Tuesday, August 6, 2019

HUKUMU YA MIUNGU (Samson Mollel 0767 664 338)


UTANGULIZI

Bwana Yesu apewe sifa!

Nimepata ufunuo wa kuandika somo hili kutokana na maswali ambayo nimekuwa nikimuuliza Mungu kwa habari ya ugumu wa kufunguliwa watu waliookoka. Kuna watu wameokoka na wanampenda Yesu na wamekiri kuwa Yesu ni Bwana wa maisha yao, lakini maisha ya watu hawa hayasogei na hata yakionesha dalili za mafanikio bado mambo huharibika na kurudi kuwa mabaya kuliko hapo mwanzo. Katika tafakari hiyo, ROHO MTAKATIFU akanipitisha katika Neno la Kristo na kunifunulia mambo yanayofanywa na miungu kwa kuwatumia wanadamu na kuharibu maisha yetu.

Hapo pia nikagundua kwanini kuna watu wameokoka na wanaitwa wachawi na wanawatokea watu kwenye ndoto na kuwadhuru lakini hao watu hata uchawi hawaujui! Kumbe kuna miungu inaweza kuwashikilia watu katika hali ya utumwa hata kama wanajiona wako huru.
Karibu tujifunze pamoja


MIUNGU NI NINI?
Mapepo ambayo yamepewa sadaka za namna mbalimbali katika familia, ukoo, kijiji, wilaya au taifa na kuabudiwa na watu wakiwemo viongozi wa familia, ukoo, kijiji, wilaya au taifa wanakuwa wakubwa na wanapokea cheo cha mungu wa eneo waliloabudiwa na kupewa sadaka, eneo linaweza kuwa na mungu zaidi ya mmoja (miungu).
Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kwamba kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu hicho ndio mungu/miungu yako, hata kama kitu hicho hakisemi/hakineni lakini kumbuka kuna nguvu ya rohoni inayokufanya ukipende hicho kitu na kukipa kipaumbele zaidi ya Mungu wa kweli.


Neno la Mungu linaonya katika amri za Mungu kwamba tusiwe na miungu mingine “3 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 23 Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie.” Kutoka 20:3-5, 23


Lakini hapo kabla injili haijaingia katika nchi ya Tanzania na hata duniani, kabla Mungu hajamtuma Yesu kuja duniani kutuokoa mataifa yote (isipokuwa Israeli) walikuwa wakiabudu miungu tangu anguko la mwanadamu, shetani alikuwa mungu kwetu na sisi tulimuabudu shetani na tukampenda kwa mioyo yetu (kwani tulikuwa katika viuno vya mababu zetu walipomuabudu shetani). Hivyo basi shetani akatufunga kwake na kutuweka katika nira yake na kupofusha ufahamu wetu ili tusimjue Mungu wa kweli kama yanenavyo maandiko kutoka 2Wakorintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”


Sasa ili tuweze kuona neema ya Mungu na maisha yetu yafanane na watu wanaomjua Mungu wa kweli, ni lazima tutoke kwenye ushirika na mashetani ili tuweze kushirikiana na Jehova sawa na Neno la Mungu kutoka 1Wakorintho 10:19-22 “19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? 20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. 21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. 22 Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?”
Ili Mungu awe upande wako lazima ukubali kuwa upande wake kwa moyo wako wote na roho yako yote na uutoe mwili wako kwa Yesu pekee. Neno la Mungu linasema “Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Luka 4:6-8


NINI KINATOKEA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO UNAPOABUDU MIUNGU?

Katika ulimwengu wa roho Mungu Jehova ni mume kwa wote wanaomwabudu na sisi tunao mwabudu ni kama wake kwake kama tunavyosoma katika maandiko


Yeremia 31:31-32 “31 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. 32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.”
Kwa maana hiyo Mungu ni mume kwa kanisa kama tunavyosoma katika Neno la Mungu Waefeso 5:23 “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.”

Mtu yoyote anayefanya ibada za miungu mingine kama vile matambiko na kuwaendea waganga wa kienyeji na wasoma nyota na watu wa namna hiyo unakuwa umefanya zinaa kwa jinsi ya roho yaani umefanya uzinzi na uasherati na hasira ya Mungu inawaka juu yako kwa wivu mkubwa.

Kwa lugha nyingine ukiwa haumjui Jehova (Mungu wa kweli) basi unakuwa umeolewa na miungu ya ukoo wenu na hiyo inakumiliki kama vile mume anavyokuwa na mamlaka kwa mke wake. Sasa pata picha ya mwanamke aliyeolewa na mume (hata iwe kwa njia ya uasherati) halafu huyo mke akataka kwenda kwa mume mwingine, unadhani itakuwa jambo rahisi? Je ni rahisi kumuachia mke aende kwa mume mwingine hata kama huyo mke haujamlipia mahari?

Ninasema hayo kwasababu shetani alituoa bure na sasa anataka kuendelea kutumiliki bure hata kama Mungu amtulipia fidia ya damu yake (Isaya 52:2-3 “2 Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa. 3 Maana Bwana asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa bila fedha.”), sasa inakubidi uchukue hatua ya kukataa ndoa ya miungu na uasherati huu wa kiroho kuanzia sasa (Walawi 17:7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.)


LAZIMA MIUNGU IHUKUMIWE NDIPO UACHIWE HURU
Mtu wa Mungu inawezekana mahali ulipo umekaa muda mrefu bila kupata majibu kwanini upo hapo hapo, kila siku uanomba na kufunga sana lakini hakuna majibu. Ni kwasababu hauwezi ukatoka katika kifungo chochote kabla ya hukumu haijatoka juu ya miungu inayokushikilia, hukumu hiyo ni kuyavunja maagano yao yote na kuondoa utawala wa miungu na kumruhusu Yesu atawale Yeye peke yake.



TAFAKARI YA WANA WA ISRAELI KUTOKA MISRI

Haikuwa jambo rahisi kuwatoa wana Israeli kutoka nchi ya Misri, Mungu alimtuma Musa na Haruni kwa ishara na miujiza lakini Farao hakuweza kuwaachi Israeli kwani miungu ya Misri ilikuwa na nguvu kuliko maamuzi ya Farao pamoja na mapigo tisa ambayo Mungu aliwapiga Wamisri. Misri walipigwa kwa mapigi yafuatayo

                     i.            Maji kuwa damu (Kutoka 7:20)
                   ii.            Vyura wakaifunika nchi ya misri (Kutoka 8:6)
                 iii.            Mavumbi kuwa chawa nchi nzima (Kutoka 8:17)
                 iv.            Inzi waliiharibu nchi ya Misri (Kutoka 8:24)
                   v.            Wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa (Kutoka 9:6)
                 vi.            Majivu kuwa majipu kwa wanadamu na wanyama (Kutoka 9:10)
               vii.            Mvua ya mawe na moto iliyoharibu mazao, miti na wanyama (Kutoka 9:23-24)
             viii.            Nzige walioukula kila kilichosazwa na mvua ya mawe (Kutoka 10:13-14)
                 ix.            Giza nchi nzima kwa muda wa siku tatu (Kutoka 10:22)
                   x.            PIGO LA MZALIWA WA KWANZA – HUKUMU YA MIUNGU (Kutoka 12:12,29)

Inawezekana hata wewe umeshawaadhibu sana miungu ya kwenu kwa kila aina ya silaha halafu wanakimbia na baadae wanarudi tena na sasa unajiuliza ufanyeje? Hilo swali lilinisumbua sana kwa muda mrefu, lakini Roho Mtakatifu amenifundisha jambo hili kwa manufaa ya wengi ili tutoke kwenye kila aina ya uonevu wa nguvu za ibilisi.
Farao (au shetani kwa lugha ya kiroho) alipigwa mapigo mengi sana na katika kila pigo alikubali kuwaachia Israeli halafu alipotafakari kwamba ni watumwa waliompa faida alikataa kuwaruhusu, alifanya hivyo mara kwa mara hata katika lile pigo la mwisho aliwaruhusu na kuwafuatia.


Kutoka 8:8, 15 “8 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu. 15 Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena……….. 28 Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni. 32 Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.”


HUKUMU YA MIUNGU

Mungu (Jehova) ni hakimu
Ili hukumu itolewe lazima awepo hakimu ambaye anayo mamlaka ya kuhukumu kesi husika. Neno la Mungu linatuthibitishia kwamba Mungu wetu Jehova ni hakimu (Zaburi 50:6 “Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.”); kama Mungu ni hakimu, basi anao uwezo wa kusimama na kutoa hukumu katika mashauri yote ya rohoni na mwilini, hivyo Jehova anao uwezo wa kuhukumu miungu ya kila namna sawasawa na Neno lake kutoka Zaburi 82:1 “Mungu asimama katika kusanyiko la Mungu; Katikati ya miungu anahukumu.”

Ili ushinde vita yoyote ile katika maisha yako ya kiroho lazima upambane na miungu kwanza


Hukumu ya Miungu ya Misri

Kama tulivyoona hapo awali katika kipengele cha “TAFAKARI YA WANA WA ISRAELI KUTOKA MISRI”. Farao (shetani/miungu/majini/mapepo/mizimu wa leo) alipigwa kwa mapigo tisa mazito sana ambayo katika hali ya kawaida angewaruhusu Israeli kutoka katika nchi ya utumwa na kwenda nchi ya ahadi kaanani; lakini haikuwa hivyo kwani kila aliposema nitawaruhusu, miungu ya Misri ilikataa kuwaruhusu Israeli kwenda nchi ya ahadi na kuendelea kuwatesa. Hii inamaana kwamba unaweza ukawa unakiri Neno la kufunguliwa na kutoka katika mateso ya maisha yako lakini kama miungu haijahukumiwa hauwezi kutoka hapo kwani itarudi na kukuvuta kila wakati, Muite Yesu aje aihukumu miungu ya ukoo na familia na kabila lako kwani Jehova ni mkuu sana sawa na Neno la Mungu katika kitabu cha Kutoka 18:11 Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.”.
Kwasababu ya nguvu ya miungu ya misri juu ya Israeli, Jehova akaamua kuachilia pigo la mwisho kuwahukumu miungu ya Misri iliyowatesa Israeli ili Farao awaachilie na waende nchi ya ahadi Kaanani.
Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.”

Ni baada ya pigo hili ndipo Farao anawaachilia wana wa Israeli waende kwao, kumbe bila kushughulika na miungu ni vigumu sana kutoka katika utumwa wa maisha yako. Mungu wetu anazo nguvu nyingi na uweza mwingi wa kuihukumu na kuimaliza kabisa miungu ya kabila na koo zetu ambazo zimeshikilia afya, uchumi, huduma, ndoa n.k.
Yeremia 43:12-13 “12 Nami nitawasha moto katika nyumba za miungu ya Misri, na kuziteketeza, na kuwachukua mateka; naye atajipamba kwa nchi ya Misri, kama vile mchungaji avaavyo nguo zake; naye atatoka huko na amani. 13 Naye atazivunja nguzo za Bethshemeshi, iliyoko huko katika nchi ya Misri, na nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza.”


Safari ya Israeli kwenda nchi ya ahadi

Katika safari ya wana wa Israeli kwenda nchi ya ahadi, kila walipotaka kumiliki eneo Jehova aliwaamuru washughulikie madhabahu na maashera ya miungu wa maeneo hayo kwanza kabla hawajaanza wao kuishi hapo, kwani usipoipiga miungu kwanza itakuzidi nguvu baadae na kukukosesha kwa Mungu aliye hai
Kutoka 34:12-14 “12 Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. 13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao. 14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.”

Kumb 7:5-6 “5 Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. 6 Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”

Kumb 12:2-3 “2 Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; 3 nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.”


Mafanikio ya Gideoni yalipatikana baada ya hukumu ya miungu

Katika kitabu cha Waamuzi mlango wa sita tunasoma habari za mtu anayeitwa Gideoni, kijana huyu mbingu zilimtambua kama shujaa na mwamuzi atakayewaokoa Israeli na mikono ya Wamidiani, lakini Gideoni alikuwa mdogo wa umri, masikini halafu muoga. Kumbe hali yote hiyo ya umasikini na woga ilitengenezwa na miungu ya baali ambayo baba yake alikuwa ni kuhani; sasa ili Gideoni kuwashinda wamidiani ilibidi kwanza avunje madhabahu za mungu baali sawasawa na maelekezo ya Jehova kama tunavyosoma katika maandiko

Waamuzi 6:25, 28 “25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa.”
Kumbe pamoja na jitihada za Gideoni kutafuta mafanikio ya maisha yake asingefanikiwa kama asingeshughulikia miungu ya baali ambayo baba yake mzee Yoashi alikuwa akiiabudu na familia nzima ikaingia kwenye kifungo cha miungu ya baali.


Ushindi wa Daudi dhidi ya Goliathi ni baada ya miungu kuhukumiwa

Vita ya Dadudi na Goliathi ilianzia rohoni kati ya Mungu na miungu, ukisoma kwa makini maneno ya Goliathi utaona kabla hajaanza kupigana na Daudi alimkabidhi Dadudi kwa miungu ya wafilisti na kwaku Daudi alifahamu vizuri ulimwengu wa roho na yeye akamkabidhi Goliathi na miungu yake kwa Jehova

1Samweli 17:43-46 “43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. ……….. 45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.”

Mtu wa mungu ni mara ngapi unakumbuka kwamba unapoingia kwenye vita yoyote iwe na wachawi au na nguvu zozote za giza inatakiwa kwanza miungu ihukumiwe halafu ndipo ushinde vita?


Nabii Eliya na manabii wa baali

Ushindi wa Eliya Mtishibi dhidi ya manabii wa baali ni baada ya hukumu kwa miungu ya baali na ndipo manabii wa baali waliogopa na kualizwa na nabii Eliya. Unaweza kuuliza ilikuwaje manabii wa baali wakahukumiwa na Jehova? Ukisoma katika kitabu cha 1Falme 18:19 utaona Eliya Mtishbi akimwambia mfalme Ahabu amkusanyie manabii wa baali na manabii wa ashera ambao jumla yao ni 850 “Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli.”. Hawa manabii walikuwa ni makuhani wa baali na baali alikuwa ndio Mungu wa madhabahu yao, maana yake walikuwa wakimuomba mungu baali na alikuwa akiwajibu ndio maana kulikuwa na makuhani, madhabahu na washirika wa hiyo madhabahu ambao ni mfalme Ahabu na mkewe na wana-Israeli.

1Falme 18:26-40 “26 Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya………..28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. 29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. 30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika……..33 Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni………37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. 38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji……….40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.”


Lakini ilipofika wakati wa Mungu au miungu kujidhihirisha, hapo Jehova alianza kwa kuhukumu miungu ya baali na utaona wakati makuhani wote wa baali wakimuita baali ajidhihirishe baali mungu wao hakuweza kufanya chochote na ndio maana hata nabii Eliya aliweza kuwaua manabii wote 850 wa baali. Kumbuka hawa manabii ndio waliokuwa wakuu kuliko manabii wa Jehova katika wakati huo na ndio sababu walikaa na kunywa katika meza ya mfalme Ahabu.


Miungu ikuhukumiwa wanaoitegemea wanapata hofu na kuanguka

Tunasoma habari ya sanduku la agano kuibiwa/kuchukuliwa na wafilisti jambo lililosababisha Israeli kushindwa vibaya kwenye vita na wafilisti, kwa lugha nyingine ni kama kusema Mungu wa Israeli alinyamaza kimya na kuibiwa na Wafilisti (1Samweli 4). Lakini baada ya kufika nchi ya Wafilisti sanduku la agano la Bwana likawekwa kwenye nyumba ya dagoni mungu wa Wafilisti. Mungu Jehova akamwadhibu dagoni kwa mapigo makali sana na baada ya kumwadhibu dagoni mungu wa wafilisti akaanza kuwapiga na wafilisti kwa majipu na panya hata wenyewe wafilisti wakashindwa mbele ya Israeli kwakuwa mungu wao (dagoni) alipigwa na Jehova

1Samweli 5:2-7 “2 Wafilisti wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka karibu na Dagoni. 3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili, kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena. 4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu. 5 Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo. 6 Lakini mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake. 7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu.”


JINSI YA KUIHUKUMU MIUNGU

Katika agano la kale Mungu alitoa maelekezo ya jinsi ya kuihukumu miungu ya Misri kama tunavyosoma katika maandiko katika kitabu cha Kutoka 12:5-7 “5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.
 6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. 7 Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.”

Lakini katika vita tuliyonayo sasa haipo kwa jinsi ya mwili kama ilivyokuwa kipindi cha Israeli kule Misri (Ijapokuwa nguvu vita ilitoka rohoni lakini vita ilifanyika mwilini). Mtume Paulo nasema 3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 2Kor 10:3-4.

Kumbe sasa tunaweza kufanya vita na miungu bila kuchinja kondoo au mwana mbuzi kwani Mungu kwa neema yake alimtoa Yesu Kristo awe ni mwanakondoo asiye na mawaa kwaajili yetu kama tunavyosoma katika maandiko

Waebrania 9:22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” Hii ndio sababu Israeli wote iliwapasa kumwaga damu ya mnyama (pasaka) ili Misri wakiwa wanapigwa pamoja na miungu yao wao Israeli wawe salama kama tunavyosoma katika Kutoka 12:5-6 “5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. 6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.”

Iliwalazimu Israeli ili kuwa salama na mauti siku ile wachinje mwanakondoo au mwanambuzi na ile damu ya mnyama huyo ipakwe kwenye miimo ya milango yao ili malaika napopita kupiga usiku asiwadhuru; lakini pia iliwabidi kufanya hivyo ili watoke katika hali ya utumwa na mateso ya zaidi ya miaka mia nne waliokuwa Misri.
Unaposoma kitabu cha Kutoka tunaona Mungu anaagiza Israeli kutoa PASAKA (Mwanakondoo asiye na hila) ili baada ya hapo Jehova apite kuihukumu miungu ya Misri na wamisri, Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.”

Tunaweza kujifunika kwa damu ya Yesu na kuruhusu mapigo kutoka kwa Mungu kwenda kwa miungu iliyoshikilia maisha yetu katika ukoo, familia, kijiji, mkoa, na nchi/taifa. Kama walivyofanya wana Israeli katika miimo ya milango yao na kuipaka damu ili hukumu ya Mungu ipite juu ya miungu ya Misri na wamisri, leo tunayo damu ya Yesu kwa jinsi ya rohoni ambayo tunaweza kujipaka na familia zetu, watoto wetu, ndoa zetu, kazi zetu n.k halafu tumruhusu Mungu kupita ili kuihukumu ile miungu iliyotufunga katika mateso ya aina mbalimbali.



*UBARIKIWE NA BWANA YESU, ENDELEA KUOMBA NA ACHILIA HASIRI YA MUNGU JUU YA miungu YA UKOO NA FAMILIA YENU*