Saturday, January 6, 2018

SOMO: HOFU YA SHETANI NI KUMDHARAU MUNGU - Samson Mollel (0767-664 338)


Bwana Yesu Kristo apewe sifa!!!

Nimefunuliwa juu ya somo hili ili kukusaidia mtu wa Mungu kwamba unapokuwa na hofu ya shetani ni kumdharau Mungu. Fahamu kwamba kuna tofauti ya kubwa hofu ya Mungu nahofu ya shetani.

Hofu ya Mungu au kumcha Mungu (fear of the Lord) ni hali ya kumheshimu na kumuogopa Mungu kwakuwa Mungu ni Mkuu mno kuliko mwanadamu (Ayubu 33:12b“Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.”) na ndiye aliyetuumba sisi na ndiye anayetupa uhai na riziki za kila siku. Hofu ya shetani ni kumuogopa shetani kuliko Mungu na kumheshimu shetani kuliko Mungu na jambo hili ni machukizo mbele za Mungu.


CHANZO CHA HOFU NI KUKOSA IMANI

Hofu ya shetani (wasiwasi/woga) hutokana na kushindwa kumuamini Mungu na kuona kuwa shetani anazo nguvu za kumshinda Mungu. Yaani unaposhindwa kuona kuwa Mungu ni Mkuu na anweza kukuvusha na ukaanza kumuona shetani ana nguvu na atakushinda basi hapo ufahamu kuwa umemuamini shetani kuliko Mungu. . Yaani unaposhindwa kuona kuwa Mungu ni Mkuu na anweza kukuvusha na ukaanza kumuona shetani ana nguvu na atakushinda basi hapo ufahamu kuwa umemuamini shetani kuliko Mungu. Wakati wanafunzi wa Yesu wanataka kuzama baharini wakamuita Yesu awasaidie, Yesu aliwaambia kuwa ni waoga (yaani wana hofu) na chanzi cha hofu yao ni ukosefu wa imani kama tunavyosoma katika maandiko matakatifu (Mark 4:40“Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”Math 8:26“Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba?Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.”)


HOFU NI ROHO

Hofu ni roho kamili (pepo) na inaweza kukuvaa wakati wowote kama vile mtu anavyoweza kuvamiwa na pepo wa udhaifu, uasherati/uzinzi, wizi, uongo, umasikini; roho hii ya hofu inatoka kwa shetani na sio kwa Mungu sawasawa na Neno la Mungu kutoka 2Tim 1:7“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.” Kumbe Neno la Mungu linasema kuwa roho ya woga (hofu) haitoki kwa Mungu bali kwa shetani.
Mtu wa Mungu fahamu jambo hili kwani ni ufunuo; kabla hofu haijaingia ndani yako lazima litangulie tukio la kipepo (la kichawi) litakalo kufanya uipokee roho ya hofu ndani yako
Sasa tutazame mifano kadha wa kadha kwenye Biblia inayotuonesha namna roho ya hofu inavyofanya kazi.


Habari ya Petro kuzama majini

Tunasoma habari za Petro kwamba aliweza kutembea juu ya maji kwa kumuamini Yesu baada ya Yesu kumita petro, lakini ni nini kilitokea hadi Petro akaanza kuzama katika yale maji?
Mathayo 14:28-30“28 Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. 29 Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. 30 Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.”

Biblia inasema kuwa “Lakini alipouona upepo, akaogopa”, kumbe upepo ndio tukio lililotengenezwa kwaajili ya Petro ili kumtia hofu, na baada ya hofu ya ule upepo (yaani pepo wa hofu) kumuingia Petro tunaona Petro anaanza kuzama majini “akaanza kuzama, akapiga yowe,”. Tunaonakuwa kilichomfanya Petro azame sio upepo bali ni ile hofu iliyoingizwa ndani yake na ule upepo aliyouona.

Mtu wa Mungu kata kila hali inayopelekea kuingiwa na hofu ndani yako kwani kinachokushinda wewe sio shetani bali ni ile hofu yako kwa shetani ndio adui yako mkuu.


Habari za Ayubu kupatwa na madhara ya hofu

Ukishaingiwa na hofu kama ni nilivyosema hapo awali, hiyo hofu ndio adui wako mkubwa na ndio itakayokutesa kwani hofu ni roho kutoka kuzimu. Ayubu aliikubali hofu nayo roho ikamvaa na kama vile alivyohofu ndivyo ilivyo tokea Ayubu3:25“Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia.”

Nataka kukuambia kuwa hofu hutokea kuwa kitu dhahiri kwakuwa vitu vyote huanzia rohoni na baadae kudhihirika katika mwili. Kuna watu wanaugua magonjwa mbalimbali ya mwili lakini kumbe ni hofu ndio chanzo cha matatizo yao, Ayubu alipata ugonjwa wa mifupa kwaajili ya roho ya hofu iliyomuingia Ayubu 4:14“Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote.”

Kuna watu wameiruhusu roho ya hofu kuwatawala katika eneo la biashara na biashara zikaanguka, wengine wameruhusu kwenye afya na wameugua magonjwa ya ajabu na wamekosa tiba, wengine wameikubali hofu ya kifo na mauti imewapata katika maeneo mbalimbali ya maisha yao.


HOFU/WOGA NI DHAMBI

Kama ulishawahi kufahamu kuwa kuna dhambi ambazo mtu akitenda hawezi kuurithi Ufalme wa Mungu, basi moja ya hizo dhambi ni hofu au woga. Biblia imeweka bayana kuwa waoga (wenye hofu) wote hawataurithi uzima wa milele Ufunuo 21:8“Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Unaweza kujiuliza kuwa inawezekanaje woga/hofu ikakupeleka kuzimu? Jibu ni rahisi sana, ni kwasababu hofu ni roho kutoka kwa shetani na ujasiri/nguvu ni Roho kutoka kwa Mungu, hivyo mwenye hofu ameingiwa na roho kutoka kwa ibilisi kama yanenavyo maandiko 2Tim 1:7“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”


MUNGU ANACHUKIA HOFU KWAKUWA NI KUMDHARAU YEYE

Kwa wale wasomaji wa Biblia mtafahamu kuwa katika agano la kale vitabu vitano vya Musa sehemu kubwa inazungumzia matendo makuu ya Mungu aliyowatendea wana wa Israeli kwa kuwatoa katika utumwa waliokaa kwa zaidi ya miaka mia nne, vilevile BWANA  aliwashindia dhidi ya adui waliokutana nao katika safari yao. Kwa ujumla ni kwamba wana wa Israeli walitembea kwa ushindi mkuu katika safari yao.

Lakini walipoikaribia ile nchi ya ahadi, wakawatuma wapelelezi na baadhi ya wale wapelelezi wakaleta habari mbaya ya ile nchi ni ya majtu na kwamba hawawezi kuingia katika nchi ile kwani wale watu wa nchi ile wana nguvu zaidi yao. Kama tunavyosoma katika kitabu cha Hesabu 13:31-33“31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. 32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 33 Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Joshua na Kalebu wakakanusha habari zile mbaya kwa imani na kusema kuwa wataingia katika nchi ya Kaanani kwa nguvu za Mungu na watawashinda adui zao kwani BWANA yupo upande wao; Hata hivyo wana wa Israeli wakachagua habari zenye hofu na kuacha habari za imani ya kushinda kama walivyosema Joshua na Kalebu kiasi cha kutaka kuwaua Joshua na Kalebu kama tunavyosoma katika Hesabu 14:6-10“6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; 7 wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8 Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope. 10 Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.”


Kwasababu  yawana wa Isareli kushindwa kumwamini Mungu hasira ya Mungu ikawaka juu yao na wakapewa adhabu kubwa ya kutoingia katika nchi ya ahadi kama ilivyoandikwa katika Hesabu 14:11, 22-24“11 Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini?Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao….. 22 kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; 23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; 24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.”


Mungu anasema “…..Je!Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini?.....” kumbe kudharau kunatokana na kushindwa kuamini, kwahiyo unaposhindwa kumuamini Mungu tayari unakuwa umemdharau na hasira ya Mungu inawaka juu yako.
Lakini tuanaona Mungu anasema kuwa  mtumishi wake Kalebu amekuwa na roho nyingine ndani yake, maana yake ile roho ya hofu na woga iliwavaa Israeli haikumvaa Kalebu na Yoshua



Samson Mollel 0767 664 338
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)
www.uzimawamileleministries.blogspot.com