TUNDA LA
UAMINIFU
Uaminifu ni mojawapo ya tunda la Roho katika
maandiko matakatifu. Tutajifunza uaminifu wa Mungu unaopatikana katika neno
lake. Yeye amesema atatimiza yale aliyoahidi katika neno lake, si tu kwa wana
wa Israel bali kwa watu wote wanaoishi sawasawa na neno lake. Kwa
hiyo, kwa upande wetu inatupasa sisi nasi kuwa waaminifu kwa kuliishi na
kulitenda neno la Mungu. “Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye
Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na
kushika amri zake, hata vizazi elfu. Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiza
hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimizia
agano na rehema aliyowaapia baba zako.” Kum 7:9, 12. “Ndivyo
litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa
changu halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo
litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.” Isa 55:11.
Tabia Ya Mtu
Mwaminifu.
1. Mtu aliye mwaminifu ni yule ambaye
anatenda sawasawa na maagizo, sheria na taratibu . Ikiwa ni mtu aliyeajiriwa
katika kazi za nyumbani au ya serikali anafanya kazi ipasavyo, si mwizi, mpokea
rushwa, mdhulumaji na wala si mwenye hila. Unaweza kuona ilivyoandikwa kuhusu
mtumishi aliyeajiriwa kazi za nyumbani ambaye alipaswa kufanya kwa
uaminifu. “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake
alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa
yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.” Mt 24:45-46.
2. Hatendi dhambi.Yusufu mtumishi wa Potifa
kwa kuwa alikuwa mwaminifu aliposhawishiwa na mke wa Potifa ili kufanya naye
dhambi ya uzinzi alikataa. “....mke wa bwana wake akamtamani Yusufu,
akamwambia, lala nami. Lakini alikataa akamwambia....Nifanyeje ubaya huu mkubwa
nikamkose Mungu?” Mwa 39:7-9.
3. Hachukui kitu cha mtu mwingine,
iwe ni fedha, mali, au kitu kingine chochote ambacho si halali
yake. Akitoa fedha kwa ajili ya malipo yoyote na akarudishiwa pesa ya
ziada hurudisha kiasi kilichozidi. Ikiwa amemwona
mtu ambaye amedondosha fedha au amepoteza kitu chochote
humrudishia. Kwa kufanya hivyo analitii na kulitenda neno la Mungu linavyosema,
“Umwonapo
ng’ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea....sharti umrudishe kwa nduguyo. Na
kwamba yule nduguyo hayuko karibu nawe, na ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani
kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie....tena fanya vivyo
kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo,....” Kum 22:1-3.
Umuhimu Wa
Kuwa Mwaminifu.
Mkristo ambaye ameokoka akiwa ni
mwaminifu, Mungu anamwamini na kumweka katika kazi ya
utumishi. Tunaweza kujifunza kwa baadhi ya watu ambao Mungu aliwaona
ni waaminifu na kuwachagua na kuwafanya kuwa watumishi wa kazi yake,
mfano wa Yesu, Musa na Paulo “....Yesu
aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika
nyumba yote ya Mungu. Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya
Mungu kama mtumishi....” Ebr 3:1,5. Mtume Paulo alikuwa ni
mwaminifu ndio maana ameandika akisema, “Namshukuru Kristo
Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka
katika utumishi wake.” 1Tim 1:12.
Yampasayo
Mtu Ili Aweze Kudumu Katika Uaminifu.
Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani
kwa sababu alikuwa ni mwaminifu kila alipojaribiwa na alizitambua hila za
shetani wala hakufanya kosa lolote. Ndio maana ulipokaribia wakati wa kukamatwa
aliwaambia wanafunzi wake akisema, “....yuaja mkuu wa ulimwengu huu hana
kitu kwangu.” Yn 14:30.
Kwa mkristo ambaye ameokoka, amejazwa Roho
mtakatifu na kudumu katika uaminifu, Roho mtakatifu humfunulia hila zote za
Shetani anapojaribiwa. Waliosimama imara katika neno la Mungu Shetani huja na
kuwajaribu katika shida na dhiki. Usikubali mawazo ya shetani, bali mpinge na
kumkemea, kwa kumwambia, nenda zako Shetani. “Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda
zako, Shetani,....Kisha Ibilisi akamwacha....” Mt 4:10-11. “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia, Mkaribieni Mungu
naye atawakaribia ninyi....” Yak 4:7-8. Kutokana na andiko
hili mtu anaweza kuwa karibu na Mungu na kumkemea Shetani naye
huondoka, ikiwa analitii neno na kuishi linavyosema.
Wale wote waliozaliwa mara ya pili imewapasa
kuushinda ulimwengu na dhiki kwa sababu aliye ndani yao ni mkuu kuliko shetani,
naye Yesu alimshinda na kushuhudia akisema, “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini
jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Kwa upande
mwingine, tunapolifahamu neno la Mungu tunazitambua hila za shetani na
kumshinda. “Nao wakamshinda kwa damu ya mwana-kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao,
ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Ufu 12:11. “....Uwe
mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima....Yeye ashindaye hatapatikana
na madhara ya mauti ya pili (Jehanum).” Ufu 2:11-11.
Kinachotokea
Kwa Mtu Anayedumu Katika Uaminifu.
1. Mungu humbariki na uzao wake. “Mtu
mwaminifu atakuwa na Baraka tele” Mit 28:20.
“Mwenye haki aendaye katika
unyofu (uaminifu) wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake.” Mit
20:7.
2. Mungu anakuwa karibu naye wakati
anapomwita au kumwomba. “Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu.” Zab 145:18.
3. Anampendeza Mungu. “Walio
wakamilifu katika njia zao humpendeza.” Mit 11:20.
Ninayo
furaha kwa ajili yako wewe kujifunza neno la Mungu, endelea kubarikiwa.
Mawasiliano: Emailtarimoisrael2012@gmail.com Simu
0754592830.
No comments:
Post a Comment