Mungu tunaye mwabudu ni
mmoja katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu
na hao wote ni umoja kwani hizo nafsi tatu ni nafasi za utendaji. Kwa mfano
wewe unaweza kuwa ni mtoto kwa wazazi wako (wanakuita mtoto) halafu unaweza
kuwa mume/mke wa mtu Fulani (unaitwa mume/mke) na unaweza kuwa mzazi wa
watoto/mtoto (Unaitwa baba au mama), katika nafasi zote kila moja inayo
majukumu yake ambayo huenda hayaingiliani kabisa lakini mtu ni mmoja. Hauwezi
kuyafanya majukumu ya mume/mke wako kwa watoto au wazazi wako na viyohivyo
hauwezi kuyafanya majukumu yako kwa wazazi kuwa ya watoto wako. Hivyo ndivyo
ilivyo kwamba Mungu wetu ni mmoja katika nafasi (tofauti ya majukumu) anazo
nafsi tatu.
Roho mtakatifu ni nafsi
(person) kamili ya Mungu katika nafsi tatu za Mungu. Roho Mtakatifu ni nafsi
tendaji (executive person) ya mambo yote ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Utendaji wa Mungu katika
maisha ya mwandamu ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu, ishara, miujiza, uponyaji na
kila namna ya kufunguliwa hufanywa na Roho Mtakatifu. Mawasiliano
(Communication) yote ya mtu aliyeokoka na ulimwengu wa roho yanawezeshwa na
Roho Mtakatifu.
NI
AHADI YA MUNGU KUTUPA ROHO WAKE
Yesu alijua vyema kwamba
sisi peke yetu hatuwezi kufanya jambo lolote ndio maana akaahidi kwamba ijapokuwa
anaondoka atamtuma Roho Mtakatifu ambaye atatupasha habari na mambo yote hata
yale ambayo Yesu haukuweza kutueleza
Yohana
16:12-13 “12 Hata bado
nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. 13
Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli
yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia
atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. 14 Yeye atanitukuza mimi,
kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. 15 Na yote aliyo nayo
Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na
kuwapasheni habari.”
ROHO
MTAKATIFU NDANI NA JUU YA MTU
Utendaji wa kazi wa Roho
Mtakatifu unatofautiana kulinga na nafasi aliyoichukuwa kwa wakati huo au
mahali alipokaa kwa wakati huo. Roho Mtakatifu akiwa ndani ya Mtu utendaji wake
ni tofauti na akiwa juu ya mtu huyo huyo.
ROHO
MTAKATIFU NDANI YA MTU
Roho Mtakatifu anaweza
kukaa ndani ya mtu, mtu yeyote aliyeokoka anaye Roho Mtakatifu kama yanenavyo
maandiko.
1Kor
6:19
“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu
la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu
wenyewe;”
1Kor
3:16
“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la
Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”
Kazi
za Roho Mtakatifu akiwa ndani ya Mtu
v Ili tuweze kumpendeza Mungu
Roho Mtakatifu anapokuja
ndani yako ni ili uweze kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi ambazo chanzo
chake ni mwili kuvutwa na mambo ya dunia. Roho Mtakatifu anatusaidia kuishi
maisha ya utakatifu kwakuwa yeye (Roho Mtakatifu) ni mtakatifu kama alivyo
Mungu.
Warumi
8:8-9 “8 Wale
waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. 9 Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa
ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote
asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”
v Kutuhuisha kutoka katika hali ya kufa
Baada ya anguko la
mwanadamu pale bustanini Edeni kilitokea kifo cha kiroho ambapo Roho wa Mungu
alimwacha mwanadamu, baada ya Yesu kuja na kuimwaga damu yake ndipo daraja la
mawasiliano likajengwa tena na sisi tuakahuishwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Rumi
8:11
“Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua
Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu
ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa
ndani yenu.”
v Kushuhudia kwamba sisi ni watoto wa
Mungu
Roho Mtakatifu anapokaa
ndani ya mwanadamu anashuhudia pamoja na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa
Mungu na tumemshinda ibilisi na tumesamehewa dhambi hivyo sisi ni warithi wa
ule uzima wa milele.
Rum
8:16
“Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho
zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”
v Ni msaidizi wetu
Baada ya kuondoka kwa Yesu
Kristo ambaye ni Mungu aliyekaa pamoja na sisi katika hali ya mwili (Emanueli)
alisema kwamba atamtuma msaidizi kwetu ambaye atausaidia katika mambo yote ya
kiroho na hata jinsi ya kunenda katika mwili ili tuweze kumpendeza Mungu
Yohana
16:7
“Lakini mimi nawaambia iliyo kweli;
yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi
hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.”
v Hutushuhudia kwa habari ya dhambi haki
na hukumu
Roho Mtakatifu ndani yetu
hutushuhudia kwa habari ya dhambi haki na hukumu. Jambo hili Roho Mtakatifu
hulifanya kwa watu wote hata wale ambao hawajaokoka kwani huwashuhudia wale
ambao hawajamwamini Yesu kwamba bado dhambi ipo ndani yao na hukumu inakuja
Yohana
16:8
“Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha
ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”
v Hutusaidia kuomba
Ni ukweli ulio dhahiri
kwamba mwanadamu hata uombe kwa bidii sana hauwezi kuomba sawasawa na mapenzi
ya Mungu, hii ndio sababu Bwana Yesu Kristo akamtuma Roho wake Mtakatifu ili
atusaidie katika kuomba kwetu tuweze kumpendeza Mungu.
Warumi
8:26
“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu
wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea
kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”
Inaweza kusemwa kwamba;
Roho Mtakatifu kutuombea ni sawa na Mungu kuomba ndani yetu wenyewe ili atujibu
mwenyewe, yaani ni sawa na kupewa mtihani na majibu yake hapohapo
ROHO
MTAKATIFU JUU YA MTU
Hapo awali nilitangulia
kusema kwamba kuna tofauti kubwa ya Roho Mtakatifu kuwepo ndani ya mtu na Roho
Mtakatifu kuwepo juu ya mtu. Neno la Mungu linatufundisha kwamba Roho Mtakatifu
anaweza kukaa juu ya mtu kama yanenavyo maandiko
Wakati wowote Roho
Mtakatifu anaposhuka juu ya mtu ni kwaajili ya kuufunua utukufu wa Mungu katika
maisha yetu, yaani kudhihirisha uweza na nguvu za Mungu katikati ya wanadamu.
Matendo
ya Mitume 1:8 “Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi.”
Roho Mtakatifu
anapoachiliwa au anapokuja na kukaa juu yako tambua kwamba unakazi ya
kukamilisha mbele yako, yaani Roho Mtakatifu akikaa juuu yako sio kwaajili ya
kukuongoza au kukufundisha au kukushuhudia, ni kwaajili ya kufanya kazi kwa
uweza na nguvu za Mungu na kwa ishara na miujiza. Ndio maana tunaona Yesu
anawaambia wanafunzi wake maneno haya “Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi.” Huyu Roho Mtakatifu akikaa juu yetu anatupa nguvu za
kuihubiri injili na kulitangaza Neno la Mungu kama walivyofanya mitume bila ya
woga na kwa ujasiri mkuu.
SWALI: Roho Mtakatifu yupo juu yako? Unaweza
kuihubiri injili? Unaweza kumshuhudia Yesu kwa mataifa (majirani, ofisini,
shambani, shuleni, hospitalini n.k), unaweza kuamuru nguvu za giza kuachia
maisha yako na ya watu wengine (Unaweza kuwafungua waliofungwa na shetani,
unaweza kuwatoa walio mashimoni)
BAADHI
YA MIFANO YA KWENYE BIBLIA INAYOONESHA MATENDO YA ROHO MTAKATIFU ANAPOKUWA JUU
YA MTU.
Mambo aliyoyafanya Yesu
kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu
Utendaji wa Yesu Kristo
uliwezeshwa na Roho Mtakatifu, hakuna Jambo alilolifanya Yesu kwa nguvu zake
pekee bali kwa uweza wa Roho Mtakatifu
i.
Kuanza
kuhubiri na kwenda Nyikani kujaribiwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Yesu alipoenda nyikani
kujaribiwa haikuwa kwa nguvu zake pekee bali ni kwanguvu za Roho Mtakatifu na
kwa uweza wa Roho Mtakatifu, kazi hii Yesu aliifanya mara baada ya kushukiwa na
Roho Mtakatifu wakati alipobatizwa
Luka
3:21-22 “21 Ikawa, watu
wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu
zilifunuka; 22 Roho Mtakatifu akashuka
juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe
ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”
Biblia inasema ………Roho
Mtakatifu akashuka juu yake…………. Baada ya Roho Mtakatifu kushuka juu ya
Yesu ndipo akaanza kufanya kazi iliyomleta hapa duniani yaani kufundisha (Luka 3:23 “Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama
miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,”) kabla Roho
Mtakatifu hajashuka juu ya Yesu hatuoni Yesu akifanya jambo lolote kubwa kama
baada ya kushukiwa na Roho wa Mungu.
Roho Mtakatifu akamwongoza
Yesu na kumpeleka nyikani ili kujaribiwa (Roho Mtakatifu alimpeleka Yesu kumfundisha
na kumpa mtihani ili afaulu)
Luka
4:1
“Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu,
alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani,”
Yesu aliweza kumshinda
ibilisi kwakuwa aliongozwa na Roho Mtakatifu
ii.
Habari
za Yesu zilienea nchi nyingi kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu anapokuwa
juu yako katika eneo la huduma uliyoitiwa habari zako zinasambaa kila mahali
kwa kasi kwakuwa sio wewe unayetenda bali ni Roho wa Mungu juu yako, habari za
Yesu zilisambaa sana mara baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu juu yake.
Luka
4: 14 “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda
Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.”
iii.
Kuwafungua
wafungwa na kuponya kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Yesu Kristo alisema
mwenyewe kwa kinywa chake kwamba matendo yote anayofanya ni kwa uweza wa Roho
Mtakatifu aliyekaa juu yake
Luka
4:18
“Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana
amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru
waliosetwa, 19 Na kutangaza mwaka wa Bwana
uliokubaliwa.”
Hapo awali nilisema kwamba
wakati wowote Roho Mtakatifu anaposhuka juu ya mtu ni kwaajili ya kuufunua
utukufu wa Mungu katika maisha yetu, yaani kudhihirisha uweza na nguvu za Mungu
katikati ya wanadamu. Tunaona Roho Mtakatifu yupo juu ya Yesu Kristo kwa kazi
zifuatazo
ü Kuwahubiri
maskini habari njema – Hawa ni maskini wa rohoni wenye kiu
na njaa ya Neno la Mungu waliopo katika mataifa na hata masikini wa mwilini
ambao Yesu amekuwa masikini ili wao wawe matajiri
ü Kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao – Walifungwa na nguvu za
giza kwenye magereza/mashimo/mapango/ majumba ya kuzimu, waliofungwa na
magonjwa na kila namna ya udhaifu
ü Vipofu
kupata kuona tena – Vipofu waliopofushwa fikra na ibilisi,
vipofu katika maisha ya kiuchumi/afya/ndoa/kazi/biashara n.k. Vipofu wa macho
ya damu na nyama
ü Kuwaacha
huru waliosetwa – Kusetwa ni ile hali ya kukanyagwa au
kuwa chini ya utawala kandamizi unao umiza, Roho Mtakatifu Yupo juu ya Yesu
kuwafungua watu wote waliosetwa
ü Kutangaza
mwaka wa Bwana uliokubaliwa
Mambo hayo yote Yesu
aliyafanya kwakuwa Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.
TAFAKARI: Kama Roho Mtakatifu hayupo juu yako unaweza
kufanya chochote? Kama Yesu Kristo ambaye ni Mungu alimuhitaji Roho Mtakatifu
kuyafanya hayo yote, si zaidi sana kwamba sisi tunamuhitaji zaidi Roho
Mtakatifu juu yetu?
iv.
Roho
Mtakatifu alitenda kazi ya kutoa mapepo Yesu alipoyakemea
Neno la Mungu
linatufundisha kwamba Yesu mwenyewe alitumia uweza wa Roho Mtakatifu kutoa
mapepo yaliyowatesa watu kipindi kile alipoishi katika mwili duniani. Yesu
mwenye amekiri katika Neno lake kwamba ametoa mapepo kwa nguvu za Roho
Mtakatifu
Luka
11:20 “Lakini, ikiwa
mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha
kuwajilia.”
Mathayo
12:28 “Lakini mimi
nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”
v.
Mitume
walihubiri Neno na kufanya ishara na miujiza kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Katika kitabu cha Matendo
ya Mitume tunaona matendo makuu ya Roho Mtakatifu katika huduma walizofanya
mitume wa Yesu. Kwanza tunaona Roho Mtakatifu akishuka juu yao kama ndimi za
moto (kumbuka kwa Yesu alishuka kama hua/njiwa)
Matendo
2:1-4 “1 Hata ilipotimia
siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. 2 Kukaja ghafula toka
mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote
waliyokuwa wameketi. 3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto
uliowakalia kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema
kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”
Baada ya kushukiwa na Roho
Mtakatifu Petro akawahubiria na tunaona watu elfu tatu wanampokea Yesu Kristo
kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao kwa uweza wa Roho Mtakatifu
Matendo
2:41
“Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa;
na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.”
Baada ya hayo tunaona
Mitume wakifanya ishara na miujiza ya hali ya juu mno kwa uweza wa Roho
Mtakatifu kama yanenavyo maandiko.
Matendo
5:12,15 “12 Na kwa
mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote
walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; 15 hata ikawa katika njia
kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija,
ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.”
Matendo
6:8
“Na Stefano, akijaa neema na uwezo,
alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.”
Matendo
19:11-12 “11 Mungu
akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; 12 hata wagonjwa
wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea,
pepo wachafu wakawatoka.”
vi.
Roho
Mtakatifu juu ya Samsoni
Samsoni ni mmoja kati ya
waamuzi wa Israeli ambao Mungu aliwapa nguvu nyingi sana za mwili, ijapokuwa
Samsoni alikuwa ni mwanadamu wa kawaida lakini aliweza kufanya peke yake jambo
lililohitaji mamia aumaelfu ya watu kulifanya. Mambo yote ya kushangaza
aliyofanya Samsoni ni baada ya kujiliwa na Roho Mtakatifu juu yake kama
tunavyosoma katika Neno la Mungu.
Waamuzi
14:6,19 “6 Roho ya Bwana
ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala
hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama
yake aliyoyafanya. 19 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye
akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na
kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira
zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.”
Waamuzi
15:14 “Alipofika Lehi,
Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa
nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani
iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.”
Kumbuka wapo Waamuzi wengi
wa Israeli ambao Roho Mtakatifu alikuja juu yao kwa nguvu (Waamuzi 3:9-10, Waamuzi 11:29)
vii.
Roho
Mtakatifu juu ya Mariamu
Yesu kuja duniani ni kwa
uweza wa Roho Mtakatifu, alifanyika mimba katika tumbo la bikra Mariamu kwa
nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu na akawa mwili hata Mungu akazaliwa katikati
ya wanadamu akiwa na sura na miili kama yetu
Luka
1:35
“Malaika akajibu akamwambia, Roho
Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama
kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa
Mungu.”
Hapa tunajifunza kwamba
ili Baraka zako (za rohoni kama ilivyoandikwa katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu,
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika
ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;”) ziumbike katika hali ya mwili na
uyaone mafanikio kwa macho yako, ni lazima Roho Mtakatifu aje juu yako na
kukuwezesha.
viii.
Roho
Mtakatifu juu ya Daudi
Mafanikio yote katika
maisha ya mfalme Daudi yalianza baada ya Roho Mtakatifu kushuka juu yake kwa
nguvu, kutokea hapo maisha ya Daudi yalibadilika akawa ni mtu wa ushindi kwa
kila jambo analolifanya, akamshinda Goliathi, akawaua wafilisti na maadui zake
wote akawashinda na hatimaye kuwa mfalme hata sasa kiti chake cha ufalme
kinatawala Dunia yote.
1Samweli
16:13 “Ndipo Samweli
akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya
Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda
zake Rama.”
Bwana Yesu akubariki sana
mtu wa Mungu, ninaamini kuna kitu umepata katika somo hili ili utoke mahali
kwenda mahali.
Jambo moja kubwa nataka
utafakari wakati wote ili upate kiu ya kutafuta ushirika na Roho Mtakatifu ni
hili; ikiwa Yesu mwenyewe alimuhitaji Roho Mtakatifu ili kuzitenda kazi za
Mungu Baba, Je? Wewe haumuhitaji huyu Roho Mtakatifu?
Ikiwa Mitume walifanya
ishara na miujiza ya kupita kawaida kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu, Je?
Wewe haumuhitaji huyu Roho Mtakatifu.
MAOMBI:
Baba
katika jina la Yesu Kristo ninaomba Toba na rehema kwa maovu makosa na dhambi
nilizozitenda katika maisha yangu na kuchafua mavazi yangu, leo ninaomba
unioshe na kuyatakatisha mavazi yangu kwa damu yako Bwana Yesu ili Roho Wako
Mtakatifu aweze kuingia ndani yangu na kukaa juu yangu kwa ishara na miujiza
katika jina la Yesu Kristo
Roho
Mtakatifu, nimetambua leo yakuwa wewe ni BWANA, wewe ni Mungu, wewe ndiye
unayetenda ishara na miujiza ya kila namna ndani ya Yesu Kristo, ninaomba
unisamehe ujinga wangu wa kutotambua nafasi yako katika maisha yangu.
Ninakukaribisha sasa ndani yangu uwe Kiongozi na Mwalimu wangu unifundishe
namna ya kumpendeza Mungu Baba, karibu juu yangu kwa Nguvu na Uweza wako ili
niweze kuzifanya kazi za Baba katika dunia hii kwa jina la Yesu Kristo
Na
sasa ninakiri ya kwamba Roho Mtakatifu upo juu yangu sasa, na umenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Umenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa kwa nguvu na uweza
wako katika jina la Yesu Kristo.
Neema
ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba na Ushirika wa Roho Mtakatifu
ukae namimi katika maisha yangu yote sasa na hata milele, Amen.
2 comments:
Asantee kwa somo,lakini naomba kujua Roho Mtakatifu anawezaje kusema ndani ya mtu MF utasikia mtu anasema "nimemsikia Roho akisema na mm ndani " huwa anamanisha nn ?
somo zuri
Post a Comment