Bwana Yesu apewe sifa kanisa la Yesu!
Napenda ufahamu kwamba yapo mambo mengi sana ambayo
ukiyafanya (kwa kujua au kutojua) unaunganishwa na madhabahu za mashetani;
inawezekana kwamba matatizo ya maisha yako huenda yameanza kutokana na kufanya
au kufanyiwa moja ya mambo hayo katika maisha yako.
Mimi binafsi kutokana na huduma nilizozifanya
na kwa kujifunza kutoka kwa watumishi wengine nimepata ufahamu wa mambo kadha
wa kadha na baadhi ya hayo nimeyaandika katika somo hili. Nakusihi mtu wa Mungu
kwamba pamoja na haya niliyoandika bado jambo muhimu na kubwa la kujiweka
salama ni kumtegemea Yesu kwa uaminifu na kuishi maisha matakatifu
yanayompendeza Mungu (Waebrania 12:14
“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu
wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”)
Nimeanza kwa kusisitiza habari ya utakatifu
kwani kuna watu wanataka kumuona mungu na kuzipata Baraka zake lakini hawamtaki
Mungu wala hawataki kuishi kwa kufuata sheria za Mungu na kuzishika amri zake;
yaani watu hawa wanaishi maisha ya kidunia/kimwili halafu wanataka kuvuna
Baraka za Mungu na kufunguliwa kutoka katika vifungo (Efeso 5:19-21)
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo
ukiyafanya unaunganishwa na madhabahu za uharibifu/za mashetani na madhara
yatatokea mahali Fulani katika maisha yako.
Kutoa sadaka na kufanya matambiko kwa miungu
(mizimu) ni moja ya njia ambayo humuunganisha mtu na madhabahu za uharibifu kwa
kujua au bila kujua. Kuna watu ambao huenda kwenye koo au familia zao na
kuchinja wanyama mbalimbali ili kutoa damu ya wanyama hao kwa mababu na baada
ya hapo mnyama aliyechinjwa huliwa kwa utaratibu maalum; kwa mfano nyama ya
kidari atakula baba mkubwa, nyamba ya paja atakula mtoto wa kwanza wa kiume na
nyama ya kichwa atakula mtoto wa kwanza wa kike. Unapokuwa umeshiriki kwa kujua
au bila kujua katika matambiko kama hayo unaunganishwa na ile madhabahu ambayo
sadaka ya matambiko imetolewa. Kwa jinsi hii watu wengi sana walioshiriki
katika matambiko wana mahusuiano na zile madhabahu zilizotolewa matambiko.
1Wafalme
11:1-8
“1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake
wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni,
na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, 2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia
wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika
wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa
kuwapenda. 3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao
wakeze wakamgeuza moyo. 4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate
miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake,
kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa
Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la
Waamoni. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala
hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. 7 Sulemani akamjengea
Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu,
na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake
zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.”
1Falme
21:25-26
“25 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu,
aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. 26
Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori,
Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”
1Falme
16:31-33
“31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu
kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali,
mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia
Baali, akamsujudia. 32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali,
aliyoijenga huko Samaria. 33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi
kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli
waliomtangulia.”
Mfalme Sulemani na mfalme Ahabu wote walio
wanawake kutoka kwenye familia za waabudu miungu, na kama unavyofahamu kwamba
hawakuiacha miungu yao bali walikuja nayo kwa Ahabu na kwa Sulemani na hivyo
walifanya matambiko (ibada za miungu) ndani ya nyumba za waume zao (Ahabu na
Sulemani) na waume zao walishiriki (kwa
kujua au bila kujua) na kilichofuata ni wafalme hawa (Ahabu na Sulemani)
kuunganishwa na miungu na madhabahu za mashetani na wao kumuacha Jehova na
hasira za Jehova zikawaka juu yao na familia zao.
Inawezekana hata wewe nyumbani kwako kuna
matatizo ya kiroho na haujui ni kwanini unapatwa na matatizo hayo, kumbe ni
mume/mke wako au mtumishi wako (House girl/House boy) amekuja na miungu ya
kwako nyumbani kwako na umeunganishwa na madhabahu za mashetani.
MAOMBI:
Baba katika
jina la Yesu Kristo, naomba toba kwa kuwa nimeshiriki kwa kujua na bila kujua
na nikatoa sadaka na matambiko kwenye madhanahu za mashetani, ninaomba rehema
Baba Yangu kwa jina la Yesu kwakuwa wakati mwingine nilitoa mali yangu nikijua
masaidia watu kumbe walinuia mabaya ili wanitenganishe na wewe wakaenda kutoa
mali na fedha zangu kwa mashetani, nirehemu Baba kwaajili yake Yesu Kristo.
Katika jina la Yesu naamuru mahali popote sadaka yangu ilipo kwenye madhabahu
za mashetani ibadilike kuwa moto wa Roho Mtakatifu na kuwateketeza makuhani
wote wa kichawi kwa jina la Yesu Kristo, naiondoa sadaka yangu niliyoitoa kwa
miungu kwa kujua au bila kujua kwa jina la Yesu! Amen!
Unaposhiriki au unaposhirikishwa kwenye mambo
ya kiganga kwa kujua au bila kujua unaunganishwa na madhabahu za mashetani na
hasira ya Mungu inakuwa juu yako hata kama haukufanya kwa ufahamu wako. Inawezekana
huo uganga ameshiriki baba/babu/dada/kaka yako na wewe bila kujua amekutaja
kwenye hiyo madhabahu, basi unakuwa mshirika na mateso yanayoletwa na hiyo
madhabahu yanakuwa juu yako pia.
Hali kama hii iliwahi kumtokea Gideoni pale
ambapo baba yake mzazi (mzee Yoashi) alipokuwa kuhani wa madhabahu ya baali;
Gideoni hakuwa akishiriki katika ile madhabahu lakini kwakuwa baba yake
alishiriki basi na yeye Gideoni akabeba adhabu ya kuwa mshiriki
Waamuzi
6:11-15, 25-26 “11 Malaika wa Bwana
akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake
Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya
shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea,
akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana
wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi
matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana,
aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono
ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe
Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana,
nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana
katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu………..
25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba
yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali,
aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee
Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule
ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera
uliyoikata.”
Kwahiyo tunajifunza kwamba hali ile ya uduni
wa Gideoni na umasikini wake na kabila lake ulitokana na madhabahu ya baali
ambayo BWANA alimuamuru kuivunja na kujenga madhabahu ya BWANA. Inawezekana
hata wewe umeunganishwa na madhabhu za mashetani lakini pasipo kufahamu.
Vilevile tunasoma habari ya mfalme wa Babeli
aliwaunganisha wananchi wa nchi yake na madhabahu za mashetani kwa kufanya
uganga na matambiko kama ilivyoandikwa katika Neno la Mungu.
Ezekieli
21:21-23
“21 Maana mfalme wa Babeli alisimama
penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga;
aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. 22
Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya
kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele
sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga
ngome. 23 Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao
waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.”
Tunaona hasira ya Mungu inaachiliwa juu ya
wote ambao mfalme amewaapia viapo hata kama hawakushiriki hicho kiapo kwa
uhiari/ufahamu wao. Hebu tafakari mtu wa Mungu; ikiwa kiongozi Fulani katika
nchi ya Tanzania alifanya uganga na kututaja wa Tanzania, hivi tuko salama?
Ikiwa mkuu wa ukoo au familia yenu alikutaja kwenye uganga, kweli uko salama.
Inawezekana hata sasa umeunganishwa na madhabahu za mashetani kwa njia hiyo;
omba maombi haya ujinasue:
MAOMBI:
Baba yangu
katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba kwakuwa nimeshiriki katika ibada za
kiganga kwa kujua au bila kujua, wakati mwingine ndugu na jamaa wametaja jina
langu kwenye madhabahu za mashetani na mimi nikaunganishwa na roho za
mashetani, ninaomba toba Kwa Damu ya Yesu na kwa Jina la Yesu Kristo. Ninajitoa
sasa kwenye madhabahu za waganga zilizopo makaburini, baharini, misituni, njia
panda, angani na kwenye nyumba za wachawi. Natoka kwenye hizo madhabahu kwa
jina la Yesu Kristo. Nauwasha moto wa Roho Mtakatifu nawateketeza mashetani
yote walionishikilia kwenye madhabahu kwa jina la Yesu! Naitoa nchi yangu
Tanzania kwenye madhabahu za mashetani kwa damu ya Yesu! na kwa jina la Yesu!
Amen!
- Majina yenye uhusiano na madhabahu yanaweza kukuunganisha na madhabahu
Ili Yusufu aweze kuwa mtawala wa misri
alipewa jina la kimisri ili apokelewe na miungu ya Misri, yaani jina lina nguvu
ya kumuunganisha mtu na madhabhu na kumpa nguvu ya ile madhabahu.Yusufu
asingetawala Misri pasipo kupatanishwa na madhabahu za wa-Misri na hilo
lilifanyika kwa njia ya kupewa jina lenye nguvu ya madhabahu za miungu ya Misri
(Kumbuka wa-Misri ni waabudu miungu na hawakumjua Mungu wa kweli)
Mwanzo
41:42-45
“42 Farao akavua pete yake ya muhuri
mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na
kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43 Akampandisha katika gari lake la
pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo
akamweka juu ya nchi yote ya Misri. 44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao,
na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. 45
Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera,
kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya
Misri.”
Wote waliomkubali Yesu na kulibeba jina la
Yesu kwa imani ndani ya mioyo yao, wamepokea nafasi katika ulimwengu wa roho na
kuunganishwa na madhabu ya Mungu Jehova
Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”
Warumi
8:16-17
“16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na
roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu
warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja
naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Wafilipi
2:8-10
“8 tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 9 Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya
duniani, na vya chini ya nchi;”
Jina la Yesu ni jina la urithi ambalo amepewa
na Baba yake (Mungu Baba), lakini alipolipokea hilo jina tu akapewa kiti cha
enzi cha Mungu na mamlaka kubwa kuanzia mbinguni mpaka duniani na kwa jina hilo
viumbe vyote vinaanguka na kusujudu.
Jina linaweza kukunganisha na madhabahu na
ukapokea nguvu ya hiyo madhabahu, inategemea umeunganishwa na madhabahu gani.
MAOMBI:
Bwana Yesu
ninaomba toba kwaajili ya majina niliyopewa yenye mahusiano na madhabahu za
mashetani, naomba toba kwaajili yangu na watoto wangu, wazazi wangu, mabibi na
mababu…… turehemu Bwana kwa jina la Yesu. Ninalidumbukiza na kulizamisha jina
langu kwenye kisima cha damu ya Yesu kwa jina la yesu Kristo. Ninaamuru mapepo
yaliyokamata jina langu na kulivuta kwenye uharibifu Achiaaaa kwa jina la Yesu
Kristo!!! Achiaaaa jina langu kwa jina la Yesu Kristo!!! Achiaaaa kwa jina la
Yesu Kristo!!! Amen!
- Mavazi yenye mfumo wa madhabahu au nembo za madhabahu yanaweza kukuunganisha na madhabahu
Yapo mavazi yenye mfumo wa kimadhabahu na
hata yametambulika katika jamii kama mavazi kwaajili ya watu fulani au kabila fulani
au dini fulani. Kuna mavazi ukiyaona tu unaanza kuhisi kwamba huyu aliyevaa
anaweza kuwa mganga wa kienyeji au mchawi. Mavazi ya namna hii yana nguvu za
madhabahu na yanaweza kukuunganisha na madhabhu za giza.
Katika Biblia tunajifunza habari za nabii
Eliya kwamba alikuwa na mavazi ambayo hayakufanana na watu wengine (2Falme 1:7-8 “7 Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia
maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? 8 Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la
manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule
Eliya Mtishbi.”)
Ulipofika wakati wa kunyakuliwa kwa Eliya
tunaona Elisha anabaki na vazi la Eliya na ule upako uliokuwa kwa Eliya unakuja
kwa Elisha mara dufu.
2Falme 2:11-15 “11 Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea,
tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili;
naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. 12 Naye Elisha akaona,
akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake!
Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
13 Kisha akaliokota lile vazi la Eliya
lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. 14 Akalitwaa
lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana,
Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha
akavuka. 15 Na hao wana wa manabii,
waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu
ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”
Katika Biblia tunajifunza pia kwa habari ya
mavazi tangu enzi za Musa na Haruni ambapo yalitengenezwa mavazi ambayo
walipovaa Haruni na watoto wake walitakasika na kuweza kusogea mbele za Mungu
kwaajili ya wana wa Israeli.
Kutoka 28:2,41 “2 Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi
matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri., 41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na
wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na
kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.”
Unachotakiwa hapa ni kuwa makini na mavazi
unayovaa, sio ukiletewa nguo yoyote wewe unaivaa tuu, unaweza kuvaa nguo
zilizotoka kwa mashetani ukaingizwa katika uharibifu wa madhabahu za mashetani.
MAOMBI:
Baba katika
jina la Yesu Kristo, ninaomba toba na msamaha mahali popote nilipojiunganisha
na mashetani kwa njia ya mavazi iwe ni rohoni au mwili, nirehemu baba yangu
kwaajili ya mwana wako mpendwa Yesu Kristo. Kwa moto wa Roho Mtakatifu
ninayateketeza mavazi yote ya kimadhabahu niliyovishwa nikiwa rohoni au mwilini,
enyi mapepo mliokuja na mavazi hayo ninawateketeza kwa moto wa Roho Mtakatifu
kwa jina la Yesu!!! Amen!
- Kutumia ishara na alama za madhabahu za giza (Chale, Hirizi, alama na ishara zinaweza kuita roho za giza)
Kuna ishara ambazo zinazoonekana kwa jinsi ya
mwilini lakini zina maana kubwa sana katika ulimwengu wa roho, ishara hizo
zinapofanyika zinakuunganisha na madhabahu inayohusiana na ishara hiyo. Katika
agano la kale kuna ishara kadhaa zilifanyika na zilikuwa na maana kubwa katika ulimwengu wa roho.
Kutahiriwa katika agano la kale ilikuwa ni
ishara ya agano la Mungu na wana wa Israeli, ilionekana kama tendo la kibindamu
lakini ilikuwa ni ibada ya utakaso na mtu ambaye hakutahiriwa alitengwa na
kuonekana kama mtu najisi (mchafu). Katika agano jipya tohara ni kumpokea Yesu
kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kama haujampokea Yesu ni sawa na mtu
asiyetahiriwa yaani upo nje ya agano (ni najisi/mchafu).
Mwanzo
17:10-11, 14 “10 Hili ndilo agano langu
utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume
wa kwenu atatahiriwa. 11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi…..14
Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa
na watu wake; amelivunja agano langu.”
Vilevile tunaona ishara ya damu ambayo kila
aliyepaka damu kwenye miimo ya mlango wake yule muharibu hakuweza kuingia
katika nyumba yake.
Kutoka
12:12-13
“12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri
usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa
mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi
ndimi Bwana. 13 Na ile damu itakuwa
ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu,
nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya
Misri.”
Ubatizo nalo ni tendo la ishara ambalo
hufanyika kwa jinsi ya mwili lakini matokeo yake yapo rohoni na kuleta
mabadiliko ya rohoni
Marko1:4 “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na
kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.”
Zipo ishara nyingi ambazo zimewaunganisha
wakristo na madhabhu za giza pasipo wao kujua na madhara yameanza kutokea
katika maisha yao lakini hawajui chanzo. Kumbe chanzo ni yale
mafuta/maji/chimvi uliyopaka kwa nabii wa uongo (vipo vitu kama hivyo vyenye nguvu za Mungu). Wapo watu wamevaa
nguo zenye ishara mbalimbali za mashetani na wanashambuliwa na nguvu za giza
lakini hawakijui chanzo cha matatizo yao.
MAOMBI:
Katika Jina
la Yesu Kristo, kila mahali penye ishara ya kishetani katika mwili wangu, nina
mimina damu ya Yesu Kristo naondoa uhalali wa ishara na alama hiyo katika
maisha yangu. Mahali ilipowekwa hilo alama na ishara napitisha Damu ya Yesu na
Moto wa Roho Mtakatifu naziteketeza kabisa hizo alama na ishara kwa jina la
Yesu. Naamuru mapepo yanayolinda hizo ishara za kishetani Toooka!!! Kwa Jina la
Yesu Kristo!!!! Toooka!!! Kwa Jina la Yesu Kristo!!!! Toooka!!! Kwa Jina la
Yesu Kristo!!!!
- Vitu vilivyo vuviwa kwa makusudi ya madhabahu za giza na vifaa vilivyowahi kutumika kwenye madhabahu za giza (Pete, Shanga, Hereni, michezo ya kipepo)
Katika ulimwengu wa roho sahau sayansi ya
viumbe hai na visivyo hai kwani rohoni vitu vyote vinatumika (watumishi) ama na
Mungu Jehova au na shetani ambaye naye ni mungu wa dunia hii.
Zaburi
119:91
“Kwa hukumu zako vimesimama imara hata
leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.”
Lakini pamoja na ukweli kwamba vitu vyote ni
watumishi wa Mungu, Neno la Mungu linatupeleka mbali zaidi kwamba vitu hivyo
vimetiishwa katika ubatili, yaani vinatumika nje ya mpango wa Mungu
Rumi 8:19-22 “19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia
kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. 20 Kwa maana viumbe vyote pia
vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye
atiyevitiisha katika tumaini; 21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru
na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa
watoto wa Mungu. 22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja,
navyo vina utungu pamoja hata sasa.”
MAOMBI:
Katika jina
la Yesu naachilia damu ya Yesu kwenye kitu chochote nilichovaa au kuvalishwa na
mashetani kupitia waganga au ndugu wa karibu, namimina damu ya Yesu naharibu
nguvu ya giza kwa jina la Yesu. Naachilia moto wa Roho Mtakatifu uteketeze kila
nguvu ya giza iliyopo kweye pete za kishetani, shanga, bangili, mikufu,
manukato, viatu, nguo za ndani n.k. naachilia Motooo!!! kwa Jina la Yesu
Kristo!!! Motooo!!! kwa Jina la Yesu Kristo!!! Motooo!!! kwa Jina la Yesu
Kristo!!!
- Kutumia vyakula/vinywaji vilivyonuiziwa kwa matumizi ya kimadhabahu na kufanyiwa ibada za tambiko linalikuunganisha na madhabahu.
Mtu wa Mungu sio kila unachokiona kinafanana
na chakula basi unakula tu, vipo vya kula vya kiibada ambavyo ndani yake
vimebeba roho za uharibifu kutoka kwa mashetani. Wana wa Israeli waliwahi kula
chakula kilichonuiziwa na kufanyiwa ibada za miungu na wao wakaanza kuiabudu
ile miungu kwakuwa kile chakula kilibeba nguvu ya uharibifu
Hesabu
25:1-3
“1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha
watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao
watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula,
wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori;
hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.”
Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa
kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki
atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa
sanamu, na kuzini.”
Vilevile vipo vyakula kutoka kwenye madhabahu
ya Jehova ambavyo ni vitakatifu na vimebeba nguvu ya Mungu wa kweli kama
tunavyosoma katika
Kutoka
29:31-34
“31 Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa
wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu.
32 Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile
kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. 33 Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili
kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni
vitu vitakatifu. 34 Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya
kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi,
ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu
vitakatifu.”
Luka
22:19-20
“19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega,
akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi
kwa ukumbusho wangu. 20 Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema,
Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.”
Yesu anatufundisha kwamba unaweza kubadili
chakula chako kuwa mwili wake na kinywaji chako kuwa ni damu ya Yesu. Kila
unapopewa chakula kumbuka kukitakasa na kukifanya kuwa mwili na damu ya Yesu
ili kila unapokula ushikiri mwili na damu ya Yesu na uliimarishe agano la
Jehova na wewe.
MAOMBI:
Bwana Yesu
ninaomba toba kwa kushiriki katika chakula cha mashetani kwenye meza ya adui,
naita damu ya Yesu Kristo ndani ya tumbo langu na mfumo mzima wa mwili wangu
ambao umepokea vyakula ambavyo ni roho kutoka kwa mashetani; ninaamuru sasa kwa
jina la Yesu, enyi vyakula mliongia ndani kichawi/kiganga iwe ni kwenye ndoto
au kwa jinsi ya mwili, tokaaa!!! Kwa jina la Yesu!!! tokaaa!!! Kwa jina la
Yesu!!! tokaaa!!! Kwa jina la Yesu!!!
- Kuishi au kwenda kwenye maeneo yenye madhabahu za giza bila ya kuwa na kinga ya damu ya Yesu/nguvu za kutosha
Kuna wakati unaweza kuwa upo mahali lakini
tayari mahali hapo panamilikiwa na miungu/mashetani, au inawezekana mahali hapo
tayari papo chini ya adhabu ya Mungu kutokana na ibada za kishetani
zilizofanyika hapo.
Walawi
18:24-25
“24 Msijitie unajisi katika mambo hayo
hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi
kwa mambo hayo yote; 25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo
naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.”
Ikiwa utaenda maeneo kama haya na wewe kiroho
chako upo chini, ndipo pale kila unachokifanya hakiendi, biashara zinakufa,
elimu, ndoa, afya vyote vinaharibika. Lakini tatizo ni kwamba umeunganishwa na
madhabahu za mashetani bila kufahamu.
Wakati mwingine unaweza kuunganishwa na madhabhu
ya Mungu Jehova kwakuwa ardhi uliyoikalia ilifanyiwa ibada za Mungu wa kweli.
Yakobo alilala mahali ambapo babu yake Ibrahim alijenga madhabahu ya Jehova na akapaita
Betheli.
Mwanzo 28:12-16 “12 Akaota ndoto; na tazama, ngazi
imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika
wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 13 Na tazama, Bwana amesimama juu
yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka;
nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. 14 Na uzao wako utakuwa kama
mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini,
na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia
watabarikiwa. 15 Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako,
nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia
hayo niliyokuambia. 16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli
Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.”
Jambo la muhimu hapa ni kuanza kutafakari
maisha yako ya kiroho, inawezekana mahali ulipokaa umekutana na madhabahu za
mashetani na uwezo wako wa kivita ni mdogo ndio maana umekwama hata sasa katika
afya, ndoa, elimu, ujenzi, biashara n.k
MAOMBI:
Kwa damu ya
Yesu ninaomba toba kwaajili ya ardhi ya mahali ninapoishi/ninapofanyia shughuli
zangu, naifuta kwa damu ya Yesu mikataba yote iliyotoa uhalali kwa mashetani
kumiliki ardhi hii na kunitesa bila mimi kujua au kwa kujua, ninaikomboa ardhi
hii na kuiamuru kuwa upande wangu sasa kwa jina la Yesu. Enyi mashetani
mlioshika eneo hili na kulifanya madhabahu yenu, ninawaamuru tokaaaa!!! Kwa
jina la Yesu……
- Kwenda kwenye ngoma au sherehe za manuizio ya nguvu za giza
Zipo sherehe na ngoma ambazo zinaonekana kama
za kawaida lakini ndani yake ipo nguvu ya madhabahu za mashetani. Wewe utaona
tu kwamba tangu umeenda kwenye ile ngoma mpaka sasa hauwezi kuacha kwenda
lakini kuna katabia kamekuingia na hata ukitaka kukiacha hauwezi kukiacha hako
katabia. Ukiona hayo fahamu kwamba umeshiriki sherehe na ngoma za mashetani.
Wakati Fulani wana wa Israeli walishiriki
kwenye sherehe ya sadaka za miungu ya wamoabu, na mara baada ya hapo wakamkosea
Mungu kwakuwa haikuwa sherehe ya kawaida ilikuwa ni ya mashetani.
Hesabu
25:1-3
“1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha
watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao
watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula,
wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori;
hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.”
Danieli 3:7 “Basi wakati huo, watu wa kabila zote
walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na
zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka,
wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.”
MAOMBI:
Kwa jina la
Yesu Kristo najitoa kwenye sherehe za mashetani ambazo nimeshiriki au
kushirikishwa, natoka kwenye hizo ibada za miungu kwa jina la Yesu Kristo!
Amen!
- Kuoa au kuolewa kuna kuunganisha na madhabahu
1Falme
11:1-9
“1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake
wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni,
na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, 2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia
wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika
wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa
kuwapenda. 3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao
wakeze wakamgeuza moyo. 4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake
wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu
kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa Sulemani
akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. …….7
Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima
uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika
ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea
miungu yao dhabihu. 9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake
umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,”
Inawezekana wewe ili uoe/uolewe ulifanyiwa
jambo la uharibifu, wengine walinyweshwa maziwa na bibi/babu wa huko ukweni,
wengine walinyolewa nywele, wengine waliketishwa kwenye kigoda cha ukoo n.k;
lakini sasa kuna uzito mkubwa kwenye maisha yako na unajua kabla ya ndoa
haikuwa hivyo.
Biblia inatufundisha habari za Isaka
alipomuoa Rebeka, akamchukua mpaka kwenye hema la mama yake (Sara) na baada
hayo Rebeka akawa tasa.
Mwanzo 24:67 “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya
mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa
ajili ya kufa kwa mamake.”
Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke
wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua
mimba.”
MAOMBI:
Bwana Yesu
inawezekana katika kuoa au kuolewa kwangu nimeingizwa katika madhabahu za
mashetani katika familia nyingine kwa kujua au bila kujua, ninaomba toba Bwana
Yesu, naomba unirehemu na kuniokoa sasa. Kwa damu yako najitenga na kila
madhabahu za mashetani lizoingia au kuingizwa. Naamuru mashetani walionifunga
kwa ibada za miungu tokaaaa!!! kwa jina la Yesu!!!
- Kutenda aina yoyote ya dhambi unaunganishwa na mashetani
Tafsiri rahisi ya dhambi ni uasi/kuhalifu
maagizo/sheria za Mungu, unapokuwa nje ya maelekezo ya Mungu wewe unatenda
dhambi sawa na neno la Mungu 1Yohana 3:4
“Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa
kuwa dhambi ni uasi.”
Kitu kikubwa
kabisa na cha kwanza ambacho dhambi hufanya kwenye maisha ya mwanadamu ni
kumtenganisha na Mungu na baada ya kumtenganisha na Mungu, shetani anapata
nafasi ya kumtesa mwanadamu.
Dhambi
inapokutenganisha na Mungu inasababisha hasira ya Mungu kuwaka juu yako na
shetani anafurahia kwani ndio mwanya wake wa kuingiza uharibifu wake katika
misha yako (Isaya 59:1-2 “1 Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata
usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; 2 lakini maovu
yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake
msiuone, hata hataki kusikia.”)
Kwakuwa dhambi ni
uasi, unapotenda dhambi unakua umeamua kwa hiari yako kufunga mkataba/agano na
mashetani kinyume na Mungu na unakuwa umemkubali shetani.
Waefeso 2:1-3 “1 Nanyi mlikuwa wafu
kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; 2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata
kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule
atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; 3 ambao zamani, sisi sote nasi
tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya
mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”
MAOMBI:
Baba katika jina la Yesu ninaomba toba kwa mambo
yote niliyoyatenda kinyume na mapenzi yako na nikaichukua sura ya uasi,
ninaomba rehema na toba kwa damu ya Yesu. Katika jina jina la Yesu, enyi mapepo
ya uasi ninawaamuru ondokeni katika maisha yangu kwa jina la Yesu