Tuesday, July 5, 2016

AJALI YA SINGIDA (Samson Mollel)

Bwana Yesu Asifiwe Watu wa Mungu!!!

Nimeona ni vyema nielezee kwa jinsi ya rohoni ajali ya Singida. Inawezekana na ndivyo watu wengi watakavyosema kuwa ni uzembe wa madereva ndio uliosababisha ajali, kwa jinsi ya kimwili ndivyo ilivyo na kama hauwezi kuitazama rohoni basi utaishia kuona uzembe wa madereva na roho za watu zitazidi kupotea kila siku kwa ajali za ajabu ajabu!!!

Lakini kwa jinsi ya rohoni kwa upande wa giza “kuzimu” ajali hizi hutengenezwa ili kupeleka kafara huko kuzimu, na ili ajali itokee lazima kupatikane sababu ya kimwili itakayoleta hiyo ajali yaani lazima kutengenezwe mtego kama Neno la Mungu linavyosema katika YEREMIA 5:26 “Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.”

Sasa kumbe kuna watu wanotega mitego ili kunasa watu. Sababu ya kunasa watu ni kuchukua roho za hao watu kabla ya wakati wa Mungu kuwachukua haujafika kama tunavyosoma katika kitabu cha EZEKIEL  13:18-19 “18 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? 19 Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo.”

Neno la Mungu linatufundisha wazi kuwa shetani anatafuta watu kwa kasi kubwa kwani anajua wakati wake ni mfupi sana hapa duniani. Sasa ni wakati wa kusimama na kuwapiga wachawi wote wanaosababisha ajali Tanzania kwa Jina la YESU KRISTO kwakuwa Mungu (JEHOVA) amesema yuko kinyume cha hao wanaochukua roho za watu (Ezekiel 13:20-21 “20 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. 21 Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.”)

***** Samson Mollel – www.uzimawamileleministries.blogspot.com *******