Friday, April 17, 2020

MAOMBI NA DUA KWAAJILI YA NCHI YA TANZANIA (TOBA KWAAJILI YA UGONJWA WA KORONA – COVID-19) - Samson Mollel 0767/0713 - 664338






_Maombi haya yanatoka (Isaya 1:18, Zaburi 103:12, Isaya 43:25, 41:21, 43:26  na Daniel 9:4-19, Isaya 53:5)_

Baba katika jina la Yesu umesema katika Neno lako kwamba; Haya, njoni, tusemezane, dhambi zetu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Umesema pia BABA yangu kwamba; Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo ulivyoweka dhambi zetu mbali nasi. BABA umesema wewe, naam, wewe, ndiwe uyafutaye makosa yangu kwa ajili yako mwenyewe, wala hutazikumbuka dhambi zangu. Na BWANA umeniagiza kuwa nilete maneno yangu, nitoe hoja zangu zenye nguvu, umesema mfalme wa Yakobo kwamba nikukumbushe, na tuhojiane; nieleze mambo yangu, nipate kupewa haki yangu kutoka kwako.

Ninaungama kwako, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ushikaye maagano na rehema kwao wakupendao, na kuzishika amri zako; mimi na familia yangu na ukoo wangu na jamaa zangu na taifa langu tumefanya dhambi sana, tumefanya ukaidi mwingi, tumetenda maovu mno, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii/wachungaji/wainjlisti/mitume/walimu, ambao kwa jina lako walisema na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa familia yangu, na kwa ukoo wangu, nan chi yangu Tanzania tulio katika hofu kuu ya ugonjwa wa korona, kwa sababu ya makosa yetu tulikukosea na maovu ya baba zetu. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, viongozi wa familia zetu, na viongozi wa jamii zetu na viongozi wa nchi yetu Tanzania, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii/wachungaji/wainjlisti/mitume/walimu. Naam, familia na ukoo wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, tusiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana ya ugonjwa huu wa korona imemwagwa juu yetu, kwa sababu tumemtenda dhambi. Basi Bwana umeyaweka mabaya hayo, ukatuletea; maana Wewe Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zako zote uzitendazo; na sisi hatukuitii sauti yako.

Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuisamehe nchi yangu Tanzania; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu na viongozi waliotutangulia, adhabu hii kali imeachiliwa juu yetu. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi yangu mimi mtumishi wako, na dua zangu, ukaangazishe uso wako juu ya nchi yangu Tanzania ambayo tumekaa katika hali ya ukiwa ukiwa, kwa ajili ya adhabu yako Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mimi mtoto wako ninayeitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mimi na familia yangu tunaitwa kwa jina lako kwakuwa tumempokea mwana wako Yesu Kristo na tumeoshwa kwa damu ya Yesu, Bwana kumbuka rehema.

Asante BABA kwani umemtuma Kristo Yesu ambaye alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona, tumepona ugonjwa huu wa kutisha katika jina la Yesu Kristo, AMEN!

*Samson Mollel 0767/0713-664 338*
*_Huduma ya Uzima wa Milele (Yohana 17:3)_*
*www.uzimawamileleministries.blogspot.com*
```© April 17, 2020```

No comments: