Monday, May 15, 2017

BARUA YA TANO KWA WANAUME - Imeandikwa na Albert Nyaluke Sanga - #SmartMind

(Maalumu kwa waliooa na watakaooa)

Wanaume wenzangu,

Ninawasalimu! Naamini mlipokea na mnaendelea kuzifanyia kazi barua zangu nne zilizotangulia.

Ninawaandikia barua hizi nikijaribu kuwaokoa na hatari inayoendelea kwa kasi ya wanaume wengi kupoteza "uanaume" wao, kiasi kwamba sasa wanawake wanapata aibu. (Rejea barua yangu ya tatu, nilivyoeleza kwa kina namna ambavyo sasa huku mitaani tunaona wanawake wengi wakifika hatua ya kumng'ang'ania mwanaume mmoja sawa sawa na ISAYA 4:1).

Ninafahamu "ulimwengu huu", unafundisha mbinu nyingi za namna ya "kumdhibiti" mwanamke. Kwa jinsi wanawake wanavyoendelea kuwashinda mlio wengi, hiyo inaonesha namna mbinu hizi zisivyo na meno. Leo ninakuja kwako na mbinu tatu kutoka kwenye Neno la Mungu, zitakazouhifadhi uanaume wako na kukuwezesha uwe mume mwema na baba uliefanikiwa.

Ndugu zangu wanaume,

Biblia inatuonesha wazi ya kwamba mwanaume ulieoa, una wajibu za aina tatu katika ndoa na familia yako. 1) Kuhani 2) Nabii 3) Mfalme. Naomba nikufafanulie kwa ufupi

1). KUHANI:- Mwanaume unatakiwa kusimama kama kuhani wa familia yako, ukimpeleka mke wako na watoto wako kwa maombi mbele za Mungu, "costantly". Mwanaume ndie unatakiwa kuongoza mapambano dhidi ya kila hila za Ibilisi katika ndoa na watoto wako.

Jambo la kusikitisha ni kwamba wanaume wengi hamsali, hamna muda na Mungu na mmewaachia wake zenu jukumu la maombi. Tunao wanaume wenzetu akina Ayubu, Ibrahim, Suleman, hebu tazameni walivyokuwa mstari wa mbele kuziombea ndoa na familia zao.

2). NABII:- Mwanaume unasimama kama nabii kwa mke wako, kwa watoto na kwa ndoa yako, ukimwakilisha Mungu katika nyumba yako. Hapa una wajibu za namna nne, a) Kuhakikisha unamsikiliza Mungu anachosema kila wakati kuhusu ndoa na familia yako b) Kuwafundisha mke wako na watoto wako, Neno la Mungu c) Kutamka baraka na kuwatia moyo watu wote wa nyumbani mwako. d) Kuziishi tabia za Mungu katika ndoa na familia yako, na hapa inajumuisha upendo kwa mkeo, kuwajali watoto na kutimiza haja zao zote kimwili, kihisia na kiroho.

Wengi wenu hamna muda na Mungu, mtamsikia saa ngapi? Kama wewe mwenyewe hujipi muda kujifunza Neno la Mungu utawafundisha nini mkeo na watoto wako? Ukiona hauna hata muda ambao iwe formal ama informal mnaoshirikishana na mkeo Neno la Mungu, ujue una-risk ndoa yako! Kama una watoto na hawana hata mstari mmoja wa maandiko walioushika kwa kufundishwa na wewe baba, hebu nenda kaji-edit unavyolea watoto wako.

3). MFALME:- Mwanaume ndie unaetakiwa kuwa na sauti na mamlaka ya mwisho kwa kila jambo katika familia yako. Wewe mwanaume ni kichwa cha mke na watoto. Kichwa kimebeba akili, macho, ubongo, na kinywa. Kinywa kikiongea hakuna namna ambayo kiwiliwili kitaongea kwa sababu kiwiliwili hakina mdomo na hakitakiwi kuwa na mdomo.

Ni jambo la kusikitisha kwamba mpo wanaume wengi ambao mmeshapoteza nafasi za Ufalme katika ndoa zenu. Mume unaongea lako, mke nae anakujia juu na ya kwake! Mume unaongea, mke anakupuuza! Hebu niwaulize, mliona wapi mfalme ambae akitoa amri wananchi wanagoma kutii? Uliona wapi mfalme ambae watu wake wakigoma kutii maagizo yake ananywea? Kama kuna sentensi ya aibu ambayo mwanaume hutakiwi kuitamka mbele ya sisi wanaume wenzio ni hii, "Mke wangu hataki kunisikiliza". Mke anaanzaje kutokukusikiliza, kwa mfano?

Sasa nisikilizeni ninapohitimisha...

a)     Biblia inasema "Mfalme aliepungukiwa na akili huwaonea watu wake", Kisha inasema tena, "Enyi waume ishini na wake zenu kwa akili". Mume ukipungukiwa na akili "automatically" utaanza kumuonea mke na kuwatesa watoto. Kutomsikiliza mkeo ni uonevu. Kutomridhisha kimapenzi mkeo ni uonevu. Kutokuwa na muda wa kukaa na watoto wako ni uonevu. Kutomtunza mkeo ni uonevu. Kutowatia moyo na kuwaombea mkeo na watoto wako ni uonevu. Kumfanya mkeo awe anashinda kwenye maombi kwa ajili ya wewe kubadilika ni uonevu.

Uonevu wako ukizidi unaowaongoza (mkeo na wanao) wanaingia msituni (yaani wanakuasi) na kuanza kupambana na wewe. Ni hapa ambapo watoto wanaweza kutokuheshimu, mke anaondoa kujivunia wewe na wakati mwingine ataanza kutafuta watawala wengine, (michepuko na wanaoweza kumfariji na kujali hisia zake hata kama sio kingono). Ukiona mke ameanza kukudharau (hakusikilizi), ama ukiona mke ameanza kufanya mambo kivyake vyake ama kisirisiri, usikimbilie "kuwaka", bali tambua kwamba "Umepungukiea na akili"

b)     Mwanaume huna haki ya kutimiza mamlaka ya kifalme katika ndoa na familia ikiwa hauwajibiki Kikuhani na Kinabii. Kama huna muda wa kuiombea familia yako(kuhani), kama huifundishi kuipenda na kuijali (nabii), kisha uka-practice ufalme, huo unakuwa ni UBABE. Lazima mfahamu kwamba, Biblia inasema, "Kumcha Mungu ni chanzo cha hekima". Hekima ni AKILI. Huwezi kuwa na akili za kuishi na mke kama mume mwema na kulea watoto kama baba bora, ikiwa haumchi Mungu. Kumcha Mungu ni kujifunza Neno lake na kuwa karibu nae kwa maombi.

Ole kwenu wanaume ambao hamumchi Mungu, na mnategemea ndoa na familia zenu viende sawa. Trust me, hata kama mnadhani mambo yanaenda sawa kwa sasa, you will surely "krashi" somewhere at some point!

KWA HIYO:-
Unaweza kuipeleka ndoa yako pasipo misingi hii, ukadhani mambo yanaenda na kumbe unaowaongoza wanaugulia ndani kwa ndani sema hawawezi kukuambia. Kama mimi ningekuwa wewe, ningeyaingiza haya maarifa mara moja katika ndoa yangu.

Ni mimi ninaewajali sana,




No comments: