Saturday, August 18, 2018

NGUVU NA UWEZA WA NENO LA MUNGU - Samson Mollel 0767 664 338


Bwana Yesu Kristo apewe sifa!!!


Ninamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa Neema kubwa ambayo amenipa kwa Roho Mtakatifu wake katika Neno lake, katika somo hili tutajifunza kwa sehemu kuhusu Neno katika somo linaloitwa “NGUVU NA UWEZA WA NENO LA MUNGU”. Tuanze kwa kuangalia mambo muhimu unayopaswa ufahamu kuhusu ‘NENO’

Neno ni nini?


Katika hali ya kawaida neno ni matamshi yenye maana yanayotoka kwenye kinywa cha mtu, au mnyama, (neno ni sauti inayotamkwa au kuandikwa pamoja na kutaja jambo fulani). Inawezekana unajiuliza kwanini nimesema mnyama! Ndiyo kuna wakati ama kwa nguvu Mungu au nguvu za giza wanyama wameweza kusema na watu, katika Biblia utaona haya kwenye kitabu cha Hesabu 22:28-30 “28 Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? 29 Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. 30 Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!”


Kibiblia neno ni yale mambo yaliyojaza moyo wa mtu , ukisoma injili ya Luka 6:45 “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”


Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe


Neno la Mungu ni yale yanayotoka katika kinywa cha Mungu, Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe hivyo si la kulifanyia mzaha. Biblia inatufundisha kwamba Neno ni Mungu kama tunavyosoma katika injili ya Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”. Unapoongelea neno la Mungu Fahamu kwamba unamzungumzia Mungu kamili mwenye uwezo wote kwa ki-Mungu.

Mungu analiangalia Neno lake


Yeremia 1:12 “Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.”
Mungu anapotaka kufanya jambo lolote huwa anaangalia Neno lake linasemaje katika hali Fulani, yaani hata kama upo katika tatizo kubwa unapiga kelele na kumuita Mungu kumbuka YEYE akikutazama hakuoni wewe bali analiona Neno lake lilipo ndani yako na umeliamini kiasi gani ili uvuke katika tatizo/changamoto uliyonayo. Kwa lugha nyingine Mungu anamuangalia Yesu Kristo amejaa kiasi gani ndani yako ndipo akutendee hitaji lako.

Neno la Mungu linatimiza mapenzi ya Mungu


Neno la Mungu ni hakika, liruhusu likae ndani yako uliamini utaona ukuu wa Mungu katika hilo Neno lake. Biblia inasema Mungu anapolituma Neno lake ni lazima litimie kama tunavyosoma katika chuo cha nabii Isaya 55:10 – 11 “10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”
Mungu anatoa mfano wa mvua na theluji kwamba lazima zifike chini (ardhini) ili kuchipusha mimea, vivyo hivyo Neno la Mungu lazima vifanye Baraka zako/Uponyaji/Kazi/Biashara/Elimu vichipuke, kuota, kuzaa na kustawi sana.

Mapenzi ya Mungu ni mema kwetu siku zote


Kama ukiitafakari pointi hii vizuri utafahamu kwamba kwa mtu aliyempokea Yesu Kristo amewekewa na Jehova mpango mzuri katika hatma yake.
Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

UWEZA ULIO KATIKA NENO LA MUNGU


Neno la Mungu lina uwezo wa kukuongoza katika njia sahihi.


Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu”.
Neno linatuonyesha tunapoelekea, linatuongoza kutenda kwa usahihi kama vile nchi bila katiba inapotea, ndivyo mtu anayemwamini Yesu kutokuwa na Neno la Mungu moyoni mwake! lazima atapotea! Kama umeokoka na unatembea na upako wa hali ya juu sana na ndani yako hauna Neno la Mungu ni sawa na gari jipya kabisa lisilokuwa na taa wakati wa usiku! Uwe na uhakika hautaweza kuliendesha pamoja na upya wake.
Joshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana”. Ni kwa kufuata/kuliishi Neno la Mungu ndipo mtu anaweza kuifanikisha njia yake, kazi yake, huduma yake, biashara yake n.k.

Neno la Mungu lina uwezo wa kutufanya hai.


Mathayo 4:4Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Neno limejaa uwezo wa kutufanya hai, kama vile mwili bila chakula unakufa ndivyo mtu aliye na Yesu bila Neno lake lazima atakufa kiroho. Neno la Mungu linatupatia nguvu ya kuishi bila Neno la Mungu maisha yetu ya kiroho yamo hatarini, Petro akamwambia Yesu “………..basi twende kwa nani wewe unayo maneno ya uzima……….. (Yohana 6:68) maneno ni uzima! Yaani Neno la Mungu ni uzima/Uhai kama alivyosema Yesu kuwa maneno yanayotoka kwake ni uzima yaani uhai (Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”)
Vilevile Yesu mwenyewe anasema kwamba alikuja ili tuwe na uzima katika utele wake Yohana 10:10 “………… mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Kumbuka maneno haya anayasema Yesu ambaye ndiye Neno la Mungu, kama Neno likikaa ndani yako unapokea uzima tele.


Neno la Mungu ni silaha na uwezo wa ushindi dhidi ya shetani.


Wakati Fulani utawasikia watu waliookoka wakisema vaeni silaha za Mungu sawasawa na Neno la Mungu Kutoka Waefeso 6:13-17 “13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;”
Ni kweli Neno la Mungu ni silaha lakini sio kwa namna hiyo! Silaha ambayo ni Neno la Mungu ni lile Neno lililopo ndani yako na limekaa na kuumbika na kuwa silaha. Yaani ninachokuambia hapa ni kwamba mstari unaousoma sio kitu mpaka umeumbika kuwa silaha ndani yako, vinginevyo utaendelea kuusoma sana na hautaweza kushindana katika ulimwengu wa roho.
Mkristo asiye na Neno la Mungu ni sawa na mwanajeshi asiye na silaha alafu yuko vitani, Neno la Mungu ni silaha kuu dhidi ya shetani
Yeremia 23:29 “Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?” Neno la Mungu ni ushindi mkamilifu dhidi ya shetani! Tukijua kulitumia ni ushindi mkamilifu!
Neno la Mungu linapokaa ndani yako ndipo unaweza kujua nguvu iliyopo katika damu ya Yesu na ushindi unaoweza kuupata kwa kuitegemea damu ya Yesu Kristo sawa na Neno la Mungu kutoka Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”


Neno la Mungu linatupa uwezo wa kupokea kutoka kwa BWANA.


Najua kwamba wengi wetu tumejifunza kwamba imani ndio mkono wa kupokelea kutoka kwa Mungu, hiyo ni sawa kabisa; lakini leo nakumbia kwamba ili uweze kupokea kutoka kwa Bwana unahitaji kwanza Neno la Mungu ili imani iumbike ndani yako. Kama hauna Neno la Kristo ndani yako uwe nauhakika kwamba hauwezi kupokea kutoka kwa Mungu. Hivyo basi; ukubwa wa mikono yako ya kupokelea (imani) inategemea na kiasi gani umeliweka Neno la Mungu ndani yako kama tunavyosoma katika Yohana 15:17 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa”.
Neno likijaa ndani yetu tutajua jinsi ya kumwomba Mungu sawa sawa, ni muhimu kuishi kwa kusoma neno la Mungu ili tuombe sawa na mapenzi yake kwani watu wengi wameshindwa kupokea na hatimaye kupotea kwakutofahamu Neno la Mungu Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Marko 12:24 “Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?” Tunakosa majibu ya maombi kwa kutojua maandiko (Neno)


Neno la Mungu linaweza kuumbika na kuwa Baraka zako


Yohana 1:1,14 “1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Ukisoma mistari hiyo hapo juu utagundua kuwa Neno linaweza kutoka katika hali ya rohoni hata kuwa katika hali ya mwili, Neno alikuwa kwa Mungu (Mbinguni) yaani rohoni halafu akaja duniani akafanyika mwili (Yesu Kristo) kama mwana pekee wa Mungu. Nataka ujifunze nini hapa? Kumbe Neno la Mungu ambalo ni Roho na lipo rohoni linaweza kuumbika na kuwa kile unachoomba kutoka kwa Mungu kila siku, linaweza kuwa Afya, Ndoa, Fedha, Biashara, Shahada ya chuo kikuu, Uongozi, n.k. unachotakiwa kufanya kuamini kwamba Neno la Mungu linaweza kugeuka kuwa Baraka zako!


Neno la Mungu lina uwezo wa kuumba.


Mungu alivyoiumba dunia ilikuwa ni kwa nguvu ya Neno, yaani hapakuwepo na material ya ujenzi mahali fulani yakatumiwa wakati dunia inaumbwa, hapana! Dunia a ilimbwa kwa Neno, yaani kila unachokiona hapa duniani sasa ni nguvu ya Neno la Mungu kama ilivyoandikwa “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.” (Waebrania 11:3) vilevile tunasoma katika Zaburi 33:9 “Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.”
Kwakuwa Mungu ametufanya sisi (wanadamu) kuwa miungu yaani punde tu baada yake Jehova, nasi tunauwezo wa kuumba kwa kutumia Neno la Mungu Zaburi 82:6 “Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”
Sasa kwa imani mtu wa Mungu anza kuumba(tabiri) mambo mema yatokee katika maisha yako kwakuwa Neno la Mungu lipo ndani yako.


Neno la Mungu ni Uponyaji wa magonjwa na matatizo yote


Unapoliamini Neno la Mungu linafanyika kuwa kitu chochote, Neno la Mungu linauwezo wa kuleta uponyaji mahali ambapo kuna magonjwa na mauti. Ukisoma Zaburi 107:19-20 “19 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. 20 Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.”
Mtu wa Mungu kama Neno la Mungu linawezwa kuumbika na kuwa mwili kama tulivyoona hapo awali, kwanini leo lishindwe kuwa ni uponyaji kwako? Mungu ameshalituma Neno lake kwako kukuponya kama anavyosema katika Isaya 53:5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Hili ndilo Neno la Mungu kwaajili ya uponyaji wa magonjwa/taabu/umasikini/shida/kuonewa n.k ukiliamini linaumbika na kuondoa shida yako.


Malaika hulisikia na kulitenda Neno la Mungu


Kwanza napenda ufahamu kwamba malaika ni roho watumikao kwa amri yetu, yaani malaika wanawatumikia wale waliompokea Yesu na kufanywa watoto wa Mungu kama ilivyoandikwa katika Waebrania 1:13-14 “13 Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? 14 Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?. Ninachotaka ufahamu hapa ni kwamba malaika wanaweza kutumwa na mtu aliyeokoka na kufanya kazi waliyotumwa kadiri walivyoamriwa au walivyoelekezwa, lakini fahamu kwamba huwezi kuwatuma malaika kwa maneno yako mwenyewe kwani wao (malaika) wanamewekewa uwezo wa kulisikia na kulitii Neno la Mungu ambalo linakaa ndani ya kila mtu aliyeokoka sawasawa na maandiko matakatifu kutoka Zaburi 103:20 “Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.” Hivyo unaweza kuwaagiza malaika kwa Neno la Mungu nao wakatenda sawasawa na maagizo yako.


Neno la Mungu humpa mtu uwezo wa kumsikia Mungu/Huleta Kumsikia Mungu


Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”
Kumbe imani inakuja kwa kusikia lakini sio kusikia kila kitu na pia sio kwa masikio haya ya damu na nyama pekee, kusikia kunakongelewa hapa ni Neno la Mungu ambalo ni Mungu mwenyewe likikaa ndani yako linakuwa ndio masikio yako ya kile ambacho Mungu anasema kwako na hivyo utasikia kila wakati Mungu anaposema na wewe.


Neno la Mungu linakuwezesha kuitambua sauti isiyo ya Mungu


Mungu wetu Jehova ni roho, ibilisi ni roho pia. Neno la Mungu linapokuwa ndani yako unapata uwezo wa kumfahamu Mungu na njia anazotumia kusema na watu, unapopata ufahamu wa kumsikia Mungu unaweza kufahamu sauti ya ibilisi kwani Neno la Mungu lililopo ndani yako linatambua kila aina ya mawazo na hakuna kiumbe kinachoweza kukaa ndani yako na kusema ndani yako bila ya wewe kufahamu ni sauti ya nani.
Waebrania 4:12-13 “12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”


Nakuombea kwa Mungu, Baba wa Bwana wangu Yesu Kristo kwamba akupe nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu katika ufahamu wa Neno la Kristo ndani yako, Nakuombea Roho ya Ufahamu na Ufunuo katika Neno la Kristo ili Kristo afunuliwe katika maisha yako (yaani umuone Yesu Kristo kupitia Neno la Mungu), Maombi haya yote ni katika jina la Yesu Kristo.