Tuesday, November 13, 2018

VITA YA KESHO YAKO - Samson Mollel 0767 - 664 338/0713 - 664 338



Bwana Yesu Kristo apewe sifa!!!


Ninamshukuru Mungu Jehova kwa neema zake na kwa ufunuo mwingine tena nilioupata katika Neno lake kuhusu “Vita ya Kesho Yako”

Kesho katika somo hili maana yake ni maono yako (Vision), ndoto yako (Dreams) au hatima yako (Destiny). Kesho yako ni kifurushi cha kiroho (package) kinachokuelezea jinsi utakavyokuwa hapo baadae au baada ya muda fulani (siku/mwezi/mwaka/miaka).

Kumbuka kwamba mtu ni roho anaekaa ndani ya nyumba inayoitwa mwili. Kabla mtu hajafanyika mwili au kabla mtu hajaumbiwa mwili ili aweze kuishi duniani (Kabla mtu hata hajawa mimba) Mungu anakuwa ameshampa kifurushi chake (Package) ambayo ndiyo hatima yake/kesho yake sawa na Neno la Mungu katika mistari ifutayo:-

Yeremia 1:5,10 “5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. 10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”

Yohana 1:6-8 “6 Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7 Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. 8 Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.”

Mungu anasema kabla hajamuumba Yeremia alimjua na alimfanya kuwa nabii wa mataifa na ukiendelea mbele zaidi katika mstari wa 10 Mungu anamwambia kwamba “angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Kumbe kutokea rohoni tayari Yeremia amekuja/ametumwa duniani kwa kazi maalum kama ulivyokuja duniani wewe msomaji wangu kwa kazi maalum.

Vilevile tunasoma habari za Yohana mbatizaji kwamba “Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.” Kumbe watu wanatumwa kutoka kwa Mungu kwa kazi maalum, hivi wewe umetumwa kutoka kwa Mungu uje duniani kufanya nini? Je! Unafanya kazi uliyokusudiwa kuifanya?

Kesho yako kwakuwa ni kifurushi cha kiroho inaweza kuonekana katika ulimwengu wa roho, hao wanaoiona kesho yako katika ulimwengu wa roho wanaweza kuwa watumishi wa Mungu Jehova (Manabii, Wachungaji, Mitume n.k.) au watumishi wa ibilisi (waganga wa kienyeji, wachawi, wanajimu, n.k.).

Kama kesho yako ikionekana na watumishi waaminifu wa Mungu Jehova basi upo salama na kesho yako ipo salama, lakini kama kesho yako ikionekana na watumishi waaminifu wa ibilisi/shetani basi kesho yako itasukwasukwa sana na huenda ikamalizwa kabisa usiione kama ilivyokusudiwa na Jehova.



KESHO YAKO INAVYOWEZA KUONEKANA


v  Mafanikio yako (Mfano wa Daudi)
Namna Baraka zinavyokufuata kwa kila jambo dogo unalolifanya, au jinsi unavyofanikiwa kwa mambo madogo unayoyafanya au hata mambo makubwa inaweza kuleta tafsiri ya kesho yako kwamba itakuwa njema sana au itakuwa nzuri sana. Kama kesho yako ikionekana kwa namna hiyo wako watu wataanza kukuandama au kukupiga vita kwa kuwa wameona kesho yako ni njema kama ilivyokuwa kwa Daudi baada ya kumuua Goliathi mfalme Sauli alianza kutafuta kumuua.


v  Ulimwengu wa ndoto/katika njozi (Mfano wa Yusufu)
Yale mambo unayoyaona katika ulimwengu wa ndoto (ulimwengu wa roho), mambo ya kufanikiwa katika maisha au kumliki au kuwa kiongozi yanaweza kukueleza kesho yako itakuwaje na wakati mwingine ndoto zinaweza kukueleza muda/majira/nyakati za kuinuliwa kwako. Jambo la namna hii lilimtokea Yusufu mwana wa Yakobo (Israeli), na baada ya yeye kuelezea ndoto zake chuki/husuda iliamka kati yake na ndugu zake na kusababisha vita kati yao.


v  Watumishi wa Jehova na watumishi wa ibilisi  (Mfano wa Yesu)
Kuna watu ambao wanaishi kama wanadamu wengine lakini wamepewa karama/zawadi na Mungu za kuona katika ulimwengu wa roho na wengine wamepewa zawadi hizo na wanatumiwa na shetani kuona katika ulimwengu wa roho. Watu hawa wanaweza kuona kesho yako hata kama wewe haujaiona kesho yako wao wakaona na wanaweza kukuambia au wasikuambie. Kama kesho yako imeonekana na mtumishi wa ibilisi basi ndio inakuwa tayari imeibiwa.
Katika Neno la Mungu (Biblia) kuna mifano ya watu wengi ambao kesho zao zilionekana na baada ya kuonekana matatizo ndipo yalipoanza katika maisha yao. Yaani kuna watu vifungo vimekazwa sana katika maisha yao lakini sababu ya kukazwa kwa vifungo hivyo kesho yao imeonekana na watu wabaya na wanataka asiifikie kesho yake. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya baadhi ya watu kutoka kwenye Biblia ambao kesho yao ilipoonekana madhara/mabaya yaliwaandama.



1.      VITA KATI YA NDUGU ZA YUSUFU NA KESHO YA YUSUFU


Mungu alimfungua Yusufu macho ya rohoni katika ndoto na kumfunulia kesho yake lakini kwa mafumbo ambayo yeye Yusufu mwenyewe hakuelewa kwa mara moja maana ya kile alichokiona. Ni kwasababu hiyo Yusufu aliwasimulia ndugu zake pamoja na baba yake ndoto alizoota, nia ya Yusufu pengine ilikuwa ni kutafuta tafsiri ya ndoto zile au pengine ilikuwa ni kutafuta maana ya ndoto alizoota.


Mwanzo 37:5-10 “5 Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 6 akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. 7 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. 8 Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. 9 Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. 10 Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?”


Katika ndoto mbili za Yusufu alikuwa akipokea taarifa kutoka rohoni kwa habari ya kesho yake, lakini Yusufu hakujua jambo sahihi la kufanya na akaanza kuwatangazia ndugu zake. Jambo la kushangaza ndugu za yusufu walielewa mara moja maana ya ndoto za Yusufu na hata baba yake Yusufu (Mzee Yakobo) alielewa mara moja maana ya ndoto ya Yusufu lakini Yusufu mwenyewe hakujua maana ya ndoto zile na kwamba zinaelezea kesho yake.


Baada ya kuwasimulia ndugu zake, vita ikainuka kati ya Yusufu na ndugu zake nao wakazidi kumchukia kwasababu tu ya zile ndoto alizoota kama tunavyosoma katika


Mwanzo 37:5,11 “5 Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 11 Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”


Tunajifunza kwamba ndugu za Yusufu walipoona kesho ya mdogo wao hasira, chuki na husuda viliamka ndani yao. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kesho ya Yusufu iliamsha vita kati ya Yusufu na ndugu zake japo yeye alikuwa mdogo sana kiumri (Miaka 17) lakini aliingia kwenye vita kubwa ya maisha yake kama tunavyosoma katika


Mwanzo 37:18-20 “18 Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. 19 Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. 20 Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”


Ukisoma kwa umakini utaona vita sio kati ya Yusufu na ndugu zake, vita ni kati ya kesho ya Yusufu na ndugu za Yusufu, ndio maana unawasikia wakisema ………… Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja………… kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake…………
Mtu wa Mungu muombe sana Mungu akupe watu sahihi watakao kusaidia katika kuifikia kesho yako kwani sio kila mtu anapenda kuona kesho yako ikitimia, jihadhari na uchunge nini unakisema mbele za watu kwa habari ya kesho yako.



MAOMBI:
Baba katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba kwa kusema habari za kesho yangu kwa watu wasiofaa na hao watu wameikwamisha kesho yangu hata sasa, ninaachilia damu ya Yesu Kristo katika kesho yangu iliyozuiliwa na kuikomboa katika jina la Yesu, Amen.


2.      KESHO YA HABILI ILIVYO NYAMAZISHWA


Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo kwamba kulikuwa na ndugu wawili watoto wa Adamu nao walimtolea BWANA sadaka zao, lakini katika kutoa sadaka hizi sadaka ya Habili ilipokelewa (iliheshimiwa) na Mungu na sadaka ya Kaini ilikataliwa.


Mwanzo 4:3-5 “3 Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. 4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”


Biblia inatuambia kwamba BWANA akamheshimu Habili pamoja na sadaka yake kama ilivyoandikwa …… Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake …….. (And Jehovah had respect unto Abel and to his offering).


Jambo ambalo sifahamu ni kwamba Kaini alijuaje kwamba sadaka ya Habili imekubaliwa, lakini ninachotaka wewe ufahamu ni hili; jifunze kutulia Mungu anapokuheshimu (anapokubariki) kwa sadaka zako, hebu jitulize kwa Mungu na uzidi kumtumikia yeye kwa uaminifu. Inawezekana kabisa kwasababu Kaini na Habili walikuwa ni ndugu basi waliongozana kutoa sadaka zao, vilevile inawezekana kabisa Habili alimwambia Kaini yale BWANA aliyomtendea kutokana na sadaka aliyomtolea. Jambo hili lilipelekea mauti ya Habili.


Mauti ya Habili haikutokana na ugomvi kati ya ndugu hao wawili bali ilitokana na wivu wa kesho ya Habili kutokana na Baraka alizozipata kutoka kwenye sadaka aliyomtolea Bwana, Mungu kuitakabali sadaka ya Habili au kuiheshimu sadaka ya Habili pamoja na Habili mwenyewe ni sawa na kusema kesho ya Habili ilikuwa ni njema kwakuwa BWANA amemuheshimu kama tulivyosoma …... Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake …….. (And Jehovah had respect unto Abel and to his offering)



3.      VITA KATI YA MADHABAHU YA BAALI NA KESHO YA GIDEONI.


Tunasoma habari za Gideoni kwenye Biblia kwamba ni mtu aliyekuwa masikini sana na mwenye umri mdogo kutoka katika familia ya watu masikini.


Waamuzi 6:12-16 “12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. 16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.”


Inawezeakana mtu wa Mungu ugumu wa maisha yaani umasikini unaokukabili leo ni kwasababu ya kesho yako ilivyokubwa na shetani ameizuia kuhakikisha kwamba hauchomoki.


Kesho ya Gideoni ilionekana na mungu baali akaikamata na kumfanya baba yake Gideoni aliyeitwa Yoashi kuwa ni kuhani wa madhabahu ya baali. Inawezekana hata wewe mtumishi wa Mungu unaishi katika umasikini uliopitiliza pamoja na jamaa yako kama Gideoni, kumbe kesho yako imeonekana kuwa ni njema na miungu imeshikilia na kuifunga kesho yako ili usichomoze. Leo kwa jina la Yesu vunja madhabahu zote zilizojengwa na kuizuia kesho yako kama alivyovunja Gideoni.


Waamuzi 6:27-29 “27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. 29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili.”



4.      VITA KATI YA HERODE NA KESHO YA YESU

Mathayo 2:1-3 “1 Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.”


Hapo awali nilisema kwamba kesho yako inaweza kuonekana kutokea rohoni na wasoma nyota/wanajimu. Hapa nyota ya Yesu imeonekana na mamajusi(wanajimu) waliokuwa na uwezo wa kuangalia kutokea rohoni, kutokea rohoni wameona jambo nao wanasema ……….. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia………. Hapa ndipo vita kati ya mfalme Herode na mtoto mchanga (Yesu) ilipoanza.


Hivi umewahi kujiuliza kwamba ilikuwaje mfalme Herode afanye vita na mtoto mchanga? Kwa uhakika mfalme Herode hakuwa anafanya vita na mtoto Yesu ila alikuwa akifanya vita na kesho ya Yesu kwani hakuelewa huo ufalme wa Yesu ni wa namna gani. Tunaona baada ya taarifa hizo Herode anaamua kuwaua watoto wote kama tunavyosoma katika Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”


Inawezekana unashangaa kwanini wewe ni mtu mdogo sana ofisini kwako lakini wakubwa wako wa kazi wanakuchukia sana na wanataka ufukuzwe kazi, unajitahidi kuwa mnyenyekevu na mtii lakini bado wanakuchukia sana! Hao wameona kesho yako na wanataka kuimaliza kabisa


Inawezekana unashangaa biashara yako ni ndogo sana na mtaji wake ni mdogo sana lakini kuna watu wenye biashara kubwa sana na mitaji mikubwa wanakupiga vita, unajitahidi kuwaheshimu hao watu lakini wanakutesa na kukuonea na kukuchukia sana! Hao wameona kesho yako wanataka kuimaliza kabisa



MAOMBI:
Katika jina la Yesu Kristo ninawakabili wale wote walioiona kesho yangu rohoni na wamepata hofu kwa habari za kesho yangu na wanataka kuiharibu, ninawaharibu kwa damu ya Yesu Kristo sasa. Ninawaamuru waganga, wachawi, wanajimu, wasoma nyota kuachia kesho yangu sasa kwa jina la Yesu Kisto, Amen.




5.      VITA KATI YA MAPEPO NA KESHO YA MUHUBIRI WA DEKAPOLI

Tunasoma habari za mtu aliyefungwa na kuteswa na mapepo kwa muda mrefu katika nchi ya Wagerasi, sababu ya mateso ya mtu huyu ni kesho yake ilikuwa kubwa na ingeuharibu ufalme wa shetani.


Marko 5:1-20 “1 Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; 4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. 6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. 8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu……………18 Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; 19 lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. 20 Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.”


Kwanini nimesema kwamba mateso ya mtu huyu yalisababishwa na kesho yake? Baada ya kufunguliwa mtu huyu aliyekuwa na mapepo kati ya 3,000 hadi 6,000 (Neno legion katika jeshi la kirumi lilimaanisha askari kati ya 3,000 hadi 6,000). Mtu huyu alienda kuwa Muhubiri wa injili katika miji kumi (Dekapoli maana yake ni miji kumi).


Shetani aliona kesho ya muhubiri huyu ambaye alikuwa na upako wa kuhubiri katika miji kumi lakini kwakuwa shetani alijua atavuruga kazi yake akamtupia maelfu ya mapepo kumkwamisha asiifikie kesho yake.



MAOMBI:
Baba yangu katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba na msamaha mahali popote nilipofungua mlango wa uovu na shetani akapata nafasi ya kuizuia kesho yangu, katika jina la Yesu Kristo ninaimiminia damu ya Yesu Kristo kila mahali penye mlango wa mateso katika maisha yangu na kuondoa kabisa uhalali wa mapepo kunitesa na kunifunga kwa jina la Yesu. Ninawaamuru mapepo yote mlioizuia kesho yangu Achia!!! Kwa jina la Yesu!!! Achia!!! Kwa jina la Yesu!!! Achia!!! Kwa jina la Yesu!!!



6.      VITA KATI YA SAULI NA KESHO YA DAUDI


Baada ya mfalme Sauli kumuasi Mungu, Mungu alimuinua mfalme mwingine lakini mfalme Sauli hakufahamu moja kwa moja kwamba kuna mfalme mwingine Mungu amempaka mafuta


1Samweli 16:1,13 “1 Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. 13 Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. ”


Kabla ya Daudi kupakwa mafuta na nabii Samweli hapakuwa na shida yoyote kati ya mfalme Sauli na Daudi. Daudi alikuwa mchungaji wa kondoo tu, alipopakwa yale mafuta akapata nafasi ya kutumika mbele ya mfalme kama mpiga kinubi ili kutuliza mapepo yaliyomvaa mfalme Sauli. Lakini baada ya kumwua Goliathi Yule mfilisti vita ya kesho ya Daudi ikaanza kwani Sauli alifahamu kwamba huyu ndiye mfalme ajaye


1Samweli 17:50-51 “50 Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. 51 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.”


1Samweli 18:6-11 “6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. 7 Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. 8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? 9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.  10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. 11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.”


Vita iliyoinuka kati ya mfalme Sauli na Daudi vilikuwa ni vita vya kesho ya Daudi ambayo mfalme alitambua kwamba Daudi atakuwa mfalme wa Israeli.


Inawezeakana kwamba kuna watu wameinuka wanataka kukumaliza wewe kwasababu ya kesho yako, nakutia moyo kwamba BWANA yupo pamoja nawe kama alivyokuwa na Daudi (1Samweli 18:12 “Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.”, Mithali 3:26 “Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.”).





MAOMBI YA KESHO YAKO


Huu ni mwongozo mfupi wa maombi kwaajili ya kesho yako, jitahidi upate muda wa ziada kuombea kesho yako kila siku na kila unapopata fursa kama hii.


Inawezekana haukujua kwamba Mungu ameshakubariki kwa Baraka zote katika ulimwengu wa roho na kesho yako ipo tayari inakusubiria uchukue hatua stahiki katika ulimwengu wa roho ili kesho yako iliyo ya mafanikio idhihirike katika ulimwengu wa mwili (Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;”)


Kwakuwa kesho yako tayari ipo katika ulimwengu wa roho, na hao wanaoipinga ni kwasababu wameiona ni kesho yako ni njema sana na hao wameiona katika ulimwengu wa roho, inatubidi kuingia rohoni na kuwashughulikia hao wanaozuia kesho yako isitimie kama Mungu alivyokupangia ; Imeandikwa:-  3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. (2Kor 10:3-4, Waefeso 6:12-13).



Pointi za Kuomba


v  Omba Toba (Rehema na Neema) kwa kutofikia kesho yako kama ulivyopangiwa na Mungu katika maisha yako.


v  Achilia damu ya Yesu Kristo kwenye milango ya dhambi na uovu iliyopelekea kutofikia kesho yako mpaka sasa


v  Vunja mikataba uliyoingia kwa kujua au bila kujua na mikataba hiyo ikakuzuia kuifikia kesho yako kama ilivyopangwa na Mungu


v  Amuru wachawi, mapepo, mizimu, majini na kila roho chafu inayoshikilia kesho yako kuachilia kwa jina la Yesu (Omba sana mahali hapa:- vunja na bomoa kila silaha, kila ngome na kila gereza ulilowekwa). Rudisha kesho yako iliyoibiwa kwa jina la Yesu


v  Waite malaika wa BWANA wailinde kesho yako kwa jina la Yesu Kristo na kwa damu ya Yesu.