Tuesday, September 18, 2018

UMKABIDHI BWANA NJIA YAKO (Zab 37:5) Samson Mollel 0767 664 338/0713 664 338


UTANGULIZI

Bwana Yesu apewe sifa kanisa la Mungu!

Mtu wa Mungu, unajua kuna wakati mambo katika dunia hii yanaenda vibaya mpaka unadhani kwamba upo peke yako na hakuna mtu mwingine wa kukusaidia. Kuna wakati unaandamwa na matatizo na shida nyingi mpaka unakata tamaa kabisa na hauoni kama kuna anayeweza kukusaidia.

Upo wakati katika maisha ya mwanadamu mambo yanakuwa mabaya hata imani yako inakuwa mashakani, hapa ndipo pale mtume Paulo anapowaambia Waefeso kwamba “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” (Waefeso 6:13), kumbe ipo siku ya uovu katika maisha ya mwanadamu ambapo inakubidi uwe umezivaa silaha za Mungu ili uweze kushindana na kushinda.

Mtume Paulo ametaja hizo silaha ambazo kimsingi zinatakiwa kuwepo ndani ya mtu yeyote aliyeokoka ambazo ni ……… kweli viunoni,…………dirii ya haki kifuani,………. miguu utayari, ……. ngao ya imani,……….. chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu. Katika silaha hizi alizozitaja mtume Paulo ipo silaha moja inaitwa ngao ya imani; silaha hii maana yake ni kuamini kwamba vyovyote itakavyokuwa BWANA atatenda kwakuwa namtumaini yeye.

Mtu wa Mungu ninao ushuhuda ambao huenda ukakusaidia kwa namna moja katika maisha yako ya kiroho na ya kimwili kwa habari ya somo hili.

Mwaka 2017 mwezi Mei niliingia katika changamoto kubwa sana ya maisha katika kipindi cha mwezi mmoja ambao niliona kama mwaka mmoja. Mke wangu aliugua sana kwani ilifika mahali hata kusimama mwenyewe hakuweza, mahitaji ya fedha kwaajili ya kuendesha familia na matibabu yalikuwa makubwa na hapo mke wangu hakuwa na kazi yeyote kwani kampuni aliyokuwa akifanyia kazi iliuzwa kwa kampuni nyingine na wafanyakazi wa mikoani wote wakaachishwa kazi, hivyo mshahara wangu pekee ndio ulikuwa ukitegemewa kwaajili ya mambo yote ya kuendesha maisha hapo nyumbani. Mwezi huohuo wa Mei, 2017 mwajiri wangu akasimamisha mshahara wangu kwa tuhuma zisizo na ukweli kwani alinituhumu kutokuwepo kazini. Maisha yangu yalibadilika ghafla ndani ya siku chache nikajikuta nikilia kama mtoto mdogo asiye na msaada. Ilifika mahali pamoja na kukopa kwa watu na msaada wa marafiki nilikuwa sina uhakika wa kesho familia yangu itakula nini.

Lakini mtu wa Mungu walikuja wana maombi ambao ni rafiki wa familia yangu ilibidi niwaeleze hali halisi, kwakweli waliomboleza pamoja na mimi kwa kumlilia Mungu na unabii ukatoka kwamba “tumtegemee Mungu naye atafanya njia ya kutokea katika jaribu hilo na nisikope tena”. Baada ya maombi hayo siku ya tatu nilipata posho iliyonilipa vizuri hata kuliko ule mshahara wangu wa mwezi mmoja uliozuiwa. Nikamwona Mungu kwa viwango vya kuniinua sana! Ushuhuda huu nimeutoa kwa sehemu kidogo tu ili ujifunze kitu kwa habari ya kumtegemea Yesu katika magumu unayopitia.

Mtu wa Mungu hayo yaliyonikuta kumbuka nimeokoka, mke wangu na watoto wameokoka, binti yetu wa kazi ameokoka, mimi ni mwalimu wa Neno la Mungu; lakini mambo hayo yote ni kama yalipotea kabisa ndani yangu nikaanza kuona matatizo yamenizidi kuliko ile neema kubwa ya Kristo Yesu.

 (Angalizo: Hapa ninazungumza na mtu aliyempa Yesu Kristo maisha yake, anayeishi kwa kumtegemea Yesu na asiyeabudu miungu mingine yaani mtu anayemcha Mungu asiyefuata kawaida ya ulimwengu huu)

Nimekuandalia pointi kadhaa ambazo zitakupa tafakari na sababu ya kumkabidhi BWANA njia zako na kumuamini yeye kwa kila jambo kwamba atafanya kama alivyofanya kwangu na kunivusha atakuvusha na wewe.


UMKABIDHI BWANA NJIA YAKO
Kuna wakati katika maisha unaona kwamba mwelekeo wako ni kama Mungu hayupo na wewe yaani amekuacha, lakini Mungu yupo pamoja na wewe ila anataka umtazame yeye peke yake na sio vile vitu alivyokupa wewe, kwamfano kuna wakati nilitazama mshahara wangu kama msaada wangu wakati wa shida, Mungu akanionesha kwamba yeye anazo njia nyingi za kunisaidia zaidi ya kutegemea mshahara; ndio maana tunasoma katika Zaburi 37:5 “Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.” Ninaposema umkabidhi Bwana njia yako ninamaanisha katika kila hali unayopitia amini kwamba Jehova anajua njia bora zaidi ya ile unayotamani wewe ifunguke. Neno la Mungu linatufundisha kwamba Bwana anazo njia ambazo ni tofauti na njia zetu Isaya 55:8-9 “8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. 9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.” Ndugu katika Kristo haijalishi unapitia katika jambo gani, wewe kabidhi njia zako kwa Bwana Yesu naye atafanya yale ulidhani hayawezekani kwa njia za Mungu yatawezekana na wewe utavuka pale ulipokwama.


