Sunday, May 19, 2019

SOMO: ROHO MTAKATIFU NDANI NA JUU YA MTU (Samson Mollel 0767/0713 664 338; Feb, 2019)


Mungu tunaye mwabudu ni mmoja katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu na hao wote ni umoja kwani hizo nafsi tatu ni nafasi za utendaji. Kwa mfano wewe unaweza kuwa ni mtoto kwa wazazi wako (wanakuita mtoto) halafu unaweza kuwa mume/mke wa mtu Fulani (unaitwa mume/mke) na unaweza kuwa mzazi wa watoto/mtoto (Unaitwa baba au mama), katika nafasi zote kila moja inayo majukumu yake ambayo huenda hayaingiliani kabisa lakini mtu ni mmoja. Hauwezi kuyafanya majukumu ya mume/mke wako kwa watoto au wazazi wako na viyohivyo hauwezi kuyafanya majukumu yako kwa wazazi kuwa ya watoto wako. Hivyo ndivyo ilivyo kwamba Mungu wetu ni mmoja katika nafasi (tofauti ya majukumu) anazo nafsi tatu.

Roho mtakatifu ni nafsi (person) kamili ya Mungu katika nafsi tatu za Mungu. Roho Mtakatifu ni nafsi tendaji (executive person) ya mambo yote ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Utendaji wa Mungu katika maisha ya mwandamu ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu, ishara, miujiza, uponyaji na kila namna ya kufunguliwa hufanywa na Roho Mtakatifu. Mawasiliano (Communication) yote ya mtu aliyeokoka na ulimwengu wa roho yanawezeshwa na Roho Mtakatifu.


NI AHADI YA MUNGU KUTUPA ROHO WAKE

Yesu alijua vyema kwamba sisi peke yetu hatuwezi kufanya jambo lolote ndio maana akaahidi kwamba ijapokuwa anaondoka atamtuma Roho Mtakatifu ambaye atatupasha habari na mambo yote hata yale ambayo Yesu haukuweza kutueleza
Yohana 16:12-13 “12 Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. 13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. 14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. 15 Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.”



ROHO MTAKATIFU NDANI NA JUU YA MTU

Utendaji wa kazi wa Roho Mtakatifu unatofautiana kulinga na nafasi aliyoichukuwa kwa wakati huo au mahali alipokaa kwa wakati huo. Roho Mtakatifu akiwa ndani ya Mtu utendaji wake ni tofauti na akiwa juu ya mtu huyo huyo.


ROHO MTAKATIFU NDANI YA MTU

Roho Mtakatifu anaweza kukaa ndani ya mtu, mtu yeyote aliyeokoka anaye Roho Mtakatifu kama yanenavyo maandiko.
1Kor 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;”
1Kor 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”


Kazi za Roho Mtakatifu akiwa ndani ya Mtu

v  Ili tuweze kumpendeza Mungu

Roho Mtakatifu anapokuja ndani yako ni ili uweze kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi ambazo chanzo chake ni mwili kuvutwa na mambo ya dunia. Roho Mtakatifu anatusaidia kuishi maisha ya utakatifu kwakuwa yeye (Roho Mtakatifu) ni mtakatifu kama alivyo Mungu.
Warumi 8:8-9 “8 Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. 9 Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”


v  Kutuhuisha kutoka katika hali ya kufa

Baada ya anguko la mwanadamu pale bustanini Edeni kilitokea kifo cha kiroho ambapo Roho wa Mungu alimwacha mwanadamu, baada ya Yesu kuja na kuimwaga damu yake ndipo daraja la mawasiliano likajengwa tena na sisi tuakahuishwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Rumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”


v  Kushuhudia kwamba sisi ni watoto wa Mungu

Roho Mtakatifu anapokaa ndani ya mwanadamu anashuhudia pamoja na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu na tumemshinda ibilisi na tumesamehewa dhambi hivyo sisi ni warithi wa ule uzima wa milele.
Rum 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”


v  Ni msaidizi wetu

Baada ya kuondoka kwa Yesu Kristo ambaye ni Mungu aliyekaa pamoja na sisi katika hali ya mwili (Emanueli) alisema kwamba atamtuma msaidizi kwetu ambaye atausaidia katika mambo yote ya kiroho na hata jinsi ya kunenda katika mwili ili tuweze kumpendeza Mungu
Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.”


v  Hutushuhudia kwa habari ya dhambi haki na hukumu

Roho Mtakatifu ndani yetu hutushuhudia kwa habari ya dhambi haki na hukumu. Jambo hili Roho Mtakatifu hulifanya kwa watu wote hata wale ambao hawajaokoka kwani huwashuhudia wale ambao hawajamwamini Yesu kwamba bado dhambi ipo ndani yao na hukumu inakuja
Yohana 16:8 “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”


v  Hutusaidia kuomba

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba mwanadamu hata uombe kwa bidii sana hauwezi kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, hii ndio sababu Bwana Yesu Kristo akamtuma Roho wake Mtakatifu ili atusaidie katika kuomba kwetu tuweze kumpendeza Mungu.
Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”
Inaweza kusemwa kwamba; Roho Mtakatifu kutuombea ni sawa na Mungu kuomba ndani yetu wenyewe ili atujibu mwenyewe, yaani ni sawa na kupewa mtihani na majibu yake hapohapo


ROHO MTAKATIFU JUU YA MTU

Hapo awali nilitangulia kusema kwamba kuna tofauti kubwa ya Roho Mtakatifu kuwepo ndani ya mtu na Roho Mtakatifu kuwepo juu ya mtu. Neno la Mungu linatufundisha kwamba Roho Mtakatifu anaweza kukaa juu ya mtu kama yanenavyo maandiko

Wakati wowote Roho Mtakatifu anaposhuka juu ya mtu ni kwaajili ya kuufunua utukufu wa Mungu katika maisha yetu, yaani kudhihirisha uweza na nguvu za Mungu katikati ya wanadamu.

Matendo ya Mitume 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Roho Mtakatifu anapoachiliwa au anapokuja na kukaa juu yako tambua kwamba unakazi ya kukamilisha mbele yako, yaani Roho Mtakatifu akikaa juuu yako sio kwaajili ya kukuongoza au kukufundisha au kukushuhudia, ni kwaajili ya kufanya kazi kwa uweza na nguvu za Mungu na kwa ishara na miujiza. Ndio maana tunaona Yesu anawaambia wanafunzi wake maneno haya “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Huyu Roho Mtakatifu akikaa juu yetu anatupa nguvu za kuihubiri injili na kulitangaza Neno la Mungu kama walivyofanya mitume bila ya woga na kwa ujasiri mkuu.

SWALI: Roho Mtakatifu yupo juu yako? Unaweza kuihubiri injili? Unaweza kumshuhudia Yesu kwa mataifa (majirani, ofisini, shambani, shuleni, hospitalini n.k), unaweza kuamuru nguvu za giza kuachia maisha yako na ya watu wengine (Unaweza kuwafungua waliofungwa na shetani, unaweza kuwatoa walio mashimoni)


BAADHI YA MIFANO YA KWENYE BIBLIA INAYOONESHA MATENDO YA ROHO MTAKATIFU ANAPOKUWA JUU YA MTU.

Mambo aliyoyafanya Yesu kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu
Utendaji wa Yesu Kristo uliwezeshwa na Roho Mtakatifu, hakuna Jambo alilolifanya Yesu kwa nguvu zake pekee bali kwa uweza wa Roho Mtakatifu

        i.            Kuanza kuhubiri na kwenda Nyikani kujaribiwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu

Yesu alipoenda nyikani kujaribiwa haikuwa kwa nguvu zake pekee bali ni kwanguvu za Roho Mtakatifu na kwa uweza wa Roho Mtakatifu, kazi hii Yesu aliifanya mara baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu wakati alipobatizwa

Luka 3:21-22 “21 Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; 22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Biblia inasema ………Roho Mtakatifu akashuka juu yake…………. Baada ya Roho Mtakatifu kushuka juu ya Yesu ndipo akaanza kufanya kazi iliyomleta hapa duniani yaani kufundisha (Luka 3:23 “Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,”) kabla Roho Mtakatifu hajashuka juu ya Yesu hatuoni Yesu akifanya jambo lolote kubwa kama baada ya kushukiwa na Roho wa Mungu.

Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu na kumpeleka nyikani ili kujaribiwa (Roho Mtakatifu alimpeleka Yesu kumfundisha na kumpa mtihani ili afaulu)

Luka 4:1 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani,”
Yesu aliweza kumshinda ibilisi kwakuwa aliongozwa na Roho Mtakatifu


     ii.            Habari za Yesu zilienea nchi nyingi kwa uweza wa Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu anapokuwa juu yako katika eneo la huduma uliyoitiwa habari zako zinasambaa kila mahali kwa kasi kwakuwa sio wewe unayetenda bali ni Roho wa Mungu juu yako, habari za Yesu zilisambaa sana mara baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu juu yake.

Luka 4: 14 “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.”


   iii.            Kuwafungua wafungwa na kuponya kwa uweza wa Roho Mtakatifu

Yesu Kristo alisema mwenyewe kwa kinywa chake kwamba matendo yote anayofanya ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu aliyekaa juu yake

Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Hapo awali nilisema kwamba wakati wowote Roho Mtakatifu anaposhuka juu ya mtu ni kwaajili ya kuufunua utukufu wa Mungu katika maisha yetu, yaani kudhihirisha uweza na nguvu za Mungu katikati ya wanadamu. Tunaona Roho Mtakatifu yupo juu ya Yesu Kristo kwa kazi zifuatazo

ü  Kuwahubiri maskini habari njema – Hawa ni maskini wa rohoni wenye kiu na njaa ya Neno la Mungu waliopo katika mataifa na hata masikini wa mwilini ambao Yesu amekuwa masikini ili wao wawe matajiri

ü  Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao – Walifungwa na nguvu za giza kwenye magereza/mashimo/mapango/ majumba ya kuzimu, waliofungwa na magonjwa na kila namna ya udhaifu

ü  Vipofu kupata kuona tena Vipofu waliopofushwa fikra na ibilisi, vipofu katika maisha ya kiuchumi/afya/ndoa/kazi/biashara n.k. Vipofu wa macho ya damu na nyama

ü  Kuwaacha huru waliosetwa – Kusetwa ni ile hali ya kukanyagwa au kuwa chini ya utawala kandamizi unao umiza, Roho Mtakatifu Yupo juu ya Yesu kuwafungua watu wote waliosetwa

ü  Kutangaza mwaka wa Bwana  uliokubaliwa
Mambo hayo yote Yesu aliyafanya kwakuwa Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.

TAFAKARI: Kama Roho Mtakatifu hayupo juu yako unaweza kufanya chochote? Kama Yesu Kristo ambaye ni Mungu alimuhitaji Roho Mtakatifu kuyafanya hayo yote, si zaidi sana kwamba sisi tunamuhitaji zaidi Roho Mtakatifu juu yetu?

   iv.            Roho Mtakatifu alitenda kazi ya kutoa mapepo Yesu alipoyakemea
Neno la Mungu linatufundisha kwamba Yesu mwenyewe alitumia uweza wa Roho Mtakatifu kutoa mapepo yaliyowatesa watu kipindi kile alipoishi katika mwili duniani. Yesu mwenye amekiri katika Neno lake kwamba ametoa mapepo kwa nguvu za Roho Mtakatifu

Luka 11:20 “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

Mathayo 12:28 “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”


      v.            Mitume walihubiri Neno na kufanya ishara na miujiza kwa uweza wa Roho Mtakatifu

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona matendo makuu ya Roho Mtakatifu katika huduma walizofanya mitume wa Yesu. Kwanza tunaona Roho Mtakatifu akishuka juu yao kama ndimi za moto (kumbuka kwa Yesu alishuka kama hua/njiwa)
Matendo 2:1-4 “1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

Baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu Petro akawahubiria na tunaona watu elfu tatu wanampokea Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Matendo 2:41 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.”

Baada ya hayo tunaona Mitume wakifanya ishara na miujiza ya hali ya juu mno kwa uweza wa Roho Mtakatifu kama yanenavyo maandiko.
Matendo 5:12,15 “12 Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; 15 hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.”

Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.”

Matendo 19:11-12 “11 Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; 12 hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”


   vi.            Roho Mtakatifu juu ya Samsoni

Samsoni ni mmoja kati ya waamuzi wa Israeli ambao Mungu aliwapa nguvu nyingi sana za mwili, ijapokuwa Samsoni alikuwa ni mwanadamu wa kawaida lakini aliweza kufanya peke yake jambo lililohitaji mamia aumaelfu ya watu kulifanya. Mambo yote ya kushangaza aliyofanya Samsoni ni baada ya kujiliwa na Roho Mtakatifu juu yake kama tunavyosoma katika Neno la Mungu.

Waamuzi 14:6,19 “6 Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya. 19 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.”

Waamuzi 15:14 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.”
Kumbuka wapo Waamuzi wengi wa Israeli ambao Roho Mtakatifu alikuja juu yao kwa nguvu (Waamuzi 3:9-10, Waamuzi 11:29)


 vii.            Roho Mtakatifu juu ya Mariamu

Yesu kuja duniani ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu, alifanyika mimba katika tumbo la bikra Mariamu kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu na akawa mwili hata Mungu akazaliwa katikati ya wanadamu akiwa na sura na miili kama yetu
Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”

Hapa tunajifunza kwamba ili Baraka zako (za rohoni kama ilivyoandikwa katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;”) ziumbike katika hali ya mwili na uyaone mafanikio kwa macho yako, ni lazima Roho Mtakatifu aje juu yako na kukuwezesha.


viii.            Roho Mtakatifu juu ya Daudi

Mafanikio yote katika maisha ya mfalme Daudi yalianza baada ya Roho Mtakatifu kushuka juu yake kwa nguvu, kutokea hapo maisha ya Daudi yalibadilika akawa ni mtu wa ushindi kwa kila jambo analolifanya, akamshinda Goliathi, akawaua wafilisti na maadui zake wote akawashinda na hatimaye kuwa mfalme hata sasa kiti chake cha ufalme kinatawala Dunia yote.
1Samweli 16:13 “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Bwana Yesu akubariki sana mtu wa Mungu, ninaamini kuna kitu umepata katika somo hili ili utoke mahali kwenda mahali.

Jambo moja kubwa nataka utafakari wakati wote ili upate kiu ya kutafuta ushirika na Roho Mtakatifu ni hili; ikiwa Yesu mwenyewe alimuhitaji Roho Mtakatifu ili kuzitenda kazi za Mungu Baba, Je? Wewe haumuhitaji huyu Roho Mtakatifu?

Ikiwa Mitume walifanya ishara na miujiza ya kupita kawaida kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu, Je? Wewe haumuhitaji huyu Roho Mtakatifu.



MAOMBI:

Baba katika jina la Yesu Kristo ninaomba Toba na rehema kwa maovu makosa na dhambi nilizozitenda katika maisha yangu na kuchafua mavazi yangu, leo ninaomba unioshe na kuyatakatisha mavazi yangu kwa damu yako Bwana Yesu ili Roho Wako Mtakatifu aweze kuingia ndani yangu na kukaa juu yangu kwa ishara na miujiza katika jina la Yesu Kristo

Roho Mtakatifu, nimetambua leo yakuwa wewe ni BWANA, wewe ni Mungu, wewe ndiye unayetenda ishara na miujiza ya kila namna ndani ya Yesu Kristo, ninaomba unisamehe ujinga wangu wa kutotambua nafasi yako katika maisha yangu. Ninakukaribisha sasa ndani yangu uwe Kiongozi na Mwalimu wangu unifundishe namna ya kumpendeza Mungu Baba, karibu juu yangu kwa Nguvu na Uweza wako ili niweze kuzifanya kazi za Baba katika dunia hii kwa jina la Yesu Kristo

Na sasa ninakiri ya kwamba Roho Mtakatifu upo juu yangu sasa, na umenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Umenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa kwa nguvu na uweza wako katika jina la Yesu Kristo.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba na Ushirika wa Roho Mtakatifu ukae namimi katika maisha yangu yote sasa na hata milele, Amen.