Friday, August 12, 2016

KONGAMANO LA MAOMBI YA KITAIFA 2016 KUOMBEA NCHI YA TANZANIA MAHALI:CHUO KIKUU CHA DODOMA (2ND – 6TH August, 2016) Mwl. Chistopher & Diana Mwakasege Imeandikwa na Samson Mollel (www.uzimawamileleministries.com)

SIKU YA KWANZA

HASARA INAYOWEZA KUTOKEA MUNGU ANAPOKOSA KUMPATA MTU WA KUOMBEA NCHI KWA JINSI MUNGU ANAVYOTAKA IOMBEWE

Ezekiel 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”

Kwanini Mungu atafute mtu wakati Biblia inatuambia kuwa Mungu anaona kila mahali?

Zaburi 139:7-12 “7 Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. 9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. 11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; 12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”

Kama Mungu anaona kila kitu kila mahali na anasema akatafuta mtu lakini hakuona mtu; basi itakuwa ni zaidi ya kutafuta ya kawaida tunayoifahamu, yaani katika maneno kutafuta yapo mambo (kuna kitu) yamejificha ndani yake. Utaona katika Biblia Mungu anaongea habari ya kutafuta waliopotea, kutafuta watendakazi (mtu anweza kuwa mtumishi wa Mungu lakini sio mtenda kazi, Mungu kupata watumishi sio jambo gumu ila kupata watenda kazi sio jambo rahisi)

Wanaoombea nchi wengi wanaombea nchi bila kujua nafasi zao katika hayo maombi ili Mungu naye afanye nafasi yake.

Mwanzo 3:9 “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?”

Mungu anamuita Adamu na kumuuliza yuko wapi wakati alikuwa anazungumza naye. Kitu cha kwanza kilichoharibika dhambi ilipoingia ni nafasi ya mtu aliyopewa na Mungu

Ø  Utaratibu wa ki-Mungu ni kwamba, Mungu anakupa nafasi kisha anatengeneza mahusiano

Ø  Ukitaka Mungu akupe unachokiomba tafuta kwanza nafasi ndipo utengeneze mahusiano, watu wengi wanaomba bila kujali nafasi

Kabla dhambi haijaingia hapakuwa na maombi kulikuwa na ushirika (fellowship). Ukitaka kumualika Mungu katika nafasi fulani lazima ujue mamlaka ya nafasi hiyo

Dhambi sio kwamba ilitutoa kwenye nafasi tu, lakini pia ilituharibu kiasi kwamba ukitaka kurudi kwenye nafasi lazima utengeneze kwanza

Daniel 17:17-21 “17 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. 18 Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza. 19 Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. 20 Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake. 21 Tena, Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.”

Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria walipewa maarifa ya kila namna na Mungu. Ni kwanini Ashpenazi (Mkuu wa matowashi) alichukua vijana wengi wakati mfalme alikuwa anahitaji watu wanne tu? Nikama kujiuliza ni kwanini serikali isomeshe wanafunzi wengi chuo kikuu wakati inahitaji wachache tu kuwaajiri katika fani wanazowasomesha

Ezekiel 22:30-31 “30 Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. 31 Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.”

Unapotaka kutengeneza chombo Fulani lazima umpate fundi sahihi wa kutengeneza chombo hicho.  Mfano huwezi kumchukua fundi wa gari atengeneze ndege, ndege inapoharibika inabidi utafute fundi wa ndege aitengeneze. Au mtu anapoumwa anahitaji daktari sahihi na vifaa sahihi ndio maana mtu anaweza kuumwa akapelekwa India kuwafuata wataalam sahihi.
Kwa kusema hayo inamaana ya kwamba Mungu anatafuta waombaji, sio tu waombe kwaajili ya uharibifu uliotokea lakini kutengeneza mahali palipoharibika (Kwamfano ni kazi ya daktari kushona mguu wako ukipata ajali, lakini ni kazi ya polisi aliyesababisha ajali)
Kipimo kwamba boma limetengenezwa ni kuona limekamilika (Mfano kama ulipeleka gari kwa fundi kwasababu ya ubovu Fulani, lishishatengenezwa utaangalia kama lile tatizo limeisha)

Zaburi 106: 26, 23 “26 Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, 23 Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.”

Musa alisimama mahali palipobomoka na kulitengeza boma, na kuiepusha hasira ya Mungu juu ya wana wa Israeli (Kutoka 32)

Mwanzo 18:17-33 “17 Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo,…….. 20 Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, 21 basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. …………. 23 Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? 24 Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? .....................26 Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao……………. 28 Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. 29 Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. 30 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. 31 Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. 32 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. 33 Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake”

Ibrahimu alishindwa kusimama mahali palipobomoka na hivyo mji ule na watu wake ukaangamizwa.

Mungu hawezi kuwapita wakina Musa na Ibrahimu bila kuwaambia anachotaka kufanya. (Yeremia 5:1 “Pigeni mbio huku na huku katika njia za Yerusalemu, mkaone sasa, na kujua, na kutafuta katika viwanja vyake, kwamba mwaweza kumpata mtu mmoja, kwamba yuko mtu mmoja awaye yote atendaye kwa haki, atafutaye uaminifu; nami nitausamehe mji huo.”)

Isaya 62:6-7 “6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya; 7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.”

Je? Ni mlinzi wa namna gani? Ni mwombaji aliye mlinzi ambaye yupo tayari kubeba mzigo wa Mungu aliowekewa kwaajili ya Mji au Nchi, kwasababu BWANA mwenyewe ameahidi tusikae kimya (Isaya 58:2 “Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu.”).

  •         Huwezi kuwa mlinzi juu ya mji kama hauna mzigo wa kuuombea mji huo
  • ü    Lazima ujue maono/sababu ya Mungu kuufanya mji huo
  • ü  Usiende mbele za Mungu kwa kulalamika kwani Mungu atajibu malalamiko yako na sio sababu za kulalamika kwako (Habakuki 1 & 2)
  • ü  Tangu anguko la mwanadamu ni sheria katika ulimwengu wa roho kumkumbusha Mungu
  • ü  Unapotaka kuombea taifa/nchi lazima ujue maono (vision) ya eneo unalotaka kuliombea

Nchi/ardhi ikipata shida kunakuwa na shida ya mvua/Ukame, tauni (magonjwa).

MAOMBI YA KUOMBEA NCHI YA TANZANIA
2Nyakati 7:13-15 “13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; 14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”



No comments: