto wa Mungu umepewa urithi wa mambo yale ya mbinguni sawa na Neno la Mungu katika Warumi 8:16 - 17 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Ubarikiwe sana Mtu wa Mungu; zaidi sana fahamu yakuwa Neno la Mungu linatuhakikishia yakuwa sisi ni washindi na tunashinda na zaidi ya kushinda kama ilivyoandikwa katika Rumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”


SAMEHE NA KUSAHAU (BY MWL, C.MWAKASEGE)

                            TABIA YA MUNGU YA KUSAMEHE NDANI YAKO
                                        (BY MWL, C.MWAKASEGE)
            Ulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, ulipokea tabia ya aina gani?
"  Bali wote waliompokea (Kristo) aliwapa uwezo wa  kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu." (Yohana 1:12,13)
            Ulipozaliwa mara ya pili kwa Neno la Kristo ulifanyika kuwa mtoto wa Mungu.
Watoto wa Mungu wana tabia ya namna gani?
            Kwa kuwa wamehamishwa toka ufalme mwingine na uzazi mwingine, na kuingizwa katika ufalme wa Mungu na uzazi wake (Wakolosai 1:13); watoto hawa wanatakiwa wawe na tabia nyingine.
             Kabla ya kuzaliwa mara ya pili, kabla ya kumkiri Kristo ya kuwa ni Bwana: ulikuwa na tabia ya dunia hii iliyoongozwa na mfalme wa dunia hii ambaye ni shetani.
             Ulipozaliwa mara ya pili na kuukiri wokovu katika Kristo, ulipokea tabia mpya inayoongozwa na Mungu mwenyewe aliye ndani yako.

"  Kwa kuwa uwezo wake wa Uungu umetukirimia  vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa (Utakatifu), kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno; za thamani,ili kwamba kwa hizo mpate kuwa Washirika wa TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa." (2 Petro 1:3,4)
             Mistari hii inatuonyesha wazi kabisa kuwa kwa uweza ule ule uliokuwezesha kuwa mwana wa Mungu, unakuwezesha kuipokea tabia ya Mungu.
             Tabia ya Mungu iliyo wazi ni Upendo kwa kuwa Mungu ni Upendo
(1 Yohana 4:8)

             Ni upendo ambao huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,huvumiliayote,huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, haupungui neno wakati wowote.Kamailivyoandikwa katika (1 Wakorintho 13:4 - 8)

 Mungu anavyosamehe:
         Ndani ya upendo, kuna tabia ya kusamehe na kusahau. Ili kuifahamu zaidi na tuitafakari tabia ya Mungu ya kusamehe na kusahau. Mungu anasema hivi:

Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako." (Isaya 43:25)
Na tuitafakari tabia hii ya Mungu katika mafungu mawili yafuatayo:
1. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; na;
2. Wala sitazikumbuka dhambi zako.

              Haya ni maneno ya Mungu ambayo aliyasema kwa kutumia kinywa cha nabii Isaya, kwa ajili ya watu, baada ya kufunga agano jipya katika damu ya Yesu Kristo pamoja nao. Kwa kuwa katika agano la kale makosa (au dhambi) yalikuwa hayafutwi ila yanafunikwa tu kwa damu ya wanyama waliotolewa sadaka (Waebrania 10:1 - 25)
             Lakini katika agano jipya, makosa yanafutwa kwa uwezo wa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.
             Kuna tofauti kubwa kati ya kuifunika dhambi kwa damu na kuifuta dhambi kwa damu. Unapofunika, kosa haliondoki linabaki pale pale, lakini linakuwa halionekani. Unapofuta, kosa linaondolewa kabisa, inakuwa kama hakuna kosa lililowahi kufanyika.
             Ukiwa darasani, mwalimu akifuta maandishi ya chaki ubaoni, ubao unabaki hauna maandishi; unakuwa safi. Lakini utakuta yale yaliyokuwa yameandikwa, ingawa hayapo ubaoni, katika akili za watu yanakuwa yapo. Na wakati mwingi inachukua muda kufutika mawazoni.
             Sasa, ile sehemu ya kwanza ya mstari, Mungu anasema anayafuta makosa yetu kwa ajili yake mwenyewe, Mungu hakusema "Anayafunika makosa," bali amesema, "anayafuta makosa".
Soma tena:
"Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe."
Soma na maneno haya:
"Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" (1Yohana 1:9)
            Ukitubu dhambi zako kwa Mungu katika Roho na Kweli, Mungu anakusamehe, na anafuta dhambi zako na mbele yake unaonekana kama hukufanya kosa lo lote. Hivyo ndiyo maana ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu katika Kristo. Kusamehe ni kufuta au kuondoa kosa na kulisahau au kutokulikumbuka tena.

 Kusamehe kosa = kufuta + kutokulikumbuka kosa
            Wakati huu tunatizama jinsi Mungu anavyotusamehe. Hatua ya kwanza anafuta kosa machoni pake.
             Kwa nini Mungu atusamehe?
             Kwa nini Mungu ayafute makosa yetu?
             Umewahi kujiuliza kwa nini Mungu aliamua kukusamehe mabaya yote uliyoyafanya maishani mwako?
             Watu wengine wanafikiri wokovu unakuja kwa kumpendeza Mungu kwa matendo yao. Na matokeo yake wanajihesabia haki wenyewe badala ya kuhesabiwa haki na Mungu.
             Utamsikia mtu anasema mimi sina dhambi, siibi, sizini, silewi, sijatengwa na kanisa, na naitunza Sabato kwa hiyo sina kosa kwa Mungu!
 Lakini neno la Mungu linatuambia mambo tofauti, kwa mfano neno linasema hivi:

" Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala SI KWA MATENDO, mtu awaye yote
 asije akajisifu
(Waefeso 2:8,9)
            Kwa hiyo, unaona kuwa matendo yako peke yake hayawezi kukupa wokovu, na ondoleo la dhambi, bila ya imani ndani ya Kristo. Imani lazima iambatane na matendo. Imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:26).
            Kitu kinachomfanya Mungu akusamehe si uzuri wa matendo yako; bali anakusamehe KWA AJILI YAKE MWENYEWE.
              Mungu anasema;
"Mimi, naam, Mimi, ndimi niyafutaye makosa yako KWA AJILI YANGU MWENYEWE"
            Huu ndiyo upendo wa ajabu!
            Kumbuka si kwa matendo yako bali kwa ajili yake mwenyewe Mungu, unapata kusamehewa makosa yako.

Mungu akisamehe anasahau:
            Hatua ya pili ambayo Mungu anaichukua mara tu anapofuta makosa yako ni kuyasahau aliyokwisha yafuta.
            Yeye mwenyewe ameahidi kwamba
".... Wala sitakumbuka dhambi zako". WALA SITAKUMBUKA DHAMBI ZAKO!
            Ina maana kuwa Mungu akiisha kukusamehe kwa ajili yake mwenyewe; anafuta na kusahau makosa uliyofanya, anakuhesabia haki bure mbele zake. Unasimama ndani yake kama mtu ambaye hajawahi kufanya kosa wala dhambi yo yote.
            Sasa kama Mungu amekwishafuta na kuyasahau mambo uliyofanya kabla hujaokoka na ukatubu, kwa nini wewe unayakumbuka? Jifunze kujisamehe mwenyewe! Mungu akikusamehe na wewe jisamehe. Mungu asipoyakumbuka makosa yako, na wewe usiyakumbuke!
            Huduma za watumishi wengi zinakwama mara tu anapokumbuka mambo aliyoyafanya zamani au maneno aliyoyasema - hata kama wamekwishayatubia!
            Kwa sababu hiyo, badala ya kusonga mbele katika Bwana, anajikuta kila wakati wanatubu juu ya dhambi hiyo hiyo. Na wanakosa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu, mbele ya shetani na mbele za watu.
            Kila wanapotaka kufanya kitu, shetani anawaletea wazo kuwa, bado hawajasamehewa kosa alilolifanya jana au juzi. Na kwamba haitakuwa rahisi kwako kupokea baraka toka kwa Mungu. Kwa hiyo watu hawo anaanza kutubu tena upya!

            Watu wengi hata sasa hawana uhakika kama Mungu amewasamehe juu ya makosa waliyoyafanya.
            Uhakika utaupata katika Neno la Mungu.
Mungu ameahidi kuwa ukitubu katika Roho na Kweli, unasamehewa.
(1Yohana 1:9)
            Paulo alifahamu siri hiyo ya kuyasahau mambo ya nyuma aliyomkosea Kristo, kwa kuwatesa wafuasi wa Yesu, kabla ya kuokoka kwake. Hii ilimsaidia kulitangaza Jina la Yesu bila yeye kujisikia vibaya moyoni mwake.
Kwa hiyo Paulo aliweza kusema:
"...... ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu" (Wafilipi 3:13,14)
            Ili uweze kusonga mbele katika wokovu, ni budi ujifunze kujisamehe na kuyasahau uliyoyafanya zamani.

Tabia hii unayo ndani yako:
            Kuyafuta makosa na kutoyakumbuka tena ni tabia ya Mungu ambayo imo ndani yako sasa.
            Ulipompokea Kristo moyoni mwako na kumkiri kuwa ni Bwana wa maisha yako, pia ulipokea ndani ya moyo wako tabia hii ya Mungu ya kufuta makosa na kutoyakumbuka.
            Hii ndiyo tabia inayotakiwa ionekane katika maisha yako unapokosewa na mtu.
            Tatizo la wengi ni kwamba wamekuwa viumbe vipya, lakini wanataka kutumia tabia yao ya zamani. Katika tabia ya zamani, walisamehe lakini hawakusahau walichokosewa. Tabia mpya ni kufuta makosa na kutoyakumbuka kabisa. Kwa hiyo na sisi tukikosewa tunatakiwa kusamehe na kusahau!

Hatua zifuatazo katika mfululuzo wa masomo yanayofuata wiki zijao zitakusaidia kuijenga na kuitumia tabia hiyo ya Mungu iliyo ndani yako. Tunaamini utakuwa pamoja nasi wiki ijayo ili kuendelea na somo hili - katika kipengele kinachosema: "Hasara za kulipiza kisasi"
HASARA ZA KULIPIZA KISASI
            Usilipize Kisasi! Unasikia? Hata ikiwa umefanyiwa ubaya wa namna gani, Biblia inafundisha na inakusihi usilipize kisasi kwa huyo aliyekufanyia ubaya. Biblia inasema hivi:

"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana" (Warumi 12:19)


            Kuna hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo! Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".
Lakini ikiwa utaona ya kuwa Mungu hawezi kukusaidia na ukaamua kujichukulia madaraka ya kujilipiza kisasi hasara zifuatazo hakika zitakupata!

Hasara ya Kwanza:
UTASHINDWA!
            Katika jambo lolote lile lililokukasirisha - liwe la kidini, au kikabila, au kifamilia, au kikazi, na kadhalika ukiamua kulipa kisasi utashindwa wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili! Tunasema hivi kwa sababu katika 2 Wakorintho 10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".

            Tena katika kitabu cha Waefeso 6:12 imeandikwa hivi: "Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".
            Uwanja wa mapambano uliyonayo ni "katika ulimwengu wa roho" na mapambano uliyo nayo "si juu ya damu na nyama" - ingawa unaona ya kuwa ni watu na ni binadamu kama wewe wanaokusonga - lakini fahamu hili ya kuwa wanatumiwa tu na ibilisi!
            Mbinu mojawapo ya shetani anayotumia akitaka kukuangamiza ni kukufanyia kitu kitakachokukasirisha ili uamue kujibu au kushindana kimwili kwa sababu anajua ukishindana "kimwili" au katika mwili utashindwa hakika, maana vita hivyo si vya mwili wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili!

Hasara ya Pili:
MATATIZO HAYATAKWISHA!
            Kumbuka imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 6:7; "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote ampandacho mtu. Ndicho atakachovuna".
            Ikiwa umeamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule aliyekufanyia - ubaya hautakwisha, kwa sababu utavuna ulichopanda.Ndiyo maana imeandikwa hivi:"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya
hayataondoka nyumbani mwake" (Mithali 17:13)

            Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako - Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.
            Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue hakika mabaya hayataondoka nchini mwako. Hili ndilo lililowapata wenzetu wa nchi za Burundi na Rwanda - kulipizana kisasi - matokeo ni uhasama usiotaka kupotea - pamoja na juhudi zote za kimataifa kutafuta suluhisho.
            Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa kazini kwako - fahamu mabaya hayataondoka kazini kwako. Ikiwa ni shuleni - mabaya hayataondoka hapo shuleni.
            Tena hali ya mwisho inakuwa mbaya zaidi,kila wakati kisasi kinapoendelea kupandwa. Kwa sababu ukiwapa watu ubaya - nawe utapewa ubaya kwa; "kipimo cha kujaa na kushidiliwa, na kusukwa - sukwa - hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile upimacho ndicho mtakachopimiwa (Luka 6:38)
            Kumbuka ubaya haushindwi na ubaya mwingine, bali unashindwa na wema - kama vile dawa ya chuki si chuki bali upendo! Ndiyo maana Warumi 12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".

Hasara ya Tatu:
UNAMZUIA MUNGU KUKUPIGANIA
            Unaweza ukashangaa, lakini ndivyo ilivyo! Ukiamua kulipa kisasi juu ya tatizo ulilonalo - unamzuia Mungu asikusaidie kulitatua.Mungu hawezi kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana".
Neno "ipisheni" limeandikwa kwa sababu kulipa kisasi "kunazuia" ghadhabu ya Mungu isipigane upande wako! Tena si hivyo tu lakini ukilipa kisasi unaingilia kazi ambayo si yako! Ni kazi ya Mungu maana anasema "Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana" Ikiwa kisasi ni juu ya Mungu kulipa, basi huhitaji wewe kulipa. Je, tunakwenda pamoja katika hili?
            Hatua yako ya kulipa kisasi inazuia mkono wa Mungu kukupigania - kwa hiyo ipishe ghadhabu ya Mungu kwa kutokujilipizia kisasi!

Hasara na Nne:
UNAJICHUMIA DHAMBI!
            Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo mabaya uliyofanyiwa. Huwezi kulipa kisasi bila ya kumchukia huyo unayejilipizia kisasi kwake. Na Biblia inasema hivi:
"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).
Umeona hilo! Chuki huzaa kisasi, na huzaa dhambi ya kuua! Na
Isaya 59:2b inasema; "dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia".
            Kwa hiyo kama umekwisha lipa kisasi au umekusudia moyoni mwako kulipa kisasi ni muhimu utubu ili Mungu akusamehe na mawasiliano yako na Yeye yawe mazuri.

Usikose kusoma wiki ya nne ya mfululizo huu tutakapojifunza juu ya:
Hatua tano Muhimu katika kusamehe na kusahau




           
JE ALIYEKUKOSEA ASIPOKUOMBA MSAMAHA UFANYEJE?
"Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwana neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11:25,26)
            Yesu Kristo aliyasema maneno haya kwa wanafunzi wake wa kwanza, alipokuwa akiwafundisha juu ya imani. Maneno haya ya Yesu Kristo, yanatuhusu hata sisi tulio wanafunzi wake siku hizi.Yesu Kristo katika maneno haya anazungumza na mwanafunzi wake aliyekosewa na mtu mwingine.Na katika somo hili, toka mwanzo tumechukua mtazamo huu wa Yesu Kristo; tunazungumza na mtu aliyekosewa na mtu mwingine.Somo hili lina maneno yenye mafundisho kwa mtu ambaye amekwazwa na mwenzake;mtu aliyefanyiwa kosa lolote lile.Kuna watu wengi sana wanaokosewa na watu wengine. Na tunaamini hata wewe kuna wakati fulani katika maisha yako umekwazwa na mtu mwingine.Katika ndoa makwazo yamekuwa kitu cha kawaida. Maofisini watu wanakosana kila siku. Hata na katikati ya watu wa Mungu, makwazo yanatokea mara kwa mara.Na sehemu mojawapo muhimu katika maisha ya mkristo ni maombi. Na ili tuwe na maisha ya maombi yenye mafanikio, ni lazima tuwe watu wenye tabia ya kusamehe waliotukosea.Yesu Kristo alijua jambo hili na umuhimu wa kusamehe KWANZA kabla ya kuanza kuomba.Yesu Kristo alisema, " Ninyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu".Maneno haya hayatupi uchaguzi wa kusamehe mtu wakati tunapopenda tu au wakati tunapotaka.Maneno haya ni agizo la Bwana Yesu Kristo ambalo linatakiwa lifuatwe na kila mwanafunzi wake, ili aweze kuwa na mafanikio katika maombi yake.
Unatakiwa kusamehe mara ngapi?
            Mama mmoja ambaye alikuwa ana matatizo katika unyumba wake, alisikika akisema maneno haya:"Mume wangu amenitesa kwa muda mrefu sasa; na hali ya mambo ilivyo, sidhani kama naweza hata kumsamehe tena; maana nimemsamehe nimechoka".Ni kweli kabisa kwamba mtu mwingine anaweza kukukosea mara nyingi sana. Hii huwa mara nyingi inatokea kwa watu ambao wanakaa pamoja au ni majirani.Hali ya mama huyu aliyesema maneno hayo, inawapata watu wengi sana, na nina uhakika watu hao wamechoka na hali hiyo.
            Inawezekana wewe ni mke wa mume ambaye ni mlevi, malaya, na mgomvi. Kila akirudi nyumbani ni kukutukana na hata wakati mwingine kukupiga. Na umeomba kwa Mungu juu ya jambo hili kwa muda mrefu bila kuona mafanikio.Sasa umeamua ufanyaje wakati unaona unazidi kuonewa na kuteswa? Inawezekana wewe ni mume wa mke ambaye ni mlevi, malaya na mgomvi. Inawezekana wewe ni mzazi wa watoto ambao hawakusikii, walevi, malaya, na wahuni.Inawezekana wewe ni mfanyakazi katika ofisi ambayo unaonewa haki zako za kupanda cheo, kupanda mshahara na marupurupu mengine, bila sababu yoyote.Sasa, nakuuliza, umeamua kuwachukulia hatua gani hao watu waliokukosea?Kumbuka wewe ni mkristo, na unatakiwa uamue mambo yako kikristo, kwa kulifuata Neno la Mungu.Hawa watu wanaotukosea tunatakiwa kuwasamehe mara ngapi? Hili swali ni muhimu, kwa kuwa watu wengine hawachoki kuwakwaza wengine!
Imeandikwa:"Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye;akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba,akisema, Nimetubu, msamehe" (Luka 17:3,4):
            Ni kweli kabisa! Mtu akikukosea na akitubu ni rahisi kumsamehe. Lakini ikiwa mtu aliyekukosea asipokuja kutubu je naye anahitaji kusamehewa?Hata asipotubu msamehe.Hili ni jambo ambalo inabidi tulizungumze kwa kufuata Neno la Mungu; maana ni jambo linalowasumbua wengi.Kuna wakati fulani tulikuwa tunalijadili jambo la kusamehe na wenzetu. Mmoja kati ya wale waliokuwepo alisema hivi: "Mimi siwezi kumsamehe mtu aliyenikosea asipokuja kutubu".Inawezekana hata wewe una mawazo kama haya. Lakini nakuuliza swali hili, "Je, kuna mstari wo wote katika biblia unaosema mtu aliyekukosea asipotubu usimsamehe?".
            Sisi hatujawahi kuuona. Kama upo tunaomba utuambie.Huhitaji kuombwa msamaha ili upate kusamehe. Biblia inasema; ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo wadeni wetu’ Biblia haikusema ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo waliotuomba msamaha!Kwa hiyo tunatakiwa kuwasamehe waliotukosea hata kama hawakutuomba masamaha.Hii ni kweli. Na sasa tuone neno la Mungu linatuambia nini:
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana,ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, si kuambii hata mara saba,bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21,22)
            Hapa hatuoni Yesu Kristo akimwambia Petro kuwa mtu ni lazima atubu ili asamehewe. Ila anamjibu kuwa "Sikuambii hata mara saba, bali saba mara sabini"Petro alifahamu ya kuwa anahitaji kusamehe hata asipoombwa msamaha. Tatizo lake lilikuwa ni asamehe mara ngapi.Kumbuka ya kuwa unayaweza mambo yote, pamoja na kusamehe bila kuombwa msamaha, katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13) Tena kumbuka ya kuwa ni tabia ya Mungu iliyo ndani yako (2Petro 1:3,4) inayokuwezesha kusamehe na kusahau hata kama hujaombwa msamaha.Kumbuka si wewe unayekosewa na kukwazwa, bali Kristo aliye ndani yako. Kwa kuwa ulipompokea Kristo katika moyo wako, ulifanyika kuwa kiumbe kipya. Si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako (Wagalatia 2:20)
MUNGU ALITUSAMEHE KABLA SISI HATUJAMUOMBA MSAMAHA WALA KUTAMBUA KOSA LETU.MUNGU ALITULIPIA DENI LETU LA DHAMBI KABLA SISI HATUJAMUOMBA MSAMAHA.
Kwa maana imeandikwa: "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi" (Warumi 5:8)."…….Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi". Maana yake tulipokuwa bado hatujaomba msamaha Yesu alikufa kwa ajili yetu. Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Na kwa kufa Kristo inamaanisha tumesamehewa na kulipiwa deni letu. Kazi tunayotakiwa kuifanya ni kuupokea msamaha kwa njia ya toba.
            Hata Yesu Kristo alipoteswa na kusulubiwa, na kufa msalabani, aliwasamehe waliomsulubisha na akawaombea msamaha (Luka 23:34); KABLA ya kuombwa msamaha.Na ni sauti ya Yesu Kristo inayosema ndani yako ukikosewa na mtu; "Msamehe kwa kuwa hajui alitendalo". Na Yesu akisema msamehe mtu, basi huna budi kusamehe.Na kumbuka unatakiwa kusamehe KWA AJILI YAKO MWENYEWE, hata kama hujaombwa msamaha ili na wewe usamehewe na Mungu. Usiposamehe unazuia maombi yako yasijibiwe na unazuia baraka zako zingine.


MKRISTO MPAMBANAJI/MPIGANAJI (Samson Mollel - Uzima wa Milele International Ministries)

KUCHELEWA SANA AU KUWAHI SANA KWA MAFANIKIO YAKO KATIKA MAISHA (KIROHO NA KIMWILI) HUTEGEMEANA NA UWEZO WAKO WA KUFANYA VITA YA KIROHO.
Kama unataka kufanikiwa mapema katika maisha yako ya kiroho au ya kimwili lazima ufahamu habari ya vita kubwa iliyopo katika ulimwengu wa roho na ufahamu namna ya kupambana na silaha zinazotumika katika vita ya kiroho. Kama unataka kukua upesi katika huduma yako (Uimbaji, ualimu, uchungaji, uinjilisti, unabii, utume, nk) au kama unataka kukua upesi katika maisha yako ya kawaida (Ndoa, biashara, kilimo/mifugo, kazi n.k) ni lazima ufahamu kuwa kuna vita unapaswa kuishinda kwanza katika ulimwengu wa roho ili hayo yote yadhihirike katika ulimwengu wa mwili. Hebu tujifunze somo hili la safari ya wana wa Israeli kutoka nchi ya utumwa - Misri kwenda nchi ya ahadi Kaanani.
Kutoka 13: 17 – 18, “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha”
SOMO LA KUJIFUNZA KUHUSU SAFARI HII:-
Sababu kubwa ya Mungu kutowapitisha wana wa Israel katika nchi ya wafilisti ni kwakuwa nguvu yao ya kivita ilikuwa ndogo (Kutoka 13:18, lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha) ndio maana wana wa Israel wakapitishwa njia ndefu mno iliyowachukua miaka 40 kufika katika nchi ile ya ahadi. Ninasema hivi kwasababu ushahidi wa kimaandiko unaonesha kuwa umbali kutoka Misri kwenda Kaanan ni mfupi sana na pia hakuna hata haja ya kuvuka bahari kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli (Mwanzo 42, 43 -  tunaona Wana wa Yakobo/Israel wakienda nchi ya Misri kununua chakula zaidi ya mara moja ndani ya muda mfupi. Vilevile tunaona wakati mfalme Herode anatafuta kumuua Yesu wazazi wa Yesu walimtoreshea Yesu Misri – Mathayo 2:13 -14)
Hapa tunawaona wana wa Israeli wakikwea kuelekea nchi ya ahadi hali wamevaa silaha lakini wenye uwezo mdogo wa kupigana ndio maana Mungu akawazungusha mbali sana mahali ambapo wangesafiri kwa wiki 2 au 3 wao wakasafiri kwa miaka 40. Sababu kuu ya kuchelewa huku ni uwezo wao mdogo wa kupambana na maadui kwani Mungu alijua wangekata tamaa (Kutoka 13:17, “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri”). Hivyo Mungu aliwaacha wapite njia ndefu sana (zaidi ya Miaka arobaini) ili wasikate tamaa na kurudi nyuma
SAFARI YA WANA WA ISRAELI NA VITA YA ROHONI
Kwanza kabisa fahamu ya kwamba mtu ni roho na pia fahamu ya kwamba agano la kale ni kivuli cha agano jipya (Kol 2:16-17, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; 17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”) pia tunasoma katika Hebr 10:1, “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao” . Kwa kusoma maandiko haya nataka ufahamu kuwa unachokiona kwa jinsi ya mwilini katika agano la kale ni dhahiri ya rohoni katika agano jipya.
Kwasababu hiyo basi; maisha tunayoishi sasa ni sawa sawa na safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Kaanani. Kufanikiwa kwako au kutofanikiwa inategemeana na uwezo wako wa kupambana kwa jinsi ya rohoni (Vita ya kiroho). Neno la Mungu linasema 2Kor 10 : 3 – 4 “3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome);”.
Inawezekana katika maisha yako umekuwa ukishindwa kufikia malengo yako kwa wakati (Yaani unachelewa kufikia malengo yako kama ulivyopanga), jambo hili lina pande mbili kama ifuatavyo


        i.            Mungu anakuepusha kwa makusudi ili usirudi upotevuni
Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli; Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu kwa kusudi wasije wakaghairi pale watakapo kutana na vita kama wangepitia njia fupi ya nchi ya wafilisti. Wafilisti ni watu ambao ni mahodari sana wa vita na kutokana na uwezo mdogo wa kivita wa Israeli kwa wakati huo ndio maana Mungu akaona ni vyema wapitie njia ndefu lakini wafike katika nchi ya ahadi (Kaanani).
Hata leo wakristo wengi wapo katika hali hii ya wana wa Israeli, wanapitia katika njia ndefu kufikia mafanikio yao (Nchi ya ahadi) kwakuwa uwezo wao wa kiroho kupambanani mdogo. Ni kweli umeokoka na umekombolewa kutoka katika nguvu za giza, ni kweli wewe ndio mteule wa BWANA (yaani Israeli wa leo) lakini uwezo wako wa kivita ni mdogo sana, hivyo Mungu kwa kuona kwamba endapo utakutana na vita kali (Nguvu za giza – wachawi, majini, mizimu nk) katika kufikia mafanikio yako upesi huenda ukakata tamaa na kushindwa kuendelea mbele, Mungu anakupitisha njia ndefu ya mafanikio ili ufike. Njia hii ndefu zaidi ya mafanikio sio kwamba haina vita; lakini vita yake ni nyepesi tofauti na njia fupi ya mafanikio ambayo vita yake ni kali sana.
     ii.            Kwakuwa shetani amefahamu kwamba wewe ni dhaifu katika vita ya kiroho
Vilevile inawezekana katika maisha yako umekuwa ukishindwa kufikia malengo yako kwa wakati (Yaani unachelewa kufikia malengo yako kama ulivyopanga) kwakuwa shetani amefahamu kwamba wewe ni dhaifu katika vita ya kiroho hivyo anakuinulia vita kali ili ushindwe. Katika safari ya wana Israeli tunaona kulikuwa na wafilisti ambao ndio walifanya mpaka Israeli wakashindwa kupitia ile njia ya karibu, leo kuna shetani na mawakala wake (Waganga wa kienyeji, mizimu, mapepo, wachawi nk) ambao ndio wafilisti wa leo katika maisha yako kukuzuia usifikie malengo kwa wakati uliokusudia au uliopangiwa na Mungu. Kwa kifupi shetani anahamisha mipaka ya mafanikio yako ili usifikie kusudi la Mungu kwa wakati uliopangwa na Mungu.
KWANINI MKRISTO UNACHELEWA KUFIKIA MAFANIKIO?
Sababu kubwa ya shetani kuwachelewesha wakristo katika kuifikia nchi ya ahadi (Mafanikio yako) ni kwakuwa wakristo wengi hawajui nguvu iliyopo katika Neno la Mungu au hawalijui kabisa Neno la Mungu, yaani wakristo hawana maarifa ya Neno la Mungu na hivyo wanaangamizwa kabisa Hosea 4:6a “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;” kwa hiyo moja ya sababu ya shetani kutushinda na kutuchelewesha katika kufikia mafanikio ni kukosa maarifa ya kiMungu. Maarifa hayo ni yapi? Tukisoma katika injili ya Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Maandiko yanaeleza wazi wazi kuwa kuna vita katika ulimwengu wa roho na yatupasa kuwa hodari na kuvaa silaha ili tupambane Efeso 6:10 – 13 (Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.).
Ukizidi kusoma utaona silaha za vita vyetu zimeorodheshwa ili kupambana na kumshinda kabisa shetani. Efeso 6: 14-18 “14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”. Tunanona kuwa kuna silaha zimetajwa ambazo ni KWELI, DIRII YA HAKI, MIGUU YA UTAYARI, NGAO YA IMANI, CHAPEO YA WOKOVU, UPANGA WA ROHO, SALA ZOTE NA MAOMBI. Hizi ni silaha alizozitaja mtume Paulo, nawewe unapoingia katika maombi hakikisha umevaa silaha hizi zote ili uweze kupambana pasipo kuumizwa na yule mwovu shetani.

Kuna silaha zaidi za kutumia kupambana na shetani na kadiri unavyosoma Biblia utazifahamu. Kwa ufupi ni kwamba silaha kubwa zaidi ya kupambana na shetani na malaika zake na mawakala zake ni JINA LA YESU, DAMU YA YESU, MOTO WA BWANA.

JINSI YA KUISHINDA DHAMBI JUMLA (Neema ya Kristo)


1. Kubali Kwamba Umeitenda Hiyo Dhambi, Na Usijaribu Kutafuta ANDIKO LA KUJIHAMI, Au MTU WA KUMSINGIZIA... "AFICHAYE DHAMBI ZAKE HATAFANIKIWA, BALI AZIUNGAMAYE NA KUZIACHA, ATAPATA REHEMA" (Mithali 28:13).

2. Ungama Dhambi Hiyo Kwa Lengo La Kutengeneza Na Mungu... "DHAMBI ZENU ZIMEWAFARAKANISHA NA MUNGU" (Isaya 59:2). Halafu Omba "NGUVU YA MUNGU" Kukusaidia "USIRUDIE KUTENDA DHAMBI ILEILE"... Yesu Alisema, "MAANA PASIPO MIMI, NINYI HAMUWEZI NENO/ JAMBO LOLOTE" (Yohana 15:5). Kuishinda Dhambi, Si Kwa Akili Na Jitihada Ya Kimwili, "SI KWA NGUVU WALA SI KWA UWEZO BALI NI KWA ROHO WA BWANA" (Zekaria 4:6).

3. Amua Kwa Dhati KUACHANA NA WATU "WANAOKUSHAWISHI" Au WANAOKUPELEKEA DHAMBINI"... "HERI MTU YULE ASIYEKWENDA KATIKA SHAURI LA WASIO HAKI [Watu Wasioipenda Haki Ya Mungu Na Neno Lake]... WALA HAKUSIMAMA KATIKA NJIA YA WAKOSAJI [Watu Ambao Wao Kutenda Makosa Ni Life Style Yao Na Hawajali Lolote]... WALA HAKUKETI BARAZANI PA WENYE MIZAHA [Makusanyiko Ya Watu Au Vijiwe Ambako Mambo Yasiyomtukuza Mungu Yanapewa Nafasi]" (Zaburi 1:1-2).

4. Badili Mfumo Wako Wa Maisha, Toka Katika Ile Njia Ikupelekayo Dhambini Upesi... Amua Kuishi Kwa Ajili Ya Kumpendeza Mungu Kuliko Yeyote Au Chochote... HII INAHITAJI KUBADILI MFUMO WAKO WA MAWAZO [CHANGE OF MIND]... "MSIIFUATISHE NAMNA YA DUNIA HII, BALI MFANYWE UPYA KWA KUGEUZWA NIA ZENU, MPATE KUYAJUA MAPENZI YA MUNGU YALIYO MEMA, YA KUPENDEZA NA MAKAMILIFU" (Warumi 12:2).

5. Dumu Kwenye Maombi Na Ushirika Na Mungu... MAOMBI YATAKUINGIZA KWENYE UWEPO WA MUNGU, NENO LAKE LITAKUFANYA USHIRIKIANE NAYE... "TENA IPOKEENI CHAPEO YA WOKOVU, NA UPANGA WA ROHO AMBAO NI NENO LA MUNGU. KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, MKIKESHA KWA JAMBO HILO NA KUDUMU KATIKA KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE" (Waefeso 6:17-18).



Rumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”

PIGO LITOKANALO NA MANENO YA KUNENEWA/KUTAMKIWA (Samson Mollel - Uzima wa Milele International Ministries)

YALIYOMO


NENO NI NINI?

Neno ni matamshi yenye maana yanayotoka kwenye kinywa cha mtu au kiumbe.
Kibiblia neno ni yale mambo yaliyojaza moyo wa mtu, ukisoma injili ya Luka 6:45
Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.

NENO LA MUNGU
Neno la Mungu ni lile neno linalotoka kwa Mungu, Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe hivyo si la kulifanyia mzaha. Yohana 1:1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Kwa hiyo neno la Mungu ndilo kweli na limejaa imani hata ya kuumba/kufanya yasiyokuwepo yakawepo. Kama tusomavyo katika Waebrania 11: 3 Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.

NENO LA MUNGU LINATIMIZA MAPENZI YA MUNGU

Tangu mwanzo Mungu Baba ameliweka Neno lake kama mwongozo wa utimilifu wa kusudi lake ambalo msingi wake ni kulitimiza Neno lake. Tunasoma katika Yeremiah 1:12…… kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize. Yapo mambo mengi ambayo katika hayo Mungu ulitimiza neno lake katika kutupatia ushindi kwa maisha yetu ya hapa duniani. Mfano, Zaburi 107:20….. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.

Hivyo neno likitoka katika kinywa cha Mungu haliwezi kumrudia bure, bali lazima litimiza mapenzi yake.  Isaya 55:10 – 11 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma

Katika kitabu cha Isaya tumeona ya kuwa Neno la Mungu linatimiza Mapezi ya Mungu, na ukisoma Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Biblia inasema mawazo ya Mungu ni ya Amani. Kwa mistari hiyo katika kitabu cha Isaya na Yeremia tunamuona Mungu ambaye analiangalia Neno lake ambalo ni la Amani kwa watu wake ili alitimize.

SHETANI NAYE NI MUNGU

Baada ya kuona ya kwamba Neno la Mungu litatimiza mapenzi ya Amani; kumbuka kilichomfanya shetani kutupwa duniani ni ile hali ya kujiinua na kutaka nafasi ya Mungu, yaani alitaka awe kama Mungu alivyo (Isaya 14:12 – 17)Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! 13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. 14 Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. 15 Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo. 16 Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme; 17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” Vilevile habari hii tunaisoma katika kitabu cha nabii Ezekieli 28:14 – 18; 14 “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. 15 Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. 16 Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. 17 Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. 18 Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao”. Baada ya kushindwa kwa mpango huo na kuangushwa na Malaika Mikaeli tunasoma katika Biblia kwamba shetani ameitwa Mungu wa dunia hii 2Kor 4:4 4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.
Kutokana na maelezo katika mistari tuliyoisoma hapo juu tunaona kuwa shetani alitafuta cheo cha Mungu na kushindwa, baada ya kushindwa akatupwa duniani na kuitwa Mungu wa dunia hii, kwasababu hiyo shetani ameigiza tabia za uungu katika hali ya uharibifu (Negatively), hivyo anamuiga Mungu (Jehova) lakini lengo la shetani ni kuharibu kabisa na kuwachukua watu wa Mungu mateka kama linavyosema Neno la Mungu kutoka katika chuo cha Isaya 42:22 “22 Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.” Vilevile Neono hili linapatikana katika Isaya 14:16-17 “16 Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme; 17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” Lakini sasa tunao ushindi kwakuwa Yesu Kristo amepakwa mafuta kwa kazi ya kutukomboa, kutufungua na kutuweka huru kutoka katika umateka wa shetani na mawakala zake kama linenavyo Neno la Mungu kutoka Injili ya Luka 4: 18-19 “18 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Sasa basi; Kama tulivyoona ya kuwa Neno la Mungu litatimiza mapenzi ya Mungu ambayo ni ya Amani kwetu sisi vivyo hivyo neno linalotoka kwa shetani na mawakala wake (waganga, wachawi, wasoma nyota, wapiga ramli nk) litatimiza mapenzi ya uovu wa shetani ikiwa ni pamoja na kuwaua watakatifu wake Mungu na kuipinga injili ya Yesu Kristo.

NAMNA SHETANI ANAVYOSHAMBULIA KWA MANENO

Zaburi 57:4Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali”.
Wanadamu hawa wanaoongelewa katika zaburi hii ni wale mawakala wa mauti yaani wachawi, washirikina, waganga nk. Wanatumia sana ndimi zao (Vinywa vyao kusababisha madhara makubwa kwa watumishi wa Mungu na wanafanya hivyo kwa siri (Faraghani) wakisema hakuna atakayeiona Zaburi 64:3-5 “3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu, 4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi. 5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona?”.
Ninakuombea mtu wa Mungu katika Jina la Yesu kuanzia leo fahamu zako zifunguke na uyaone hata yale manuizo ya kipepo yanayorushwa kwako kwa njia usiyoifahamu kwa jinsi ya kibinadamu. Fuatilia ushuhuda huu kisha utajifunza jambo namna shetani anavyowashambulia watu kwa njia ya maneno (Ndimi) kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yakobo 3:5-9 “5 Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. 6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum……………. 8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. 9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.”

USHUHUDA


Tarehe 11/04/2015 jioni muda wa saa kumi nikiwa Kanisani nafanya usafi akaja binti mmoja ili kufanya usafi kwani ilikuwa ni zamu ya jumuiya yetu; kabla hajaanza tuliongea kidogo huku nikimuuliza kwanini hafiki kwenye maombi na pia nilimuuliza ni kwanini alipata mimba akiwa mdogo sana “alipata mimba akiwa na miaka 16”. Yule binti akaniambia “kaka unataka kufahamu maisha yangu?” nikamjibu ndio, akaniambia “twende tukakae nikueleze habari zangu”. Yule binti alinieleza habari za maisha yake takribani muda wa saa mbili na nusu, aliniambia namna alivyoacha shule akiwa darasa la nne kutokana na umasikini, alinieleza kuwa hakuwahi kumfahamu baba yake mzazi mpaka alipofikisha miaka 16, aliniambia namna mama yake mzazi anavyosumbuliwa na nguvu za giza na jinsi alivyo masikini pia alinieleza jinsi alivyotangatanga katika maisha yake ya kufanya kazi za ndani kutoka nyumba moja hadi nyingine na pia aliniambia jinsi watu walioonesha mapenzi kwake ghafla waligeuka na kumchukia sana wakiwepo baadhi ya dada zake, vilevile alinieleza jinsi alivyopata mimba na matatizo makubwa aliyonayo. Baada ya kunieleza yote hayo nilimuuliza kama ameokoka kasema hajaokoka, nikamuuliza kama yuko tayari akasema yuko tayari. Ndani yangu Roho wa BWANA akanielekeza kuomba naye na maeneo ya kumfungua. Tukaendelea na usafi wa maeneo ya kanisa na baada ya usafi tukaingia katika maombi ya Ukombozi, baada ya maombi yule binti akafunguliwa na kutueleza kuwa yeye hakuwepo duniani bali alikuwa mahali penye giza sana na taa za kule ni macho ya nyoka na kunguru na ndio walikuwa walinzi wake, alituambia kuwa magari ya kule ni majeneza na ndani ya hayo magari “majeneza” ndio kuna taa. Alitueleza jinsi alivyokuja mara tatu kumchukua mchungaji wa kanisa la KKKT – Ngudu bila mafanikio na baada ya kushindwa alipewa adhabu ya kutokula kwa muda wa wiki tatu. Tulipomuhoji ya kuwa ni chakula gani wanakula huko alisema ni nyama na damu za watu, alitueleza hata namna ya kuchukuwa nyama na namna wanavyochukua damu za watu, alitueleza namna wanavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, na mambo mengine mengi sana kuhusu ufalme wa giza (Binti huyu alieleza mambo mengi sana ambayo hapa sijayataja ili kutopoteza lengo la somo hili). Baada ya ukombozi tulimrudisha nyumbani kwao na kuwaeleza mambo yanayowapasa kufanya. Siku moja baadae (Tarehe 13/04/2015) nilipigiwa simu na dada wa huyo binti ambaye ndiye anayekaa naye, alinigombeza sana kwa njia ya simu na kuniambia nikome kabisa kuombea watoto wa watu bila ridhaa ya wazazi wao, nikajitahidi kuongea nae kwa upole na kumueleza kuwa huyo binti anahitajika kuendelea kufanyiwa maombi na kufundishwa ili kuimarishwa zaidi kiroho; Lakini huyo dada mtu akazidi kuwa mkali na kunikemea sana hadi nikanyamaza kimya kisha akakata simu. Baada ya kukata simu ghafla hali yangu ilibadilika na kuwa kama mgonjwa mwenye homa kali hadi nilishindwa kuendelea na kazi za ofisi, nikajitenga chumba tofauti na kutafakari nini kimetokea lakini sikupata jibu hadi baada ya saa moja wazo likanijia nikampigia simu mtumishi mmoja (Mwalimu Samson wa Ukombozi Ministries for All Nations) na baada ya kumueleza akaniambia nimeshambuliwa na silaha nisiyoifahamu ambayo ni maneno ya kichawi na yalikuwa na lengo la kunidhoofisha ili wanimalize kwa silaha nyingine. Nilipofahamu hivyo nikawajulisha wanamaombi wenzangu kwa ujumbe mfupi wa maneno (Message) nami nikaanza kuomba kwa kuchomoa mishale yote ya kipepo niliyorushiwa kwa njia ya maneno, baada ya maombi hayo nikapata nguvu mpya na kuendelea na kazi kama kawaida.

Baada ya haya yote ndipo nikapata maarifa ya kuandika somo hili ili watu wa Mungu wajifunze

NAMNA DAUDI NA GOLIATHI WALIVYOPAMBANA KWA MANENO

1Samweli 17:44-47 44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. 45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.

Tunaona vita ya Daudi na Goliathi ilianzia katika maneno, Goliathi alianza kumtisha Daudi kwa maneno ya kudhoofisha na kumuonesha kwamba hawezi na atampiga Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni” lakini Daudi alifahamu kuwa vita tayari ilikuwa imeanzia katika maneno kwahiyo akaanza kukiri maneno ya ushindi na kumuonesha Goliathi kwamba atamshinda kwa jina la BWANA ……Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli……..

Ninataka kukutia moyo mtu wa Mungu kuwa usinyamaze kimya unaposhambuliwa kwa maneno na watesi wako bali wewe ukiri ushindi kama vile Daudi alivyokiri ushindi na kisha kumuua Goliathi

WATU WA MUNGU HUPIGWA KWA MANENO

Watumishi wengi wa Mungu hupigwa kwa maneno na hata kuangushwa katika utumishi na wao (watumishi wa Mungu) huacha kulitumikia kusudi la Mungu na kuanguka kabisa. Nabii Yeremia alifanyiwa mpango wa kupigwa na watesi wake kwa maneno (Yeremia 18:18  Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.). Mawakala wa shetani (wachawi, waganga, nk) hukaa vikao na kutamka maneno yenye nguvu za giza (manuizo ya kipepo), maneno hayo huja kutumika katika hali ya maisha ya kawaida na pale unaponenewa maneno hayo, hali yako ya kiroho huanza kuporomoka ghafla na kupungukiwa nguvu za kiroho kama ilivyonitokea katika ushuhuda huo hapo juu; hali hii hutokana na ukweli kwamba yapo mapepo (roho za kuzimu) ambazo huchukua maneno yote ya uovu yaliyonenwa na kuyasimamia kuhakikisha yanatimia katika uovu uliotamkwa. Kumbuka kila wakati unapokuwa katika kuomba, futa kila maneno ya kipepo uliyonuiziwa kwa kufahamu au pasipo kufahamu.

TUNALO TUMAINI NA USHINDI MKUU

1Yohana 3: 8 “……. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
Pamoja na mawakala wa shetani (Wachawi, waganga, wapiga ramli, nk) kutumia maneno kama mishale ya kuwapiga wenye haki wa Mungu kama tunavyosoma katika Zaburi 64:3-6 “3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu, 4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi. 5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona? 6 Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa”; Uhakika ni kwamba tunalo tumaini ya kuwa BWANA atatupigania na kuwakwaza watesi wetu na kuwapiga kwa maneno yao wenyewe; yaani yale maneno (Manuizo ya kipepo) yanayotoka katika vinywa vyao yatawapata wenyewe na kuwapiga wao; ikiwa utafahamu haya mtu wa Mungu unayo nguvu na ujasiri wa kupambana na kila nguvu za giza na mishale yote ya yule adui Zaburi 64:7-10 (7 Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa. 8 Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa. 9 Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya Mungu, Na kuyafahamu matendo yake. 10 Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia, Na wote wenye moyo wa adili watajisifu.)

MAOMBI YA KUFUTA MANENO YA KIPEPO/KICHAWI

1.     Omba Rehema
ü  Tumia Zaburi ya 51:1 – 19
2.     Jifunike kwa Damu ya Yesu, Vaa Silaha na Omba Nguvu za Mungu
ü  Katika Jina la Yesu najifunika kwa Damu ya Yesu kuanzia utosini mpaka unyayoni, naifunika familia yangu yote, kazi, biashara, mashamba na huduma yangu (Taja na vingine); Sawasawa na Neno lako kutoka Waefeso 6:14 – 18 nina vaa silaha zote za Mungu (14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;). Ninaipokea ile nguvu kwakuwa Roho Mtakatifu yu ndani yangu sasa (Matendo1:8 8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.)
3.       Msihi Mungu akutie nguvu na upako wa kumshinda adui.
ü  Zaburi 89:20-24 Nimemwona ………..(taja jina lako), mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. 21 Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu.  22 Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.  23 Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia. 24 Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
4.     Anza maombi ya VITA
ü  Katika Jina lenye uweza Mkuu, Jina la Yesu; Ninabatilisha kila maneno yaliyonenwa kwa faragha kwaajili yangu katika ulimwengu wa giza
ü  Kwa Damu ya Yesu; Ninayafuta maneno yote yaliyonakiliwa au kuandikwa na makatibu wa wachawi katika ulimwengu wa giza
ü  Katika Jina la Yesu; Ninaichomoa mishale yote ya ibilisi na mawakala wake katika Ndoa, Kazi, Biashara, Mashamba, Uchumi, Afya, Mahusiano (Endelea kutaja na maeneo mengine)
ü  Mahali popote nilipochomwa mshale wa kipepo kwa njia ya maneno najiosha kwa Damu ya Yesu inenayo mema (Waebrania 12:24 na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.)
5.     Omba ulinzi kwa kujifunika kwa Damu ya Yesu na Moto wa Roho Mtakatifu
6.     Mshukuru Mungu kwa matendo yake makuu kwako.

7.      Mwimbie Mungu wimbo wa ushindi (Zaburi 144)