Tuesday, August 23, 2016

UWATAKASE KWA ILE KWELI

UWATAKASE KWA ILE KWELI
Samson Mollel 0767 – 664 338

Kweli ni nini? – Kweli ni Roho kutoka kwa Mungu Neno la Mungu yaani Yesu mwenyewe

ü  Kweli inatakasa

Unaposoma kitabu cha Injilia ya Yohana 17 tunaona maombi ya Yesu kwa Baba yake akituombea sisi wanadamu, zaidi sana anatuombea ulinzi dhidi ya nguvu za giza (shetani) na kumuomba Baba atutakase kwa ile kweli ambayo ni Neno la Baba.

Yohana 17:17 “14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. 15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 Uwatakase kwa ile kweli; NENO LAKO NDIYO KWELI.”

ü  Neno Yaani Yesu ndio Kweli

Tukisoma katika Yohana 1, tunajifunza jambo jingine ambalo linafungua macho ya mioyo yetu na kutufundisha kuwa Neno (Yaani ile kweli) alikuwa tangu mwanzo na Neno aliumba vitu vyote na wala pasipo Yeye (Neno) hakuna kitu amabacho kingeumbwa

Yohana 1:1, 14 “1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu……… 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; AMEJAA NEEMA NA KWELI.”

ü  Kweli Itakuweka Huru mbali na kuonewa

Napenda ufahamu sasa kama ukimpokea Yesu kwa kumaanisha ndani yako, unakuwa umeipokea ile kweli na ukiipokea ile kweli ndipo utakapokuwa huru mbali na uongo na kuonewa.

Yohana 8:31-32 “31 Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; 32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo KWELI ITAWAWEKA HURU.”


SHETANI NI CHANZO CHA UONGO

Fahamu ya kwamba shetani ni baba wa uongo ambaye anaweza kulitumia Neno la Mungu na kukupotosha kama wewe hauna nguvu ya Mungu na ufahamu wa ki-Mungu ndani yako

Mwanzo 3:1-5 “1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. 4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

Ninachotaka ufahamu hapa ni kwamba shetani alifahamu wazi wazi kuwa wakila tunda lile watakufa lakini aliwaambia uongo ili wapotee kwakuwa Mungu alishawaonya na kumwambia Adamu kuwa asile yale matunda ya mti wa katikakati na kama atakula basi atakufa hakika.

Mwanzo 2:16-17 “16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”


WOTE WAUPENDAO UONGO WANAMTUMIKIA SHETANI
Kimsingi au jambo la muhimu unapaswa kulifahamu ni kwamba shetani ndie uongo mwenyewe, yaani kila uongo unaotokea chanzo chake ni shetani kama Neno la Mungu linavyotufundisha.

Yohana 8:44-45 “44 Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. 45 Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.”


UONGO NI ROHO
Kama vile zilivyo roho zingine za uzinzi/uasherati/umasikini…. uongo nao ni roho, yaani pepo linaweza kutoka kuzimu au katika madhabahu yoyote ya kichawi na kuwa roho ya uongo na kumtawala mtu kwa lengo la kuwapotosha watu au mtu Fulani.

1Wafalme 22:20-22 “20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. 22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.”


Samson Mollel 0767 – 664 338

No comments: