Sunday, July 20, 2014

NINAMSHUKURU BWANA YESU KWA VILE ALIVYOONEKANA KATIKA HUDUMA HII YA LEO (20/07/2014) TUKIWA KIJIJI CHA KILYABOYA. WATU WA MUNGU WAMEFUNGULIWA KUTOKA KATIKA VIFUNGO MBALIMBALI VYA IBILISI KWA JINA LA YESU

 Wakati wa Ibada ya Kusifu na kuabudu ikiongozwa na Mtumishi wa Mungu Samson Mollel

 Wakati wa Ibada ya Kusifu na kuabudu ikiongozwa na Mtumishi wa Mungu Samson Mollel


 Judith (Mrs Renatus Philibert) katika ibada ya kusifu 

 Mtumishi wa Mungu Renatus Philbert akinena Neno la Mungu kabla ya kuingia katika Ibada ya Maombi

Mtumishi wa Mungu Renatus Philbert akinena Neno la Mungu kabla ya kuingia katika Ibada ya Maombi

UAMSHO "Je! Ni laana au ni baraka?"

UAMSHO
(Mwl.C.Mwakasege)

Je! Ni laana au ni baraka?
(Sehemu ya Kwanza)
Hili swali linakuja kwako – tena kwa wakati wake hasa! Nilikuwa nafundisha katika kanisa fulani hapa nchini – nilipouliza swali hili wengi wakajibu kwa pamoja – ni baraka! Lakini wakati huo huo walikuwako wazee wa kanisa ambao walikuwa wanauona uamsho ya kuwa ni laana!
Nilipokuwa nahubiri kwenye kanisa moja huko Marekani ya kaskazini – Mchungaji na wakristo wa kanisa hilo walinieleza juu ya uamsho uliotokea kanisani hapo miaka michache ya nyuma – na baada ya kipindi si kirefu kanisa likagawanyika na wakristo wengine wakahama, wengine wakarudi nyuma kiroho. Nilipowauliza chanzo cha mgawanyiko huo ni nini – wakajibu bila hata kusita, wakasema “Ni Uamsho!”
  Je! unakubalina na jibu hili ya kwamba uamsho ukitokea katika kanisa huwa unagawa wakristo?
  Sehemu zingine vimetokea vikundi vya uamsho katika makanisa mbalimbali – mahali pengine vimefurahiwa na mahali pengine vimechukiwa, hata kufika hatua hata ya kuvipiga marufuku! Je! hii ni sawa?
  Ni wakati gani uamsho unakuwa ni laana na ni wakati gani uamsho – unakuwa ni baraka? Katika mfululizo huu wa maswali na majibu tutajifunza na kujibu maswali mbalimbali kuhusu Uamsho.
  Ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa mafundisho utakayoyapata katika majibu ya maswali katika mfululizo huu yatakuimarisha zaidi katika maisha yako ya wokovu, na katika kumtumikia Mungu.
  Pia, ni maombi yangu kwa Mungu, katika Jina la Yesu Kristo ya kuwa mafundisho haya juu ya uamsho yatasaidia kutatua matatizo mengi yaliyopo katikati ya Wakristo – hasa yanayotokana na uamsho.
  Ndiyo maana ni vizuri hata wewe uyasome majibu haya ukiwa katika hali ya maombi ili Mungu afungue moyo wako na akili zako upate kuyaelewa na maandiko. Maswali tutakayojibu ni haya yafuatayo:
  SWALI LA KWANZA: Uamsho ni kitu gani?
  Ni rahisi sana kuchanganya maana za maneno na matukio yake, hasa tunapozungumza juu ya Uamsho. Wengine wanachanganya maana ya uinjilisti na ile ya uamsho. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno haya Uinjilisti na Uamsho yana maana zinazotofautiana.
  Neno ‘Uamsho’ limetafsiriwa toka kwenye neno la Kiingereza ‘revival’. Na neno ‘revival’ linatokana na neno ‘revive’ ambalo lina maana ya kuhuisha, kuchochea, kurudishia nguvu, kufufua na kuamsha.
  Kwa mfano Nabii Habakuki alipokuwa anaomba alisema; “ Ee Bwana, FUFUA kazi yako katikati ya miaka …..” (Habakuki 3:2). Na katika Biblia ya Kiingereza ya King James mstari huu umeandikwa hivi; “O Lord, REVIVE thy work in the midst of the years …” kwa maneno mengine Nabii Habakuki alikuwa anaomba juu ya uamsho

Uamsho unatokea wakati ambapo Mungu, kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu anaposhuka ndani ya mioyo au roho za watu wake ambao wamepoa, au wamerudi nyuma kiroho, au wamekuwa vuguvugu au wamelala. Hawa watu mwanzo walikuwa  wameonja nguvu za Mungu, lakini baada ya muda walirudi nyuma kiroho au wakapoa. Uinjilisti maana yake ni kuitangaza habari njema – au kutangaza habari za Yesu Kristo. Uinjilisti hutumika wakati wa kuwaleta watu wasiookoka katika ufalme wa Mungu. Uinjilisti ni matokeo ya Uamsho katika Kanisa. Kanisa  lililopoa au kulala kiroho huwa halina mzigo wa Uinjilisti wala wa kuleta mavuno ya roho za watu kwenye ufalme wa Mungu.
  Kwa kusisitiza tu ni kwamba Uamsho ni matokeo ya nguvu za Mungu kuwatembelea upya WATU WAKE.
  Nguvu za Mungu zinapowatembelea watu ambao hawajaokoka, na kuwafanya waokoke, hatuliiti tendo hili kuwa ni uamsho, bali ni uinjilisti. Lakini nguvu hizi za Mungu zinapowatembelea watu waliokwisha kuokoka tayari, na kuamsha upya kiu ya kumjua na kumtumikia Mungu, huwa tunaliita tendo hili kuwa ni Uamsho.
  Ndiyo maana ukienda katika madhehebu ambayo kuna wakristo waliookoka na ambao hawajaokoka; wale waliookoka huwa mara nyingi huitwa ‘Wakristo wa uamsho’. Ndiyo maana mara kwa mara unasikia maneno kama haya; mikutano ya uamsho, vijana wa uamsho, watu wa uamsho, maombi ya uamsho, n.k.
  Tunapozungumzia juu ya uamsho, ujue ya kuwa ni lazima kuna kitu cha kuamsha. Kunakuwa na Uamsho, kwa kuwa kuna kitu cha kuamsha. Kunakuwa na ufufuko, kwa kuwa kuna kitu cha kufufuka. Kunakuwa na kuhuisha, kwa kuwa kuna kitu cha kuhuisha.
  Kazi ya kuamsha roho za wakristo waliopoa, au waliorudi nyuma kiroho, au waliolala kiroho, ni kazi ya Mungu mwenyewe, kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu.
  Mtu aliyekuwa ameokoka akirudi nyuma na kufa kiroho, kazi ya kumfufua au kumwamsha upya si ya mwanadamu bali ya Roho Mtakatifu.
  Ingawa ni kweli kwamba Mungu humshirikisha mtu amtakaye katika kazi zake mbalimbali kama tutakavyoona kadri tunavyoendelea; bado mwanzilishi na msimamishaji wa uamsho ndani ya mtu ni Mungu mwenyewe.
  Si vyema kumpa mwanadamu sifa ya kuleta uamsho mahali fulani, badala ya kumpa Mungu ambaye amemtumia mtu huyo kama chombo tu.
  Fahamu “si kwa uwezo (wa mwanadamu), wala si kwa nguvu (za mwanadamu), bali ni kwa ROHO YANGU, ASEMA BWANA WA MAJESHI” (Zakaria 4:6)
SWALI LA PILI: Kwa nini Mungu analeta Uamsho?
  Ukisoma katika Biblia utaona ya kuwa kuna sababu mbili kubwa ambazo zinamfanya Mungu alete uamsho katikati ya watu wake.
  Sababu ya Kwanza ni UAMSHO WA KAZI YA BWANA. Nabii Habakuki aliomba hivi, “Ee Bwana, FUFUA KAZI YAKO katikati ya miaka; katikati ya miaka tangaza habari yake; katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2).
  Sababu ya Pili ni UAMSHO WA MIOYO YA WATU WA MUNGU. Mtunga Zaburi aliomba hivi; “Je hutaki kurudi na KUTUHUISHA (Kutuamsha), watu wako WAKUFURAHIE? (Zaburi 85:6). Na katika kitabu cha Nabii Isaya 57:15 imeandikwa hivi; “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu na kuifufua mioyo yao waliotubu”.
1.Uamsho wa kazi ya Bwana
  “Ee Bwana, FUFUA KAZI YAKO katikati ya miaka; katikati ya  miaka tangaza habari yake; katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2)
  Nilipoyasoma maombi haya ya Nabii Habakuki nilijiuliza maswali kadhaa, na baadhi yake ni haya: Je! kazi ya Bwana maana yake nini? Je! kazi ya Bwana nayo inahitaji kufufuliwa? Kitu gani kinaua kazi ya Bwana hata ihitaji kufufuliwa?
  Maswali haya yalinifanya nianze kukisoma kitabu cha Nabii Habakuki kwa makini. Nilipokuwa nakisoma, niliyakuta mambo ambayo ningependa kukushirikisha hapa.
  Kitabu cha Habakuki kwa sehemu kubwa kinaeleza mazungumzo kati ya Mungu na nabii wake Habakuki. Habakuki anaanza kwa manung’uniko na malalamiko juu ya uharibifu wa haki, na kutokuonekana kwa kazi au uwepo wa Mungu katikati yao.
  “ Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia    kwa sababu ya UDHALIMU, ila hutaki KUOKOA. Mbona wanionyesha uovu, na unitazamisha UKAIDI? Maana UHARIBIFU NA UDHALIMU u mbele yangu; kuna UGOMVI, na MASHINDANO yatokea. Kwa sababu hiyo SHERIA INALEGEA, wala HUKUMU HAIPATIKANI;  kwa    maana watu wabaya huwazunguka wenye haki, kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka” (Habakuki 1:2-4).
  Ni wazi kwamba katikati ya wana wa Israeli – uzao wa Ibrahimu, kulitokea UDHALIMU, UKAIDI, UHARIBIFU, UGOMVI, MASHINDANO, UVUNJAJI WA SHERIA, na HAKI  KUTOKUWEPO. Habakuki hakuona ya kwamba ni halali kwa mambo hayo kuwepo katikati ya watu wa Mungu, na Mungu wao akae kimya.
  Na Mungu alimjibu kuwa atalitumia kabila la Wakaldayo kuwaadhibu wana wa Israeli (Habakuki 1:5 – 11)
  Katika mahojiano yake na Mungu, Habakuki anakubali kabisa ya kuwa wana wa Israeli wamekosa. Lakini anamwuliza Mungu ya kuwa kwa nini Yeye, aliye mtakatifu, tena mwenye macho safi asiweze kuuona uovu huo (Habakuki 1:12 – 13), na kwamba amewachagua Wakaldayo wapagani, ili watwae kisasi juu ya taifa teule.
  Nabii Habakuki alitaka kujua kwa nini Mungu ameamua kuwaadhibu wana wa Israeli kwa uovu wao kwa kuwatumia Wakaldayo walio waovu zaidi kuliko wao. Tena, kwa nini amsaidie Mkaldayo aliye mjeuri asiye na haki, ili apate ushindi? Kwa maneno mengine alitaka kufahamu kwa nini ujeuri, ugomvi na dhuluma vitawale mataifa na si haki na amani?
  Mungu alimpa Nabii wake Habakuki majibu mawili muhimu; 1. Mwishoni haki itashinda;
2. “Mwenye haki ataishi kwa imani yake” (Habakuki 2:4).
  Baada ya mazungumzo hayo, ndipo Nabii Habakuki alipoomba sala hii “ Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka, katikati ya miaka tangaza habari zake, katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2)
  Kwa maneno mengine alikuwa anamwomba Mungu kuwa badala ya kuadhibu akumbuke rehema ili awarehemu watu wake. Utendaji wa kazi yake ufufuke au uamke kwa upya katikati ya watu wake. Palipo na ugomvi alete amani. Palipo na dhuluma alete haki. Palipo na mashindano alete ushirikiano. Palipo na ukaidi alete upole na unyenyekevu.  
Je! huoni kuwa na sisi tunahitaji kuungana na Nabii Habakuki kuomba juu ya uamsho wa kazi ya Mungu katika makanisa na vikundi vya watu wa Mungu kama vya maombi vilivyopoa? Katikati ya Wakristo kazi ya Mungu haionekani. Kumejaa dhuluma, ukaidi, ugomvi na mashindano.
  Wakati umefika wa wewe na mimi kumwomba Mungu kwa juhudi ili kazi yake na matendo yake yaonekane tena katikati yetu. Palipo na ugomvi atuletee amani ipitayo fahamu zote. Palipo na mashindano atuletee ushirikiano katika Roho na kweli. Palipo na dhuluma atuletee haki na hukumu za kweli zisizokuwa na upendeleo. Palipo na ukaidi atuletee upole na kunyenyekea. Palipo na kuuchukia wokovu, alete kuupenda wokovu. Palipo na uchovu na uzito wa kuifanya kazi ya Mungu, alete utayari na wepesi badala yake! Kama ulikuwa hujaanza kuomba, basi anza sasa kwa ajili ya mahali unapotaka mabadiliko yatokee kwa wakristo wote kwa ujumla. Pia umwombe Mungu kuwa “katika ghadhabu akumbuke rehema”.
  2.   Uamsho wa mioyo ya watu wa Mungu
“Je! hutaki kurudi na KUTUHUISHA, Watu  wako  AKUFURAHIE?" Zaburi 85:6)
  Tafsiri nyingine ya maneno haya inasema hivi:
“Je hutatujalia tena maisha mapya ili watu wako wakufurahie?”
  Na katika maneno ambayo Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake yanayozungumza juu ya FURAHA MIOYONI MWAO – alisema hivi;
  “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea   kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. FURAHINI    NA KUSHANGILIA; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa   mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 5:11,12).
  Ukiona mtu aliyeokoka anakosa amani na furaha wakati anaposhutumiwa, anapoudhiwa, na anaposingiziwa uongo kwa sababu ya KUMWAMINI YESU, ajue ya kuwa amepoa kiroho na anahitaji uamsho. Yesu alisema yanapotokea hayo FURAHI na KUSHANGILIA.
  Pia, Yesu Kristo alisema hivi:
  “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa FURAHA. Mwanamke azaapo yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya FURAHA YA KUZALIWA MTU ULIMWENGUNI. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na MIOYO YENU ITAFURAHI, na FURAHA YENU hakuna awaondoleaye. Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin, nawaambia, mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata furaha yenu iwe timilifu  " (Yohana 16:20 – 24).  
Furaha ya Bwana ndani ya mioyo yetu sisi tulio wakristo, ndiyo nguvu ya kutuwezesha kuendelea katika wokovu bila manung’uniko. Ukiona mtu anasema ameokoka na huku amekosa FURAHA YA BWANA ndani yake, basi ujue kuna shida fulani katika maisha yake ya kiroho!
  Katika kitabu cha matendo ya Mitume furaha inaonekana wazi katikati ya wakristo hawa wa kwanza. Furaha inaonekana walipopokea nguvu za Roho Mtakatifu (Matendo ya Mitume 13:52). Furaha inaonekana Bwana alipofanya miujiza katikati yao (Matendo ya Mitume 13:8). Furaha inaonekana katikati yao walipoona watu wengine wakiokoka na kumfuata Yesu (Matendo ya Mitume 15:3). Na pia furaha inaonekana walipokuwa wakiumega mkate (Matendo ya Mitume 2:46).
  Na mtume Paulo katika nyaraka zake kwa waumini anazungumzia furaha katika maeneo mawili muhimu. Kwanza, anazungumzia juu ya furaha aliyonayo anapowaona wale aliowaongoza kwa Yesu wakiendelea katika imani ya wokovu (1Wathesalonike 2:19; Wafilipi 2:2). Pili, anazungumzia furaha anayopata yeye na mkristo yoyote yule anapoteswa kwa ajili ya Kristo, kwa kuwa si furaha ya kibinadamu, bali ni furaha iliyo tunda la Roho ndani ya mtu (Wagalatia 5:22).  
Ni wazi kabisa ya kuwa Mkristo asipoonekana ana FURAHA YA BWANA, basi hata maisha yake ya kiroho yanakosa changamoto. Na wengine hufikia hata kuacha wokovu.
Nakumbuka wakati fulani mtu mmoja alinifuata kwa ajili ya ushauri na akasema hivi; “Mimi nimeokoka, lakini naona napata mawazo ya kutaka kuacha wokovu, na niliona kabla ya kufikia uamuzi huo nije kwako unishauri”
Mara moja nilifahamu ya kuwa amekosa FURAHA katika njia hii ya wokovu. Baada ya kuzungumza na kumweleza kitu cha kufanya kufuatana na maandiko, nilimwambia asiache wokovu. Nikamuuliza “Ukimwacha Yesu utakwenda kwa nani? Namshukuru Mungu ya kuwa huyo mtu alipokea ushauri niliompa na anaendelea na wokovu.
  SWALI LA TATU: Uamsho ukitokea mahali kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu, mambo gani yanatokea?
  Uamsho unapotokea katikati ya watu wa Mungu, kuna mambo mengi yanayotokea, lakini mambo makubwa yafuatayo hujitokeza:
  1.  Hofu ya Mungu
Palipo na uamsho pana hofu ya Mungu. Kuna wakati unafika ambapo watu wa Mungu wanapoa na kutokujali sana mambo ya Mungu, na kutokupenda maombi ya muda mrefu, na hata kufikia kutokwenda kanisani au kwenye vipindi vya masomo ya biblia, kwa kujisingizia shughuli nyingi.
  Ukiona mambo haya yanajitokeza au yamejitokeza, basi ujue ya kuwa hofu ya Mungu haipo kati yao.
  Na Mungu anapoamua kujidhihirisha upya katikati yao kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, kunatokea uamsho, na uwepo wa Mungu unakuwa wazi kwa kila mtu. Na palipo na uwepo wa Mungu, pana hofu ya Mungu.
  Hofu ya Mungu inapotokea katikati ya watu wa Mungu inaleta mambo mpya. Ikiwa umekaa na watu waliookoka utakuwa umeona ya kuwa, hofu ya Mungu isipokuwepo katikati yao, huwa wengi wao wanaenenda bila ushuhuda na bila hekima, na matokeo yake ni kuleta makwazo na kuufanya udharauliwe.

Lakini hofu ya Mungu inaporudi katikati yao kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu, wanaanza upya kutembea katika ushuhuda na hekima. Je, unafahamu ni kwa nini? Kwa kuwa imeandikwa; “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, ……” (Zaburi 111:10).
  Tafsiri nyingine ya hofu ya Mungu ni kumcha Bwana. Mungu anapojidhihirisha upya katikati ya watu wake, kila mmoja wao anaona kama vile Mungu ameshuka kwa ajili yake tu na ameshuka kumshughulikia yeye tu! Kwa hiyo utaona watu wakiwa wepesi kutubu dhambi zao na kutengeneza maisha yao ya kiroho.
  Na kinachofuata ni watu hao kuanza kujishughulisha upya na mambo ya Mungu. Utaona wanapenda utakatifu, utaona wanapenda maombi na kumtumikia Mungu. Kunapotokea uamsho watu huona Mungu yuko karibu nao zaidi kuliko alivyokuwa zamani.
  Nakumbuka nilikuwa nahubiri mahali fulani hapa nchini, na niliposema wale wanaotaka kutubu waje mbele, watu wengi walikuja na kutubu kwa machozi, Roho wa Mungu alishuka kwa nguvu katika mkutano ule.
  Na nilipowafuatilia hao waliotubu, nikaona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni watu waliokuwa wameokoka zamani lakini wakarudi nyuma na kuanguka dhambini. Na neno lilipohubiriwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, wakachomwa mioyo yao, wakawa kama watu walioamshwa toka usingizini, wakaamua kutubu na kumrudia Bwana.
  Na matokeo yake ni vikundi vya maombi kuanza kwa upya; ‘Fellowship’ na kanisa kupata nguvu mpya, na watu kushuhudia kwa ujasiri na bila woga. Hii si kazi ya mtu, ni kazi ya Roho Mtakatifu aichunguzaye mioyo ya watu na kuijua ilivyo.


  2.   Watu wengi wanaokoka
  Watu wa Mungu wakipoa, hata watu wanaozaliwa upya mara ya pili wanakuwa wachache. Watu wa Mungu wakiamka upya kiroho, watu wengi wanaokoka. Ni wazi kwamba kunapotokea uamsho, mavuno ya roho za watu yanakuwa mengi – kwa kuwa watu wanapata msukomo mpya wa kushuhudia.
  Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo.
  Siku ya Pentekoste ilipotimia. Roho wa Uamsho aliwashukia wale wanafunzi wa kwanza wa Kristo, ambao walikuwa wamejaa hofu na wasiwasi; na baada ya kuwaamsha na kuwavika ujasiri walianza kumsifu Mungu kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.  
Uamsho huu katikati ya wanafunzi wa Kristo, ulileta mafadhaiko na mshangao kwa wale ambao hawakuwa wanafunzi wa Kristo. Imeandikwa: “Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa …. Wakashangaa wote ….” (Matendo ya Mitume 2:6,7).
  Na wakati ule ule Petro ambaye alikuwa amewahi kumkana Yesu Kristo mara tatu Roho Mtakatifu alimpa ujasiri wa kusimama na kuhubiri kwa nguvu habari za Yesu Kristo.
Mtu aliyeamshwa na Roho Mtakatifu akisema maneno yake huwa yamejaa moto ambao huwachoma wale ambao wanamsikiliza!
  “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo Yao, wakamwambia Petro na Mitume wengine, Tutendeje ndugu zetu? Petro akawaambia, tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina la Yesu   Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashu hudia Kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake (walioamua kuokoka) wakabatizwa na    siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu”  (Matendo ya Mitume 2:37 – 41).
  Kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu katikati ya watu wa Kristo, watu wengine ELFU TATU waliokoka kwa siku moja na kwa mahubiri ya mtu mmoja, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu!
  Na hawa waliookoka si kwamba walitubu na kutawanyika bali biblia inasema, “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu …… Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa” (Matendo ya Mitume 2:42 – 47).
3.  Uamsho unaleta Umoja
  Watu wa Mungu wakipoa kiroho, matengano, magomvi na mashindano hutokea katikati yao. Watu wa Mungu wakipoa kiroho, huwa wanapambana wao kwa wao badala ya kupambana na shetani.
  Watu wa Mungu wakipoa kiroho hata baraka za Mungu hazionekani katika makusanyiko yao, ndoa zao, na kazi zao. Wanakuwa ni watu wanaoishi kwa kujitahidi, na siyo kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
  Imeandikwa hivi:
“Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana (Wagalatia 5:25 – 26)
“Tazama jinsi ilivyo vema, na kupendeza ndugu wakae pamoja,   kwa  UMOJA.………….. maana ndiko Bwana ALIPOAMURU BARAKA, Naam uzima hata milele” (Zaburi 133:1-3).
  Hii ni habari njema kusikia ya kwamba BWANA AMEAMURU BARAKA ZAKE ZIENDE KWA WATU WANAOKAA PAMOJA NA KWA UMOJA!
  Ni kweli kwamba vitu vingi vinaweza kutukusanya pamoja, kama vile ndoa, harusi, misiba, mikutano, ibada, ugomvi, mashauri; nakadhalika. Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mnao umoja.  
Narudia tena: Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mnao umoja. Mnaweza kuwa pamoja katika ibada au harusi huku moyoni hampatani. Na hivi ndivyo ilivyo kwa watu wengi wa Kristo, wanakaa au wanakutana pamoja lakini hawana Umoja!
  Umoja wa kweli hauletwi na taratibu za kibinadamu hata kama ni nzuri sana. Zinaweza kutufanya tuwe pamoja, lakini haziwezi kutufanya tuwe na umoja. Umoja wa kweli huletwa na Roho Mtakatifu.
  Ndiyo maana Roho Mtakatifu akijidhihirisha kwa upya katikati ya watu wa Mungu huwa wanapatana na kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti ya madhehebu yao! Mipaka ya mapokeo ya kidhehebu, ya kikabila, ya kiutajiri, ya kimaskini, huwa inavunjika!
  Ndiyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Kristo wa kwanza walipohuishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

katika kitabu cha Mtendo ya Mitume 2:41 – 42 utaona jinsi wenzetu walivyoishi kwa Umoja.
  Imeandikwa:  “Nao waliolipokea Neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika USHIRIKA, na katika kuumega mkate, na katika KUSALI ……. Na wote  walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu  vyote SHIRIKA wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa MOYO MMOJA walidumu katika   hekalu, wakimega mkate NYUMBA KWA NYUMBA na kushiriki chakula chao kwa FURAHA na kwa MOYO MWEUPE, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa   WAKIOKOLEWA”.
  Kunapotokea uamsho, umoja wa kweli hutokea. Kulipo na uamsho wa Roho Mtakatifu, ushirikiano wa kweli hutokea. Kunapotokea uamsho, uchoyo unahama, ugomvi unahama, wivu unahama, uvivu unahama, na ubinafsi unahama. Na tabia ya uamsho ni kuleta umoja wa kweli – watu waliopoa kiroho wanaamka toka katika uchoyo, toka katika ugomvi, toka katika ubinafsi na wivu, na badala yake wanaanza kushirikiana, kusaidiana, kupendana na kusali pamoja katika Roho Mtakatifu.  
Wakristo wenzentu wa mwanzo ndivyo ilivyotokea kwao Roho Mtakatifu alipotawala maisha yao na uhusiano wao – tunasoma hivi:
“Na jamii ya watu waliamini (waliookoka) walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali WALIKUWA NA VITU VYOTE SHIRIKA. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu miongoni mwao mwenye MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile walivyouza, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadri ya alivyohitaji”  (Matendo ya Mitume 4:32 – 35)
  Hata hivi leo maisha ya namna hii yanatokea na ushirikiano wa namna hii unatokea ikiwa Roho Mtakatifu ataruhusiwa kuleta uamsho kwa utaratibu wa Mungu wenye kuleta baraka na siyo utaratibu wa kibinadamu au wa kishetani unaoleta laana.
  (Mwezi ujao tutaendelea kujibu maswali mengine juu ya Uamsho – usiache kututembelea katika ukurasa huu).














(Sehemu ya Pili)
Uamsho unapotokea mahali kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kunatokea upinzani. Katika mfululizo wa maswali na majibu mwezi uliopita, tuliona ya kuwa uamsho unapotokea mahali kunatokea mambo yafuatayo:
1.       Hofu ya Mungu
2.       Watu wengi wanaokoka
3.       Umoja unaimarishwa.
             Mwezi huu napenda tuangalie jambo la 4 la matokeo ya uamsho unapotokea mahali – nalo ni upinzani. Upinzani unaotokea kwa sababu ya uamsho una sehemu tatu kubwa:
1.       Upinzani dhidi ya watumishi wanaotumiwa na Mungu wakati wa  uamsho.
2.       Upinzani dhidi ya kazi ya Roho Mtakatifu katikati ya watu.
3.       Upinzani dhidi ya watu wanaokoka kwa sababu ya uamsho.
             Ni vizuri tufahamu na tukumbushane ya kuwa uamsho wa Mungu unaletwa na Roho Mtakatifu. Katika kambi ya watu wa Mungu kunapotokea uamsho - shetani naye huwa anaamsha watu wa kambi yake ili waendeshe upinzani juu ya uamsho wa Mungu.
            Kambi la watu wa Mungu likilala, si rahisi kuona upinzani wa mambo ya kiroho. Lakini kukitokea uamsho hata kama ni kwa mtu mmoja – ghafla anazungukwa na upinzani mkali – labda aaumue kujificha na kutojionyesha kwa watu kuwa amehuishwa na Roho Mtakatifu au ya kuwa ameokoka

            Upinzani dhidi ya uamsho ni jambo la kawaida. Wala huhitaji kushituka. Lakini jambo lisilo la kawaida ni kwa watu waliookoka kuamua ‘kupoa’ na kurudi nyuma kiroho kwa sababu ya upinzani.
            Pia ni budi kufahamu ya kuwa shetani ndiye mpinzani wa uamsho usitokee au unapotokea mahali. Shetani anaweza kupinga mwenyewe au kwa kuwatumia pepo wake au kwa kuwatumia binadamu katika maeneo mbalimbali, kwa mfano:
MFANO: 1.     Upinzani dhidi ya watumishi wanaotumiwa na Mungu wakati wa uamsho.
        Yesu Kristo alisema maneno haya na wanafunzi wake: ‘’Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo,kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu’’ (Mathayo 5:11,12)
Wanafunzi walipomuuliza dalili za siku za mwisho – kati ya mambo mengi aliyowaambia ya kuwa yatatokea ni pamoja na mambo haya yafuatayo: ‘’Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa, nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kuwa ushuhuda kwao’’ (Marko 13:9)
Yesu alijua upinzani mkali utatokea dhidi ya watumishi wake, na aliwaeleza mapema. Kwa hiyo tunapoona upinzani unatokea dhidi ya watumishi wa Kristo tusishangae, yaliandikwa ya kuwa yatatokea.
Kwenye Waebrania 11:36-38 inatueleza baadhi ya mambo yaliyowapata watumishi wa Mungu katika utumishi wao – imeandikwa hivi; ’wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga kwa misumeno, walijaribiwa, walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi’’.
             Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume utaona upinzani na mateso yaliyowapata Stefano, Paulo, Yakobo, Petro na watumishi wengine wa Mungu. hata leo hivi upinzani huu upo. Lakini tunapata neno la faraja katika I Petro 4:14 tukiambiwa hivi: ’mkilaumiwa kwa ajili ya njia ya Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia’’.
MFANO 2: Upinzani dhidi ya kazi ya Roho Mtakatifu katikati ya watu.

             Kati ya mambo yanayotokea Roho Mtakatifu anapokuwa kazini katika uamsho ni uponyaji wa miili ya watu. Lakini kazi hii ya Roho Mtakatifu huwa mara nyingi inapingwa na kupata upinzani mzito ili isiendelee. Jambo lililo wazi tunaposoma kwenye Biblia ni kwamba upinzani dhidi ya uponyaji unatokea zaidi katikati ya watu wa dini – hasa wanapoona ya kuwa uponyaji umeingilia taratibu za dini au ibada zao au ukiwa tofauti na mafundisho wanayofundisha.
Ukisoma Marko 3:1,2 utaona habari za Yesu zinasema hivi:
          "Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwapo huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki’’.
            Hawa Mafarisayo na Maherodi walikuwa watu wa ajabu - wakati wengine wanatamani kumwona Yesu akiponya ili Mungu atukuzwe na mgonjwa apone - wao walijali zaidi utaratibu wao wa Sabato. Wakamvizia Yesu ili wamshitaki, ikiwa atamponya yule aliyekuwa na mkono uliopooza. Yesu aliyajua mawazo yao na baada ya mahojiano nao – akamponya yule mgonjwa naye akapona! Lakini angalia upinzani ulioinuka.
           "Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi jinsi ya kumwangamiza’. (Marko 3:6). Kosa ambalo waliona Yesu alifanya sio katika kumponya mgonjwa bali kumponya mgonjwa siku ya Sabato ambapo dini yao ilikuwa inakataza.
             Ukisoma tena kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya 3 na 4 utaona upinzani uliotokea wakati Mungu alipomponya yule mtu aliyezaliwa kilema – kwa kumtumia Petro. Baada ya kuwafunga Petro na Yohana gerezani na halafu kuwahoji – mwisho kuhani Mkuu akishauriana na wenzake wakaamua kuipinga kazi hiyo isienee;
            "Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu’’ (Matendo ya Mitume 4:17,18).
             Baada ya kuambiwa hivi, Petro na Yohana hawakutishika wala kuyumba, bali wakajibu wakawaambia hivi; ‘’kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia’’ (Matendo ya Mitume 4:19,20)
            Je, umewahi kuona, kusikia au kukutana na upinzani wa jinsi hii unaolelekezwa katika kazi anayoifanya Roho wa uamsho katikati ya watu?
MFANO 3: Upinzani dhidi ya watu wanaookoka kwa sababu ya Uamsho
            Tuliona mwezi uliopita tulipokuwa tunaanza kujibu maswali juu ya uamsho ya kuwa mojawapo ya matokeo ya uamsho mahali ni watu wengi kuokoka!
Lakini sehemu nyingi watu wanapookoka wanapata upinzani mkubwa au kutoka kwa ndugu zao au kutoka kwa rafiki zao, au kutoka kwa watu wanaosali nao, au kutoka kwa watu aliokuwa akisali nao kabla ya kuokoka; au kutoka kwa viongozi wa serikali, au kutoka kwa viongozi wa kazini kwake.
            Kosa lake wanaloliona ni kwa sababu ameokoka-hilo tu. Je! kuokoka ni dhambi? Hebu soma habari hizi:“Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa  Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii (wale waliookoka), waume kwa wake awafunge na kuwaleta Yerusalemu’’(Matendo 9:1,2).
           Hawa watu walikuwa wanauawa, wanateswa na kufungwa kwa sababu wameokoka – hilo tu! Kwa sababu wameokoka! Hata hivi leo kuna waliookoka ambao wamezungukwa na upinzani kwa sababu tu wameokoka! Je! kuokoka ni dhambi? Je! kuokoka ni kosa?
            Lakini Yesu alijua ……..
            Pamoja na kwamba upinzani wa namna hii ulikuwepo na upo hata sasa – Yesu Kristo alijua ya kuwa utakuwepo na kwamba tutakumbana nao katika maisha haya.
            Katika mwezi ujao nitakufundisha kile ambacho Biblia inasema tufanye tunapokumbana na upinzani kama tulivyoona katika mwezi huu. Yesu alijua ya kuwa tutakutana na upinzani katika dunia hii kwa hiyo -usiogope!

UPINZANI UNAPOTOKEA KUPINGA UAMSHO NA WOKOVU,
BIBLIA INAKUSHAURI UFANYE NINI?
Katika majibu ya maswali yaliyopita tuliona ya kuwa Uamsho wa kweli ni kazi ya Roho Mtakatifu katikati ya Kanisa. Pia, tuliona yale yanayotokea Uamsho unapokuwepo mahali. Kitu kimoja-wapo kilicho dhahiri ni kwamba palipo na uamsho pana upinzani pia.
Mara nyingi upinzani unaotokea unakuwa katika maeneo ya kupinga uamsho, kupinga wokovu, kupinga mafundisho ya kweli, kupinga miujiza ya kweli ya Mungu inayotokea na pia, kuwapinga watumishi wa Mungu wanaotumiwa na Mungu katika uamsho.
Katika jibu la swali la mwezi huu ningependa nikuwekee mistari mbalimbali kutoka katika Biblia inayotushauri tuwe tunafanya nini unapotokea upinzani dhidi ya uamsho.
Ni vizuri kujua ya kuwa si kila mtu anakubaliana na mambo ya uamsho, pia si kila dhehebu la kikrsto linakubaliana na uamsho wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ni vizuri ujiandae na ujue cha kufanya unapokutana na upinzani.
Unaposongwa na upinzani Biblia inakushauri ufanye yafuatayo:
1.    FURAHI WALA USIKASIRIKE! (Mathayo 5:11,12; I Petro 4:12-16):
    "Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi, na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili (ya Yesu) yangu. Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu’’.
‘’Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo (au ikiwa kwa sababu ameokoka) asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo”.
2.    BARIKI WALA USILAANI! (Warumi 12:14; Luka 6:28, I kor 4:12,13)
    "Wabariki wanaowaudhi, barikini, wala msilaani pia, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi’’.
Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho jinsi wao walivyofanya anasema; “tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi’’.
            Na wewe fanya kama Mtume Paulo ukitukanwa kwa sababu ya kuokoka bariki, ukiudhiwa kwa sababu ya wokovu stahimili au vumilia, ukisingiziwa uongo, jifunze kujibu kwa hekima!
3.   TENDA WEMA USILIPIZE KISASI! (Warumi 12:17,18; Waebrania 12:14,15; Warumi 12:19-21; Luka 6:27
    "Msilipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo’’.
‘’Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu(mwachie Mungu jambo hilo linalokuletea hasira); maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema’’.
‘’lakini nawaambia ninyi mnaosikia wependeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi.’’
4.   WAOMBEE WANAOWAUDHI! Luka 6:28b; Mathayo 5:43-45, Mathayo 26:41)
    ‘’Waombeeni wale ambao wawaonea ninyi’’. ‘’Mmesikia kwamba menenwa, umpende jirani yako, na umchukie adui yako, lakini mimi (Yesu) awaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki’’.
    “ Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribu; roho ii radhi, lakini mwili ni  dhaifu’’.
5.   USIKATISHWE TAMAA ENDELEA KUFANYA ANALOKUAMBIA MUNGU KATIKA UTII NA HEKIMA! (Warumi 16:17-19)
    ‘’Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza (ya kweli); mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu. Maana utii wenu umewafikilia watu wote… lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya. Naye Mungu wa amani atamseta shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi’’.
6.   WASHIRIKISHE WATEULE WENZAKO WAKUOMBEE KATIKA UPINZANI UNAOKUZUNGUKA! (Warumi 15:30-32).
            Ndivyo Mtume Paulo alivyofanya alipowaandikia wateule wenzake aliposema;
‘’Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi’’.
            Yamkini Mungu atajibu maombi ya wateule hao wakiomba kwa imani na kwa bidii juu yako. Kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya 12 kinatueleza jinsi ambavyo Mtume Petro alipokumbwa na upinzani hata akafungwa-lakini (Kanisa) wenzake waliokoka waliomba kwa juhudi kwa ajili yake na Mungu akamfungua toka gerezani.

7.   JIEPUSHE NA MABISHANO! (Tito 3:9; Wakolosai 4:5)
            Mara nyingi upinzani wa wokovu na mambo ya uamsho unapotokea-kunatokea pia maswali na mabishano yasiyokuwa na msingi wala maana yoyote. Wengi bila kujua wamejikuta wameingia katika majibizano na mabishano juu ya wokovu na neno la Mungu. Biblia inasema hivi:
‘’Lakini maswali ya upuuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria (Neno la Mungu). Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana’’ enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu’’.
8.    USIKATE TAMAA, VUMILIA MPAKA MWISHO! (I Petro 3:13-17; Mathayo 24:13)
    ‘’Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu’’.
      Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya’’. ‘’lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka’’.
9.   USIONE HAYA- SONGA MBELE KATIKA WOKOVU (Waebrania 12:1-3; I Petro 4:15,16)
    ‘’Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu’’. ‘’Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni mkristo (au ameokoka) asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo’’.
10.   USIJIULIZE – ULIZE UTAKACHOJIBU! (Marko 13:9, 11)

   
‘’Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa;; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili (ya Yesu), kuwa ushuhuda kwao …. Na watakapowachukuwa ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakavyosema, lakini lolote mtakalopewa saa ile, lesemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu’’.
11.   MUWE NA KIASI NA KUKESHA! (I Petro 5:8-9; Yakobo 1:2-4; Yakobo 4:7; I Petro 5:10)
    ‘’Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka – zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani…’’ ‘’Ndugu zangu, hesabuni yakuwa ni furaha tupu, mkiangikia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi (uvumilivu). Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno’’. ‘’Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia’’.
    “ Na Mungu wa neema yote aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na  kuwatia nguvu’’





BIBLIA INAWASHAURI NINI VIONGOZI WA KANISA
WALIOKO MAHALI PALIPO NA UAMSHO?
 
            Tuliona katika mfululizo wa kujibu maswali miezi iliyopita ya kuwa uamsho unapotokea mahali fulani mambo yafuatayo hutokea:
 
1.   Hofu ya Mungu
2.   Watu wengi wanaokoka
3.   Umoja unaimarishwa
4.   Upinzani
 
            Viongozi wa Kanisa waliopo katika maeneo yaliyo na uamsho wana mtihani mkubwa wakati huo. Biblia ina mambo mengi ya kuwashauri yanayoweza kuwasaidia katika kuongoza makundi ya kondoo wa Mungu ambao wako chini yao. Biblia inashauri viongozi wa Kanisa uamsho unapotokea, mambo yafuatayo:
 
1.     WASIMZIMISHE ROHO BALI WAPIME MAMBO YOTE! (1Thesalonike 5:19 – 22; 1 Timotheo 4:1; 1Yohana 4:1)
            Kuna hatari ya kiongozi kukubaliana na kila kitu kinachosemwa na kinachotokea katikati ya uamsho. Pia, si vizuri kwa kiongozi kukataa na kupinga kila kitu kinachotokea katikati ya uamsho. Ndiyo maana Biblia inawashauri hivi viongozi:
             “Msimzimishe Roho; msitweze (msizuie) Unabii; jaribuni (pimeni) mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna”.
            Kila wakati unaposikia au kuona jambo likitokea katikati ya uamsho jiulize ikiwa liko sawa na neno la Mungu katika Biblia; Imeandikwa hivi; “wapenzi msiiamini kila roho, bali zijaribuni (zipimeni) hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” Pia “Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani”
 
            Uwe mwangalifu – Biblia haisemi mambo ambayo hayawezi kutokea – ndiyo maana inasema “zijaribuni hizo roho”
 
2.    MAMBO YOTE YAFANYIKE KWA UTARATIBU! (1Wakorintho 14:39,40,33)
            Uamsho si chanzo cha machafuko makanisani, bali ni makusudi ya Mungu kuwa uamsho ulete umoja zaidi kati ya watu wa Mungu.
            “Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu. Kwa maana Mungu si Mungu wa machufuko, bali wa amani, vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.”
 
3.     WASIKILIZE KILE ROHO MTAKATIFU ANACHOSEMA! (Waebrania 2:1 – 4; Ufunuo 2:29; Warumi 10:17)
             “Kwahiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo yaliyosikiwa tusije tukayakosa kwa maana, ikiwa lile Neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia?” (Waebrania 2:1)     
             “ Mungu naye akishuhudia pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.” Kwa hiyo “ Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.  (Ufunuo wa Yohana 2:29)
            Hii ina maana ya kuwa kiongozi inampasa kuwa mtu wa maombi sana, na mwenye kulisoma neno la Mungu, na kulijua, na kulitumia katika hekima yote, kwa sababu ‘kusikia huja kwa Neno la Kristo’.  (Warumi 10:17)
 
4.     WASIWE WATAZAMAJI TU, WALA WATAWALA TU KATIKA MAMBO YA UAMSHO, BALI WAWE WASHIRIKI NA VIONGOZI! (1Wakorintho 11:1; 1Timotheo 4:12b, 15, 16; Matendo ya Mitume 20:28 – 31)
            Ndiyo maana Mtume Paulo aliwaambia Wakristo waliokuwa Korintho hivi; “ Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo”
            Mtume Paulo alipomwandikia Timotheo alisema mambo haya ambayo yanaweza kukusaidia hata wewe katika nafasi uliyonayo ya uongozi
           
“Uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo, ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote, jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.”
            Mtume Paulo alipokuwa anawaaga wazee wa kanisa pale Efeso alisema maneno yanayoweza kuwa msaada mkubwa katika nafasi yako ya uongozi, aliposema
           “
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha Kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.“Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi”.
 
5.       MAMBO YOTE YATENDEKE KWA KUSUDI LA KUJENGA! (1Wakorintho 14:26)
            Si mpango wa Mungu ya kwamba Roho Mtakatifu anapoleta uamsho mahali – Kanisa limeguke na kuharibika, la hasha! Bali kusudi kubwa la uamsho ni kuliimarisha na kulijenga kanisa.
            Ndiyo sababu kiongozi katikati ya uamsho ni muhimu sana ayashike na kuyafuata maneno haya: “Basi, ndugu, imekuaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga”.
 
6.    WAJIFUNZE KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WENGINE WA KANISA! (Matendo ya Mitume 15:1 – 35)
             Biblia inatuambia wazi ya kuwa Paulo na Barnaba walikutana na Wayahudi waliookoka wakifundisha wakisema; “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.”
            Katika mashindano na mahojiano yaliyotokea ilibidi “Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande Yerusalemu kwa Mitume na wazee kwa habari ya swali hilo
            Ukiendelea kuisoma habari hii utaona jinsi tatizo hili lilivyotatuliwa. Ni muhimu hata sasa viongozi wa Kanisa kushauriana na viongozi wenzao kwa kadri Roho Mtakatifu atakavyowaongoza wanapokutana na mambo yanayowasumbua katika maombi ya uamsho.
            Lakini ni vizuri kufahamu ya kuwa ushauri mzuri ni ule unaosimama katika Neno la Kristo, na siyo katika mapokeo ya dini kama Wayahudi walivyokuwa wanafundisha kama tunavyosoma katika Kitabu cha matendo ya Mitume 15:1,2.
 
7.    WAWE WAOMBAJI! (Mathayo 26:40b, 41; Matendo ya Mitume 29:28 – 31)
           Yesu anasema hivi:
            “Je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? kesheni,  mwombe, msije mkaingia   majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”.
            Paulo anasema hivi: “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi   wawaandamie wao. Kwa hiyo, KESHENI  mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi”
 
8.    WAWE WA MASIMAMO! (Wagalatia 2:11 – 14)
            Petro alikuwa mwanafunzi wa Yesu kati ya wale wanafunzi wa kwanza, tena alikuwa kiongozi wa kiroho katika Kanisa lile la kwanza.
            Lakini ukisoma Wagalatia 2:11 – 14 utaona ya kuwa kuna wakati alionyesha hali ya kutokuwa na msimamo hasa mahali pale ambapo Wayahudi waliookoka walipokutana na wale waliookoka wasio Wayahudi. Mtume Paulo anaandika anasema; “Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu ….”.
            Ni vizuri viongozi popote palipo na Uamsho, wawe na msimamo unaokwenda sawa na Injili ya Kristo na Neno lake. Wasiwe na misimamo yenye lengo la kuwafurahisha wanadamu – isipokuwa wawe na misimamo ya kumfurahisha Mungu kwa kusimamia Neno la Mungu bila kuchanganya na mapokeo ya dini.

                                         (By mwl C. Mwakasege)