Friday, March 3, 2017

TATIZO SUGU LINALOTESA MAISHA YAKO LINATOKA WAPI? (KWENYE MADHABAHU AU KWENYE ARDHI) (Samson Mollel 0767 664 338 – www.uzimawamileleministries.blogspot.com)

UTANGULIZI

Kumekuwa na mitazamo mingi ya tofauti tofauti ya namna ya kushughulikia matatizo sugu ambayo yamewakabili watoto wa Mungu kwa muda mrefu sana. Kuna watu wametaka kutoka katika umasikini kwa muda mrefu lakini hawajatoka mpaka sasa na hawajui tatizo limekaa wapi, wengine wametaka kutoka katika matatizo ya ndoa, wengine wametaka kuoa au kuolewa lakini mambo hayo yameshindikana kabisa hata kwa kufunga na kuomba hawajaweza kutoka katika matatizo hayo na mpaka sasa hawana majibu ya matatizo yao. Kuna watu familia zao zimekuwa na vifo vya kutatanisha au vya ghafla, wengine wamekuwa na magonjwa ya kutisha kutoka kizazi hadi kizazi na hata sasa hawana majibu ya maswali yao.

Matatizo sugu huwa chanzo chake na hayatokei pasipo chanzo/sababu. Chanzo au msingi wa matatizo sugu ni kuvunjika kwa makubaliano (maagano/mikataba) yaliyoingiwa na pande mbili au zaidi, anayevunja makubaliano anaingia kwenye matatizo ambayo ni matokeo yaliyokubaliwa (kwa kujua au bila kujua) wakati wa kufunga mkataba/mikataba hiyo (Kumbukumbu 28:15-68 “15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata…………..”). Kwa utaratibu na sheria za kiroho mikataba/maagano hayo hufanyika katika madhabahu ambazo ndio kiunganishi kati ya ulimwengu wa mwili na ulimwengu wa roho alkini madhabahu hizi huonekana kwa macho ya kibinadamu (kwakuwa hujengwa katika ardhi)

Kwa kawaida ardhi inayo uwezo wa kunakili (kuweka kumbukumbu ya matukio yanayofanyika juu yake, na pale yanapohitajika ardhi huyatoa na kuonekana tena kama vile yametokea leo), mambo hayo ardhi inayonakili na kuweka kumbukumbu yanaweza kuwa yamefanyika kwenye madhabahu au kwa nguvu ya manuizio ya namna yoyote (mazuru au mabaya). Hivyo ardhi inaweza kukaa na jambo likisubiria muda na wakati uliopangwa kulitimiliza katika maisha ya mtu/jamaa Fulani. Yeremia 22:29-30“29 Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana. 30 Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.”

Sasa basi kama ukivunja madhabahu ya familia/ukoo wako na kuacha kushughulikia mambo yalihifadhiwa na ardhi ni hakika kuwa utabaki ukijiuliza kila siku mbona tatizo sugu haliishi katika maisha yako, ni lazima mambo yaliyo katika ardhi yatolewa kwa toba hadi yaachie kabisa maisha yako.

Vilevile unaweza kushughulika na ardhi na madhabahu lakini ukasahau kuwa kuna vitabu vya kuzimu ambavyo huweka kumbukumbu ili mapepo  yaweze kufuatilia uovu kutoka kizazi hadi kizazi, hizi huitwa hati za mashitaka ambazo makatibu wa wachawi hundika huko kuzimu.
Ndugu unayeteswa na matatizo sugu; yapo maeneo manne (4) ambayo lazima uyafahamu vizuri na kuyashughulikia kwa uhakika ili kuyamaliza matatizo sugu yaliyofunga maisha yako; maeneo hayo ni pamoja na Madhabahu, Ardhi, Vitabu/hati za mashitaka na mbingu.


MADHABAHU
Madhabahu ni nini?
Ni daraja la kuunganisha kati ya ulimwengu wa roho (wa Mungu au shetani) na ulimwengu wa mwili, mara zote madhabahu ni kitu ambacho huonekana au hushikika katika ulimwengu wa mwili kwakuwa madhabahu hujengwa kwa mikono ya wanadamu, hata hivyo nguvu yake huonekana zaidi katika ulimwengu wa roho
Kuna aina 2 za madhabahu, Madhabahu ya Mungu Jehova (ya Nuru) na madhabahu ya shetani (ya giza), madhabahu iwe ya nuru au ya giza sheria zake zinafanana sana.

Madhabahu ya Mungu Jehova
Ili kuwepo na mawasiliano yasikatika katika ya ulimwengu wa roho na uliwengu wa mwili ni lazima kuwe na chombo kinacho hakikisha mawasiliano hayo hayakatiki na chombo hicho ni madhabahu, watu/watumishi wa Mungu katika Biblia walianza kwa kujenga madhabahu ili kuweka namna nzuri ya kuwasiliana na Mungu. Hebu tazama mifano michache ya watu waliomjengea Jehova madhabahu katika Biblia

NUHU:- Mwanzo 8:20 “Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.”

MUSA:- Kutoka 17:15 “Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi;”

YOSHUA:- Yoshua 8:30 “Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.”

GIDEONI:- Waamuzi 6:24 “Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.”

SAMWELI:- 1Samweli 7:17 “Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea Bwana madhabahu.”

Kwahiyo tunajifunza kuwa madhabahu haijileti yenyewe inajengwa na watu na hivyo hivyo ikitakiwa kubomolewa hubomolewa na watu, hapa tumewaona watumishi wa Mungu ambao ni Nuhu, Musa, Samweli na Gideoni wakimjengea Jehova madhabahu.

Madhabahu ya ibilisi/shetani
Kama nilivyosema hapo awali sheria za ulimwengu wa roho zinafanana sana, vilevile shetani na watumishi wake wana madhabahu ambayo hutumia kupitisha mambo mabaya/maovu kutoka katika ulimwengu wa roho (giza) kuingia katika ulimwengu wa mwili, mambo haya ndio yale matokeo ya kukataa agano ambalo shetani amefunga na mababu na mabibi miaka mingi iliyopita. Kwa kuvunja agano lililofanyika katika madhabahu ya ibilisi laana na mikosi, magonjwa ya kila namna humpata mtu. Baadhi ya mifano ya madhabahu za shetani ni:-

Madhabahu ya Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi

Kutoka 34:11-13 “11 Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. 12 Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. 13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.”

Mungu anawaagiza wana wa Israeli wasifanye maagano na wenyeji bali wabomoe madhabahu zao kwani matatizo ili yakupate lazima yatokee katika madhabahu.

Kumb 12:2-3 “2 Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; 3 nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.”



MAMBO MUHIMU YANAYOUNDA MADHABAHU

Ili uweze kushughulikia tatizo sugu lililoshikiliwa kwenye madhabahu ni lazima ufahamu vizuri kuwa madhabahu sio jina pekee bali ni muunganiko wa mambo sita (6) ambayo hayo yanafanya madhabahu kuwepo na kuwa na nguvu, mambo hayo ni kama yafuatayo:-
1.       Madhabahu yenyewe
2.       Kuhani wa madhabahu
3.       Kafara ya madhabahu
4.       Washirika wa madhabahu
5.       Mungu wa madhabahu
6.       Nguvu ya madhabahu

1.     Madhabahu yenyewe

Madhabahu hujengwa na watu kwa kusudi la kufanya ibada kwa Mungu wanaye mwamini. Kwa kawaida kila mwanadamuanaamini kuwepo kwa nguvu ambayo ni kubwa kuliko nguvu ya kibinadamu (existence of super natural power). Ili kuwasiliana na nguvu hii mwanadamu inambidi kutengeneza utaratibu wa kuifikia nguvu hiyo (kujenga madhabahu). Iwe ni kwa upande wa nuru au giza madhabahu lazima ijengwe kwa jinsi ya mwili kabisa. Eliya alijenga madhabahu ya Bwana (1Wafalme 18: 32 “Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu”)
Vilevile makuhani wa shetani nao hujenga madhabahu 1Wafalme 16:33 “Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.”
Ninachotaka ufahamu hapa ni kwamba madhabahu hujengwa kwa jinsi ya mwilini iwe ya Jehova au ya miungu.


2.     Kuhani wa madhabahu
Kuhani wa madhabahu ni mtu anayejua taratibu za madhabahu na mwenye uwezo(nafasi au cheo kilichokubalika) wa kuleta vitu vya kiroho (Baraka au laana) kutoka ulimwengu wa roho kuingiza katika ulimwengu wa mwili na kutoa vitu (sadaka/kafara/manuizio) kutoka katika  ulimwengu wa mwili kwenda katika ulimwengu wa roho

a.      Makuhani wa Jehova
Katika uliwengu wa nuru kuhani ni mtu yoyote aliyempokea Yesu na kuzishika amri zake (Ufunuo 5:10 “ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” Vilevile kuhani anaweza kuwa mtu yoyote aliyejifunza taratibu za kiibada yak i-Mungu kama mchungaji, shemasi, mwinjilisti, askofu, paroko n.k. mfano katika Biblia tunamuona Melkizedeki alikuwa kuhani wa Jehova.

Mwanzo 14:18 “Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.”

b.     Kuhani wa madhabahu za kishetani
Katika ulimwengu wa giza kuhani ni mtu yoyote ambaye anamtumikia shetani kwa kujua au bila kujua kwa lengo la kuleta uharibifu, nasema kwa kujua au bila kujua kwani kuna watu wanaitumikia mizimu ya nyumbani kwao wakidhani wanafanya kawaida kama walivyofanya baba na babu zao (mfano kuchinja kila mwaka, kuomba kwenye makaburi), lakini bila wao kujua kuwa wameshakabidhiwa ukuhani wa madhabahu za kishetani. Watu hawa huja kushtuka pale mambo yanapowaendea vibaya kwa kukiuka kanuni za kimadhabahu bila wao kujua. Mfano wa makuhani wa madhabahu za kishetani katika biblia ni makuhani wa dagoni na baali.
1 Samweli 5:5 “Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo.”
1Wafalme 18:25-26 “25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. 26 Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya.”

3.     Kafara/sadaka ya madhabahu
Madhabahu haiwezi kukamilika kama hakuna kafara kwasababu kila mungu/Mungu wa madhabahu huhitaji kafara. Haijalishi uko upande gani lazima unapoenda madhabahuni uende na kafara/sadaka.

a.      Kafara katika madhabahu ya Jehova
Katika agano la kale kafara iliyotolewa ilikuwa ni mfahali na mbuzi na kondoo na wanyama na ndege, lakini katika agano jipya Yesu Kristo ndiye kafara/sadaka katika madhabahu ya Jehova.

Walawi 2:2 “kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana;”

Zaburi 50:8 “Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima.”

