Friday, January 6, 2017

SOMO: UMUHIMU WA KUWA NA MALENGO MBELE ZA MUNGU KWA UONGOZI WA ROHO MTAKATIFU


NINI MAANA YA MALENGO?

Malengo ni hatua Fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na anatarajia kuifikia. Jambo la msingi unalopaswa kulielewa; Ni muhimu kulifahamu lengo lako vizuri ambalo unatakiwa kulifikia. Ni vizuri ulifafanue vizuri lengo lako ili lieleweke kwani ufafanuzi mzuri wa lengo/malengo yako utakusaidia katika kujiwekea mikakati mizuri ya utekelezaji.
Ni vizuri kujua mahitaji ili kufikia malengo yako, hii itakusaidia ili ujue unatakiwa kuomba nini na kwa kiasi gani.
Mtu wa Mungu tuutazame mfano wa Hana katika Biblia na namna alivyo muomba Mungu (1Samweli 1:1-20)

1.      Hana alijua kuwa alikuwa na lengo kubwa (Kuomba mtoto kwa Mungu) hivyo alisukuma maombi mwaka baada ya mwaka-1Samweli 1:3 (sio siku moja, sio mwezi mmoja, sio mwaka mmoja ni miaka ilipita). Uchokozi wa Penina haukumkatisha tamaa bali ulikuwa ni mtaji (chachu) kwa Hana na akendelea kushughulikia lengo lake.
Inawezekana wewe mtu wa Mungu unatafuta mume/mke lakini siku ya kwanza ulipotukanwa au kudhalilishwa kwamba hautaolewa/hautaoa basi umekiri na kukubali kabisa kwamba kwakuwa miaka imepita mingi basi siwezi kufanikiwa tena; Hapana usikate tamaa angalia malengo yako (stay focused) kwani unapoongea maneno ya kujifunga shetani anaenda nayo mbele za Mungu kukushitaki (Mithali 18:20-21 “20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. 21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”). Wana wa Mungu wengi wamejifunga wenyewe kutofikia malengo yao


2.      Fahamu kwamba wapo watu ambao wataendelea kukupa moyo ili uridhike na hali mbaya ya maisha uliyonayo na kuishia kuteseka bila kufikia malengo. Hana alijua kuwa sadaka na maneno mazuri aliyopewa na Elikana (mume wake) ni kitanzi cha kuendelea kukaa katika hali ngumu (1Samweli 1:4-8), yaani vilimfanya akubaliane na matatizo yake kuwa ni sehemu ya maisha yake. Mtu wa Mungu amka na umgeukie BWANA ili uweze kutimiza malengo yako ya miaka mingi katika mwaka huu 2017 kama alivyofanya Hana (1Samweli 1:9-10).

3.      Jambo lingine napenda kukukumbusha mtu wa Mungu kuhusu kuweka nadhiri, kuweka nadhiri lazima upime gharama ya nadhiri yako. Wapo watu kutokana na uzito wa matatizo yao wameweka nadhiri kwa Mungu, halafu malengo yao yanapotimia wanasahau kuondoa nadhiri zao na kumsahau Mungu (Kumbukumbu 8:12-14 “12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13 na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;”)



4.      Jambo jingine ambalo unahitaji kujua ili kufikia malengo yako nmna ya kukabiliana na dharau ya kuhani (Mchungaji, Padre, Shemasi, Kasisi, Mwinjilisti, Katekista, Nabii, Mtume n.k). Tunamuona kuhani Eli anamwita Hana kuwa ni mlevi (1Samweli 1:14), lakini Hana hakuumizwa na dharau ya kuhani bali  alizidi kuwa mnyemnyekevu na kumtazama BWANA ili lengo lake litimie. Kuna watu wanatathimini mazingira yako ya maombi na kukuambia mambo ya kukukatisha tamaa, usikate tama songa mbele na malengo yako


5.      Ni muhimu kuomba mpaka ufikie malengo yako, fahamu kuwa unapoona dalili za kufikia malengo sio uhakika ya kwamba malengo yametimia (Yaani kupata mimba sio kupata mtoto) unahitajika kuendelea kuomba bila kukoma mpaka maleengo yako yatimie. Kumbuka unapoomba madhabahuni, unapofanikiwa rudi madhabahuni kumshukuru Mungu.

ü  Kwa muombaji/mwanamaombi ni vyema kuweka malengo mapema kabla ya mwaka mpya haujaingia na kama ulikuwa na malengo ya mwaka unaomalizikia fanya tathimini kwanza kisha fanya maamuzi ya kuweka malengo mapya. Inawezekana mpaka sasa ulikuwa haujaweka malengo kwa mwaka huu mpya 2017, bado unaweza kuweka malengo yako na ukapanga mikakati ya utekelezaji.


ü  Kumbuka kuwa matatizo au changamoto ulizokabiliana nazo mwaka jana (2016) zifanye ziwe mtaji wa kukuongezea umakini unapoweka malengo mapya mwaka huu mpya 2017. Kuna waombaji/wanamaombi wengine changamoto walizokutana nazo katika huduma/kazi/ndoa/biashara n.k. zimewavunja moyo kabisa na hawawezi kuendelea tena na yale malengo ambayo hawajayafikia; mkumbuke Hana alivyoweza kugeuza changamoto kuwa mtaji wake *(1Samweli 1:1-20)*  Hana aliomba kwa bidii kubwa pamoja na ukweli kwamba alitukanwa sana na kudharauliwa na kuchokozwa na Rebeka.


ü  Fahamu pia kwamba ni hatari sana kubaki unafikiri au unawaza juu ya matatizo yaliyokupata au yaliyopo katika kukamilisha malengo yako, jambo la kufanya ni kufikiri zaidi juu ya kukabiliana na matatizo na kusonga mbele.


ü  Ukweli ni kwamba malengo yanafungwa ndani ya muda, ukiweka malengo pia upange na mikakati na jinsi ya kuitekeleza hiyo mikakati ndani ya muda maalum; yaani kila lengo lipe muda wa utekelezaji wake *(Muhubiri 3:1-8 _“1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu………………………..”)_* Fahamu majira na nyakati katika utekelezaji wa malengo yako; yaani kama wewe ni mkulima lazima ulime na kupanda kwa kufuata kalenda ya kilimo kwa zao husika na sio upande wakati wa palizi au uaplilie wakati wa kuvuna, fahamu mafanikio ya malengo yako yamefungwa na muda. Kwasababu hiyo, Muda ni ufunguo muhimu sana wa kukusaidia kufikia malengo yako; kwahiyo lazima ujifunze kufikiri ki-muda na kufanya kazi kwa kufuata muda.

*MAMBO MATANO MUHIMU KATIKA KUPANGA MALENGO*
A.      Weka malengo yako mapema kwa kufuata vipaumbele vya kwako kwa uongozi wa Roho Mtakatifu

B.      Weka mikakati ya kukusaidia kutekeleza lengo lako kwa uongozi wa Roho Mtakatifu


C.      Fanya tathimini ya utekelezaji wa malengo yako kila baada ya muda kwa uongozi wa Roho Mtakatifu

D.     Boresha malengo yako kwa kadiri muda unavyokwenda kwa kuzingatia tathimini uifanyayo mara kwa mara kwa uongozi wa Roho Mtakatifu


E.      Jenga mazoea ya kuyasoma na kufanya tafakari juu ya malengo yako mara kwa mara na kuwashirikisha watu wanaoweza kukusaidia kwa uongozi wa Roho Mtakatifu

*MUHIMU:*

v  Kumbuka kuwa mtu aliye mwana wa Mungu hawezi kuweka malengo yeye binafsi kwasababu yeye (mtu aliyeokoka) anao ubia (Ushirika) na Mungu kuanzia rohoni hadi mwilini, yaani kwa kila kitu anachokifanya lazima amshirikishe Mungu. *(Yohana 14:23, 15:1-8, Wakolosai 1:29)*

v  Fahamu kwamba kuwa mwanamaombi haimaanishi kuwa haupaswi kutumia akili kwani unapokosa akili unakuwa mpumbavu *(Mathayo 7:24)* na hata kama utaomba kiasi gani pasipo kutumia akili na maarifa hauwezi kufikia malengo (Hosea 4:6)


v  Kila unachotaka kufanya lazima umuulize Mungu kama ndilo kusudi lake ufanye jambo hilo au lah! Kwani unapokuwa umeokoka sio wewe tena bali ni Yesu aishiye ndani yako. Hapo ulipo mtu wa Mungu upo pamoja na Mungu *(Yohana 14:23)* hivyo kila unachokifanya umshirikishe Mungu.

v  Kwahiyo jifunze kushirikiana na Roho Mtakatifu katika kila hatua za maisha yako, ukifanya hivyo utakuwa katika mahali pazuri katika hatua za maisha yako *(Warumi 8:12-17)*. Ni muhimu kutambua kuwa unaishi kwaajili ya kutimiza kusudi la Mungu na sio la kwako, ukijua hilo utatafuta malengo ya Mungu zaidi kuliko malengo yako binafsi *(Waefeso 2:8-10, Yeremia 1:4-10)*.

Katika miili yetu (Damu na nyama) tumebebeshwa sheria ya mwili inayotupele kinyume na mapenzi ya Mung (yaani kuikataa sheria ya Mungu); kwasababu hiyo kuna watu wanaotegemea kuongozwa na Roho Mtakatifu wakati wa Ibada, lakini katika mambo mengine ya maisha hawapo na Roho Mtakatifu. Mungu anachosema ni kwamba unapomkubali Yesu unaingia kwenye Mkataba na Mungu *(Yohana 14:23)*, Roho Mtakatifu anakuwa ndiye kiongozi wetu na unapomshirikisha ROHO hautaweza kukwama.
Kumbuka hata Yesu aliongozwa na ROHO kwenda jangwani, na kama ROHO alimuongoza kwenda kujaribiwa vilevile ROHO alimuongoza kujibu/kushinda mitego ya shetani.

*_KWANINI UNATAKIWA KUONGOZWA NA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUPANGA MALENGO YA MWAKA HUU MPYA 2017 NA SIO KUONGOZWA NA AKILI AU MAWAZO YAKO?_*

1.     *ILI TUSITIMIZE TAMAA ZA MWILI*

*(Wagalatia 5:16, Warumi 8:7)*

Kwa kawaida mwili huwa na “mvutano” na Roho wa Mungu. Roho wa Mungu atakuongoza katika njia yake na mwili nao utakuongoza katika njia zake, hivyo nafsi yako inategemea ni roho yupi kapewa kipaumbele. Kumbuka siku zote Roho Mtakatifu na roho ya shetani, wote hutumia nafsi ya mwanadamu kupeleka kwenye mawazo ili kuchujwa, na ufahamu kuwa nia ya mwili imebeba uadui juu ya Mungu. Unapoongozwa na Roho Mtakatifu unaweza kuushinda ulimwengu na ukafanya mambo sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Bila kuongozwa na Mungu ile nia ya mwili itakutawala na kukufanya ufuate mambo ya dunia na hautaweza kufanya mapenzi ya Mungu.

2.     *ILI TUPATE KUYAELEWA MAFUMBO YA MUNGU*

Moja ya sababu ya muhimu ya kuongozwa na roho mtakatifu katika kupanga malengo ya mwaka huu mpya 2017, ni ili uweze kuayelewa mafumbo ya Mungu na kuatafakari mambo ya rohoni katika roho. Roho wa Mungu ndiye mwenye ufahamu na kuyachunguza na kuyafasiri mambo ya rohoni na kutusaidia kuelewa kilichopo (Makusudi ya Mungu) kwenye ufalme wa Mungu kuhusu wewe na mipango yako ya kila siku
Roho Mtakatifu akiisha kukufahamisha malengo unayopaswa kuweka, anakusaidia katika kuyatekeleza ili yalete faida juu ya maisha yako. *(1Wakorintho 2:10)*


3.     *ILI TUPATE KUYAJUA TULIYOKIRIMIWA NA MUNGU*

Jambo lingine linalo jibu swali la kwanini unatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kupanga malengo ya mwaka huu mpya 2017, ni ili upate kuyajua yale uliyokirimiwa na Mungu na kuyapokea mambo ya roho wa Mungu kwa uaminifu (1Wakorintho 2:10-16).

Yapo mambo ambayo ni lugha ya rohoni sana kiasi ambacho hata Mungu akisema na wewe hauwezi kuelewa, ukikubali kuongozwa na Roho Mtakatifu; yeye ROHO atakupa kuyajua yote ambayo Mungu amekukirimia katika maisha yako kwa ujumla.

Unapokubali kuongozwa na Roho Mtakatifu ndipo unapopata msaada wa kujijua wewe mwenyewe, maana atakusaidia kujua tabia yako, Baraka zako na uelekeo wako wa maisha ya sasa nay a baadae. Nje ya Roho Mtakatifu ni vigumu kutambua hayo, ukiwa ndani ya Roho Mtakatifu atakusaidia kufanya kazi pamoja nawe katika kila hatua *(Zaburi 32:8)*.

4.     *ILI ATUSAIDIE KUOMBA YALE TUNAYOTAKIWA KUOMBA*

Sababu nyingine ya kuongozwa na Roho Mtakatifu ni ili ROHO atusaidie kuomba yale tunayotakiwa kuomba kwa wakati ule. Mtu wa Mungu usijijengee mfumo wa kuomba kwa mazoea kwa kufuata ratiba ulizopanga wewe, lazima umruhusu ROHO akuongoze kuomba kwa wakati unaostahili, ROHO akikuambia uombe usisubiri mpaka muda uliopanga wewe ndio uombe; ukifanya hivi hautaweza kuyafikia malengo yako kwa mwaka huu mpya.

 Unapokataa muongozo wa Roho Mtakatifu basi yeye (ROHO) anakuacha na wewe na unaanza kuwa dhaifu katika kutekeleza mikakati ya kufanikisha malengo yako, udhaifu unatokana na kushindwa kumruhusu ROHO aongoze maisha yako, Roho Mtakatifu anapoacha kuongoza maisha yako utaona hizi ishara:-

v  Sio rahisi kuomba kwa muda mrefu na wakati mwingine unavutwa na mawazo mbalimbali (Mfano:-Matatizo ya siku hiyo au changamoto unazokabiliana nazo katika maisha yako).

v  Kushindwa kuomba jinsi itupasavyo. Unapomshirikisha Roho Mtakatifu anatusaidia kuomba itupasavyo na anatuwezesha hata tunapochoka, pia anatufundisha namna ya kuomba na anatuongoza yapi tuyaombee kwa wakati huu. Pia ROHO anatufunulia vita iliyoko mbele yetu na kufundisha namna ya kuishinda. *(Warumi 8:26-27, 1Yohana 5:13-15)*


5.     *ILI ATUONGOZE KATIKA KUFANYA MAAMUZI*

Hakuna namna unayoweza kufanya maamuzi sahihi kama ndani yako hauna msaada wa Roho Mtakatifu, bila Roho Mtakatifu utavutwa na tama za mwili, utavutwa na shetani kisha utafanya maamuzi mabaya.

Kufanya maamuzi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, yako maamuzi mengi sana ambayo anatakiwa kuyafanya na hawezi kuyakwepa; maamuzi hayo yatafanyika kwa usahihi tu kama utakuwa na Roho Mtakatifu ndani yako na kumruhusu akusaidie kufanya maamuzi yako. *(2Wakorintho 3:17, Warumi 8:1-2, Kumbukumbu 16:18-20, 17:8-13)*

Unaweza kumzuia Roho Mtakatifu asikuongoze, Roho Mtakatifu ni Mungu mwenye nguvu zote na maarifa yote, Yeye pia (ROHO) anayo hiari ya kufanya kazi na mtu. Kumbuka kuwa Roho Mtakatifu ni msaidizi kwetu (Yaani yupo mwenye majukumu {wewe} lakini yeye ROHO anasaidia) *[Yohana 4:24, 14:18-23, 1Wakorintho 3:16-17, 6:19-20, 2Wakorintho 6:16]*

*MUHIMU:* Fahamu ya kuwa unaweza ukamzimisha Roho Mtakatifu ndani yako *(1Wathesalonike 5:19)*; unamzimisha Roho Mtakatifu kwa kukataa uongozi wake kwani yeye ROHO halazimishi kukuongoza ila anatamani mfanye mashauriano kwa kila jambo *(Yohana 14:16)*


Samson Mollel 0767 664 338
_Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)_
*_www.uzimawamileleministries.blogspot.com_*


No comments: