1Yohana 4:1 “Wapenzi,
msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa
sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.”
UTANGULIZI
Katika
kanisa la leo kuna roho ya mpinga Kristo ambayo inafanya kazi kwa kasi sana,
roho hii inafanya kazi ndani ya wakristo kuliko inavyofanya kazi kwa watu wa
mataifa (wasio Wakristo). Hali hii imefanya Wakristo wengi kukosa imani na
wahubiri (mitume, manabii, waalimu, wachungaji na wainjilisti) kutokana na aina
za mahubiri yanayofundishwa, vilevile imesababisha Wakristo wengi kuzusha
(Kuongea mambo ya uongo yasiyokuwepo kana kwamba yapo) na kwasababu hiyo uzushi
mwingi umezuka ndani ya kanisa la Mungu na kuwasema vibaya watumishi wa Mungu.
Hali hii ni mbaya sana kwani makuhani wa Mungu wameumizwa na maneno yasiyofaa
na Wakristo wamejiingiza katika laana pasipo kujua kwakuwa Neno la Mungu
linasema katika 1Nyakati 16:21-22 “21 Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme
aliwakemea kwa ajili yao; 22 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru
nabii zangu.” na Zaburi 105:14-15
“14 Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme
aliwakemea kwa ajili yao. 15 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru
nabii zangu.”
Unapofanya
jambo lolote kinyume na maelekezo ya Mungu huo ni uasi na katika uasi kuna
adhabu, hivyo usitegemee jambo zuri unapokuwa unasema uzushi juu ya watumishi
wa Mungu kwani wewe hujui ni gharama gani Mungu ametumia kuwakuza kufikia hapo
walipo sasa. Hata kama unaona wamekengeuka ni bora ukafanya kama Daudi
alivyokataa kumhukumu (Kumuua) Sauli pamoja na kwamba alikuwa na uwezo wa
kufanya hivyo, sababu kubwa ilimzuia Daudi asimuue Sauli ni kwakuwa Sauli
alipakwa mafuta na BWANA na Daudi alilifahamu Neno “…….Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.” Hivyo
hakumdhuru Sauli japokuwa Sauli alikwisha kataliwa na BWANA.
Kwanini
nimeanza na utangulizi mrefu hivyo? Ni kwasababu Wakristo wa leo wako tayari
kwenda kwa waganga wa kienyeji na wakifika huko hutumia gharama kubwa bila
kupona matatizo yao, lakini hata kama hawaponi huwezi kuwasikia Wakristo hao
wakimsema mganga wa kienyeji kuwa ni muongo na mambo anayofanya hayafai. Sasa
umkute mkristo huyo amejua jambo baya/ovu kuhusu mtumishi wa Mungu, yaani
atazisambaza habari hizo kila atakapoweza kuzifikisha zitafika. Wakati mwingine
hata hajashuhudia isipokuwa amesikia kuwa mtu wa Mungu amefanya uovu, basi mtu
huyu atasimama na kulihubiri lile jambo baya kwa nguvu zote; hawa ndio huitwa
watu wasiofaa ambao wako tayari kusema lolote baya ili injili ya Kristo
isihubiriwe. Watu wa namna hii walikuwepo kuanzia agano la kale na hata wakati
wa Yesu wanaonekana wakisema uongo ili kumzuia Yesu kuhubiri habari za wokovu.
Tazama
habari za mfalme Ahabu, mkewe Yezebel na Nabothi katika 1Wafalme 21:1-16 “……8 Basi,
akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile
nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa
pamoja na Nabothi. 9 Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya
watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, 10 mkainue watu wawili, watu
wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme.
Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.”……….. 13 Na
hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu
wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana
Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa……….”
Nataka
nikuoneshe kwamba kuna watu wasiofaa wanaoweza kuzusha maneno ya uongo ambayo
hayana ukweli na wakatoa ushahidi wa uongo na mwisho kupotosha ukweli wote.
Vievile tunasoma katika Mathayo 26: 3-4
“3 Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee
wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; 4 wakafanya
shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.”. Tunaona viongozi wa
dini wa wakati huo walifanya hila ili kumkamata Yesu, yaani waliandaa uzushi tu
ili kumkamata Yesu kama unavyofahamu walizusha mashataka mengi ya uongo juu ya
Masihi wa BWANA.
Nimeanza
na utangulizi huu ili unaposoma somo hili ujue kwamba manabii wa uongo na
wapinga Kristo wapo kwa pande mbili, yaani wale wanaosimama madhabahuni na wale
washirika/waumini wanaozusha uongo ili kuizuia injili ya Yesu isisonge mbele.
NI KWELI WAPO WANAOMPINGA KRISTO?
Ni
kweli kabisa wapo watu ambao ndani yao kuna roho zinaofanya kazi maalum ya kupinga
ukristo usikue, yaani wanaudhoofisha ukristo usifike kwa wale waliokusudiwa na
hata kama ikiwafikia iwe imepotoshwa au kuifanya mioyo ya watu kuwa migumu
kiasi cha kushindwa kulipokea Neno la Kristo watu hawa hujiingiza kwa siri ili
kuliharibu kusudi la Mungu katikati ya watu wake sawa na Neno la Mungu kutoka Yuda 1:3-4, 12-13 “3 Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya
wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye
kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. 4 Kwa maana
kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii,
makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye
peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo…..12 Watu hawa ni miamba yenye hatari
katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo
hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika,
isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; 13 ni mawimbi ya
bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo,
ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.”.
Wapinga
Kristo hawa nimewagawanya katika makundi haya yafuatayo:-
Ø Manabii wa uongo
Wapo
manabii ambao ni wa uongo, hao hunena yakwao na kuwaambia watu kuwa BWANA
amesema ile hali sio BWANA aliyesema ila wamesema wenyewe kwa tamaa zao wenyewe,
Yesu anasema katika Mathayo 7:15 “15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu
wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.”
Hivyo ni kweli wapo manabii wa uongo na kwa muonekano ni kama wanamuhubiri
Kristo lakini kiuhalisia wanayo makusudi tofauti na kumhubiri Kristo. Hii ni
hatari kwa wakristo hasa kanisa la Mungu, ndio maana Yohana anaonya katika moja
ya nyaraka zake, 1Yohana 4:1 “Wapenzi,
msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa
sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” Ndio
maana hata mimi leo nakuambia usiamini kila roho, ukisikia hili neon “USIAMINI
KILA ROHO” tafadhali kuwa makini kwani haimaanishi kuwa roho ya nabii itakuja
na kukusemesha nje ya mwili, Hapana! Maana yake ni kwamba roho hizi hukaa ndani
ya mwili/miili ya watu/wanadamu kisha kuwahubiria watu wa Mungu kwa nia ya kuwapotosha.
Ø Roho zidanganyazo
Wengi
wetu tayari tunafahamu kwamba moja ya kazi zilizo kuu kabisa za ibilisi ni
kudanganya. Yeye anaitwa baba wa uongo, kazi yake kubwa ni kuudanganya
ulimwengu wote. (Ufunuo 12:9 “Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa
pamoja naye.”). vilevile Yesu mwenyewe anamtaja shetani kama baba wa uongo
katika Injili ya Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za
baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala
hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna
hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa
sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Zipo roho zinazodanganya kabisa na
kusema uongo kwa habari ya Kristo Yesu, lengo ni kuwapa watu mafundisho
yasiyofaa na kuwaaminisha kuwa ndio mafundisho ya kweli ili kulipotosha lile
kusudi la Mungu ambaye ndiye KWELI. Na kwasababu hiyo Roho Mtakatifu
anatufunulia wazi kuwa zipo roho zidanganyazo ndani ya kanisa la Mungu 1Timotheo 4:1 “1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine
watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya
mashetani;”
Ø Wapinga Kristo katika watu wa Mungu
Wapo
watu ambao ni wanamaombi wenzetu na tunaabudu nao katika faragha (Fellowship),
lakini watu hawa hawaamini katika matendo ya Roho Mtakatifu na hivyo kushindana
na kazi za Mungu zinazofanywa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; watu hawa utawasikia
wakisema kuwa anayetenda hayo matendo sio Mungu (Labda kwasababu ya wivu wa
kihuduma unaoletwa na ibilisi) na kuleta mafarakano na kutoelewana katikati ya
watoto wa Mungu. Tunasoma kuwa roho hii ilianza kupambana na Yesu mwenyewe pale
alipoanza kuwafungua watu waliosetwa Marko
3:22 “Nao waandishi walioshuka kutoka
Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.”
Kumbe upinzani haujaanza leo, ndio maana mtume Yohana anasema katika waraka wake
1Yohana 2:18-19 “18 Watoto, ni wakati wa
mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga
Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa
mwisho. 19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa
kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote
walio wa kwetu.”. anachosema Yohana hapa ni hiki, watu hawa (wenye roho ya
mpinga Kristo) wanatoka katikati yetu.
Ø Walimu wa uongo
Neno la
Mungu linatuthibitishia uwepo wa waalimu wa uongo katika kipindi cha
mitume na pia Neno linatuthibitishia kuwa hata sasa hao walimu wa uongo wapo! 2Petro 2:1“Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu
kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza,
wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.” Hawa
ni wale wanotoa mafundisho ya uongo, yapo mafundisho mengi sana ya uongo; wapo
wanaosema Yesu hakufufuka, wengine wanasema sio Mungu, wapo wasemao hakuna
ulimwengu wa roho na hakuna ufufuo wa wafu n.k. Vilevile tunasoma katika 2Thesalonike 2:1-4 “1 Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu
Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, 2 kwamba msifadhaishwe upesi hata
kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka
unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. 3 Mtu
awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule
ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; 4 yule mpingamizi,
ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye
mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba
yeye ndiye Mungu.” Hivyo tuwe wasomaji wa Neno la Mungu ili tuijue kweli
tusipotoshwe na mambo ya ulimwengu huu.
UNABII WA UONGO UNALETWA NA NANI?
Unabii
wa uongo/roho ya mpinga Kristo inaletwa na shetani mwenyewe kwakuwa yeye ndiye
baba wa mafarakano na kazi yake ni kuhakikisha anaharibu kwa kutumia njia
zozote, ndio maana Yesu anasema katika Injili
ya Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba
yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa
mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo
uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”
Vilevile tunasoma kuwa kazi ya shetani (mwizi) ni uharibifu Yohana 10:10 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na
uzima, kisha wawe nao tele.”
Hebu
tuutazame mfano mmoja wa jinsi shetani anavyoweza kuleta unabii wa uongo wakati
watu wakidhani kuwa ni Mungu kasema. 1Wafalme
22:20-23 “20 Bwana akasema, Ni nani
atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema
hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi
nitamdanganya. 22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa
pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na
kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. 23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa
uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.”
Hapa tunajifunza kuwa nguvu za giza zinaweza kugeuka kuwa kitu chochote
kwamfano huyu pepo hakuwa pepo wa uongo ila alisema atageuka kuwa pepo wa uongo
“……Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa
uongo kinywani mwa manabii wake wote…….” Hii ndio hali ya kanisa la sasa,
mtu yoyote hata mchungaji/mwinjilisti/padre/n.k anaweza kuingiwa na roho (akawa
nabii wa uongo/mpinga Kristo).
UTAWATAMBUAJE MANABII WA UONGO?
Namna
kuu ya kuwatambua manabii wa uongo ni kwa kutumia Neno la Mungu ambalo lipo
ndani yetu; nasema “NENO LA MUNGU AMBALO
LIPO NDANI YETU”na sio Neno la Mungu lililoandikwa katika kitabu kitakatifu
yaani Biblia, kwakuwa wakati unapokutana na mafundisho ya uongo/udanganyifu
kutoka kwa manabii wa uongo unapaswa kupima kwa kutumia Neno lililopo ndani
yako; ndio maana Biblia inasema katika Wakolosai
3:16 “16 Neno la Kristo na likae kwa
wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na
nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”
Vilevile
wakati unakabiliana na manabii wa uongo pamoja na mafundisho ya uongo (nguvu za
giza), Neno la Mungu lililopo ndani yako linageuka na kuwa taa ya kumulika ili
kukuonesha ni wapi uendako sawasawa na linavyosema Neno la Mungu katika Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”
Zaidi
sana Neno la Mungu likiwa ndani yetu
linaishi na linatenda mambo makuu ikiwa ni pamoja na kuijua nia ya mtu yeyote
iliyo mbaya, hivyo Neno la Mungu lililopo ndani yetu linatuambia yupi ni nabii
wa kweli na yupi ni wa uongo kwani linakuwa ni mizani ya kupimia unabii wowote,
ukisoma Waebrania 4:12-13 “12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina
nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata
kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li
jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa
wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye
aliye na mambo yetu.”
Maelezo
machache ya kutumia Neno la Mungu kuwatambua manabii wa uongo
i.
Msikilize mtumishi (nabii/mwalimu/….) anasema
nini kuhusu Yesu, katika Mathayo 16:15-16 “15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? 16 Simoni Petro
akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Tunaona hapa
Petro anamkiri Yesu kuwa ni Kristo mwana wa Mungu aliye hai, ukimkuta mtumishi
hawezi kumkiri Yesu kuwa ni Kristo na mwana wa Mungu aliye hai basi huyo ni
nabii wa uongo, Neno la Mungu linasema katika 2 Yohana 1:9-10 “9 Kila
apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye
adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. 10 Mtu akija kwenu,
naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.”
Mafundisho hayo ni yapi ambayo Yohana anasisitiza kuwa watu wanaofundisha
wasikaribishwe? Ukisoma 1Yohana 2:22-23
“22 Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye
ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana.
23 Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.” Yoyote
amkanaye Yesu Kuwa ni Kristo huyo ndiye
mpinga Kristo na ndio zile roho zidanganyazo
watu wa Mungu na kuleta mafarakano katika kanisa la Mungu.
ii.
Je! Huyo mwalimu anamiliki tabia ambazo zinamtukuza
Mungu? Anaonya juu ya walimu wa uongo kama vile tunavyosoma katika Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa
la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya
Kora.” Kwa njia nyingine, mwalimu wa uongo anaweza kujulikana kwa kiburi
chake (Kaini aliukataa mpango wa Mungu), tamaa (Balaamu anatabiri kwa ujira),
na maasi (Kora anajinua zaidi ya Musa). Yesu alisema tuwe macho na watu kama hao
na kwamba tutawajua kwa matunda yao (Mathayo 7:15-20).
Kama
nilivyoanza hapo awali, sio lengo la mafundisho haya kukufanya usiamini manabii
wa Mungu aliye hai ila ni kukupa ufahamu ili uweze kujitambua na kutambua kuwa
hizi ni nyakati za mwisho na sehemu kubwa ya unabii ulionenwa na Manabii na
Mitume imekwishatimia, kama tunavyosoma katika 1Wathesalonike 5:16-22 “16
Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo; maana
hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. 19 Msimzimishe Roho; 20
msitweze unabii; 21 jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; 22 jitengeni na
ubaya wa kila namna.” Maana yake ni kwamba, kwa nguvu ya Neno la Mungu
tunaweza kuupima unabii na manabii wa namna zote na kujiridhisha kama
wametokana na Mungu au la!.