Nimefunuliwa
juu ya somo hili kwaajili yako ili kukupa ujasiri na nguvu zaidi za rohoni kwa
kuifahamu kweli na kuwa na maarifa ya Mbinguni yatakayo kuwezesha kujua Neno la
Mungu na uweza wa Mungu. Neno la Mungu linasema katika injili ya Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala
uweza wa Mungu.” Hatujui yakuwa sisi ni watoto wa Mungu kwakua Neno la
Mungu linasema hivi “Bali wote
waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio
jina lake” Yohana 1:12. Kama
wewe ni mtoto wa Mungu na Mungu wetu anakaa mbinguni basi wewe pia ni wa asili
ya Mbinguni. Kuthibisha hili; Biblia inasema katika 1Yohana 3:9-10 “9 Kila mtu
aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake;
wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. 10 Katika
hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote
asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” Katika
mistari hii tunajifunza yakuwa Mungu anazaa watoto ambao ni wale waliompokea
Yesu Kristo, na wale waliozaliwa na Mungu uenyeji wao ni Mbinguni yaani wanayo
asili ya Mbinguni. Hata hivyo usisahau kwamba kuna watoto wa ibilisi ambao
watachomwa moto pamoja na baba yao ibilisi.
Ninakupa
moyo mtu wa Mungu ya kuwa ukiijua nafasi yako katika ufalme wa Mungu na
kuliamini Neno la Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya 55:10-11 “10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala
hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu
apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 11 ndivyo litakavyokuwa neno langu,
litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi
yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.” Basi hakika ni
kwamba utafanikiwa katika mambo yote sawasawa na Neno laMungu.
Karibu
msomaji wangu ujifunze baadhi ya mambo yatakayokupa ujasiri wa nafasi yako
katika ufalme wa Mungu.
1. MIMI NI MFANO NA SURA YA MUNGU
Biblia
inasema wazi kwamba hapo mwanzo Mungu aliamua kumuumba mtu kwa mfano wake
(Mungu) na kwa sura yake (Mungu) mwenyewe kama tunavyosoma katika maandiko
matakatifu katika kitabu cha Mwanzo 1:26
– 27 “26 Mungu akasema, Na tumfanye
mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa
angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu
ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba,
mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Nataka ufahamu kwa uhakika ya kwamba mtu
anayeongelewa hapa ni ROHO na sio mwili kama vile watu wengi wanavyodhani,
unaposikia wewe ni mfano wa Mungu, basi fahamu anayeongelewa hapa ni mtu wa
ndani (Roho yako) ndiye mfano wa Mungu. Uhakika wa kwamba mtu ni roho tunaupata
katika maandiko matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu yeye ni ROHO hivyo
yoyote aliye mfano wa Mungu naye pia ni ROHO kama tunavyosoma katika kitabu cha
Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na
kweli.”.
Nataka
nikupe uhakika ya kwamba umepewa nafasi kubwa sana katika ulimwengu wa mwili na
ulimwengu wa roho, nafasi hiyo ni kuwa sura yake Mungu kama vile alivyo Kristo
Yesu (2Korintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha
fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”),
kumbe nasisi tumepewa nafasi kama ile ya Yesu kama tunavyosoma katika Mwanzo 1:26 “26 Mungu akasema, Na tumfanye
mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege
wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho
juu ya nchi.”
Kuwa
sura yake Mungu maana yake ni kuwa ishara na kielelezo cha Nguvu, Uweza,
Mamlaka, Utukufu na Ukuu wa Mungu kila tutakapokuwa na ndio maana tukapewa
kumiliki na kutawala.
2. NDINYI MIUNGU (MIMI NI MIUNGU)
Muimba
zaburi anasema katika Zaburi 8:4-5 “4 Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na
binadamu hata umwangalie? 5 Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji
ya utukufu na heshima”. Mungu amemfanya Mtu/Mwanadamu kuwa baada tu ya
Mungu, yaani kimamlaka unaweza kusema Mtu/Mwanadamu ndi wa pili kwa nguvu
kutoka kwa Mungu. Ni kama vile nchi ambayo inayoviongozi wakuu wawili yaani
raisi (mwenye nchi) na waziri mkuu (Mtendaji mkuu wa serikali) ndivyo ilivyo
katika utawala wa Mungu, yaani Mungu (Muumbaji wa vitu vyote) na Mwandamu
(Mmiliki na mtawala/mtendaji). Katika injili kama ilivyoandikwa na Yohana 10:34 “Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi
nimesema, Ndinyi miungu?” vile vile tunasoma katika Zaburi 82:6 “6 Mimi nimesema,
Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”. kwahiyo tunao uthibitisho
kwamba sisi tumepewa nafasi ya UUNGU, yaani baada ya Mungu ni mimi mwanadamu.
3. MIMI NI HEKALU LA MUNGU
Bwana
Yesu alipoileta kweli ulimwenguni, alihamisha hekalu la Yerusalemu na kuwa
mwili wake kwa yule mwenye kuamini kama vile alivyoamisha sanduku la agano na
kutufanya sisi ndio sanduku la agano jipya amabapo Mungu anakaa ndani yetu.
Bwana Yesu akaleta wokovu kwa mwanadamu kwamba inatupasa tuokoke ili miili yetu
ifanyike hekalu la Roho mtakatifu kama ilivyoandikwa katika 1Kor 3:16 - 17 “16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa
Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu
atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo
ninyi.” Vilevile imeandikwa katika 2Kor
6:16, 18 “16 Tena pana mapatano gani
kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai;
kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea,
nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu…………18 Nitakuwa Baba kwenu,
Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”. Mtu wa Mungu hebu turudi
nyuma kidogo tuangalie katika hekalu la wayahudi ambapo Mungu alikaa ndani yake
na kulikuwa na nguvu kubwa kiasi gani.
Tunasoma
katika Kutoka 30:10 “Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya
pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya
upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu
vyote; ni takatifu sana kwa Bwana.” Tunaona katika patakatifu pa patakatifu
ndipo Haruni alipokutana na Mungu mara moja tu kwa mwaka ili kufanya upatanisho
wa dhambi za wana wa Israeli, kwa kifupi Mungu alishuka ndani ya hekalu
patakatifu pa patakatifu ili kukutana na kuhani aliyebeba sadaka ya upatanisho.
Baada ya kufa kwa Yesu Kristo kuna jambo lililotokea ambalo lilibadisha kabisa
taratibu za awali kama tunavyosoma katika
Waebrania 9:12-14 “12 wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali
kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata
ukombozi wa milele. 13 Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya
ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili;
14 basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa
nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na
matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”. Sasa miili yetu ndiyo
imekuwa hekalu la Mungu mwenyewe na ndiye anaishi ndani yetu.
Ndugu
fahamu kwamba Mungu aishiye ndani yako (Kwakuwa wewe ni hekalu la Mungu) ndiye
Mungu yuleyule aliyeumba mbingu na dunia, ndiye yule aliyewavusha Israeli
katika bahari ya shamu, ndiye yuleyule aliwaokoa Shedrack, Meshack na Abednego
kutoka katika ule moto mkali sana na ndiye aliyemuokoa Daniel na makanwa ya
samba wenye njaa kali; vile vile huyu ndiye Mungu wa Eliya, Elisha, Daudi na
manabii na mitume wakubwa katika Biblia. Swali ni hili sasa; Iweje huyu Mungu
mwenye nguvu kuu namna hii anaishi ndani yako halafu wewe kila siku unalalamika
kwamba unaonewa na nguvu za giza, unalalamika kuporomoka kiuchumi, unalalamika
afya yako kuvurugika; AMKA!!! Tambua nguvu inayofanya kazi ndani yako! Tambua
ya kwamba Mungu mwenye nguvu za kutisha yupo ndani yako, amini kwamba anaweza
nayeye atatenda jambo kubwa sana katika maisha yak oleo.
MAOMBI
Katika jina la Yesu Kristo nimetambua
leo yakwamba mimi ni hekalu la BWANA na Roho wa BWANA anakaa ndani yangu, na
kwakuwa Mungu anakaa ndani yangu Neno la Mungu linasema katika Waebrania 12:29 “maana Mungu wetu ni moto ulao”.
Chochote kilichokaa ndani yangu kutoka katika ufalme wa giza nakiamuru
kiteketee kwa moto wa BWANA aishiye ndani yangu, vyakula vya kichawi/kipepo
nilivyolishwa katika ulimwengu wa roho naamuru viteketee kwa moto ulao katika
jina la Yesu. Magonjwa ya aina zote naamuru yateketee kwa moto ulao katika jina
la Yesu, Amen.
4. MIMI NI TAWI NA MUNGU NI SHINA LANGU
Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye
ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi
kufanya neno lo lote.”
Ukiisha
kumpokea Yesu, Yesu anasema wewe unakuwa tawi lake na yeye (Yesu Kristo)
anakuwa Shina. Sasa ufahamu ya kuwa mti hutambulikana kwa matawi yake kasha kwa
matunda yake, maana yeke ni; Mti/Shina ni Yesu Kristo, ili uweze kuutambua
mti/shina inabidi utazame matawi yake na matunda yake yaani Mkristo na yale
anayoyatenda (Ukitaka kumtambua Kristo Yesu inabidi umuangalie Mkristo na
matendo yake). Kama ilivyo kwa mti wa kawaida, chakula kinachopita katika shina
ndicho kinachoingia katika matawi, hii inamaanisha kwamba kwakuwa sisi ni
matawi ya Kristo Yesu, basi kila kinachotoka kwake Yesu ndicho kinaingia kwetu.
Nguvu alizonazo Yesu zinaingia kwetu kwani tumeunganishwa na Yesu sawasawa na
Neno lake kutoka Yohana 14 : 5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi……..)
Mtu
wa Mungu AMKA!!! Fahamu yakuwa upako alionao Yesu Kristo unaingia na kwako pia,
fahamu ya kuwa Nguvu, Uponyaji, Baraka, Maarifa, Uweza na kila kilichopo kwa
Yesu ni cha kwako. Fahamu yakuwa hakuna kinachopita katika shina kisiingie
katika matawi.
MAOMBI (Omba kwa sauti kama unaweza)
Wewe shetani!! Wewe ni nani hata uweze
kukaa katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi, Kazi, Mahusiano, Kibali na
upendeleo!!!! Mimi nimejua, nifahamu ya kuwa mimi ni sehemu ya Yesu Kristo na
kila kinachotoka kwa Yesu Kristo kinaingia na kwangu. Katika Jina Lenye Nguvu
sana Jina la Yesu Kristo nakuamua TOKAAAA!!! Katika Afya, Ndoa, Baraka, Uchumi,
Kazi, Mahusiano, Kibali na upendeleo, ACHIAAA!!! Kwa Jina la Yesu kila
ulichoshikilia katika maisha yangu katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareth.
Chochote kilichojishikamanisha na maisha yangu naamuru kikutane na nguvu ya
damu ya Yesu kwakuwa imeandikwa katika Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao;
ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Namimi nakushinda shetani kwa damu
ya Yesu Kristo katika jina la Yesu, Amen.
5. MIMI NI MBONI YA JICHO LA MUNGU
Zekaria 2:8. “Kwa maana Bwana
wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale
waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.”
Jaribu kufikiri
katika hali ya kawaida kabisa ambayo wewe ni mwanadamu ambaye unavyo viungo
vingi na kimojawapo ni jicho, ndani ya jicho kuna kitu muhimu sana ambacho ni
“mboni”. Kama ikitokea mdudu au kitu chochote kinaelekea kuingia ndani ya jicho
lako utafanya jambo lolote kuhakikisha kwamba hicho kitu hakiingii ndani ya
mboni ya jicho lako, unaweza kutumia mkono wako, au ukainama au ukakimbia au
vyovyote vile lakini kitu chochote kisiingie ndani ya jicho lako. Kwa kutumia mfano
huu jenga picha ya kwamba Mungu amekufanya wewe kuwa ni mboni ya jicho lake,
yaani Mungu amekuweka wewe kuwa ni sehemu muhimu kabisa ambayo hakuna kitu
kitapita au kitakuja kudhuru mboni ya jicho bila kuonekana, na kama hicho kitu
kitakaribia jicho hata kabla ya kuleta madhara kitakuwa tayari kimeondolewa na
Mungu mwenyewe. Tunasoma pia katika Kumbukumbu
la torati 32:9-10 “9 Maana, sehemu ya
Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. 10 Alimkuta katika nchi ya
ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho;” Biblia
inatueleza kuwa katika jangwa tupu litishalo Mungu alimzunguka
akamhifadhi/akamlinda kama mboni ya jicho lake yaani mboni ya jicho la Mungu wa
Israeli.
Kwa lugha
nyingine unaweza kusema kwamba yoyote anayeshindana na wewe uliyeokoka (Kwa
maana ukiokoka unakuwa ndani ya Mungu) anashindana na Mungu mwenyewe na wala
hashindani na wewe. Na kama ikiwa yeyote yule (shetani na mawakala wake wote,
mapepo na roho zote chafu kutoka kuzimu) watashindana na wewe basi
wananshindana na Mungu na Neno la Mungu linasema “Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia
radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na
kuitukuza pembe ya masihi wake.” 1Samweli
2:10. Basi sasa fahamu mtu wa Mungu yakuwa yeyote aliyesimama kinyume na
wewe anapingana na Mungu.
MAOMBI
Katika jina la Yesu kristo wa Nazarethi; yeyote
anayeshindana namimi anashindana na BWANA. Kila roho inayotoka kuzimu majini,
mapepo, mizimu, wachawi, wasoma nyota, waganga …….. mnaoshindana namimi;
sawasawa na Neno la Mungu nawaponda kwa nyundo ya Mungu, nawaagizia radi kutoka
mbinguni, nawaagizia umeme mkali kutoka mbingu, nawateketeza kabisa kwa jina la
Yesu. Amen
6. MIMI NI MTOTO WA MUNGU
Neno
la Mungu linaweka bayana kwamba, mara unapokubali kuokoka (Yaani unapomkiri
Yesu kwa kinywa chako kuwa ni BWANA na Mwokozi wa maisha yako) basi unakuwa
motto wa Mungu sawa na Neno la Mungu katika Yohana 1:12 – 13 “12 Bali
wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake; 13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya
mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Vilevile tunapata
ushuhuda zaidi yakwamba Roho Mtakatifu (Ambaye ni Mungu) hushuhudia pamoja na
roho zetu yakwamba wale waliompokea Yesu ni watoto wa Mungu kama tunavyosoma
katika Warumi 8:16 - 17 “16 Roho mwenyewe hushuhudia
pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto,
basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa
pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” Zaidi tunaona katika 2Kor 6: 18 “Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu
wanangu wa kiume na wa kike”
Mtu
wa Mungu kwanza pata picha ya kuwa wewe ni mtoto wa Mfalme/Rais/Waziri mkuu
katika nchi Fulani au katika nchi yako unayokaa, halafu jaribu kuvuta picha ya
heshima unayopewa wewe kama mtoto wa kiongozi katika nchi yako, watu wengine
hata viongozi watakuheshimu kwakulinda nafasi zao za uongozi kwani wanajua
wakikutendea vibaya na ukamweleza baba yako ambaye ni rais/waziri mkuu huenda
wakashughulikiwa hata kupoteza nafasi zao, kwa ujumla kila mru atakuheshimu
hata kama hapendi kufanya hivyo.
Sasa
nikupe uhakika kuwa wewe ambaye umeokoka nafasi yako ni kubwa mno katika
ulimwengu wa roho, baada yaw ewe kumpokea Yesu umezaliwa upya katika ulimwengu
wa roho na baba yako ni Mungu mwenyewe. Mungu huyu ambaye ni baba yako ndiye
Mungu wa Israeli yule aliyetenda mambo makuu kwa manabii na mitume
waliomtegemea yeye tu. Hebu pata ujasiri sasa mtoto wa Mungu kwakuwa wewe ni
mtoto wa Mungu umepewa urithi wa mambo yale ya mbinguni sawa na Neno la Mungu
katika Warumi 8:16 - 17 “16 Roho mwenyewe hushuhudia
pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17 na kama tu watoto,
basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa
pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Ubarikiwe sana Mtu wa Mungu;
zaidi sana fahamu yakuwa Neno la Mungu linatuhakikishia yakuwa sisi ni washindi
na tunashinda na zaidi ya kushinda kama ilivyoandikwa katika Rumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa
yeye aliyetupenda.”
1 comment:
Barikiwa Sana MTU wa Mungu nimejifunza kitu KIKUBWA Sana Mungu aendelee kulitumia katika uandishi na kufundisha Neno la Mungu naitwa mch. Aderick kalugila. Wa kanisa la TCRC MASWA MJINI
BARIKIWA SANA MTUMISHI
Post a Comment