Thursday, July 23, 2015

MKRISTO MPAMBANAJI/MPIGANAJI (Samson Mollel - Uzima wa Milele International Ministries)

KUCHELEWA SANA AU KUWAHI SANA KWA MAFANIKIO YAKO KATIKA MAISHA (KIROHO NA KIMWILI) HUTEGEMEANA NA UWEZO WAKO WA KUFANYA VITA YA KIROHO.
Kama unataka kufanikiwa mapema katika maisha yako ya kiroho au ya kimwili lazima ufahamu habari ya vita kubwa iliyopo katika ulimwengu wa roho na ufahamu namna ya kupambana na silaha zinazotumika katika vita ya kiroho. Kama unataka kukua upesi katika huduma yako (Uimbaji, ualimu, uchungaji, uinjilisti, unabii, utume, nk) au kama unataka kukua upesi katika maisha yako ya kawaida (Ndoa, biashara, kilimo/mifugo, kazi n.k) ni lazima ufahamu kuwa kuna vita unapaswa kuishinda kwanza katika ulimwengu wa roho ili hayo yote yadhihirike katika ulimwengu wa mwili. Hebu tujifunze somo hili la safari ya wana wa Israeli kutoka nchi ya utumwa - Misri kwenda nchi ya ahadi Kaanani.
Kutoka 13: 17 – 18, “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha”
SOMO LA KUJIFUNZA KUHUSU SAFARI HII:-
Sababu kubwa ya Mungu kutowapitisha wana wa Israel katika nchi ya wafilisti ni kwakuwa nguvu yao ya kivita ilikuwa ndogo (Kutoka 13:18, lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha) ndio maana wana wa Israel wakapitishwa njia ndefu mno iliyowachukua miaka 40 kufika katika nchi ile ya ahadi. Ninasema hivi kwasababu ushahidi wa kimaandiko unaonesha kuwa umbali kutoka Misri kwenda Kaanan ni mfupi sana na pia hakuna hata haja ya kuvuka bahari kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli (Mwanzo 42, 43 -  tunaona Wana wa Yakobo/Israel wakienda nchi ya Misri kununua chakula zaidi ya mara moja ndani ya muda mfupi. Vilevile tunaona wakati mfalme Herode anatafuta kumuua Yesu wazazi wa Yesu walimtoreshea Yesu Misri – Mathayo 2:13 -14)
Hapa tunawaona wana wa Israeli wakikwea kuelekea nchi ya ahadi hali wamevaa silaha lakini wenye uwezo mdogo wa kupigana ndio maana Mungu akawazungusha mbali sana mahali ambapo wangesafiri kwa wiki 2 au 3 wao wakasafiri kwa miaka 40. Sababu kuu ya kuchelewa huku ni uwezo wao mdogo wa kupambana na maadui kwani Mungu alijua wangekata tamaa (Kutoka 13:17, “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri”). Hivyo Mungu aliwaacha wapite njia ndefu sana (zaidi ya Miaka arobaini) ili wasikate tamaa na kurudi nyuma
SAFARI YA WANA WA ISRAELI NA VITA YA ROHONI
Kwanza kabisa fahamu ya kwamba mtu ni roho na pia fahamu ya kwamba agano la kale ni kivuli cha agano jipya (Kol 2:16-17, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; 17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”) pia tunasoma katika Hebr 10:1, “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao” . Kwa kusoma maandiko haya nataka ufahamu kuwa unachokiona kwa jinsi ya mwilini katika agano la kale ni dhahiri ya rohoni katika agano jipya.
Kwasababu hiyo basi; maisha tunayoishi sasa ni sawa sawa na safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Kaanani. Kufanikiwa kwako au kutofanikiwa inategemeana na uwezo wako wa kupambana kwa jinsi ya rohoni (Vita ya kiroho). Neno la Mungu linasema 2Kor 10 : 3 – 4 “3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome);”.
Inawezekana katika maisha yako umekuwa ukishindwa kufikia malengo yako kwa wakati (Yaani unachelewa kufikia malengo yako kama ulivyopanga), jambo hili lina pande mbili kama ifuatavyo


        i.            Mungu anakuepusha kwa makusudi ili usirudi upotevuni
Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli; Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu kwa kusudi wasije wakaghairi pale watakapo kutana na vita kama wangepitia njia fupi ya nchi ya wafilisti. Wafilisti ni watu ambao ni mahodari sana wa vita na kutokana na uwezo mdogo wa kivita wa Israeli kwa wakati huo ndio maana Mungu akaona ni vyema wapitie njia ndefu lakini wafike katika nchi ya ahadi (Kaanani).
Hata leo wakristo wengi wapo katika hali hii ya wana wa Israeli, wanapitia katika njia ndefu kufikia mafanikio yao (Nchi ya ahadi) kwakuwa uwezo wao wa kiroho kupambanani mdogo. Ni kweli umeokoka na umekombolewa kutoka katika nguvu za giza, ni kweli wewe ndio mteule wa BWANA (yaani Israeli wa leo) lakini uwezo wako wa kivita ni mdogo sana, hivyo Mungu kwa kuona kwamba endapo utakutana na vita kali (Nguvu za giza – wachawi, majini, mizimu nk) katika kufikia mafanikio yako upesi huenda ukakata tamaa na kushindwa kuendelea mbele, Mungu anakupitisha njia ndefu ya mafanikio ili ufike. Njia hii ndefu zaidi ya mafanikio sio kwamba haina vita; lakini vita yake ni nyepesi tofauti na njia fupi ya mafanikio ambayo vita yake ni kali sana.
     ii.            Kwakuwa shetani amefahamu kwamba wewe ni dhaifu katika vita ya kiroho
Vilevile inawezekana katika maisha yako umekuwa ukishindwa kufikia malengo yako kwa wakati (Yaani unachelewa kufikia malengo yako kama ulivyopanga) kwakuwa shetani amefahamu kwamba wewe ni dhaifu katika vita ya kiroho hivyo anakuinulia vita kali ili ushindwe. Katika safari ya wana Israeli tunaona kulikuwa na wafilisti ambao ndio walifanya mpaka Israeli wakashindwa kupitia ile njia ya karibu, leo kuna shetani na mawakala wake (Waganga wa kienyeji, mizimu, mapepo, wachawi nk) ambao ndio wafilisti wa leo katika maisha yako kukuzuia usifikie malengo kwa wakati uliokusudia au uliopangiwa na Mungu. Kwa kifupi shetani anahamisha mipaka ya mafanikio yako ili usifikie kusudi la Mungu kwa wakati uliopangwa na Mungu.
KWANINI MKRISTO UNACHELEWA KUFIKIA MAFANIKIO?
Sababu kubwa ya shetani kuwachelewesha wakristo katika kuifikia nchi ya ahadi (Mafanikio yako) ni kwakuwa wakristo wengi hawajui nguvu iliyopo katika Neno la Mungu au hawalijui kabisa Neno la Mungu, yaani wakristo hawana maarifa ya Neno la Mungu na hivyo wanaangamizwa kabisa Hosea 4:6a “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;” kwa hiyo moja ya sababu ya shetani kutushinda na kutuchelewesha katika kufikia mafanikio ni kukosa maarifa ya kiMungu. Maarifa hayo ni yapi? Tukisoma katika injili ya Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Maandiko yanaeleza wazi wazi kuwa kuna vita katika ulimwengu wa roho na yatupasa kuwa hodari na kuvaa silaha ili tupambane Efeso 6:10 – 13 (Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.).
Ukizidi kusoma utaona silaha za vita vyetu zimeorodheshwa ili kupambana na kumshinda kabisa shetani. Efeso 6: 14-18 “14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”. Tunanona kuwa kuna silaha zimetajwa ambazo ni KWELI, DIRII YA HAKI, MIGUU YA UTAYARI, NGAO YA IMANI, CHAPEO YA WOKOVU, UPANGA WA ROHO, SALA ZOTE NA MAOMBI. Hizi ni silaha alizozitaja mtume Paulo, nawewe unapoingia katika maombi hakikisha umevaa silaha hizi zote ili uweze kupambana pasipo kuumizwa na yule mwovu shetani.

Kuna silaha zaidi za kutumia kupambana na shetani na kadiri unavyosoma Biblia utazifahamu. Kwa ufupi ni kwamba silaha kubwa zaidi ya kupambana na shetani na malaika zake na mawakala zake ni JINA LA YESU, DAMU YA YESU, MOTO WA BWANA.

No comments: