Thursday, February 20, 2020

SOMO: ADHABU ILIYOBEBWA NA KITI CHA ENZI (Samson Mollel 0767/0713 – 664 338)


Kiti cha enzi ni nafasi ya utawala iliyopo katika ulimwengu wa roho ambayo ina mamlaka kwenye maisha ya watu, nafasi ya kiti cha enzi ipo rohoni lakini utendaji wake unaonekana kwa jinsi ya mwili pia. Nafasi inaweza kuwa katika ngazi ya kifamilia, Kijamii, Ofisini, Kanisani, Kisiasa, Ukoo n.k
Viti vya enzi viliumbwa na Yesu Kristo kwa ajili yake yeye kuvitumia kwa utukufu wake.

Wakolosai 1:16 “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.”

Yohana 1:1-3 “1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

Mifano ya viti vya enzi vya Yesu Kristo:

v  Kiti cha rehema
Walawi 16:2 “Bwana akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema.”

v  Kiticha Hukumu
2Korintho 5:10 “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”

v  Kiti cha Daudi
Luka 1:31-3231 Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. 32 Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.”

v  Kiti cha enzi cha Mwana-Kondoo
Ufunuo 22:1 “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,”

HATA SHETANI NAYE ANA VITI VYA ENZI
Ufunuo 13: 1-2 “1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. 2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”

Ufunuo 2:12-13 “12 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili. 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.”


MAMBO MUHIMU YA KUFAHAMU KUHUSU VITI VYA ENZI
a.      Unaweza kukalia nafasi inayomilikiwa kiroho na mtu mwingine na ukafanya maamuzi nje ya ufahamu wako kwa kuongozwa na kiti cha enzi ulichokalia

Mathayo 23:1-3 “1 Kisha Yesu akawaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, 2 Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; 3 basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.”

Inawezekana umekaa kwenye kiti cha enzi cha babu wa ukoo au bibi wa ukoo au mganga wa ukoo au mzimu wa ukoo na hata sasa maamuzi unayofanya sio unayotaka kufanya bali unalazimishwa na kiti ulichokalia. Inawezekana uzito wa kusoma Neno la Mungu na kuomba umetokana na kiti ulichokalia, inawezekana umasikini na magonjwa n.k. vimetokana na kiti ulichokikalia

b.      Kiti cha enzi kinaweza kufanya vita kutoka rohoni na kuyaharibu maisha ya mtu kabisa

Ufunuo 13:1-7 “2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. ……..4 Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? ……… 7 Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.”

Kiti cha enzi kinaweza kufanya vita na kazi yako, huduma yako, ndoa yako, biashara yako, elimu ya watoto wako na kiti kikakushinda na ukaathirika na kuaibika vibaya sana. Kwa lugha rahisi naweza kusema kwamba kiti ni silaha na ndio maana joka anatoa kiti kama sila na yule mnyama anawashinda hadi watakatifu wa Mungu.

c.       Kiti cha enzi kinaweza kumilikiwa na Mungu au miungu

Kutoka 12:12, 29 “12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. 29 Hata ikawa, usiku wa manane Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. 30 Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu.”

Swali la kujiuliza hapa; ni kwanini Mungu anapiga wazaliwa wa kwanza na hukumu juu ya miungu inatolewa? Kumbe kiti cha enzi cha farao kilitolewa kwa miungu na wazaliwa wa kwanza ndio waliokuwa sadaka (kafara) katika viti hivyo. Kwahiyo viti vya enzi vya Misri vilikwisha kutolewa kafara ili vimilikiwe na miungu ya Misri na kafara yenyewe ni mzaliwa wa kwanza; hivyo basi ukipiga mzaliwa kwanza unaiharibu nguvu ya kiti cha enzi inayotegemea kafara ya mzaliwa wa kwanza.


KITI CHA ENZI KINAWEZA KUBEBA ADHABU/LAANA NA WEWE UKAKETI KATIKA KITI CHA ENZI NA KUIPOKEA HIYO LAANA HATA KAMA WEWE NI MTAKATIFU

ü  Daudi alitumikia adhabu ya kiti cha enzi iliyosababishwa na mfalme Sauli

2Samweli 21:1-3 “1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni. 2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;) 3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa Bwana?”

Kumbuka aliyewaua Wagibeoni ni Sauli akiwa katika kiti cha enzi cha mfalme wa Israeli, lakini baada ya Sauli kufa na kuachia madaraka bado adhabu ipo katika kiti cha enzi. Daudi alikuwa mtu aliyempenda sana Mungu na kumpendeza sana kwani hakufanya kosa lolote ispokuwa lile la Uria, lakini adhabu ilimfuata pamoja na uhusiano mzuri na Mungu wake.

Ninasema na wewe mtu uliyeokoka ambaye leo upo kwenye adhabu ya kiti cha enzi kutokana na makosa ambayo hukuyatenda wewe bali walitenda watangulizi wako. Inawezekana adhabu katika kazi yako ilitokana na mtangulizi wako, inawezekana adhabu ya umasikini imetokana na wazazi wako inawezekana tatizo katika huduma yako imetokana na watangulizi wako.

ü  Yoramu alitumikia adhabu ya mauti katika kiti cha enzi iliyosababishwa na mfamle Ahabu (baba yake)

Kwa wewe ambaye unapenda kusoma Neno la Mungu utakumbuka kwamba hakuna mfalme katika Israeli aliyetenda mambo ya hovyo na maovu kama mfalame Ahabu kwa kushawishiwa na mke wake ambaye alikuwa mzinzi na mchawi

1Wafalme 21:25-26 “25 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. 26 Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”

Kutokana na uovu huo aliotenda katika nafasi yake ya ufalme ambao ulimkasirisha sana Mungu, Mungu akatuma Neno la kinabii kupitia mtumishi wake nabii Eliya Mtishbi na kumueleza juu ya adhabu inayokuja mbele yake kwaajili ya dhambi aliyoitenda.

1Falme 21:17-24 “17 Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, 18 Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. 19 Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. 20 Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana. 21 Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. 22 Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. 23 Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. 24 Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla.”

Lakini mfalme Ahabu alipoyasikia maneno yale alianguka mbele za Mungu na kuomba toba na Mungu akamsikia na kumsamehe Ahabu yeye binafsi, lakini kumbe Ahabu hakukumbuka kuomba toba kwaajili ya nafasi/kiti cha enzi cha mfalme. Kwasababu hiyo adhabu ikabakia katika kiti cha mfalme ikisubiria atakayekuja ili aitumikie.

1Falme 21:28-29 “27 Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.28 Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, 29 Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.”

Baada ya mfalme Ahabu kufa, mtoto wake aitwaye Yoramu akachukua nafasi katika kiti cha enzi cha ufalme kutoka kwa baba yake. Kipindi Yoramu anachukua nafasi ya ufalme kumbuka kwamba nabii Eliya aliyeleta taarifa za adhabu alikuwa ameshachukuliwa mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.

Mungu akamtumia nabii Elisha, Elisha akamtuma kijana ampake mafuta Yehu ili akaingamize familia ya mfalme Ahabu (2Falme 9:1-10)

Huku Yoramu akijua kwamba kuna amani, Mungu akamtumia Yehu mmoja wa majemedari wake kumwangamiza kwa kosa ambalo alilifanya Mfalme Ahabu. Yoramu pamoja na mama yake (Yezebeli) wakaangamia.

2Falme 9:21-24 “21 Yoramu akasema, Tandika gari. Wakalitandika gari lake. Yoramu mfalme wa Israeli akatoka, na Ahazia mfalme wa Yuda, kila mtu katika gari lake. Wakatoka ili kumlaki Yehu, wakamkuta katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli. 22 Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi? 23 Yoramu akageuza mikono yake, akakimbia, akamwambia Ahazia, Ni uhaini, Ahazia. 24 Yehu akavuta upinde wake kwa nguvu zake zote, akampiga Yoramu kati ya mikono yake, hata mshale ukamtoka penye moyo wake, akaanguka katika gari lake.”

ü  Wazaliwa wa kwanza katika nchi ya Misri walitumikia adhabu ya kiti cha enzi
Kutoka 12:12, 29 “12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. 29 Hata ikawa, usiku wa manane Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. 30 Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu.”

Swali la kujiuliza hapa; ni kwanini Mungu anapiga wazaliwa wa kwanza na hukumu juu ya miungu inatolewa? Kumbe kiti cha enzi cha farao kilitolewa kwa miungu na wazaliwa wa kwanza ndio waliokuwa sadaka (kafara) katika viti hivyo. Kwahiyo viti vya enzi vya Misri vilikwisha kutolewa kafara ili vimilikiwe na miungu ya Misri na kafara yenyewe ni mzaliwa wa kwanza; hivyo basi ukipiga mzaliwa kwanza unaiharibu nguvu ya kiti cha enzi inayotegemea kafara ya mzaliwa wa kwanza.

Inawezekana wazaliwa wa kwanza katika nchi ya Misri hawakujua mahusiano yao na viti vya enzi vya miungu ya Misri, hata wewe inawezekana haujui kwanini unapata taabu kila ndugu zako wakitoa kafara katika familia yako. Tatizo ni kwamba umeungamanishwa na kiti cha enzi cha mizimu ya nyumbani kwenu na kila wanapopewa sadaka wanakuadhibu wewe kwa kutofuata sheria yao.

ü  Biashara kuanguka kutokana na kiti cha enzi kuanguka

Kuna watu wamerithi biashara kutoka kwa wazazi wao au kutoka kwa marafiki/ndugu. Halafu baadae Yule mwanzilishi wa biashara anapokufa na biashara zake zote zinaanguka na kufa kabisa.

Kuna watu walikuwa wakifanya biashara na babeli mkuu mama wa makahaba na machukizo ya nchi, ulipoangushwa ule mji (unaoonekana kwa sura ya mwanamke kahaba) wafanyabiashara nao wakaanguka
Ufunuo 17:1-3 “1 Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi; 2 ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake. 3 Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.”

Ufunuo 18:1-3, 17-19 “1 Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. 2 Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; 3 kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake….. 17 kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa. Na kila nahodha na kila aendaye mahali popote kwa matanga, na mabaharia, nao wote watendao kazi baharini, wakasimama mbali; 18 wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio mfano wa mji huu mkubwa! 19 Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa.”

ü  Ibada ya miungu inayobebwa na kiti cha enzi cha familia/ukoo

Wafalme wawili waliotawala nchi ya Israeli kwa wakati mmoja walikalia kiti kilichokabidhiwa kwa miungu na baba yao (mfalme Sulemani) pasipo wao kujua na kile kiti kikawalazimisha wao kutenda uovu mbele za Mungu wa Israeli. Mfalme Sulemani alipendwa na Mungu na alibarikiwa sana, Mungu alimtokea mara mbili na kumuonya Sulemani asioe wake wa nchi za kigeni lakini yeye hakusikia akawaoa nao wakambadilisha kutoka kuwa mtumishi wa Mungu wa kweli hadi kuwa muabudu miungu ya kigeni kama tunavyosoma katika Neno la Mungu:

1Falme 11:4-13 “4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. 5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. 7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. 8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu. 9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, 10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana. 11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. 12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako. 13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.”

Baada ya Sulemani kumaliza utawala wake ufalme ukaenda kwa Yerobuamu (mtumishi wa mfalme) ambaye alichukua kabila 10 za Israeli na mtoto wa mfalme Rehoboamu alibakiwa na kabila 2 tu za Yuda na Yerusalemu.

Kumbe bila kujua kiti alichokalia kina nguvu ya miungu, Yeroboamu akaanza na yeye kuyafanya machukizo mabaya hata kuliko aliyafanya mfalame Sulemani kama yanenavyo maandiko

1Falme 12:25-29 “25 Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli. 26 Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. 27 Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda. 28 Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng'ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. 29 Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani.”

Kilichomsumbua Yeroboamu ni kiti (nafasi) ambayo tayari Mfalme Sulemani alikuwa ameikabidhi kwa miungu ya kigeni. Lakini haikushia hapo, Rehoboamu pamoja na kupewa kabila mbili tu bado alizidiwa na nguvu ya kiti ambacho kilikabidhiwa kwa miungu sawa na Neno la Mungu:

1Falme 14:21-24 “21 Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. 22 Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa Bwana; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. 23 Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. 24 Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.”

Kumbe inawezekana uzinzi, uasherati, uganga, ushirikina, umbea, wizi, uongo, ulevi, ugojwa wako wewe unasukumwa tu na kiti cha enzi cha ukoo ambacho umekalia (inawezekana ni nafasi ya mzaliwa kwanza au wa mwisho, nafasi ya mkuu wa ukoo au baba/mama wa familia n.k.).

ü  Kiti cha enzi kinaweza kubeba mauti ya yule aliyeikalia

Inawezekana tangu ulipokalia kiti cha enzi (nafasi uliyopewa mahali fulani) ndipo shida na matatizo ya maisha yako yalipoanzia mpaka sasa. Unaweza kukalia kiti (nafasi) ambayo ndani yake imebeba mauti ya ndoa yako, kazi yako, uchumba wako, elimu yako, uchumi wako, maisha yako n.k.

Biblia inatufundisha habari za mtu ambaye alipewa nafasi iliyobeba mauti yake mwenyewe na alikufa mara baada ya kukalia hicho kiti

2Samweli 11:14-17 “14 Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. 15 Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. 16 Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. 17 Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.”

UNAPOKETI KWENYE KITI CHA ENZI UNAPOKEA MAMLAKA YA KITI

Kila anayekiti katika kiti chochote cha enzi anapokea mamlaka ya kile kiti katika utendaji wake, hii ndio sababu mapepo na wachawi wanawasumbua sana wanadamu pamoja na ukweli kwamba shetani aliye mkuu wao amefungwa kuzimu na muda wake ukifika atafunguliwa kwa muda mfupi tu; (Ufunuo 20:1-3 “1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; 3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.”).

Kinachowapa nguvu mapepo na wachawi ni kwasababu yule joka baada ya kuona hawezi kutoka na kuwatesa watoto wa Mungu yeye mwenyewe ameamua kutoa urithi wa kiti chake cha enzi (nafasi yake katika ulimwengu wa roho) kwa wale waliokubali kumtumikia kwa uaminifu kama yanenavyo maandiko

Ufunuo 13:1-2,7 “1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. 2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi….7 Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.”

Wote walipokea kiti cha enzi cha shetani (Yule joka) wanatenda kama yule joka, wana nguvu na uweza wa yule joka.
Jambo ambalo wakristo wengi hawafahamu ni kwamba Mungu (Jehova) ametupa kiti chake cha enzi ili tutembee na nguvu zake na uweza wake. Baada ya kuona tumeteswa sana na yule joka, Mungu kwa neema yake akamtuma mwana wake Yesu Kristo ilia aje duniani na kufa kwaajili ya kuturithisha agano ambalo linatupa nafasi kuwa wana wa Mungu (Waebrania 9:16-18 “16 Maana agano la urithi lilipo, lazima iwepo mauti yake aliyelifanya. 17 Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya. 18 Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu.”)

Kwasababu Yesu alimwaga damu yake na akafa mauti ili agano la urithi litimie, kwahiyo wote wanaomkubali Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao wanaingizwa katika agano la urithi kwa njia ya damu ya Yesu na mauti ya Yesu pale msalabani.

Unapopokea urithi huu unakuwa na nguvu za Mungu na uweza wa Mungu katika kutenda kama Mungu mwenyewe (Rumi 8:16-17 “16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”).

Urithi tulioupata ni kupewa kuketi katika Kiti cha Enzi cha Mungu Mwenyewe pamoja na Kristo na kutiisha na kutawala viti vingine vyote hata kile kiti cha enzi cha joka (shetani), tumepewa mamlaka kubwa sana inayotoka katika kiti tulichopewa kukikalia sawasawa na Neno la Mungu.

Waefeso 2:6, 1:21-22 “6 Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;….. 21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”

Unapokaa kwenye kiti cha enzi cha Yesu unapokea mamlaka ya kimbingu na uweza wa kutenda kama Yesu kwa jina la Yesu.


MAOMBI:

ü Maombi ya toba ya kujitoa katika viti vya enzi vya ukoo, mizimu, uganga, uchawi, uzinzi, ushirikina, umasikini, ulevi………. (Zaburi 51:1-19, Danieli 9:1-19)

ü Pindua viti vya enzi vya ukoo, mizimu, uganga, uchawi, uzinzi, ushirikina, umasikini, ulevi…………….. (Ezekieli 21:26-27, Yeremia 1:10)


ü Simamisha/ketisha kiti cha enzi cha Yesu katika miasha yako (Familia, ukoo, kazini, ofisini, kanisani, huduma, ndoa……), ukiisha kukisimamisha/kukiketisha na wewe ukae katika kiti hicho cha Yesu Kristo na umiliki na kutawala (Ezekieli 21:26-27, Yeremia 1:10, Waefeso 2:6)

No comments: