Bwana Yesu Kristo apewe
sifa!!!
Ninamshukuru Mungu Jehova
kwa neema zake na kwa ufunuo mwingine tena nilioupata katika Neno lake kuhusu
“Vita ya Kesho Yako”
Kesho katika somo hili maana
yake ni maono yako (Vision), ndoto yako (Dreams) au hatima yako (Destiny).
Kesho yako ni kifurushi cha kiroho (package) kinachokuelezea jinsi utakavyokuwa
hapo baadae au baada ya muda fulani (siku/mwezi/mwaka/miaka).
Kumbuka kwamba mtu ni roho
anaekaa ndani ya nyumba inayoitwa mwili. Kabla mtu hajafanyika mwili au kabla
mtu hajaumbiwa mwili ili aweze kuishi duniani (Kabla mtu hata hajawa mimba)
Mungu anakuwa ameshampa kifurushi chake (Package) ambayo ndiyo hatima
yake/kesho yake sawa na Neno la Mungu katika mistari ifutayo:-
Yeremia
1:5,10 “5 Kabla
sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;
nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. 10
angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na
kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”
Yohana
1:6-8 “6 Palitokea mtu,
ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7
Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa
yeye. 8 Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.”
Mungu anasema kabla
hajamuumba Yeremia alimjua na alimfanya kuwa nabii wa mataifa na ukiendelea
mbele zaidi katika mstari wa 10 Mungu anamwambia kwamba “angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa,
na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Kumbe
kutokea rohoni tayari Yeremia amekuja/ametumwa duniani kwa kazi maalum kama
ulivyokuja duniani wewe msomaji wangu kwa kazi maalum.
Vilevile tunasoma habari za
Yohana mbatizaji kwamba “Palitokea mtu,
ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.” Kumbe watu wanatumwa kutoka
kwa Mungu kwa kazi maalum, hivi wewe
umetumwa kutoka kwa Mungu uje duniani kufanya nini? Je! Unafanya kazi uliyokusudiwa
kuifanya?
Kesho yako kwakuwa ni
kifurushi cha kiroho inaweza kuonekana katika ulimwengu wa roho, hao wanaoiona
kesho yako katika ulimwengu wa roho wanaweza kuwa watumishi wa Mungu Jehova
(Manabii, Wachungaji, Mitume n.k.) au watumishi wa ibilisi (waganga wa
kienyeji, wachawi, wanajimu, n.k.).
Kama kesho yako ikionekana
na watumishi waaminifu wa Mungu Jehova basi upo salama na kesho yako ipo
salama, lakini kama kesho yako ikionekana na watumishi waaminifu wa
ibilisi/shetani basi kesho yako itasukwasukwa sana na huenda ikamalizwa kabisa
usiione kama ilivyokusudiwa na Jehova.
KESHO
YAKO INAVYOWEZA KUONEKANA
v Mafanikio
yako (Mfano wa Daudi)
Namna Baraka zinavyokufuata
kwa kila jambo dogo unalolifanya, au jinsi unavyofanikiwa kwa mambo madogo
unayoyafanya au hata mambo makubwa inaweza kuleta tafsiri ya kesho yako kwamba
itakuwa njema sana au itakuwa nzuri sana. Kama kesho yako ikionekana kwa namna
hiyo wako watu wataanza kukuandama au kukupiga vita kwa kuwa wameona kesho yako
ni njema kama ilivyokuwa kwa Daudi baada ya kumuua Goliathi mfalme Sauli
alianza kutafuta kumuua.
v Ulimwengu
wa ndoto/katika njozi (Mfano wa Yusufu)
Yale mambo unayoyaona katika
ulimwengu wa ndoto (ulimwengu wa roho), mambo ya kufanikiwa katika maisha au
kumliki au kuwa kiongozi yanaweza kukueleza kesho yako itakuwaje na wakati
mwingine ndoto zinaweza kukueleza muda/majira/nyakati za kuinuliwa kwako. Jambo
la namna hii lilimtokea Yusufu mwana wa Yakobo (Israeli), na baada ya yeye
kuelezea ndoto zake chuki/husuda iliamka kati yake na ndugu zake na kusababisha
vita kati yao.
v Watumishi
wa Jehova na watumishi wa ibilisi (Mfano
wa Yesu)
Kuna watu ambao wanaishi
kama wanadamu wengine lakini wamepewa karama/zawadi na Mungu za kuona katika
ulimwengu wa roho na wengine wamepewa zawadi hizo na wanatumiwa na shetani
kuona katika ulimwengu wa roho. Watu hawa wanaweza kuona kesho yako hata kama
wewe haujaiona kesho yako wao wakaona na wanaweza kukuambia au wasikuambie.
Kama kesho yako imeonekana na mtumishi wa ibilisi basi ndio inakuwa tayari
imeibiwa.
Katika Neno la Mungu
(Biblia) kuna mifano ya watu wengi ambao kesho zao zilionekana na baada ya
kuonekana matatizo ndipo yalipoanza katika maisha yao. Yaani kuna watu vifungo
vimekazwa sana katika maisha yao lakini sababu ya kukazwa kwa vifungo hivyo
kesho yao imeonekana na watu wabaya na wanataka asiifikie kesho yake. Ifuatayo
ni baadhi ya mifano ya baadhi ya watu kutoka kwenye Biblia ambao kesho yao
ilipoonekana madhara/mabaya yaliwaandama.
1.
VITA
KATI YA NDUGU ZA YUSUFU NA KESHO YA YUSUFU
Mungu alimfungua Yusufu
macho ya rohoni katika ndoto na kumfunulia kesho yake lakini kwa mafumbo ambayo
yeye Yusufu mwenyewe hakuelewa kwa mara moja maana ya kile alichokiona. Ni
kwasababu hiyo Yusufu aliwasimulia ndugu zake pamoja na baba yake ndoto alizoota,
nia ya Yusufu pengine ilikuwa ni kutafuta tafsiri ya ndoto zile au pengine
ilikuwa ni kutafuta maana ya ndoto alizoota.
Mwanzo
37:5-10 “5 Yusufu akaota
ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 6 akawaambia,
Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. 7 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga
miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda
yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. 8 Ndugu zake wakamwambia, Je!
Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa
ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. 9 Akaota tena ndoto nyingine,
akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama,
jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. 10 Akawaambia baba yake na
ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je!
Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?”
Katika ndoto mbili za Yusufu
alikuwa akipokea taarifa kutoka rohoni kwa habari ya kesho yake, lakini Yusufu
hakujua jambo sahihi la kufanya na akaanza kuwatangazia ndugu zake. Jambo la
kushangaza ndugu za yusufu walielewa mara moja maana ya ndoto za Yusufu na hata
baba yake Yusufu (Mzee Yakobo) alielewa mara moja maana ya ndoto ya Yusufu
lakini Yusufu mwenyewe hakujua maana ya ndoto zile na kwamba zinaelezea kesho
yake.
Baada ya kuwasimulia ndugu
zake, vita ikainuka kati ya Yusufu na ndugu zake nao wakazidi kumchukia
kwasababu tu ya zile ndoto alizoota kama tunavyosoma katika
Mwanzo
37:5,11 “5 Yusufu akaota
ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 11 Ndugu zake
wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”
Tunajifunza kwamba ndugu za
Yusufu walipoona kesho ya mdogo wao hasira, chuki na husuda viliamka ndani yao.
Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kesho ya Yusufu iliamsha vita kati ya Yusufu
na ndugu zake japo yeye alikuwa mdogo sana kiumri (Miaka 17) lakini aliingia
kwenye vita kubwa ya maisha yake kama tunavyosoma katika
Mwanzo
37:18-20 “18 Wakamwona toka
mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. 19
Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. 20 Haya, twende,
tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla;
kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”
Ukisoma kwa umakini utaona
vita sio kati ya Yusufu na ndugu zake, vita ni kati ya kesho ya Yusufu na ndugu
za Yusufu, ndio maana unawasikia wakisema …………
Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja………… kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake…………
Mtu wa Mungu muombe sana
Mungu akupe watu sahihi watakao kusaidia katika kuifikia kesho yako kwani sio
kila mtu anapenda kuona kesho yako ikitimia, jihadhari na uchunge nini
unakisema mbele za watu kwa habari ya kesho yako.
MAOMBI:
Baba
katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba kwa kusema habari za kesho yangu kwa
watu wasiofaa na hao watu wameikwamisha kesho yangu hata sasa, ninaachilia damu
ya Yesu Kristo katika kesho yangu iliyozuiliwa na kuikomboa katika jina la
Yesu, Amen.
2.
KESHO
YA HABILI ILIVYO NYAMAZISHWA
Tunasoma katika kitabu cha
Mwanzo kwamba kulikuwa na ndugu wawili watoto wa Adamu nao walimtolea BWANA
sadaka zao, lakini katika kutoa sadaka hizi sadaka ya Habili ilipokelewa
(iliheshimiwa) na Mungu na sadaka ya Kaini ilikataliwa.
Mwanzo
4:3-5 “3 Ikawa hatimaye
Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. 4 Habili naye akaleta wazao wa
kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali
Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini
akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”
Biblia inatuambia kwamba
BWANA akamheshimu Habili pamoja na sadaka yake kama ilivyoandikwa …… Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake
…….. (And Jehovah had respect unto Abel
and to his offering).
Jambo ambalo sifahamu ni
kwamba Kaini alijuaje kwamba sadaka ya Habili imekubaliwa, lakini ninachotaka
wewe ufahamu ni hili; jifunze kutulia Mungu anapokuheshimu (anapokubariki) kwa
sadaka zako, hebu jitulize kwa Mungu na uzidi kumtumikia yeye kwa uaminifu.
Inawezekana kabisa kwasababu Kaini na Habili walikuwa ni ndugu basi
waliongozana kutoa sadaka zao, vilevile inawezekana kabisa Habili alimwambia
Kaini yale BWANA aliyomtendea kutokana na sadaka aliyomtolea. Jambo hili
lilipelekea mauti ya Habili.
Mauti ya Habili haikutokana
na ugomvi kati ya ndugu hao wawili bali ilitokana na wivu wa kesho ya Habili
kutokana na Baraka alizozipata kutoka kwenye sadaka aliyomtolea Bwana, Mungu kuitakabali
sadaka ya Habili au kuiheshimu sadaka ya Habili pamoja na Habili mwenyewe ni
sawa na kusema kesho ya Habili ilikuwa ni njema kwakuwa BWANA amemuheshimu kama
tulivyosoma …... Bwana akamtakabali
Habili na sadaka yake …….. (And
Jehovah had respect unto Abel and to his offering)
3.
VITA
KATI YA MADHABAHU YA BAALI NA KESHO YA GIDEONI.
Tunasoma habari za Gideoni
kwenye Biblia kwamba ni mtu aliyekuwa masikini sana na mwenye umri mdogo kutoka
katika familia ya watu masikini.
Waamuzi
6:12-16 “12 Malaika wa
Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni
akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote
yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu,
wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa,
naye ametutia katika mikono ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda
kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi
ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani?
Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye
mdogo katika nyumba ya baba yangu. 16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja
nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.”
Inawezeakana mtu wa Mungu
ugumu wa maisha yaani umasikini unaokukabili leo ni kwasababu ya kesho yako
ilivyokubwa na shetani ameizuia kuhakikisha kwamba hauchomoki.
Kesho ya Gideoni ilionekana
na mungu baali akaikamata na kumfanya baba yake Gideoni aliyeitwa Yoashi kuwa
ni kuhani wa madhabahu ya baali. Inawezekana hata wewe mtumishi wa Mungu
unaishi katika umasikini uliopitiliza pamoja na jamaa yako kama Gideoni, kumbe
kesho yako imeonekana kuwa ni njema na miungu imeshikilia na kuifunga kesho
yako ili usichomoze. Leo kwa jina la Yesu vunja madhabahu zote zilizojengwa na kuizuia
kesho yako kama alivyovunja Gideoni.
Waamuzi
6:27-29 “27 Ndipo Gideoni
akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana
alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake,
na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda
usiku. 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya
Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule
ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. 29
Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na
kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili.”
4.
VITA
KATI YA HERODE NA KESHO YA YESU
Mathayo
2:1-3 “1 Yesu
alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama,
mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Yuko wapi yeye
aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi
tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na
Yerusalemu pia pamoja naye.”
Hapo awali nilisema kwamba
kesho yako inaweza kuonekana kutokea rohoni na wasoma nyota/wanajimu. Hapa
nyota ya Yesu imeonekana na mamajusi(wanajimu) waliokuwa na uwezo wa kuangalia
kutokea rohoni, kutokea rohoni wameona jambo nao wanasema ……….. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa
Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia……….
Hapa ndipo vita kati ya mfalme Herode na mtoto mchanga (Yesu) ilipoanza.
Hivi umewahi kujiuliza
kwamba ilikuwaje mfalme Herode afanye vita na mtoto mchanga? Kwa uhakika mfalme
Herode hakuwa anafanya vita na mtoto Yesu ila alikuwa akifanya vita na kesho ya
Yesu kwani hakuelewa huo ufalme wa Yesu ni wa namna gani. Tunaona baada ya
taarifa hizo Herode anaamua kuwaua watoto wote kama tunavyosoma katika Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi,
alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko
Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua,
kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”
Inawezekana unashangaa
kwanini wewe ni mtu mdogo sana ofisini kwako lakini wakubwa wako wa kazi
wanakuchukia sana na wanataka ufukuzwe kazi, unajitahidi kuwa mnyenyekevu na
mtii lakini bado wanakuchukia sana! Hao wameona kesho yako na wanataka
kuimaliza kabisa
Inawezekana unashangaa
biashara yako ni ndogo sana na mtaji wake ni mdogo sana lakini kuna watu wenye
biashara kubwa sana na mitaji mikubwa wanakupiga vita, unajitahidi kuwaheshimu
hao watu lakini wanakutesa na kukuonea na kukuchukia sana! Hao wameona kesho
yako wanataka kuimaliza kabisa
MAOMBI:
Katika
jina la Yesu Kristo ninawakabili wale wote walioiona kesho yangu rohoni na
wamepata hofu kwa habari za kesho yangu na wanataka kuiharibu, ninawaharibu kwa
damu ya Yesu Kristo sasa. Ninawaamuru waganga, wachawi, wanajimu, wasoma nyota
kuachia kesho yangu sasa kwa jina la Yesu Kisto, Amen.
5.
VITA
KATI YA MAPEPO NA KESHO YA MUHUBIRI WA DEKAPOLI
Tunasoma habari za mtu
aliyefungwa na kuteswa na mapepo kwa muda mrefu katika nchi ya Wagerasi, sababu
ya mateso ya mtu huyu ni kesho yake ilikuwa kubwa na ingeuharibu ufalme wa
shetani.
Marko
5:1-20 “1 Wakafika
ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2 Na alipokwisha kushuka chomboni,
mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3 makao
yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena,
hata kwa minyororo; 4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na
minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna
mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako
makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. 6 Na alipomwona
Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7 akapiga kelele kwa sauti kuu,
akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu
usinitese. 8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu……………18 Naye
alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja
naye; 19 lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa
watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi
alivyokurehemu. 20 Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo
gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.”
Kwanini nimesema kwamba
mateso ya mtu huyu yalisababishwa na kesho yake? Baada ya kufunguliwa mtu huyu
aliyekuwa na mapepo kati ya 3,000 hadi 6,000 (Neno legion katika jeshi la
kirumi lilimaanisha askari kati ya 3,000 hadi 6,000). Mtu huyu alienda kuwa
Muhubiri wa injili katika miji kumi (Dekapoli maana yake ni miji kumi).
Shetani aliona kesho ya
muhubiri huyu ambaye alikuwa na upako wa kuhubiri katika miji kumi lakini
kwakuwa shetani alijua atavuruga kazi yake akamtupia maelfu ya mapepo
kumkwamisha asiifikie kesho yake.
MAOMBI:
Baba
yangu katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba na msamaha mahali popote
nilipofungua mlango wa uovu na shetani akapata nafasi ya kuizuia kesho yangu,
katika jina la Yesu Kristo ninaimiminia damu ya Yesu Kristo kila mahali penye
mlango wa mateso katika maisha yangu na kuondoa kabisa uhalali wa mapepo
kunitesa na kunifunga kwa jina la Yesu. Ninawaamuru mapepo yote mlioizuia kesho
yangu Achia!!! Kwa jina la Yesu!!! Achia!!! Kwa jina la Yesu!!! Achia!!! Kwa
jina la Yesu!!!
6.
VITA
KATI YA SAULI NA KESHO YA DAUDI
Baada ya mfalme Sauli
kumuasi Mungu, Mungu alimuinua mfalme mwingine lakini mfalme Sauli hakufahamu
moja kwa moja kwamba kuna mfalme mwingine Mungu amempaka mafuta
1Samweli
16:1,13 “1 Bwana
akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa
asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa
Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. 13 Ndipo Samweli
akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya
Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda
zake Rama. ”
Kabla ya Daudi kupakwa
mafuta na nabii Samweli hapakuwa na shida yoyote kati ya mfalme Sauli na Daudi.
Daudi alikuwa mchungaji wa kondoo tu, alipopakwa yale mafuta akapata nafasi ya
kutumika mbele ya mfalme kama mpiga kinubi ili kutuliza mapepo yaliyomvaa
mfalme Sauli. Lakini baada ya kumwua Goliathi Yule mfilisti vita ya kesho ya
Daudi ikaanza kwani Sauli alifahamu kwamba huyu ndiye mfalme ajaye
1Samweli
17:50-51 “50 Hivyo Daudi
akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua;
walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. 51 Ndipo Daudi akapiga mbio,
akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua,
akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao
amekufa, wakakimbia.”
1Samweli
18:6-11 “6 Hata ikawa,
walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti,
wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili
kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. 7 Nao wale
wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi
makumi elfu yake. 8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza;
akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na
mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?
9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.
10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli
kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi
kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. 11
Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani.
Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.”
Vita
iliyoinuka kati ya mfalme Sauli na Daudi vilikuwa ni vita vya kesho ya Daudi
ambayo mfalme alitambua kwamba Daudi atakuwa mfalme wa Israeli.
Inawezeakana
kwamba kuna watu wameinuka wanataka kukumaliza wewe kwasababu ya kesho yako,
nakutia moyo kwamba BWANA yupo pamoja nawe kama alivyokuwa na Daudi (1Samweli 18:12 “Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila
amemwacha Sauli.”, Mithali 3:26 “Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye
atakulinda mguu wako usinaswe.”).
MAOMBI YA KESHO YAKO
Huu
ni mwongozo mfupi wa maombi kwaajili ya kesho yako, jitahidi upate muda wa
ziada kuombea kesho yako kila siku na kila unapopata fursa kama hii.
Inawezekana
haukujua kwamba Mungu ameshakubariki kwa Baraka zote katika ulimwengu wa roho
na kesho yako ipo tayari inakusubiria uchukue hatua stahiki katika ulimwengu wa
roho ili kesho yako iliyo ya mafanikio idhihirike katika ulimwengu wa mwili (Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa
baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;”)
Kwakuwa
kesho yako tayari ipo katika ulimwengu wa roho, na hao wanaoipinga ni kwasababu
wameiona ni kesho yako ni njema sana na hao wameiona katika ulimwengu wa roho,
inatubidi kuingia rohoni na kuwashughulikia hao wanaozuia kesho yako isitimie
kama Mungu alivyokupangia ; Imeandikwa:- 3 Maana
ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana
silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha
ngome;) 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu
ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya
katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate
kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. (2Kor 10:3-4, Waefeso 6:12-13).
Pointi za Kuomba
v Omba Toba (Rehema na Neema) kwa kutofikia
kesho yako kama ulivyopangiwa na Mungu katika maisha yako.
v Achilia damu ya Yesu Kristo kwenye
milango ya dhambi na uovu iliyopelekea kutofikia kesho yako mpaka sasa
v Vunja mikataba uliyoingia kwa kujua au
bila kujua na mikataba hiyo ikakuzuia kuifikia kesho yako kama ilivyopangwa na
Mungu
v Amuru wachawi, mapepo, mizimu, majini na
kila roho chafu inayoshikilia kesho yako kuachilia kwa jina la Yesu (Omba sana mahali hapa:- vunja na bomoa
kila silaha, kila ngome na kila gereza ulilowekwa). Rudisha kesho yako iliyoibiwa
kwa jina la Yesu
v Waite malaika wa BWANA wailinde kesho
yako kwa jina la Yesu Kristo na kwa damu ya Yesu.
No comments:
Post a Comment