SAFARI YA WANA WA ISRAELI
Safari ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri kwenda nchi ya ahadi Kaanani ilikuwa na mambo mengi ambayo tunapaswa kujifunza sasa.
Kwanza nataka ufahamu kwamba ni kweli kabisa wana wa Israeli walisafiri safari ya kimwili kabisa na walikutana na changamoto za kimwili kabisa kama wewe na mimi tunavyoishi katika hali ya mwili na tunakutana na changamoto amabazo nyingine ni za kimwili kabisa. Vilevile katika safari yao ya kimwili waliongozwa kiroho na Yesu mwenyewe (alitambulika kama malaika wa Bwana) na walilishwa vitu vya kiroho (mana).
Mtu wa Mungu fahamu kwamba kile unachoona katika agano la kale yaani safari ya wana wa Israeli hata sasa tunaendelea katika safari hiyo lakini kwa jinsi ya rohoni. Neno la Mungu linatuambia katika Wakolosai 2:16-17 ‘’ 16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; 17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.’’ Pia tunasoma katika Waebrania 10:1a “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, …………….”
Kumbe agano la kale ni kivuli cha agano jipya, yaani agano halisi ni agano jipya na torati (agano la kale) ni kivuli chake.


Bahari ya shamu
Tuendelee na safari ya wana wa Israeli! Wakati Fulani katika safari yao walikutana na bahari ya Shamu ambapo wao walijua kuwa mwisho wa safari yao umefika hata wakaanza kumlalamikia Musa na kutamani kama wangebaki Misri; lakini pamoja na kukata kwao tamaa, Musa alimgeukia Mungu naye Mungu akafanya njia pale walipokuwa wao wameona hakuna njia tena.
Tunasoma kitabu cha Kutoka 14:11-22 “11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? …………….13 Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. 14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya……………………………21 Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. 22 Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto.”

Mtu wa Mungu hebu jipe muda utafakari katika hali ya kawaida umekutana na bahari na unataka kwenda upande wa pili wa bahari, unadhani kama hauna boti au nyenzo ya kukuvusha na mali zako zote utafanyaje? Mwangalie Yesu kwani ni kazi yake kukuvusha na wewe ni kazi yako kuamuamini Bwana Yesu.
Inawezekana upo sehemu umekata tama kama wana wa Israeli, mwangalie Jehova kwani yeye anazo njia ambazo ni juu sana ya fikra zetu naye atatuvusha, atakuvusha kwenye mkwamo wa magonjwa, uchumi, ndoa, kazi biashara.


Maji ya kunywa jangwani
Changamoto katika safari ya wana wa Israeli haikuishia hapo, walipofika mahali panaitwa Mara (kwasababu maji ya mahali pale yalikuwa machungu)  Neno la Mungu linatuambia “22 Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji. 23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 24 Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?” Kutoka 15:22-24

Kitu ninachotaka nikuoneshe hapa ni kwamba wana wa Israeli bado walikuwa hawamwamini Mungu aliyewavusha katika bahari ya shamu, bado walikuwa na wasiwasi na Jehova, jambo hili lilipelekea changamoto nyingi kuinuka katika safari yao. Sikiliza nikufahamishe, Mungu anataka watu wanaomuamini na kumtegemea yeye pekee, ukimtilia shaka Mungu anaona kwamba unamdharau kama ilivyotokea kwa wana wa Israeli (Hesabu 14:11,23 “11 Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao……. 23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;.”) Kumbe kwa kumtilia shaka Mungu Jehova wana wa Israeli wote walioona shaka hawakuweza kuingia ile nchi ya ahadi.

Ukiendelea kusoma maandiko utagundua kuwa wana wa Israeli waliendelea kukutana na changamoto ya kukosa maji mara kwa mara na hii ilitokea ili waweze kuamini kwamba Mungu ndiye anayeweza kuwasaidia na sio mwanadamu (Kutoka 17:3-4, Hesabu 20:3-5).

Napenda ufahamu kuwa, ikiwa utakuwa na shakashaka juu ya ukuu wa Mungu kukuvusha katika eneo lenye changamoto katika maisha yako basi uwe na uhakika kwamba maisha yako katika eneo hilo yatakuwa na changamoto kila wakati mpaka utakapoamua kumuamini Mungu na kumkabidhi njia zako. Mkabidhi Bwana Yesu njia zako naye atakuvusha pale kwenye changamoto.


MKONO WA BWANA HAUSHINDWI KUKUSAIDIA
Ikiwa umemkubali Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako, nawe unaamini kwamba damu ya Yesu imekukomboa, basi kabidhi njia zako kwa Bwana Yesu naye atakutendea mambo makubwa sawa na Neno lake kutoka Isaya 59:1 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;”

Yesu mwenye amesema katika injili ya Mathayo 7:11 “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

Ukimkabidhi Yesu njia zako halafu umwamini kwamba atakutendea jambo hilo basi uwe na  uhakika kwamba atafanya kwa utukufu wa jina lake.

Yesu anatoa mfano wa wewe na mimi jinsi unavyoweza kuwajali watoto wako na kuwatunza ili wasitindikiwe na unafanya hivyo pamoja na mapungufu yako ya kibinadamu, Yesu anasema kama wewe unaweza kufanya hivyo katika hali yako ya uovu, je? Baba wa mbinguni si atafanya na kuzidi?

Mtu wa Mungu mkabidhi Bwana njia zako, haijalishi unapitia jambo gani, mkabidhi Bwana njia zako na umwamini naye atafanya.