Sunday, July 22, 2018

SOMO : MILANGO YA FAHAMU YA ROHONI - Samson Mollel (0767-664338)



MILANGO YA FAHAMU KATIKA HALI YA MWILI


Milango ya fahamu ni ogani za mwili zinazoturuhusu kujua na kuyamudu mazingira yetu kwa usahihi. Kibailojia inaelezwa kuwa ogani yenye uwezo wa kupokea habari za nje ya mwili kama vile; Nuru, Sauti, Halijoto, Mwendo, Harufu na ladha ili kuzibadilisha katika mfumo wa kiumeme inachukuliwa kwa njia ya mfumo wa neva hadi kwenye ubongo.

Kuna milango mitano ya fahamu katika mwili wa mwanadamu ambayo ni Jicho/Macho (Kuona), Sikio/Masikio (Kusikia), Pua (Kunusa), Ulimi (Kuonja) na Ngozi (Kugusa)

Kama milango ya fahamu imeharibika, tunasema mtu ni kipofububu au kiziwi, ana matatizo kuelewa mazingira yake sawa na jinsi wanavyoweza watu wengine.
Milango ya fahamu ni muhimu sana kwa viumbe hai kutokana na kwamba inasadia kiumbe hai katika shughuli zake za kila siku, hasa katika kufatuta mahitaji muhimu.

MTU NI ROHO


Biblia inasema wazi kwamba hapo mwanzo Mungu aliamua kumuumba mtu kwa mfano wake (Mungu) na kwa sura yake (Mungu) mwenyewe kama tunavyosoma katika maandiko matakatifu katika kitabu cha Mwanzo 1:26 – 27 “26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Nataka ufahamu kwa uhakika ya kwamba mtu anayeongelewa hapa ni roho na sio mwili kama vile watu wengi wanavyodhani, unaposikia wewe ni mfano wa Mungu, basi fahamu anayeongelewa hapa ni mtu wa ndani (Roho yako) ndiye mfano wa Mungu. Uhakika wa kwamba mtu ni roho tunaupata katika maandiko matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu yeye ni Roho hivyo yoyote aliye mfano wa Mungu naye pia ni Roho kama tunavyosoma katika kitabu cha Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Hivyo basi kama mtu ni roho na milango yake ya fahamu ipo rohoni pia kama ilivyo milango ya fahamu ya mwilini.

FAHAMU ZA ROHONI


Kama vile ulivyo mwili, mtu ambaye ni roho anazofahamu katika hali ya roho ambazo zinamuwezesha kuwelewa/kutambua mazingira ya rohoni kama vile mwili unavyoweza kutambua mazingira yake ya mwilini. Fahamu zilizopo katika ulimwengu wa roho ni kama zile za ulimwengu wa mwili zinazohusiana na Kugusa, Kuona, Kusikia, Kuonja na Kunusa/Harufu.

KUONA ROHONI (MACHO YA ROHONI)


Ili uweze kupata uelewa sawasawa kwanza vuta picha ya mwanadamu mwenye macho ambaye anaangalia na kuona mambo mbalimbali katika maisha ya kawaida, macho yanampa uwezo wa kutambua watu na vitu. Kwa kutumia macho mtu anaweza kuweka kumbukumbu ya matukio fulani katika ufahamu wake na mambo hayo aliyoyaweka yakamsadidia kuja kufanya maamuzi sahihi au kuwasaidia wengine kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao ya kila siku. Ndivyo ilivyo kwa mtu wa rohoni, mtu wa rohoni anayo macho ambayo yanamsaidia kuona vya rohoni na kufahamu vitu vya rohoni vilevile kuweka katika ufahamu wake kumbukumbu za rohoni kwa matukio aliyoyaona ili imsaidie katika kufanya maamuzi ya kiroho.

Neno la Mungu linatuthibitishia kuwepo kwa macho ya rohoni ambayo mtu wa rohoni anaweza kuyatumia kuona na kutambua mambo ya rohoni kama tunavyosoma katika Waefeso 1:17-18 “17 Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; 18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;”

Hapo mtume Paulo anawaombea Waefeso kwamba macho ya mioyo yao yatiwe Nuru, kumbe waefeso walikuwa na macho ya rohoni lakini yenye giza sawa na vipofu, walikuwa hawaoni ukuu wa Kristo Yesu na utajiri wa Utukufu wa Yesu. Inawezekana hata wewe unayesoma sasa hivi umepewa neema ya kupata somo hili ili macho yako ya rohoni yatiwe Nuru ya Kristo upate kuuona Ukuu wake na utukufu wa Kristo; Mwambie Bwana Yesu aachilie nuru yake katika macho yako sasa ili giza likuondoke upate kuona rohoni sasa kwa jina la Yesu!

Neno la Mungu linazidi kututhibitishia kwamba yapo macho ya rohoni na watu wenye macho hayo wamefungwa (wamepofushwa) macho yao na hata hawaoni kama tunavyosoma habari ya mtumishi wa Nabii Elisha katika 2Wafalme 6:15-17 “15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? 16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. 17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.” Loh! Kumbe unaweza kuwa na macho na wakati huo usione kinachoendelea! Sema na Yesu sasa kwamba macho yako yafunguke na upate kuona tena Utukufu wa Jehova.

KUSIKIA ROHONI (MASIKIO YA ROHONI)


Katika hali ya kawaida (hali ya mwili wa damu na nyama) mwandamu anakuwa na masikio ambayo yanaweza kuwa na uwezo wa kusikia au yasiwe na uwezo wa kusikia, kama masikio yakiweza kusikia hiyo ndio sahihi lakini kama hayawezi kusikia basi hapo kuna shida; yaani inawezekana mtu huyu ni kiziwi au anayomatatizo ya yanayomzuia kusikia sawasawa.

Katika ulimwengu wa roho yapo masikio ya rohoni yanayomuwezesha mtu wa rohoni kusikia sauti za rohoni na kufahamu/kuelewa yale yanayonenwa katika ulimwengu wa roho. Kama mtu hana masikio ya rohoni basi huyo ni mlemavu wa rohoni na anahitaji kuponywa mlango huo wa fahamu ili aondoke katika ulemavu huo.

Tunasoma katika kitabu cha Ufunuo 1:9-11 “9 Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. 10 Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, 11 ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”Yohana anasema alikuwa katika Roho akasikia sauti, kumbe unaweza kuwa rohoni ukasikia. Kama mtu aliyeko rohoni anasikia basi mtu huyo anayo masikio ya rohoni yanayofanya kazi sawasawa. Hivi umeshawahi kuwaza kwamba kama hausikii ukiwa rohoni basi ni hakika kwamba umekuwa kiziwi wa rohoni! Achilia damu ya Yesu katika masikio yako ya rohoni uondowe kwa jina la Yesu uziwi wa kiroho.

Wakati mwingine unaweza kuwa unasikia sauti ya rohoni lakini hauelewi wala hauwezi kutambua unaongea na nani, Neno la Mungu linatufundisha kwamba hali ya namna hiyo inaweza kutokea kama ilivyomtokea mtoto Samweli, tunasoma katika 1Samwel 3:1-10 “1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. 2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), 3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; 4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. 5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. 6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. 7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. 8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. 9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. 10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.”

Kilichomkuta mtoto Samweli kinaweza kumkuta mtu yeyote aliyeokoka hata sasa hivi, inawezekana kwamba bado ufahamu wako haujafunguliwa kuweza kuitambua sauti ya Mungu hivyo sauti ikitoka rohoni huwezi kuitambua. Neno la Mungu linasema kwa ……..7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake…………. Kumbe samweli pamoja na kwamba alikuwa anamtumikia Jehova lakini alikuwa haijui sauti ya Mungu anayemtumikia.

Hebu fungua kinywa chako Omba maombi haya pamoja na mimimi “Bwana Yesu Ninakuomba Uyafungue Masikio Yangu Ya Rohoni Na Unipe Roho Ya Ufahamu Ili Niweze Kutambua Sauti Yako Unaposema Namimi, Ninaomba Katika Jina La Yesu, Amen!”

Mwana wa Mungu aliye hai inawezekana kabisa ukasikia sauti ya mtu akisema kutoka rohoni hata kama kinywa chake cha milini kimefungwa. Neno la Mungu linatufundisha kwamba Sara mke wa Ibrahim alicheka rohoni na Bwana akamsikia Mwanzo 18:12-15 “12 Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13 Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14 Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. 15 Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.”
Lakini pia tunajifunza kuwa hata shetani alipoamua kuasi alisema maneno ambayo yalisikika rohoni kama ilivyoandikwa katika Isaya 14:12-15 “12 Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! 13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. 14 Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. 15 Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.”

Hapa tunajifunza kuwa mtu anaweza kunena kutokea rohoni/moyoni maneno ambayo yanasikika katika ulimwengu wa roho na hata kumtenda Mungu dhambi au kumpa shetani nafasi ya kushambulia maisha yako.

KUONJA ROHONI (ULIMI WA KIROHO)


Kuna watu wamekua wakiota ndoto ama wanakula wenyewe au wanalishwa katika ndoto vitu vya aina mbalimbali, mwingine atakuambia nilipewa maji machungu kwenye ndoto au nilikula chakula kibaya sana kwenye ndoto au nilikula chakula kitamu kwenye ndoto (Kumbuka ndoto ni ulimwengu wa roho). Kama inavyokuwa katika hali ya mwili huu wa damu na nyama kwamba unaweza kujua ladha mbalimbali za vyakula/vinywaji au chochote kinachoingia kinywani, ndivyo ilivyo na kwa ulimwengu wa roho. Unapokuwa rohoni unaweza kutambua ladha ya vitu kwani Biblia inatufundisha kwamba upo ulimi wa rohoni kama tunavyosoma katika Luka 16:22-24 “22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. 23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. 24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.” Kumbuka mfano huu alioutoa Yesu alikuwa anazungumzia habari za roho ya masikini Lazaro na roho ya Yule tajiri baada ya kufa kwao, sasa tunaona kumbe tajiri alitani kuburudishwa ulimi wake kwa tone la maji katika ulimwengu wa roho.

Mtu wa Mungu ukizidi kusoma Neno la Mungu utafahamu kwamba mtu akiwa rohoni kwa kutumia mlango wa fahamu wa kuonja (ulimi) anaweza kujua ladha ya vitu katika ulimwengu wa roho kama tunavyosoma katika Ezekiel 3:1-3 “1 Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. 2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. 3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.

Kumbe nabii wa Mungu Ezekiel aliweza kula na kutambua ladha ya gombo kuwa lilikuwa na utamu wa asali. Mwombe Yesu leo ahuishe milango yako ya fahamu katika ulimwengu wa roho uweze kufahamu kile kinacholetwa kwako kama chakula cha rohoni, hii itakusaidia kujua nini kimeletwa kwako na kama ni kitu kibaya au kizuri.

HARUFU YA ROHONI/KUNUSA ROHONI (PUA ZA ROHONI)


Ukiwa katika hali ya mwili na kama hauna kasoro zozote katika pua zako, unaweza kufahamu/kutambua harufu za aina Fulani na ukaziweka katika kumbukumbu zako na zikakusaidia katika kufanya maamuzi siku za mbele/baadae. Kwamfano unaweza kufahamu harufu ya kitu kinachoungua na siku ukinusa hata bila kuona utatambua kwamba kuna kitu kinaungua; hivyo ndivyo ilivyo kwa jinsi ya rohoni, kama pua zako za kiroho zinafanya kazi sawasawa unaweza kugundua mambo ya rohoni hata kabla ya kuyaona.
Ukisoma 2Kor 2:14-16 “14 Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. 15 Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; 16 katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?”

Mtume Paulo akijaa Roho Mtakatifu anaongelea habari ya manukato (Perfume) katika ulimwengu wa roho. Kama ukiweza kugundua aina ya manukato katika ulimwengu wa roho, maana yake ni kwamba mlango wako wa fahamu wa kunusa (pua) wa rohoni unafanya kazi sawasawa. Hii ndio sababu Mtume Paulo anazungumzia harufu za aina mbili yaani harufu ya mauti na harufu ya uzima, ………….katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima…………..

Vilevile tunamuona Yohana akiwa rohoni anatambua kwamba maombi ya watakatifu yalikuwepo kwa Mungu kwenye mabakuli (vitasa) kama manukato; aliwezaje kujua kwamba yale maombi ni manukato? Maana yake mlango wa Yohana wa fahamu katika kunusa (pua za rohoni) ulimfahamisha kwamba yale ni manukato kwa kunusa. Ufunuo 5:8 “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.”

Hii inazidi kudhihirishia kwamba ukiwa rohoni unaweza kunusa na kutambua harufu ya vitu vya rohoni.

KUGUSA/KUGUSWA ROHONI (NGOZI YA KIROHO)


Siku moja Yesu alikuwa katika kazi ya kuihubiri injili, watu wengi mno walimsonga huku na kule pengine wengine walimvuta na kumuita ili awaponye. Lakini kuna mwanamke mmoja ambaye aligusa vazi la Yesukwa imani na Yesu akatambua kwamba kuna mtu amemgusa na kuuliza kwamba ni nani huyo kama ilivyoandikwa katika Luka 8:43-46 “43 Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga asipate kuponywa na mtu ye yote, 44 alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma. 45 Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. 46 Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.”

Swali la msingi sana la kujiuliza hapa ni hili, Yesu aligunduaje kwamba ameguswa na nguvu zimemtoka wakati alikuwaamezongwa na watu wengi? Iwezje mtu mmoja amguse na afahamu dhahiri na kusisitiza kwamba ameguswa? Kwa uhakika kabisa mama yule alimgusa Yesu kwa imani kutokea rohoni na kwakuwa yesu alikuwa wa rohoni alitambua mara ile ile, alitambua kwakuwa alitumia mlango wa fahamu wa rohoni wa kugusa na kufahamu kwamba kuna mtu amemgusa.

Vilevile tunasoma katika Ufunuo 1:17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,” Yohana alitambua kwamba Yule mtu ameweka mkono juu yake kwakuwa akiwa rohoni mlango wake wa ufahamu katika kugusa ulikua ukifanya kazi.

MAOMBI YA KUFUNGULIWA MILANGO YA FAHAMU YA ROHONI


Mungu wa Bwana wangu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, unipe mimi roho ya hekima na ya ufunuo katika kukujua wewe; milango ya fahamu (Macho, Masikio, Ngozi, Ulimi na Pua) ya roho yangu itiwe nuru, nijue tumaini la mwito wako jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wako kwangu mimi mtakatifu jinsi ulivyo; Nijue ubora wa ukuu wa uweza wako ndani yangu mimi niaminie jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wako; ulioutenda katika Kristo ulipomfufua katika wafu, ukaniketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho. Ukamweka mkono wako wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; ukavitia vitu vyote chini ya miguu yake, ukamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake.