Thursday, August 25, 2016

UCHAWI NDANI YA KANISA LA MUNGU

Samson Mollel – Uzima wa Milele International Ministries +255 767 664 338

www.uzimawamileleministries.blogspot.com

Uchawi ni nguvu ya giza isiyoonekana na macho ya kibinadamu ikiwa na lengo la kuleta uharibifu kwenye maisha ya watu. Nguvu hii hutenda kazi kwa kuloga, kuloga ni maneneo/manuizo ya uharibifu yanayotamkwa kwa imani kubwa ili kuleta madhara kwa mtu aliyekusudiwa.
Biblia inamtambua mchawi katika mazingira tofauti tofauti, moja kati ya mazingira hayo ni pale mtu anapokuzuia wewe kutimiza lile kusudi ambalo Mungu amekupangia katika maisha yako, huyo anayekuzuia kulitimiza kusudi la Mungu ni mchawi hata kama ni mtumishi wa Mungu (Askofu, Nabii, Mtume, Mchungaji, Padri, Katekista n.k.). yeyote anayekukwamisha usifikie lengo lako katika kuylitimiza kusudi la Mungu huyo ni mchawi wako hata kama ni ndugu yako wa karibu (Baba, Mama, Kaka, Dada, Shangazi, Mjomba n.k.) kwani Yesu alisema “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.” (Mathayo 10:36). Maana yake ni kwamba yeyote anayekukwamisha katika maisha yako (Mchawi) lazima awe anakufahamu vizuri njia zako, uimara wako na udhaifu wako, kimsingi lazima awe anakujua ili aweze kukusababishia ukwazo/kukwama.

MAKUHANI WA KICHAWI
Ninasema kuwa mtu yeyote anayekusababishia ukwazo/mkwamo katika maisha yako ili ushindwe kulifikia lile kusudi la Mungu huyo ni mchawi kwani Biblia imewatambua hivyo. Ukisoma habari ya Baalamu katika kitabu cha Hesabu utaona jinsi gani Baalamu alikuwa ni Nabii wa Mungu na alimtegemea Mungu na alikuwa akipokea maelekezo kutoka kwa Mungu, pamoja na kuwa yeye ni kuhani wa Mungu aliye hai, Baalamu alianza kukubali kumsadia Balaki mfalme wa Moabu Hesabu 22:7-8 “7 Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. 8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu..”.
Baada ya Balaki mfalme wa Moabu kuwaona wana wa Israeli wakiijia nchi ya Moabu kwa mbali wakielekea nchi ya ahadi aliogopa kwakua alisikia mambo makuu Mungu aliyotenda kwa habari ya Israeli juu ya mataifa mengine kwamba Israeli iliwapiga mapigo makuu, hivyo akwatuma wajumbe wake Nabii Baalamu aliyejua habari za Mungu wa kweli ili awalaani Israeli Hesabu 22:5-6 5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. 6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”

Ukiendelea kwa wakati wako soma Hesabu mlango wa 22 na 23 utaona kuna wakati BWANA alitaka kumwangamiza kabisa Baalamu kwakuwa alitia nia ya kuweka ukwazo kwa wana wa isareli japokuwa BWANA alimkataza hapo awali Hesabu 22:12 “Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”. Lakini Baalamu aliendelea kumsadia mfalme wa Moabu kufanya jitihada mbalimbali ili kuwazuia wasifike katika nchi ya Moabu wakielekea nchi ya ahadi.

Hayo yote aliyoyafanya Baalamu pamoja na kuwa ni Nabii wa Mungu ni uchawi, na ndio maana tunasoma katika Yoshua 13:22 “Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.”.

Sasa kumbe inawezekana kabisa kuwa na kuhani wa Mungu aliyekengeuka na kufuata namna ya dunia na akafanya uchawi katika maisha ya watu wa Mungu, yaani akawa anatia ukwazo/kukukwamisha katika kila mipango inayokupelekea kulitimiliza kusudi la Mungu kama alivyofanya Baalamu pamoja na maonyo yote aliyopewa na Mungu juu ya kuwalaani wana wa Israeli. Ashukuriwe BWANA anayetupigania na kutushindia ambaye aliwawezesha Israeli kushinda na kumwua kabisa Baalamu na kuthibitisha lile Neno la Mungu alilonena kupitia kinywa cha Baalamu yakwamba “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!” (Hesabu 23:23)

MANABII WA KICHAWI
Wakati mwingi wachungaji wamekuwa wakiwafundisha washirika wao habari za wokovu na kuacha dhambi lakini washarika wanonekana kama wameelewa ila wakitoka nje ya kanisa wanakuwa kama vile sio wao waliokuwa wakifundishwa habari wokovu, utawakuta ni walevi, wazinzi waasherati na kila jambo la uovu linafanywa kupitia hao washarika waliofundishwa habari za Kristo.

Baadhi ya makanisa hata wameweka utaratibu wa kuwatenga wakristo wao (kuwaweka kwenye uangalizi maalum au kuwaonya) ili wasishiriki katika baadhi ya huduma za kikanisa na hata makanisa mengine yamewafukuza kabisa baadhi ya waumini bila kujua hilo sio suluhisho kwani mara nyingi sio wakristo wanao fanya hayo ila ile roho ya mpinga Kristo ndio inayotekeleza hayo na wakati mwingine kupitia hao hao viongozi wa kanisa.

Tunasoma katika Matendo 13:6 – 12 “6 Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; 7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. 9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, 10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? 11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. 12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.” Kuna wakati sio tatizo la Mkristo kutoelewa ila ni tatizo la kiongozi kutoangalia kwa macho ya rohoni kwanini wakristo hawafunguliwi na mafundisho/mahubiri yanayotolewa kila siku katika nyumba za ibada. Hapa tunamuona mtu anaitwa Bar-Yesu au Elima akimzuia Yule liwali aliyeitwa Sergio Paulo asiweze kuelewa anachofundishwa na mtume Paulo. Yaani wapo watu ambao wanajifanya kuilewa njia ya kweli lakini lengo lao ni kuipotosha na kuwaangusha wakristo, inawezekana ni kwa matamshi yao au kwa kutumia nguvu za giza kuwapiga bumbuwazi la mawazo washarika na hii inapelekea washarika kukaa wakisikiliza pasipo kuelewa kila jumapili na miaka inazidi kwenda nao wanzidi kupotea.

Vilevile wapo manabii wa uongo (ambao kimsingi ni manabii wa Jehova lakini kwa tamaa zao binafsi wameamua kusema uongo). Tunasoma katika 1Falme 13:1-24 “1 Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba …………... 5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana………………………….7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu. 8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa; 9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. ……………………11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao…………………………..14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye. 15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula. 16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa; 17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. 18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo. 19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake. 20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha; 21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, 22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako………………..24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.” Kumbe wapo manabii wanosema BWANA kasema lakini wanatumia akili zao wenyewe na wala BWANA hajasema Neno lolote, manabii kama hawa ni wa uongo kwakuwa huyasema mawazo yao na maneno yao na sio kusudi la BWANA.

Kazi hii (Unabii wa uongo) unafanywa na shetani mwenyewe kupitia mawakala wake ambao wanahakikisha ile kazi ya kuwapofusha wakristo inaenda kwa kasi kubwa ili wazidi kutiwa giza na wasiione Nuru (Yaani Yesu Kristo) 2Korintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

Ni maombi yangu kwako mtu wa Mungu Nuru ya BWANA ikujie sawa na Isaya 60:1 “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.”  na pia namuomba Mungu akufungue macho yako wewe unayesoma somo hili uelewe ulichokisoma na utakachoendelea kusoma kama vile Paulo alivyowaombea Waefeso katika Waefeso 1:17-19 “17 Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; 18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; 19 na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;”

MADHABAHU ZA KICHAWI
Inawezekana umestuka kuwa inawezekanaje ndani ya kanisa kukawa na madhabahu za kichawi, ni kweli kuna madhabahu za kichawi ndani ya kanisa ambazo kazi yake ni kupingana na kazi ya Mungu. Hii madhabahu ni ya shetani mwenyewe lakini ipo ndani ya kanisa la Mungu na wapo makuhani wa shetani wanaoihudumia; kama inavyofahamika kuwa panapokuwa na madhabahu lazima awepo na kuhani wa madhabahu hiyo. Ufunuo 2:12-13 “12 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili. 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.” Hapa Bwana Yesu mwenyewe anatuma barua yake kwa kanisa la Pergamo ambalo mahali lilipo ndipo penye kiti cha enzi cha shetani, na kama tunavyofamu kuwa mahali penye kiti cha enzi cha ufalme Fulani ndipo makao makuu ya ufalme huo yalipo (Ikulu), vilevile mahali penye kiti cha enzi cha shetani ndipo mahali palipo na madhabahu ya shetani. Hii ndio maana utashangaa kuona Yesu analiambia kanisa la Pergamo kwamba katikati ya kanisa ndipo alipouwawa shahidi wa Yesu Antipa “…….hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.”.

Unaweza kuwa unawaza kuwa haya yalitendeka zamani na sasa hayapo, ninakuhakikishia yapo tena kwa wingi ajabu. Ninaposema yapo usije ukamtazama mchungaji wako ukadhani yeye ndiye tatizo au mwinjilisti n.k.; inawezekana kabisa wakatumiwa na shetani kuweka ukwazo katika kazi ya Mungu ili isisonge mbele, lakini hata mkristo wa kawaida au mzee wa usharika au kiongozi yeyote ndani ya kanisa la Mungu anaweza kutumika kama kuhani wa madhabahu ya shetani. Kulingana na maneno ya Yesu mwenyewe inaonekana kuwa kanisa la Mungu (Watakatifu) wamejitahidi kuishi kwa uaminifu “…………..nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu………” lakini pamoja na kulishika jina la Yesu kwa uaminifu bado kuna shida ndani ya kanisa kwani yesu anasema katika Ufunuo 2:14-15 “14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. 15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.” Yesu anasema kuna watu ndani ya kanisa wanaohudhuria kanisani lakini hawafuati mafundisho matakatifu ila wanashika mafundisho ya mizimu na kipepo (yaani ya kichawi)


2 comments:

the power of vision tz said...

Worth reading

Monalyee said...
This comment has been removed by a blog administrator.