Tuesday, May 16, 2017

PASAKA WETU AMESHATOLEWA - Samson Mollel

PASAKA NI NINI?

Pasaka ni sikukuu ya kihistoria ya Israeli kukumbuka kutoka utumwani Misri, siku kuu hii hufanyika kwa siku saba hadi nane kuanzia tarehe 14 ya mwezi wa nisani ambao ni mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kiyahudi, Kutoka 12:5-6 “5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. 6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.”

Kimsingi pasaka ni jina la sadaka ambayo BWANA aliwaagiza wana wa Israeli kumchinja ili BWANA awapige wamisri  kwa kusudi la kuwaweka huru Israeli kutoka utumwani Misri. Ukisoma kitabu cha Kutoka 12:11 “Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; NI PASAKA YA BWANA.”

Baada ya Mungu kuwapiga wa-Misri kwa mapigo tisa lakini Farao hakutaka kuwaachia Israeli, Mungu akasema kuwa liko pigo moja limebakia ambalo ni pigo linalotokana na guvu ya sadaka ya PASAKA iliyotolewa kwa maelekezo ya Mungu mwenyewe, Kutoka 11:1-2 “1 Bwana akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa. 2 Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu.”

NGUVU YA SADAKA ZA DAMU

Tunaposoma maandiko matakatifu tunaona katika agano la kale kila mara damu ilitakiwa kumwagika ili mtu atakaswe au afunguliwe katika kifungo cha uovu na ndipo awe salama kabisa ili aweze kusogea kwa Bwana. Kama mtu alikuwa na ukoma ilimbidi atakaswe kwa damu ya mnyama na upatanisho na Mungu ilihitajika damu kutoka kwa wanyama safi wasio na madoa wala mawaa ili kuchinjwa kwaajili ya utakaso wa dhambi (Kut 12:5; Law 1:3, 10)

Waebrania 9: 18-22 18 Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu. 19 Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, 20 akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. 21 Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. 22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”

Kulingana na andiko hilo la Waebrania 9:22; kama mtu alitenda dhambi aina yoyote ilibidi damu ya mnyama imwagike kama fidia ya kosa lile alilotenda ndipo apate ondoleo la dhambi.

Mpendwa unayenifuatilia maana yake haswa ni hii; Ilibidi uhai wa mnyama utolewe kufidia uhai wa mtu (yaani aliyepaswa kufa ni mwanadamu kwa dhambi aliyoitenda lakini badala yake anakufa mnyama aliye safi asiye na waa lolote). Sababu ya kutaka uhai wa mnyama kuwa fidia ya kosa/dhambi ni kwakuwa unapotenda dhambi unastahili ujira wa kifo sawasawa na Neno la Mungu Warumi 6:23a Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; hivyo kifo cha mnyama kinakuwa ni mshahara wa kosa lile alilofanya mwanadamu. Damu ya mnyama Yule inapomwagika ndipo uhai wake unapotoka na kuwa fidia ya kwa mwanadamu aliyetenda dhambi ili aishi (Walawi 17:11,14 “11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi…….. 14 Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”)

Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo baada ya uasi wa Adam na mkewe walivaa majani ya miti lakini hayakuweza kuificha wa kuihifadhi dhambi yao mbele za Mungu Mwanzo 3:7 “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.” Lakini Mungu aliua mnyama kwa mnyama (maana yake damu ilimwagika Warumi 6:23, Waebrania 9:22) na kuwatengenezea Adama na Eva mavazi ya ngozi (Mwanzo 3: 21 “Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.”). Hii ni ishara kuwa damu ilihitajika ili kuweka upatanisho kati ya Adam na Mungu kwa kosa lile walilofanya.

Vilevile tuajifunza kuwa damu ya wanyama ilihitaji ili kwenda madhabahuni pa BWANA au katika kutoa sadaka kwa Jehova (Fahamu Kuwa Kuzimu Mpaka Sasa Wanatumia Damu Za Watu Na Wanyama Katika Kufanya Uharibifu Kwakuwa Wanayafahamu Maarifa Na Nguvu Iliyopo Katika Damu)

Katika agano la kale kama mtu alitaka kumtolea Mungu au alitaka kusema na Mungu ilimlazimu aende na sadaka ya damu kwa Mungu, tutazame mifano michache katika Biblia.

KAINI NA HABILI

Kaini hakutambua umuhimu wa damu kati yake yeye na Mungu kwaajili ya upatanisho ndio maana akapeleka mazao ya ardhi kama sadaka, lakini Mungu hakumkubali Kaini kwaajili ya aina ya sadaka aliyoitoa kwani haikuweza kufanya upatanisho kati yake na Mungu (Mwanzo 4:3, 5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. 5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”), lakini Habili ndugu yake alipeleka wanyama kama sadaka kwa BWAN na pakwa na upatanisho kati ya Habili na Mungu na hatimaye Mungu akamkubali kwaajili ya sadaka ya damu ya wanyama aliyoitoa (Mwanzo 4:4 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;”)

Kuna watu wengi hata sasa wanaishi maisha kama ya Kaini, yaani wanaishi pasipo kufahamu nguvu ya damu ya Yesu kwaajili ya kutupatanisha na Mungu katika kila jambo na kila mara tunapotaka kusogea mbele za Mungu.

IBRAHIMU

Mungu alipomjaribu Ibrahimu; alitaka sadaka ya Damu kutoka kwa mtoto wake wa pekee (Hapa ndipo kwenye kivuli cha Isaka akiwakilisha wanadamu wa leo na mwanakondoo akimuwakilisha Yesu Kristo). Ilibidi damu ya kondoo asiye na hatia kumwagika ili Isaka apone na mauti iliyokuwa mbele yake kama tunavyosoma katika Mwanzo 22:1-13 “1 Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia……… 9 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. 11 Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. 13 Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.”
Tunamwona Isaka anapona kutoka katika mauti kwa mauti ya mwanakondoo asiye na hatia na kwa Neno la Bwana alilomwambia Ibrahimu asimchinje Isaka tena.

SULEMANI

Sulemani anafahamika kama mfalme alipewa hekima kuliko wafalme wote waliokuwapo na hata sasa hajatokea mfalme wa mfano wa Sulemani, vilevile Sulemani alipewa utajiri kuliko wafalme wote wa wakati wake. Lakini unafahamu haya yoye aliyapataje? Tusome kwa pamoja Neno hili:-

1Wafalme 3:4-5 “4 Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. 5 Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.”

Kumbe Sulemani alitoa sadaka elfu, maana yake alichinja maelfu ya ngombe kwaajili ya BWANA. Hii inatofunulia zaidi kwa habari ya nguvu iliyopo katika damu, kwani kwa sadaka za damu Mungu alishuka na kumuuliza mfalme Sulemani aseme anachokitaka.

Unataka nini mtu wa Mungu, fahamu nguvu iliyopo katika damu ya sadaka na pia fahamu kuwa sadaka wetu ameshatolewa ambaye ni Yesu Kristo.

ELIYA

Tunaposoma habari za Eliya tunaona kuwa alitembea na nguvu za Mungu kwa miujiza mikubwa na matendo makuu ya Mungu tena ya kustaajabisha, lakini mahali fulani Eliya alikuwa akipambana na manabii wa baali ; katika mpambano huo kila mmoja alitaka kuonesha kuwa Mungu wake ni bora zaidi ya mwingine. Katika kukamilisha ubishi au pambano hilo wote kwa pamoja walikubaliana kuwa kuwepo na sadaka ya damu ili kuona ni Mungu yupi mwenye nguvu (hapa tunazidi kujifunza nguvu ya damu katika madhabahu za kuzimu na madhabahu ya Jehova).

1Wafalme 18:22-39 “….……….... 31 Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli……33 Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni…… 36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. 38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. 39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.”

Tunaona nguvu ya sadaka ya damu katika kushusha nguvu za Mungu, kumbe unaweza kutumia nguvu ya damu ya Mwana Kondoo kuita Moto nao moto ukala madhabahu zote katika maisha yako na kuuleta uftukufu wa Mungu katika maisha yako.

Mungu akaona zoezi hili ni gumu kwa wanadamu na watu wanazidi kuasi na dhambi zinazidi kuongezeka kwa maana damu za wanyama zimeshindwa kuondoa dhambi kabisa Waebrania 10:1-4 “1 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao. 2 Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? 3 Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. 4 Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.”, akaamua kutoa damu ya Mungu mwenyewe (Bwana Yesu Kristo) ili kwa damu hiyo tukombolewe moja kwa moja na hakutakuwa na damu ya mnyama itakayohitajika tena. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

AGANO LA KALE NI KIVULI TU!

Mtu wa Mungu jambo hili imekubidi kulifahamu sana! tena sana!! Ya kwamba Agano la kale sio kitu halisi bali ni kivuli au tuseme ni taswira ya agano jipya lakini uhalisia wenye upo katika agano la damu ya Yesu (yaani agano jipya). Kama vile binadamu au kiumbe au kitu chochote kinapowekwa mahali hutengeneza kivuli mbele yake au nyuma yake kutegemea na mahali mwanga unapotokea, ndivyo ilivyo kwa agano la kale na agano jipya. Mambo unayoyaona katika agano la kale uhalisia wake upo katika agano jipya.

Kwa mfano kumwaga damu za wanyama wasio na madoa wala mawaa ilikuwa ni kivuli cha kumwagwa kwa damu ya Yesu asiye na dhambi wala kosa lolote kama mwanakondoo wa Mungu kama alivyofunuliwa na Yohana mbatizaji (Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”)

Mfano mwingine kuandikwa kwa amri kumi katika mawe na mbao uhalisia wake ni kuandikwa kwa sheria ya Mungu katika mioyo yetu (Yeremia 31:31-33 “31 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. 32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. 33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”)

Neno la Mungu linatuthibitishia kuwa agano la kale ni kivuli tu cha agano jipya na kwamba agano jipya ni uhalisia ulidhihirika katika agano jipya kama tunavyosoma katika Wakolosai 2:16-17 “16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; 17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Vilevile tunasoma katika Waebrania 10:1, Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.)


AGANO LA KALE NI KIONGOZI KUTULETA KATIKA AGANO JIPYA!

Mtume Paulo anawafundisha wagalatia kuwa agano la kale (torati) imekuwa ni kiongozi wa kutupeleka katika agano jipya; Wagalatia 3:24-25 “24 Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. 25 Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.”.

Maandiko haya yanatuthibitishia kuwa mambo yaliyotokea katika agano la kale (torati) yalikuwa ni kwaajili ya kutuongoza kufika katika agano jipya (agano la damu ya Yesu Kristo)

PASAKA WETU AMESHATOLEWA

Ukisoma Waebrania 9: 18-22 18 Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu. 19 Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, 20 akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. 21 Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. 22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” Hii ndio sababu Israeli wote iliwapasa kumwaga damu ya mnyama (pasaka) ili Misri wakiwa wanapigwa wao wawe salama kama tunavyosoma Kutoka 12:5-6 “5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. 6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.”

Iliwalazimu Israeli ili kuwa salama na mauti siku ile wachinje mwanakondoo au mwanambuzi na ile damu ya myama huyo ipakwe kwenye miimo ya milango yao ili malaika napopita kupiga usiku asiwadhuru; lakini pia iliwabidi kufanya hivyo ili watoke katika hali ya utumwa na mateso ya zaidi ya miaka mia nne waliokuwa Misri.

Unaposoma kitabu cha Kutoka mlango wa 12 tunaona Mungu anaagiza Israeli kutoa PASAKA, Kutoka 12:11 “Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; NI PASAKA YA BWANA.”

Kama tulivyojifunza kuwa Agano la kale ni kiongozi wa kutuleta katika agano jipya (Wagalatia 3:24), maana ya sadaka hii katika agano jipya ni Yesu Kristo aliyetolewa sadaka na Mungu mwenyewe kwaajili yetu kama tunavyosoma katika 1Wakorintho 5:7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;”


Mtu wa Mungu hebu jiulize maswali haya:-

a.       Ikiwa damu za wanyama ziliweza kutakasa watu wa Mungu katika torati, Je si zaidi sana damu ya Mungu mwenyewe (Yesu Kristo) inaweza kutakasa na kuponya zaidi ya damu za wanyama!


b.      Ikiwa kwa damu ya wanyama Nguvu za Mungu zilishuka kama moto na kuteketeza sadaka ya nabii Eliya pamoja na kuni, maji, na mawe; Je sadaka aliyoitoa Mungu (Yesu Kristo) si zaidi sana inaweza kushusha moto wa kiroho na kuharibu falme za giza!


c.       Ikiwa kwa damu za ngombe elfu Mungu alishuka kuongea na Mfalme Sulemani na kumwambia aseme jambo lolote analohitaji, si zaidi sasa kwamba atashuka karibu zaidi na kutupa mema mengi zaidi kwa damu ya mwana wake wa pekee!


d.      Ikiwa kwa damu ya mwanakondoo/mwanambuzi Misri yote ilipigwa kwa kuuliwa mzaliwa wa kwanza wa binadamu na mnyama; Je? Si zaidi sana kwamba kwa damu ya Yesu Kristo tunawapiga na kuwamaliza kabisa wote wanaotutesa katika maisha ya sasa (shetani, majini, mapepo, mizimu na mawakala wa shetani wote)!


e.       Ikiwa kwa damu ya wanyama, Habili alipata kibali mbele za Mungu, Je si zaidi sana kwa damu ya Yesu tunaitwa watoto wa Mungu, yaani ametuzaa yeye mwenyewe!


f.        Ikiwa damu ya kondoo na mbuzi iliweza kuzuia mauti isiwapate Israeli, je si zaidi sana damu ya Yesu Kristo inaweza kutuzuia tusipatwe na mauti ya namna yoyote!


Samson Mollel – Uzima wa Milele International Ministries +255 767 664 338


Monday, May 15, 2017

BARUA YA TANO KWA WANAUME - Imeandikwa na Albert Nyaluke Sanga - #SmartMind

(Maalumu kwa waliooa na watakaooa)

Wanaume wenzangu,

Ninawasalimu! Naamini mlipokea na mnaendelea kuzifanyia kazi barua zangu nne zilizotangulia.

Ninawaandikia barua hizi nikijaribu kuwaokoa na hatari inayoendelea kwa kasi ya wanaume wengi kupoteza "uanaume" wao, kiasi kwamba sasa wanawake wanapata aibu. (Rejea barua yangu ya tatu, nilivyoeleza kwa kina namna ambavyo sasa huku mitaani tunaona wanawake wengi wakifika hatua ya kumng'ang'ania mwanaume mmoja sawa sawa na ISAYA 4:1).

Ninafahamu "ulimwengu huu", unafundisha mbinu nyingi za namna ya "kumdhibiti" mwanamke. Kwa jinsi wanawake wanavyoendelea kuwashinda mlio wengi, hiyo inaonesha namna mbinu hizi zisivyo na meno. Leo ninakuja kwako na mbinu tatu kutoka kwenye Neno la Mungu, zitakazouhifadhi uanaume wako na kukuwezesha uwe mume mwema na baba uliefanikiwa.

Ndugu zangu wanaume,

Biblia inatuonesha wazi ya kwamba mwanaume ulieoa, una wajibu za aina tatu katika ndoa na familia yako. 1) Kuhani 2) Nabii 3) Mfalme. Naomba nikufafanulie kwa ufupi

1). KUHANI:- Mwanaume unatakiwa kusimama kama kuhani wa familia yako, ukimpeleka mke wako na watoto wako kwa maombi mbele za Mungu, "costantly". Mwanaume ndie unatakiwa kuongoza mapambano dhidi ya kila hila za Ibilisi katika ndoa na watoto wako.

Jambo la kusikitisha ni kwamba wanaume wengi hamsali, hamna muda na Mungu na mmewaachia wake zenu jukumu la maombi. Tunao wanaume wenzetu akina Ayubu, Ibrahim, Suleman, hebu tazameni walivyokuwa mstari wa mbele kuziombea ndoa na familia zao.

2). NABII:- Mwanaume unasimama kama nabii kwa mke wako, kwa watoto na kwa ndoa yako, ukimwakilisha Mungu katika nyumba yako. Hapa una wajibu za namna nne, a) Kuhakikisha unamsikiliza Mungu anachosema kila wakati kuhusu ndoa na familia yako b) Kuwafundisha mke wako na watoto wako, Neno la Mungu c) Kutamka baraka na kuwatia moyo watu wote wa nyumbani mwako. d) Kuziishi tabia za Mungu katika ndoa na familia yako, na hapa inajumuisha upendo kwa mkeo, kuwajali watoto na kutimiza haja zao zote kimwili, kihisia na kiroho.

Wengi wenu hamna muda na Mungu, mtamsikia saa ngapi? Kama wewe mwenyewe hujipi muda kujifunza Neno la Mungu utawafundisha nini mkeo na watoto wako? Ukiona hauna hata muda ambao iwe formal ama informal mnaoshirikishana na mkeo Neno la Mungu, ujue una-risk ndoa yako! Kama una watoto na hawana hata mstari mmoja wa maandiko walioushika kwa kufundishwa na wewe baba, hebu nenda kaji-edit unavyolea watoto wako.

3). MFALME:- Mwanaume ndie unaetakiwa kuwa na sauti na mamlaka ya mwisho kwa kila jambo katika familia yako. Wewe mwanaume ni kichwa cha mke na watoto. Kichwa kimebeba akili, macho, ubongo, na kinywa. Kinywa kikiongea hakuna namna ambayo kiwiliwili kitaongea kwa sababu kiwiliwili hakina mdomo na hakitakiwi kuwa na mdomo.

Ni jambo la kusikitisha kwamba mpo wanaume wengi ambao mmeshapoteza nafasi za Ufalme katika ndoa zenu. Mume unaongea lako, mke nae anakujia juu na ya kwake! Mume unaongea, mke anakupuuza! Hebu niwaulize, mliona wapi mfalme ambae akitoa amri wananchi wanagoma kutii? Uliona wapi mfalme ambae watu wake wakigoma kutii maagizo yake ananywea? Kama kuna sentensi ya aibu ambayo mwanaume hutakiwi kuitamka mbele ya sisi wanaume wenzio ni hii, "Mke wangu hataki kunisikiliza". Mke anaanzaje kutokukusikiliza, kwa mfano?

Sasa nisikilizeni ninapohitimisha...

a)     Biblia inasema "Mfalme aliepungukiwa na akili huwaonea watu wake", Kisha inasema tena, "Enyi waume ishini na wake zenu kwa akili". Mume ukipungukiwa na akili "automatically" utaanza kumuonea mke na kuwatesa watoto. Kutomsikiliza mkeo ni uonevu. Kutomridhisha kimapenzi mkeo ni uonevu. Kutokuwa na muda wa kukaa na watoto wako ni uonevu. Kutomtunza mkeo ni uonevu. Kutowatia moyo na kuwaombea mkeo na watoto wako ni uonevu. Kumfanya mkeo awe anashinda kwenye maombi kwa ajili ya wewe kubadilika ni uonevu.

Uonevu wako ukizidi unaowaongoza (mkeo na wanao) wanaingia msituni (yaani wanakuasi) na kuanza kupambana na wewe. Ni hapa ambapo watoto wanaweza kutokuheshimu, mke anaondoa kujivunia wewe na wakati mwingine ataanza kutafuta watawala wengine, (michepuko na wanaoweza kumfariji na kujali hisia zake hata kama sio kingono). Ukiona mke ameanza kukudharau (hakusikilizi), ama ukiona mke ameanza kufanya mambo kivyake vyake ama kisirisiri, usikimbilie "kuwaka", bali tambua kwamba "Umepungukiea na akili"

b)     Mwanaume huna haki ya kutimiza mamlaka ya kifalme katika ndoa na familia ikiwa hauwajibiki Kikuhani na Kinabii. Kama huna muda wa kuiombea familia yako(kuhani), kama huifundishi kuipenda na kuijali (nabii), kisha uka-practice ufalme, huo unakuwa ni UBABE. Lazima mfahamu kwamba, Biblia inasema, "Kumcha Mungu ni chanzo cha hekima". Hekima ni AKILI. Huwezi kuwa na akili za kuishi na mke kama mume mwema na kulea watoto kama baba bora, ikiwa haumchi Mungu. Kumcha Mungu ni kujifunza Neno lake na kuwa karibu nae kwa maombi.

Ole kwenu wanaume ambao hamumchi Mungu, na mnategemea ndoa na familia zenu viende sawa. Trust me, hata kama mnadhani mambo yanaenda sawa kwa sasa, you will surely "krashi" somewhere at some point!

KWA HIYO:-
Unaweza kuipeleka ndoa yako pasipo misingi hii, ukadhani mambo yanaenda na kumbe unaowaongoza wanaugulia ndani kwa ndani sema hawawezi kukuambia. Kama mimi ningekuwa wewe, ningeyaingiza haya maarifa mara moja katika ndoa yangu.

Ni mimi ninaewajali sana,