Thursday, March 12, 2020

MAMBO AMBAYO UKIYAFANYA UNAUNGANISHWA NA MADHABAHU ZA MASHETANI (Samson Mollel 0767/0713 – 664 338)



Bwana Yesu apewe sifa kanisa la Yesu!

Napenda ufahamu kwamba yapo mambo mengi sana ambayo ukiyafanya (kwa kujua au kutojua) unaunganishwa na madhabahu za mashetani; inawezekana kwamba matatizo ya maisha yako huenda yameanza kutokana na kufanya au kufanyiwa moja ya mambo hayo katika maisha yako.

Mimi binafsi kutokana na huduma nilizozifanya na kwa kujifunza kutoka kwa watumishi wengine nimepata ufahamu wa mambo kadha wa kadha na baadhi ya hayo nimeyaandika katika somo hili. Nakusihi mtu wa Mungu kwamba pamoja na haya niliyoandika bado jambo muhimu na kubwa la kujiweka salama ni kumtegemea Yesu kwa uaminifu na kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu (Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;)

Nimeanza kwa kusisitiza habari ya utakatifu kwani kuna watu wanataka kumuona mungu na kuzipata Baraka zake lakini hawamtaki Mungu wala hawataki kuishi kwa kufuata sheria za Mungu na kuzishika amri zake; yaani watu hawa wanaishi maisha ya kidunia/kimwili halafu wanataka kuvuna Baraka za Mungu na kufunguliwa kutoka katika vifungo (Efeso 5:19-21)

Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo ukiyafanya unaunganishwa na madhabahu za uharibifu/za mashetani na madhara yatatokea mahali Fulani katika maisha yako.


  •  Kutoa sadaka na matambiko
Kutoa sadaka na kufanya matambiko kwa miungu (mizimu) ni moja ya njia ambayo humuunganisha mtu na madhabahu za uharibifu kwa kujua au bila kujua. Kuna watu ambao huenda kwenye koo au familia zao na kuchinja wanyama mbalimbali ili kutoa damu ya wanyama hao kwa mababu na baada ya hapo mnyama aliyechinjwa huliwa kwa utaratibu maalum; kwa mfano nyama ya kidari atakula baba mkubwa, nyamba ya paja atakula mtoto wa kwanza wa kiume na nyama ya kichwa atakula mtoto wa kwanza wa kike. Unapokuwa umeshiriki kwa kujua au bila kujua katika matambiko kama hayo unaunganishwa na ile madhabahu ambayo sadaka ya matambiko imetolewa. Kwa jinsi hii watu wengi sana walioshiriki katika matambiko wana mahusuiano na zile madhabahu zilizotolewa matambiko.

1Wafalme 11:1-8 “1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, 2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. 3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. 4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. 7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.”

1Falme 21:25-26 “25 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. 26 Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”

1Falme 16:31-33 “31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. 32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. 33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.”

Mfalme Sulemani na mfalme Ahabu wote walio wanawake kutoka kwenye familia za waabudu miungu, na kama unavyofahamu kwamba hawakuiacha miungu yao bali walikuja nayo kwa Ahabu na kwa Sulemani na hivyo walifanya matambiko (ibada za miungu) ndani ya nyumba za waume zao (Ahabu na Sulemani)  na waume zao walishiriki (kwa kujua au bila kujua) na kilichofuata ni wafalme hawa (Ahabu na Sulemani) kuunganishwa na miungu na madhabahu za mashetani na wao kumuacha Jehova na hasira za Jehova zikawaka juu yao na familia zao.
Inawezekana hata wewe nyumbani kwako kuna matatizo ya kiroho na haujui ni kwanini unapatwa na matatizo hayo, kumbe ni mume/mke wako au mtumishi wako (House girl/House boy) amekuja na miungu ya kwako nyumbani kwako na umeunganishwa na madhabahu za mashetani.


MAOMBI:
Baba katika jina la Yesu Kristo, naomba toba kwa kuwa nimeshiriki kwa kujua na bila kujua na nikatoa sadaka na matambiko kwenye madhanahu za mashetani, ninaomba rehema Baba Yangu kwa jina la Yesu kwakuwa wakati mwingine nilitoa mali yangu nikijua masaidia watu kumbe walinuia mabaya ili wanitenganishe na wewe wakaenda kutoa mali na fedha zangu kwa mashetani, nirehemu Baba kwaajili yake Yesu Kristo. Katika jina la Yesu naamuru mahali popote sadaka yangu ilipo kwenye madhabahu za mashetani ibadilike kuwa moto wa Roho Mtakatifu na kuwateketeza makuhani wote wa kichawi kwa jina la Yesu Kristo, naiondoa sadaka yangu niliyoitoa kwa miungu kwa kujua au bila kujua kwa jina la Yesu! Amen!

  •  Kushiriki au kushirikishwa katika mambo ya kiganga
Unaposhiriki au unaposhirikishwa kwenye mambo ya kiganga kwa kujua au bila kujua unaunganishwa na madhabahu za mashetani na hasira ya Mungu inakuwa juu yako hata kama haukufanya kwa ufahamu wako. Inawezekana huo uganga ameshiriki baba/babu/dada/kaka yako na wewe bila kujua amekutaja kwenye hiyo madhabahu, basi unakuwa mshirika na mateso yanayoletwa na hiyo madhabahu yanakuwa juu yako pia.

Hali kama hii iliwahi kumtokea Gideoni pale ambapo baba yake mzazi (mzee Yoashi) alipokuwa kuhani wa madhabahu ya baali; Gideoni hakuwa akishiriki katika ile madhabahu lakini kwakuwa baba yake alishiriki basi na yeye Gideoni akabeba adhabu ya kuwa mshiriki

Waamuzi 6:11-15, 25-26 “11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu……….. 25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.”

Kwahiyo tunajifunza kwamba hali ile ya uduni wa Gideoni na umasikini wake na kabila lake ulitokana na madhabahu ya baali ambayo BWANA alimuamuru kuivunja na kujenga madhabahu ya BWANA. Inawezekana hata wewe umeunganishwa na madhabhu za mashetani lakini pasipo kufahamu.

Vilevile tunasoma habari ya mfalme wa Babeli aliwaunganisha wananchi wa nchi yake na madhabahu za mashetani kwa kufanya uganga na matambiko kama ilivyoandikwa katika Neno la Mungu.

Ezekieli 21:21-23 “21 Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. 22 Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. 23 Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.”

Tunaona hasira ya Mungu inaachiliwa juu ya wote ambao mfalme amewaapia viapo hata kama hawakushiriki hicho kiapo kwa uhiari/ufahamu wao. Hebu tafakari mtu wa Mungu; ikiwa kiongozi Fulani katika nchi ya Tanzania alifanya uganga na kututaja wa Tanzania, hivi tuko salama? Ikiwa mkuu wa ukoo au familia yenu alikutaja kwenye uganga, kweli uko salama. Inawezekana hata sasa umeunganishwa na madhabahu za mashetani kwa njia hiyo; omba maombi haya ujinasue:


MAOMBI:
Baba yangu katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba kwakuwa nimeshiriki katika ibada za kiganga kwa kujua au bila kujua, wakati mwingine ndugu na jamaa wametaja jina langu kwenye madhabahu za mashetani na mimi nikaunganishwa na roho za mashetani, ninaomba toba Kwa Damu ya Yesu na kwa Jina la Yesu Kristo. Ninajitoa sasa kwenye madhabahu za waganga zilizopo makaburini, baharini, misituni, njia panda, angani na kwenye nyumba za wachawi. Natoka kwenye hizo madhabahu kwa jina la Yesu Kristo. Nauwasha moto wa Roho Mtakatifu nawateketeza mashetani yote walionishikilia kwenye madhabahu kwa jina la Yesu! Naitoa nchi yangu Tanzania kwenye madhabahu za mashetani kwa damu ya Yesu! na kwa jina la Yesu! Amen!


  • Majina yenye uhusiano na madhabahu yanaweza kukuunganisha na madhabahu
Ili Yusufu aweze kuwa mtawala wa misri alipewa jina la kimisri ili apokelewe na miungu ya Misri, yaani jina lina nguvu ya kumuunganisha mtu na madhabhu na kumpa nguvu ya ile madhabahu.Yusufu asingetawala Misri pasipo kupatanishwa na madhabahu za wa-Misri na hilo lilifanyika kwa njia ya kupewa jina lenye nguvu ya madhabahu za miungu ya Misri (Kumbuka wa-Misri ni waabudu miungu na hawakumjua Mungu wa kweli)

Mwanzo 41:42-45 “42 Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43 Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. 44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. 45 Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri.”

Wote waliomkubali Yesu na kulibeba jina la Yesu kwa imani ndani ya mioyo yao, wamepokea nafasi katika ulimwengu wa roho na kuunganishwa na madhabu ya Mungu Jehova

Yohana 1:12Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

Warumi 8:16-17 “16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

Wafilipi 2:8-10 “8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;”

Jina la Yesu ni jina la urithi ambalo amepewa na Baba yake (Mungu Baba), lakini alipolipokea hilo jina tu akapewa kiti cha enzi cha Mungu na mamlaka kubwa kuanzia mbinguni mpaka duniani na kwa jina hilo viumbe vyote vinaanguka na kusujudu.
Jina linaweza kukunganisha na madhabahu na ukapokea nguvu ya hiyo madhabahu, inategemea umeunganishwa na madhabahu gani.


MAOMBI:
Bwana Yesu ninaomba toba kwaajili ya majina niliyopewa yenye mahusiano na madhabahu za mashetani, naomba toba kwaajili yangu na watoto wangu, wazazi wangu, mabibi na mababu…… turehemu Bwana kwa jina la Yesu. Ninalidumbukiza na kulizamisha jina langu kwenye kisima cha damu ya Yesu kwa jina la yesu Kristo. Ninaamuru mapepo yaliyokamata jina langu na kulivuta kwenye uharibifu Achiaaaa kwa jina la Yesu Kristo!!! Achiaaaa jina langu kwa jina la Yesu Kristo!!! Achiaaaa kwa jina la Yesu Kristo!!! Amen!


  • Mavazi yenye mfumo wa madhabahu au nembo za madhabahu yanaweza kukuunganisha na madhabahu
Yapo mavazi yenye mfumo wa kimadhabahu na hata yametambulika katika jamii kama mavazi kwaajili ya watu fulani au kabila fulani au dini fulani. Kuna mavazi ukiyaona tu unaanza kuhisi kwamba huyu aliyevaa anaweza kuwa mganga wa kienyeji au mchawi. Mavazi ya namna hii yana nguvu za madhabahu na yanaweza kukuunganisha na madhabhu za giza.

Katika Biblia tunajifunza habari za nabii Eliya kwamba alikuwa na mavazi ambayo hayakufanana na watu wengine (2Falme 1:7-8 “7 Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? 8 Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi.”)

Ulipofika wakati wa kunyakuliwa kwa Eliya tunaona Elisha anabaki na vazi la Eliya na ule upako uliokuwa kwa Eliya unakuja kwa Elisha mara dufu.

2Falme 2:11-15 “11 Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. 12 Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. 13 Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. 14 Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. 15 Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.

Katika Biblia tunajifunza pia kwa habari ya mavazi tangu enzi za Musa na Haruni ambapo yalitengenezwa mavazi ambayo walipovaa Haruni na watoto wake walitakasika na kuweza kusogea mbele za Mungu kwaajili ya wana wa Israeli.

Kutoka 28:2,41 “2 Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri., 41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.”

Unachotakiwa hapa ni kuwa makini na mavazi unayovaa, sio ukiletewa nguo yoyote wewe unaivaa tuu, unaweza kuvaa nguo zilizotoka kwa mashetani ukaingizwa katika uharibifu wa madhabahu za mashetani.


MAOMBI:
Baba katika jina la Yesu Kristo, ninaomba toba na msamaha mahali popote nilipojiunganisha na mashetani kwa njia ya mavazi iwe ni rohoni au mwili, nirehemu baba yangu kwaajili ya mwana wako mpendwa Yesu Kristo. Kwa moto wa Roho Mtakatifu ninayateketeza mavazi yote ya kimadhabahu niliyovishwa nikiwa rohoni au mwilini, enyi mapepo mliokuja na mavazi hayo ninawateketeza kwa moto wa Roho Mtakatifu kwa jina la Yesu!!! Amen!


  • Kutumia ishara na alama za madhabahu za giza (Chale, Hirizi, alama na ishara zinaweza kuita roho za giza)
Kuna ishara ambazo zinazoonekana kwa jinsi ya mwilini lakini zina maana kubwa sana katika ulimwengu wa roho, ishara hizo zinapofanyika zinakuunganisha na madhabahu inayohusiana na ishara hiyo. Katika agano la kale kuna ishara kadhaa zilifanyika na zilikuwa na maana  kubwa katika ulimwengu wa roho.

Kutahiriwa katika agano la kale ilikuwa ni ishara ya agano la Mungu na wana wa Israeli, ilionekana kama tendo la kibindamu lakini ilikuwa ni ibada ya utakaso na mtu ambaye hakutahiriwa alitengwa na kuonekana kama mtu najisi (mchafu). Katika agano jipya tohara ni kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kama haujampokea Yesu ni sawa na mtu asiyetahiriwa yaani upo nje ya agano (ni najisi/mchafu).

Mwanzo 17:10-11, 14 “10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. 11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi…..14 Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.”

Vilevile tunaona ishara ya damu ambayo kila aliyepaka damu kwenye miimo ya mlango wake yule muharibu hakuweza kuingia katika nyumba yake.

Kutoka 12:12-13 “12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. 13 Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”

Ubatizo nalo ni tendo la ishara ambalo hufanyika kwa jinsi ya mwili lakini matokeo yake yapo rohoni na kuleta mabadiliko ya rohoni

Marko1:4 “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.”

Zipo ishara nyingi ambazo zimewaunganisha wakristo na madhabhu za giza pasipo wao kujua na madhara yameanza kutokea katika maisha yao lakini hawajui chanzo. Kumbe chanzo ni yale mafuta/maji/chimvi uliyopaka kwa nabii wa uongo (vipo vitu kama hivyo  vyenye nguvu za Mungu). Wapo watu wamevaa nguo zenye ishara mbalimbali za mashetani na wanashambuliwa na nguvu za giza lakini hawakijui chanzo cha matatizo yao.


MAOMBI:
Katika Jina la Yesu Kristo, kila mahali penye ishara ya kishetani katika mwili wangu, nina mimina damu ya Yesu Kristo naondoa uhalali wa ishara na alama hiyo katika maisha yangu. Mahali ilipowekwa hilo alama na ishara napitisha Damu ya Yesu na Moto wa Roho Mtakatifu naziteketeza kabisa hizo alama na ishara kwa jina la Yesu. Naamuru mapepo yanayolinda hizo ishara za kishetani Toooka!!! Kwa Jina la Yesu Kristo!!!! Toooka!!! Kwa Jina la Yesu Kristo!!!! Toooka!!! Kwa Jina la Yesu Kristo!!!!


  • Vitu vilivyo vuviwa kwa makusudi ya madhabahu za giza na vifaa vilivyowahi kutumika kwenye madhabahu za giza (Pete, Shanga, Hereni, michezo ya kipepo)
Katika ulimwengu wa roho sahau sayansi ya viumbe hai na visivyo hai kwani rohoni vitu vyote vinatumika (watumishi) ama na Mungu Jehova au na shetani ambaye naye ni mungu wa dunia hii.

Zaburi 119:91 “Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.”

Lakini pamoja na ukweli kwamba vitu vyote ni watumishi wa Mungu, Neno la Mungu linatupeleka mbali zaidi kwamba vitu hivyo vimetiishwa katika ubatili, yaani vinatumika nje ya mpango wa Mungu

Rumi 8:19-22 “19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. 20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini; 21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. 22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.”


MAOMBI:
Katika jina la Yesu naachilia damu ya Yesu kwenye kitu chochote nilichovaa au kuvalishwa na mashetani kupitia waganga au ndugu wa karibu, namimina damu ya Yesu naharibu nguvu ya giza kwa jina la Yesu. Naachilia moto wa Roho Mtakatifu uteketeze kila nguvu ya giza iliyopo kweye pete za kishetani, shanga, bangili, mikufu, manukato, viatu, nguo za ndani n.k. naachilia Motooo!!! kwa Jina la Yesu Kristo!!! Motooo!!! kwa Jina la Yesu Kristo!!! Motooo!!! kwa Jina la Yesu Kristo!!!


  • Kutumia vyakula/vinywaji vilivyonuiziwa kwa matumizi ya kimadhabahu na kufanyiwa ibada za tambiko linalikuunganisha na madhabahu.
Mtu wa Mungu sio kila unachokiona kinafanana na chakula basi unakula tu, vipo vya kula vya kiibada ambavyo ndani yake vimebeba roho za uharibifu kutoka kwa mashetani. Wana wa Israeli waliwahi kula chakula kilichonuiziwa na kufanyiwa ibada za miungu na wao wakaanza kuiabudu ile miungu kwakuwa kile chakula kilibeba nguvu ya uharibifu

Hesabu 25:1-3 “1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.”

Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”

Vilevile vipo vyakula kutoka kwenye madhabahu ya Jehova ambavyo ni vitakatifu na vimebeba nguvu ya Mungu wa kweli kama tunavyosoma katika

Kutoka 29:31-34 “31 Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. 32 Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. 33 Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. 34 Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu.”

Luka 22:19-20 “19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. 20 Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.”

Yesu anatufundisha kwamba unaweza kubadili chakula chako kuwa mwili wake na kinywaji chako kuwa ni damu ya Yesu. Kila unapopewa chakula kumbuka kukitakasa na kukifanya kuwa mwili na damu ya Yesu ili kila unapokula ushikiri mwili na damu ya Yesu na uliimarishe agano la Jehova na wewe.


MAOMBI:
Bwana Yesu ninaomba toba kwa kushiriki katika chakula cha mashetani kwenye meza ya adui, naita damu ya Yesu Kristo ndani ya tumbo langu na mfumo mzima wa mwili wangu ambao umepokea vyakula ambavyo ni roho kutoka kwa mashetani; ninaamuru sasa kwa jina la Yesu, enyi vyakula mliongia ndani kichawi/kiganga iwe ni kwenye ndoto au kwa jinsi ya mwili, tokaaa!!! Kwa jina la Yesu!!! tokaaa!!! Kwa jina la Yesu!!! tokaaa!!! Kwa jina la Yesu!!!


  • Kuishi au kwenda kwenye maeneo yenye madhabahu za giza bila ya kuwa na kinga ya damu ya Yesu/nguvu za kutosha
Kuna wakati unaweza kuwa upo mahali lakini tayari mahali hapo panamilikiwa na miungu/mashetani, au inawezekana mahali hapo tayari papo chini ya adhabu ya Mungu kutokana na ibada za kishetani zilizofanyika hapo.

Walawi 18:24-25 “24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; 25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.”

Ikiwa utaenda maeneo kama haya na wewe kiroho chako upo chini, ndipo pale kila unachokifanya hakiendi, biashara zinakufa, elimu, ndoa, afya vyote vinaharibika. Lakini tatizo ni kwamba umeunganishwa na madhabahu za mashetani bila kufahamu.

Wakati mwingine unaweza kuunganishwa na madhabhu ya Mungu Jehova kwakuwa ardhi uliyoikalia ilifanyiwa ibada za Mungu wa kweli. Yakobo alilala mahali ambapo babu yake Ibrahim alijenga madhabahu ya Jehova na akapaita Betheli.

Mwanzo 28:12-16 “12 Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 13 Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. 14 Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. 15 Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. 16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.”

Jambo la muhimu hapa ni kuanza kutafakari maisha yako ya kiroho, inawezekana mahali ulipokaa umekutana na madhabahu za mashetani na uwezo wako wa kivita ni mdogo ndio maana umekwama hata sasa katika afya, ndoa, elimu, ujenzi, biashara n.k


MAOMBI:
Kwa damu ya Yesu ninaomba toba kwaajili ya ardhi ya mahali ninapoishi/ninapofanyia shughuli zangu, naifuta kwa damu ya Yesu mikataba yote iliyotoa uhalali kwa mashetani kumiliki ardhi hii na kunitesa bila mimi kujua au kwa kujua, ninaikomboa ardhi hii na kuiamuru kuwa upande wangu sasa kwa jina la Yesu. Enyi mashetani mlioshika eneo hili na kulifanya madhabahu yenu, ninawaamuru tokaaaa!!! Kwa jina la Yesu……


  • Kwenda kwenye ngoma au sherehe za manuizio ya nguvu za giza
Zipo sherehe na ngoma ambazo zinaonekana kama za kawaida lakini ndani yake ipo nguvu ya madhabahu za mashetani. Wewe utaona tu kwamba tangu umeenda kwenye ile ngoma mpaka sasa hauwezi kuacha kwenda lakini kuna katabia kamekuingia na hata ukitaka kukiacha hauwezi kukiacha hako katabia. Ukiona hayo fahamu kwamba umeshiriki sherehe na ngoma za mashetani.

Wakati Fulani wana wa Israeli walishiriki kwenye sherehe ya sadaka za miungu ya wamoabu, na mara baada ya hapo wakamkosea Mungu kwakuwa haikuwa sherehe ya kawaida ilikuwa ni ya mashetani.

Hesabu 25:1-3 “1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.”

Danieli 3:7 “Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.”


MAOMBI:
Kwa jina la Yesu Kristo najitoa kwenye sherehe za mashetani ambazo nimeshiriki au kushirikishwa, natoka kwenye hizo ibada za miungu kwa jina la Yesu Kristo! Amen!


  • Kuoa au kuolewa kuna kuunganisha na madhabahu
Inawezekana unadhani kuoa au kuolewa ni kitu cha kawaida kawaida tu. Kuna watu wameo/kuolewa lakini ili wakubaliwe katika familia ya mke/mume imewabidi kuingizwa katika mikataba fulani fulani. Jambo hili halikuanza leo, inawezekana umeshao/kuolewa kabisa na baada ya hapo mume/mke anakuletea utaratibu wa nyumbani kwao (Yaani anakuungamanisha na miungu ya kwako).

1Falme 11:1-9 “1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, 2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. 3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. 4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. …….7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu. 9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,”

Inawezekana wewe ili uoe/uolewe ulifanyiwa jambo la uharibifu, wengine walinyweshwa maziwa na bibi/babu wa huko ukweni, wengine walinyolewa nywele, wengine waliketishwa kwenye kigoda cha ukoo n.k; lakini sasa kuna uzito mkubwa kwenye maisha yako na unajua kabla ya ndoa haikuwa hivyo.

Biblia inatufundisha habari za Isaka alipomuoa Rebeka, akamchukua mpaka kwenye hema la mama yake (Sara) na baada hayo Rebeka akawa tasa.

Mwanzo 24:67 “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.”



MAOMBI:
Bwana Yesu inawezekana katika kuoa au kuolewa kwangu nimeingizwa katika madhabahu za mashetani katika familia nyingine kwa kujua au bila kujua, ninaomba toba Bwana Yesu, naomba unirehemu na kuniokoa sasa. Kwa damu yako najitenga na kila madhabahu za mashetani lizoingia au kuingizwa. Naamuru mashetani walionifunga kwa ibada za miungu tokaaaa!!! kwa jina la Yesu!!!


  • Kutenda aina yoyote ya dhambi unaunganishwa na mashetani
Tafsiri rahisi ya dhambi ni uasi/kuhalifu maagizo/sheria za Mungu, unapokuwa nje ya maelekezo ya Mungu wewe unatenda dhambi sawa na neno la Mungu 1Yohana 3:4 “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.”

Kitu kikubwa kabisa na cha kwanza ambacho dhambi hufanya kwenye maisha ya mwanadamu ni kumtenganisha na Mungu na baada ya kumtenganisha na Mungu, shetani anapata nafasi ya kumtesa mwanadamu.

Dhambi inapokutenganisha na Mungu inasababisha hasira ya Mungu kuwaka juu yako na shetani anafurahia kwani ndio mwanya wake wa kuingiza uharibifu wake katika misha yako (Isaya 59:1-2 “1 Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; 2 lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”)

Kwakuwa dhambi ni uasi, unapotenda dhambi unakua umeamua kwa hiari yako kufunga mkataba/agano na mashetani kinyume na Mungu na unakuwa umemkubali shetani.

Waefeso 2:1-3 “1 Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; 2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; 3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”

MAOMBI:
Baba katika jina la Yesu ninaomba toba kwa mambo yote niliyoyatenda kinyume na mapenzi yako na nikaichukua sura ya uasi, ninaomba rehema na toba kwa damu ya Yesu. Katika jina jina la Yesu, enyi mapepo ya uasi ninawaamuru ondokeni katika maisha yangu kwa jina la Yesu



No comments: