Thursday, July 23, 2015

MIMI NI ASILI YA MBINGUNI (Samson Mollel - Uzima wa Milele International Ministries)

Nimefunuliwa juu ya somo hili kwaajili yako ili kukupa ujasiri na nguvu zaidi za rohoni kwa kuifahamu kweli na kuwa na maarifa ya Mbinguni yatakayo kuwezesha kujua Neno la Mungu na uweza wa Mungu. Neno la Mungu linasema katika injili ya Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Hatujui yakuwa sisi ni watoto wa Mungu kwakua Neno la Mungu linasema hivi “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” Yohana 1:12. Kama wewe ni mtoto wa Mungu na Mungu wetu anakaa mbinguni basi wewe pia ni wa asili ya Mbinguni. Kuthibisha hili; Biblia inasema katika 1Yohana 3:9-10 “9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. 10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” Katika mistari hii tunajifunza yakuwa Mungu anazaa watoto ambao ni wale waliompokea Yesu Kristo, na wale waliozaliwa na Mungu uenyeji wao ni Mbinguni yaani wanayo asili ya Mbinguni. Hata hivyo usisahau kwamba kuna watoto wa ibilisi ambao watachomwa moto pamoja na baba yao ibilisi.
Ninakupa moyo mtu wa Mungu ya kuwa ukiijua nafasi yako katika ufalme wa Mungu na kuliamini Neno la Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya 55:10-11 “10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.” Basi hakika ni kwamba utafanikiwa katika mambo yote sawasawa na Neno laMungu.
Karibu msomaji wangu ujifunze baadhi ya mambo yatakayokupa ujasiri wa nafasi yako katika ufalme wa Mungu.



1.      MIMI NI MFANO NA SURA YA MUNGU
Biblia inasema wazi kwamba hapo mwanzo Mungu aliamua kumuumba mtu kwa mfano wake (Mungu) na kwa sura yake (Mungu) mwenyewe kama tunavyosoma katika maandiko matakatifu katika kitabu cha Mwanzo 1:26 – 27 “26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Nataka ufahamu kwa uhakika ya kwamba mtu anayeongelewa hapa ni ROHO na sio mwili kama vile watu wengi wanavyodhani, unaposikia wewe ni mfano wa Mungu, basi fahamu anayeongelewa hapa ni mtu wa ndani (Roho yako) ndiye mfano wa Mungu. Uhakika wa kwamba mtu ni roho tunaupata katika maandiko matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu yeye ni ROHO hivyo yoyote aliye mfano wa Mungu naye pia ni ROHO kama tunavyosoma katika kitabu cha Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”.
Nataka nikupe uhakika ya kwamba umepewa nafasi kubwa sana katika ulimwengu wa mwili na ulimwengu wa roho, nafasi hiyo ni kuwa sura yake Mungu kama vile alivyo Kristo Yesu (2Korintho 4:4  “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”), kumbe nasisi tumepewa nafasi kama ile ya Yesu kama tunavyosoma katika Mwanzo 1:26 “26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Kuwa sura yake Mungu maana yake ni kuwa ishara na kielelezo cha Nguvu, Uweza, Mamlaka, Utukufu na Ukuu wa Mungu kila tutakapokuwa na ndio maana tukapewa kumiliki na kutawala.


2.      NDINYI MIUNGU (MIMI NI MIUNGU)
Muimba zaburi anasema katika Zaburi 8:4-5 “4 Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? 5 Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima”. Mungu amemfanya Mtu/Mwanadamu kuwa baada tu ya Mungu, yaani kimamlaka unaweza kusema Mtu/Mwanadamu ndi wa pili kwa nguvu kutoka kwa Mungu. Ni kama vile nchi ambayo inayoviongozi wakuu wawili yaani raisi (mwenye nchi) na waziri mkuu (Mtendaji mkuu wa serikali) ndivyo ilivyo katika utawala wa Mungu, yaani Mungu (Muumbaji wa vitu vyote) na Mwandamu (Mmiliki na mtawala/mtendaji). Katika injili kama ilivyoandikwa na Yohana 10:34 “Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?” vile vile tunasoma katika Zaburi 82:6 “6 Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”. kwahiyo tunao uthibitisho kwamba sisi tumepewa nafasi ya UUNGU, yaani baada ya Mungu ni mimi mwanadamu.

3.      MIMI NI HEKALU LA MUNGU
Bwana Yesu alipoileta kweli ulimwenguni, alihamisha hekalu la Yerusalemu na kuwa mwili wake kwa yule mwenye kuamini kama vile alivyoamisha sanduku la agano na kutufanya sisi ndio sanduku la agano jipya amabapo Mungu anakaa ndani yetu. Bwana Yesu akaleta wokovu kwa mwanadamu kwamba inatupasa tuokoke ili miili yetu ifanyike hekalu la Roho mtakatifu kama ilivyoandikwa katika 1Kor 3:16 - 17 “16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” Vilevile imeandikwa katika 2Kor 6:16, 18 “16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu…………18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”. Mtu wa Mungu hebu turudi nyuma kidogo tuangalie katika hekalu la wayahudi ambapo Mungu alikaa ndani yake na kulikuwa na nguvu kubwa kiasi gani.
Tunasoma katika Kutoka 30:10 “Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa Bwana.” Tunaona katika patakatifu pa patakatifu ndipo Haruni alipokutana na Mungu mara moja tu kwa mwaka ili kufanya upatanisho wa dhambi za wana wa Israeli, kwa kifupi Mungu alishuka ndani ya hekalu patakatifu pa patakatifu ili kukutana na kuhani aliyebeba sadaka ya upatanisho. Baada ya kufa kwa Yesu Kristo kuna jambo lililotokea ambalo lilibadisha kabisa taratibu za awali kama tunavyosoma katika  Waebrania 9:12-14 “12 wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; 14 basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”. Sasa miili yetu ndiyo imekuwa hekalu la Mungu mwenyewe na ndiye anaishi ndani yetu.
Ndugu fahamu kwamba Mungu aishiye ndani yako (Kwakuwa wewe ni hekalu la Mungu) ndiye Mungu yuleyule aliyeumba mbingu na dunia, ndiye yule aliyewavusha Israeli katika bahari ya shamu, ndiye yuleyule aliwaokoa Shedrack, Meshack na Abednego kutoka katika ule moto mkali sana na ndiye aliyemuokoa Daniel na makanwa ya samba wenye njaa kali; vile vile huyu ndiye Mungu wa Eliya, Elisha, Daudi na manabii na mitume wakubwa katika Biblia. Swali ni hili sasa; Iweje huyu Mungu mwenye nguvu kuu namna hii anaishi ndani yako halafu wewe kila siku unalalamika kwamba unaonewa na nguvu za giza, unalalamika kuporomoka kiuchumi, unalalamika afya yako kuvurugika; AMKA!!! Tambua nguvu inayofanya kazi ndani yako! Tambua ya kwamba Mungu mwenye nguvu za kutisha yupo ndani yako, amini kwamba anaweza nayeye atatenda jambo kubwa sana katika maisha yak oleo.
MAOMBI
Katika jina la Yesu Kristo nimetambua leo yakwamba mimi ni hekalu la BWANA na Roho wa BWANA anakaa ndani yangu, na kwakuwa Mungu anakaa ndani yangu Neno la Mungu linasema katika Waebrania 12:29 “maana Mungu wetu ni moto ulao”. Chochote kilichokaa ndani yangu kutoka katika ufalme wa giza nakiamuru kiteketee kwa moto wa BWANA aishiye ndani yangu, vyakula vya kichawi/kipepo nilivyolishwa katika ulimwengu wa roho naamuru viteketee kwa moto ulao katika jina la Yesu. Magonjwa ya aina zote naamuru yateketee kwa moto ulao katika jina la Yesu, Amen.

4.      MIMI NI TAWI NA MUNGU NI SHINA LANGU
Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”
Ukiisha kumpokea Yesu, Yesu anasema wewe unakuwa tawi lake na yeye (Yesu Kristo) anakuwa Shina. Sasa ufahamu ya kuwa mti hutambulikana kwa matawi yake kasha kwa matunda yake, maana yeke ni; Mti/Shina ni Yesu Kristo, ili uweze kuutambua mti/shina inabidi utazame matawi yake na matunda yake yaani Mkristo na yale anayoyatenda (Ukitaka kumtambua Kristo Yesu inabidi umuangalie Mkristo na matendo yake). Kama ilivyo kwa mti wa kawaida, chakula kinachopita katika shina ndicho kinachoingia katika matawi, hii inamaanisha kwamba kwakuwa sisi ni matawi ya Kristo Yesu, basi kila kinachotoka kwake Yesu ndicho kinaingia kwetu. Nguvu alizonazo Yesu zinaingia kwetu kwani tumeunganishwa na Yesu sawasawa na Neno lake kutoka Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi……..)
Mtu wa Mungu AMKA!!! Fahamu yakuwa upako alionao Yesu Kristo unaingia na kwako pia, fahamu ya kuwa Nguvu, Uponyaji, Baraka, Maarifa, Uweza na kila kilichopo kwa Yesu ni cha kwako. Fahamu yakuwa hakuna kinachopita katika shina kisiingie katika matawi.
MAOMBI (Omba kwa sauti kama unaweza)
Wewe shetani!! Wewe ni nani hata uweze kukaa katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi, Kazi, Mahusiano, Kibali na upendeleo!!!! Mimi nimejua, nifahamu ya kuwa mimi ni sehemu ya Yesu Kristo na kila kinachotoka kwa Yesu Kristo kinaingia na kwangu. Katika Jina Lenye Nguvu sana Jina la Yesu Kristo nakuamua TOKAAAA!!! Katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi, Kazi, Mahusiano, Kibali na upendeleo, ACHIAAA!!! Kwa Jina la Yesu kila ulichoshikilia katika maisha yangu katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareth. Chochote kilichojishikamanisha na maisha yangu naamuru kikutane na nguvu ya damu ya Yesu kwakuwa imeandikwa katika Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Namimi nakushinda shetani kwa damu ya Yesu Kristo katika jina la Yesu, Amen.

5.      MIMI NI MBONI YA JICHO LA MUNGU
Zekaria 2:8.Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.”
Jaribu kufikiri katika hali ya kawaida kabisa ambayo wewe ni mwanadamu ambaye unavyo viungo vingi na kimojawapo ni jicho, ndani ya jicho kuna kitu muhimu sana ambacho ni “mboni”. Kama ikitokea mdudu au kitu chochote kinaelekea kuingia ndani ya jicho lako utafanya jambo lolote kuhakikisha kwamba hicho kitu hakiingii ndani ya mboni ya jicho lako, unaweza kutumia mkono wako, au ukainama au ukakimbia au vyovyote vile lakini kitu chochote kisiingie ndani ya jicho lako. Kwa kutumia mfano huu jenga picha ya kwamba Mungu amekufanya wewe kuwa ni mboni ya jicho lake, yaani Mungu amekuweka wewe kuwa ni sehemu muhimu kabisa ambayo hakuna kitu kitapita au kitakuja kudhuru mboni ya jicho bila kuonekana, na kama hicho kitu kitakaribia jicho hata kabla ya kuleta madhara kitakuwa tayari kimeondolewa na Mungu mwenyewe. Tunasoma pia katika Kumbukumbu la torati 32:9-10 “9 Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. 10 Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho;” Biblia inatueleza kuwa katika jangwa tupu litishalo Mungu alimzunguka akamhifadhi/akamlinda kama mboni ya jicho lake yaani mboni ya jicho la Mungu wa Israeli.
Kwa lugha nyingine unaweza kusema kwamba yoyote anayeshindana na wewe uliyeokoka (Kwa maana ukiokoka unakuwa ndani ya Mungu) anashindana na Mungu mwenyewe na wala hashindani na wewe. Na kama ikiwa yeyote yule (shetani na mawakala wake wote, mapepo na roho zote chafu kutoka kuzimu) watashindana na wewe basi wananshindana na Mungu na Neno la Mungu linasema “Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.” 1Samweli 2:10. Basi sasa fahamu mtu wa Mungu yakuwa yeyote aliyesimama kinyume na wewe anapingana na Mungu.
MAOMBI
Katika jina la Yesu kristo wa Nazarethi; yeyote anayeshindana namimi anashindana na BWANA. Kila roho inayotoka kuzimu majini, mapepo, mizimu, wachawi, wasoma nyota, waganga …….. mnaoshindana namimi; sawasawa na Neno la Mungu nawaponda kwa nyundo ya Mungu, nawaagizia radi kutoka mbinguni, nawaagizia umeme mkali kutoka mbingu, nawateketeza kabisa kwa jina la Yesu. Amen

6.      MIMI NI MTOTO WA MUNGU
Neno la Mungu linaweka bayana kwamba, mara unapokubali kuokoka (Yaani unapomkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni BWANA na Mwokozi wa maisha yako) basi unakuwa motto wa Mungu sawa na Neno la Mungu katika Yohana 1:12 – 13 “12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; 13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Vilevile tunapata ushuhuda zaidi yakwamba Roho Mtakatifu (Ambaye ni Mungu) hushuhudia pamoja na roho zetu yakwamba wale waliompokea Yesu ni watoto wa Mungu kama tunavyosoma katika Warumi 8:16 - 17 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” Zaidi tunaona katika 2Kor 6: 18 “Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”
Mtu wa Mungu kwanza pata picha ya kuwa wewe ni mtoto wa Mfalme/Rais/Waziri mkuu katika nchi Fulani au katika nchi yako unayokaa, halafu jaribu kuvuta picha ya heshima unayopewa wewe kama mtoto wa kiongozi katika nchi yako, watu wengine hata viongozi watakuheshimu kwakulinda nafasi zao za uongozi kwani wanajua wakikutendea vibaya na ukamweleza baba yako ambaye ni rais/waziri mkuu huenda wakashughulikiwa hata kupoteza nafasi zao, kwa ujumla kila mru atakuheshimu hata kama hapendi kufanya hivyo.
Sasa nikupe uhakika kuwa wewe ambaye umeokoka nafasi yako ni kubwa mno katika ulimwengu wa roho, baada yaw ewe kumpokea Yesu umezaliwa upya katika ulimwengu wa roho na baba yako ni Mungu mwenyewe. Mungu huyu ambaye ni baba yako ndiye Mungu wa Israeli yule aliyetenda mambo makuu kwa manabii na mitume waliomtegemea yeye tu. Hebu pata ujasiri sasa mtoto wa Mungu kwakuwa wewe ni mtoto wa Mungu umepewa urithi wa mambo yale ya mbinguni sawa na Neno la Mungu katika Warumi 8:16 - 17 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Ubarikiwe sana Mtu wa Mungu; zaidi sana fahamu yakuwa Neno la Mungu linatuhakikishia yakuwa sisi ni washindi na tunashinda na zaidi ya kushinda kama ilivyoandikwa katika Rumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”


1 comment:

Kalugila furniture said...

Barikiwa Sana MTU wa Mungu nimejifunza kitu KIKUBWA Sana Mungu aendelee kulitumia katika uandishi na kufundisha Neno la Mungu naitwa mch. Aderick kalugila. Wa kanisa la TCRC MASWA MJINI
BARIKIWA SANA MTUMISHI