FAHAMU
UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO
(BY
MWL, C.MWAKASEGE)
Utangulizi
Siku moja usiku
nikiwa katika chumba cha hoteli moja hapa hapa nchini, baada ya kutoka kwenye
semina ya kiroho; Roho Mtakatifu alisema ndani ya roho yangu kuwa; “Fundisha
juu ya Damu ya Yesu Kristo”.
Tangu
wakati huo nimekuwa na maombi ya mara kwa mara, nikiomba Roho Mtakatifu
anifundishe juu ya Damu ya Yesu Kristo. Nimekuwa nikisoma na kutafakari neno la
Mungu linalofundisha juu ya damu ya Yesu Kristo. Ni muda umepita sasa tangu
nipate agizo hili. Ndani ya moyo wangu naona ya kuwa muda umefika wa mimi
kuanza kuwashirikisha wenzangu yale ambayo tayari yamo ndani yangu ingawa ni
machache, juu ya Damu ya Yesu Kristo.
Katika mfulilizo wa
somo hili,tutashirikiana juu ya mambo manne tunayopata katika Damu ya Yesu
Kristo. Ukweli ni kwamba katika damu ya Yesu Kristo kunapatikana zaidi ya mambo
manne nitakayokushirikisha humu; lakini kwa sasa naona nianze na haya manne:-
- Uwezo
wa Damu ya Yesu Kristo katika kuondoa dhambi. Imeandikwa katika kitabu cha
1Yohana 1:9 kuwa; “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa
haki hata ATUONDOLEE dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote”.
- Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kupatanisha.
Imeandikwa katika kitabu cha Waefeso 2:13-16 kuwa; “Lakini sasa, katika
Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake
Kristo. Kwa maana yeye ndiye amanin yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa
wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye
akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo
katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya
nafsi yake; akafanya amani. AKAWAPATANISHA wote wawili na Mungu katika
mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba”
- Uzima wa Milele katika Damu ya Yesu Kristo.
Imeandikwa katika kitabu cha Yohana 6:53-54 kuwa; “Basi Yesu akawaambia
Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili wake mwana wa Adamu nakuinywa
damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu
yangu anao UZIMA WA MILELE…..”
- Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo katika kutulinda.
Imeandikwa katika kitabu cha ufunuo wa Yohana 12:11a kuwa; “Nao
wakamshinda (shetani) kwa damu ya mwana-Kondoo….”
Mtihani mkubwa sana kwetu sisi wakristo ni kuyaweka katika matendo yale
tunayofahamu katika Biblia. Nakushauri kwa Jina la Yesu Kristo kuwa uwe
mtendaji wa neno, na usiwe msomaji tu.
Ni maombi yangu kwa
Bwana ya kuwa Roho wa ufahamu wa Bwana atakuwa juu yako unaposoma na kutenda
unayofundishwa katika kitabu hiki.
UWEZO
WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUONDOA DHAMBI
“Heri
aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake” (Zaburi 32:1).
“Basi
torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya
mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati
wowote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! dhabihu hazingekoma
kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishw mara moja, wasingejiona
tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko KUMBUKUMBU LA
DHAMBI KILA MWAKA. Maana HAIWEZEKANI damuya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi”.
(Waebrania 10:1-4).
Kuna
tofauti kubwa sana
kiuwezo juu ya dhambi, kati ya damu ya mafahali na mbuzi ukilinganisha na Damu
ya Yesu Kristo.
Biblia
inatuambia wazi kabisa kuwa kuna mapungufu yaliyomo katika dhabihu ya damu ya
mafahali na mbuzi. Imeandikwa hivi; “Lakini katika dhabihu hizo liko
kumbukumbu la dhambi kila mwaka maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi
kuondoa dhambi” (Waebrania 10:3,4).
Katika
dhabihu ya damu ya mafahali na mbuzi kuna; ‘kumbukumbu la dhambi kila mwaka’
kwa kuwa dhabihu hizi HAZIWEZI KUONDOA DHAMBI.
Dhabihu hizi zilipokuwa zinatolewa; dhambi za taifa la Israeli zilikuwa
haziondolewi, bali zilikuwa zinasitiriwa au kufunikwa.
Kwa hiyo Kuhani Mkuu wa wakati huo wa Agano la Kale ilimbidi atoe dhabihu hizo
kila mwaka ili Mungu aweze kukaa KATI YAO na wala SIYO NDANI YAO!
Kwa
maneno mwengine naweza kusema hivi, katika agano la kale Mungu aliwasamehe watu
dhambi zao walipotubu LAKINI HAKUZISAHAU BALI ALIZIKUMBUKA!
Ndiyo
maana ilibidi kuwekwe agano jipya, kwa kuwa agano la kale lilikuwa na upingufu
(Waebrania 8:7)! Kwa sababu hiyo tunasoma ya kuwa Yesu Kristo “amepata
huduma iliyo bora zaidi, kwa kadri alivyo mjumbe wa agano lililo bora,
lililoamriwa juu y ahadi zilizo bora” (Waebrania 8:6).
Katika
agano jipya, Mungu anawasamehe watu wanaotubu dhambi zao, wala hazikumbuki
tena! Katika dhabihu ya Yesu Kristo halipo kumbukumbu la dhambi kila mwaka,
kwakuwa damu ya Yesu Kristo haifuniki dhambi bali HUIFUTA au KUIONDOA DHAMBI
ISIWEPO KABISA! Hebu soma maneno yafuatayo ya biblia; “Na kila Kuhani
husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi
ambazo (Yesu Kristo), alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja
idumuyo hata milele aliketi mkono wa kuume wa Mungu;tangu hapo akingojea
hata adui wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja AMEWAKAMILISHA
HATA MILELE hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye atushuhudia; kwa
maana, baada ya kusema, Hili ni agano (Jipya) ni takaloagana nao
baada ya siku ziel, anena Bwana, nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na
katika nia zao nitaandika; ndipo anenapo, dhambi zao na uasi wao
sitaukumbuka tena kabisa. Basi ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena
kwa ajili ya dhambi” (Waebrania 10:11 –18)
Oh!
Mpendwa msomaji, ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa Roho wake akufunulie zaidi
na zaidi juu yauwezo wa damu ya Yesu Kristo. Utaifahamu kweli, nayo hiyo kweli
unayoifahamu juu ya damu ya Yesu Kristo itakuweka huru kabisa!
Biblia
inatuambi ayakuwa kwa toleo MOJA TU! Haleluya! – ametukamilisha HATA MILELE
sisi tunaotakaswa. Pia, kwa toleo moja la dhabihu ya damu ya Yesu Kristo, Mungu
hakumbuki TENA KABISA dhambi na uasi tuliotubu. Kwa nini? Kwa sababu Damu ya
Yesu Kristo ina uwezo wa kuondoa dhambi zilizo MIOYONI MWETU na zile
zilizoandikwa katika VITABU MBINGUNI ili tuhukumiwe.
Hati za Kutushtaki
Mtu
anapotubu dhambi zake na kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha
yake; Damu ya Yesu Kristo inafuta dhambi hizo moyoni mwake, pamoja na kufuta
dhambi zilizoandikwa katika vitabu vya mbinguni kwa ajili ya kutushitaki.
“Na
katika Torati Karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu
hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe
kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu
zilizo bora kuliko hizo. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu
palipofanyika kwa mikono ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia
Mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si
kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani Mkuu aingiavyo katika
patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake;kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa
mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa MARA MOJA TU,
katika utimilifu wa nyakati amefunuliwa, AZITANGUE DHAMBI KWA DHABIHU YA NAFSI
YAKE” (Waebrania 9:22-26)
Je!
umewahi kujiuliza kwa nini Yesu Kristo baada ya kufufuka alimkataza Mariamu
Magdalena asimguse pale kaburini – Huku baadaye akamruhusu Tomaso aitwaye Pacha
amguse?
Je! Yesu Kristo alikuwa hawapendi wanawake? Je! Yesu
Kristo alikuwa na kinyongo na Mariamu Magdalena? La hasha – si hivyo! Yesu Kristo alipomkataza
Mariamu Magdalena asimguse, alikuwa njiani kwenda kwa Baba – Patakatifu pa
Mbinguni, kama Kuhani Mkuu aliyebeba damu yake mwenyewe ili tupate ondoleo la
dhambi mbkele ya Mungu na kutupatanisha naye.
Ndiyo maana Yesu Kristo alimwambia Mariamu Magdalena “Usinishike
kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni baba Yenu.., kwa Mungu wangu
naye ni Mungu wenu” (Yohana 20:17).
Yesu Kristo aliingia patakatifu kwa ajili yetu kwa damu
yake mwenyewe baada ya kupata ushindi mkuu dhidi ya shetani na majeshi yake.
Hebu tusome maneno yafuatayo;“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya
makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye,
akiisha kutusamehe makosa yote; akiishakuifuta ile hati iliyoandikwa
ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na auadui kwetu; akaiondoa
isiwepo tena,akaigongomea msalabani isiwepo tena, akaigongome msalabani;
akiisha kuzivua enzi na mamlaka na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri,
akizishangilia katika msalaba huo” (Wakolosai 2:13-15).
Katika tafsiri ya Kiswahili cha kisasa maneno hayo
yanaeleweka vizuri zaidi kwani yanasomeka hivi; “Wakati mmoja nanyi
mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa
mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi Uzima pamoja na Kristo MUNGU
AMETUSAMEHE DHAMBI YA DENI ILIYOKUWA INATUKABILI NA MASHARTI YAKE, na kuifuta
kabisa kwa kuipigilia msalabani. Huko Kristo ALIWAPOKONYA NGUVU ZAO HAO PEPO
WATAWALA NA WAKUU; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwa-buruta
kama mateka katika msafara wa ushindi wake” (Wakolosai 2:13-15)
Mungu Baba alipoiona damu ya Kristo imeletwa mbele yake
kwa ajili yetu, ALITUSAMEHE DHAMBI TULIZOMFANYIA, AKATUMIA HIYO DAMU KUFUTA
DHAMBI HIZO KATIKA VITABU AU HATI ZILIZOANDIKWA ILIKUTUSHITAKI – NA BAADA
YAKUZIFUTA DHAMBI HAZIKUMBUKI TENA!
Kama nilivyokuoambia hapo mwanzoni katika agano jipya
Mungu anasamehe dhambi na kuzisahau – wala hazikumbuki tena (Isaya 43:25;
Waebrania 10:17
Ikiwa umetubu dhambi zako – Mungu amekusamehe na wala
hazikumbuki tena kabisa. Kwa kuwa Mungu hazikumbuki dhambi zako tena kabisa,
kwa nini wewe unazikumbuka na hata wakati mwingine unamkumbusha Mungu?
Ukizikumbuka dhambi ulizokwishatubu na kusamehewa
utajisikia kuhukumiwa rohoni mwako. Na ukijisikia kuhukumiwa moyoni unakosa
ujasiri wa kufanya maombi na huduma zingine ulizopewa na Bwana mwisho wake ni
kupoa kiroho na kurudi nyuma.
Imeandikwa hivi; “Wapenzi mioyo yetu isipotuhukumu
tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa
twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (1Yohana
3:21).
Ujasiri wa kupaingia Patakatifu
Kutokufahamu na kutokuamini juu ya uwezo wa Damu ya Yesu
Kristo katika kuondoa dhambi, kumewanya wakristo wengi waishi maisha yaliyo
duni sana kiroho, kimwili na kiakili.
Ili Mtume Paulo aweze kutumika vizuri katika ule wito
alioitiwa na Bwana, ilimbidi ASAHAU KWANZA dhambi alizofanya na kutubu. Mtume
Paulo alisema hivi;
“Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha
kushika; ila natenda neno moja tu; NIKISAHAU YALIYO NYUMA, nikiyachuchumilia
yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito
mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu”
(Wafilipi 3:13,14).Ni mambo gani ya nyuma ambayo Paulo anasema anayasahau kabla
ya kuchuchumilia yaliyo mbele?
Kwa msomaji wa Biblia ni rahisi kukumbuka jinsi ambavyo
Mtume Paulo, wakati huo akiitwa Sauli, alivyowatesa Wakristo na hata kushiriki
katika Kifo cha Stefano. Lakini kwa rehema za Mungu Paulo alitubu na
kusamehewa, na wala Mungu hakumbuki tena kama Paulo aliwahi kushiriki katika
mambo hayo.
Unadhani Mtume Paulo angekuwa bado anasumbuliwa moyoni
mwake na matendo hayo aliyoyafanya kabla ya kutubu angeweza kumtumikia Mungu
vizuri? Ukweli ni kwamba angekwama na kudumaa kihuduma. Ndiyo maana anasema “…ila
natenda neno moja tu; NIKIYASAHAU YALIYO NYUMA nikiyachuchumilia yaliyo
mbele….”.
Je! Unakumbuka baadhi ya maneno aliyomwandikia Timotheo
juu ya kuushinda mtihani huu? Kama unakumbuka ni vizuri. Bali kama hukumbuki
naomba tusome pamoja 1Timotheo 1:12-16). Imeandikwa hivi:-
“Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu aliyenitia nguvu
kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake,
ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri;
lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga na kwa
kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na
pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili
kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe
wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata
rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote
niwe kielelezo kwa wale watakaomwamin baadaye, wapate Uzima wa Milele”.
Ni wazi kwamba Mtume Paulo alifanya mambo makubwa mawili
kabla ya kusonga mbele kwenye wito wake, ambayo tunahitaji kujifunza kutoka
kwake ili na sisi tusonge mbele katika kazi ya Bwana na katika ukristo wetu.
Baada ya kujua ya kuwa amesamehewa na Mungu, Mtume Paulo
alifanya mambo haya mawili (1) Mtume Paulo alijisamehe makosa aliyofanya; na
pia (2) Aliyasahau yaliyo nyuma.
Nakumbuka nilikwenda wilaya fulani na nilikuwa nazunguka
katika vikundi na makanisa mbalimbali kuhubiri na kufundisha neno la Mungu;
Kuna mtu mmoja ambaye alijitokeza kutubu kila nilipoita watu waliokuwa
wanahitaji kutubu.
Mtu huyo alipojitokeza tena mahali pengine Kabla ya
kumwombea, niliamua kumuuliza shida yake.“Je! Ni kosa gani ulilolifanya
linalokufanya utubu kila wakati?” Nikamuuliza
Akajibu akaniambia, “Nilianguka katika dhambi ya
uasherati, naomba uniombee Mungu anisamehe”.
Nikamuuliza tena “Je! ulipoanguka katika dhambi hiyo
ulitubu?”
Akasema; “Ndiyo – tena si mara moja bali mara nyingi, na
naendelea kutubu; kwa hiyo naomba uniombee na wewe kwani nataka kwenda
mbinguni”.
Baada ya kuzungumza naye kwa muda, pia alinieleza ya kuwa
imembidi aache hata kufanya kazi ya Mungu mpaka tatizo hilo liishe, kwani
anajisikia kuhukumiwa moyoni anaposimama mbele za watu kuhubiri, kufundisha au
kuimbisha nyimbo.
Kwa kuyaangalia maandiko nilifahamu ya kuwa huyo Mkristo
alikuwa na matatizo matatu makubwa; (1) Haamini kuwa Mungu anasikia maombi
yake; (2) Haamini kuwa alipoomba msamaha mara tu baada ya kutenda dhambi Mungu
alimsamehe na kusahau;(3) Ameshindwa kujisamehe mwenyewe baada ya kutubu, kwa
hiyo moyo wake unamhukumu, na kwa ajili hiyo amekosa ujasiri wa kusimama na
kuhudumu mbele za Mungu.
Ndipo nilipompa mistari ya Biblia ya kutafakari na baadhi ya mistari hiyo
ambayo nataka na wewe uitafakari ni hii ifuatayo:-
“Mimi, naam, mimi, ndimi niiyafutaye makosa yako kwa
ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako” (Isaya 43:25)
“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa
haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).
“Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa
Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri
zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (1Yohana 3:21,22).
“Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia
Patakatifu kwa DAMU YA YESU…” (Waebrania
10:19)
“Basi
na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupate rehema, na kupata neema
ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:16).
“Na huu
ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake,
atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba atusikia tunazo haja
tulizomwomba” (1Yohana 5:14,15).
Ujasiri
wa kusimama mbele za Mungu katika maombi na katika kumtumikia tunaupata katika
imani tuliyonayo juu ya uwezo wa Damu ya Yesu Kristo kuondoa dhambi.
Baada
ya miezi michache kupita huyo mtu aliyekuwa na shida alivyosaidika na mistari
hiyo; na jinsi anavyosonga mbele vizuri katika wokovu na katika kumtumikia
Mungu.
Fahamu
na amini kuwa Damu ya Yesu Kristo ni ufunguo wa kwenda mbele za Mungu na
kukubaliwa naye. Damu ya Yesu Kristo inakukaribisha mbele za Mungu ili uongee
naye, huku ukimkumbusha ahadi alizokuahidi ndani ya Kristo.
UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUTUPATANISHA
Mzee Yohana alipokuwa akituandikia waraka wake wa kwanza sura ya tatu
mstari wa nne, alisema; “ Kila atendaye dhambi, afanya uasi, kwa kuwa
dhambi ni uasi”.
Dhambi ilipoingia ndani ya moyo wa mwanadamu ilileta mafarakano kati ya
Mungu na mwanadamu. Uhusiano uliokuwapo hapo mwanzo mtu alipoumbwa ulitoweka;
na sura ya Mungu ndani ya mtu ikaondoka, badala ya mwanadamu kuishi katika baraka
alijikuta amejiingiza katika maisha ya laana.
Usiwasingizie jirani zako, au wazazi wako, au watoto wako; au ndugu zako,
au shida uliyonayo ya kuwa ndivyo vinakufanya utengwe na baraka za Mungu.
Fahamu ya kuwa dhambi iliyo ndani yako ndiyo iliyoleta mafarakano kati yako na
Mungu, dhambi hiyo inafanya hata maombi yako yasijibiwe. “Tazama mkono wa
Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa; wala sikio lake si zito, hata lisiweze
kusikia; lakini maovu yenu yamewafarakisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha
uso wake msiuone hata hataki kusikia” (Isaya 59:1,2)
Habari njema iliyomo katika injili ni kwamba Yesu Kristo ndiye MPATANISHI
PEKEE kati yetu na Mungu. Imeandikwa hivi;
“Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye
hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa
sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu ni mmoja, na
mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo
Yesu” ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa
kwa majira yake” (1Timotheo 2:3-6).
Ikiwa Mungu anaona ni ZURI na KUKUBALIKA MBELE ZAKE watu wote
waokolewe, kwa nini watu wengine wanapinga na kuuchukia wokovu mkuu namna hii
ulio ndani ya Yesu Kristo?
Kwa nini hawataki kuiamini na kuipokea injili yenye uwezo wa kuokoa?
(Warumi 1:16).Mtume Paulo anatupa jibu anaposema, “Lakini ikiwa injili
yetu imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao Mungu wa dunia hii
amepofusha fikira zao wasiamini (wasiookoka), isiwazukie nuru ya injili ya
utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu” (2 Wakorintho 4:3,4).
Jambo ambalo Ibilisi hataki watu waone, ni uwezo wa damu ya Yesu Kristo
kama sadaka ya kuwapatanisha kati yao na Mungu. Shetani hataki watu wafahamu ya
kuwa milango ya gereza la dhambi, ugonjwa, mauti, ugomvi na umaskini
imefunguliwa – wasije wakatoka wakamwacha peke yake.
Shetani amewadanganya watu wengi, yamkini hata waliookoka, kuwa
watakubalika mbele za Mungu kwa kushi matendo mazuri peke yake bila kujali
umuhimu wa Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yao.
Ndiyo maana madhehebu mengi ya Kikristo na yale yasiyo ya Kikristo
yamewafundisha waumini wake kuwa wakifuata na kutimiza masharti fulani
waliojiwekea, Mungu atawasamehe na kuwakubali.
Ndiyo maana utawasikia kundi fulani la waliookoka wakiwashutumu kundi
lingine la waliookoka kuwa hawajaokoka sawasawa kwa kuwa hawajafanya kitu
fulani – sijui huwa wanasoma Biblia ipi;
Naamini Biblia unayosoma ni sawa na ninayoisoma mimi wakati huu nayo
inaniambia hivi;“Kwa maana mmekombolewa kwa neema, kwa njia ya
imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu ni kipawa cha Mungu; wala si
kwa matendo mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8,9).
“….hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya
sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili
tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria;
maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. Siibatili
neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi
Kristo alikufa bure” (Wagalatia 2:16,21).
Ni kweli kabisa ikiwa wokovu unapatikana kwa njia ya mtu kujitahidi
kutimiza sheria fulani, au utaratibu wa dhehebu fulani, basi Kristo wetu
alikufa bure, na damu yake ya thamani ilimwagika bure!
Lakini nataka nikukumbushe ya kuwa, Yesu Kristo hakufa bure, wala damu yake
haikumwagika bure!
Kwa nini? “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi bali
kwetu sisi tunaookolewa ni NGUVU YA MUNGU” (1Wakorintho 1:180.
Hakuna sababu ya kuendelea kukaa ndani ya jela ya dhambi, magonjwa shida,
mauti huzuni na umaskini.
Karibu kila mwaka tunasikia viongozi wa nchi mbalimbali wakitangaza msamaha
kwa wafungwa kadhaa kwa ajili ya kusherehekea sikukuu zao.
Nadhani tutashangaa sana kama bado tutasikia kuwa wafungwa hao
wameng’ang’ania kukaa gerezani hata baada ya msamaha kutangazwa, na milango ya
gereza kufunguliwa.
Mungu wetu ametutangazia msamaha ndani ya Kristo, tunatakiwa kuupokea, na
kuwaeleza watu wengine upatanisho huu ulio katika damu ya Yesu Kristo. Hii
ndiyo Injili ya kweli – kuwatangazia watu msamaha wa dhambi na ushindi dhidi ya
dhambi unaopatikana ndani ya Kristo Yesu.
Wakristo wanahitaji kujua ya kuwa baada ya kupatanishwa na Mungu katika
Kristo, shetani hana mamlaka tena ya kuweka dhambi, magonjwa, huzuni, faraka,
na umaskini juu yao. Shetani hana mamlaka tena juu ya yule aliyepatanishwa na
Mungu katika damu ya Yesu Kristo.
Kwa nini? Kwa sababu Mungu mwenyewe, “alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake; ambaye katika
yeye (Kristo) tuna ukombozi, Yaani msamaha wa dhambi” (Wakolosai
1:13,14).
Unapotakaswa na Damu ya Yesu Kristo, unawekwa huru mbali na dhambi na
hukumu yake – tena unakuwa huru kweli kweli.
Kwa Damu ya Yesu Kristo unaweza ukasimama na kuomba mbele za Mungu bila
hofu. Imeandikwa hivi; “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia
patakatifu kwa damu ya Yesu; ….”(Waebrania 10:19)
Kwa Damu ya Yesu Kristo unaweza ukasimama mbele ya shetani na majaribu yake
bila hofu – kwa kuwa hana kitu anachokudai wala cha kukushitaki mbele ya Mungu.
Bwana Yesu Kristo amekwisha kukulipia deni lako! Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata imekuwa,
mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita
tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha
sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho” (2 Wakorintho 5:17,180.
Ewe Mkristo, Usikubali dhamiri yako ikuhukumu kwa kosa ulilokwisha litubia,
na kufutwa na damu ya Yesu Kristo. Pokea msamaha na upatanisho kwa imani ndani
ya Kristo kama yanenavyo maandiko. Songa mbele katika ahadi na utumishi wa
Bwana. Usichoke wala kuona aibu kuwaeleza watu wengine habari hii njema ya kuwa
Mungu amewasamehe dhambi zao katika Kristo, - wampokee Yesu Kristo mioyoni mwao
kama Bwana na Mwokozi wao.
Ulimwengu mzima na kila mtu akaaye ndani yake anapaswa kujua ya kuwa “MUNGU
ALIKUWA NDANI YA KRISTO, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie
makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” (2Wakorintho
5:19).
UPATANISHO KATI YA MTU NA MTU
Nakumbuka mtu mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri juu ya tatizo lililokuwa
linamkabili, akasema; “ Kuna mtu ambaye tulikwaruzana na kugombana na mimi
nimemsamehe; lakini tatizo nililonalo ni kwamba naona hanisemeshi wala
hanisalimii. Mimi nikimsalimia haitiki. Naona kuna uzito fulani unaokwamisha
uhusiano wetu na mimi sijui nifanye nini – kwa kuwa si vizuri tuishi namna
hii”.
Mara kwa mara nimekutana na watu wenye matatizo yanayofanana ya shida ya
mtu huyu niliyokueleza. Wengine hawaelewani na wenzao kazini. Wengine
hawaelewani na ndugu zao. Wengine hawaelewani katika ndoa zao. Mume na mke
hawazungumzi, ingawa wakati mwingine wanaishi chumba kimoja.
Swali kubwa nililokuwa nalipata katika maelezo yao ni – wafanyeje ili
wapatane tena na hao waliogombana nao? Swali hili naamini lilikuwa linawasumbua
kwa sababu wanafahamu imeandikwa kuwa; “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani
na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa
nao, mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije
likachipuka na kuwasumbua, na watu wengine wakatiwa unajisi kwa hilo”
(Waebrania 12:14,15).
Baada ya kukabiliwa na swali hili mara kwa mara; sikuchoka kumwomba Mungu
ili anipe jibu sahihi la kuwapa watu hao, ili WAPATANE UPYA na hao ambao
hawaelewani nao.
Ndipo Roho Mtakatifu akaniongoza kusoma mistari ifuatayo kwa upya;“Lakini
sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu
kwa DAMU YAKE KRISTO. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi
sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati
KILICHOTUTENGA. Naye akiisha kuuondoa ule UADUI KWA MWILI WAKE; ndiyo
sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa MTU MPYA
MMOJA ndani ya nafsi yake; akafanya AMANI. AKAWAPATANISHA WOTE
WAWILI NA Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya MSALABA, AKIISHA KUUFISHA
ULE UADUI KWA HUO MSALABA” (Waefeso 2:12-17).
Baada ya kusoma na kuyatafakari maneno haya nilijua hakika ya kuwa Roho
Mtakatifu ananionyesha ya kuwa kuna UWEZO KATIKA DAMU YA YESU KRISTO
kuwapatanisha watu wawili ambao hawaelewani.
Niliamini hivyo; na bado naamini hivyo na nitaendelea kuamini hivyo kuwa
kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo – kuwapatanisha watu wawili waliogombana,
na kuuondoa uadui uliokuwa katikati yao ukiwatenganisha. Nadhani sitakosea
nikisema na wewe unaamini hivyo – Je! ni kweli?
Ingawa niliamini katika uwezo wa damu ya Yesu Kristo katika kuwapatanisha
watu wawili waliogombana – bado nilikuwa nimekabiliwa na swali moja kubwa.
Swali hilo nililojiuliza ni hili; “ Nitawezaje kuichukua damu ya Yesu
Kristo toka mbele ya kiti cha enzi ilipowekwa na Yesu Kristo mwenyewe miaka
karibu 2,000 iliyopita – niichukue ili inisaidie kuondoa ugomvi uliopo kati
yangu na mtu mwingine na hatimaye kutupatanisha?”
Hili swali halikuwa jepesi – kwa hiyo nilianza tena kumwomba Mungu ili
anifafanulie na kunifundisha juu ya jambo hili.
Roho Mtakatifu akanikumbusha tena mistari ifuatayo;“Hata imekuwa, mtu
akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama!
Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha
nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu
alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu NENO LA UPATANISHO! Basi tu wajumbe
kwa ajili ya Kristo, kana kwamba MUNGU ANASIHI KWA VINYWA VYETU; twawaomba
ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu” (2Wakorintho
5:17-20).
Kwa kuniongoza kusoma na kutafakari maneno haya, Roho Mtakatifu alitaka
nifahamu ya kuwa;
(a) Mtu aliye ndani ya Kristo (aliyeokoka),
Mungu mwenye uwezo wa kupatanisha anakaa ndani yake, naye amempa HUDUMA YA
UPATANISHO na NENO LA UPATANISHO.
(b) Ugomvi kati ya mtu na mtu umeletwa na UASI na
upatanisho unaletwa na UTII – kutii maagizo ya Mungu.
Ndipo Roho Mtakatifu aliponikumbusha Marko11:22,23, nayo inasema hivi; “Yesu
akajibu, akamwambia, Mwamini Mungu. Amin, nawaambia, Yeyote atakayeuambia mlima
huu ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake ila aamini kwamba
hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.”
Kwa kuniongoza kusoma na kutafakari maneno haya Roho Mtakatifu alitaka
nifahamu ya kuwa NATAKIWA KUSEMA KILE NINACHOKIAMINI WALA NISIONE SHAKA
MOYONI MWANGU, BALI NIAMINI KWAMBA KILE NIKISEMACHO KIMETUKIA NACHO
KITAKUWA CHANGU!
Naamini kitu gani? Kumbuka nilikuambia naamini kuwa kuna uwezo katika Damu
ya Yesu Kristo kupatanisha watu wawili wasiopatana au waliogombana.
Kwa hiyo nikiona uzito fulani unaingia kati yangu na mtu mwingine na hata
kusababisha kutoelewana, NILISEMA NINACHOKIAMINI JUU YA DAMU YA YESU KRISTO.
Huwa nasema maneno haya; “ Katika jina la Yesu Kristo nanyunyiza damu ya
Yesu Kristo juu ya Uadui na Kiambaza kinachotufanya tusielewane mimi na –
(nataja jina la mtu huyo). Uadui na ugomvi uondoke kwa damu ya Yesu Kristo,
tupatane na tuwe na Amani na maelewano – Amina”.
Halafu baada ya kusema hivyo, naamini kuwa hayo niliyoyasema yametukia,
nayo yamekuwa yangu – yaani uadui haupo tena, bali tumepatanishwa na Damu ya
Yesu Kristo.
Nataka nikuambie, namshukuru sana Mungu kwa kunifundisha hili, kwa kuwa
nimepata msaada mkubwa wa kutatua matatizo yangu na ya wengine pia.
Mama mmoja aliwahi
kuja kuomba ili tusaidiane kuomba kwa kuwa alikuwa amefukuzwa toka nyumbani
kwake na mume wake, bila nguo za kubadili wala fedha. Mpaka wakati huo tulipokuwa
tukiongea alikuwa anakaa kwa jirani.
Katika mazungumzo
tuliyokuwa nayo na yule mama nilifahamu kuwa alikuwa hajaokoka – yaani hayuko
ndani ya Yesu Kristo. Nikamshauri nikasema; ‘Mama, ukimpokea Yesu Kristo moyoni
mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, Yeye ni kazi yake kutua mizigo ya uliolemewa
nayo ili akupumzishe. Na Yeye ukimpa maisha yako atakusaidia kuondoa tatizo
lako’.
Huyu mama alikubali
ushauri huo, kwa hiyo nikamwongoza kusema sala ya toba na ya kumpokea
Yesu Kristo moyoni mwake.
Nikamuuliza; “Unataka
tuombe nini juu ya tatizo lako?”
Yule mama alinieleza
mambo mengi aliyotaka aombewe, na mojawapo ya hayo ni kwamba uadui uliopo kati
yake na mume wake uondoke, waishi kwa amani, pia amwite arudi nyumbani bila
masharti.
Baada ya kusema
mahitaji hayo tukaanza kuomba. Kati ya maneno niliyosema katika sala ile ni
haya “Katika jina la Yesu Kristo
nauondoa uadui uliopo kati ya mama huyu na mume wake – uondoke kwa damu ya Yesu
Kristo , wapatane na kuwa na amani. Mume wake asipate
amani moyoni mwake mpaka amrudishe mke wake nyumbani bila masharti …..” Halafu nikaamini
kuwa hayo niliyosema yametukia nayo ni yangu. Tukaagana na mama huyo baada ya
maombi hayo.Kesho yake nililetewa ushuhuda ya kuwa mume wa yule mama
alimrudisha mke wake siku ile ile baada ya maombi hayo.
Damu ya Yesu Kristo ibarikiwe! Jina la Yesu Kristo libarikiwe! Nataka
usikate tamaa unapokosa maelewano na mtu, kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo
wa kukupatanisha naye.
Kabla ya kuchapa
mafundisho haya ya Damu ya Yesu Kristo katika kitabu, nilikuwa kwanza
nimeyasambaza kwa watu wachache kwa njia ya jarida. Baada ya muda nilipata
barua ifuatayo toka kwa mtu mmoja aliyekuwa amesoma mafundisho hayo:
“Ninamshukuru Mungu
kwa ajili ya upendo uliomo ndani yako katika kuzihudumia roho za watu wake
ambao wanaangamia kwa kukosa MAARIFA.
Ninamshukuru Mungu
mwenye uweza wote, katika jina la Yesu Kristo kwa nguvu na uweza wa Roho
Mtakatifu, jinsi alivyokuamsha kuweza kuniletea masomo kwa wakati unaohitajika
sana kwangu – MUNGU AKUBARIKI SANA.
Nakala ya somo la
FAHAMU UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO nililipata. Kwa kweli
baada ya kuisoma hiyo nakala, kukatokea upingamizi mkubwa sana katika ulimwengu wa roho kiasi kwamba ni
wiki mbili sasa sijapata usingizi vizuri. Nafahamu ni kwa sababu ya kujua UWEZO WA
DAMU YA YESU KRISTO – Hasa katika UPATANISHO KATI YA MWANADAMU NA MWANADAMU na
pia katika ULINZI NA KINGA. Hivyo nikasoma kwa uangalifu sana na kuweka katika matendo niliyoyasema.
Jambo la kushangaza ni kuwa jirani yangu ambaye alikuwa haongei nami baada ya
kuomba toba kwa ajili yake na kunyunzia damu ya Yesu katika ukuta unaoleta adui
sasa tunaongea vizuri. Na pia nguvu za kichawi ambazo zinaelekea zilikuwa
zinazunguka sana
nyumba yangu ziliweza kujidhihirisha wazi usiku kwa kuzungumza dhahiri huko nje
ya nyumba kwenye saa 9:30 usiku wakati ninapoamka ili kufanya maombi ya usiku
wa manane; sasa zimetoweka kabisa…
Pia nilikuwa kwa
muda wa miezi mingi kiasi cha nusu mwaka nilikuwa nashindwa kuamka usiku wa
manane ili kufanya maombi kama ilivyokuwa kawaida yangu siku za nyuma, maana
usingizi ulinizonga kiasi cha kukosa kuzinduka usiku, lakini la KUMSHUKURU
MUNGU ni kuwa baada ya kumkemea shetani na kuifunga roho ya usingizi na
kunyunyizia DAMU YA YESU kwa ajili ya ULINZI NA KINGA, sasa naamka usiku wa
manane na kufanya maombi mpaka saa 11:30 asubuhi. JINA LA BWANA LIBARIKIWE SANA .”
UZIMA
WA MILELE KATIKA DAMU YA YESU KRISTO
“Basi Yesu
akawaambia, Amini, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na
kunywa damu yake, hamna Uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa
damu yangu anao UZIMA WA MILELE; nami nitamfufua siku ya
mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli; na damu yangu ni
kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani
yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba
aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila
atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:53-57).
Mtu ambaye ameula
mwili wa Kristo na kuinywa damu yake ile iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye
anakaa ndani ya Yesu Kristo, na Yesu Kristo anakaa ndani yake. Kwa maneno
mengine amepokea uzima wa Mungu, ambao ni uzima wa milele.
Unapompokea Yesu
Kristo moyoni mwako unapokea uzima wa milele; kwa kuwa, “Ndani yake ndimo
ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yohana 1:4).
Inatupasa tukumbuke
ya kuwa, kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo
mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.
Pia, inatupasa
tukumbuke ya kuwa, “ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu
ya yule mmoja, zaidi sana
wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika UZIMA
kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).
Dhambi inapoingia
mahali inaleta mauti, magonjwa, uasi, ubishi, umaskini na kutokufanikiwa. Uzima
wa milele unapoingia ndani ya mtu unaleta, - Uzima, uponyaji, amani, upendo,
utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu.
UZIMA WA MILELE NA
UPONYAJI
Kabla sijampokea
Yesu Kristo moyoni mwangu awe Bwana na Mwokozi wangu, nilisumbuliwa sana na magonjwa.
Nakumbuka nilikuwa
nasumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara. Nilipokwenda kupimwa hospitali
kwa daktari, niliambiwa nina ugonjwa wa vidonda vya tumbo ‘Ulcers’ na
pia ‘High blood pressure’.
Nilipewa dawa za
kutumia, na pia niliambiwa nisile vyakula vya aina fulani maana vitaniongezea
ugonjwa.
Niliyafuata
masharti ya daktari, na nilipata nafuu kidogo. Lakini kitu cha kushangaza ni
kwamba mara kwa mara magonjwa yalinirudia na kunisumbua sana – sikujua kitu cha kufanya. Baada ya
miaka kadha neema ya Bwana ilifuniliwa moyoni mwangu, nikaokoka baada ya kutubu
na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wangu. Mabadiliko yaliyotokea
katika maisha yangu ni makubwa mno. Wakati huo nilikuwa sijajua ni kitu gani
kimetokea – lakini nilijua kuwa ninaishi maisha mapya.
Nilishangaa kuona
kuwa miezi kadhaa imepita bila kusumbuliwa na magonjwa. Kichwa hakikiniuma
tena, moyo uliacha kwenda mbio tena vyakula vingine nilivyokatazwa nisile na
daktari havikunidhuru nilipovila tena kama
mwanzo. Nilijua hakika kuwa nimepona!
Wakati huo sikuweza
kufahamu kitu kilichotokea hata nikapona mara moja namna hiyo. Lakini kwa kadri
ambavyo Roho Mtakatifu alivyoendelea kunikuza katika wokovu nilikuja kufahamu
ya kuwa MSAMAHA WA DHAMBI UNAONGOZANA NA UPONYAJI WA MWILI.
Kabla ya mwanadamu
kutenda dhambi, hakukuwa na magonjwa. Dhambi ilipoingia ilileta na magonjwa
pia. Sadaka ya uhai wa Yesu Kristo msalabani ilileta msamaha na ondoleo la
dhambi na madhara yake yote ikiwa ni pamoja na MAGONJWA.
Unapompokea Yesu
Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, unampokea MPONYAJI. Roho wa
Uzima wa milele anayeingia kutawala maisha yako, ni Roho wa Uponyaji
anayefukuza magonjwa yote ndani yako na kukupa afya.
Ndiyo maana
imeandikwa hivi; “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea (Yesu Kristo) wengi
wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,
ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa
udhaifu wetu, na KUYACHUKUA MAGONJWA YETU” (Mathayo 8:16,17). Soma pia
(Isaya 53:4,5)
Kwa kuwa alichukua
dhambi zetu, dhambi hizo zimeondolewa kwetu, na tumepokea utakatifu wake. Kwa
kuwa alichukua magonjwa yetu, hakuna sababu ya sisi kuendelea kuumwa kwa kuwa
tumepokea uponyaji wake. Ndiyo maana imeandikwa hivi;
“Yeye mwenyewe
(Yesu Kristo) alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili
tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki;
na KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA” (1Petro 2:24).
Angalieni anasema, “
Kwa kupigwa kwake MLIPONYWA” na siyo ‘MTAPONYWA’. Ikiwa TULIPONYWA
kwa hiyo sasa TUMEPONA!
Ndiyo maana watu
wengi sana
nimewasikia wakishuhudia ya kuwa magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua kwa muda
mrefu yamepona baada ya kumpokea Yesu Kristo mioyoni mwao na kuokoka.
Kuna mama mmoja
alinishuhudia ya kuwa alisumbuliwa sana
na majini kwa muda wa miaka kumi na mitatu. Alikwenda hospitali – hakupona.
Alikwenda kwa waganga wa kienyeji – hakupona. Mwili wake ulidhoofu sana .
Siku moja neema ya
Mungu ilimzukia aliamua kuokoka. Mhubiri aliposema watu wanaotaka kuokoka waje
mbele, huyo mama naye alikwenda – akafanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu
Kristo moyoni mwake.
Mama huyo alinambia
tangu wakati huo maumivu aliyokuwa nayo mwilini kwa miaka 13 yaliondoka. Mume
wake na ndugu zake walishangaa sana .
Tangu wakati huo aliookoka na kupona hadi alipokuwa ananisimulia ilikuwa
imepita miaka minne, na bado alikuwa amepona na afya njema.
UZIMA WA MILELE NA
MABADILIKO YA TABIA:
“Hata imekuwa, mtu
akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama!
Yamekuwa mapya”
(2Wakorintho 5:17)
“Naye
alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme
wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi yaani,
msamaha wa dhambi”.(Wakolosai 1:13,14).
Yesu Kristo alisema
ukiula mwili wake na ukiinywa damu yake yeye anakaa ndani yako na wewe unakaa
ndani yake – unapokea uzima wake au uzima wa milele.
Mtu akiwa ndani ya Kristo, anakuwa mtu mpya. Mtu anapokuwa ndani ya Kristo
anabadilika tabia yake kwa kuwa amehamishwa toka katika nguvu za giza na tabia
yake na kuingia katika ufalme wa Kristo na tabia ya Kikristo.
Mtu akiwa ndani ya Kristo anavua utu wake wa kale na kuvaa utu mpya –
anavaa tabia mpya.
Wakati fulani nilikuwa mji fulani hapa nchini nikihubiri mkutano wa siku
nane, asubuhi moja alikuja mzee mmoja kuniona katika hotel niliyokuwa ninakaa.
Yule mzee akasema; “ Unakumbuka jana ulipoita watu wanaotaka kuokoka waje
mbele waombewe, kuna mtoto mmoja alikuwa wa kwanza kufika mbele”.
“Ndiyo, nakumbuka”; Nikamjibu.
Yule mzee akaendelea kusema; “Yule mtoto ni wa kwangu, na tangu jana
kumetokea mabadiliko makubwa mno ya tabia, nikaona heri nije nikushirikishe”.
Nikamuuliza, “Kumetokea mabadiliko gani?”
“Huyu mtoto wangu”; yule mzee alieleza; “Kabla ya jana alipoamua kuokoka,
alikuwa si mtii, alikuwa hapendi usafi, alikuwa hawezi hata kutandika kitanda
chake akiamka asubuhi. Hata tukimwambia afagie uwanja unaozunguka nyumba yetu
alikuwa hasikii. Kweli, tumempiga fimbo mpaka tuliogopa tutamuumiza. Lakini
kuanzia jana alipookoka (sisi tulifikiri anatania) tabia yake imebadilika
kabisa. Amekuwa mtii, kazi anajituma kufanya, amekuwa msafi, hata wakati
wa usiku, anachukua biblia na kusali yeye mwenyewe – maajabu haya”.
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na kuinywa damu yake, yeye atakaa
ndani yako na wewe utakaa ndani yake unapokea uzima wake wa milele unaokuvika
tabia ya Uungu.
Haya ndiyo yaliyotokea kwa huyu mtoto mdogo wa umri wa miaka kumi na
miwili. Huyu mtoto alipompokea Yesu Kristo na kuokoka – Kiroho aliula mwili wa
Yesu na kuinywa damu yake – akapokea uzima wa milele, Yesu Kristo aliingia
ndani ya mtoto, na mtoto akaingia ndani ya Yesu Kristo – yote yalifanyika kwa
Uwezo wa Roho Mtakatifu.
Unadhani mtoto huyu alipata wapi ujasiri wa kufanya sala yeye mwenyewe,
kitu ambacho alikuwa anaogopa kufanya kabla hajaokoka?
Jibu lake ni – Damu ya Yesu Kristo! Imeandikwa hivi; “Basi ndugu, kwa
kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu…….” (Waebrania
10:19).
Niliwahi kukaribishwa katika mkoa mwingine kuhubiri katika Kanisa fulani,
nakumbuka kuwa nilihubiri juu ya Bartimayo yule kipofu aliyeponywa na Yesu
Kristo kule Yeriko. Nilipomaliza mahubiri nilikaribisha watu waje mbele wale
wanaotaka kuokoka na kuombewa magonjwa.
Watu wengi waliokoka na pia kuponywa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua.
Baada ya wiki moja kupita, alikuja mtu mmoja nyumbani kwangu tukasalimiana
na nikamkaribisha aingie ndani. Alipokwisha kukaa kwenye kiti, akaniuliza
akasema; “ Mlimpa kitu gani ndugu (alitaja jina lake) siku mlipokuja kuhubiri
kanisani kwetu – maana mimi sikuwepo.”
Nikamuuliza, “Kwani kumetokea nini?”
Yule mgeni akasema; “Huyo ndugu alikuwa hawezi kunywa chai ya maziwa wala
maziwa – akinywa maziwa alikuwa anaugua. Nilishangaa siku moja alifika
nyumbani, nilipomkaribisha chai ya rangi alikataa, akasema sasa anakunywa chai
ya maziwa bila shida yoyote."
“Nilipomuuliza ameanza lini kunywa chai ya maziwa, akasema tangu baada ya
maombi ya Jumapili pale Kanisani. Lakini pia, niliona tabia yake imebadilika.
Alikuwa hachani nywele- sasa anachana. Alikuwa mlevi sana – sasa haonji tena
pombe. Alikuwa mchafu, hajijali – nilishangaa kumwona amevaa nguo safi. Ni kitu
gani mlimpa?”
Nikamjibu nikasema; “ Sisi tulichokifanya ni kuhubiri habari za Yesu Kristo
na uwezo wake. Ndugu yako alifungua moyo wake siku ile, akampokea Yesu Kristo
moyoni mwake ili awe Bwana na Mwokozi wake akaokoka. Pia tukamuombea tatizo la
ugonjwa alilokuwa nalo na Bwana akamponya”.
Ni jambo la kumsifu Mungu sana katika Kristo, kwa sababu baada ya huyo
ndugu kuokoka, na maisha yake kubadilika – sasa hivi ana kazi nzuri ya
kuajiriwa na pia, ni mhubiri wa injili. Jina la Bwana libarikiwe!
Huwezi ukampokea Yesu Kristo moyoni mwako na bado ukawa na tabia uliyokuwa
nayo zamani. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako – unapokea Uzima wa milele
unaokupa tabia ya Uungu.
Yesu Kristo alisema hivi; “ Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili
wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna Uzima ndani yenu…..Aulaye mwili
wangu na kuinywa DAMU YANGU hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kaeni
ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa pekee yake,
lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni
mzabibu; ninyi ni matawi akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;
maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote…….Ninyi mkikaa ndani yangu,
na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana
6:53,56; Yohana 15:4,5,7)
Mtume Paulo
alisema; “ Hata imekuwa, mtu akiwa NDANI YA KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya
kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
Mtume Paulo alisema
hivi katika waraka wake wa pili kwa watu wote, sura ya kwanza mstari wa tatu na
wa nne; “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo
uzima wa utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake
mwenyewe. Tena kwa hayo atumetukirimia ahadi kubwa mno, za THAMANI, ili kwamba
kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo
duniani kwa sababu ya tamaa”.
UWEZO WA DAMU YA YESU KRISTO KATIKA KUTULINDA
Wajenzi wa nyumba huwa wanasubiri msimu wa mvua ili kuwa na uhakika wa
kusema nyumba imekamilika au bado. Wakati huo wa mvua inakuwa rahisi kufahamu
kama nyumba inavuja au haivuji.
Watu wengi walio wakristo hawaamini kuwa kuna nguvu na uwezo wa ajabu,
usiotamkika, na usiopimika katika DAMU YA YESU KRISTO unaoweza kutulinda dhidi
ya mshambulizi ya adui yetu shetani.
Wakristo wengi wanaamini ya kuwa katika damu ya Yesu Kristo kuna utakaso,
kuna msamaha, na pia kuna upatanisho. Lakini ni wakristo wachache wanaofahamu
ushindi wa ulinzi uliomo ndani ya damu ya Yesu Kristo.
Kwa mfano kwa muda mrefu nilikuwa naisoma mistari ifuatayo bila kufahamu
maana yake hasa ya kiroho. Imeandikwa hivi;
“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao;
ambao hawakupenda maisha yao hata kufa” (Ufunuo 12:11)
Hatua kwa hatua, Roho Mtakatifu alianza kunionyesha na kunifafanulia maana
ya maneno hayo.
Niliwahi kusoma ushuhuda ufuatao katika gazeti moja juu ya uwezo wa damu ya
Yesu Kristo, ambao ulinifanya nitafakari mara kwa mara juu ya uwezo wa damu ya
Yesu Kristo ili kutaka kujua undani wake hasa.
Hilo gazeti liliandika ya kuwa kuna mhubiri mmoja aliyekuwa akifanya kazi
ya kueneza neno la Kristo katika kijiji fulani.
Siku moja huyo mhubiri alikuwa sehemu moja ya kijiji hicho akifungua –
fungua mizigo, mara ghafla akasikia maumivu makali mkononi, kama vile ameumwa
na kitu fulani. Alipoinua mkono unaoumwa ili auangalie alimwona nge mwenye sumu
kali ameng’ang’ania katika mkono wake. Wanakijiji wengi waliokuwa wakisaidiana
naye mahali hapo walipomwona huyo nge akimuuma – wakaingiwa na hofu kubwa
wakidhani ya kuwa mhubiri huyo hakika atakufa.
Mhubiri huyo wa neno la Kristo, alikuwa si mwenyeji wa kijiji hicho. Yeye
hakufahamu kuwe nge wa aina hiyo kama aliyemuuma ana sumu kali ya kuua. Kwa
hiyo alibaki anashangaa kwa nini wanakijiji waliomzunguka wameingiwa na hofu
kubwa kwa tukio hilo.
Huyo mhubiri akakung’uta mkono wake uliokuwa umeng’ang’aniwa na nge huku
akisema; “Katika jina la Yesu Kristo nanyunyiza damu ya Yesu”. Yule nge akaanguka
chini.
Baada ya hapo, huyo mhubiri akaondoka hapo alipokuwa akiangalia mizigo, na
kuelekea ofisini kwake karibu na jengo la kuabudia. Wanakijiji wengi wakamfuata
nyuma kwa huzuni wakijua kuwa atanguka chini afe kwa sababu ya sumu ya nge
huyo. Pia walijua kijijini hapo hapakuwa na dawa ya kuondoa sumu ya nge huyo
katika damu ya mtu – kwa hiyo walijua mhubiri huyo atakufa tu.
Yule mhubiri alipoona watu wengi wamemfuata, akaamua kuhubiri injili na
kuwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi ya kuwa hatakufa kwa kuwa hatakufa maana
alisema “ Katika jina la Yesu Kristo nanyunyizia damu ya Yesu dhidi ya sumu ya
nge”. Na kweli yule mhubiri hakufa kwa sababu ya ile sumu ya nge.
Nilipoisoma habari hii katika gazeti hilo, nilianza kutafakari kwa upya juu
ya damu ya Yesu Kristo. Nilikuwa sijawahi kusikia – mpaka nilipoona katika
gazeti hilo – kuwa mtu anaweza kutumia Jina la Yesu Kristo na damu yake kwa
pamoja namna hiyo.
Ndipo Roho Mtakatifu aliponikumbusha ya kuwa uwezo tuliopewa wa kulitumia
jina la Yesu Kristo, unatokana na uhusiano wetu na Kristo tulionao katika agano
jipya ndani ya DAMU YA YESU KRISTO. Na bila kujua kazi ya damu ya Yesu Kristo
kwetu, ni vigumu kujua siri ya kulitumia na kuliamini jina la Yesu Kristo kama
inavyostahili.
Wakati fulani tulikuwa tunafanya maombi nyumbani kwangu na wenzetu fulani,
Roho Mtakatifu alisema maneno yafuatayo “ Waambie watu wangu, wajitakase,
wapake damu yangu katika miimo ya milango. Waambie watu wajitakase, kila mtu na
nyumba yake.
Waomboleze kwa ajili ya jambo hilo…..Watu wangu wamenitenda dhambi.
Lakini kama watatubu na kuacha nitaghairi….Nataka Kanisa (Wakristo)
linalofaa. Wote mvae vazi jeupe lisilo na doa wala waa. Muwe tayari kwa arusi –
arusi i karibu ndiyo maana nimekueleza hayo…….”
Nilipousikia ujumbe huo, nilikumbuka maneno ambayo Mungu alimwambia Musa
kabla ya kuwapiga wamisri pigo la kumi. Baada ya Musa kupokea maneno ya Mungu
biblia inatuambia ya kuwa;
“Hapo ndipo Musa akawaita Wazee wa Israeli, na
kuwaambia Nendeni, mkajitwalie wana-Kondoo kama jamaa zenu
zilivyo mkamchinje pasaka. Nanyi twaeni tawi la hisopu,
mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini, na kukipiga kizingiti
cha juu na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika
bakuli, tena mtu yeyote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba
yake hata asubuhi. Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na
hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo
miwili, Bwana atapita juu ya mlango, WALA HATAMWACHA MWENYE
KUHARIBU AINGIE NYUMBANI MWENU KUWAPIGA NINYI. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa
ni amri kwako na kwa wanao milele” (Kutoka
12:21-24).
Jambo hili tanatakiwa tulitunze kuwa amri kwetu na watoto wetu milele kwa
DAMU YA YESU KRISTO ambaye ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili
yetu. Katika msamaha na Upatanisho wa damu yake tunapata ULINZI juu yetu na
watoto wetu dhidi ya mashambulizi ya shetani aliye mharibifu.
Nilipokuwa nikiyalinganisha maneno aliyoambiwa Musa na Mungu, na yale
tuliyoambiwa sisi na Roho Mtakatifu tulipokuwa tunaomba nilifahamu ndani ya moyo
wangu mambo mawili yanayokwenda kutokea juu ya kizazi hiki cha sasa.
Jambo la KWANZA litakalotokea ni; hukumu au pigo juu ya watu na
familia zao kwa sababu wamemtenda Mungu dhambi – wameasi maagizo yake.
Jambo la PILI litakalotokea ni; Mungu atawalinda wasipatwe na hukumu
au pigo hilo wale wote watakaotubu dhambi zao. Damu ya Yesu Kristo itakuwa
ulinzi juu ya roho zao, miili yao, akili yao, watoto wao na mali zao. Yule
mharibu hatawadhuru kwa kuwa ATAIONA DAMU YA YESU KRISTO IKIFANYA KAZI KATIKA
MAISHA YAO.
Nilipokuwa naendelea kuomba na kutafakari juu ya ujumbe huu, Roho Mtakatifu
alinikumbusha maneno yafuatayo;
“Ninyi nanyi kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho,
UKUHANI MTAKATIFU, mtoe dhahibu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa
njia ya Yesu Kristo……. Ninyi ni mzao mteule, UKUHANI WA KIFALME, taifa
takatifu, watu wa Milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye
aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:5,9)
Kuhani wa agano la kale alipokuwa anakwenda mbele za Mungu kufanya
upatanisho wa watu wa Israeli na Mungu – alikuwa kwanza anachukua damu ya
mafahali au ya kondoo- halafu anafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zake
mwenyewe halafu ndipo afanye upatanisho kwa ajili ya watu. Baada ya toba hiyo
wana wa Israeli walikuwa wana uhakika wa msamaha na kwamba MUNGU ATAWALINDA
TOKA MASHAMBULIZI YA MAADUI NA YA MAGONJWA.
Katika agano jipya lililosimikwa kwa damu ya Yesu Kristo, kila mtu
aliyeokoka au aliye mkristo wa kweli na si mkristo wa jina tu – ni KUHANI MTAKATIFU,
KUHANI WA KIFALME, MZAO MTEULE, MTU WA MILKI YA MUNGU, ANAO UJASIRI WA
KUPAINGIA PATAKATIFU KWA DAMU YA YESU KRISTO kwa ajili yake, ndugu zake na watu
wengine pia!
WEKA KATIKA MATENDO MANENO ULIYOYASIKIA
Musa aliposikia maneno hayo toka kwa Mungu, ALITII akawaita wazee wa
Israeli na kuwaeleza yote maagizo hayo. Wazee wa Israeli waliposikia WALITII,
na wakawaeleza na kuwaongoza wana wa Israeli kufanya maagizo hayo. Wana wa
Israeli wasingetii maneno hayo waliyoyasikia toka kwa Mungu, wao pia wangepatwa
na pigo lile lililowapata Wamisri.
Wana wa kwanza wa familia za Israeli walipona kufa kwa sababu WALISIKIA,
WAKATII, WAKAYAFANYA MAAGIZO YA MUNGU. Na sisi tukitaka kupona mapigo
yanayozidi kushuka juu ya kizazi hiki kwa sababu ya dhambi basi tunahitaji KUSIKIA
MANENO AMBAYO ROHO MTAKATIFU ANAWAAMBIA WATU WAKE LEO; TUTII NA KUYAFANYA
MAAGIZO YAKE – TUSIPOTII NA KUTUBU HAKIKA TUTAANGAMIA!
Kwa hiyo ukitaka wewe na wote walio katika nyumba yako mlindwe na DAMU YA
YESU KRISTO – fanya hivi;
1. Tubu kwa ajili yako mwenyewe
kwanza, halafu;
2. Tubu kwa ajili ya kila mmoja aliye
pamoja nawe katika nyumba hiyo unayokaa.
Mungu atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi
nyote KUWALINDA dhidi ya mashambulizi ya Ibilisi, soma Kutoka 12:21-24.
Ukitaka wewe na wote walio katika nchi yako mlindwe na DAMU YA YESU KRISTO
–fanya hivi;
1. Tubu kwa ajili yako mwenyewe
kwanza, halafu;
2. Tubu kwa ajili ya watu wote walio
katika nchi hiyo pamoja na wewe.
Mungu atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi
nyote humo nchini KUWALINDA dhidi ya maharibifu ya Ibilisi, soma 2 Mambo ya
Nyakati 7:14.
Ukitaka wewe na wote walio katika chombo unachosafiria, gari dogo au basi
la abiria, au ndege au meli mlindwe na DAMU YA YESU KRISTO – fanya hivi kabla
ya kuanza safari;
1. Tubu kwa ajili yako mwenyewe
kwanza, halafu;
2. Tubu kwa ajili ya wote
mtakaosafikiri nao hata kama hawafahamu.
Mungu Baba atasikia na kuwasamehe. Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi
katika safari hiyo KUWALINDA dhidi ya mashambulizi na mitego ya Ibilisi soma,
Matendo ya Mitume 27:21-26.
Nakumbuka wakati
fulani mimi na rafiki yangu (wawili tu) tulikuwa tunasafiri kwenda Tukuyu
kwenye mkutano wa injili. Tulikuwa kwenye gari lenye uwezo wa kuchukua abiria
watano, lakini tulikuwa wawili tu na mimi nikiendesha. Kabla hatujaondoka
tulifanya sala kama ninayokuambia hapo juu.
Tulipofika kati ya miji ya Dodoma na Morogoro, tulisimamishwa na askari wa
usalama barabarani. Niliposimamisha gari, yule askari wa usalama barabarani
akatusalimu, na tukaona kuwa ameongozana na mtu mwingine aiyekuwa na mizigo. Na
tuliwaza kuwa alitaka kutuomba tumchukue,ingawa alikuwa hajatuambia.
Basi, yule askari baada ya kutusalimia, akatazama – tazama ndani ya gari
letu, halafu kama vile mtu aliyeona kitu akasema ‘Aaa” naona MMJAA – basi
unaweza kwenda.
Na mimi nikamjibu; “kweli TUMEJAA, ahsante sana”. Halafu nikawasha gari –
tukaondoka.
Tulipofika Morogoro tukaamua kumpumzika ili tupate chakula cha mchana.
Ndipo mwenzangu akaniuliza; “Hivi yule askari alipokuwa anasema tumejaa, aliona
watu wangapi kwenye gari wakati tulikuwa wawili tu?”
Ndipo na mimi niliposhituka, nikasema; “Lakini kweli, hata mimi sijui kwa
nini nilimjibu kuwa tumejaa wakati nilikuwa nafahamu kuwa gari lilikuwa bado na
nafasi ya watu watatu!”
Wote tukabaki tunashangaa! Lakini ni wazi kwamba Mungu aliyekuwa pamoja
nasi alijua hatari iliyokuwa mbele yetu kama tungemchukua yule mtu, Kwa hiyo
Mungu alimfungua macho ya kiroho yule askari, naye akawaona watu wamejaa kwenye
gari – lakini ukweli walikuwa ni malaika ambao Mungu aliwatuma watulinde njiani
– ingawa sisi tulikuwa hatuwaoni!
Soma Zaburi 91:1-12. Yote haya yanafanyika kwa sababu ya imani katika Damu
ya Yesu Kristo!
Ukitaka wewe na wote unaowahubiria neno kwenye mikutano ya hadhara au ndani
ya nyumba mlindwe na Damu ya Yesu Kristo – fanya hivi kabla ya kwenda
kuwahubiria;
1. Tubu kwa ajili yako mwenyewe,
halafu;
2. Tubu kwa ajili ya wote
utakaowahubiria ingawa wewe huwafahamu. Kumbuka Mungu anawafahamu.
Basi Mungu wetu tunayemwabudu katika Yesu Kristo atasikia na kuwasamehe.
Damu ya Yesu Kristo itakuwa pamoja nanyi KUWALINDA katika kusanyiko hili dhidi
ya mashambulizi na machafuzi ya Ibilisi.
Ndiyo maana imeandikwa kuwa; “Hao wakamshinda (shetani-mshitaki wao) kwa
DAMU YA MWANA-KONDOO na kwa neno la ushuhuda wao…..” (Ufunuo 12:11) Fahamu
hili ya kuwa PALIPO NA DAMU YA YESU KRISTO – shetani HAWEZI KUSTAHIMILI KUKAA.
Kwa hiyo HAKIKISHA kila wakati unaishi na kutembea katika TOBA YA KWELI ili
DAMU YA YESU IWE PAMOJA NAWE KILA MAHALI ULIPO NA UENDAKO.
SHUHUDA
Siku moja msichana mmoja aliyekuwa anahitaji msaada wa maombi- alinieleza
jinsi ambavyo usiku akilala anajikuta anafanya uasherati na watu asiowaona.
Kilichoshangaza ni kuona ya kuwa huyu msichana alikuwa ameokoka, lakini
aliendelea kupata shida hiyo ya kufanya uasherati usiku na watu asiowaona.
Nikamuuliza; “ Unataka nikusaidie kitu gani katika tatizo hili?”
Huyu msichana akajibu akasema; “nahitaji maombi na ushauri juu ya jambo la
kufanya ili shida hii iniondokee”
Nikamuuliza tena; “Je! unafahamu uwezo uliomo katika damu ya Yesu Kristo wa
kutulinda ili usipatwe na shida za namna hii?
Kabla hajajibu hilo swali, nilimwambia nitampa jarida linalo-zungumza juu
ya Damu ya Yesu Kristo (ambalo ndilo mwanzo wa mawazo ya kitabu hiki), na
kwamba alisome na kutafakari yaliyo ndani yake. Pia, nikamsisitizia ya kuwa
kabla ya kulala kila siku aombe damu ya Yesu Kristo imfunike na ulinzi wa
Mungu, ili nguvu za shetani zisimsumbue.
Yule msichana
aliondoka na akaenda akafanya kama nilivyomweleza; - baada ya wiki moja akarudi
tena na kuniambia ya kuwa baada ya kufanya kama
nilivyomweleza ile shida ya kufanya uasherati na watu asiowajua usiku au kwenye
ndoto ilikwisha na wala ilikuwa haijarudi tena.
Bwana wetu Yesu Kristo
asifiwe kwa maana fadhili zake ni za milele zilizomo katika Damu yake
iliyomwagika pale msalabani kwa ajili yetu.
Kwa hiyo wewe
unayesoma kitabu hiki nakushauri ya kuwa usisahau kuomba damu ya Yesu Kristo
ikufunike usiku unapolala na mchana pia.
Na kwa wale walio
na watoto, kumbuka kila siku kuomba ulinzi wa Damu ya Yesu juu yao – wakiwa nyumbani au
shuleni au po pote pale.
Kumbuka Biblia inasema; “Mwe na kiasi na kukesha kwa
kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba
angurumaye, huzunguka zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1Petro 5:8). Lakini
Biblia inatutia moyo na kutuangaliza juu ya uwezo wa damu ya Yesu Kristo
inaposema; “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo……” (Ufunuo wa
Yohana 12:11)
Usiogope vitisho
vya shetani ikiwa umejificha ndani ya Damu ya Yesu Kristo. Shetani hawezi
kupenya mahali palipo na Damu ya Yesu Kristo kwa maana anaiogopa sana .
SALA YA TOBA
Inawezekana kabisa
ya kuwa wewe unayesoma somo hili hujaokoka-hujampokea Yesu Kristo ndani ya moyo
wako kama Bwana na Mwokozi wako- na baada ya
kusoma somo hili umeona umuhimu wa Damu ya Yesu Kristo katika maisha yako.
Naamini Roho
Mtakatifu amekiweka kitabu hiki mikononi mwako kwa mpango maalum wa Mungu ili
ufike mahali pa kutubu na kuokoka. Inawezekana kabisa, pia ya kuwa hujawahi
kuambiwa juu ya umuhimu wa wewe kuokoka. Lakini napenda kukuambia ya kuwa ni
mpango wa Mungu uokoke. Soma Wakolosai 1:13,14 na Yohana 1:12-14 na 1 Timotheo
2:3-6 na Warumi 1:16,17 na Yohana 3:7. Ni vigumu kuona baraka za Damu ya Yesu
bila ya kuokoka.
Kwa hiyo kama unataka kuokoka-tafuta mahali palipo na utulivu, na
usome kwa sauti sala ifuatayo: (ukiweza unaweza kupiga magoti unapoomba sala
hii)
“Ee Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi.
Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu.
Ninatubu kweli. Naomba damu ya Yesu Kristo iliyomwagika msalabani kwa
ajili yangu initakase sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu.
Nimefungua moyo wangu. Bwana Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia
kwa uwezo wa Roho wako – uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote.
Ahsante kwa kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako nikutumikie
katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu yangu katika
jina la Yesu Kristo. Amina.
Ikiwa umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe
umeokoka na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na
alivyoandika katika neno lake. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.
Unapoanza maisha haya mapya katika Yesu Kristo nakushauri mambo yafuatayo:
1.
Zungumza na Mungu kwa maombi kila siku (Yohana 15:7)
2.
Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku (Matendo ya Mitume 17:11)
3.
Mruhusu Roho Mtakatifu akutawale (Wagalatia 5:16-25; Warumi 8:14-17)
4.
Umtumaini Mungu kwa kila jambo katika maisha yako (1Petro 5:7; Zekaria 4:6)
5.
Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu Kristo kuwa
Mwokozi wao kama wewe ili uimarike zaidi
(Waebrania 10:25)
Ukipenda unaweza
kuniandikia kwa anwani hii hapa chini juu ya uamuzi uliofikia leo wa kuokoka,
ili tumshukuru Mungu pamoja, na tuzidi kukuombea; na pia, tukutumie maandiko
mengine ya kukusaidia: KWA WALE WANAOTAKA KUJISOMEA
ZAIDI JUU YA DAMU YA YESU
Mungu aliwahi
kuwaangalia watu wake jinsi wanavyohangaika na kuangamia kiroho, na kwa
masikitiko makubwa alitamka maneno haya kwa kinywa cha nabii wake Hosea;
“Watu wangu
wanaangamizwa kwa kukosa maarifa….” (Hosea 4:6)
Hata hivi leo kuna
watu wengi sana
wa Mungu wanaangamizwa kiroho, siyo kwa sababu hawapendi kuishi maisha ya
ushindi kiroho, bali wanaangamizwa kwa kukosa maarifa!
Yesu Kristo aliwahi
kuwaambia wanafunzi wake maneno yafuatayo alipokuwa anajibu moja wapo ya
maswali waliyokuwa wanamuuliza mara kwa mara:
“…Mwapotea, kwa
kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29).
Hata hivi leo ukisikiliza na kufuatilia sababu kubwa zinazowafanya wakristo
wapotee kimafundisho, mojawapo ya sababu hizo ni kutoyajua maandiko
yanayozungumzia juu ya uweza wa Mungu katika Damu ya Yesu Kristo.
Hapa chini nimeorodhesha
sehemu chache ambazo katika Biblia zinazungumzia juu ya sehemu ya Damu ya Yesu
Kristo katika maisha yako ya kila siku.
Unaweza kuzisoma
sehemu zote hizi kwa siku moja, lakini nimezipanga kwa muda wa siku saba ili
mpango huu ukusaidie kusoma na kutafakari kwa undani juu ya Damu ya Yesu
Kristo:
Siku ya 1
Agano jipya na
Maisha mapya ( sehemu ya 1):
Yohana 6:53-56;
Mathayo 26:28; 1Wakorintho 11:17-34
Siku ya 2
Agano Jipya na
Maisha mapya ( Sehemu ya 2):
Waebrania 8:1-13;
Waebrania 9:1-28; Waebrania 10:1-25
Siku ya 3
Ushindi dhidi ya
dhambi (sehemu ya 1):
1Yohana 1:9; 1Petro
2:24; Wakolosai 1:13,14; Ufunuo wa Yohana 1:4-6
Siku ya 4
Ushindi dhidi ya
dhambi (sehemu ya 2):
Wakolosai 2:13-15;
Waebrania 10:17; Isaya 43:25
Siku ya 5
Ulinzi na nguvu za
Mungu katika Damu ya Yesu:
Ufunuo wa Yohana
12:11; 1 Wakorintho 1:18; Kutoka 12:21-24
Siku ya 6
Upatanisho katika Damu ya Yesu:
Waefeso 2:12-17; 2Wakorintho 5:17-20
Siku ya 7
Ujasiri katika maombi:
Waebrania 10:19; Waebrania 4:14-16
Pamoja na vifungu hivi nilivyokuwekea hapa, Biblia ina vifungu vingine
zaidi ambavyo kwa pamoja ukivitafakari mara kwa mara – Roho Mtakatifu atakutia
nuru katika macho yako ya ndani ili sehemu ya Damu ya Yesu Kristo katika maisha
yako ionekane kwa wazi kwako kuliko ilivyo sasa.
5 comments:
Amina!
Mungu azidi kuwabariki katika huduma hii ya mafunzo ya mtandaoni, inanisaidia sana hata mimi ninaekuwa sikuhudhuria aidha ni kwenye makongamano au mikutano ili kupata mafunzo hayo.
Nabarikiwa mnooo!
mungu aikumbuke sadaka yenu
Mungu awabariki sana na kuwatia nguvu katika huduma hii aliyowapatia.
Amina nimebakiwa Sana, Mungu azidi kumwinua Mtumishi wake katika huduma aliyo weka ndani yake.
Nimelisoma andiko hili kwa wakati sahihi,la zaidi ni juu ya uwezo wa Damu ya Yesu katika maisha yetu ya kila siku .
Post a Comment