UTANGULIZI
Bwana Yesu apewe
sifa!
Nimepata ufunuo wa
kuandika somo hili kutokana na maswali ambayo nimekuwa nikimuuliza Mungu kwa
habari ya ugumu wa kufunguliwa watu waliookoka. Kuna watu wameokoka na
wanampenda Yesu na wamekiri kuwa Yesu ni Bwana wa maisha yao, lakini maisha ya
watu hawa hayasogei na hata yakionesha dalili za mafanikio bado mambo
huharibika na kurudi kuwa mabaya kuliko hapo mwanzo. Katika tafakari hiyo, ROHO
MTAKATIFU akanipitisha katika Neno la Kristo na kunifunulia mambo yanayofanywa
na miungu kwa kuwatumia wanadamu na kuharibu maisha yetu.
Hapo pia
nikagundua kwanini kuna watu wameokoka na wanaitwa wachawi na wanawatokea watu
kwenye ndoto na kuwadhuru lakini hao watu hata uchawi hawaujui! Kumbe kuna
miungu inaweza kuwashikilia watu katika hali ya utumwa hata kama wanajiona wako
huru.
Karibu tujifunze
pamoja
MIUNGU NI NINI?
Mapepo ambayo yamepewa
sadaka za namna mbalimbali katika familia, ukoo, kijiji, wilaya au taifa na
kuabudiwa na watu wakiwemo viongozi wa familia, ukoo, kijiji, wilaya au taifa
wanakuwa wakubwa na wanapokea cheo cha mungu wa eneo waliloabudiwa na kupewa
sadaka, eneo linaweza kuwa na mungu zaidi ya mmoja (miungu).
Kwa lugha rahisi
tunaweza kusema kwamba kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu hicho ndio
mungu/miungu yako, hata kama kitu hicho hakisemi/hakineni lakini kumbuka kuna
nguvu ya rohoni inayokufanya ukipende hicho kitu na kukipa kipaumbele zaidi ya
Mungu wa kweli.
Neno la Mungu
linaonya katika amri za Mungu kwamba tusiwe na miungu mingine “3 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 4
Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu
mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5
Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu
mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne
cha wanichukiao, 23 Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala
miungu ya dhahabu, msijifanyie.” Kutoka
20:3-5, 23
Lakini hapo kabla
injili haijaingia katika nchi ya Tanzania na hata duniani, kabla Mungu
hajamtuma Yesu kuja duniani kutuokoa mataifa yote (isipokuwa Israeli) walikuwa
wakiabudu miungu tangu anguko la mwanadamu, shetani alikuwa mungu kwetu na sisi
tulimuabudu shetani na tukampenda kwa mioyo yetu (kwani tulikuwa katika viuno
vya mababu zetu walipomuabudu shetani). Hivyo basi shetani akatufunga kwake na
kutuweka katika nira yake na kupofusha ufahamu wetu ili tusimjue Mungu wa kweli
kama yanenavyo maandiko kutoka 2Wakorintho
4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia
hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake
Kristo aliye sura yake Mungu.”
Sasa ili tuweze
kuona neema ya Mungu na maisha yetu yafanane na watu wanaomjua Mungu wa kweli,
ni lazima tutoke kwenye ushirika na mashetani ili tuweze kushirikiana na Jehova
sawa na Neno la Mungu kutoka 1Wakorintho
10:19-22 “19 Basi niseme nini? Ya
kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni
kitu? 20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala
si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea
kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. 21 Hamwezi kushirikiana katika meza
ya Bwana na katika meza ya mashetani. 22 Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu
zaidi ya yeye?”
Ili Mungu awe
upande wako lazima ukubali kuwa upande wake kwa moyo wako wote na roho yako
yote na uutoe mwili wako kwa Yesu pekee. Neno la Mungu linasema “Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye
peke yake.” Luka 4:6-8
NINI KINATOKEA KATIKA ULIMWENGU WA
ROHO UNAPOABUDU MIUNGU?
Katika ulimwengu
wa roho Mungu Jehova ni mume kwa wote wanaomwabudu na sisi tunao mwabudu ni
kama wake kwake kama tunavyosoma katika maandiko
Yeremia 31:31-32 “31 Angalia, siku
zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na
nyumba ya Yuda. 32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika
siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano
langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa
mume kwao, asema Bwana.”
Kwa maana hiyo Mungu
ni mume kwa kanisa kama tunavyosoma katika Neno la Mungu Waefeso 5:23 “Kwa maana mume
ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa
mwili.”
Mtu yoyote
anayefanya ibada za miungu mingine kama vile matambiko na kuwaendea waganga wa
kienyeji na wasoma nyota na watu wa namna hiyo unakuwa umefanya zinaa kwa jinsi
ya roho yaani umefanya uzinzi na uasherati na hasira ya Mungu inawaka juu yako
kwa wivu mkubwa.
Kwa lugha nyingine
ukiwa haumjui Jehova (Mungu wa kweli) basi unakuwa umeolewa na miungu ya ukoo
wenu na hiyo inakumiliki kama vile mume anavyokuwa na mamlaka kwa mke wake.
Sasa pata picha ya mwanamke aliyeolewa na mume (hata iwe kwa njia ya uasherati)
halafu huyo mke akataka kwenda kwa mume mwingine, unadhani itakuwa jambo
rahisi? Je ni rahisi kumuachia mke aende kwa mume mwingine hata kama huyo mke
haujamlipia mahari?
Ninasema hayo
kwasababu shetani alituoa bure na sasa anataka kuendelea kutumiliki bure hata
kama Mungu amtulipia fidia ya damu yake (Isaya
52:2-3 “2 Jikung'ute mavumbi;
uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti
Sayuni uliyefungwa. 3 Maana Bwana asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa
bila fedha.”), sasa inakubidi uchukue hatua ya kukataa ndoa ya miungu na
uasherati huu wa kiroho kuanzia sasa (Walawi
17:7 Wala hawatatoa tena sadaka zao
kwa wale majini, ambao huwafuata ili
wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi
baada ya kizazi.)
LAZIMA MIUNGU IHUKUMIWE NDIPO UACHIWE
HURU
Mtu wa Mungu
inawezekana mahali ulipo umekaa muda mrefu bila kupata majibu kwanini upo hapo
hapo, kila siku uanomba na kufunga sana lakini hakuna majibu. Ni kwasababu
hauwezi ukatoka katika kifungo chochote kabla ya hukumu haijatoka juu ya miungu
inayokushikilia, hukumu hiyo ni kuyavunja maagano yao yote na kuondoa utawala
wa miungu na kumruhusu Yesu atawale Yeye peke yake.
TAFAKARI YA
WANA WA ISRAELI KUTOKA MISRI
Haikuwa jambo
rahisi kuwatoa wana Israeli kutoka nchi ya Misri, Mungu alimtuma Musa na Haruni
kwa ishara na miujiza lakini Farao hakuweza kuwaachi Israeli kwani miungu ya
Misri ilikuwa na nguvu kuliko maamuzi ya Farao pamoja na mapigo tisa ambayo
Mungu aliwapiga Wamisri. Misri walipigwa kwa mapigi yafuatayo
i.
Maji kuwa damu (Kutoka 7:20)
ii.
Vyura wakaifunika nchi ya misri (Kutoka 8:6)
iii.
Mavumbi kuwa chawa nchi nzima (Kutoka 8:17)
iv.
Inzi waliiharibu nchi ya Misri (Kutoka 8:24)
v.
Wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa (Kutoka
9:6)
vi.
Majivu kuwa majipu kwa wanadamu na wanyama (Kutoka
9:10)
vii.
Mvua ya mawe na moto iliyoharibu mazao, miti na
wanyama (Kutoka 9:23-24)
viii.
Nzige walioukula kila kilichosazwa na mvua ya mawe
(Kutoka 10:13-14)
ix.
Giza nchi nzima kwa muda wa siku tatu (Kutoka
10:22)
x.
PIGO LA MZALIWA WA KWANZA – HUKUMU YA MIUNGU
(Kutoka 12:12,29)
Inawezekana hata
wewe umeshawaadhibu sana miungu ya kwenu kwa kila aina ya silaha halafu
wanakimbia na baadae wanarudi tena na sasa unajiuliza ufanyeje? Hilo swali
lilinisumbua sana kwa muda mrefu, lakini Roho Mtakatifu amenifundisha jambo
hili kwa manufaa ya wengi ili tutoke kwenye kila aina ya uonevu wa nguvu za
ibilisi.
Farao (au shetani
kwa lugha ya kiroho) alipigwa mapigo mengi sana na katika kila pigo alikubali
kuwaachia Israeli halafu alipotafakari kwamba ni watumwa waliompa faida
alikataa kuwaruhusu, alifanya hivyo mara kwa mara hata katika lile pigo la
mwisho aliwaruhusu na kuwafuatia.
Kutoka 8:8, 15 “8 Ndipo Farao
akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa
kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili
wamtolee Bwana dhabihu. 15 Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya
moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena……….. 28 Farao akasema,
Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani;
lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni. 32 Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo
nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.”
HUKUMU YA MIUNGU
Mungu (Jehova) ni hakimu
Ili hukumu itolewe
lazima awepo hakimu ambaye anayo mamlaka ya kuhukumu kesi husika. Neno la Mungu
linatuthibitishia kwamba Mungu wetu Jehova ni hakimu (Zaburi 50:6 “Na mbingu
zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.”); kama Mungu ni
hakimu, basi anao uwezo wa kusimama na kutoa hukumu katika mashauri yote ya
rohoni na mwilini, hivyo Jehova anao uwezo wa kuhukumu miungu ya kila namna
sawasawa na Neno lake kutoka Zaburi 82:1
“Mungu asimama katika kusanyiko la Mungu;
Katikati ya miungu anahukumu.”
Ili ushinde vita yoyote ile katika maisha yako ya kiroho lazima upambane
na miungu kwanza
Hukumu ya Miungu ya Misri
Kama tulivyoona
hapo awali katika kipengele cha “TAFAKARI
YA WANA WA ISRAELI KUTOKA MISRI”. Farao
(shetani/miungu/majini/mapepo/mizimu wa leo) alipigwa kwa mapigo tisa mazito
sana ambayo katika hali ya kawaida angewaruhusu Israeli kutoka katika nchi ya
utumwa na kwenda nchi ya ahadi kaanani; lakini haikuwa hivyo kwani kila aliposema
nitawaruhusu, miungu ya Misri ilikataa kuwaruhusu Israeli kwenda nchi ya ahadi
na kuendelea kuwatesa. Hii inamaana kwamba unaweza ukawa unakiri Neno la
kufunguliwa na kutoka katika mateso ya maisha yako lakini kama miungu
haijahukumiwa hauwezi kutoka hapo kwani itarudi na kukuvuta kila wakati, Muite
Yesu aje aihukumu miungu ya ukoo na familia na kabila lako kwani Jehova ni mkuu
sana sawa na Neno la Mungu katika kitabu cha Kutoka 18:11 “Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko
miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.”.
Kwasababu ya nguvu
ya miungu ya misri juu ya Israeli, Jehova akaamua kuachilia pigo la mwisho
kuwahukumu miungu ya Misri iliyowatesa Israeli ili Farao awaachilie na waende
nchi ya ahadi Kaanani.
Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya
Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri,
wa mwanadamu na wa mnyama; nami
nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.”
Ni baada ya pigo
hili ndipo Farao anawaachilia wana wa Israeli waende kwao, kumbe bila
kushughulika na miungu ni vigumu sana kutoka katika utumwa wa maisha yako.
Mungu wetu anazo nguvu nyingi na uweza mwingi wa kuihukumu na kuimaliza kabisa
miungu ya kabila na koo zetu ambazo zimeshikilia afya, uchumi, huduma, ndoa
n.k.
Yeremia 43:12-13 “12 Nami nitawasha moto katika nyumba za miungu
ya Misri, na kuziteketeza, na kuwachukua mateka; naye atajipamba kwa nchi
ya Misri, kama vile mchungaji avaavyo nguo zake; naye atatoka huko na amani. 13
Naye atazivunja nguzo za Bethshemeshi, iliyoko huko katika nchi ya Misri, na
nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza.”
Safari ya Israeli kwenda nchi ya ahadi
Katika safari ya
wana wa Israeli kwenda nchi ya ahadi, kila walipotaka kumiliki eneo Jehova
aliwaamuru washughulikie madhabahu na maashera ya miungu wa maeneo hayo kwanza
kabla hawajaanza wao kuishi hapo, kwani usipoipiga miungu kwanza itakuzidi
nguvu baadae na kukukosesha kwa Mungu aliye hai
Kutoka 34:12-14 “12 Ujihadhari nafsi
yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego
katikati yako. 13 Bali utabomoa
madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.
14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye
wivu, ni Mungu mwenye wivu.”
Kumb 7:5-6 “5 Lakini watendeni hivi;
zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao,
ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. 6 Kwa maana wewe u taifa takatifu
kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi
ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”
Kumb 12:2-3 “2 Vunjeni kabisa mahali pote
walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima
mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; 3 nanyi
zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa
moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni
mbali na mahali hapo.”
Mafanikio ya Gideoni yalipatikana baada
ya hukumu ya miungu
Katika kitabu cha
Waamuzi mlango wa sita tunasoma habari za mtu anayeitwa Gideoni, kijana huyu
mbingu zilimtambua kama shujaa na mwamuzi atakayewaokoa Israeli na mikono ya
Wamidiani, lakini Gideoni alikuwa mdogo wa umri, masikini halafu muoga. Kumbe
hali yote hiyo ya umasikini na woga ilitengenezwa na miungu ya baali ambayo
baba yake alikuwa ni kuhani; sasa ili Gideoni kuwashinda wamidiani ilibidi
kwanza avunje madhabahu za mungu baali sawasawa na maelekezo ya Jehova kama
tunavyosoma katika maandiko
Waamuzi 6:25, 28 “25 Ikawa usiku uo huo
Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka
saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile
iliyo karibu nayo; 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema,
tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo
imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu
iliyojengwa.”
Kumbe pamoja na
jitihada za Gideoni kutafuta mafanikio ya maisha yake asingefanikiwa kama
asingeshughulikia miungu ya baali ambayo baba yake mzee Yoashi alikuwa
akiiabudu na familia nzima ikaingia kwenye kifungo cha miungu ya baali.
Ushindi wa Daudi dhidi ya Goliathi ni
baada ya miungu kuhukumiwa
Vita ya Dadudi na
Goliathi ilianzia rohoni kati ya Mungu na miungu, ukisoma kwa makini maneno ya
Goliathi utaona kabla hajaanza kupigana na Daudi alimkabidhi Dadudi kwa miungu
ya wafilisti na kwaku Daudi alifahamu vizuri ulimwengu wa roho na yeye
akamkabidhi Goliathi na miungu yake kwa Jehova
1Samweli 17:43-46 “43 Mfilisti akamwambia
Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. ……….. 45 Ndipo Daudi
akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana
wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46 Siku hii ya leo Bwana
atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami
leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti,
ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.”
Mtu wa mungu ni
mara ngapi unakumbuka kwamba unapoingia kwenye vita yoyote iwe na wachawi au na
nguvu zozote za giza inatakiwa kwanza miungu ihukumiwe halafu ndipo ushinde
vita?
Nabii Eliya na manabii wa baali
Ushindi wa Eliya
Mtishibi dhidi ya manabii wa baali ni baada ya hukumu kwa miungu ya baali na
ndipo manabii wa baali waliogopa na kualizwa na nabii Eliya. Unaweza kuuliza
ilikuwaje manabii wa baali wakahukumiwa na Jehova? Ukisoma katika kitabu cha 1Falme 18:19 utaona Eliya Mtishbi
akimwambia mfalme Ahabu amkusanyie manabii wa baali na manabii wa ashera ambao
jumla yao ni 850 “Basi sasa upeleke watu,
unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali
mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa
Yezebeli.”. Hawa manabii walikuwa ni makuhani wa baali na baali alikuwa
ndio Mungu wa madhabahu yao, maana yake walikuwa wakimuomba mungu baali na
alikuwa akiwajibu ndio maana kulikuwa na makuhani, madhabahu na washirika wa hiyo
madhabahu ambao ni mfalme Ahabu na mkewe na wana-Israeli.
1Falme 18:26-40 “26 Wakamtwaa yule
ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata
adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala
aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya………..28 Wakapiga
kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu
ikawachuruzika. 29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati
wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala
aliyeangalia. 30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote
wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika……..33 Kisha
akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya
kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya
kuteketezwa, na juu ya kuni………37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa
wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo
wakurudie. 38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa,
na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika
mfereji……….40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata
mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua
huko.”
Lakini ilipofika
wakati wa Mungu au miungu kujidhihirisha, hapo Jehova alianza kwa kuhukumu
miungu ya baali na utaona wakati makuhani wote wa baali wakimuita baali
ajidhihirishe baali mungu wao hakuweza kufanya chochote na ndio maana hata
nabii Eliya aliweza kuwaua manabii wote 850 wa baali. Kumbuka hawa manabii ndio
waliokuwa wakuu kuliko manabii wa Jehova katika wakati huo na ndio sababu
walikaa na kunywa katika meza ya mfalme Ahabu.
Miungu ikuhukumiwa wanaoitegemea wanapata
hofu na kuanguka
Tunasoma habari ya sanduku la agano
kuibiwa/kuchukuliwa na wafilisti jambo lililosababisha Israeli kushindwa vibaya
kwenye vita na wafilisti, kwa lugha nyingine ni kama kusema Mungu wa Israeli
alinyamaza kimya na kuibiwa na Wafilisti (1Samweli 4). Lakini baada ya kufika
nchi ya Wafilisti sanduku la agano la Bwana likawekwa kwenye nyumba ya dagoni
mungu wa Wafilisti. Mungu Jehova akamwadhibu dagoni kwa
mapigo makali sana na baada ya kumwadhibu dagoni mungu wa wafilisti akaanza
kuwapiga na wafilisti kwa majipu na panya hata wenyewe wafilisti wakashindwa
mbele ya Israeli kwakuwa mungu wao (dagoni) alipigwa na Jehova
1Samweli 5:2-7 “2 Wafilisti
wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka
karibu na Dagoni. 3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili,
kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa
Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena. 4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi,
kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na
kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo
vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu. 5 Kwa hiyo makuhani
wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi
kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo. 6 Lakini mkono wa Bwana
ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko
Ashdodi na mipakani mwake. 7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa,
walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono
wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu.”
JINSI YA KUIHUKUMU MIUNGU
Katika agano la
kale Mungu alitoa maelekezo ya jinsi ya kuihukumu miungu ya Misri kama
tunavyosoma katika maandiko katika kitabu cha Kutoka 12:5-7 “5 Mwana-kondoo
wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika
mbuzi.
6 Nanyi
mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano
wa Israeli watamchinja jioni. 7 Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia
katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba
watakazomla.”
Lakini katika vita
tuliyonayo sasa haipo kwa jinsi ya mwili kama ilivyokuwa kipindi cha Israeli
kule Misri (Ijapokuwa nguvu vita ilitoka rohoni lakini vita ilifanyika
mwilini). Mtume Paulo nasema 3 Maana
ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana
silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha
ngome;) 2Kor 10:3-4.
Kumbe sasa
tunaweza kufanya vita na miungu bila kuchinja kondoo au mwana mbuzi kwani Mungu
kwa neema yake alimtoa Yesu Kristo awe ni mwanakondoo asiye na mawaa kwaajili
yetu kama tunavyosoma katika maandiko
Waebrania 9:22 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo
kumwaga damu hakuna ondoleo.” Hii ndio sababu Israeli wote iliwapasa
kumwaga damu ya mnyama (pasaka) ili Misri wakiwa wanapigwa pamoja na miungu yao
wao Israeli wawe salama kama tunavyosoma katika Kutoka
12:5-6 “5 Mwana-kondoo wenu
atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.
6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote
la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.”
Iliwalazimu
Israeli ili kuwa salama na mauti siku ile wachinje mwanakondoo au mwanambuzi na
ile damu ya mnyama huyo ipakwe kwenye miimo ya milango yao ili malaika napopita
kupiga usiku asiwadhuru; lakini pia iliwabidi kufanya hivyo ili watoke katika
hali ya utumwa na mateso ya zaidi ya miaka mia nne waliokuwa Misri.
Unaposoma
kitabu cha Kutoka tunaona Mungu anaagiza Israeli kutoa PASAKA (Mwanakondoo
asiye na hila) ili baada ya hapo Jehova apite kuihukumu miungu ya Misri na
wamisri, Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku
huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu
na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu
ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.”
Tunaweza
kujifunika kwa damu ya Yesu na kuruhusu mapigo kutoka kwa Mungu kwenda kwa
miungu iliyoshikilia maisha yetu katika ukoo, familia, kijiji, mkoa, na
nchi/taifa. Kama walivyofanya wana Israeli katika miimo ya milango yao na
kuipaka damu ili hukumu ya Mungu ipite juu ya miungu ya Misri na wamisri, leo
tunayo damu ya Yesu kwa jinsi ya rohoni ambayo tunaweza kujipaka na familia
zetu, watoto wetu, ndoa zetu, kazi zetu n.k halafu tumruhusu Mungu kupita ili
kuihukumu ile miungu iliyotufunga katika mateso ya aina mbalimbali.
*UBARIKIWE NA BWANA YESU, ENDELEA KUOMBA
NA ACHILIA HASIRI YA MUNGU JUU YA miungu YA UKOO NA FAMILIA YENU*
1 comment:
Nimependa machapisho yako, naomba uwe unanitumia kupitia rvctsemmanuel@gmail.com
Post a Comment