Monday, September 12, 2016

MANABII WA UONGO NA ROHO ZIDANGANYAZO - Samson Mollel (+255 767 664 338)

1Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.”

UTANGULIZI

Katika kanisa la leo kuna roho ya mpinga Kristo ambayo inafanya kazi kwa kasi sana, roho hii inafanya kazi ndani ya wakristo kuliko inavyofanya kazi kwa watu wa mataifa (wasio Wakristo). Hali hii imefanya Wakristo wengi kukosa imani na wahubiri (mitume, manabii, waalimu, wachungaji na wainjilisti) kutokana na aina za mahubiri yanayofundishwa, vilevile imesababisha Wakristo wengi kuzusha (Kuongea mambo ya uongo yasiyokuwepo kana kwamba yapo) na kwasababu hiyo uzushi mwingi umezuka ndani ya kanisa la Mungu na kuwasema vibaya watumishi wa Mungu. Hali hii ni mbaya sana kwani makuhani wa Mungu wameumizwa na maneno yasiyofaa na Wakristo wamejiingiza katika laana pasipo kujua kwakuwa Neno la Mungu linasema katika 1Nyakati 16:21-22 “21 Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; 22 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.” na Zaburi 105:14-15 “14 Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. 15 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Unapofanya jambo lolote kinyume na maelekezo ya Mungu huo ni uasi na katika uasi kuna adhabu, hivyo usitegemee jambo zuri unapokuwa unasema uzushi juu ya watumishi wa Mungu kwani wewe hujui ni gharama gani Mungu ametumia kuwakuza kufikia hapo walipo sasa. Hata kama unaona wamekengeuka ni bora ukafanya kama Daudi alivyokataa kumhukumu (Kumuua) Sauli pamoja na kwamba alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, sababu kubwa ilimzuia Daudi asimuue Sauli ni kwakuwa Sauli alipakwa mafuta na BWANA na Daudi alilifahamu Neno “…….Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.” Hivyo hakumdhuru Sauli japokuwa Sauli alikwisha kataliwa na BWANA.

Kwanini nimeanza na utangulizi mrefu hivyo? Ni kwasababu Wakristo wa leo wako tayari kwenda kwa waganga wa kienyeji na wakifika huko hutumia gharama kubwa bila kupona matatizo yao, lakini hata kama hawaponi huwezi kuwasikia Wakristo hao wakimsema mganga wa kienyeji kuwa ni muongo na mambo anayofanya hayafai. Sasa umkute mkristo huyo amejua jambo baya/ovu kuhusu mtumishi wa Mungu, yaani atazisambaza habari hizo kila atakapoweza kuzifikisha zitafika. Wakati mwingine hata hajashuhudia isipokuwa amesikia kuwa mtu wa Mungu amefanya uovu, basi mtu huyu atasimama na kulihubiri lile jambo baya kwa nguvu zote; hawa ndio huitwa watu wasiofaa ambao wako tayari kusema lolote baya ili injili ya Kristo isihubiriwe. Watu wa namna hii walikuwepo kuanzia agano la kale na hata wakati wa Yesu wanaonekana wakisema uongo ili kumzuia Yesu kuhubiri habari za wokovu.
Tazama habari za mfalme Ahabu, mkewe Yezebel na Nabothi katika 1Wafalme 21:1-16 “……8 Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. 9 Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, 10 mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.”……….. 13 Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa……….”

Nataka nikuoneshe kwamba kuna watu wasiofaa wanaoweza kuzusha maneno ya uongo ambayo hayana ukweli na wakatoa ushahidi wa uongo na mwisho kupotosha ukweli wote. Vievile tunasoma katika Mathayo 26: 3-4 “3 Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; 4 wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.”. Tunaona viongozi wa dini wa wakati huo walifanya hila ili kumkamata Yesu, yaani waliandaa uzushi tu ili kumkamata Yesu kama unavyofahamu walizusha mashataka mengi ya uongo juu ya Masihi wa BWANA.

Nimeanza na utangulizi huu ili unaposoma somo hili ujue kwamba manabii wa uongo na wapinga Kristo wapo kwa pande mbili, yaani wale wanaosimama madhabahuni na wale washirika/waumini wanaozusha uongo ili kuizuia injili ya Yesu isisonge mbele.

NI KWELI WAPO WANAOMPINGA KRISTO?

Ni kweli kabisa wapo watu ambao ndani yao kuna roho zinaofanya kazi maalum ya kupinga ukristo usikue, yaani wanaudhoofisha ukristo usifike kwa wale waliokusudiwa na hata kama ikiwafikia iwe imepotoshwa au kuifanya mioyo ya watu kuwa migumu kiasi cha kushindwa kulipokea Neno la Kristo watu hawa hujiingiza kwa siri ili kuliharibu kusudi la Mungu katikati ya watu wake sawa na Neno la Mungu kutoka Yuda 1:3-4, 12-13 “3 Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. 4 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo…..12 Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; 13 ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.”.
Wapinga Kristo hawa nimewagawanya katika makundi haya yafuatayo:-

Ø  Manabii wa uongo
Wapo manabii ambao ni wa uongo, hao hunena yakwao na kuwaambia watu kuwa BWANA amesema ile hali sio BWANA aliyesema ila wamesema wenyewe kwa tamaa zao wenyewe, Yesu anasema katika Mathayo 7:15 “15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.” Hivyo ni kweli wapo manabii wa uongo na kwa muonekano ni kama wanamuhubiri Kristo lakini kiuhalisia wanayo makusudi tofauti na kumhubiri Kristo. Hii ni hatari kwa wakristo hasa kanisa la Mungu, ndio maana Yohana anaonya katika moja ya nyaraka zake, 1Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” Ndio maana hata mimi leo nakuambia usiamini kila roho, ukisikia hili neon “USIAMINI KILA ROHO” tafadhali kuwa makini kwani haimaanishi kuwa roho ya nabii itakuja na kukusemesha nje ya mwili, Hapana! Maana yake ni kwamba roho hizi hukaa ndani ya mwili/miili ya watu/wanadamu kisha kuwahubiria watu wa Mungu kwa nia ya kuwapotosha.


Ø  Roho zidanganyazo
Wengi wetu tayari tunafahamu kwamba moja ya kazi zilizo kuu kabisa za ibilisi ni kudanganya. Yeye anaitwa baba wa uongo, kazi yake kubwa ni kuudanganya ulimwengu wote. (Ufunuo 12:9 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.”). vilevile Yesu mwenyewe anamtaja shetani kama baba wa uongo katika Injili ya Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Zipo roho zinazodanganya kabisa na kusema uongo kwa habari ya Kristo Yesu, lengo ni kuwapa watu mafundisho yasiyofaa na kuwaaminisha kuwa ndio mafundisho ya kweli ili kulipotosha lile kusudi la Mungu ambaye ndiye KWELI. Na kwasababu hiyo Roho Mtakatifu anatufunulia wazi kuwa zipo roho zidanganyazo ndani ya kanisa la Mungu 1Timotheo 4:1 “1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

Ø  Wapinga Kristo katika watu wa Mungu
Wapo watu ambao ni wanamaombi wenzetu na tunaabudu nao katika faragha (Fellowship), lakini watu hawa hawaamini katika matendo ya Roho Mtakatifu na hivyo kushindana na kazi za Mungu zinazofanywa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; watu hawa utawasikia wakisema kuwa anayetenda hayo matendo sio Mungu (Labda kwasababu ya wivu wa kihuduma unaoletwa na ibilisi) na kuleta mafarakano na kutoelewana katikati ya watoto wa Mungu. Tunasoma kuwa roho hii ilianza kupambana na Yesu mwenyewe pale alipoanza kuwafungua watu waliosetwa Marko 3:22 “Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.” Kumbe upinzani haujaanza leo, ndio maana mtume Yohana anasema katika waraka wake 1Yohana 2:18-19 “18 Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. 19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.”. anachosema Yohana hapa ni hiki, watu hawa (wenye roho ya mpinga Kristo) wanatoka katikati yetu.

Ø  Walimu wa uongo
Neno la Mungu linatuthibitishia uwepo wa waalimu wa uongo katika kipindi cha mitume na pia Neno linatuthibitishia kuwa hata sasa hao walimu wa uongo wapo! 2Petro 2:1“Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.” Hawa ni wale wanotoa mafundisho ya uongo, yapo mafundisho mengi sana ya uongo; wapo wanaosema Yesu hakufufuka, wengine wanasema sio Mungu, wapo wasemao hakuna ulimwengu wa roho na hakuna ufufuo wa wafu n.k. Vilevile tunasoma katika 2Thesalonike 2:1-4 “1 Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, 2 kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. 3 Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; 4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” Hivyo tuwe wasomaji wa Neno la Mungu ili tuijue kweli tusipotoshwe na mambo ya ulimwengu huu.

UNABII WA UONGO UNALETWA NA NANI?

Unabii wa uongo/roho ya mpinga Kristo inaletwa na shetani mwenyewe kwakuwa yeye ndiye baba wa mafarakano na kazi yake ni kuhakikisha anaharibu kwa kutumia njia zozote, ndio maana Yesu anasema katika Injili ya Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Vilevile tunasoma kuwa kazi ya shetani (mwizi) ni uharibifu Yohana 10:10 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”

Hebu tuutazame mfano mmoja wa jinsi shetani anavyoweza kuleta unabii wa uongo wakati watu wakidhani kuwa ni Mungu kasema. 1Wafalme 22:20-23 “20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. 22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. 23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.” Hapa tunajifunza kuwa nguvu za giza zinaweza kugeuka kuwa kitu chochote kwamfano huyu pepo hakuwa pepo wa uongo ila alisema atageuka kuwa pepo wa uongo “……Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote…….” Hii ndio hali ya kanisa la sasa, mtu yoyote hata mchungaji/mwinjilisti/padre/n.k anaweza kuingiwa na roho (akawa nabii wa uongo/mpinga Kristo).

UTAWATAMBUAJE MANABII WA UONGO?

Namna kuu ya kuwatambua manabii wa uongo ni kwa kutumia Neno la Mungu ambalo lipo ndani yetu; nasema “NENO LA MUNGU AMBALO LIPO NDANI YETU”na sio Neno la Mungu lililoandikwa katika kitabu kitakatifu yaani Biblia, kwakuwa wakati unapokutana na mafundisho ya uongo/udanganyifu kutoka kwa manabii wa uongo unapaswa kupima kwa kutumia Neno lililopo ndani yako; ndio maana Biblia inasema katika Wakolosai 3:16 “16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”

Vilevile wakati unakabiliana na manabii wa uongo pamoja na mafundisho ya uongo (nguvu za giza), Neno la Mungu lililopo ndani yako linageuka na kuwa taa ya kumulika ili kukuonesha ni wapi uendako sawasawa na linavyosema Neno la Mungu katika Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”

Zaidi sana Neno la Mungu likiwa ndani yetu linaishi na linatenda mambo makuu ikiwa ni pamoja na kuijua nia ya mtu yeyote iliyo mbaya, hivyo Neno la Mungu lililopo ndani yetu linatuambia yupi ni nabii wa kweli na yupi ni wa uongo kwani linakuwa ni mizani ya kupimia unabii wowote, ukisoma Waebrania 4:12-13 “12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”

Maelezo machache ya kutumia Neno la Mungu kuwatambua manabii wa uongo
         i.            Msikilize mtumishi (nabii/mwalimu/….) anasema nini kuhusu Yesu, katika Mathayo 16:15-16 “15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? 16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Tunaona hapa Petro anamkiri Yesu kuwa ni Kristo mwana wa Mungu aliye hai, ukimkuta mtumishi hawezi kumkiri Yesu kuwa ni Kristo na mwana wa Mungu aliye hai basi huyo ni nabii wa uongo, Neno la Mungu linasema katika 2 Yohana 1:9-10 “9 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. 10 Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.” Mafundisho hayo ni yapi ambayo Yohana anasisitiza kuwa watu wanaofundisha wasikaribishwe? Ukisoma 1Yohana 2:22-23 “22 Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. 23 Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.” Yoyote amkanaye Yesu Kuwa ni Kristo  huyo ndiye mpinga Kristo na ndio zile roho zidanganyazo  watu wa Mungu na kuleta mafarakano katika kanisa la            Mungu.

       ii.            Je! Huyo mwalimu anamiliki tabia ambazo zinamtukuza Mungu? Anaonya juu ya walimu wa uongo kama vile tunavyosoma katika Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora.” Kwa njia nyingine, mwalimu wa uongo anaweza kujulikana kwa kiburi chake (Kaini aliukataa mpango wa Mungu), tamaa (Balaamu anatabiri kwa ujira), na maasi (Kora anajinua zaidi ya Musa). Yesu alisema tuwe macho na watu kama hao na kwamba tutawajua kwa matunda yao (Mathayo 7:15-20).


Kama nilivyoanza hapo awali, sio lengo la mafundisho haya kukufanya usiamini manabii wa Mungu aliye hai ila ni kukupa ufahamu ili uweze kujitambua na kutambua kuwa hizi ni nyakati za mwisho na sehemu kubwa ya unabii ulionenwa na Manabii na Mitume imekwishatimia, kama tunavyosoma katika 1Wathesalonike 5:16-22 “16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. 19 Msimzimishe Roho; 20 msitweze unabii; 21 jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; 22 jitengeni na ubaya wa kila namna.” Maana yake ni kwamba, kwa nguvu ya Neno la Mungu tunaweza kuupima unabii na manabii wa namna zote na kujiridhisha kama wametokana na Mungu au la!.




1 comment:

Anonymous said...

Slot Search: Play Free Online Casino Sites
Welcome to LuckyClub. Live Slot Search and Win Cash Prizes for over 100 online casinos with different luckyclub.live game modes including video slots, video poker, Top Real Money: $7 Million (2020)Best Real Money: $1,000,000 (2020)Best for: Top 5Most Popular Online Slots: Play For Free And Win BigSlot Name: Free Slot Games & MoreAre there other options to get the best experience playing free slots online?Is it safe to play free slot games online?