Thursday, September 22, 2016

UFALME WA SHETANI DUNIANI (Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016)

UFALME WA SHETANI DUNIANI
Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)

www.uzimawamileleministries.blogspot.com


UTANGULIZI

Sio mpango wa Mungu shetani ammiliki na kumtawala mwanadamu lakini mwanadamu alipewa na Mungu kumiliki na kutawala (Mwanzo 1:28 “28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”), ila kwasababu ya ile dhambi pale bustani ya edeni ndipo shetani alipouchukua tena umiliki ambao Mungu alimpa mwanadamu.

Ashukuriwe Mungu (Jehova) kwa upendo na neema yake kwa kumtoa Yesu Kristo kuwa kafara (sadaka) ili atukomboe kutoka katika uovu ule tuliofanya sisi kama ilivyoandikwa katika Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Pamoja na jambo hili kubwa la ukombozi, shetani ameendelea kufanya mbinu nyingi za kuwaumiza na kuwashinda watakatifu wa Mungu kama tunavyosoma katika Ufunuo 13:2, 7 “2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. 7 Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.”

Kama anavyosema mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso 3:20 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;”, namimi naungana na mtume Paulo kwa kumtukuza Mungu kwa mamb makuu anayoyatenda katika maisha yetu na kutupa ushindi dhidi ya shetani na nguvu zote za giza kama ilivyoandikwa kuwa tumemshinda shetani kwa damu ya Yesu Kristo (Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”)

Na kwasababu hiyo basi Mungu ametupa silaha saba muhimu za kumshinda shetani na kumuondoa katika mipaka yetu kwa Jina la Yesu, ukisoma Waefeso 6:13-18 “13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI, na kuvaa DIRII YA HAKI KIFUANI, 15 na kufungiwa miguu UTAYARI TUPATAO KWA INJILI YA AMANI; 16 zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni CHAPEO YA WOKOVU, na UPANGA WA ROHO AMBAO NI NENO LA MUNGU; 18 KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”


Kama linavyosema Neno la Mungu katika Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya FALME na MAMLAKA, juu ya WAKUU WA GIZA HILI, juu ya MAJESHI YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho.” Ninachotaka ukione hapa ni mgawanyiko wa kiutawala katika ulimwengu wa roho ambao sisi watakatifu (waliookoka) ndio tunapambana nao katika ulimwengu wa roho.


UFALME WA ROHONI UNAVYOFANYA KAZI DUNIANI
Jambo la muhimu la kufahamu hapa ni kwamba katika nchi mmoja kunakuweko na falme mbili, yaani ufalme/utawala wa kiroho na ufalme/utawala wa kibinadamu. Na utawala/ufalme  ule wa kiroho unakuwa na nguvu sana kuliko ule ufalme/utawala wa kimwili/kibinadamu. Kimsingi utawala/ufalme uliopo rohoni ndio unaoongoza tawala za kibinadamu. Mfano mzuri ni pale ambapo Yesu Kristo anaitwa Mfalme wa wayahudi (Luka 23:3 “Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema.” Vilevile tunasoma katika (Luka 23:28 “Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.”) wakati huo huo kulikuwa na Herode ambaye ndiye aliyekuwa mfalme wa wayahudi (Mathayo 2:1 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,….”;) Yaani Yesu yupo rohoni kwenye kiti cha enzi cha Daudi baba yake na Herode yupo mwilini kama mfalme wa kawaida


MUNGU (JEHOVA) ANAO UFALME
Wakati Fulani Bwana Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake nanma ya kusali akawaambia katika Mathayo 6:9-13 9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE…………….. KWA KUWA UFALME NI WAKO, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.”

Kwahiyo tunaona kuwa Mungu anao ufalme wake unaoweza kuja na kumiliki hapa duniani kama Mbingu. Soma mistari ifuatayo kuona Yesu akiongelea ufalme wa Mungu/Mbinguni
Mathayo 3:2 “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”

Marko 4:11 “Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,”

Kwahiyo tunajifunza kuwa Mungu anao ufalme wake ambao kama ukiukaribisha hapa duniani unaweza kutawala, maana yake unakuwa na utawala wa kibinadamu lakini unapokea maelekezo kutoka kwa Mungu mwenyewe.


SHETANI ANAO UFALME (KINGDOM)

Baada ya Yesu kumponya Yule mtu mwenye pepo kipofu na bubu na mtu Yule akapata kuona na kusikia vizuri, mafarisayo wakamdhihaki kwamba anatoa pepo kwa beelzebuli mkuu wa pepo, lakini Yesu alifahamu mawazo yao na kuwajibu.

Mathayo 12:25-26 25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. 26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”

Majibu haya ya Yesu yanatuonesha kuwa shetani anao ufalme ambao uko imara (haujafitinika) na umesimama “Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”

Vilevile ukiendelea kusoma Biblia yako utagundua kuwa shetani kama mfalme anacho kiti chake cha enzi kama tunavyosoma katika Ufunuo 13:2 “2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”
Vilevile ufalme wa shetani unaweza kutawala katikati ya falme za wanadamu kama ukikaribishwa.


1.     UFALME WA SHETANI KATIKA NCHI YA TIRO

Ezekiel 28:1-19 “1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 2 Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. ………………….. 9 Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha. ……………….11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema, 12 Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri. 13 Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. 14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. ……………..”


Tiro ni nchi kama nchi nyingine, yaani kama ilivyo Tanzania, lakini katika nchi ya Tiro kuna kuna watawala wa aina mbili wenye mamlaka juu ya nchi ya Tiro, kwanza kuna mkuu wa nchi ya Tiro Ezekiel 28:2 Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.”

Hapa mkuu wa Tiro ni mkuu wa nchi ya Tiro katika ulimwengu wa mwili ambaye anaonekana kwa macho ya mwilini kuwa ndiye anyetawala nchi ya Tiro. Hii ni kama vile unavyoweza kumuona Raisi wan chi au Waziri mkuu wa nchi au kiongozi yoyote katika nchi mwenye mamlaka ya mwisho katika ulimwengu wa mwili.

Lakini tunaona nchi hiyo hiyo moja ya Tiro kuna kiongozi mwingine mwenye madaraka makubwa katika nchi ya Tiro kama tunavyosoma katika Ezekiel 28:12 “Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.”

Huyu ni mkuu wa Tiro katika ulimwengu wa roho, nasema ulimwengu wa roho kwasababu; kwanza nchi moja haiwezi kuwa na viongozi wakuu wawili wenye mamlaka sawa, halafu pili Biblia imemtaja mmoja kuwa ni mwanadamu na wa pili kuwa ni kerubi, hivyo mtawala wa pili wa Tiro yupo rohoni japo anaitawala nchi ya Tiro.

Hapa ndipo tunapopata ufahamu kuwa nchi moja ya Tiro imetawaliwa mwilini na imetawaliwa rohoni, na rohoni imetawaliwa na ibilisi na mwilini imetawaliwa na mwanadamu


2.     UFALME WA SHETANI KATIKA NCHI YA UAJEMI

Daniel 10:1-21 1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo. 2 Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. 3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia. 4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli; 5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi………….. 20 Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja…….”
Uajemi ni nchi ambayo inayo kiongozi wake anaitwa mfalme koreshi kama tunavyosoma katika Daniel 10:1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi,……….” Huyu ni binadamu ambaye katika hali ya maisha ya kawaida anaonekana kuwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi ya Uajemi na ndiye mwenye mamlaka kwa jinsi ya mtazamo wa kawaida.
Lakini jambo la kustaajabisha; baada ya maombi ya Daniel, Mungu (Yesu) alikuja kumletea majibu na alipokuwa anakuja Biblia inasema alizuiwa na mkuu wa uflame wa Uajemi kwa muda wa siku 21 kama ilivyoandikwa katika Daniel 10:13 “Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja;………………….

Sasa huyu mkuu wa mfalme wa uajemi ni nani hasa wakati tayari uajemi inayo mfalme na jina lake ni Koreshi? Ukiendelea kusoma Daniel 10:13, Yesu anasema maneno haya “………..bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi Kwahiyo tunajifunza jambo kubwa hapa kwamba kama malaika Mikaeli alishuka kuja kumsaidia Yule alitumwa; basin i dhahiri kwamba alizuiwa rohoni na sio mwili; na kwasababu hiyo tunapata jibu kuwa mkuu wa ufalme wa uajemi ni roho iliyokuwa inamiliki na kutawala nchi ya uajemi na ndio ilikuwa na nguvu ya kuruhusu nini kingie uajemi na nini kisiingie uajemi. Na kwakuwa roho hiyo ilifanya vita na Mungu (Jehova) basi ni wazi kabisa kuwa ni roho ya ibilisi.


VITA NA UFALME WA SHETANI DUNIANI
Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya FALME na MAMLAKA, juu ya WAKUU WA GIZA HILI, juu ya MAJESHI YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho.”

Maana yake ni kwamba katika ulimwemgu wa roho unaotawala ulimwengu wa mwili, umegawanyika katika ngazi mbalimbali za uongozi kama ifuatavyo

  •   FALME
  •  MAMLAKA
  •  WAKUU WA GIZA
  •  MAJESHI


Ndio maana tunaona katika nchi ya Tiro kuna mfalme (FALME) katika ulimwengu wa roho ambaye anaongoza na kuimiliki Tiro, vilevile tunaona katika nchi ya Uajemi kuna mkuu (WAKUU WA GIZA) mwenye mamlaka na sauti ya mwisho katika nchi ya Uajemi.
Nasema hao viongozi wa rohoni (katika ulimwengu wa roho) wanayo mamlaka kubwa kwa kuzingatia kuwa waliweza kumzuia Malaika wa BWANA kwa muda wa siku 21 asiingie katika nchi ya Uajemi na Pia waliweza kumpa kiburi na maarifa mengi mkuu wa tiro (ambaye ni mwanadamu) na kumpa kujiinua hadi akajiita mungu.


TUMEPEWA MAMLAKA YA KUSHINDA UFALME WA SHETANI

Baada ya anguko la mwadamu pale bustani ya Edeni, shetani alinyakuwa mamlaka ya kumiliki na kutawala tuliyoipewa na Mungu wakati wa uumbaji, lakini unapo mpokea Yesu Kristo unahamishwa kutoka utawala wa giza na kuingizwa kwenye utawala wa nuru kwa kufufuliwa pamoja na Kristo na unaketishwa pamoja na Kristo na kupewa mamlaka juu ya tawala zote za muovu.

Waefeso 2:6, 1:21-23 “6 Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; 21 juu sana kuliko UFALME wote, na MAMLAKA, na NGUVU, na USULTANI, na KILA JINA LITAJWALO, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”
Tumepewa mamlaka juu ya falme na mamlaka za giza katika ulimwengu wa roho, yaani tunayo mamlaka ya kumshinda mwovu shetani kwa jina la Yesu, kwasababu tumewekwa juu ya mamlaka zote katika ulimwengu mwili na ule wa roho.


FAHAMU KWAMBA KUNA MAMLAKA YA ROHONI INAYOKUTAWALA

Katika maisha ya kawaida tunayoishi kuna mamlaka/falme/wakuu katika ulimwengu wa roho wanao miliki maisha ya wanadamu waliopo mwilini. Kuna mamlaka ya rohoni inayoshughulika na mambo yako ya kiukoo, kifamilia, kikazi, kiafya, kibiashara, kielimu, ndoa na mengine mengi. Kama usipoweza kushughulika na mamlaka za giza zinazoruhusu au kuzuia mafanikio yako lazima utakwama katika mambo mengi ya maisha yako. Utaona mfano wa Daniel alivyochukua muda mrefu kupokea majibu ambayo yapo tayari yalishatolewa na Mungu lakini hayakumfikia kwa wakati kwasababu roho Yule anayetawala katika ulimwengu wa roho katika nchi ya Uajemi alikataa kufungua njia kuruhusu majibu ya BWANA yamfikie Daniel.

Jambo la muhimu sana la kufanya ili uweze kushinda hizo mamlaka za giza ni kumkubali/kumpokea ili Mungu akutoe katika umiliki wa falme za giza na kukupa nafasi ya kutawala kutokea rohoni sawasawa na Neno la Mungu kutoka katika maandiko; Wakolosai 1:13, Waefeso 2:6, Ufunuo 5:10 na Waefeso 1:21-23 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

Kama jinsi nilivyosema hapo awali kuwa tumepewa mamlaka juu ya falme na mamlaka za giza katika ulimwengu wa roho, yaani tunayo mamlaka ya kumshinda mwovu shetani kwa jina la Yesu, kwasababu tumewekwa juu ya mamlaka zote katika ulimwengu wa mwili na ule wa roho.
Nakushauri mtu wa Mungu utumie mamlaka uliyopewa kuuharibu utawala wa giza katika anga la maisha yako.



Samson Mollel 0767/0713 664 338; Sept, 2016
Uzima wa Milele International Ministries (Yohana 17:3)

www.uzimawamileleministries.blogspot.com

No comments: