- HATUA NA VIPENGELE MUHIMU
KATIKA KUOMBA -
MKARIBISHE
ROHO MTAKATIFU. *Rum 8:26-27 *Yoh 14:16-17
Yesu alisema Roho
Mtakatifu ni msaidizi wetu. Atatusaidia na kutufundisha yote, kwa maana pasipo
yeye, sisi hatuwezi neno lolote. Na sisi peke yetu hatujui kuomba ipasavyo,
bali yeye (Roho) ajua kutuombea kwa Mungu kama vile Mungu apendavyo. Hivyo
kabla ya kuanza maombi au kusoma neno au ibada au safari au mitihani au kikao
n.k. jifunze kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, uombe msaada wake, akupe
ufanisi/ubora katika yote yakupasayo kufanya.
Tambua Utu wake, Uungu na
Uweza wake.
Jikabidhi katika Nguvu ya
Uongozi wake.
Tii kila Uongozi
anaokupa.
FANYA
TOBA NA UTAKASO. *Isa 59:1-2, Yoh 9:31, 1Yoh 1:8-9,7
Sikio la Bwana si zito
kusikia wala mkono wake si mfupi kushindwa kututendea mambo tumwombayo, bali
maovu yetu ndiyo yanatufarakanisha na Mungu wetu. Mungu hawasikii wenye dhambi.
Hivyo chukua muda wa kutafakari na kuungama dhambi zako mbele za Mungu na
kuzitubu kwa kumaanisha kuziacha. Mungu ni mwaminifu kutusamehe na kututakasa
na uchafu wote. (Isa 1:18). Lakini, kabla hujafanya toba yako binfsi;
(i)
- Kwanza, samehe wote
waliokukosea,
hata kama hawajaja kukuomba msamaha.Usipowasamehe waliokukosea, na Mungu
hataweza kukusamehe wewe. (Math 6:12,14-15)
(ii)
- Ndipo nawe ufanye toba
yako binafsi.
Na Mungu atakusamehe kabisa. Hata kama ni nyekundu
sana, zitakuwa nyeupe sana. (Isa 1:18, Isa 43:25)
3. MSIFU,
MUABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Zab 147 na Zab 148
Msifu Bwana kwa Matendo
yake makuu, mwabudu Bwana kwa uzuri wake na kwa sifa zake. Mwadhimishe Mungu
kwa Tabia zake, wema wake, fadhili zake na baraka zake mbalimbali
anazotutendea. Sifa yako ikifika vizuri mbele za Mungu, ndipo atakuwa tayari
kukupa haja za moyo wako. Haja zetu zimefichwa nyuma ya mgomgo wa sifa. Ndio
maana Neno linasema;
‘Nawe
utajifurahisha kwa Bwana (kwa kumsifu, kumwabudu na kumshukuru), naye atakupa
haja za moyo wako’ (Zab37:4).
Yesu anatuonyesha mfano;
angalia sentensi yake ya kwanza katika kuomba kwake imekuwa “Baba
yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.” (Math 6:9). Anaanza
maombi kwa kumsifu Mungu. Msifu Mungu kwa kuimba na kwa kunena/kusema/kuelezea.
Mungu anataka kusifiwa na kutukuzwa. Ukifanya sifa nzuri, ya kuufurahisha moyo
wake, atakupa hata na vile ambavyo hukutegemea/hukuomba.
4. MWELEZE
MUNGU MAHITAJI NA HOJA ZAKO. *Wafilipi 4:6-7,19 Isa 43:26
Mweleze Mungu zile hoja
zilizokusukumwa kwenda kumwomba. Nenda mbele za Mungu kama ‘kuhani’ (1Pet 2:9).
Kwa
unyenyekevu na heshima. Lakini kabla ya kumweleza mahitaji yako binafsi;
(i) Kwanza
fanya ‘maombezi’ – ombea watu wengine; (1Tim 2:1-4)
Viongozi mbalimbali na
wenye mamlaka, watumishi wa Mungu, marafiki zako, wenye shida, ndugu zako, nchi
yako, shule yako, shirika lenu, ofisi yenu, chama chenu, n.k. Usianze kujiombea
mwenyewe tuu, zoea kuwatanguliza wengine.
(ii) Kisha
fanya ‘maombi yako’– ombea haja za moyo wako. (Math 7:7-11)
Mweleze Mungu haja zako.
Ongea na Mungu kwa uwazi na ukweli. Japo anazijua haja zetu, lakini ameagiza
kuwa tumwombe ndipo atafanya. ‘aombaye hupokea’ yaani; asiyeomba, hapati.
Mungu anasema tumpelekee hoja zenye nguvu (Isa 41:21). Omba vitu vizuri na
mambo makubwa ili upewe (pray for good things and big things)
5. FANYA
MAOMBI YA VITA VYA ROHONI. *Efe 6:10-13 *2Kor 10:3-5
Baada ya kumwendea Mungu
na kumweleza mahitaji yako, sasa simama kama ‘mfalme’, kwasababu wewe ni
‘mfalme’ (Ufu 5:8), tumia mamlaka yako ya kifalme, ongea na hali/hitaji
ulilokuwa unaliombea, na kwa mamlaka, amuru iwe kama vile
ulivyoomba/unavyotamani. Ndio maana Bwana Yesu alipokabidhiwa mamlaka yote na
Mungu, naye akatukabidhi sisi (kanisa lake) “Tazama,
nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Wala hakuna
kitakachowadhuru” (Luk 10:19, Yer 1:10, Yak 4:7). Tuma neno lenye mamlaka
katika hali/jambo ulilokuwa unaliombea, Amuru iwe vile ulivyokuwa unamwomba
Mungu iwe. Kemea kila roho ya shetani inayoweza kuwa inasababisha tatizo katika
swala lako.
6. OMBEA
ULINZI JUU YA ULIYOYAOMBEA. *Math 6:13a
Baada ya kupiga vita vya
kiroho, weka ulinzi katika yale uliyoyaombea, ili shetani na mapepo yake
wasiweze kuirudia hali/jambo/mtu yule uliyemkomboa kwa maombi ya vita. Yesu
alisema shetani akifukuzwa mahali, haendi mbali, anasubiri kuona kama atapata
upenyo wa kuparudia mahali pale alipokuwa kwanza. (Math 12:43-45). Kwahiyo,
usipoweka ulinzi, kuna uwezekano wa adui kurudi na kuliharibu zaidi lile jambo
uliloliombea na kulipata.
Kumbuka, unapoomba
vizuri, unapokea papo hapo (katika ulimwengu wa roho), lakini udhihirisho wake
katika ulimwengu wa mwili, unaweza kuchukua muda fulani. Hivyo katika muda huo
wa kusubiri, shetani anaweza akapita na kuzuia au kuharibu kile unachokisubiri
kidhihirike katika ulimwengu wa mwili. Ndio maana Yesu alitufundisha kuombea
ulinzi, “tuokoe na yule mwovu” (Math 6:13a). Weka ulinzi juu ya mambo
yako yote. Jengea wigo wa moto wa mbinguni (2Fal 6:16-17), Yafunike kwa damu ya
Yesu na agiza malaika walinzi walinde mambo yako masaa yote. Omba hivyo kila
siku. (Zab 34:7, Zab 91:9-11, Ebr 1:13-14)
MSIFU,
MWABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Math 6:13b
Yesu alianza maombi kwa
kumsifu Mungu na kumtukuza. Na akamaliza maombi yake kwa kumtukuza Mungu tena.
Akasema “kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu ni zako,
sasa na hata milele” akamaliza. Kwahiyo nawe kwa kumaliza
maombi yako, msifu na kumshukuru Mungu tena, kwa ukuu wake, uaminifu wake, na ahadi
zake juu yetu. Ndipo
ufunge maombi yako.
MUHIMU:
TUMIA MAANDIKO KATIKA KUOMBA *Kol 3:16
-Katika kuomba kwako,
mara zote tumia maandiko kumkumbusha Mungu ahadi zake .(Isa 43:26). Mungu
analiangalia neno lake ili alitimize. Sababu pekee itakayomfanya Mungu akupe
alichoomba, ni ili kulitimiza neno lake. Hivyo, baada ya kumweleza unachohitaji
(kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu unayemwombea) mpe Mungu andiko/neno lake
linalokupa wewe uhalali wa kuomba hicho kitu mbele zake na kupewa.
-Hata unapompinga na kumkemea
shetani, baada ya kutoa amri yako dhidi yake, shetani atasubiri kusikia
andiko/neno linalomnyima yeye uhalali wa kushika alichoshika. Ndio maana Yesu
alimshinda shetani kwa neno la Mungu. Alisema “imeandikwa” na shetani
akashindwa. “Nao wakmshinda (shetani) kwa damu ya Yesu
na kwa Neno” (Ufu 12:11)
MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI KWA MUDA
MREFU
1.
CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU. *Mk 1:35
ili uweze kuomba kwa
utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri patakapokupa utulivu
katika kuomba (concentration in prayer). Ndio maana Mungu alipenda kuongea na
Musa juu ya mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda kuombea mlimani,
mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani. (Math
14:22-23). Tafuta mahali patulivu; chumbani, kanisani, mlimani (Math 6:5-6)
2.
CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7 Ili uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua
muda mzuri ambao akili yako ma mwili wako viko fresh. Usilazimishe kuomba hata
kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama
umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali wa kupumzika. Usilazimishe ratiba.
ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri baadaye. Usije ukajikuta
unamkemea Yesu badala shetani. Penda kuomba wakati una nguvu ya akili na mwili,
ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana Yesu alipenda
kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. (Mk 1:35, Luka 4:42)
3.
OMBA KATIKA ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe 6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine nzuri ya
kuomba kwa muda mrefu na kwa ufanisi, ni kuomba kwa Roho; yaani kuomba kwa
kunena kwa lugha. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, Mungu anasikia pia,
lakini maombi yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu akili ya mtu haijui
kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba
kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Mk 16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)
4.
OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE. *Math 6:16-18
Kufunga kula kunasaidia
kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi.
Mwili huu siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili ukiwa umeshiba,
unakuwa na uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu mojawapo ya
kuudhibiti, ni kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili ukidhoofika
kiasi, roho yako inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab 35:13). Mashujaa wote
wa imani walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu anasema ‘mfungapo’ akimaanisha
ratiba ya kufunga, ipo. Inasaidia.
5.
OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER). *Mhu 4:9-10
Neno la Mungu linasema,
ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki yako.
Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba zaidi. Si
rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho
inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja, bali
wakiwa wawili, wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi! Shangaa! (Kumb
32:20) Hiyo ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka,
nguvu ya Mungu huongezeka.
Kwahiyo, wakati mwingine,
omba na rafiki yako, unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako ya
binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki wa kiroho. (Prayer
Partners). Kwa Mfano:- Math 17:1-9
Musa - alikuwa na Joshua,
Haruni na Huri
Eliya - alikuwa na Elisha
Daniel - alikuwa na
Shadrack, Meshack na Abednego.
Yesu - alikuwa na Petro,
Yakobo na Yohana.
Paul - alikuwa na
Barnaba, Timotheo na Tito.
Wewe Je? Uko na nani
katika urafiki wa kiroho?
Kama huna rafiki wa
karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichagulia. Tulia umwombe Mungu akupe mtu
atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata
kama mmetengana kijiografia, lakini katika roho, mko na umoja mzuri wa imani. (Math 18:18-19)
6.
OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU NA NGUVU ZAIDI.
Katika kuomba kwa muda
mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu. Yakupasa kujua nguvu
yako na udhaifu wako (strong point and weak point). Wakati wa kuomba, epuka
mikao inayokuchosha haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi. Kwa Mfano:-
Ukiwa umechoka, usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea kitandani. Ni
bora uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka usingizi na uchovu.
Waombaji hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi marefu. Wengine
hawana mikao maalum, bali wakiwa katika maombi, huwa wanabadilisha-badilisha mikao
ili wasichoke. Hiyo ni mbinu nzuri pia.
Mifano ya Mashujaa wa
imani;
Ibrahim – aliomba kwa
kusimama (Mwa 18:22)
Daniel - aliomba kwa
kupiga magoti (Dan 6:10)
Paul - aliomba kwa kupiga
magoti (Efe 3:14)
Yesu - aliomba kwa kulala
chini (Math 26:38-39)
Eliya - aliomba kwa kukaa
chini na
kuweka kichwa kati ya
miguu (1Fal 18:42)
Mimi - huwa napenda
kuomba kwa kutembea tembea
Naweza kumaliza kilomita
nyingi chumbani kwangu. Nikitembea huku nikiomba.
Wewe Je? Unaujua mkao wa
nguvu? Kama
hujui, Tafuta kujua.
OMBA
NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa kiroho, na
wataratibu, unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda
mrefu. Muziki wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee. Neno
linasema, waimbaji na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama
mtu mmoja, utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani
hawakuweza tena kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila
malaika wa sifa, ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga kinubi
alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokija juu yake,
naye akatabiri.
Najaribu kukuonyesha, kuna connection kati ya muziki wa kiroho na utukufu
wa Mungu. Kwahiyo, ukiweza kuomba huku umeweka kanda au CD ya nyimbo za kiroho za
taratibu, utapata (experience) hamasa ya kiroho (motivation) na utasikia una
nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama unaweza, tengeneza kanda au CD maalum
yenye nyimbo nzuri unazozipenda wewe, ili uwe unaipiga wakati wa maombi.
Utajikuta unaweza kuomba kwa muda mrefu na kwa bubujiko zuri zaidi
Mwl.
Mgisa Mtebe,Bsc Economics
Mzumbe
University,+255 713 497 654
mgisamtebe@yahoo.com
No comments:
Post a Comment