Waebrania 9:27-28 “27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; 28 kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.”

b.     Kafara kwenye madhabahu ya kishetani
Madhabahu za shetani nazo zinadai kafara, hata kama unaiona mdhabahu ni ya kinyago katika macho ya damu na nyama lakini katika ulimwengu wa roho hiyo sanamu inawakilisha mungu wa kipepo na anadai sadaka kila wanapoenda kufanya ibada kwake (hizi ki-Biblia huitwa ibada za sanamu)

Zaburi 106:36-38 “36 Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao. 37 Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. 38 Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.”

Matendo 15:29 “yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu”

4.     Washirika wa madhabahu
Washirika wa madhabahu ni watu muhimu sana kwenye madhabahu, ni vigumu sana kuwa na madhabahu ambayo haina washirika. Iwe ni ya Jehova au ya ibilisi, madhabahu lazima iwe na washirika ambao wanaamini au wameaminishwa kwa habari ya mungu/Mungu wa madhabahu hiyo.

c.      Washirika wa madhabahu ya Jehova
Kama ilivyo hata sasa wewe unayesoma inawezekana kabisa ni mshirika wa kanisa Fulani ambalo linamuabudu Jehova; hii haikuanza leo kwani Mungu anakaiwada ya kujitengea watu wa kumuabudu (washirika) ambao wapo tayari kumuabudu yeye Jehova peke yake. Eliya alifahamu umuhimu wa kuwa na washirika ndio maana aliojiona yupo mwenyewe alikata tama.

1Wafalme 19:9-10 “9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? 10 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.”

Mungu anamtoa Eliya hofu na kumwambia kuwa amejisazia washirika wake 1Wafalme 19:18 “Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.”

Katika agano jipya tunaona Mungu akisema kwa habari ya washirika/ushirika katika Kristo Yesu

1Wakorintho 1:9 “Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.”

1Wakorintho 10:18 “Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?”

Waebrania 3:14 “Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;”


d.     Washirika wa madhabahu za kishetani

Kama vile wewe ulivyo ni mshirika wa kanisa fulani vivyo hivyo kila madhabahu ya kishetani inayo washirika wake. Hawa ni watu hatari sana, kwakuwa matatizo yote huanzia kwenye madhabahu za kishetani, wanao peleka jina lako/kazi yako/ndoa yako/elimu yako n.k ni washirika wa madhabahu ili lijadiliwe kwa lengo la kuharibu maisha yako.

Washirika wa madhabahu ya kishetani mara zote ni watu wako wa karibu kama vile Delila alivyokuwa karibu na Samsoni (Waamuzi 16:5 “Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja.”)

Mathayo 10:36 “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.” Na Mika 7:5-6 “5 Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. 6 Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.”

5.     Mungu wa madhabahu
Neno “mungu” ni nafasi au cheo kama ilivyo kwa Rais. Kwa maana hiyo unapotaja jina la mungu inakubidi uainishe ni mungu yupi unayemtaja.

a.      Mungu Wa Madhabahu (Jehova)
Kutoka 6:1-3 “1 Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. 2 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; 3 nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.”
Utaona kuwa kila Mungu aliwatokea watumishi wake walimjengea madhabahu, huyo ndiye Mungu wa madhabahu aliyoijenga Nuhu, Musa, Eliya, Ibrahim na watumishi wengine wa Jehova

b.     mungu wa madhabahu za kishetani
shetani ndiye mungu wa madhabahu za wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota, wapiga ramli, wasihiri na mawakala wote wa mauti.
2Kor 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”
1Wafalme 16:32 “31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. 32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria.”


6.     NGUVU YA MADHABAHU
Nguvu ya madhabahu inategemea mambo yote yanayounda  madhabahu yaani Madhabahu yenyewe, Kuhani wa madhabahu, Kafara ya madhabahu, Washirika wa madhabahu na Mungu wa madhabahu.
Nguvu ya madhabahu hupatikana pale ambapo vitu vyote vinavyounda madhabahu vimefanyika au vimefanywa ipasavyo ndipo utapata matokeo (nguvu) ya madhabahu hiyo.


Tuutazame mfano wa wa nabii Eliya na manabii wa baali
1Wafalme 18:21-40 “21 Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. 22 Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. 23 Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. 24 Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.………….. 26 Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya……………. 28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. 29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia………….. 32 Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.…………... 36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. 38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. 39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu. 40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.”
Tunachokiona hapa ni nguvu ya Jehova ilivyokubwa kuliko nguvu ya mungu baali (ibilisi). Hawa manabii wa baali mpaka walipoamua kukubaliana na wazo la Eliya kwamba Mungu atakayeshusha moto na awe ndiye Mungu ina maana waliamini kuwa mungu (baali) anazo nguvu na tayari manabii wa baali walishawahi kumuona baali akishusha moto wakati fulani ndio maana wakakubaliana haraka haraka. Hata hivyo hasira za BWANA zinapowaka hakuna miungu inayoweza kujihudhurisha mahali alipo BWANA hivyo nguvu ya mungu baali ilinyamazishwa mara moja. Neno la Mungu linatufundisha kuwa “Mara moja amenena Mungu; Mara mbili nimeyasikia haya, Ya kuwa nguvu zina Mungu” Zaburi 62:11. Nguvu za kweli na uweza unatoka kwa Jehova kwakuwa yeye ndio chanzo cha nguvu, hata nguvu alizonazo shetani (mungu wa dunia hii) alizipata kutoka kwa Jehova kwakuwa aliumbwa pia.

MAMBO AMBAYO MADHABAHU INAFANYA
Kama nilivyotangulia kusema kuwa madhabahu ni daraja katika ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili, sasa katika kutengeneza muungano huo kutoka rohoni kuja mwilini na kutoka mwilini kwenda rohoni, kuna mambo ambayo madhabahu inayafanya kama ifuatavyo:-

1.     Inaleta zile roho zilizoabudiwa na zinachanganyika na dhabihu/ kafara/ sadaka
Wana wa Israeli walipokuwa wanakaribia kuingia nchi ya Moabu, Mfalme wa Moabu (Balaki) alitafuta namna ya kuwalaani (kuwaloga) wana wa Israeli kwa nijia mbalimbali lakini hakufanikiwa hata akamtumia kuhani wa Mungu wa kweli (Balaamu) ambaye alirubuniwa kwa ujira wa uganga kuwalaani Israeli lakini hakufanikiwa kabisa kuwalaani Israeli (Hesabu 22:1-41).

Baada ya kushindwa kuwapiga Israeli kwa njia ya kutoa sadaka kwa mashetani, ndipo alipotumia mbinu nyingine (ONGEZA UMAKINI HAPA MPENDWA MSOMAJI). Balaamu akachukua vyakula (wanyama) wakavifanyia ibada na kuvitoa kama sadaka kwa shetani na zile roho za madhabahu za kishetani zikaingia ndani ya zile sadaka/dhabihu/kafara yaani zile roho zikachanganyika  na ile sadaka, baada ya kufanya hayo Balaamu na Balaki wakawapa Israeli kile chakula (ambacho kilitolewa kama sadaka katika madhabahu ya shetani) na Israeli wakakila bila ya kujua tayari walikuwa wanakula vyakula vya kiibada Hesabu 25:1-3 “1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.” Vilevile kwa habari hii tunasoma katika  Ufunuo 2:12-15 “12 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili. 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani. 14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. 15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.”

Kwa sababu hiyo Israeli wakamchukiza Mungu kwani walikula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa mashetani. Unapokula chakula ambacho kimetolewa sadaka kwa mashetani unamtia Mungu (Jehova) wivu kwakuwa unakuwa umeshiriki ibada za kishetani moja kwa moja hata kama hukufahamu, habari hii ya Balaamu na Balaki tunzidi kuiona katika 1Korintho 10:14-22 “14 Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. 15 Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. 16 Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. 18 Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? 19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? 20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. 21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. 22 Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?” kwa sababu hii mtu wa Mungu ndio maana kabla ya kula chochote ni muhimu sana kuomba na kutakasa chakula unachokula kwa Neno la Mungu

2.     Inaleta zile roho zilizoabudiwa zinamiliki ardhi ya eneo ambalo madhabahu inakaa
Madhabahu inapokaa mahali inaleta zile roho zilizoabudiwa/zinazoabudiwa kumiliki ardhi ya mahali ilipo madhabahu hata kama aliyejenga/waliojenga madhabahu hiyo hawapo hapo. Kama wewe ni msomaji wa Biblia utakumbuka habari ya Ibrahimu alipomjengea Bwana madhabahu na kuita mahali pale Betheli Mwanzo 12:6-8 “6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. 7 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea. 8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana.” Vilevile tunasoma kuwa Yakobo alijenga madhabahu na kubadilisha jina la Luzu kuwa Betheli Mwanzo 28:11-19 “11 Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. 12 Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 13 Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. ……………………….. 16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. 17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. 18 Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. 19 Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

Yakobo alilala mahali ambapo palikuwa na madhabahu iliyojengwa na Baba yake Ibrahimu wakati bado anaitwa Abramu, alipokuwa amelala akaona malaika wakipanda na kushuka kutoka mbinguni na akamuoa BWANA, haya yote yalitokea kwasababu madhabahu iliyojengwa hapo ilimkaribisha BWANA kumiliki mahali pale (Luzu) ambapo Yakobo alibadilisha jina la mahali hapo na kupaita Betheli.

Miaka mingi baadae wana wa Israeli walimkosea BWANA na kuitumikia miungu mingine BWANA akakasirika na kuwatoa wote katika nchi yao (ambapo pana madhabahu ya Jehova) na kuwapeleka mbali na uso wake isipokuwa kabila la Yuda. Baada ya Israeli kuondolewa katika nchi yao Mfalme wa Ashuru akawaleta wageni kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu wasiomjua Jehova, wakakaa katika ardhi ya Samaria (Betheli) palipokuwa na madhabahu ya Jehova. Wageni hawa walianza kupokea mapigo makali kwani hawakujua madhabahu ya Betheli ilimkaribisha Mungu mahali pale na kama Mungu alikuwepo basi lazima taratibu na kanuni zake zizingatiwe, na hao wageni walikuja na miungu yao hawakufuata tarajibu za Jehova nao wakliwa na Simba kama tunavyosoma katika 2Falme 17:24-28“24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. 25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. 26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. 27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. 28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana.”

Ninachotaka kukufundisha hapa ni kwamba, kwa kujenga ile madhabahu ya Betheli Abramu (Ibrahimu) na Yakobo (Israeli) walimkaribisha Roho wa Mungu katika ardhi waliyoikalia na walipojenga hiyo madhabahu na kwaajili hiyo Jehova alimiliki ardhi ya nchi ile ambayo madhabahu ya Jehova ilijengwa. Swali langu kwako ni haya;

         i.Unafahamu aliyekutangulia mahali ulipo sasa alimjengea nani madhabahu na kumpa milki ya ardhi hiyo? (Nyumba unayoishi, Ofisini, Kwenye Biashara, Shule/chuo unaposema, Kanisa unaloabudu n.k)

       ii.Unafahamu ardhi unayoikalia inamilikiwa na Mungu yupi? Je ni Jehova au ni mizimu
     iii.Unafahamu kuwa matatizo ya maisha yako yametokana na wewe kukaa katika ardhi inayomilikiwa na miungu mingine?

     iv.Unafahamu matatizo ya maisha yako yanasababishwa na wewe kuiacha sheria ya BWANA katika ardhi ya watakatifu wa Mungu?

Unapokuwa unajibu maswali hayo zingatia kuwa huwezi kumiliki na kutawala mahali kama haujamjengea BWANA madhabahu kwanza na kuhakikisha madhabahu zilizotangulia zimevunjwa zote.


3.     Inaleta zile roho zilizoabudiwa zinamiliki anga na hali ya hewa ya eneo ambalo madhabahu inakaa
Jambo lingine ambalo madhabahu inafanya mahali ilipojengwa ni kuleta roho zilizoabudiwa kumiliki anga la mahali hapo. Kwa wale wenyeji wa mkoa wa Mwanza utakuwa unafahamu kuwa wakati wa ukame wazee wa mila huchukua sadaka za nafaka kwa kila mwanajamii (mwananzengo) na kuzipeleka sadaka hizo kwa miungu yao ili miungu hiyo iruhusu mvua kwakuwa madhabahu za miungu hiyo imewapa uhalali wa kumiliki anga la mahali pale pamoja na hali ya hewa ya eneo hilo.

Unaposoma kwa habari ya nchi ya uajemi ambayo walikuwa wakiabudu miungu, Biblia inatufundisha kuwa anga la nchi ile lilikabidhiwa kwa miungu ya nchi hata wakamzuia Yesu asiweze kumfikia Danieli kwa wakati alipomuita Daniel 10:1-21 1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo. 2 Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. 3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia. 4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli; 5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi………….. 20 Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja…….”

Ukisoma kwa makini mstari wa kwanza utaona habari ya mfalme wa uajemi, kwa maana kuwa nchi ilikuwa na mwanadamu kiongozi aliyeitwa Koreshi ambaye ndiye mfalme wa uajemi; lakini pia katika mstari wa 13 utaona kuwa nchi hiyo hiyo inae mkuu wa ufalme wa uajemi (Huyu yupo rohoni) ambaye amelishikilia anga la Uajemi na anayo mamlaka na jeshi kwani alimpinga Yesu kwa siku ishirini na moja.

Hata kwa upande wa Nuru (Jehova); kama Mungu akijengewa madhabahu katika nchi vivyo hivyo anamiliki anga na hali ya hewa ya nchi ambayo madhabahu yake imejengwa, na ndio maana kama kukiwa na tatizo la ukame makuhani (wachungaji, wainjilisti nk) huenda mbele za mungu kuomba mvua na inanyesha (Soma habari za Eliya 1Falme 18).

Ukisoma Kumbukumbu la torati 28:15, 23-24 “15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. 23 Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma. 24 Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.

Bwana Mungu anaongea na watu wake Israeli na kuwapa maonyo ikiwa hawataisikia sauti yake, katika maonyo haya inaonesha uwezo wa Mungu juu ya hali ya hewa ikiwa Israeli watamuacha Mungu.

Ukisoma 2Nyakati 7:12-14 “12 Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. 13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; 14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”
Mtu wa Mungu nataka ufahamu kuwa panakuwepo madhabahu mahali fulani (Nchi, Mkoa, Wilaya n.k), madhabahu hiyo inaleta zile roho zinazoabudiwa/zilizoabudiwa kumiliki anga na hali ya hewa ya mahali hapo. Unapoaliangali suala la roho kumiliki anga na hali ya hewa usiangalie kwa mfumo wa nchi na mkoa tu! Kuna watu katika familia/biashara/kazi/ndoa na anga lao limemilikiwa na mizimu kwa sababu familia yao imejenga madhabahu na hiyo madhabahu imeruhusu roho za mizimu kutawala anga la familia katika ndoa, kazi, biashara.


4.     Inaleta zile roho zilizoabudiwa zinakamata ufahamu/moyo/nafsi za watu wa eneo ambalo madhabahu inakaa
Jambo lingine muhimu kufahamu ni hili; madhabahu inapokuwepo mahali fulani inaleta zile roho zilizoabudiwa/zinazoabudiwa na zile roho zinakamata ufahamu/moyo/nafsi ya watu wanaoiabudu madhabahu hiyo. Neno la Mungu linatufundisha kwamba watu wanaiabudu miungu wanafana nayo kama tunavyosoma katika Zaburi 115:4-8 “4 Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. 5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, 6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu, 7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. 8 Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.”

Kama wewe ni muombaji na unataka kulishughulikia jambo katika eno fulani lazima ushughulikie kwanza madhabahu inayoita roho zinazoabudiwa mahali hapo, bila kufanya hivyo (kuvunja madhabahu kwanza) hizo roho haziwezi kuachia ufahamu wa watu ambao wamekabidhiwa katika hizo madhabahu, ndio maana BWANA alimuagiza Gideoni kuvunja madhabahu ya baali iliyojengwa na baba yake Gideoni mzee Yoashi (Waamuzi 6:25 “Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;”)na mara baada ya  kuvunja ile madhabahu zile roho zikamuachia mzee Yoashi na watu wote wa mji ule ufahamu wao ukahuishwa (Waamuzi 6:28-32)

Mtu mmoja aliyeitwa Yeroboamu alifahamu nguvu ya madhabahu katika kukamata ufahamu wa watu. Hivyo basi, Yeroboamu alipokuwa mfalme (Ufalme huu aliupata kwa kosa la mfalme Sulemani, yaani haikuwa haki yake kuwa mfalme ila alipewa na Mungu badala ya Rehoboamu kama adhabu kwa Sulemani alipomuacha Mungu) alijenga madhabahu ya miungu ili kuwazuia Israeli wasiende Yerusalemu kwa kuofia kuwa ufahamu wao utashikwa kwa nguvu ya madhabahu iliyokuwapo Yerusalemu na watu watamrudia Rehoboamu na yeye Yeroboamu kuukosa ufalme.

1Wafalme 12:25-30 “25 Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli. 26 Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. 27 Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda. 28 Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng'ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. 29 Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani. 30 Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani.”

Ukisoma mstari wa 27 Yeroboamu anasema “Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda” alifahamu nguvu ya kubadilisha mioyo/ufahamu/fikra za watu upo kwenye madhabahu.


5.     Madhabahu inatoa mwelekeo wa maisha ya watu wa eneo lote ambapo hiyo madhabahu inamiliki
Hali ya maisha ya watu katika eneo fulani kuanzia mtu binafsi, familia, mkoa au nchi inategemea sana na madhabahu iliyopo katika eneo hilo, kimsingi muonekano wan chi kwa macho ya kibinadamu (iwe ni jangwa au misitu, milima au mabonde) hauwezi kutoa mwelekeo wa sehemu hiyo kama madhabahu inavyoweza kufanya. Hapa utapata majibu ya maswali mengi yanayouliza ni kwanini nchi za Afrika ziko nyuma kimaendeleo japo zimebarikiwa kwa rasilimali nyingi na nchi kama Israeli iliyopo jangwani haina rasilimali nyingi lakini imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo, jibu ni madhabahu! Madhabahu iliyopo ndio inayoamua muelekeo wa maisha ya watu waishio mahali hapo.

Hata kama umeokoka na unakaa mahali penye madhabahu za kichawi/kiganga fahamu ya kwamba mwelekeo wa maisha yako utakuwa sawa na wanaomiliki hiyo madhabahu, jambo kama ndilo lilimpata Gideoni; Malaika wa Bwana anamuita kuwa ni shujaa lakini yeye amekuwa masikini kutokana na madhabahu ya baali ilikuwa imejengwa na baba yake (Waamuzi 6)

Vilevile ukisoma 2Falme 17:24-28“24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. 25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. 26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. 27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. 28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana.”

utaona kuwa hata namna ya ibada huamuliwa na madhabahu iliyopo mahali unapokaa wewe ndio maana mfalme wa Ashuru alipowaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria ambapo Israeli walikaa na palikuwa na mdhabahu ya Jehova, madhabhu ya Jehova ndio iliyoamua aina ya maisha (lifestyle) ya kuishi katika nchi ya Samaria.

Jambo muhimu lakufahamu hapa ni kwamba unapoenda kuishi mahali popote iwe umepanga au umejenga, kumbuka kujenga madhabahu ya Jehova kabla ya jambo lolote ili maisha ya mahali hapo yaamuliwe na madhabahu ya Jehova na sio madhabahu za kichawi.


MAMBO AMBAYO ARDHI INAWEZA KUFANYA/KUFANYIWA NA KUSHIKILIA TATIZO KATIKA MAISHA YAKO


1.     Inaweza kupokea laana kwaajili ya mtu na kuitekeleza hiyo laana

Katika kitabu cha Mwanzo baada ya Adam na Mkewe kuasi jambo la ajabu na kushangaza linatokea na Bwana Mungu anaisemesha ardhi tunaona kuwa ardhi inalaaniwa kwaajili ya Adamu, hapo tunajifunza kuwa ardhi inaweza kupokea laana kwaajili ya mtu fulani na ikaibeba kwaajili yake tu!

Mwanzo 3:17-19“17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; 18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; 19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”

2.     Ardhi inaposemeshwa kwa habari za mtu Fulani au kitu Fulani inaweza kutunza kumbukumbu za maisha yako

Ardhi inaweza kuwa kama chombo cha cha kunasia kumbukumbu na kuzihifadhi mpaka muda na wakati ambao kumbukumbu hizo zinazhitajika kwaajili ya utekelezaji wa mpango fulani kama tunavyosoma katika Yeremia 22:29-30“29 Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana. 30 Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.”

Hii ndio sababu kuna mambo ambayo yanaipata familia yako kwa watu wenye umri fulani tu au baada ya miezi/miaka fulani kuna jambo la uharibifu lazima litokee, mambo haya yanakuwa yalifanyika katika madhabahu na ardhi inayanakili/inayahifadhi mpaka utakapotimia muda na wakati muafaka wa kuliacha hilo jambo.

3.     Ardhi inaandika na kutoa taarifa juu yako
Vilevile ardhi inaweza kuwa karani wa kikao ambaye anaandika taarifa za vikao vingi na kuzitoa taarifa hizo pale zinapohitajika kutolewa. Na hii ndio maana kuna watu wameandikiwa taarifa za kuwa waganga/wachawi katika familia zao na kila anapohama wilaya/mkoa/nchi bado anakutana na wachawi/waganga wan chi hiyo wakimfahamu vizuri. Kuna watu wameandikiwa kuwa hawataoa au hawataolewa, kila anapotokea mchumba basi ardhi inafungua kumbukumbu hiyo na kutoa habari kuhusu mtu kutoolewa au kutooa kama tunavyosoma katika Yeremia 17:13 “Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha Bwana, kisima cha maji yaliyo hai.”

4.     Ardhi inaweza kuolewa na miungu mingine
Isaya 62:4“Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa.”
Ardhi ya eneo unalotoka/unapoishi/unapofanya kazi/unaposoma/unapoabudu inaweza kuolewa na kuwa chini ya bwana fulani (mfano inaweza kuolewa na ibilisi/miungu/mizimu) hivyo watu wote wakaao mahali hapo kwenye ardhi iliyoolewa wanakuwa chini ya mamlaka ya aliyeioa hiyo ardhi na ardhi inatekeleza maelekezo ya aliyeioa.
Mtu wa Mungu nataka nikueleweshe zaidi juu ya jambo hili; kama vile mwanamke anapoolewa na kuwa chini ya utawala wa mume wake kama yanenavyo maandiko “22 Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. 24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.” Waefeso 5:22-24. Kwa namna hiyo hiyo ardhi iliyoolewa inaongozwa na mume aliyeioa; sasa basi pale ardhi ilipoolewa na mashetani uwe na hakika italazimisha mambo yote yanayotendeka katika ardhi hiyo yawe ya kishetani kwani itakuwa inatii maelekezo ya bwana wake yaani ibilisi. Hakikisha ardhi unayoikalia katika eneo lolote (kazini,  nyumbani, kanisani, shuleni …) umeifungisha ndoa na Kristo Yesu ili kila anayekuja juu ya ardhi hiyo atiishwe kufanya yale ya Kristo Yesu.

5.     Uzao wa ardhi unaweza kubarikiwa na pia unaweza kulaaniwa
Ardhi haiwezi kuzaa pasipo kuolewa na kuzaa huko kunategemea na Mungu/mungu aliyeioa ardhi hiyo, Kumb 28:4,18“4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako…………….. 18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.” Neno la Mungu linazungumzia habari ya kubarikiwa na kulaaniwa kwa uzao wa tumbo (mwanadamu) na uzao wa nchi (ardhi). Ndio maana kuna maeneo hata ulime kwa kufuata kanuni bora za kilimo, uweke mbolea mvua inyeshe bado hauwezi kuvuna na kufuga, sababu ni ardhi imelaaniwa katika uzao wake. Ardhi inaweza kuwa haizai kutokana na laana. Ukiisemesha tu kwa toba ardhi inaweza kuzaa kwaajili yako hatakama haizai kwaajili ya wengine. Na kama watu wa Mungu wakimlilia Mungu (toba), Mungu anasema “13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; 14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” 2Nyakati 7:13-14

6.     Ardhi inaweza kutumika kupeleka maangamizi kwa familia/mji fulani
Ardhi inaweza kusemeshwa ili kupeleka uharibifu/maangamizi kuelekea kwenye mji ambao unalengwa kupokea maangamizi hayo.
Ezekiel 21:18-24“18 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 19 Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. 20 Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. 21 Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. 22 Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. 23 Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. 24 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono.”
Neno la Mungu linamjia nabii Ezekiel na kumuelekeza kuweka upanga kwenye njia mbili (njia panda) na kuandika kwa maelekezo katika ardhi ya njia hizo mbili ili upanga ukaipige miji ya Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu kutokana na uganga uliofanywa na mfalme wa Babeli. Mistari hii inatuonesha kwamba ardhi inaweza kupokea maelekezo ya uharibifu na kwenda kuyatekeleza kwa muhusika.
Mtu wa Mungu achilia damu ya Yesu futa maandiko/maelekezo yote ya uharibifu ambayo shetani kupitia mawakala wake waliandika katika ardhi ili ikifika muda na wakati jambo baya likupate (Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”)

7.     Ardhi inaweka kumbukumbu ya nyayo za kila anayeikanyaga na wachawi wanaweza kuchukua nyayo zako kwenye ardhi.
Mtu wa Mungu usishangae pale unaposikia kuwa nyayo zako au za mtu fulani zimechukuliwa na kuhifadhiwa na wachawi ili kukuloga, jambo hilo linawezekana kabisa kwani ardhi inauwezo wa kuifadhi kumbukumbu ya nyayo zako. Ukisoma katika Zaburi 56:5-6“5 Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya. 6 Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.”
Vilevile tunasoma katika Ayubu 33:11 “Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza.” Ayubu 13:27“Waitia miguu yangu katika mkatale, na kuyaaua mapito yangu yote; Wajiandikia alama kuzizunguka nyayo za miguu yangu;”
Mikatale ni kitu kinachofunga, watu wanaweza kuzichukua nyayo zako na kuzifunga ili wewe usifanikiwe, njia/mapito yako yote wanayaua na mipango yako ya mafanikio inateketea kabisa, wanaandika na kusemesha nyayo za miguu yako ili usifanikiwe. Kupitia ardhi ambapo ndipo zinpokanyaga nyayo, shetani anafunga watu na mafanikio yao yote.
Ndugu fahamu kwamba mipango yote unayoipanga inaweza kuharibiwa na wachawi kupitia nyayo zako, hivyo basi kwa mtu uliyeokaka unapaswa kuombea nyayo zako ili kila unapokanyaga unaachilia damu ya Yesu, moto wa Mungu na unamiliki na kutawala sawasawa na Neno la Mungu kutoka Yoshua 1:3 “Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.”

8.     Ardhi inaweza kuwatapika wenyeji na kuwatoa
Mtu wa Mungu usishangae kuona katika miji/mikoa/wilaya fulani wenyeji wa sehemu hizo sio waliojenga na sio wanaoishi katika miji hiyo bali ni wageni ndio wamemiliki na kutawala maeneo yao, hali hii inaelezeka kibiblia kabisa kwamba ardhi inaweza kuwakataa/kuwatapika wenyeji kwaajili ya dhambi zao na maovu yao (unajisi).
Walawi 18:24-25 “24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; 25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.”

9.     Ardhi inaweza kuzaa mapooza
Ardhi ikiwa najisi kwasababu ya wanadamu kuifanya iwe najisi, Mungu anaachilia adhabu juu ya hiyo nchi na nchi inaanza kuzaa mapooza.
2Wafalme 2:19-22 “19 Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. 20 Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. 21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. 22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.”
Ndio maana Mungu anasema ataiponya nchi ikiwa watu wake walioitwa kwa jina lake watajinyenyekesha na kuomba, hii inamaana kuwa ardhi inaweza kuwa na ugonjwa na ndio maana Mungui anaweza kuiponya kwani hauwezi kuponya kisichoumwa.

10.Damu ikimwagika kwenye ardhi, ardhi haiwezi kunena mema
Damu ya mwanadamu au mnyama yoyote ikimwagika kwenye kwenye ardhi inayotabia ya kuita damu nyingine ili kufidia ile iliyomwagika, kama hali hii isiposhughulikiwa mapema basi huendelea na kuwa ni mzunguko usio katika
2Samwel 21:1-4“1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni. 2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;) 3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa Bwana? 4 Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.”

Baada ya damu ya Wagibeoni kumwagika ardhi ilinasa mara moja taarifa zilizoko katika ile damu kuwa imemwagwa damu isiyo na hatia na ardhi ikatoa taarifa kwa mbingu kwamba mvua isinyeshe. Hii ni kwasababu ardhi inao uwezo wa kusikia, kutunza kile ilichosikia na kutekeleza kile ilichosemeshwa

Kumb 30:19-2019 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; 20 kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

Musa anapoongea na wana wa Israel anafanya mbingu na nchi kuwa shahidi ili ikumbukwe daima
Kumb 31:14-30“24 Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha, 25 ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la agano la Bwana akawaambia, 26 Twaeni chuo hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako. 27 Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi nikali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya Bwana; siuze nitakapokwisha kufa! 28 Nikutanishieni wazee wote wa kabila zenu, na maakida yenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao. 29 Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa Bwana kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu. 30 Musa akasema maneno ya wimbo huu masikioni mwa kusanyiko la wana wa Israeli hata yakaisha.” Kumb 32:1“1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.”

Yeremia 22:29-30“29 Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana. 30 Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.”

11.Ardhi inao uwezo wa kufurahi na kuwafurahisha wanaokaa juu yake kwasababu ya toba iliyofanywa ili kuirejesha ardhi kwa Mungu
Ardhi inayoomboleza inanyima Baraka kwa watoto wa Mungu, Yoeli 1:10“10 Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka.” Baada ya kwenda mbele za Mungu kwa toba Mungu anatoa Baraka juu ya ardhi, ardhi inafurahi na kutoa matunda kama tunavyosoma katika Yoeli 2:21“Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa Bwana ametenda mambo makuu.”
Unapoomba toba na kubomoa madhabahu za giza na kubariki ardhi nayo ardhi inafurahi

12.Mapepo yanaweza kumilikishwa ardhi na yakadai kisheria kuwa na uhalali wa kuwepo mahali pale walipomilikishwa
Hii ni moja ya sababu kubwa kwanini mapepo hukataa kuwaacha baadhi ya watu na kung’ang’ani kwa muda mrefu ili kuwatesa sana. Ikiwa ardhi imemilikishwa kwa miungu/mizimu/mapepo kwa njia ya ibada ya kipepo, uwe na hakika kuwa mapepo hayo hayawezi kukubali kuondoka katika hiyo ardhi kiurahisi rahisi kwani kisheria yamepewa uhalali wa kumiliki na kutawala eneo nao wanakuwa na hati miliki katika ulimwengu wa roho. Jambo hili lilimtokea Yesu mwenyewe alipoenda katika nchi ya wagerasi kama tunavyosoma katika Marko 5:1-17“1 Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; 4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. 6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. 8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. 9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. 10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. 11 Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. 12 Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. 13 Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. 14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea. 15 Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. 16 Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. 17 Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao.”
Hebu soma maneno haya kwa kutafakari ………10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile……….17 Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Mapepo yanamsihi Yesu asiwatoe nje ya mipaka ya nchi ile kwani walijua umiliki wao upo ndani ya mipaka ya nchi ile kisheria na jambo la kushangaza Yesu akawaacha ndani ya mipaka ya nchi ile.
Jambo la pili, wenyeji wa nchi ile wanamsihi Yesu aondoke mipakani mwao; yaani wamegundua kuwa Yesu anawaharibia mahusiano na miungu yao walioingia nao mikataba ili waimiliki ardhi ya Wagerasi.


HITIMISHO
Unapoona jambo limekusumbua muda mrefu na haupati majibu ya tatizo lako, shughulikia madhabhu na ardhi kwa kadiri ya mafundisho uliyopata katika somo hili

*Samson Mollel 0767 664 338*
_Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)_
*www.uzimawamileleministries.blogspot.com*