Sunday, June 12, 2016

SEMINA YA MANA - MOROGORO Na Mwl. Chritopher Mwakasege (08-12/06/2016) SOMO:KUA KATIKA NEEMA ILI UNUFAIKE NA MSALABA

SIKU YA TATU (10/06/2016)
Somo linaongozwa na Neno kutoka:- 2Petro 3:18 “Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.” 2Timoth 2:1 “Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu.”
Kumbuka kuwa NEEMA ni jambo unalopewa bila ya kulifanyia kazi (Warumi 4:4-6 “4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. 5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. 6 Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,” )
Kama unataka kuipokea hii NEEMA mpokee Yesu ndani yako (Yohana 1:14, 16 “14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. 16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.”)
Inaendelea………………..Mungu anavyotumia Damu ya Yesu kukurudishia na kukupa haki zako ulizonyimwa/zilizopotea
Warumi 4:25, 3:22-28 “25 ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki. 22 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; 23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; 25 ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa. 26 apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu. 27 Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani. 28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.”
Kinachotufanya tuhesabiwe haki ni kwaajili ya imani tuliyonayo katika damu ya Yesu, (Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Waebrani 11:1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”)
Ile kwambauna imani kwa Yesu haina maana kuwa unayo imani kwa damu yake, unaweza kumwamini Yesu lakini usiamini katika damu yake, au ukaamini nusu nusu katika damu yake au ukaamini nusu katika Neno lake.
Kuna mambo kadha wa kadha ya kuangalia jinsi Mungu anavyoitumia damu ya Yesu kutufanya tukubalike kwake
a.      Mungu anaangalia na kusikiliza damu ya Yesu inasema nini juu ya dhambi zako
Walawi 17:11 “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.”
Kwa sheria za kimbingu ili utake kupatana na Mungu lazima kuwe na damu itakayonena kwa niaba yako (niaba ya nafsi yako) mbele za Mungu, hivyo ni damu pekee yenye kuweza kukupatanisha na Mungu kwa sheria aliyojiwekea katika ulimwengu wa roho. Hii ni kwasababu damu inabeba uhai lakini pia damu inaongea/ina nena (Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”)
Waebrani 9:22-24 “22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. 23 Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo. 24 Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu;” Mungu haangalii mtu anaangalia damu inasema nini, Yesu hakuingia patakatifu mwenyewe aliingia kwa damu yake aliyoimwaga
1Yohana 5:8-9 “8 Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. 9 Kisha wako watatu washuhudiao duniani, Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.” Kwa lugha nyingine kuna mashahidi Mbinguni na duniani, damu haipo mbinguni ilimwagika duniani ili upatane nayo ukiisha kupatana nayo ROHO anabeba ushuhuda na kuupeleka Mbinguni
b.     Anasamehe dhambi akishasikia damu inataja jina lako
Mungu anaisikiliza damu inayonena mema (Damu ya Yesu) ili ikutetee na ndio maana ya toba, Warumi 4:4-8 “4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. 5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. 6 Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, 7 Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. 8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.” (Msisitizo upo katika mstari wa 7a)
Baraka zinaachiliwa kwa waliosamehewa dhambi ndipo wanapewa haki zao, Wakolosai 1:13-14 “13 Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; 14 ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”
Ukombozi maana yake ni kufunguliwa kutoka kwenye adhabu uliyopewa na ukashindwa kuilipa wewe ile adhabu (ukashindwa kulipa malipo stahiki ya adhabu ile), na baada ya wewe kushindwa akatokea mtu mwingine na kukulipia malipo stahiki kwa adhabu uliyoistahili wewe, na hivyo ndivyo Yesu alivyofanya kwa kutulipia malipo stahiki ya adhabu ya mauti kutokana na dhambi zetu. Neno la Mungu linasema mshahara wa dhambi ni mauti (na hii ni sheria ya Mbinguni), na hivyo imekuwa ni sheria katika ulimwengu wa roho, sasa Mungu anadai na shetani anadai mauti (kwakuwa mauti ndio malipo stahiki) ili kukumbolewa na dhambi. Ukikombolewa, damu inaenda na jina lako kwa Mungu kwamba umekombolewa tayari na umeachwa huru na adhabu ya mauti.
Ndani ya msamaha wa dhambi kuna ukombozi, Luka 5:17-26 “………….. 18 Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. 19 Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. 20 Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako……………….. 24 Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. 25 Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza Mungu……………..”
Kwakuwa ndani ya msamaha wa dhambi kuna ukombozi, Yesu alimwambia “Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako” na mara ile akapona ugonjwa wa kupooza. Ni muhimu kushughulika na dhambi ilikufunga, amini katika damu ya Yesu. Mungu anaangalia damu ya Yesu inasema nini, ikisema msamehe tu huyo anafunguliwa.
c.      Anasitiri dhambi
Warumi 4:7 “Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao
Isaya 43:25, 44:22 “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.”
Ukisitiri kitu maana yake hujakiondoa, yaani kipo ila kimefunikwa kwa muda fulani tu.
Zaburi 19:12-14 “12 Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri. 13 Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. 14 Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.” Zaburi 90:8 “Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako.”
Dhambi inapokuwa siri ni siri kwa wanadamu lakini sio siri kwa Mungu maana anaiona na kuisitiri, anaifunika kwa muda huku akitafuta namna ya kuufikia moyo wako uachane na dhambi, muda huu wa kuisitiri dhambi yako Mungu anakunyanyulia watu wa kukuombea (waombaji) watakaobeba kwa mzigo shida yako.
Zakaria 3:1-10 “1 Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. 2 Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? 3 Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. 4 Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi………………”
Matendo ya mtu kujihesabia haki mbele za Mungu ni mavazi machafu, damu ilisimama kumsitiri Yoshua mpaka hapoYoshua alipoondolewa dhambi yake. Kumbuka kusitiriwa dhambi ni kwa muda tu.
Kumbuka habari ya Yesu na Yule mwanamke aliyezini katika Biblia, Yohana 8:3-11 “3 Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. 4 Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. 5 Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? 6 Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. 7 Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. 8 Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. 9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. 10 Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? 11 Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”
Waandishi na Mafarisayo hawakujua kwamba zao zilikuwa zimesitiriwa kwaajili ya nafasi zao ili wapate muda wa kutengeneza na BWANA, na ndio maana walipomleta Yule mwanamke dhambi zao zikafunuliwa ndani yao na hakuna hata mmoja wao aliyebaki pale.

Usiwe kama Waandishi na Mafarisayo, Roho Mtakatifu akikushudia dhambi yako unayofanya kwa siri rudi kwa Yesu usikimbie mbali na Yesu.

No comments: