Friday, August 26, 2016

KUKATA KAMBA ZA UOVU NA LAANA NA KUFUTA MAAGANO NA MAUTI

Imefundishwa na Mtumishi Isaac Ridhiwan Omary (Semina ya MVUMO – Morogoro, 25th August 2016)
Imeandikwa na Samson Mollel – 0767 664 338 (www.uzimawamileleministries.blogspot.com)


Ezekieli 18:1-4 “1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 2 Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? 3 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. 4 Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.”

Isaya 28:15-18 “15 Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; 16 kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka. 17 Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri. 18 Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.”

Jambo la kwanza la kuangalia katika somo hili:
Nakubalina kabisa na wala sipingani na ukweli kwamba laana/uovu/mapigo kutoka kwa wazazi hufutilia vizazi hata kama mtoto hakufanya jambo hilo ubaya uliosababishwa na wazazi unaweza kumpata, huu ni ukweli kabisa na inawezeka kutokea kabisa kwakuwa ni Mungu mwenyewe amesema, imeandikwa katika Kutoka 20:5 “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”)
Lakini kuna sehemu tunaacha katika hilo agizo la Mungu ya kuwa Mungu anawarehemu wale wanaoshika amri zake, tunasahau kuwa Mungu ni wa rehema, imeandikwa katika Kutoka 20:6 “nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.”
Haijalishi umefungwa kiasi gani na laana/uovu wa kifamilia. Katika dunia nzima ufunguo wa kutoka katika kifungo haujakabidhiwa kwenye dini au dhehebu Fulani au taifa lolote unalolijua au usilolijua, hata taifa la Mungu Israeli hawajaachiwa huo ufunguo wa kumng’oa mtu kwenye hiyo laana. Funguo anazo Yesu peke yake kama tunavyosoma katika Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.. Usidanganywe kuwa kuna dini/dhehebu ambalo limeshikilia hizo funguo kwamba hakuna mtu mwingine anayemiliki na anayeweza kufungua, usiwasema watu wa dini au dhehebu lingine; unapokaa katikati ya watu wa madhehebu/dini tofauti ongelea habari ya ubora wa Yesu mwenye funguo na sio ubora wa dini/dhehebu.

Unapotaka kufunguliwa na Yesu ili kuwa huru kabisa zingatia mambo yafuatayo
  •          i.            Tembea na Neno la BWANA
  •        ii.            Kuwa muombaji/Fanya maombi
  •      iii.            Kuwa mtoaji wa sadaka

Ukitembea na mambo hayo lazima utafanikiwa
Kama kuna jambo lolote la laana/uovu au majini/mizimu, hilo jambo linalokusumbua libebe na ulipeleke pale msalabani, haijalishi watu wamekunenea maneno ya jinsi gani au laana za jinsi gani, wewe beba na upeleke pale msalabani kwa Yesu (Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”) Vilevile imeandikwa katika Wakolosai 2:3-4 “13 Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; 14 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;” 
Kuna nguvu ya ziada kwenye madhabahu ya Yesu Kristo inayozidi nguvu zingine zote, inazidi nguvu za majini , laana, mizimu, makaburi, ajali, magonjwa. Ni kazi ya Yesu kubeba laana na madhaifu mengine yote na akiisha kubeba hizo laana anaachilia Baraka, anaachilia uzima na afya. Ndipo linatimia lile Neno kutoka Ezekiel 18:3 “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli.” Hautakuwa na sababu tena ya kuitwa umeirithi laana ya mababu au umeurithi ugonjwa au taabu yoyote ile kwani Yesu anakuwa amezichukua zote na kukuachia Baraka zake.


Jambo la pili la kuangalia katika somo hili:
Kuna watu wanayo maagano na mauti na mapatano na kuzimu Isaya 28:15 “15 Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;” Watu hawa vita yao kubwa wanaielekeza kwa wana wa amani (Yerusalemu).
Yaani baada ya kukata kamba za laana na kuzipeleka msalabani, baada ya kutoka kwenye balaa na mikosi ya kifamilia kwa nguvu ya madhabahu ya Yesu Kristo. Huko duniani kuna watu wanayo maagano na mauti na mapatano na kuzimu ambao ukikutana nao tu wanakunenea/unabii wa kipepo kuharibu maisha yako na Baraka zako.
Zipo roho za uonevu ambazo zinawavaa watu wasiojua kutembea na ulinzi wa Yesu Kristo, roho hizi zinaweza zikakuvaa darasani, kazini, shambani, kwenye biashara, uwanjani unapocheza mpira, njiani unapopita, kwenye basi/daladala unapopanda. Yaani unakuta kuna mtu/watu wameweka mazindiko yao kwa sababu zao ambazo hata hazikuhusu lakini kwakuwa umepita maeneo yao kama nilivyotaja hapo juu hizo roho zinakuvaa na kukutesa.
Isaya 28:16 “kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka”.
Yesu Kristo ndio jiwe la pembeni, ukiwa ndani ya Yesu Kristo kama BWANA na mwokozi wa maisha yako hawataweza kukuonea au kukunyanyasa.
Unapokuwa na Yesu Kristo yeye ambaye ni jiwe la pembeni; kila jambo unalolifanya fanya ukiwa juu ya jiwe, ukijenga jenga juu ya jiwe, ukihudumu hudumu juu ya jiwe, ukisafiri safari juu ya jiwe, ukisoma, ukifanya biashara, ukilima, ukifanya kazi vyote fanya juu ya jiwe na hakuna kitu kitakushinda. Hakuna laiyefanya mapatano/maagano na mauti na kuzimu atakayekuweza kwa jina la YESU.

 KWA MAFUNDISHO ZAIDI TEMBELEA: www.uzimawamileleministries.blogspot.com


No comments: